Sudan ya Kusini: Nuksi za ukabila na uroho [Wa-TZ- Someni ni POLITICS 101]

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,869
1,225

Makala
BARAZANI KWA AHMED RAJABAhmed Rajab Toleo la 331 25 Dec 2013


SUDAN ya Kusini inatokota.Taifa hili changa lisilotimu hata umri wa miaka mitatu hivi sasa limo hatarini. Liko ukingoni likiichungulia Jahannam. Likisukumwa kidogo tu taifa hilo litatumbukia katika hiyo Jahannam.

Matokeo ya hayo ni kwamba mataifa mengine nayo yatajikuta yanaingilia mzozo usioyahusu ndewe wala sikio. Hivi sasa tayari Kenya na Uganda zimekwishapeleka majeshi yao kwenye mipaka yao na Sudan ya Kusini. Kwa hakika, kuna shtuma kwamba majeshi ya Uganda yameingia hasa ndani ya Sudan Kusini kuyasaidia majeshi ya serikali.

Kwa sasa Sudan Kusini imegeuka jungu kubwa linalotokota. Ndani ya jungu hilo mna kila aina za nuksi: ukabila, uroho, ufisadi, utawala mbovu na mapato ya mafuta. Huo ni mchanganyiko wa hatari unaoweza kulifanya taifa hilo jipya linalotambaa lisiweze kusimama.


Kuna mambo kadhaa yanayoweza kuifanya nchi hiyo isiweze kusimama. Kwanza serikali inaendeshwa msege mnege, haina uwazi wala haiwajibiki.


Fedha za misaada ya kigeni zenye thamani ya mabilioni ya dola za Marekani zimeliwa na wakuu. Mapato ya mauzo ya mafuta yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 20 hayajulikani yamekwenda wapi.


Mwaka jana Rais Salva Kiir alikiri kwamba watumishi wa serikali wapatao 75 waliokuwa chini yake, waliiba dola za Marekani bilioni nne wakati wa utawala wa mpito kabla ya nchi hiyo kuwa taifa huru.


Kuna tuhuma kwamba akaunti za benki za viongozi binafsi ambazo miaka mitano tu iliyopita zilikuwa na vijisenti viwili vitatu sasa zinaonyesha kuwa zina mamilioni ya dola za Marekani.


Uzembe serikalini na ufisadi umeikwamisha serikali isiweze kuendeleza sekta za madini, misitu na kilimo. Hizo ndizo sababu kwa nini nchi hiyo haina miundo mbinu wala maendeleo yoyote ya maana. Kilomita 50 tu za barabara zake zina lami.

Halafu jeshi lake limesambaratika. Watu wa kabila la Dinka wanalalamika kwamba wenzao wa kabila la Nuer wanapandishwa vyeo jeshini bila ya kuwa na sifa zinazohitajika.

Wasio Wadinka nao wanalalamika kwamba Wadinka wamevihodhi vyeo vyote vyenye ulwa serikalini.


Sudan Kusini ina makabila yapatayo 64. Wadinka (au Wajieng, kama wenyewe wanavyopenda kujiita) ndio walio wengi wakiwa kama asilimia 15 ya wakaazi wote wa huko na Wanuer (au Wanaath) ni asilimia 10.


Kabila la Dinka limegawika na lina matawi yake kama lile la Dinka Ngok na lile la Dinka Bor; hawa Wadinka wa Bor ndio Wadinka wa mwanzo kuwa Wakristo na kusomeshwa na Wazungu.


Mapigano yalipozuka mjini Juba Jumapili ya wiki iliyopita kati ya wafuasi wa Rais Salva Kiir na Dkt Riek Machar, makamu wake wa zamani, vyombo vya habari vya nje ya Sudan Kusini vilicharuka na vikayaelezea mapigano hayo kuwa ni ya kikabila. Sababu yao ni kuwa Kiir ni Mdinka na Machar ni Mnuer.


Ukweli halisi ni kwamba ingawa mzozo huo baadaye ulichukuwa sura ya kikabila chanzo chake si tafauti za kikabila bali kilikuwa tafauti za kisiasa baina ya Kiir na hasimu yake mkuu Machar ambaye anaungwa mkono na Rebecca Garang, mjane wa Dkt. John Garang, kiongozi muasisi wa vuguvugu la kupigania Sudan ya Kusini. Rebecca ni Mdinka kama Kiir.


Kigogo mwengine mwenye kumuunga mkono Machar ni Pagan Amum, katibu mkuu wa zamani wa chama kinachotawala cha SPLM. Huyu ni Mshilluk. Makabila ya Nuer na Shilluk ndiyo yenye idadi kubwa ya watu katika majimbo ya Bahr al Ghazal na Upper Nile.


Wadinka na Wanuer wamekuwa mahasimu tangu jadi na jadi. Daima wamekuwa wakizozana kuhusu ardhi na wakiibiana ng’ombe. La ajabu ni kwamba makabila hayo mawili yamekuwa na uhasama mkubwa hivyo licha ya kwamba yana mila zinazofanana sana na tamaduni zao zinalingana.


Wadinka wa Bor wanawaogopa watu wa kabila dogo la Murle ambao raha yao ni kuyavamia mazizi ya ng’ombe wa Wadinka karibu na mji wa Bor. Wadinka siku zote wanawakashifu Wanuer kwa kusema kwamba ni wakali, wanaksirika mara moja na Wamurle kuwa ni vichaa.


Wadinka wanasema kwamba hawasahau aliyoyafanya Machar mwaka 1991. Mwaka huo Machar alipapurana na Garang na Kiir, akawaacha mkono na akaunda vuguvugu lake la ambalo likiungwa mkono na watu wa kabila lake.


Baadaye wapiganaji wa kabila la Nuer waliokuwa wafuasi wa Machar waliwaua elfu kadhaa ya raia Wakidinka, wakiwemo wanawake na watoto. Wanasema kwamba mshambulizi hayo yaliongozwa na Machar mwenyewe.


Kwa muda wa miaka kadhaa baadaye Machar akawa anashirikiana na Serikali ya Khartoum ili kuwadhoufisha akina Garang, Kiir na chama chao cha SPLM.

Mwaka 1997 Machar alitia saini mkataba wa amani na Khartoum akijitenga rasmi na kina Kiir na viongozi wengine wa SPLM. Mwaka 2002 alipatana na Garang na Kiir na akarudi katika chama cha SPLM na akawa kamanda mkuu katika jeshi la chama hicho, SPLA.


Sudan Kusini ilipokuwa taifa kamili lililo huru Julai 9, 2011 Machar aliteuliwa makamu wa Rais lakini Kiir alimfukuza kazi Julai, mwaka huu.

Wananchi wa Sudan Kusini wakitaraji kwamba taifa lao jipya litajengwa juu ya misingi ya makabila yote kuwa na haki sawa, demokrasia na utawala wa sheria.
Mwaka 1994 Garang aliwaambia watu wake wa Sudan ya Kusini kwamba “dhalimu hana rangi”. Wengi hawakumfahamu.

Zamani kabla ya Sudan Kusini kuwa taifa huru kwa Wasudan wa Kusini dhalimu alikuwa Mwislamu aliyepiga kilemba kutoka kaskazini mwa Sudan. Sasa wanatambua kwamba dhalimu anaweza kuwa Mdinka, mweusi kama wao, akiwa na chanja usoni madhali Mdinka huyo ni mtawala anayewanyima raia haki zao, hatawali kwa njia za kidemokrasia na utawala wake si wa kisheria.

Kina Machar wanasema kwamba hivyo ndivyo alivyo Salva Kiir wanayemtuhumu kuwa ana mkakati wa kuselelea madarakani. Na wanamtaka aong’oke halan.

Wanamshtumu pia kwamba serikali yake inaushadidia ukabila. Wanasema kwamba ukabila ulianza kuzagaa serikalini tangu wakati wa kipindi cha mpito kilichoanza mwaka 2005. Wengi wa wafanya kazi katika wizara ya sheria na maendeleo ya kikatiba, kwa mfano, walikuwa Wadinka. Hali hiyohiyo ilikuwako katika wizara ya fedha.


Baada ya uhuru Salva Kiir aliendelea na mtindo huohuo. Idadi ya mawaziri wa kabila la Dinka ni wengi kushinda mawaziri kutoka makabila mingine. Na kati ya hao Wadinka, kumi wametoka katika jimbo lake la Warrap pamoja na mkuu wa usalama, jaji mkuu wa mahakama kuu na gavana wa Benki Kuu.Kwa upande wa mabalozi pia zaidi ya nusu yao ni Wadinka na wengi wao ni kutoka eneo lake Rais. Serikali ya Kiir pia imekuwa ikiwavumilia Wadinka wanaonyakua ardhi katika maeneo kadhaa yakiwa pamoja na Juba, Numeli na Yei.


Nyingi ya shtuma hizo za utawala mbovu zilitolewa Aprili, 2011 katika lile liitwalo ‘Tangazo la Mayom’. Waraka huo ulitiwa saini na watu watatu: makamanda wawili wa jeshi na wa tatu alikuwa mbunge.


Mmoja wa hao makamanda wawili, Meja-Jenerali Peter Gadet Yak, alikuwa kati ya makamanda mahodari wa Sudan
ya Kusini lakini punde tu kabla ya uhuru aliwaacha mkono kina Salva Kiir akiwatuhumu kwamba ni wabaguzi na watawala wabovu. Alhamisi iliyopita majeshi yake yaliuteka Bor, mji mkuu wa Jimbo la Jonglei, yakimuunga mkono Machar.- See more at: Raia Mwema - Sudan ya Kusini: Nuksi za ukabila na uroho
 

tofyo

JF-Expert Member
Jul 18, 2013
2,690
2,000
marekani na washirika wake ndio waliosababisha.
yeye ndie alie shawishi s.sudan ijitenge ili mchina afutiwe mkataba wa uchimbaji wa mafuta.
problem
reaction
and solutio.
this is the major tactics of exploitation now adays.
 

reandle

JF-Expert Member
May 6, 2009
11,211
2,000
Nilipata kuzungumza hapa kwamba Watanzania, tupige kazi badala ya kuingiwa na kihoro kutokana na Collision Of Willing! COW inaundwa na very volatile countries na nikasema endapo Kagame angekuwa smart enough, angeogopa sana kuitegemea Bandari ya Mombasa wakati kutoka Rwanda hadi Mombasa ni lazima upite nchi mbili; and so its effectiveness inategemea usalama wa nchi zote mbili; Uganda na Kenya!

Uganda, huenda mwakani wakaanza kuuza mafuta...god forbid, lakini ni kama naiona vita ndani ya Uganda few years to come. Msumbiji, RENAMO wameshaanza kazi wakati hata pipa moja la gas halijazalishwa! Kila cku story zisizoeleweka kuhusu Joseph Kony...mara amejificha, mara amejisalimisha Jamhuri ya Afrika ya Kati; mara US inamsaka! Nani asiyefahamu uroho wa US inapokuja suala la nchi yenye wese? Kony ameisumbua Uganda since 1980s, kwanini US wajifanye ndo wanamsaka sasa?! Wawe wanamsaka kweli na isiwe kumuandalia mamluki wa kumsaidia kurudi UG kwa nguvu mpya!
 

reandle

JF-Expert Member
May 6, 2009
11,211
2,000
Zamani kabla ya Sudan Kusini kuwa taifa huru kwa Wasudan wa Kusini
dhalimu alikuwa Mwislamu aliyepiga kilemba kutoka kaskazini mwa Sudan. Sasa wanatambua kwamba dhalimu anaweza kuwa Mdinka, mweusi kama wao, akiwa na chanja usoni madhali Mdinka huyo ni mtawala anayewanyima raia haki zao, hatawali kwa njia za kidemokrasia na utawala wake si wa kisheria.
Hotuba za Nyerere zinapaswa kutafsiriwa kwa lugha mbalimbali na kurushwa nchi mbalimbali, si za Afrika tu bali kote duniani. Nyerere wakati akiwa Afrika Kusini akihutubia Bunge la nchi hiyo, alisema, nukuu si rasmi "Afrika Kusini mwa Jangwa Sahara tunapaswa kushirikiana kwavile mataifa ya magharibi hayawezi kuwa concerned na sisi kwavile ni mbali sana huku. Lakini watu wa Magharibi wanaweza kuwa concerned na nchi za Afrika zilizo kaskazini kwavile wanafahamu, wasipozisaidia nchi hizo; ni rahisi sana kwa wananchi wa nchi hizo(afrika kaskazini mwa sahara) kuzamia Ulaya kutokana na proximity." Mwisho wa nukuu isiyo rasmi lakini iliyobeba content ya nini Nyerere alisema!

Wazungu endapo wange-take note ya kauli hii ya Hayati Mwalimu; wimbi la wazamiaji haramu kutoka Kaskazini mwa Afrika kwenda Ulaya lisingekuwa na kasi kubwa kama lilivyo sasa! Endapo Wazungu wange-take note kauli hii ya Mwalimu, basi wangejizuia sana kuchochea migogoro na yeyote mwenye kuchochea wangemuendea na vifaru! Blindly, hawaku-take note na matokeo yake hivi sasa wanaisoma namba!!
 

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,869
1,225
marekani na washirika wake ndio waliosababisha.
yeye ndie alie shawishi s.sudan ijitenge ili mchina afutiwe mkataba wa uchimbaji wa mafuta.
problem
reaction
and solutio.
this is the major tactics of exploitation now adays.

Mkataba wa MCHINA bado UPO wanapeleka Majeshi yao KULINDA hivyo VITALU VYA MAFUTA HUKO SOUTH SUDAN
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Similar Discussions

Top Bottom