SoC01 Suala la machinga Serikali iache kujifungia na kuwaamini tu Watumishi/Wataalamu wake, iwashirikishe Wataalamu wenye elimu ya mtaani

Stories of Change - 2021 Competition

May Day

JF-Expert Member
May 18, 2018
6,162
8,820
Nadhani inafahamika namna ambavyo kipaumbele cha kuajiri serikalini huwa ni vyeti bila kujali uwezo wa Watu hao kiutendaji.

Labda ndio maana mpaka sasa bado imebaki ni mtihani mkubwa kwa Watendaji wetu hawa kuja na ufumbuzi wa nini wafanye kuhusu suala hili la Wamachinga zaidi ya kutamani tu waondolewe.

Haina ubishi kwamba Wamachinga na Mama mboga hawa wamevuruga sana miji yetu, na bado wanaendelea kuvuruga, na kadri siku zinavyosonga ndio ugumu wa kupata ufumbuzi wa hili tatizo unavyoongezeka.

Huenda Viongozi wetu wakishirikiana na Watendaji hawa wanaowaamini sana kwa vyeti vyao ndio huja na matamko rahisi tu "waondoke" wakiamini ndio namna bora pekee ya kupata suluhu ya tatizo. Wakae wakijua kumtoa Mtu kwenye sehemu anayopatia riziki yake ni sawa na kumwambia Mtu huyo kuanzia leo wewe utashinda njaa. Na sijui ni Mtu mzima gani Mwenye akili timamu atajiona salama kando ya Mtu Mwenyenjaa.

Kuna hotuba moja ya Mwalimu Nyerere alisema, salama ya Mwenye nacho ni pale asiyenacho awe ameshiba. Tunaweza kufanikiwa kuwaondoa lakini swali litabaki kuwa suluhu hiyo itadumu kwa muda gani?. Wakati wake Hayati Magufuli ailizitaka Mamlaka kuja kwanza na jibu la wapi wanawapeleka kabla ya kuwaondoa mahali walipo kwa sasa.

Wanachokihitaji Wamachinga na Mama mboga hawa ni mazingira Wanayoweza kukutana na Mikusanyiko/Wateja. Kwa hiyo Wataalamu wetu wa Kupanga miji wanatakiwa wafanye kazi na waje na majibu sahihi kabla ya kusema sasa waondoke.

KUSHIRIKISHA WALIO NJE YA MFUMO
Ikibidi serikali itafute maoni ya Wananchi, Wafanyabiashara Wakubwa na Wadogo, Wamachinga na Kina Mama mboga. Mtaani kuna Watu wengi wenye akili ya biashara ambao wameifanya kwa vitendo na wanajua kila linalohusiana na biashara hizo za mtaani, wapo wenye uwezo mkubwa wa kufikiria nje ya boksi kuliko Wataalamu wetu wengi wenye utitiri wa vyeti na tunaowaamini sana. Tukae chini na Watu kama hawa mpaka tupate namna bora ya kuwasimamia Wamachinga na kina Mama mboga wafuate taratibu.

MTAZAMO WANGU
Ikibidi serikali iingie gharama ya kuinua sehemu za miji, kutokana na ufinyu wa nafasi uliopo kwenye hii Miji mikubwa. Mfano kwa Arusha maeneo kama pale Samunge au Kilombero yainuliwe kama 'flyovers', au yachimbwe kama 'subways' na kugeuzwa makutano ya Daladala za jiji, kwa mazingira ambayo Abiria wakishushwa watapita kwenye floor mbili au tatu kabla ya kufika nje. Maeneo haya yote yageuzwe masoko makubwa.

Pia kwa yale maeneo ambayo Mamlaka zitaridhia Wamachinga wabaki kuandaliwe utaratibu mpya ambapo ata/watatafutwa wabunifu wa vibanda/meza ambazo zitakuwa na mfanano na vipimo maalumu vyenye mvuto, ambavyo Mpewa tenda ataingia makubaliano na Wamachinga au Mama mboga wa eneo husika na watamlipa gharama zake. Hata hivyo vibanda au meza hizi zinaweza pia kutumika kama mabango ya biashara hivyo vikawa pia vyanzo vya mapato endelevu kwa mamlaka.

Pia Mamlaka za Miji zitafute maeneo ya nje ya Mji, kama kwa Arusha wanaweza kutumia Nanenane Njiro au Kisongo ambapo wataandaa Masoko ya mara moja kwa mwezi au Wiki, kama shughuli inavyofanyika wakati wa siku ya nanenane pale Nanenane.

Bila shaka kwa mambo kama hayo inaweza ikapunguza adha ya msongamano wa Wamachinga na kina Mama mboga katikati ya miji na barabarani, na watabaki Wachache watakaoweza kusimamiwa hivyo kubakiza hadhi ya Miji yetu.
 
Back
Top Bottom