Mtambuzi
Platinum Member
- Oct 29, 2008
- 8,810
- 15,398
Kujadili dini ni mojawapo ya mijadala inayokwepwa na baadhi ya wanajamii ili kuepusha shari na kudumisha amani. Lakini linapokuja swala mahusiano hususan pale watu wawili wenye imani tofauti za kidini wanapotaka kuoana, unaweza kuzuka mjadala mzito miongoni mwa ndugu na jamaa wa wapenzi hao na wakati mwingine hata marafiki hutokea kupinga muunganiko huo.
Ninao mfano unaonihusu. Mdogo wangu anayenifuatia kuzaliwa alipata mchumba (mume) mwenye imani tofauti na imani yetu, jambo hilo lilizusha mtafaruku katika familia yetu kila mmoja akisema lake. Ilitokea tu mimi na baadhi ya ndugu zangu akiwemo baba tuliafiki ule muunganiko wao na ndoa ikafungwa na sasa ndoa yao ni imara na imetimiza miaka tisa mwaka huu wakiwa na watoto watatu.
Ukweli ni kwamba jambo hili limekuwa likileta mtafaruku katika baadhi ya familia na wakati mwingine familia hujikuta ikisambaratika hasa pale ambapo familia moja inashindwa kukubali utashi wa mtoto wao kuolewa au kuoa mtu mwenye imani tofauti na mara nyingi hii hutokea katika familia zenye msimamo mkali wa kidini. Kama inavyofahamika mapenzi ni kitu cha ajabu sana. Pale ambapo penzi linapochipua hufunika imani zetu kiasi cha kujikuta wakati mwingine tunazisaliti imani hizo ambazo hata hivyo baadhi yetu hazikuwa utashi wetu bali tu tumejikuta tukiwa humo kwa sababu ni imani ambazo tumezaliwa na kukuta wazazi wetu wakiwa ni wafuasi wa imani hizo.
Huu ni mtihani mgumu sana kwetu na mara nyingi waathirika wa mtihani huu wengi wao ni wanawake na watoto ukilinganisha na wanaume. Wakati mwingine huwa najiuliza inakuwaje mtu anampata mpenzi anayempeda sana na mwenye sifa azitakazo lakini anashindwa kufunga naye ndoa kwa sababu ya kuwa na imani tofauti? Lakini pia wapo ambao wanalazimika kufunga ndoa na wapenzi wao sio kwa sababu wamependana, bali ni kwa sababu tu imani zao zinafanana !
Kuna wanawake wengi sana wa kiasi cha kutosha wanalazimika kuishi katika ndoa ngumu kwa sababu ya imani zao, kilichowavuta kuingia katika muunganiko huo ni imani zao lakini sio upendo. Lazima tukubali kwamba mapenzi ni kitu kingine na imani ni kitu kingine. Kuingia katika ndoa kwa kigezo cha imani kunakuwa na changamoto zake ambazo mara nyingi hazina matokeao mazuri.
Naamini hata humu JF wapo ambao wamewahi kukabiliana na mtihani huu au wako katika hati hati ya kukabiliana na mtihani huu. Hebu tupeane uzoefu juu ya jambo hili linalowatatiza wengi.
Swali: Iwapo wewe ni single, Je uko tayari kufunga ndoa na mtu mwenye imani tofauti na imani yako? Je umejiandaaje kukabiliana na changamoto za wazazi, ndugu, marafiki na jamii kwa ujumla watakapopinga muunganiko wenu ?
Nisingependa mjadala huu uwe ni wa kidini.
Nadhani mmenielewa.........