Stori ya David Masha: Ajali iliyompa ulemavu wa kudumu, kukubali matokeo na kutokata tamaa

Pole sana mwanangu na hongera kwa kutokubali kushindwa. Maisha yana sura nyingi mojawapo ni hiyo ila kuna nyingine kama kumpata Jessica. Keep on fighting and cheers.
 
Dah speaking from the bottom of my heart hii story imenipa funzo kubwa sana. Pole sana bro kwa magumu uliyoyapitia but most of all hongera kwa hatua uliyofikia na MUNGU aendelee kukumiminia baraka zake Amen
🤝🤝
 
Nilianza kwa kusikitika na kuwaaza sana magumu uliyoyapitia mzee Dave, lkn mwishoni umenifurahisha na kunijenga kwa somo zuri. Hongereni sana wewe na familia yako.
Hakika ni stori yenye kubadilisha mtazamo.
 
Kama ningeweza kumshauri David, basi ningemshauri aandike kitabu cha maisha yake...

Kuna mengi ya kujifunza ambayo naona katika makala hii kayaandika nusu nusu...
 
Hii ni historia ya maisha aliyopitia David tangu 2007 alipopata changamoto na namna alivyopambana mpaka kufika alipofika leo hii. Stori hii David anasema ina nia ya kuwapa nguvu wote ambao leo hii wapo kitandani wanapambana na maumivu ya jeraha la uti wa mgongo na pengine wameshaanza kukata tamaa na ndugu zao pia kuumia mioyo yao. Anawataka warudishe imani.

View attachment 1778472
David "Mcharo" Masha

Imeandikwa na David Masha Mambea

Miaka 35 iliopita alizaliwa mtoto anaitwa Mcharo lakini baada ya kubatizwa na wazazi wake, akapewa jina David, huko Kilimanjaro kijiji cha Usangi.

Makuzi, shule ya msingi mpaka sekondari aliipatia huko kijijini kwao ambapo msingi alisoma shule moja inayoitwa Shule ya Msingi na Mazoezi Kivindu na kumaliza 1998.

View attachment 1778398
David (aliyemshika mbwa kichwani) akiwa kijijini kwao huko Usangi, Kilimanjaro

Wakati anamaliza, bahati mbaya au nzuri matokeo ya darasa la saba yalifutwa kwa baadhi ya wanafunzi akiwemo David na hii kumpelekea kutochaguliwa shule ya serikali kidato cha kwanza, ila wazazi wangu waliamua kunitafutia shule binafsi na kuanza kidato cha kwanza shule inayoitwa Lomwe High School.

Nikiwa shule ya msingi nilipendelea sana michezo, hasa mpira wa miguu. Na hata upande wa shule nikawa kidogo nazembea. Na hii ilikuwa inawapa shida sana wazazi wangu na mara kwa mara ilikuwa ni kesi kati yangu na wao.

Sasa baada ya kufanikiwa kuingia sekondari, wazazi hawakutaka nisome kama day scholar. Waliamua niende boarding ili niwe na muda mwingi wa kusoma na kuwa katika uangalizi mzuri. Maisha ya boarding kiukweli wengi mnafahamu; changamoto ni nyingi lakini niliweza kuyamudu na kufanikiwa kumaliza Form 4 mwaka 2002.

View attachment 1780367
David akiwa Form 5, Lomwe High School, 2003

Kipindi nipo sekondari sikuacha kucheza mpira maana ulikuwa damuni na hata wakati namaliza nilipewa cheti cha mwanamichezo bora. Basi bwana, baada ya kumaliza Form 4 matokeo yangu yalikuwa mazuri na hata kuchaguliwa kwenda A Level Tambaza High school, ila baba akanigomea kwenda mjini na kuamua niendelee hapo hapo maana alihisi mjini labda ningeharibikiwa na nisingesoma.

Shule ikaendelea hapo mpaka nilipofanikiwa kumaliza A Level mwaka 2005.

SAFARI YA MASOMO CHUO CHA WANYAMAPORI MWEKA
Wakati nimemaliza sasa A Level 2005 nikaanza mchakato wa kutafuta vyuo binafsi. Nilipenda sana kusomea WILDLIFE. Na hii nilipenda kwasababu nilivutiwa na kaka yangu ambaye kwa sasa ni marehemu. Yeye alikuwa kwenye hio field na niliona alivyofanikiwa mapema sana kimaisha.

Kuna kipindi nilivyomaliza Form 4 ule muda ambao tunasubiri matokeo, nilienda kwake Arusha kukaa naye na familia yake nikaona namna alivyofanikiwa hivyo na mimi nikapenda sana.

Wakati natafuta chuo, baba alitaka sana nisomee Sheria ila mimi sikutaka. Yani focus yangu ilikuwa ni porini na wazungu tu. Nikaenda Dar kwa ajili ya matriculation ambayo tuliifanya UDSM miaka hiyo ya 2005, bahati mbaya au nzuri sikupata nafasi. Sasa usiku nikapokea simu kutoka kwa baba akaniambia, "Wewe si unataka wildlife, kuna chuo kipo Moshi kinaitwa Mweka Wildlife. Kwahiyo kesho panda basi hadi Moshi ukakitafute"

Basi nikafanya hivo na kweli nilikipata na nilifurahi sana kwasababu kwanza vhuo ni bab'kubwa kimazingira na kila kitu na hasa viwanja vya mpira na vifaa vyake. Basi nikapewa utaratibu nikaambiwa muhula utaanza Agosti na mimi hapo nilifika Julai mwishoni hivi. Nikaomba nisome short course ya mwezi ili kusubiri Agosti. Ikawa hivyo ikafika Agosti nikaanza rasmi Diploma ya Wildlife.

View attachment 1780391
Enzi za kabumbu Chuo cha Wanyamapori - Mweka, 2006

Kiukweli nilikuwa na-enjoy sana masomo. Nilipata marafiki wazuri sana ambao mpaka leo tunawasiliana. Wakati niko hapo 2007 mwanzoni nilipata fursa moja hivi kwasababu ya mpira. Siku moja tulialikwa kucheza mpira KCMC. Baada ya pale alinifuata jamaa mmoja hivi akaniomba namba za simu, kesho yake alinipigia na kuja chuo tukaonana na akaniomba anipeleke timu ya AFC Arusha nikamwambia sasa niko na ratiba ya masomo. Akaniambia kila weekend niwe naenda Arusha kufanya mazoezi nao. Basi nikamwelewa akawa kila weekend ananitumia nauli na posho naenda Arusha nikiwa na nafasi. Basi maisha yakawa yanaendelea. Mungu ni mwema.

View attachment 1778476
David (wa pili kutoka kulia, waliosimama) akiwa na wanakikosi wenzake Chuo cha Mweka, 2006

SIKU ILIYOBADILISHA MAISHA YANGU
Sasa bwana, tarehe 31 Agosti, 2007 siku ya Ijumaa kwenye mida ya saa kumi hivi jioni, hii siku ndiyo kila kitu kilibadilika katika maisha yangu. Hii siku sitokuja kuisahau maishani mwangu. Hata ndugu, familia na marafiki hawataisahau hii siku.

Siku hii ya Ijumaa kulikucha vizuri tu na nikahudhuria vipindi vyangu kama kawaida darasani na mchana wake kulikuwa na Test nikajiandaa nikaenda kufanya vizuri tu. Sasa baada ya kumaliza, nikapokea simu kutoka kwa ndugu yangu akiniomba tukutane mjini na yeye anatokea Arusha. Si unajua mambo ya weekend bana?

Basi mimi nikatoka darasani nikajiandaa 'bling bling' nikawa nipo sasa nasubiri usafiri nishuke mjini. Kule chuoni huwa kuna daladala chache za kusubiria. Basi wakati nasubiri, akaja rafiki yangu mmoja akaniuliza: "Vipi man, leo hatupigi tizi?" (yani mazoezi uwanjani) Nikamjibu: "Nina ki-date mjini" Kimasihara akanitukana kisha akasema twende uwanjani halafu baadae nitakuitia taxi ije ikuchukue, mimi nikamkatalia.

Akaja mwingine akaniambia kiutani: "Dogo, wakati unasubiri gari twende ukapate moja moto moja baridi" Nikacheka nikamjibu, "Nazifuata mjini" na yeye akanitukana.

Baada ya dakika chache ikaja Hiace imejaa sana. Kuna wadada nilikuwa nao wakaniambia, "Dave, tupande" Nikawajibu kimasihara, "Nipande nichafuke? Gari imejaa hivyo, siwezi"

Basi wao wakapanda. Sasa mbele yangu kulikua na gari Pickup imepaki. Nikaisogelea nikauliza gari inaenda mjini nikajibiwa ndio. Dereva yupo wapi, nikaoneshwa mshikaji mmoja hivi alikuwa ni mwanafunzi pia akaniambia panda twende anamsubiri mwenzake, basi mimi nikapanda. Akatokea mwalimu wangu akaniuliza: "Wewe leo hufanyi mazoezi?" Nikamjibu, "Hapana, nawahi mjini" Akasema, "Nenda mazoezini, ukimaliza mimi nitakupeleka mjini kwa gari yangu" Nikamkatalia na akanionya kwa non-verbal kuwa dereva amelewa, shuka usiende. Mimi nikajikuta napuuzia.

Basi jamaa akawasha gari tukaanza safari. Nakumbuka alikua spidi sana halafu ni mteremko. Kuna sehemu kuna kona kali nikawa naangalia nikipiga hesabu naona kabisa hapigi kona bali anaenda kugonga; mbele kulikuwa na nguzo mbili za umeme na mtaro. Nilichofanya niligonga dirisha lake dereva na kumwambia, "Angalia mbele kuna kona". Nadhani alistuka na kukata kona kwa nguvu, lile gari likageuka tulikotoka na kutumwaga na mimi nikajirusha, kumbe sikuwa najiokoa. Baada ya dakika chache nastuka nimelala chini niliokuwa nao kwenye gari ndio nawaona na wengine wananipa pole.

Kumbukumbu zikanijia zote za tukio lilivyotokea. Basi nikasema ngoja nikae ili nisimame, daaaah nilipata maumivu makali sana kwenye sehem ya shingo na hapohapo nikawa naishiwa pumzi napumua kwa tabu sana. Nikaingiwa uoga mwili ukawa umekufa ganzi kabisa nikawa sielewi mikono ikakosa nguvu nikijaribu kuinyanyua siwezi kabisa. Wale wenzangu wakaniambia "Dave, tulia umeumia". Nikajitahidi kunyanyua mkono wa kushoto kushika maana nilikuwa nasikia maumivu kichwani nikapagusa hapo palipokuwa panauma nikaangalia nikaona damu, nikaogopa sana nikajua nimepasuka kichwa; nikawa mpole kimoyomoyo nikajisemea "Dave nimeumia".

Basi, kuna ile gari iliokuwa imejaza sana ilipofika sehemu tupo ikashusha abiria ili inibebe mimi kuniwahisha hospitali. Sasa wakati wananinyanyua, nilikuwa nasikia maumivu mno shingoni nakosa pumzi mwili unakufa ganzi. Zaidi ikawa hata sijui mguu wa kushoto upo wapi au wa kulia, basi nikapandishwa gari ikanishusha mpaka KCMC.

HOSPITALI KCMC
Kulikuwa na baadhi wa wanachuo walishuka na mimi wakachukua simu kupiga kwa ndugu zangu kuwapa taarifa. Nilipofika KCMC nikaingizwa emergency room. Nakumbuka walinichana nguo zangu wakanifunika na shuka then wakanitoa wakanipeleka wodini nikawa nasikia: "Vyumba vimejaa, akae hapa kwenye korido" Hapo niko kwenye stretcher.

Basi, usiku baadaye wakaja madaktari watatu. Mmoja raia wa kizungu na wa pili Mchina; mwingine Mwafrika, wakanipa pole kisha wakaniambia nifunge macho kisha kuna ring moja ya chuma wakanivisha kichwani kisha wakaikaza kwa kutumia screw wakamaliza halafu wakaweka mawe huko nyuma yamening'inia ili kusaidia shingo inyooke isilete madhara zaidi. Usiku ukapita asubuhi kukakucha baba na mama na ndugu wengine wakaja kunitazama. Moyoni na akilini mwangu nilikuwa nawaza vitu vingi sana, yani nilikuwa nahisi it's over, ujanja kwisha!

Hapo ndipo maisha yangu yalianza kubadilika; nikawa naona giza mbele. Baba na Mama waliumizwa sana mioyo yao, ndugu hivyo hivyo.

KUHAMISHIWA MUHIMBILI
Baada ya kukaa KCMC kama wiki 1 hadi 2, familia yangu iliamua nihamishiwe Dar hospitali ya Muhimbili. Nakumbuka nilipelekwa na gari ya wagonjwa hadi KIA; ndio mara ya kwanza kupanda ndege, lakini sasa niliipanda kwa style hio. Siku-enjoy kiukweli. Nikafika Dar nikapokewa na ndugu zangu nikapandishwa kwa gari wa wagonjwa hadi Muhimbili Wodi ya Sewa Haji nafikiri, au ile nyingine.

Sio utani, nilikua naogopa sana. Hofu imenikaa nikatafutiwa kitanda nikalazwa. Daah, nyie hospitali sio mahali pa kupazoea wala kukaa. Yaani wewe kama ni mzima mshukuru sana Mungu wako. Nilikua naona watu wanavyoumwa pale, inasikitisha. Binadamu ule uthamani wetu ukifika hospitali haupo. Mimi nawashangaa sana binadamu wanaoringa; wenye majivuno na kujisikia. Laiti wangejua! Ila wacha niwaambie leo. Kama unaringa, acha! Kama una kiburi, acha! Kama unajisikia, acha! Kwasababu iko siku...

Basi nikakaa pale wodini. Sasa kwasababu ya ile hofu, wagonjwa ni wengi sielewi, ilibidi niwe namuomba nurse awe anakaa jirani na mimi usiku kama mlinzi, na yule nurse alinielewa sana. Mungu ambariki huko aliko. Baada ya kukaa kama wiki hivi nikahamishiwa wodi ya MOI.

CHANGAMOTO KUU ZILIZONIKABILI

(i) Changamoto ya Kisaikolojia
Unajua unapopata hiLi tatizo la Uti wa mgongo, kuna changamoto kama tatu hivi zinatokea tu automatically (1)Kiafya kuna mambo yanatokea (2)Changamoto ya kimahusiano (3)Familia wanawaza nini kifanyike hapo, hasa suala la uchumi ili kumtibu mtu.

Tuanze na changamoto Ya kiafya inayotokea. Ni hivi; ukiumia uti wa mgongo kwa kesi kama yangu (C6, C7) kwanza unapooza. Ukishapooza ina maana mikono miguu haifanyi kazi. Pia kupata haja ndogo na kubwa kwa kawaida ni tatizo, haviwezekani. Kinachofanyika wanakuwekea mpira wa mkojo, lakini pia unavalishwa pampers kwa ajili ya haja kubwa na ikitokea hata hujui wala kuhisi, yani hiki kipindi kiliniharibu akili. Nilikuwa sijiamini kabisa (self-esteem yangu ilikua chini). Sikuwa na ujanja. Nilikua mtu wa hasira sana. Kila kitu nahisi kama naonewa.

Basi ikaenda hivo nikakaa MOI mpaka niliitwa Balozi kwasababu nilikaa muda mrefu. Nakumbuka hata kuona nje sikuwahi; mimi ni ndani tu. Akija mgonjwa atatibiwa ataondoka mimi nipo. Ilinivuruga sana. Psychologically I was not okay kabisa. Kuna siku walikuja darasa langu la Mweka walitokea hunting Selous Game Reserve ndio nikaomba wanitoe nje kwenye korido ili niweze kuwasalimu. Nilifurahi sana hio siku na nilibahatika hata kuona jua nje na kupata fresh air.

Kuna wakati mwili ulikuwa unawaka moto sana nikaomba niwe nawashiwa AC mpaka mwisho yani ukija chumba nilichokuwepo unaweza kuhisi ni chumba cha maiti kwasababu ya baridi. Niliambiwa huo moto ni ganzi inaachia taratibu. Nakumbuka daktari alisema kwa injury yangu kulikuwa hakuna ulazima sana wa kwenda nje kutibiwa bali mazoezi na kujipa muda itapona. Basi nikaliamini hilo.

KURUDI KUUGULIA NYUMBANI
Tukapata ruhusa tukarudi nyumbani ndipo dada angu kipenzi anaitwa Idda na familia yake wakachukua jukumu la kunilea na kunitunza nyumbani kwake. Kumbuka natoka MOI bado hali yangu ni mbaya; yaani kukaa bado mimi ni kulala tu 24/7 natumia hio mipira ya mkojo natumia pampers na bahati mbaya nilipata vidonda (bed sore). Hivi vidonda ni vibaya, vinatisha. Vilinichimba sehemu za makalio na kwenye mapaja kwahio tukawa tunatibu vidonda na hio hali ya kupooza mwili.

Tumehangaika sio siri kutafuta tiba zote dunia hii. Naambiwa: "Dave, huwezi jua uponyaji wako upo wapi" Basi kila ukiambiwa sehemu fulani ipo dawa, basi dada yangu na mumewe wanaitafuta napewa. Kiukweli ilifika kipindi nilikata tamaa kabisa na hii ni baada ya mwaka unaofuata kumpoteza dada yangu kwa ajali ya gari huko Uganda na mwaka huo huo kumpoteza baba yangu. Niliumia sana na kupoteza matumaini ya kuishi. Hamu ya kula haikuwepo; yaani nakumbuka nilikuwa nakula ugali maziwa mgando na soda basi. Vingine havipandi, najitahidi lakini wapi!

Kwenye msiba wa baba sikuruhusiwa kusafiri umbali mrefu ila nililazimisha kwenda kumzika baba kijijini, nikasema potelea mbali. Lakini nilifika salama nikamzika baba nikarudi Dar kuendelea na mapambano.

MAPAMBANO YA KUKUBALI HALI HALISI
Baada ya kurudi Dar kiukweli nilipoteza tumaini sikuona mbele yangu kiufupi nilikata tamaa, japo dada yangu na familia yake hawakuchoka waliendelea kunihudumia. Walipambana huku na kule ili mimi niweze kupona. Tulitumia tiba zote unazozijua wewe. Niliombewa na watumishi mbalimbali wenye majina na wasio na majina. Dini zote nilipita kuombewa.

Kipindi hiki hata marafiki nilikua nawakwepa wengine kuja kuniona nilikua sijiamini najiuliza: ''Sasa akija rafiki yangu yoyote na akiniona na huu mpira wa mkojo au akijua nimevaa pampers itakuaje?''

Nilikuwa najisikia vibaya sana. Nilikonda mno kwasababu kwanza nilikuwa sili chakula, sina hamu ya kula; maumivu ya vidonda (bed sores); sindano nilizokuwa nachomwa (powersafe) mpaka nilikuwa namchukia mchomaji (dada yangu mmoja hivi ni nurse Muhimbili). Sema kwa sasa namshukuru maana alinipa huduma ya kipekee. Usiku kuamka kunigeuza nilale ubavu au na mgongo.

Basi 2008 ikapitaa yote ni kupambana tu unakutana na huyu anakwambia lake ili tu akusaidie basi unaamua kulipokea. Kiukweli maneno ya ushauri wa watu yalikuwa ni mengi lakini hayakunisaidia kwasababu moja kubwa SIKUIKUBALI HALI NA NILISHAKATA TAMAA kwahiyo ikawa ni kama sikio la kufa.

Sasa 2009 siku hiyo tu kumekucha nikakutana na ndugu mmoja. Sikuwa namjua hata. Alikuja tu akashinda na mimi siku nzima tunaongea tu na story za hapa na pale akaongea vitu vingi sana vya kimaisha. Alikuwa mtumishi nadhani, mwanamke, kumbe mimi bila kujua alikuwa kazini ananifanyia Pyschosocial Support (PSS). Alikuja kama mara 3 hivi nyumbani. Asubuhi anaondoka jioni. Ile session ilinisaidia; alinipa munkari wa kuendelea kuishi na nikajiona nina nafasi nyingine Mungu amenipa. Ndipo nilipoanza kuikubali hali yangu nikasema kama ni kupotea msituni nishapotea kwahiyo nikubali nimepotea nianze kutafuta namna ya kutoka msituni na nilikumbuka maneno ya Baba siku moja aliniambia: "Unatakiwa uamke hapo; mama yako ndiyo anakutegemea mtoto wa kiume. Mimi sitokuwepo duniani muda wote"

Na ninakumbuka alinipa dawa ya kuleta hamu ya kula inaitwa Phamactin. Hii dawa ilinisaidia sana mpaka leo huwa nawashauri watu watumie kwa nilivyokuwa na imani nayo.

KUKUBALIANA NA HALI HALISI
Nikaanza kuikubali hali yangu nikawa nafanya mazoezi kwa nguvu. Nakumbuka kuna watu wawili dada aliwaleta hawa watu walikua spesho kwa ajili ya kuchua mwili. Aisee walikuwa wanachua mwili na dawa zao yani wakimaliza uko hoi ila ilikuwa inasaidia kurudisha uhai wa mishipa ya damu. Walikuwa wakinisimamisha huku wanachua nilikuwa mpaka nazimia baada ya dakika kadhaa naamka.

Basi ikawa huku kuchua huku maombi na mazoezi halafu nikaanza kawakaribisha marafiki nyumbani. Nakumbuka dada alininunulia simu ili nijiunge na Facebook kipindi hicho ndio habari ya mjini. Nikajiunga nikaanza ku-interact na walimwengu. Ilinisaidia pia nilikutana na ndugu huko na marafiki. Mazoezi yakakolea nikatoa mpira wa mkojo nikaanza kujifunza kubana mkojo japo haikuwa rahisi nikaacha kuvaa pampers nikawa nikisikia haja napelekwa chooni.

View attachment 1778427
David akiwa amekalia wheelchair miaka mingi baada ya ajali iliyobadili maisha yake

Appetite ilirudi kusoma 100%, nikauliza: "Je, pombe naruhusiwa?" Nikaambiwa subiri umalize dozi ya sindano. Kujikubali kukawa ndio nguzo ya mimi kuona mabadiliko. Nikaanza hata kutoka kwenda nje hadi saa nyingine marafiki wanakuja wananichukua tunaenda beach kidogo au hata live band; yaani basi tu ni-interact na walimwengu nijione na mimi nipo. Ilinisaidia sana.

Ile hali ya kuzimia ikaisha baada ya kupigishwa nyungu za kutosha tena za mavi ya tembo na mazagazaga mengine. Nilikuwa nazurura jamani; sema hapo bado vidonda havijapona vizuri. Nakumbuka hadi kwa Babu wa Loliondo nilifika kutafuta uponyaji wangu. Sasa kuna siku nikaenda CCBRT kutafuta daktari wa mazoezi nikakutana na mzungu mmoja. Alivyonichunguza akaniambia hatuwezi kufanya mazoezi huku una vidonda utaumia na hivi vidonda vitaweza leta infection na vitakuua. Akanishauri nikulaze kesho asubuhi nikufanyie surgery tuvifunge nikakubali na nikawataarifu ndugu zangu.

Basi vikafungwa. Ila sasa nililala miezi 2 kasoro kwa tumbo tu nakula kwa style hiyo, yani ilikuwa ni shidaa sana kwa kweli ila nilipona nikarudi mazoezini na mitikasi mingine ikaendelea, furaha ikarudi tena. Sikumwacha Mungu wangu. Maisha yalinibadilisha ila ikafika point nikayabadili maisha na kuji-adapt na hali halisi. Kipindi hiki niwashukuru watu wafuatao: Dada Idda na familia yake, Doris, Anna, Mama na wale wote marafiki zangu hamkunichoka.

(ii) Changamoto ya Kimahusiano
Baada ya kuongelea changamoto hio ya kwanza ya kiafya sasa changamoto nyingine ilikuwa ni ya kimahusiano. Haha! Hapa najua wengii mnataka kujua "Eheee! Ikawaje?"

Kabla na baada ya Ajali nisingependa niongelee sana hii part ila mahusiano yalikuwa kiukweli ni HOVYO. Wapare wanasema, HORRIBLE and TERRIBLE!! Someone atakuwa hapo just for feeling pity lakini hata kwa upande wangu nilikuwa na makosa kama binadamu. Lakini zaidi, hali niliokuwa nikipitia nilikuwa najistukia; nahisi kama muda wote nadanganywa japo kuna muda Mungu alikuwa ananionesha ikitokea nadanganywa.

Binafsi nilipitia mahusiano; mengine nilipenda kweli na hata kunigharimu muda na hata pesa na mahusiano mengine hivyo hivyo tu ilimradi (just triping myself). Lakini nawashukuru sana mliowahi kupita katika maisha yangu maana mmenifikisha hapa na kumpata MKE wangu Jesca ambaye Mungu aliniandalia wa Maisha. Asante Jesca kwa Kunipenda!

(iii) Changamoto ya Kiuchumi
Changamoto nyingine ya tatu ilikuwa ni uchumi kwa maana kwamba unapokuwa kwenye hali hii matibabu yake ni gharama mno. Ninyi nyote ni mashahidi. Labda unatakiwa uende nje ya nchi na ukiangalia hali ya uchumi wa familia ni mbaya unashindwa. Najua wapo wenzangu huko hata kwenda tu mazoezi wanashindwa kwasababu ya pesa, wanaohitaji labda wheelchair wanakosa. Wanaohitaji labda dawa na vifaa tiba lakini kwasababu ya pesa wanashindwa. Mimi binafsi mpaka leo kuna vitu natamani niwe navyo lakini ndio hivyo ukiangalia gharama zake siziwezi; basi unaamua kuji-adapt tu na hali halisi. Kikubwa pumzi.

======
Basi niwaombe wale wote wanaopigania afya zao msichoke; ipo siku mtatoboa, mtaamka hapo kitandani. Lakini pia, niwaombe ndugu zenu na wapendwa wenu; msiwachoke wapendeni simameni nao kwa kuwa mnapata thawabu kwa Mungu bila ninyi kujua. Mungu awabariki sana!
======


BIASHARA, KURUDI MASOMONI NA CHANGAMOTO ZAKE
Baada ya kuikubali hali yangu na kuona maisha acha yaendelee, nikajiuliza kwahiyo nini kinafuata. Nikapata wazo la kufungua biashara ili nisikae tu nyumbani lakini pia nipate hela ya mahitaji yangu madogo madogo kila siku. Nikawa na idea ya biashara kuuza nguo mtumba za kike grade one. Mtaji bahati nzuri chuo nilichokuwa nasoma walinipa nusu ada ambayo kimsingi sikuitumia lakin pia nilikuwa na hela ambayo nilikuwa naiweka mfano akija ndugu au rafiki kunipa pole akinipa hela nikawa natunza.

Lakini pia, nilipata hela kwa kaka mkubwa basi nikatafuta frame maeneo ya nyumbani Kimara nikailipia nikaierebisha ikawa sawa nikafuata mzigo nakumbuka Ilala Sokoni asubuhi sana. Nilichukua taxi hadi huko. Hii ilikuwa mwaka 2012. Nikafanikiwa kupata nguo nikarudi nyumbani nikaziandaa nikaziweka dukani nikaanza biashara. Hii ilinisaidia kutokukaa tu nyumbani lakini pia kutengeneza network na watu wapita njia na hasa ku-socialize.

Nilifanya hiyo biashara almost mwaka mzima ndipo nikatamani kurudi tena chuo kusoma maana nilikuwa naona bado elimu yangu haitoshi na niliamini kwa hali yangu hii ili niheshimike na nitoke kimaisha lazima niwe na vitu flani moja ELIMU kisha PESA itafuata.

Basi nikamshirikisha dada yangu then na ndugu baadhi na kuanza kutafuta chuo bahati nzuri ni kapata Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na nikaomba nafasi nikapata mwaka 2013 kusomea Sociology.

View attachment 1780385
David akiwa UDSM, 2014

Ile biashara niliamua kuifunga ili focus kubwa iwe shule. Sasa kuna maisha ya chuo baada ya kuanza na changamoto zake na namna nilivyopambana hadi kumaliza; haikuwa kitu rahisi kabisa but it's very interesting hapa ndipo niliuona Ukuu wa MUNGU na nikaamini zaidi kweli Mungu yupo ukimwita Atakuitika.

Wakati napewa barua ya admission nilifurahi sana ila nikawa nawaza moyoni ntaweza kweli kwasababu moja nikiwaza miundombinu ya chuo ilivyo. Kwanza chuo kikubwa kwa wanaoijua UDSM unaweza kupata picha halisi. Mfano una kipindi Yombo 4 kikiisha unatakiwa uwahi kipindi COET. Ufike bado unakuta darasa liko juu gorofa ya 4 na hamna lift. Imagine utafanyaje hapo ndio mgeni hujuani na mtu yoyote yani wala huna mazoea na mtu. Sasa mimi nilichofanya nikuanzisha mazoea na wanadarasa haraka sana na hii ilinisaidia kutengeneza marafiki na wakajua nini nahitaji kwahio wakawa wananipa kampani kunisukuma kutoka pointi moja kwenda nyingine kama ni darasani au kwenda canteen.

Nakumbuka nilikuwa nilikuwa na kipindi COET juu gorofa ya 3 hivi au 4 basi wanadarasa wakawa wananinyanyua kutoka chini mpaka juu kipindi kikiisha wananibeba tunashuka hadi chini. Nawashukuru sana sana lile darasa. Miezi ya mwanzoni kiukweli nili-hustle kuna muda ikawa vipindi vingine sihudhurii vya usiku naamua kurudi zangu nyumbani tu ila kesho yake lazima nipate desa nisome na nielekezwe na wenzangu.

Sasa siku zinavyozidi kwenda nikaanza kuzoea zoea mazingira siku moja nikakutanishwa na kitengo flani hivi kinacho-deal na watu wenye changamoto za ulemavu chuoni nikasajiliwa na nikawasilisha mapendekezo yangu nini nahitaji ili maisha yawe mepesi kwangu chuoni. Tukaanza na swala la vipindi vyote madarasa yawe ni ya chini hili likafanikiwa, pili kutafutwe bajaji mpya kwa ajili ya kutuchukua hostel kutupeleka madarasani na kuturudisha hostel na hata maeneo mengine tukihitaji. Hili lilifanikiwa japo kwa kuchelewa.

View attachment 1778412
David akijisomea wakati akiwa chuoni UDSM
Njia tunazopita hasa maofisini kuwekwe pavement ili kupita wheelchair hii pia ilifanikiwa lakini pia niliomba lift moja ya jengo la ofisi za wahadhiri wa course yangu itengenezwe hili pia lilifanikiwa. Naushukuru sana uongozi wa UDSM kwa kipindi kile.

Pia, wakati napewa hostel, chumba niliambiwa na Dean kuwa naweza kuishi na mtu msaidizi wangu kutoka nyumbani au nitafute mwanafunzi mwenzangu (wa kiume) ambae atajitolea kuishi na mimi chumba kimoja na kusaidiana ili niwe naishi chuo na kuacha kuwa narudi nyumbani. Basi walinipa chumba lakini ilinichukua muda kuhamia.

Baadae nikakutana na vijana wawili hivi, dah kama bahati kwangu wao walikuwa wanaishi Mabibo Hostel nikawaomba kwakuwa tayari walikuwa marafiki zangu kuwa mnaonaje tukiishi wote hostel chuo mkanipa sapoti na huku tukiendelea kusoma pamoja kwakuwa pia tulikuwa darasa moja? Walinielewa na tukakubaliana tukae wote (Niwashukuru sana Imma & Nasoro) Mungu awabariki huko mlipo, muendelee kuwa na moyo huo huo.

View attachment 1778415
David akiwa na marafikize enzi akiwa masomoni UDSM
Basi nikahamia rasmi chuo na kazi ikawa moja tu kusoma kusoma kusoma. Ulikuwa Hall 7 chumba namba 103 ground floor. Haha shule ilipigwa pale. Kwanza huyo Imma ndio CR wetu huyo Nasoro sasa ndio shule ilikuwa ipo hapo. Mimi binafsi siwezi kujiongelea. Niliosoma nao watasema wenyewe. Tuliishi kama mapacha watatu; tulipendana sana!

Mwaka 2013 ukaisha sasa ishu ikawa mwaka unaofuata halafu Ada haijulikani itatokea wapi.

Basi baada ya mwaka wa kwanza unakaribia kuisha na kufanikiwa kupambana na machangamoto yote kama nilivyoeleza ya mazingira, lakini pia hata upande wa ada tulipambana na ndugu kwa kuungaunga ikatimia nikasoma. Sasa mwaka wa pili unakuja nikawa nawaza sana ada itakuaje. Nakumbuka nili-apply mkopo serikalini na niliamini ningepata tangu First Year kwasababu nilikuwa na vigezo vyote. Mzazi mmoja hayupo mama ni wa nyumbani hakuwa na uwezo haya hali ya ulemavu pia lakini nilitoswa.

Basi nikaanza kupata wasiwasi nikiangalia kwa ndugu nako mtihani. Mambo yalikuwa magumu nikawaza au niahirishe chuo ili siku nikipata hela nirudi kusoma? Niliwaza mno mno ndipo nikakumbuka yupo Mungu, cha kufanya nianze kufunga na kusali kwa ajili ya hiyo ada ya mwakani. Ndipo nikanza kusali na kufunga haswa kwa imani. Nakumbuka nilipungua sana mpaka narudi nyumbani likizo nimeisha, hapo UE nazo zilichangia.

MSAMARIA MWEMA ALIYEJITOLEA KUNILIPIA ADA YA CHUO KIKUU
Basi nikawa nipo kwenye maombi ya kufunga basi tunakaribia kufungua chuo dada yangu Idda akaniambia: "Mdogo wangu, nina pesa kidogo kalipe hiki then tutajua mbeleni". Basi nikafanya hivo nikarudi lakini bado nina mashaka wasije kunigomea chuo. Nikarudi nikalipa hicho kiasi nikaendelea na masomo huku bado nafunga na kusali.

Sasa kuna siku moja nimetoka kanisani misa ya asubuhi Jumapili nimekaa sehemu nje ya darasa namsubiri Nasoro aje anikokote nirudi hostel kwangu kupumzika, ndipo akatokea mama mmoja hivi akanishika bega na kuniambia: "Mwanangu, hujambo?" Nikageuka kuangalia ni nani nikamjibu: "Sijambo mama, shikamoo" Akajibu marahaba. Akaniuliza: "Mbona uko hapa, unamsubiri nani?" Nikamjibu, "Mwenzangu anakuja kunifuata" Akasema sawa. Akauliza, "We ni mwanafunzi?" Nikamjibu ndio, akasema, "Nakuonaga kila Jumapili nikahisi ni ndugu wa staff hapa chuo" nikamjibu hapana. Akasema, "Basi kila Jumapili nikikuona natamani kukusalimu roho wa Mungu ananiambia kaongee na yule kijana lakini nashindwa ila leo nimeweza" Nikatabasam kidogo nikamwambia: "Sawa mama, karibu" Akaniomba namba yangu ya simu akaniambia kesho nikitoka darasani mchana atanitafuta nikamjibu, "Sawa, mama" Basi akaondoka na mimi nikaondoka nikarudi hostel kupumzika.

Kesho yake nakumbuka saa saba simu yangu ilikuwa inaita nilikuwa nakumbuka nimekaa nje ya chumba changu, simu ikapigwa. Ilikuwa Jumatatu mchana. Nikapokea. Alikuwa ni yule mama nikamsalimia pale akanijibu basi maongezi yakaendelea.

Kwanza akaniuliza: "Mwanangu upo mwaka wa ngapi?" Nikamjibu wa pili. "Wazazi wako wako wapi?" Nikamjibu: "Mama yupo Upareni ila baba alishafariki", "Ulipata shida gani mpaka ukawa kwenye hiko kiti?" Nikamjibu nilipata ajali ya gari mwaka 2007. Akaniambia "Pole sana" Nikamjibu asante mama. Akaniambia: "Sasa mwanangu, mimi Roho wa Mungu muda mrefu alitaka niongee na wewe na nikusaidie ila nikawa kila nikikuona kanisani nashindwa, hivo jana niliweza kwa kuwa roho mtakatifu alinipa hio nguvu sasa mwanangu hapo chuo unachangamoto gani ambayo unaipitia ili nikusaidie?"

View attachment 1780389
David na Mama kijijini Usangi, 2012

Dah! Nilishusha pumzi na nikamuliza: 'Mama, upo serious?" Akanijibu, "Ndio. Wewe niambie nini unahitaji kwa sasa ili nikusaidie". Nilijikuta tu machozi yananilengalenga nikamwambia mama subiri nikajisogeza pembeni kidogo nikachukua simu nikamwambia mama changamoto ni nyingi sana napitia ila huwezi amini nina mda mrefu nafunga na kusali kwa ajili ya kupata ada ya chuo nimelipa kidogo hata ya nusu semester haijafika kwahio naomba nisaidie ada ya chuo. Akanijibu usijali ada yako ni shilingi ngapi kwa mwaka, nikamjibu ni kiasi kadhaa. Akaniambia basi sawa nitakupa.

Unajua sikuamini, akaniambia nipe namba yako inayopokea pesa nikampa akaniambia basi subiri kama masaa 2 hivi nikawa bado siamini akakata simu, mimi nikarudi room huku nafurahi wenzangu wakaanza kuniambia, "Oya vipi, mbona hatukusomi?" Nikawaadithia wakafurahi. Basi baada ya masaa hayo mawili ikaingia hela. Sikuamini nikampigia simu mama kumshukuru, akasema: "Mwanangu, kalipe hiyo ada iliobakia ya nusu semester halafu inayobaki ni pocket money yako"

Dah nilifurahi na kumshukuru sana. Basi kesho asubuhi tukaenda bank tukalipa, amani ikarudi moyoni mwangu. Aisee nikaamini Mungu yupo na aliyasikia maombi yangu. Nikampigia simu mama nikamwambia nimeshalipa risiti ntakuonesha Jumapili akanijibu, "Kuwa na amani, nitakuja Alhamisi kukusalimia hapo chuoni" Nikamjibu, "Karibu sana mama yangu" Ilipofika Alhamisi akaja.

Alipofika Hall 7, parking ya magari akanipigia simu, akauliza: "Upo wapi, mwanangu?" Nikamjibu nakuja kukuchukua. Basi bwana, yule mama amekuja na hizi gari za serikali anaendeshwa huwezi mdhania; ukimwangalia akashuka kwenye VX moja matata, nikampokea akaja mpaka room akapaona kisha akaniambia, "Tukae nje hapa kwenye upepo" Tukampa kiti tukaanza kuongea.

Kwanza nikamshukuru tena, akanijibu: "Kuwa na amani" kisha akaniambia yeye ni nani, "Mwanangu mimi Mungu amenibariki sana na huwa natoa sadaka kwa Mungu kwa kusaidia watu wenye shida mbalimbali, hivyo Mungu alinionesha wewe na akamtuma roho mtakatifu nije niongee na wewe na ukaniambia hitaji lako. Wewe ni mwanangu wa 5 kati wale ninaowasaidia" Nikamwambia asante sana maana nilikuwa katika kipindi kigumu sana akaniambia kuwa na amani akaniambia subiri kidogo akaenda kwenye gari akarudi na mfuko hivi, akaniambia hii ni zawadi yako.

Nikamuliza naweza kuangalia akanijibu sawa nilivyofungua ndani nikaona laptop ndogo ya Samsung pamoja na mafuta ya TB Joshua na stika zake akaniambia najua chuo laptop ni muhimu na hizo stika bandika chumbani kwako na haya maji uwe unajipuliza ukiwa unatoka ukiwa unasoma na hata ukitaka kulala.

Nikamshukuru sana sana, sana. Basi akaniambia naondoka tutaonana Jumapili kanisani, akafungua pochi yake akanipa pesa kama laki moja nikamwambia mama nina ile balance iliobaki akajibu ongezea kwa ajili ya pocket money. Pia akaniambia uwaambie ndugu zako na mama pia nikamjibu sawa. Basi akaondoka ilipofika jioni nikampigia Idda; alifurahi na kushukuru nikampigia mama naye akashukuru na kuniambia nimpe namba za huyo mama ampigie amwambie asante nae akafanya hivyo.

Maisha yakaendelea nikawa nasoma huku nina amani sana. Yule mama ilikuwa kila mwisho wa mwezi ananitumia elfu 50. Mungu yupo nyie, ukiwa umekwama ukasali na kufunga kwa imani anajibu!

Namshukuru sana Mama Lyimo huko aliko na Mungu ambariki sana.

NILIVYOSAIDIWA KUPATA MKOPO WA MASOMO
Sasa ujue Mungu ni mwema, siku moja niko zangu darasani simu ikawa inaita nikaipokea kulikuwa hakuna mwalimu nikasikia, "Hallo! Naongea na David?" Nikamjibu, "Ndio, nani wewe?" nikauliza akajibu mimi mtu flani alikuwa ni mdada.

"Uko wapi?" Nikamjibu darasani akauliza mnatoka saa ngapi nikamjibu saa 10 jioni akajibu sawa naomba ukitoka naomba nibeep nikajibu sawa, basi tulivyotoka saa kumi darasani tukaamua leo tusipande bajaji twende mdogo mdogo hadi room. Kulikuwa mbali kidogo. Tulifanya hivyo kwasababu hiyo siku ilikuwa ijumaa na hatukuwa na kipindi kingine. Basi nikam-beep yule dada akanipigia akaniambia niko hapa Hall 7 nakusubiri, nikamjibu sawa.

Tulivyokuwa tunakaribia Hall 7 nikaona mtu mbele yetu anachukua video kwa kamera hizi kubwa nikamuliza Nasoro na Imma, "Kuna mtu anatuchukua video mnamuona?" Wakajibu ndio tusimame tukasimama. Basi yule dada alinigundua akaniita nikamwitikia. Wanachuo wengine walihisi kuna movie ya Kibongo inachezwa sababu zile kamera zilikuwa zaidi ya moja. Basi yule dada akaniomba tuendelee kuja tu, hamna shida, basi tukapanda mpaka kufika parking ya Hall 7.

Yule dada na timu yake wakatusalimia na nikawauliza nini kinaendelea akasema twende room kwako tukaongee nikamkaribisha tulipofika kwanza akauliza mmekula tukamjibu hapana akasema agizeni chakula, tukaagiza ndio mazungumzo yakaanza.

Akajitambulisha, "Mimi nipo Germany nimekuja kufanya research yangu Tanzania ya PhD ya Mazingira na Miundombinu ya Watu wenye Ulemavu Vyuoni, Tanzania nzima. Hivyo nilivyofika hapa nikapewa namba yako nikaambiwa wewe unaweza nipa info vizuri"

Nikamjibu, "Ooh! Karibu sana". Basi akaandaa kamera zake na kuanza kunifanyia interview, tukaimaliza kisha tukatoka nje na kwenda baadhi ya madarasa na kuona namna inavyokuwa ninavyokaa huku wakichukua video. Tukamaliza tukarudi hostel kisha tukaanza stories za kawaida. Katika stori stori akaniuliza hivi umepata mkopo wa serikali nikamjibu hapana akastuka sana yule dada. Akauliza "Kwanini hujapata, uli-apply?" Nikamjibu nili-apply na sijajua mpaka leo kwanini sijapata licha ya kufuatilia sana.

Akaniuliza una baki ya documents zako nikamjibu ndio, nikampa akaziangalia akasema una haki ya kupata mkopo, nikamwambia ndio hivyo sijapewa. Akauliza kesho una ratiba gani nikamjibu kesho ni Jumamosi nipo tu akaniambia asubuhi nakuja twende Bodi ya Mikopo. Mungu huyu...

Basi ilipofika asubuhi siku ya Jumamosi yule dada alikuja chuoni hostel akanichukua mimi na Nasoro kwenye gari tukaelekea mpaka Bodi ya Mikopo. Kufika pale tukaingia kwenye ofisi moja nadhani yule muhusika alikuwa ndio boss pale na walikuwa wanafahamiana na yule dada. Wakasalimiana pale story mbili tatu kisha yule dada akamwambia nimekuja na mdogo wangu yupo chuo UDSM na ana vigezo vyote vya kupata mkopo lakini ameingia mwaka wa pili hajapata mkopo. Akamuliza yupo wapi ndio nikaitwa nikaingia ndani akamwambia huyu hapa.

Yule boss akaniuliza uko mwaka wa ngapi nikamjibu wa pili, uliwahi kuapply mkopo ulivyoanza chuo nikamjibu ndio na nina nakala ya viambatanisho vyote, akauliza loan officer wa chuo chako anajua hili nikamwambia analifahamu sana na amekuwa analifuatilia mno bila mafanikio akaniomba nimpatie zile nakala nikampa akapitia kisha akaniambia una vigezo vya kupata mkopo sijajua kwanini hukupata, basi akanichukua akanipeleka ghorofa ya chini yake akamkabidhi dada mmoja hivi taarifa zangu na kumwambia aziingize kwenye mfumo huku anamwangalia. Alivyomaliza akaniambia pole sana na subiri awamu inayofuata utapata basi nikamshukuru sana.

Basi yule dada alienichukua akabaki na yule boss sisi tukashuka chini kabisa tukamsubiri akaja tukarudi zetu chuo nikamshukuru sana sanaa jina lake nimelisahau nadhani kama sio Devota ni Vick, not sure. Kisha tukaagana akaondoka baada ya wiki kadhaa majina yakatoka kwenda kutazama nikalikuta jina langu nilimshukuru Mungu sana nikazidi kuwa na amani moyoni. Sasa nikasema nimtafute yule dada nimshukuru sikumpata kabisa ila baadae niligundua atakuwa amerudi Germany maana namba zake za Tanzania hazipatikani. Maisha yakaendeleaa sikuchoka kumtafuta yule dada siku alinitext na namba yake ya Ujerumani nikafurahi na kumpa taarifa kuwa nilipata mkopo asilimia 80% akasema sawa kila la heri.

Baada ya hapo shule ikaendelea kama kawaida nikawajulisha ndugu zangu wakafurahi zile stress zikaisha. Mungu ni mwema Jumapili moja nikaenda kutoa sadaka ya shukrani kwa kweli.

KUHITIMU MASOMO NA HARAKATI ZA MTAA
Maisha yakaendelea nikapambana mpaka ilipofika mwaka 2016 ndipo nilifanikiwa kumaliza masomo yangu chuoni nikarudi zangu mtaani sasa kupambana na maisha mengine huku nikisubiria matokeo ya mwisho nijue je joho litavaliwa au ndio mambo ya Supp. Basi wakati niko mtaani nikawa najichanganya na shughuli za kijamii ndipo nilipokutana na Smile Volnteers under the founder Kelvin Mwita.

Huyu ndugu alikuja na hio idea akiwa chuo cha MUCCoBS, lecturer na kuamua kuwaunganisha vijana wote vyuoni hapo na hata nje ya chuo na nia ni kusaidia jamii kwa watu wenye uhitaji au makundi maalumu kwa kujichangisha kidogo kidogo ili kupata fedha kununua mahitaji ya hayo makundi na kwenda kuwasaidia.

Sasa Smile Volunteers ikawa na wanachama wengii mpaka Dar na Morogoro sasa mimi ndio nika-join branch ya Dar na nikawa najitolea humo nikawa mmoja wa viongozi wake basi tukawa kweli tunajitolea hivo hivo sisi wenywe na kwenda kusaidia makundi maalumu.

(i) Mahafali baada ya kuhitimu
Baadaye matokeo ya chuo yakatoka namshukuru Mungu matokeo yangu yalikuwa mazuri sana. Ikawa sasa nina mhaho wa graduation. Wiki moja kabla ya tarehe ya graduation nikawa nikilala naota ndoto za ajabu ajabu sana, nikawa nazitafakari mno mara niote joho limepotea mara kofia ile imeungua yani ndoto ambazo zilikuwa zinanipa picha ya kuwa labda graduation sitoifanya. Huwezi amini wiki nzima naota nikawa sijamwambia hata Idda. Sasa ilipofika siku yenyewe sikutaka hata sijui niende salon, nilimwita kinyozi nyumbani nikaoga nikamaliza nikavaa ndio nikamhadithia dada angu Idda akaniambia tu usijali utakuwa sawa.

Tukasali pale then nikamuita dereva taxi nikamwambia nipeleke Mlimani City ila nikampa sharti unipeleke mdogo mdogo hadi eneo la tukio na nikifika nipeleke hadi ndani. Tulivyofika nikamshukuru Mungu nikaingia ndani ya ukumbi nikatulia tuliiii sikutaka hata kutoka nje kupiga sijui selfie mpaka shughuli ilipoanza na mpaka ikaisha. Sasa nikawa najua baada ya hapa ni nyumbani kusherekea na familia yangu na marafiki baadhi, haikuwa hivyo. Kumbe kulikuwa na kamati maalum iliyoundwa tangu mwezi mzima kwa ajili ya party yangu; walikuwa marafiki baadhi na familia yangu (Idda's family) na mama yangu.

View attachment 1778432
David akiwa na wanafamilia baada ya kuhitimu chuo kikuu, 2016

Baada ya kutoka ukumbini nikawa sijui lolote kumbe kuna kitu kimeandaliwa na hiyo kamati. basi wakanizugazuga wakanipeleka Msasani kula kidogo. Sasa ikawa inaingia jioni nikawa namwambia ndugu yangu anaitwa Goodluck (na Mama alikuwepo) twendeni home basi wasije kuja marafiki wakanikosa itakuwa sio vizuri kumbe wananichora tu. Basi yule ndugu akaniambia tupite hapa Triple 7 kuna wadau wanataka kukupa hongera nikaanza kuchukia tulipofika pale wakaja ma-bouncer wakanibeba hadi kwenye venue. Nafika ndio nakutana na ndugu zangu wote na marafiki zangu. Aisee ilikuwa suprise nzurii sana. Basi tukafurahi pale siku ikaisha usiku sana tukarudi nyumbani.

(ii) Kutafuta kazi na kuanza biashara
Kesho kukakucha nikaanza kuwaza nifanye nini, nikaanza ku-apply kazi hasa katika mashirika binafsi huku nikiwa na wazo la kufanya biashara ya chakula. Marafiki zangu nakumbuka walinipa zawadi ya jiko kubwa la kuchomea nyama ndio nikaanza nalo. Nikatafuta hela huku na kule kuna mama mmoja mwanae nilisoma naye chuo alikuwa my best friend, akaniambia: "Unaweza kufanya biashara yako ya kuchoma nyama hapa kwenye lounge ya mama Mwananyamala, utauza kwa hawa wanywaji. Nikaona ni wazo zuri. Nikatoka Kimara hadi Mwananyamala nikafungua jiko na kumweka mtu wa kupikapika hapo.

View attachment 1778438
Picha ya tangazo la biashara ya chakula ambayo David aliwahi kufanya

Basi ikawa natoka asubuhi Kimara naenda Mwananyamala kuchek-chek ila changamoto ikaja kuwa ni usafiri unanigharimu sana, yani faida yote inaishia kwenye usafiri kwa kuwa mimi kupanda daladala ngumu nilikuwa natumia bajaji. Nikahangaika hivyo hivyo lakini nikashindwa nikapata wazo jingine. Sikuchoka, nilikuwa naamini biashara ndio itanitoa kuliko hata kazi za kuajiriwa ila sasa ishu ikawa usafiri, nifanyeje? Nikapata wazo kutoka kwa rafiki yangu mmoja hivi nikamshirikisha Idda akaniambia sawa tujaribu tuone.

Basi lile wazo lilikuwa hivi: Niandike waraka ambao utaelezea maisha yangu na nini nataka kufanya na changamoto iliopo ili Watanzania wanichangie niweze kununua bajaji yangu ili kutatua changamoto ya usafiri. Kweli nikaliandaa hilo andiko na huyo rafiki yangu na baadae tukalirusha mitandaoni Facebook na ma-group mbalimbali ya WatsApp kiukweli watu wengi liliwafikia nikaanza kupokea michango. Nikajiongeza nikachukua jiko la gas na baadhi ya materials ya kuanza kufanya biashara huku nakusanya michango, huku nikawa nimeanza kutangaza biashara yangu. Nikaajiri chef na mtu wa wa kufanya delivery kwa kutumia daladala au bodaboda.

Michango ikawa inaenda vizuri hapo target ni kukusanya milion 7 nipate bajaji mpya. Zile pesa nilizokuwa nakusanya nikazitoa kwenye simu kama milion 3 hivi nikasema nizihifadhi ili nikipata time niende kuziweka bank. Wakati napata hela ya chakula kuuza nikasema ngoja nianzishe biashara nyingine ya kuuza vitenge wax basi nikatafuta connection Kigoma huko nikawa nachukua mzigo then nauza Dar. Wazo la kutafuta kazi likaisha. Basi ikaenda hivoo kwa muda.

(iii) Kupoteza pesa nilizochangiwa na wasamaria wema
Sasa siku moja ilikuwa Jumatatu hivi tumeamka asubuhi dada yangu Idda akawa ameenda kazini akanipigia simu, "Mdogo wangu naomba nikopeshe kiasi cha pesa, mpe shemeji yako nikirudi jioni ntakurudishia", nikamwabia sawa nikasema ngoja niende kuchukua ndani nilikozificha zile pesa ili nimpatie. Kwenda kuzitazama hakuna pesa. Mh! nikastuka sana nikamuliza kaka wa kazi alikuwepo akasema hafahamu. Aisee nilihisi kuchanganyikiwa. Niliona presha kama inashuka nikakosa nguvuukabisa, nikampigia dada simu kumweleza kuwa pesa nilizificha sehemu hazipo. Dada naye akawa haelewi. Kiukweli nilivunjika moyo sana nikaumia mno, nikajiuliza nani amechukua hela yangu maana nilificha kabatini na ndio nilikuwa nataka kuipeleka bank.

Sikupata majibu, nilipaniki sana dada akarudi home tukaanza kujiuliza nani alikuja nyumbani weekend maana Ijumaa zilikuwepo, Jumamosi tulienda harusini, Jumapili tukashinda tu nyumbani na Jumatatu ndio hazipo. Tukataka kujua nani alikuja tukaambiwa kuna ndugu walikuja wawili tukawapigia simu waje home tuwaulize, wakaja.

Walivyokuja wale ndugu tukawauliza wakasema hawahusiki. Nilikosa matumaini kwa kweli nikasema yani mtu unapambana ili utoke kimaisha halafuu anatokeaa mpuuzi mmoja ananirudisha nyuma. Nikamwambia dada hii sikubali ita shehe asome albadiir, na ambaye amehusika basi akutane na balaa lolote huko. Kweli tukafanya hivo lakini moyoni sina amani, nimekosa pozi la kuendelea na biashara tena.

Ila baadae nikakaa nikamuliza Mungu kwanini unaruhusu haya au una mipango mikubwa zaidi ya hii? Nikamwachia Mungu nikasema nifanyeje sasa. Sikuwahi kuwaambia hili marafiki walionichangia ila leo nawaambia na naomba MNISAMEHE SANA SANAA.

(iv) Kazi serikalini, jina kwenye tangazo la kupata ajira kukosewa
Basi nikasema kilichobaki ni kuomba kazi tu serikalini niajiriwe nifanye mambo mengine. Nilikuwa na balance kidogo nikasema hii pesa ninunue TV na ving'amuzi nianze kuonesha mpira mtaani nikusanye hizo mia tano tano na buku buku, nikafanya hivo na nikapata sehemu hapo mtaani huku nikitafuta kazi.

Basi Mungu si Athumani zikatoka nafasi za kazi na kuomba hio ni 2017 nikaitwa kwenye interview ya kuandika. Nakumbuka ilikuwa kule Kigamboni Chuo cha Nyerere nikakuta watu ni wengi mno, kama watu 2000. Tukafanya zile interview lakini moyoni najisemea "Mmh hapa hamna kitu" Tukarudi nyumbani baada ya siku 3 nikapokea meseji kuwa natakiwa kwenye oral interview, Posta, Maktaba House. Nikaenda nikaambiwa tupo 54.

Basi nikakutana na Jopo nikapigwa maswali pale ya Kingereza, daah nikamaliza nikaambiwa utapewa majibu yako. Baada ya miezi kupita nikawa nishajikatia tamaa nikasema hapa mjini kumeshanishinda nirudi tu kijijini kupumzika na mama huku naiwaza pesa yangu iliyoibiwa.

Sasa baadae ilikuwa December 2018 mwanzoni nikatumiwa meseji na rafiki yangu oyaa nimeona jina lako hongera kwa kupata kazi. Mmh! Mikamwambia unazinguaa akanitumia link niangalie kila nikiangalia sioni jina, nikaacha kuangalia. Kuna mtu mwingine akani-text hongera kwa kupata kazi nikamjibu mbona mimi sioni.

Sasa ndio kutulia nikaona jina, ila hilo jina la mwisho halikuwa langu nikasema sio mimi huyu, nikamuonesha Idda akaniambia hili jina wamekosea ni wewe. Kesho nenda kawaulize. Nikaanza kumgomea maana nahisi ni kujichosha tu. Asubuhi Idda akaniamsha ili niende nikaamka kivivu vivu. Ila shetani huyu ni mshenzi!

=======
"Never misuse the one who likes you; never say busy to the one who really needs you. Never cheat the one who really trusts you; never forget the one who always remember you."
=====

Nilikuwa nasikia uvivu sana nikaamka hivo nikaitisha bajaji nikaenda pale Maktaba nikaonana na yule mwenyekiti wa ile sekretareti nikamweleza shida yangu akajaribu kuangalia na yeye akaniuliza majina yako matatu nani nikamjibu, alivyoangalia majina mawili ni sahihi ila la mwisho sio langu akaniuliza ulitumia anuani gani nikamjibu kuangalia ile anuani ilikuwa yangu akaniambia ni wewe hili jina la mwisho litakua ni typo. Basi moyoni nikafurahi sana akamuita sekretari wake akamwambia lile file la Bumbuli lilete, jina limekosewa. Akabadili pale akaniambia njoo keshokutwa uchukue barua yako ukaripori kazini.

View attachment 1780381
David na Dada Idda
Basi nikatoka pale nikampigia Idda akaniambia si unaona nilikwambia mimi watakua walikosea, basi nikafurahi nikasema Mungu huyu ana makusudi lakini pia nikajiuliza hivi nisingekuja ingetokea nini nafasi yangu angepewa mwingine. Shetani ashindwee na alegee au akakamae! Nikawa nasubiri usafiri nirudi mtaani akatokea dereva mmoja hivi yupo na STL akanipa lift hadi sehem moja hivi kunaitwa Cheer Sandbeers, iko Sayansi Kijitonyama. Hapa kuna chakula na vinywaji maana nilikuwa na njaa sana na ndiyo sehemu I feel like home, nikiwa mjini naendaga hapo ku-chill.

(v) Safari ya kwenda kazini Bumbuli
Basi nikala na kunywa kwa kushangilia ushindi then nikarudi home kupumzika. Nikaanza kuuliza habari za Bumbuli kulivyo nikaambiwa Dave kwa situation yako hutakuweza ni milima mwanzo mwisho. Nikajaribu ku-Google nikawa naona mazingira yatakuwa changamoto.

Nilivyofika kuchukua ile barua nikamuomba yule boss nibadilishiwe kituo nikae mjini alichonijibu sikuamini, nikasema Mungu huyu! Alisema, "Dave, ningekusaidia kama kungekuwa na mtu mwingine ambae amepata nafasi kama yako; mngebadilishana. Ila hamna"

Nafasi ya Ustawi wa Jamii ilikuwa moja tu Tanzania nzima na wewe ndio umepata kwahiyo nenda karipoti tu. Ukikaa baada ya muda omba uhamisho. Daah! nikasema hamna shida, basi tukaja Bumbuli Mimi, Idda na mume wake na mjomba angu mmoja hivi na mtoto wa dada yangu mwingine tukasafiri. Safari tuliiona ndefu kwasababu ilikuwa ni siku ya kwanza na ugeni wa mazingira.

Mungu akatusaidia tukafika salama mpaka ofisi ya mkurugenzi. Bahati mbaya hatukumkuta ikabidi tulale ili asubuhi tuonane naye. Tukalala kesho yake asubuhi tukafika na tukamkuta pale. Alinipokea vizuri mkurugenzi na wasaidizi wake na kunipa ushirikiano wote. Basi nikajaza jaza mafomu pale, yote nikamaliza. Nikaambiwa kituo chako cha kazi ni hospitali hivyo utakuwa chini ya ofisi ya DMO. Akaitwa DMO pale akapewa taarifa zangu akanipokea pia tukamaliza pale na nikaomba siku 14 za kujipanga nyumbani ili nije kuanza kazi rasmi.

Safari ya kurudi Dar ikaanza na tukafika Dar salama. Zile siku 14 zikaisha nikaja kazini rasmi nilipokewa vizuri nikatafutiwa mahali pa kukaa na daktari mfawidhi katika Hospitali ya Bumbuli mzee wangu Erasto Mungu ambariki pia. Nikatambulishwa kwenye timu ya CHMT wakanipokea vizuri maisha yakaendeleaa na kufanya kazi za watu.

SAFARI YA KUMPATA MKE WANGU
Changamoto zilikuwepo mazingira ya huku ila nilipata msaada pale ninapokwama hali ya hewa baridii mno. Basi ukapita mwaka 2018 nikaona mbona naeza kuishi tu kwahio wazo lile la kuhama likapotea mwaka 2019 nao ukaisha naona maisha fresh tu nikaanza kuwaza kuoa sasa. Nikasema nitafute Msambaa wangu mie tuishi lakini kila nikicheki sioni. Nikavuta subira. Basi mwaka 2020 ndio huku na huku ndio nakutana na Jesca.

View attachment 1778462
David na Jesca siku ya harusi

Nakumbuka niliweka nadhiri kwa Mungu kuwa anisaidie nikifika umri fulani ambao ni 35 niwe nimeshakutana na mke wangu na niweze kumuoa na sio sogea-tuishi. Basi ikawa hivyo.

Jesca kwa kifupi tunafahamiana tangu watoto huko kijijini lakini hatukuwahi kufikiri leo hii tungeoana ila baada ta muda mrefu kupita miaka mingi tangu 1998 tukaja kukutana 2020 huko Facebook.

Siku tu nili-post picha aka-comment DM na hapo ndipo tulianza kuwasiliana na tukaanzisha mahusiano mpaka kuja kuoana 2021 tarehe 10 April. Mungu ni mwema tunafuraha familia zetu zina furaha na hata ndugu zetu na hata marafiki ninyi pia mnafuraha na mnatupongeza sana.

View attachment 1778460
David na Jesca

-----------------MWISHO-----------------


SHUKRANI NA FUNZO NILILOPATA KATIKA MAISHA YANGU

Namshukuru Mungu kwa kunipa hekima na busara nikaweza kueleza stori ya maisha yangu niliopitia baada na kabla ya ajali. Naamini kuna baadhi mmeguswa na mmejifunza vitu viwili vitatu. Mimi binafsi kupitia hii changamoto nilijifunza mambo kadhaa:

1. Binadamu sisi si lolote. Hatupaswi kuwa na viburi maana hatujui kesho yetu
2. Kipindi cha shida ndiyo utamjua ndugu yako na rafiki yako wa kweli
3. Kukata tamaa ni dhambi kubwa na uvumilivu ndio kila kitu hata kama una maumivu ya namna gani.
4. Kumbe maisha ni hayahaya tu, cha msingi ni kuzidi kumtegemea Mungu na kusali kwa Imani huwa Mungu anatenda. just the matter of time.

Kwahiyo basi, ninawasihi wale wote ambao wana changamoto kama yangu kuwa msikate tamaa; pambana hadi kutimiza ndoto zako -- uwe wa kike au kiume. Lakini pia, wale ndugu na familia ambao mnaishi na ndugu mwenye changamoto yoyote; msiwachoke, wapendeni, simameni nao hadi mwisho. Msioneshe kuchoka Mungu atawabariki.
Credits: Picha na maandishi yote kutoka ukurasa wa Instagram wa David.
stori imenifundisha sana hii!!
 
175 Reactions
Reply
Back
Top Bottom