STORY: Jesus Freak

B. WATU WANGU WANAANGAMIZWA KWA KUSOMA MAARIFA HOSEA 4:6A!


LISA:

Unajua unapoamua kujiingiza full time kwenye mambo ya imani kusema ukweli kabisa unakuwa kama mtoto mdogo, namaanisha hivi mambo mengi ya Imani inakuwa huyajui kwahiyo unaamua kuwa mpole kujifunza, unakuwa mjinga flani, ni kama kwenda kuanza shule, siku ya kwanza au miezi ya kwanza au siku za mwanzo unakuwaga mpole, hujui kitu, unakuwa mnyenyekevu lakini ukifundishwa ukishajua unakuwa mjanja.
Vivo hivyo na imani, hujui hujui tu unakuwa mpole mpaka ujue kila kitu ndio unaanza kuwa mjanja.
Na kufahamu kilakitu kwenye Imani inaweza ikachukua miaka au miezi inategemea na spidi yako na utayari wako kwenye kumpenda Mungu na kiu yako ya kumjua Mungu katika Imani!
Leo nipo na shoga yangu mmoja, nimekutana nae hapa Steers mjini, nae alikuwaga ameokoka tulipokuwa shuleni, shuleni namaanisha huko form 5 na form 6 niliposomaga na Azonto!
Shoga yangu huyu anaitwa Nyanjige, ndio ni Msukuma alieokoka, tena msukuma full mama na baba wote wasukuma, tukapiga stori pale Steers akaniambia anafanya biashara zake mwenyewe!
Kwa kuwa siku zilikuwa zimepita nyingi nikatamani kujua maendeleo yake maana imeshapita miaka 20 tangu tuachane shule, mwenyewe kapendeeeza na ule mshepu doh anang’ara kweli kweli!

LISA: NYANJIGE MZIMA? Za siku mami?

NYANJIGE: Nzuri ZA KWAKO?

LISA: salama vipi uko wapi sasa?

NYANJIGE: Nafanya Biashara zangu mwenyewe!

LISA: Wow! hongera sana, familia wazima? sijakuona muda rafiki yangu tangu tuachane form 6?

NYANJIGE: Hawajambo wanaendelea vizuri

LISA: Shemeji hajambo na watoto? unawatoto wangapi sasa?

NYANJIGE: Sina hata mmoja, sijaolewa pia.

LISA: Nikashtuka moyoni na tumboni, nasikia kama tumbo linanikata hapo doh! Hajaolewa mpaka leo? hapo mimi nina miaka 45 na wote tuna miaka sawa! Oh jamaani, lakini umeshachumbiwa sasa hivi?

NYANJIGE: Bado nipo singo!

LISA: Eh! imekuwaje Nyanjige tena au hautaki kuolewa?

NYANJIGE: Nataka sana kuolewa ila sijaolewa mpaka sasa!

LISA: Je Kuzaa? haukutaka kuzaa?

NYANJIGE: Sikupata wa kuzaa nae.

LISA: Bado umeokoka Nyanjige?

NYANJIGE: Ndio bado nimeokoka mwaka wa 20 sasa natembea na Yesu

LISA: Kwani Yesu kasemaje? hataki kukuoza au wewe tu unapataga wanaume unawakataa?

NYANJIGE: mmh! acha tu stori ndefu ndugu yangu!

LISA: Muda ninao kama utapenda kunieleza!

NYANJIGE: Vipi wewe una watoto wangapi umeolewa?

LISA: Nina watoto 4, nimeolewa mke wa mume mmoja

WOTE: Tukacheka

NYANJIGE: Hongera sana nakutamania, uliwahi maisha ukawahi kuzaa!

LISA: Namshukuru Mungu, sasa hivi nataka niokoke na mimi

NYANJIGE: mmmh! sikushauri kwakweli!

LISA: Hunishauri? kwanini?

NYANJIGE: Kwenye wokovu wasanii wameshakuwa wengi!

LISA: sijaelewa, kwani naokokea walokole au naokokea nafsi yangu na roho yangu na uhusiano wangu na Mungu wangu?!

NYANJIGE: Utakuwa unasali wapi sasa?

LISA: Kanisani Kwangu nilipofungiwa ndoa Lutheran, kwani lazima nikiokoka nikasali kwa walokole?!

NYANJIGE: Bora iwe hivyo!

LISA: Kwani wasanii kanisani kwenu wametokea wapi?

NYANJIGE: ah! wapo kibao

LISA: Ndio waliokufanya usiolewe wala kuzaa watoto!

NYANJIGE: Ya kwangu yalikuwa tofauti kidogo my

LISA: Utapenda kuolewa tena nikutafutie mchumba akuoe najua miaka 45 hujachelewa kuolewa na kupata watoto

NYANJIGE: Tatizo sio kuolewa tatizo ni kupata watoto!

LISA: Sijaelewa kwani huwezi kuzaa?

NYANJIGE: ndio

LISA: kwanini? dokta kakuambia huwezi kuzaa?

NYANJIGE: ndio!

LISA: Kivipi tena!?

NYANJIGE: Kwasababu unataka kuokoka ngoja nikueleze! uyajue yote, maana watu hujifunza kutokana na makosa ya wengine na ukiona mwenzio amenyolewa wewe weka maji!

LISA: Aya Mama Mchungaji


NYANJIGE: Hapa kuna mambo 3 unatakiwa uyajue!
1. Wakati nipo msichana wa miaka 20 mpaka 35, nilikuwa napata wachumba, kila nikipeleka kwa wachungaji wanawaangalia wametokea kanisa gani, kama sio huku kwenye makanisa yetu ya wokovu wanawakataa
Ninaweza kukutajia wanaume waliokuja wananipenda wanataka kunioa hawapungui chini ya 50, lakini wachungaji wanawarudisha,
Nilipata mpaka watoto wa Matajiri, watoto wa Viongozi, lakini kwasababu hawajaokoka tu walikuwa wanarudishwa na wachungaji kuwa lazima waokoke ndio wanioe!

2. Kanisani tunafundishwa na sio kanisani tu, Biblia pia inatufundisha tusizini kabla ya ndoa, sasa wanaume wengine ninaowapata wanataka tujamiiane kwanza ndio wanioe, nikawa nashindwa kukubali wanachoniomba, maana YESU alishasema wadada mabinti sayuni tunatakiwa tutunze utakatifu na kufungaa miguu.
Miaka yote hiyo ya mimi kufunga miguu na kutunza utakatifu na kumwomba Mungu anipe Mume sahihi Mume wangu, miaka ikawa inaenda na kwenda na kwenda mpaka nilipofika miaka 34 nikaanza kusikia maumivu ya tumbo.

LISA: Tumbo? Doh pole sana enhe…

NYANJIGE: Nikaenda hospital kupimwa tumbo wakaniambia fanya Ultra Sound, kweli nikafanya kipime cha Ultra Sound majibu kutoka nina Fibroids! tena zimeota pabaya ndani ya kizazi!


LISA: Doh! Pole sana, sasa ukazitoa?!

NYANJIGE: Hapana nikarudi nyumbani sina hela sina nini unajua hii ajira nimeipata miaka 3 iliopita, tangu nimemaliza form 6 nilikuwa sijapata kazi nikawa nafanya kazi Kanisani.
Kanisani nalipwa elfu 50 kwa mwezi, hapo hapo natakiwa nipange chumba changu nikawa naishi mwananyamala ambapo kodi ni elfu 20 inayobakia ni chakula na nauli kwenda kazini, Mungu akimgusa mtu ndio nashikwa mkono elfu 10 elfu 5 elfu 2 maisha yanaenda, nikakaa hapo kanisani nafanya kazi kuanzia nikiwa na umri wa miaka 20 mpaka 40.

LISA: Miaka 20 unafanya kazi Kanisani? hata Mchungaji hajakuoza kwa mchungaji yeyote?!

NYANJIGE: Hapana hajawahi aliniambia mwombe Mungu na endelea kumwamini Mungu, kwa Mungu hakuna kuwahi wala kuchelewa kwenye swala la ndoa maana sisi tunaishi Milele!

LISA: Doh ila una moyo, ina maana chuo haukusomaga?

NYANJIGE: Umesahau form 6 nilipataga divishen 4 Lisa, chuo gani kingenichukua miaka hiyo ya zamani?

LISA: ungeanza hata certificate uende Diploma mpaka chuo, hivi kwanza wazazi wako walikuwa wapi mpaka ukateseka hivi?

NYANJIGE: wazazi wangu walinifukuza nyumbani baada ya kuokoka Lisa, nilifukuzwa nikiwa na miaka 18, Kanisani wakanipokea nikawa naishi nyumbani kwa Mchungaji na familia yake, nilipofikisha miaka 23 nikaambiwa nikajitegemee nimeshakuwa mkubwa nikalipiwa kodi ya nyumba miaka 3 mpaka miaka 26 wakaacha kunilipia.
sasa angalia Kanisani nimepokelewa baada ya kufukuzwa kwa wazazi, naendaje kinyume nao labda si ningelaaniwa mwanzo mwisho! ndio maana kila nilipopata mchumba nakataliwa, naanzaje kwenda kinyume nao labda!

LISA: Maskini Lisa, pole sana sikujua mpenzi pole mno! sasa ulipokutwa na Fibroid unatakiwa ukatolewe ukafanyaje? ulipata wapi hela au Kanisa lilikuchangia!?

NYANJIGE: mmmh! acha tu, nilipopata yale majibu,nikafunga siku 3 kavu namlilia Mungu kwenye maombi azitoe hizo fibroid sijui, nilipomaliza kufunga kavu 3 nikarudi kupima nikakutwa zimeongezeka zaidi! Dokta akaniambia harakisha tuitoe maana itaweza kuleta madhara na ikafanya ukatolewa kizazi, pia haya mafibroid husababisha kansa pia!

LISA: Mungu wangu, enhe ukafanyaje?!

NYANJIGE: Nikaamua sasa kwenda kwa Mchungaji alienipokea nilipofukuzwa nyumbani nikamwelezea nikamwonyesha na karatasi nikamwambia na gharama
Mchungaji akasema hakuna linalomshinda Mungu tutaomba zitaondoka kwa Jina la Yesu!

LISA: Tobaaa enhe!

NYANJIGE: Nikamwambia kuwa nimeshafunga kavu 3 na nikarudi kupima lakini bado zinakua
Mchungajia akaniambia tufunge siku 40 lakini tunafungua saa 12 jioni, yaani mfungo wa masaa 12, kama Yesu alivyofunga kipindi kile, nikaona sawa, tukaanza maombi, kila siku jioni tunakutana kanisani na mke wake tunamaliza maombi kwa pamoja,
zikapita siku 30, zimebakia siku 10 tukamaliza mfungo, nikaambiwa nenda hospital kucheki tuje kumchukuru Mungu, na hela ya kwenda hospital na mtu wa kunipeleka hospital nikakabidhiwa niende nae… kesho yake asubuhi naamka miguu inaniuma kushuka kitandani siwezi nyonga zimenishika naumia, nikamwita dada niliekabithiwa nikamweleza hali yangu akaenda kuchukua Taxi nikabebwa juu juu na majirani mpaka hospitali kwa dokta yule yule kwasababu anaijua hali yangu ikawa rahisi kunihudumia
Nikakimbizwa theater, kuangaliwa fibroid zimekuwa kubwa zinatakiwa zitolewe, dokta akaongea na yule dada atoe hela maana anahisi naweza kupata madhara makubwa zaidi, yule dada akatoa namba ya mchungaji dokta akampigia wakaongea sana kama Dk 20 Mchungaji akaruhusu nifanyiwe opereshen, kweli nikafanyiwa opereshen baada ya masaa mengi mbele nikajikuta nipo wodini nimelazwa!
Dokta akaja kunijulia hali akaniambia opereshen imeenda vizuri sana anafurahi ninaendelea vizuri maana alikuwa na wasiwasi, akaniuliza kuhusu wazazi nikamweleza kama nilivyokueleza, akachoka sana, akaniambia kama itatokea utapona usirudi tena kwa huyo mchungaji, akaanza kunitania atanioa nimkubali basi tukaishia kucheka lakini sikuelewa kwanini aliongea hivyo!
Alipoona nina cheka nina furaha, akanionyesha mabonye ya Fibroid yalionitoka mwilini mwangu, maana tumbo lilikuwa limeshaanza kuwa kubwa Lisa kama nina mimba ni vile nilikuwa mdogo mdogo navaa manguo makubwa ikawa haionyeshi!
Akanionyesha kwenye kamera yake mabonye ya Fibroid yalionitoka, Lisa nilipiga makelele mpaka wakahisi nakuwa chizi wakanipiga sindano nitulie

LISA: Nikalia, machozi yalinitoka tu ghafla sikujua yametokea wapi, tukaanza kulia wote pale kwa watu chini chini aibu watu wanatushangaa ikabidi nimwombe tukamalizia maongezi kwenye gari yangu akakubali! doh masikini Nyanjige,
Jamani sijui nikuelezeeje kuhusu Nyanjige, alikuwa msichana mreeembo ana mshepu wa kisukuma, ana liguu la bia jamani alikuwa anampendaje Mungu sasa, doh sikujua kama yatakuja kumkuta haya
Tulipofika kwenye gari Nyanjige akakaa sawa akapata na nguvu za kumalizia kuongea tukaendelea na maongezi

NYANJIGE: Basi nilipokuja kuzinduka nikamkuta mama mchungaji na mumewe wamekuja kunichukua!
Tukaondoka mpaka nyumbani nikawa naishi kwa mchungaji tena mpaka nitakapokaa sawa, kule nilipokuwa naishi nikarudisha nyumba nikakaa sana kwa mchungaji kama mwaka mzima, sikumoja nikamwambia Mchungaji naona maisha yangu yanasonga nataka nitafute kazi nje ya kanisani, akakubali akaongea na mzee wa kanisa mwenye kampuni yake ya micro finance ndio nikaanza kufanya kazi kwake, natoka asubuhi na kurudi jioni saa 1 inategemea na foleni
sikumoja nikaamua kurudi kwa yule dokta anionyeshe tena zile picha za fibroid kama zipo niondoke nayo maana ile ilikuwa ni haki yangu, namshukuru Mungu nikamkuta kweli akanipokea vizuri tukaongea sana, akanipatia kopi ya picha ya zile fibroid, nikamwuliza kama naweza kuzaa kwa njia mbadala tofauti na kuzini!

Dokta: Akacheka sana akasema labda niende ulaya kwa kuwa huku Bongo hamna hio njia kwa wakati huo, ila kuna jambo ambalo sikukueleza sikuile na kwa vile yule Mchungaji sikumuelewa nikaona nisimueleze nikijua utakuja tu, kipindi kile tunaondoa Fibroid zako, zilikuwa zimekula sana kizazi kama tungeacha kizazi zingeota tena, imebidi tuondoe na kizazi ina maana hapo ulipo hauna kizazi!
Kama unapenda watoto nakushauri uisaidie jamii kwa kulea watoto yatima, unaweza kwenda ustawi wa jamii ukaongea nao wakaangalia na maisha yako wanakupatia mtoto unamlea kama wako, usijali Nyanjige maisha lazima yaendelee, na hakuna mwanaume atakaekubughudhi kwasababu ripoti zote za ishu yako nimekupatia wasije kukudanganya umetoa mimba, haihusiani na kupata fibroid kabisa
Niliishiwa na nguvu Lisa, kulia nataka lakini haitarudisha kizazi, nilichanganyikiwa mwenzio nikaondoka sidhani hata kama nilimuaga dokta, nikaanza kuongea mwenyewe barabarani mpaka naingia nyumbani kwa mchungaji nimeshakuwa kichaa waliniwahi mlangoni, nikawa kichaa nikafungwa kamba, nikaombewa sijijui, nikapelekwa hospital napiga watu, ikabidi nipelekwe milembe, nimekaa milembe nikiwa na miaka 35 mpaka 40, mwaka wa 42 nikatoka milembe nimekuja kuchukuliwa na mchungaji na mkewe mpaka nyumbani, nikaishi miezi 6 nikawaambia wanipeleke kwa wazazi wangu

LISA: oh jamaani Nyanjige pole sana mpenzi wangu!

NYANJIGE: Nikapelekwa kwa wazazi wangu, nikawakuta na baba yangu alikuwa anaumwa sana, nikamuangukia nikaomba msamaha kwake, Baba akaniangalia akataka kuinuka wakamzuia, akaniambia nimsogelee nimkumbatie, nikamkumbatia akaniambia nimekusamehe, nakupenda mwanangu, rudi kanisani nilipokukuza na Mungu atakubariki, alipomaliza kuongea akafariki!

LISA: Mungu wangu wee! nikaanza kulia na Nyanjige nae akalia sana, doh siku hio ilikuwa bonge la Reunion!

NYANJIGE: Baada ya Msiba na mazishi, nikamwomba msamaha mama pia, akakubali kunisamehe akaniambia rudi nyumbani, nikarudi nyumbani mwaka wa 42, tangu nilipoondoka nikiwa na miaka 18 nilipofukuzwa kwa ajili ya Imani!
Nikamweleza Mama kuhusu yalionikuta, Mama alilia sana, tena sana akanisamehe akaniambia rudi kanisani kwetu kama Baba alivyosema utabarikiwa usijali, mama alilia kwa uchungu kwasababu alijua kuwa hatopata wajukuu kupitia mimi, lakini alinishangaza kwa kitu kimoja akaniambia yeye na Baba walishaokoka ila hawajahama Kanisa walilokuwa wanasali, Mama akaniambia walishangazwa sana na imani yangu Kwa Mungu ndio waliokuwa na maswali mengi wakajiuliza huko alikokimbilia mtoto kuna nini mpaka leo mwaka wa 24 hajatamani kurudi nyumbani!
Nilifurahi Baba alikufa akiwa anamjua Mungu mwenye imani tele na nashukuru Mungu aliweka msamaha kwake ndio maana kichaa nilipona, baba aliokoka miaka 2 tu lakini alipotamka kunisamehe ndio nilipona kichaa kumbe alikuwa amenikasirikia miaka yote hii sikujua kwanini

LISA: Sasa ukafanyaje sasa kanisani kwa zamani hawajakuita!

NYANJIGE: Baada ya mazishi tuliitwa na mwanasheria kwa ajili ya Mirathi, nikakuta Baba ameniweka kuwa kiongozi na mwangalizi wa mali zake zote, ndio nipo nafanya kazi hapo
Sasa hivi ninasali kanisani kwa wazazi wangu na mama yangu, ndio sijaolewa lakini nina amani zote, nina hela zangu naizunguka dunia kama kichaa, nina safiri mno, na biashara za familia Mungu ametubariki sana!
Ndio sina mtoto sina mume lakini nina amani tele wala hainisumbui kichwa tena!
Yesu sijamuacha ila Yesu ameniongezea wafuasi kwenye familia yangu,mimi na familia yangu yote sasa tunamtumikia Mungu.

LISA: Doh pole sana Lisa, nimefurahi uliishia kupata mwisho mzuri na uliwahi baraka za Baba, pole sana, ungejuaga tangu hapo zamani ungerudigi tu nyumbani yasingekupata haya yote, pole sana na Mungu azidi kukubariki.

NYANJIGE: Amen Sister! sasa niambie bado unataka kuhamia kule nilipotoka!

LISA: Nooo waaaay, mimi Yesu wangu nakuwa nae huku huku nilipo, sitaki matatizo mengine, niliyo nayo yananitosha!
Sasa umenieleza mambo mawili tu je jambo la 3 ni lipi?

NYANJIGE: 3. IMANI ZA UONGO
Kama ningejuaga kuhusu hasira ya wazazi inaweza ikaniharibia maisha ningesharudi nyumbani mapema, kule Kanisani nilipoenda waliniambia Mchungaji na Mke wake ndio wazazi wangu wa kwanza, baraka zote zinatoka kwao, niwasahau wale wazazi wangu walionitupa nje, Mungu ameshanipeleka pale kwa wachungaji wale ndio wazazi wangu

LISA: Kwani Biblia ulikuwa hauisomi au ulilogwa? tangu lini Mzazi aliekuzaa akaachwa kuwa Mzazi wako wa kwanza?!

NYANJIGE: Ndio nilivyofundishwa nikajua ndio hivyo! kumbe nilikuwa nadanganywa, unajua imani bwana ukiingia kwenye mambo ya imani unakuwa kama mtoto mdogo, vitu vingi huvijui na itachukua muda, sasa ukiangukia mikononi mwa wachungaji waongo unaishia kuteseka kama mimi nilivyoteseka na imenigharimu kizazi changu, Mungu tu anajua! Uwe macho Lisa na uwe mjanja sana kwenye mambo ya Imani usije angukia kwenye imani za uongo maana zimeshakuwa nyingi sana mjini sasa hivi na bado zingine nyingi zitakuja maana hizi ni siku za mwisho! Mimi niliangamia kwa kukosa maarifa lakini isiwe hivyo kwako LISA!!





ITAENDELEA KESHO JUMAMOSI TAREHE 20 APRIL 2019 SAA 10 JIONI YA TANZANIA
NAWATAKIA SIKUKUU NJEMA YA IJUMAA KUU

STDVII std vi kanali mstaafu Nas Jr sab Daby lara 1 DOUGLAS SALLU Ekuweme presider Mtende Kamwene Tee Bag Vumbi la congo Viatu vya Samaki Viatu vya Mtumba Nyoka mwenye makengeza Jokajeusi ni ngumu steveachi Monseur Jason Statham2 bartenderznz wined Dark Rahl jiwe angavu Dhul Shark
 
Azonto na yeye alizingua sana,yani hadi mke anashika mimbe yeye hajawahi tu kufanya mashambulizi yeyote ya kijeshi.
 
Back
Top Bottom