Stori ya kusisimua - Taxi

Taxi - (50)

Sammy alimfungulia mlango wa abiria Pendo ili apande, kisha aliliingiza lile gari ndani ya uzio na kutulia ndani ya gari akiliacha liungurume taratibu. Baada ya dakika kama mbili alizima injini.

Alichomoa ufunguo na kuushika mkononi kisha aliteremka kutoka ndani ya lile gari akiwa kashika ufunguo wake na mkono mwingine alimshika mkono Pendo huku akitabasamu.

Winifrida aliendelea kumtazama Sammy kwa mshangao kisha akaligusa lile gari katika namna ya kulishangaa kabla hajageuka kumtazama Sammy.

“Kaka, hili gari la nani?” Winifrida alimuuliza Sammy kwa shauku.

“Kwani unalionaje! Zuri au baya?” Sammy alimtupia swali badala ya kumjibu.

Winifrida alikunja sura yake huku akilitazama lile gari kwa makini kwa namna ya kulikagua zaidi na kushusha pumzi za ndani kwa ndani kama aliyekuwa akitafuta jibu, kisha alifungua mlango wa mbele upande wa abiria na kuingia, akaketi kwenye siti ya abiria huku akiendelea kulitazama kwa mshangao.

“Unalionaje, zuri au baya?” Sammy aliuliza tena swali lile lile huku akiachia tabasamu.

Winifrida alimtazama na kunyanyua juu mabega yake huku akibetua midomo. “Sijui!”

“Basi na mimi sikwambii ni la nani,” Sammy alisema huku akiendelea kutabasamu.

“Ayi jamani, kaka!” Winifrida alilalama huku akimtazama Sammy kwa shauku ya kutaka kusikia kuwa ni gari lake. Sammy na Pendo wakaanza kucheka.

Joyce alikuwa amesikia muungurumo wa gari lakini aliamua kusubiri kwanza huku akitaraji kuona wageni wakiingia ndani lakini hakuwaona bali alikuwa akisikia wanaongea na kucheka. Aliamua kuchungulia nje kupitia mlango wa barazani uliokuwa umefunguliwa nusu, akamuona Sammy akiwa amemshika Pendo na wakati huo Winifrida alikuwa ameketi kwenye siti ndani ya gari.

Joyce aliwatazama kwa mshangao mkubwa asijue kilichokuwa kikiendelea pale nje ya nyumba. Hata hivyo, hakutoka nje bali alirudi ndani na kuendelea na shughuli yake.

Sammy alimshika Pendo akamwongoza kuelekea ndani huku wakimwacha Winifrida anaendelea kulikagua lile gari kama aliyekuwa akilifanyia matengenezo. Kwanza alivuta droo iliyokuwa kwenye dashibodi na kuanza kuchakurachakura akitafuta kilichomfaa. Kisha alianza kuchunguza hapa na pale, na baadaye aliinama kuchungulia chini ya dashibodi.

Hakuridhika, aliinama zaidi na kusukuma siti ya abiria huku akitazama chini kabisa ya siti, akaona kadi ndogo itumikayo kuhifadhi kumbukumbu kwenye simu maarufu kama memory card (Micro SD) iliyokuwa imepachikwa kwa ustadi mkubwa chini ya ile siti ya abiria.

Winifrida aliitoa ile kadi huku akiitazama kwa udadisi zaidi, alikunja sura yake akijaribu kufikiria. Alidhani labda Sammy au mtu mwingine yeyote alikuwa ameidondosha, lakini akajiuliza mbona kama ilioneka kama imefichwa!

Muda huo huo Sammy alitoka nje huku akimwangalia kwa makini. Winifrida alimuona na kuificha ile kadi. Alifungua mlango wa gari na kushuka huku akicheka, kisha akaelekea ndani na kumwacha Sammy akimsindikiza kwa macho hadi alipoingia ndani.

Sammy aliachia tabasamu na kubetua mabega yake juu huku akitingisha kichwa chake taratibu. Hakujua nini kilichokuwa kinaendelea kwenye akili ya Winifrida. Alifunga milango ya gari vizuri na kurejea ndani.

* * * * *

Ilikuwa saa moja jioni, Mr. Oduya alikuwa amewaacha ndugu wawili; Madame Norah na Zainab wameketi kitandani wakiongea kwa furaha na kusimuliana masaibu waliyopitia kwa kila mmoja wao hadi kufika hapo. Kwa kweli ilikuwa ni jioni ya kusisimua sana kwa ndugu wale wawili.

Aliyeanza ni Zainab aliyemsimulia kila kitu Madame Norah pasipo kuacha kitu, alisimulia tangu makuzi yake baada ya Madame Norah kupata ujauzito na kutorokea kusikojulikana, masomo yake hadi kuajiriwa Kilimanjaro Hotel alikokutana na Hemed Kimaro.

Hakuacha kitu jinsi mgogoro katika ndoa yao ulivyoanza na hatimaye kuingia katika mtego wa Mr. Oduya na mauaji ya Hemed, kisha alilazimika kwenda uhamishoni Canada, alikoanza maisha mapya akiitwa Suzanne Ross.

Muda wote Madame Norah alikuwa akimsikiliza kwa makini, kuna wakati alisisimkwa mwili na kuna wakati alihuzunika, hata hivyo kubwa zaidi ilikuwa kumpata mdogo wake akiwa mzima wa afya.

Madame Norah naye alimsimulia Zainab maisha aliyopitia, tangu alipomtelekeza mtoto wake nyumbani kwa Rafael Jengo kule Ngamiani Tanga na kutorokea jijini Dar es Salaam, maisha aliyoyaishi jijini Dar es Salaam na jinsi jina la Madame Norah lilivyopatikana kabla hajakutana na Karl Johan aliyempeleka nchini Sweden alikokutana na Andreas Gunnar.

Masimulizi kuhusu maisha ya ndugu wale wawili yalikuwa mfano wa filamu mbili za kusisimua sana, kila mmoja alikuwa akisisimkwa kusikia mapito ya mwingine.

“Sikutegemea kabisa kukutana na wewe tena, nilijua umeshakufa dada’angu,” Zainab alimwambia Madame Norah huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani.

“Hapana mdogo wangu, Mungu ni mwema japo maisha yangu yamekuwa ya huzuni sana, hasa kwa kuwa mama alikufa kabla hajanisamehe na mtoto pia nimemkosa. Bora hata ya kwako,” Madame Norah alijibu huku akishusha pumzi ndefu.

“Hata hivyo, suala la wewe kuhusishwa na kifo cha mumeo kabla haijaripotiwa kuwa umetoweka ni moja ya mambo yaliyoniumiza kichwa na kunifanya niishi maisha ya huzuni miaka yote hii nikiwa sijui kama uko hai au umekufa, nilihuzunika kuwapoteza wote, wewe na mama,” Madame Norah aliongeza huku akimtazama Zainab kwa huzuni.

“Kwa kweli mdogo wangu umepitia mambo makubwa sana,” Madame Norah aliongeza akisema kwa sauti tulivu huku akiwa ameyatuliza macho yake kwenye uso wa Zainab.

“Sikufikii wewe, dada!” Zainab alisema huku akibetua mabega yake juu, na kuongeza, “Hivi una taarifa zozote za dada Zuena?”

“Zuena yupo Ghana, mambo yake si mabaya. Ameolewa na Dk. Aden Mafuru, Balozi wa Tanzania nchini Ghana,” Madame Norah alisema na kumfanya Zainab ashtuke.

“Huyo balozi ana uhusiano gani na huyu Mafuru, mwanasheria wa Mr. Oduya?” Zainab aliuliza kwa mshangao.

“Ni mapacha. Yule balozi ni mkubwa huyu mwanasheria ni mdogo,” Madame Norah alisema huku akijiweka sawa pale kitandani kisha akainua mkono wake kutazama saa yake ya mkononi.

“Kwa hiyo dada Zuena anaishi Ghana?” Zainab aliuliza tena kwa mshangao uliochanganyika na furaha.

Mambo yanazidi kunoga, tukutane tena kesho, hapa hapa ili kujua mwendelezo wa safari yetu ndefu ya kusisimua...
 
Taxi - (51)

Ilipoishia jana

“Kwa kweli mdogo wangu umepitia mambo makubwa sana,” Madame Norah aliongeza akisema kwa sauti tulivu huku akiwa ameyatuliza macho yake kwenye uso wa Zainab.

“Sikufikii wewe, dada!” Zainab alisema huku akibetua mabega yake juu, na kuongeza, “Hivi una taarifa zozote za dada Zuena?”

“Zuena yupo Ghana, mambo yake si mabaya. Ameolewa na Dk. Aden Mafuru, Balozi wa Tanzania nchini Ghana,” Madame Norah alisema na kumfanya Zainab ashtuke.

“Huyo balozi ana uhusiano gani na huyu Mafuru, mwanasheria wa Mr. Oduya?” Zainab aliuliza kwa mshangao.

“Ni mapacha. Yule balozi ni mkubwa huyu mwanasheria ni mdogo,” Madame Norah alisema huku akijiweka sawa pale kitandani kisha akainua mkono wake kutazama saa yake ya mkononi.

“Kwa hiyo dada Zuena anaishi Ghana?” Zainab aliuliza tena kwa mshangao uliochanganyika na furaha.

Sasa endelea...

“Ndiyo maana yake, ila yeye hakupata changamoto nyingi kama sisi. Baadaye nitampigia simu nimtaarifu jambo hili…” Madame Norah alikatishwa na simu yake ya mkononi iliyoanza kuita, aliitazama vizuri na kuguna, kisha alipokea na kuongea kwa kitambo kifupi.

“Nilisahau, nina kikao muhimu sana na wadau wangu wa mitindo, nitakutafuta kesho tuongee vizuri, mdogo wangu,” Madame alisema huku akiinuka, waliagana na Madame Norah akatoka.

* * * * *

Saa tatu na nusu usiku iliwakuta Sammy na Joyce wakiwa chumbani kwao, Sammy alikuwa amevaa bukta na singlet na kuketi kwenye pembe ya kitanda na Joyce alikuwa amevaa nguo ya kulalia na alijilaza chali huku akiegemeza kichwa chake kwenye mto laini.

Usiku ule Sammy alikuwa amedhamiria kumweleza ukweli Joyce, kama alivyokuwa ameshauriwa na Elli. Alikohoa kusafisha koo lake akijiandaa kusema jambo lakini alionekana kusita sana.

Joyce alimtupia jicho Sammy kwa makini na kuminya midomo yake. alijua kuwa lipo jambo lililomtatiza Sammy, hata hivyo, aliendelea kubaki kimya akisubiri kuona mwisho wake.

Sammy alikuwa anaangalia chini akionekana kuwaza kwa kitambo kirefu kisha aliinua uso wake kumtazama Joyce na kushusha pumzi ndefu za ndani kwa ndani.

“Mbona sasa hutaki kusema ulichotaka kuniambia!” Joyce alimuuliza Sammy baada ya kumwona muda mrefu akiwa kimya.

Sammy alishusha tena pumzi za ndani kwa ndani na kujisogeza karibu ya Joyce, alijiegemeza kwenye mto huku akimwangalia Joyce kwa makini zaidi. Alikohoa tena kusafisha koo lake.

“Amm…” Sammy alitaka kusema neno lakini alisita kidogo, alijikuta akipata wakati mgumu, mawazo yalianza kumjia, akajiuliza vipi kama Joyce angepokea taarifa tofauti na matarajio yake?

Alianza kupata wakati mgumu sana. Picha ya mtafaruku kati yake na Joyce ilianza kujengeka kichwani kwake, alihisi huenda mambo yangekuwa kama hivi:

“Unajua… nilikuwa nimekuficha ila ukweli ni kwamba nimefukuzwa kazi,” Sammy alimwambia Joyce kwa sauti tulivu.

Joyce alishtuka sana na kumkodolea macho Sammy.

“Sijakuelewa, hebu fafanua,” Joyce alisema huku akijiinua kutoka pale alipokuwa amelala na kuegemea ukuta huku akimtumbulia macho Sammy.

“Nimefukuzwa kazi takriban mwezi sasa, siku ile niliporudi nimelewa chakari ndiyo siku niliyokuwa nimepewa barua ya kuachishwa kazi, tangu wakati huo nipo tu kijiweni… na hili gari nimelinunua kwa fedha ya…” Sammy alijaribu kujieleza.

Stop!” Joyce alimkata kauli huku akiyatuliza macho yake usoni kwa Sammy, “Umefukuzwa kazi takriban mwezi sasa halafu unakuja kuniambia leo! Hivi wewe ni mume wa aina gani!” alisema kwa hasira na kunyanyuka, akasimama mbele ya Sammy huku akiwa kashika kiuno chake. Alimtazama Sammy kwa kitambo huku akiwa kachukia sana.

Sammy naye alisimama, akataka kusema neno lakini Joyce alimfanyia ishara ya kuwa hakutaka kabisa kumsikiliza.

“Uliamua kunificha, sasa kilichokutuma leo kunieleza ni nini?” Joyce alimuuliza Sammy huku akiendelea kumkazia macho kwa hasira.

“Lakini…” Sammy alitaka kujitetea lakini Joyce alimkata tena kauli.

“Sihitaji kusikia chochote kwa sasa, kama umeweza kuniaminisha siku zote kuwa unakwenda kazini na kumbe kazini ulikuwa huendi, unadhani nitaweza tena kukuamini!” Joyce alibwata kwa hasira. Sasa alikuwa anatokwa na machozi. Sammy alibaki kimya akimkodolea macho.

“Au unaye mtu unayemweleza matatizo yako? Ndiyo maana unaniona mimi mpumbavu, siyo?” Joyce aliuliza huku akilia kwa uchungu.

“Sioni kwa nini unapaniki kiasi hiki, hili ni suala la kukaa na kuongea, mke wangu. Sioni kama…” Sammy aliongea lakini Joyce alimkatisha.

How could you do this to me, Sammy, uh? Umekuwa ukiniaminisha kuwa unakwenda kazini kumbe huendi, nitakuamini vipi huko ulikokuwa unashinda?” Joyce aliuliza kwa hasira, alikuwa anapumua kwa nguvu.

“Kwa vyovyote ningekwambia, wewe ni mke wangu na ndiye mtu muhimu kwangu…”

Liar! Mimi nina umuhimu gani kwako?” Joyce aliuliza huku akimkazia macho Sammy.

“Swali gani hilo unauliza Joyce? You are my wife and you are important to me,” Sammy alijaribu kujitetea.

Save your breath, Sammy. I mean nothing to you.”

“Una hakika na hayo unayoyasema?” Sammy alimuuliza Joyce huku akimkazia macho.

“Ningekuwa na thamani kwako basi ungenithamini na kunieleza ukweli siku ile ile na usingefanya uamuzi wa kipumbavu kama ulivyofanya. Sikutegema kama…” Joyce alisema kwa hasira lakini sammy alimkatisha.

“Mama Pendo, naomba iwe mwanzo na mwisho kunitusi, sawa!” Sammy aliongea kwa hasira huku akinyoosha kidole chake kumwelekea Joyce.

“Huwezi kunizuia kuongea, Sammy, nitaongea chochote na hutanifanya kitu,” Joyce alifoka huku akimtazama Sammy kwa hasira. Hakuwa akimwita tena Baba Pendo bali Sammy.

Maneno yale ya Joyce yalionekana kumuumiza sana Sammy, alimsogelea Joyce na kumshika kwa nguvu, akamtingisha kwa hasira.

“Mama Pendo, nakupa onyo la mwisho, naomba tafadhali usithubutu kunijibu namna hiyo…”

“Usinitishe, kama umenichoka ni bora uniache kwa amani…” Joyce aliongea kwa sauti ya juu na kwa kujiamini.

Sammy alimshika shingoni kwa hasira, akamminya. “Nilikuoa kwa sababu nakupenda, kwa hiyo usijaribu kutaka kunitingisha, ukiendelea kutoniheshimu nitakuvunja shingo yako,” Sammy alisema kwa hasira na kutoka mle chumbani. Akaubamiza mlango.

Joyce alionekana kuogopa, ujasiri wote aliokuwa nao ulianza kutoweka, alijikuta akiogopa ghafla kwani hakuwahi kumwona Sammy akiwa amekasirika namna ile.

What a stupid husband,” Joyce alisema kwa sauti ndogo huku akijibwaga juu ya kitanda.

Inaendelea...

CC the_legend Norshad bobefu zoefu Pablo PAKAYA Ibney blackstarline Bryece Tater Bigjahman moneytalk marybaby nipo2 ram kisukari Smart911 Madame S carbamazepine Astelia culture gal Prisoner of hope Mine eyes kuku mweus Thad hearly Shunie moneytalk Tumosa Mine eyes Kudo swahiba92 ludist Toyota escudo Clkey macson3 boga la kiangazi LEGE Smart911 Richard irakunda skfull popie Krizy Beat hearly nipo2 MWINDAJI HARAMU kakhulu Katavi Norami mbududa iron2012 popie Bughy Harry Mlenge Kacheda mjasiliamali Laki Si Pesa cocochanel kinusikwetu big jambo mludego Shupavu Kacheda mjasiliamali Mweweso Songa Heri esiankiki
 
Taxi - (52)

Sammy alikwenda kuketi kwenye sofa sebuleni, mara akawaona Pendo na Winifrida wakimfuata pale kwenye sofa huku wakionesha wasiwasi mkubwa. Sammy alimkumbatia Pendo na wakati huo Winifrida aliketi kimya kwenye sofa huku akimtazama Sammy kwa makini.

“Joyce hajawahi kunidharau kama alivyofanya leo. Nlijua tu mambo kama haya lazima yatatokea ndiyo maana nilikuwa nasita kumweleza ukweli. Cha msingi hapa ni kukabiliana na chochote kitakachojitokeza,” Sammy aliwaza huku akiwa amefura kwa hasira.

Aliendelea kuketi pale akiwa amemkumbatia Pendo aliyekuwa akimtazama kwa makini pasipo kusema chochote. Sammy alikuwa bado ameduwaa, hakujua afanye nini.

Mara walimuona Joyce akitoka chumbani akiwa amevaa gauni na mkononi alikuwa anaburuza begi kubwa la magurudumu. Wote walimtazama kwa mshangao.

“Nashukuru kwa kunionesha kuwa mimi ni mtu nisiye na maana, narudi kwa wazazi wangu Tanga,” Joyce alisema na kuanza kupiga hatua zake taratibu kuelekea kwenye mlango mkubwa ili aondoke.

Sammy alionekana kuchanganyikiwa, aliinuka haraka na kujaribu kumshika Joyce katika hali ya kutaka kumzuia lakini Joyce alimsukuma kisha akamzaba kibao kikali cha shavuni. Alikuwa amekasirika sana na macho yake yalikuwa yanawaka kwa hasira.

“Niache niondoke. Siwezi kukuamini tena!” Joyce alisema kwa hasira.

“Ungenisikiliza kwanza basi…” Sammy alisema huku akimkodolea macho yaliyokuwa yakibembeleza.

“Muda huo sina, wapo watu wa muhimu kwako watakaokusikiliza siyo mimi!”

Pendo alianza kulia kwa uchungu huku akimshika mama yake miguuni kumzuia asiondoke. Winifrida alikuwa amesimama akiwaangalia wote kwa zamu, hakujua afanye nini. Alimshika Pendo aliyekuwa analia kwa uchungu na kumtoa eneo lile akitaka kumpeleka chumbani, japo Pendo alikuwa akirusharusha miguu akitaka aachwe.

“Mwache!” Joyce alisema kwa hasira na kumshika Pendo mkono huku akiwatazama Sammy na Winifrida kwa uchungu.

“Naondoka na mwanangu, siwezi kumwacha kwa mwanaume mwongo na laghai kama wewe,” Joyce alisema na kuanza kupiga hatua huku kamshika Pendo aliyekuwa bado analia. Walitoka nje wakimwacha Sammy amepigwa butwaa.

Sammy alitaka kusema neno lakini sauti haikutoka. Winifrida alisimama akimtazama Sammy kwa huzuni na kushusha pumzi, kisha alitingisha kichwa chake kwa huzuni na kuelekea chumbani kwake…

“Baba Pendo, mbona umenikodolea macho tu na husemi ulichotaka kunimbia, kwani kuna nini!” sauti ya Joyce ilimgutusha Sammy kutoka kwenye mawazo yake.

Sammy alimtazama Joyce na kushusha pumzi za ndani kwa ndani, alishukuru Mungu kuwa yalikuwa ni mawazo tu yaliyompeleka mbali sana kiasi cha kumwogopesha hata kumweleza Joyce alichokusudia kusema. Uso wake ulikuwa umefifia na alionekana kusita sana.

Joyce alimtazama kwa udadisi zaidi, akajiinua kutoka pale kitandani na kujiegemeza kwenye ukuta huku akiendelea kuyatuliza macho yake kwenye uso wa Sammy.

“Una nini, Baba Pendo, mbona unanitisha!” Joyce alisema huku akimeza mate kutowesha koo lake lililoanza kukauka.

Sammy alimtazama Joyce kwa makini na kushusha pumzi huku akilazimisha tabasamu, alionekana kusita sana. Picha aliyoiona mawazoni kwake iliendelea kumtisha, alihisi kuwa endapo angemweleza ukweli Joyce basi hali ingekuwa kama ambavyo picha ile ilionekana mawazoni mwake.

“Amm… amm… hakuna kitu!” Sammy alimudu kusema na kumfanya Joyce ashangae zaidi. Alimkodolea macho Sammy kama vile alikuwa ameona kiumbe cha ajabu kutoka sayari ya mbali.

“Hakuna kitu! Mbona sikuelewi? Ni nini kinachoendelea ambacho hutaki nikijue?” Joyce aliuliza huku akimtazama Sammy kwa udadisi.

Sammy alionekana kupata kigugumizi, aliangalia chini kwa kitambo kifupi akiwa hana cha kusema, aliogopa kumpoteza Joyce. Wakati huo Joyce aliendelea kumkazia macho Sammy kwa udadisi.

“Mimi ni mkeo, kama unanificha jambo unadhani ni nani wa muhimu kwako wa kumweleza? Halafu hadi sasa hujanieleza kuhusu hili gari ulilokuja nalo!” Joyce aliuliza na kumfanya Sammy ahisi kijasho chembamba kikimtoka, hata hivyo aliamua kuuvaa ujasiri. Aliachia tabasamu, akakohoa kusafisha koo lake.

“Nimeamini kweli unanijali mumeo, nilitaka kukupima nione… ukweli ni kwamba niliamua kukufanyia sapraizi…” Sammy alisema huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani.

“Sapraizi ya nini?” Joyce aliuliza huku akiendelea kuyatuliza macho yake kwenye uso wa Sammy akijaribu kuyapima yale maneno.

“Nimepandishwa cheo kuwa Naibu Meneja Mkuu, na hilo gari nimepewa, ni la kwangu. Ni la kwetu, Mama Pendo!” Sammy alisema huku akiachia tabasamu pana na kumfanya Joyce amtazame kwa kitambo bila kusema neno akiwa haamini alichokisikia.

Sammy alimtazama Joyce kwa wasiwasi hadi pale alipoliona tabasamu pana likichanua usoni kwake.

“Ooh… hongera sana mume wangu!” Joyce alisema kwa furaha huku akimkumbatia Sammy kwa nguvu

“Ni wewe unayestahili pongezi, mafanikio yangu yote yamechangiwa na wewe,” Sammy alisema huku akishusha pumzi za ahueni, hata hivyo, dhamiri yake ilikuwa inamsuta.

* * * * *

Saa tatu na nusu za usiku Mr. Oduya alitoka kwenye jengo lake la ghorofa kumi na mbili katika barabara ya Bagamoyo, Kijitonyama, jijini Dar es Salaam, baada ya kuwa na kikao kifupi na Balozi Aldolf Mageuzi.

Balozi Mageuzi alikuwa amefika ofisini kwa Mr. Oduya kwa mazungumzo mafupi ili kumpa mrejesho wa kile walichokubaliana walipokutana mara ya kwanza. Hakutaka kumweleza kwenye simu kwa kuogopa mawasiliano yao yangeweza kudukuliwa.

“Enhe, nipe mrejesho mheshimiwa Balozi,” Mr. Oduya alisema kwa shauku baada ya Balozi Mageuzi kuketi.

“Mambo siyo mabaya, mzee Fabian Magulu ameonesha kukuunga mkono katika harakati zako kutokana na jinsi unavyojitoa kukisaidia chama na jamii, hii ni habari njema na kama ujuavyo, huyu mzee ni mtu mwenye ushawishi mkubwa ndani ya chama na serikalini…” Balozi Mageuzi alisema na kumfanya Mr. Oduya aachie tabasamu pana.

Inaendelea...
 
Taxi - (53)

“Pia amesikitiswa sana na kitendo cha mheshimiwa Tumbo kuanza kampeni mapema huku akitumia siasa za majitaka kuchafua wengine. Kwa kutumia umaarufu na nguvu alizo nazo ndani ya chama amekwishaanza kukigawa chama, tumenasa mawasiliano ya simu akipanga mambo machafu dhidi ya wanasiasa anaodhani ni tishio kwake, jambo hili limemkasirisha sana mzee Magulu na anatarajia kupeleka maoni yake kwa Rais ili Tumbo aitwe Kamati Kuu na kujadiliwa. Hili peke yake linaweza kumpotezea sifa…”

Wow! Hahahaaaa… that’s good news! Hahahaaaaa,” Mr. Oduya alisema na kucheka kicheko kikubwa sana kwa furaha baada ya kusikia taarifa ile.

“Ila kuna jambo sijakueleza bado,” Balozi Mageuzi alisema baada ya kicheko kile kwisha, huku akimtazama Mr. Oduya kwa makini.

“Jambo gani tena Balozi?” Mr. Oduya aliuliza kwa pupa huku akionekana kushtuka kidogo, lile tabasamu pana usoni kwake liliyeyuka ghafla na badala yake alimkazia macho Balozi Mageuzi.

“Katika uchunguzi wangu nimegundua kwamba mzee Magulu ana imani kubwa na Dk. Hussein Abbas, na anampa nafasi ya kwanza wakati wewe amekuweka ya pili…” Balozi Mageuzi alisema kwa sauti tulivu.

Maneno yale yalikuwa kama msumali wa moto uliochoma moyo wa Mr. Oduya, alijikuta akiwa hana la kusema na kubaki kimya akimkodolea macho Balozi Mageuzi.

“Najua wewe ni mpambanaji… hili ni jambo dogo sana, kama mheshimiwa Tumbo mwenye mtandao mkubwa na tishio ndani ya chama anamalizwa kirahisi, kwa vyovyote vile Dk. Hussein Abbas ni kazi ndogo zaidi,” Balozi Mageuzi alisema huku akiachia tabasamu.

“Una uhakika, Balozi?” Mr. Oduya aliuliza huku sura yake ikionesha shaka kidogo.

“Naomba uniamini, ninao watu wa kusaidia kwenye hili, ni suala la muda tu na kila kitu kitakaa sawa.”

Oh, thank you, Mr. Ambassador, sijajua hadi sasa nikutunuku zawadi gani…” Mr. Oduya alisema huku matumaini yakirejea.

“Usijali, suala la kuvuka daraja tutalijadili tukishaufikia mto,” Balozi Mageuzi alisema huku akiinuka kutaka kuondoka, kisha kama aliyekumbuka jambo alimkabili tena Mr. Oduya.

“Jambo lingine, tafuta mtu ambaye ni mwanamkakati mzuri wa kiufundi na matukio, mkutanishe na mimi ili nimpe mbinu za kukuandalia mikakati na utekelezaji wa jinsi gani utafanikisha mambo yako,” Balozi Mageuzi alisema huku akimpa mikono wake Mr. Oduya, wakaagana wakiahidiana kupeana taarifa kila kunapotokea jambo jipya.

Kwa kweli ilikuwa ni habari njema kwa Mr. Oduya iliyomuongezea matumaini fulani. Mr. Oduya aliingia kwenye gari lake la kifahari aina ya Range Rover Velar la rangi nyeupe, Madjid Chege akaliondoa gari na safari ya kuelekea nyumbani kwake ikaanza.

Kauli ya kwamba atafute mwanamkakati mzuri wa kiufundi na matukio ilimfanya amfikirie Sammy, hakuona mtu mwingine mzuri zaidi ya Sammy.

Sasa alipanga kwenda ofisini kwa Dk. Masanja kesho yake asubuhi ili kumtaka amshawishi Sammy akubali kujiunga na timu yake, na kama angeendelea kukataa basi angetafuta njia nyingine ya kumlazimisha.

Kutoka pale ofisini kwake Kijitonyama waliifuata barabara ya Bagamoyo iliyokuwa na msongamano mkubwa wa magari, hivyo safari yao ilikuwa ya taratibu na muda huo ilikuwa inakaribia kabisa saa nne ya usiku.

Moyoni Mr. Oduya alikuwa ana amani ya kutosha sana kwani Balozi Mageuzi alikuwa ameusuuza sana moyo wake kwa habari mpya alizompa kuhusu uamuzi wa Fabian Magulu kumuunga mkono.

Hata hivyo, alijua kuwa akifika nyumbani tu ni lazima kungekuwa na kitimtim kwani alikuwa na takriban wiki nzima hajalala nyumbani kwake. Alimfahamu sana mke wake Dk. Oduya. Alikuwa mwanamke mwenye hasira za karibu sana na alikuwa radhi kufanya uamuzi wowote ule. Ilikuwa yataka moyo sana kuishi na mwanamke yule.

Madjid alipofika katika eneo la Tume ya Sayansi na Teknolojia aliingia kulia akaifuata barabara ya Rose Garden iliyokwenda kutokea eneo la Mikocheni kwa Mwalimu Nyerere. Barabara ile ilifunikwa na vivuli vya matawi makubwa ya miti kando yake.

Muda wote Mr. Oduya alikuwa amezama kwenye kutazama nje kupitia ukuta msafi wa kioo cha dirisha akiangalia mandhari ya ile barabara. Kupitia pale dirishani aliweza kuona mawingu mepesi yaliyokuwa yakijikusanya angani kana kwamba mvua ya rasharasha ilitaka kunyesha.

Walipofika mwisho wa barabara ile ya Rose Garden katika eneo la Mwalimu Nyerere, Madjid alikunja kona kuingia kushoto akaifuata barabara ya Mwai Kibaki akiwa katika mwendo wa wastani.

Waliyavuka majengo mazuri ya makazi ya viongozi wastaafu, maduka, supermarket, vituo vya kujazia mafuta, ofisi za binafsi na migahawa ya kisasa iliyopakana na barabara.

Baada ya safari fupi hatimaye wakaja kukutana na barabara ya CocaCola kwa upande wa kushoto. Barabara ya CocaCola ilikuwa ni barabara maarufu eneo lile na yenye msongamano mkubwa wa magari yaliyotoka na kwenda eneo la Mwenge yakipitia eneo la kiwanda cha soda za CocaCola.

Baada ya umbali mfupi walifika kwenye daraja, wakalivuka na mbele kidogo wakayavuka majengo ya Makao Makuu ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT Mlalakua) upande wao wa kushoto, hapo dereva akaongeza mwendo na kulipita lori la mafuta lililokuwa mbele yao.

Baada ya mwendo wa dakika kadhaa mbele yao wakalivuka jengo la kampuni ya teknolojia ya Infortech upande wao wa kulia halafu wakaufikia mzunguko wa barabara ulioziunganisha barabara za Mwai Kibaki na Old Bagamoyo.

Dereva akauvuka ule mzunguko na kuifuata barabara ya Mwai Kibaki iliyoelekea eneo la Mbezi Beach huku wakipishana na magari mengi ya kifahari katika barabara ile.

Baada ya safari ndefu katika barabara ile ya Mwai Kibaki wakayafikia makutano ya barabara ile za Mwai Kibaki na Ally Sykes, wakavuka na baadaye wakaikuta barabara ya Bahari kwa upande wao wa kulia. Dereva akaingia upande ule akiufuata ile barabara iliyopita katikati ya majumba ya kifahari yaliyozungukwa na kuta zenye ulinzi hadi alipokutana na barabara nyingine ya Ufukweni iliyoelekea kushoto, akakunja kuelekea kushoto akiifuata ile barabara.

Inaendelea...
 
Taxi - (54)

Baada ya mwendo wa dakika mbili wakaikuta barabara nyingine ya Hassan Oduya, iliyopewa jina kwa heshima ya bilionea Hassan Oduya iliyoingia upande wa kulia ikielekea ufukweni mwa Bahari ya Hindi kwenye majumba ya kifahari.

Ilikuwa barabara ya kisasa yenye lami na isiyokuwa na msongamano ikikatisha katikati ya yale majumba makubwa ya kisasa yenye ulinzi madhubuti. Kulikuwa na utulivu wa hali ya juu katika barabara ya Hassan Oduya na hata msongamano wa watu na magari haukuwepo.

Baada ya kitambo kifupi cha safari dereva alipunguza mwendo na hatimaye akasimama nje ya geti kubwa jeusi kwenye kasri la kifahari la Mr. Oduya, kisha akapiga honi mara mbili. Haukupita muda mrefu geti dogo lililokuwa kando ya lile geti kubwa likafunguliwa na askari mmoja wa kampuni binafsi ya ulinzi akachungulia.

Alipoliona gari la Mr. Oduya hakuuliza chochote, alifungua lile geti kubwa la mbele na Madjid akaingiza gari ndani ya uzio wa lile jumba na geti likafungwa nyuma yao, na hapo akajitokeza askari mwingine aliyeshika bunduki yake mikononi na kusimama kando akilitazama lile gari kwa makini.

Gari lilianza kupita katika barabara ya vitofali iliyopakana na bustani nzuri ya maua, miti ya kivuli na nyasi laini na kwenda kusimama mbele ya baraza pana ya jumba lile. Na hapo wale askari wa ulinzi wakarejea kwenye kibanda chao cha ulinzi mle ndani kando ya lile geti.

Madjid aliposimamisha gari, alifungua mlango na kushuka kutoka garini pasipo kuzima injini na kuzunguka upande alikokuwa amekaa Mr. Oduya. Alimfungulia mlango, na muda huo huo kijana wa kazi alitoka haraka ndani ya nyumba baada ya kusikia gari limesimama mbele ya nyumba na kumpokea Mr. Oduya kwa adabu zote.

Wakati huo ilikuwa kama majira ya saa tano kasoro dakika tano hivi. Hali ya jumba lile ilikuwa ya ukimya sana na ilitisha kweli kweli. Mr. Oduya aliingia na kupanda ngazi haraka haraka hadi ghorofa ya kwanza.

Alipoingia tu chumbani alimkuta mkewe Dk. Oduya akiwa amefura kwelikweli, alikuwa amesimama mlangoni huku akimsubiri kwa hamu.

“Haya niambie mwanaume wewe, wiki nzima ulikuwa unalala wapi na nani hadi leo ndiyo unarudi usiku wote huu?” Dk. Oduya aliuliza kwa sauti iliyoonesha wazi kuwa alikuwa amechukia kwelikweli.

“Sasa ndiyo maswali gani hayo, mke wangu? Inamaana hujui kuwa niko bize na mchakato wa kukutana na watu muhimu wa kunisapoti kuwania nafasi ya urais wa nchi hii?” Mr. Oduya alimjibu kwa swali.

“Mimi ni mke wako hivyo ninapaswa kujua ulikuwa unashinda na kulala wapi na ulikuwa na nani!”

“Hivi humu ndani nani ni mwanamume hasa? Mbona unazidi kunipanda kichwani wewe mwanamke?” Mr. Oduya alimjibu mkewe kwa fedhuli.

Okay! Kwa kuwa wewe ni mwanamume na mimi mwanamke ndiyo unaniletea dharau siyo?” Dk. Oduya aliongea kwa hasira, na kuongeza, “Kumbuka mimi si mtoto mdogo na wala si mpumbavu kama unavyofikiria, naelewa kila kitu kinachoendelea kwako.”

“Humu ndani mimi ndiye kichwa cha familia na ndiye ninayevaa suruali, kwa hiyo naomba unipe heshima yang...”

Mr. Oduya alikatishwa na kibao kikali cha ghafla ambacho hakukitegemea kabisa kilichotua kwenye shavu lake na kumpeleka sakafuni. Alishangaa sana, akajishika shavu lake akiwa haamini macho yake huku akimkodolea macho Dk. Oduya.

Hakupewa hata nafasi ya kutafakari, Dk. Oduya akaanza kumshushia makofi mfululizo yaliyopigwa pasipo mpangilio mwilini mwa Mr. Oduya huku akilia kwa uchungu. Aliporidhika alifungua mlango na kutoka nje ya kile chumba huku akimwacha Mr. Oduya akiugulia maumivu makali.

Hakurudi, alikwenda kulala kwenye chumba cha wageni katika ghorofa ya tatu na kujifungia humo hadi asubuhi.

* * * * *

Wiki mbili baadaye, majira ya saa tano asubuhi, katika eneo la Ilala Sharif Shamba, bibi mmoja mwenye umri wa miaka sitini na ushee alikuwa anatembea kwa kujikongoja akielekea katika uelekeo wa mgahawa wa kisasa wa Elli’s.

Yule bibi alikuwa nadhifu na mfupi mwenye ngozi ya rangi ya maji ya kunde na alikuwa amevaa vazi la kitenge lililoshonwa na kudariziwa vizuri na kilemba kikubwa kichwani. Mkononi alikuwa amebeba begi lake dogo na mfuko mdogo wa plastiki uliopigwa marufuku na serikali.

Alikuwa akiyakaza macho yake kutazama eneo la nje la maegesho ya magari mbele ya mgahawa wa Elli’s, eneo ambalo gari la Sammy aina ya Cadillac DeVille la rangi nyeupe lenye muundo wa kizamani lililokuwa na kibao chenye maandishi ya “Taxi” juu yake lilikuwa limeegeshwa.

Sammy alikuwa amesajili kampuni ya magari ya kukodisha (car rental), lakini kwa kuwa alikuwa na gari moja aliamua kulitumia kama teksi. Alikuwa amejiegemeza kwenye gari lake na alionekana mtanashati kwelikweli. Alivaa suti nzuri ya rangi ya kijivu, shati la rangi ya samawati na tai ya rangi ya bluu.

Yule bibi alizidi kusogea karibu huku akimkazia macho Sammy aliyekuwa kashika simu yake ya mkononi akionekana kuperuzi. “Hiyo ni teksi?” yule bibi aliuliza kwa shauku alipokuwa takriban mita ishirini kutoka lilipokuwa lile gari la Sammy.

“Ndiyo bibi, ni teksi,” Sammy alisema baada ya kugeuka na kumwona yule bibi akimtazama kwa makini.

“Niwekee kwenye gari,” yule bibi alisema huku akimwashiria Sammy amsaidie mzigo wake kuuweka kwenye gari.

Sammy alimfuata yule bibi akionekana kuchangamka, akapokea lile begi dogo na ule mfuko wa plastiki, akafungua mlango wa nyuma wa gari lake na kuviweka kwenye siti. Kisha alimshika mkono yule bibi kwa upole na kumsaidia kuingia ndani ya lile gari, akaketi kwenye siti ya nyuma. Yule bibi alimtazama Sammy kwa jicho la shukrani.

“Asante sana mjukuu wangu,” yule bibi alisema huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani.

“Usijali bibi… natakiwa kuwatendea wateja wangu kwa namna ambayo ningependa mama yangu atendewe,” Sammy alisema huku akifungua mlango wa dereva, akaingia na kuketi.

Mambo yanazidi kunoga... Usikose kufuatilia stori hii ya kusisimua kuijua safari ya Sammy aliyekuwa Meneja Matukio wa hoteli kubwa ya kitalii ya Udzungwa Beach Resort na sasa amekuwa Taxi Driver! Pia utajua kwa nini stori inaizungumzia taxi na si Sammy wala mtu mwingine, nini kimejificha nyuma ya taxi?
 
TV aina ya Sony ila story yako umeshindwa kutaja aina king'amuzi kama ni azam,dstv,gostv hata zuku? nk 😂😂😂
 

Similar Discussions

13 Reactions
Reply
Back
Top Bottom