Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 20,912
- 30,253
Suleiman Kumchaya anasema kuwa Julius Nyerere alipokuwa Makerere alikuwa anawasiliana na wazee wa Dar es Salaam akiwataka waanzishe chama cha siasa.
Ukisoma makala hizi mbili utazania ni jibu la mtihani la wanafunzi wawili watukutu walioangaliana mtihani jambo amabalo mwalimu hodari ataligundua mara moja katika kusahihisha.
Suleiman Kumchaya karudia maneno ya Mzee Msekwa kuwa TAA kazi yake ilikuwa, ''kutetea maslahi ya wafanyakazi Waafrika,'' na Julius Nyerere ndiye aliyeibadilisha TAA kuwa, ''chama cha siasa cha kudai uhuru,'' kazi ambayo aliifanya kwa kushirikiana na ''wazee wa pwani.''
Maneno haya yote ya Kumchaya hayana ushahidi katika historia ya uhuru wa Tanganyika na nathubutu kusema kuwa Kumchaya haijui historia ya TANU na inashangaza sana katika historia ya TANU kwa kila aizungumzae atataja, ''wazee,' ambao hawana majina kama vile hakuna awajuae.
Nyerere kabla hajafika Dar es Salaam hakuwa anajuana na mzee yeyote katika wazee wa Dar es Salaam ambao walikuwa katika siasa kwa hiyo hakuwa anaandikiana barua na mzee yoyote kuwataka waunde chama cha siasa.
Nyerere alikuja kujuana na wazee wa Dar es Salaam baada ya yeye kujuana na Abdul Sykes mwaka wa 1952 na kugombea nafasi ya urais dhidi ya Abdul Sykes katika uchaguzi wa mwaka wa 1953 na kushinda.
Kuanzia mwaka huu wa 1953 ndiyo Abdul Sykes akamjulisha Nyerere kwa wazee wa Dar es Salaam kuanzia na Mufti Sheikh Hassan bin Ameir, Jumbe Tambaza, Mshume Kiyate, Sheikh Suleiman Takadir na Said Chamwenyewe kwa kuwataja wachache na hii kazi ya kumtambulisha Nyerere kwa wazee na masheikh maarufu wa Dar es Salaam ilifanywa vilevile na ndugu wawili, Iddi Faiz Mafungo na nduguye Iddi Tosiri kwa kumpeleka Nyerere Bagamoyo kumtambulisha kwa Sheikh Mohamed Ramiya ambae wao alikuwa binamu yao.
Kila anaejisikia kuwataja ''wazee,'' utasikia, ''wazee'' lakini majina yao hayatajwi.
Kwa nini iwe hivi?
Historia ya TANU nimeieleza mara nyingi hapa kiasi naona tabu kuirudia tena.
Katika uchaguzi wa mwaka wa 1953 Nyerere aliingia katika uongozi na timu ya vijana watupu kama Abdul Sykes, Ally Sykes Tewa Said Tewa, Dossa Aziz, Joseph Kasella Bantu, Dome Budohi kwa kuwataja vijana wachache na mzee katika timu hiyo alikuwa John Rupia.
Wazee wa mwisho katika uongozi awamu yao ilikwisha mwaka wa 1950 baada ya mapinduzi yaliyofanywa na Abdul Sykes na Hamza Mwapachu yaliyowatoa madarakani Thomas Plantan na Clement Mtamila na nafasi zao za urais na katibu kuchukuliwa na Dr. Vedasto Kyaruzi kama Rais na Abdul Sykes Katibu.
Inaelekea Kumchaya kama Mzee Msekwa haijui historia hii na ndiyo sababu ya haya makosa ambayo kwa hakika hayana sababu ya kufanywa.
Hawa wangejitahidi lau kufanya utafiti kidogo katika Maktaba ya CCM wangelikuta pale Dodoma kuna majalada ya Hamza Mwapachu, Abdul Sykes na ya wazalendo wengine ingawa ndani hakuna nyaraka majalada ni matupu.
Mimi katika utafiti wa kitabu cha Abdul Sykes nimefika hapo.
Wangeanzia hapo wangeweza lau kwa uchache kupata historia ya TANU na wagelijua kuwa historia ya TANU inaanza na historia ya African Association chama kilichoundwa na Kleist Sykes mwaka wa 1929 na katika uasisi wa TANU wanae wawili Abdul na Ally Sykes walishiriki na wana historia ndefu ya chama hicho kushinda Julius Nyerere.
Wangelijua pia kuwa Abdul alifanya mazungumzo na Chief David Kidaha Makwaia kuanzia 1951 wakijadiliana kuhusu kuasisi TANU mazungumzo ambayo Abdul alikuwanayo na Hamza Mwapachu kwa miaka mingi na ilikuwa Hamza ndiye aliyemleta Nyerere katika harakati za TAA Dar es Salaam kuishia na Nyerere kuchaguliwa kuwa kiongozi wa TANU mwaka wa 1954 na kukabidhiwa jukumu la kuongoza mapambano ya kudai uhuru.
Jambo la kuhuzunisha katika magazeti haya ni kuwa baada ya kuandika makosa na mtu akasahihisha na kuwapelekea makala wanakataa kuchapa makala hizo wakitaka wabakie na historia ile rasmi yenye makosa.
Hakika huu ni msiba mkubwa pasi na mfano katika historia ya nchi yetu.