Staili za zimamoto na ziara za kushitukiza haziendeshi serikali

ndevu mzazi

JF-Expert Member
Nov 6, 2011
687
237
Staili za ?zimamoto? na ziara za kushitukiza haziendeshi serikali


NIMEANDIKA huko nyuma kwamba iwapo tunataka kufanya mabadiliko ya kweli katika jinsi tunavyoendesha mambo yetu hatuna budi kuyawekea mifumo na mipangilio ya kuyafanya hayo mabadiliko. Aidha nimeandika kwamba ili kutimiza hilo hatuna budi kwanza kuanza na katiba mpya ambayo itatuwezesha kutunga sheria, taratibu na kanuni mwafaka zitakazosimamia utekelezaji wa vipengele vya katiba hiyo.

Jinsi alivyoanza Rais Magufuli aliwatia matumaini watu wengi humu nchini na hata nje ya nchi wanaoitakia mema nchi yetu. Hatua alizochukua katika maeneo muhimu yanayohusiana na ukusanyaji wa mapato ziliwatia moyo watu wengi, na walimuunga mkono.

Alichofanya Magufuli na timu yake ya watu wachache kabisa kabla ya kutangaza timu nzima ya baraza la mawaziri ilikuwa ni tiba ya mshituko (?shock therapy?) kuwaamsha watendaji wa serikali waliokuwa wamelala usingizi wa pono kwa muda mrefu chini ya Rais Jakaya Kikwete.
Ukali aliouonyesha Magufuli na waziri mkuu wake uliwafanya Watanzania na majirani zetu kuanza kusema kwamba mabadiliko sasa yanaweza yakatokea hapa nchini. Alivyotumia muda mrefu kuliko kawaida kuteua mawaziri wake, hisia za wengi zilidhani kwamba alikuwa anafanya uchambuzi na uchunguzi yakinifu ili asije akafanya makosa ya kuwarudisha mawaziri ambao walikuwa wamekwisha kudhihirisha kwamba ni mizigo katika serikali iliyopita.

Alipokuja kulitaja baraza lake, ukweli ninaouzungumzia ukajitokeza mara moja, nao ni kwamba kitakacholeta mabadiliko si hamasa na nishati binafsi ya mtu mmoja au watu wawili, bali ni kazi ya mfumo ambamo timu itafanya kazi kama timu yenye lengo moja linaloiunganisha.

Baraza la mawaziri aliloliteua halionyeshi kwamba kuna jambo kubwa litakalobadilishwa kupitia baraza hilo. Kwanza amewarudisha watu ambao tayari wanabeba shutuma za kufanya vibaya kutoka baraza lililopita, ama kwa utendaji mbovu ama kwa kushutumiwa kwa utovu wa uadilifu. Kuwarejesha katika baraza linaloitwa jipya ni kujipunguzia nguvu aliyoanza nayo Magufuli kabla hajawa na baraza.

Aidha, inaelekea mawaziri walioteuliwa walikuwa wamedurusu bosi wao mpya na kubaini kwamba staili yake pamoja na waziri mkuu wake ni kwenda kwenye maeneo yenye matatizo na kutoa maelekezo ya papo kwa hapo, na baadhi yao wakaanza kuiga staili hiyo. Hili ni tatizo litakalokuja kutusumbua huko tuendako.

Niliwahi kusema mara kadhaa kwamba mojawapo ya matatizo yetu ni watu kufanya kazi za watu wengine na kuacha kazi zao. Rais anafanya kazi ya waziri, waziri anafanya kazi ya katibu mkuu, katibu mkuu anafanya kazi ya kamishna na kamishna anafanya kazi ya ofisa wa chini. Wakati mwingine, waziri wa wizara X anafanya kazi ya wizara Y na waziri wa wizara Y anafanya kazi ya wizara Z. Dalili hizi tutazidi kuzishuhudia chini ya baraza hili kama hatua hazikuchukuliwa kuwaelekeza mawaziri kuhusu kazi zao.

Katika hali ninayoijadili hapa, tunapata mfano wa Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue, aliyeonekana akikimbizana na vitanda kwenda Hospitali ya Muhimbili kwa sababu rais katoa maagizo vitanda vipelekwe huko. Mimi nilijiuliza, hata kama ni rais kaagiza hilo lifanyike, ni kwa nini ofisa wa wizara husika asilitekeleze badala ya mkuu wa utumishi nchini?
Inabidi tukumbushane. Isipokuwa kama kuna maelekezo mbadala, kazi ya waziri ni usimamizi wa sera za serikali wizarani kwake, kusimamia utekelezaji wa maamuzi ya serikali yanayotokana na ilani ya uchaguzi wa chama chake. Hata hivyo, tunashuhudia mawaziri wakitoa maelekezo kwa watumishi wa ngazi za kati na ngazi za chini, ambao kiutaratibu wako chini ya katibu mkuu

Katibu mkuu ndiye mtawala wa rasilimali-watu, fedha na vifaa ndani ya wizara. Yeye ndiye anapaswa kusimamia utendaji, nidhamu na uwajibikaji wa maofisa wote wa wizara, na yeye ndiye mwenye uwezo wa kusimamia nidhamu yao, upandishwaji vyeo na hata kuwafuta kazi.

Pia yeye ndiye mlipaji mkuu wa wizara kwa kuwa ndiye mshika kasma mkuu wa wizara. Vile vile, ni katibu mkuu anayewajibika kufanya manunuzi ya vifaa vinavyotumika wizarani (magari, samani, mashine nk.) na kusimamia matumizi yake.
Ofisa anayehusika na taaluma katika wizara si mmoja wa hawa wawili hapo juu. Mtu wa taaluma ni kamishna au kurugenzi, kutegemea wizara husika. Katika wizara inayoshughulikia afya atakuwa ni mganga mkuu wa serikali; katika wizara inayohusu elimu atakuwa kamishna wa elimu, na katika wizara nyingine kuna makamishna na wakurugenzi wanaohusika na utaalamu wa wizara zao.

Lakini katika mvurugano tulioukubali ukajijenga katika serikali yetu, tunawaona mawaziri wakitoa maelekezo kuhusu utawala, na makatibu wakuu wakitoa maelekezo ya kitaaluma. Wakati mwingine, mawaziri na makatibu wakuu wanatoa maelekezo ya kitaaluma kwa sababu tu zamani waliwahi kuwa watumishi katika fani hiyo au ni fani waliyoisomea.

Hata kama mhusika ni daktari kwa taaluma, wizarani hatakiwi kufanya kazi ya taaluma kwa sababu mwenye taaluma yupo, na waziri ni mkuu wa siasa wizarani pale. Pia, hata kama katibu mkuu ana shahada za uhandisi, katika wizara ya ujenzi hawi mtaalamu wa uhandisi bali mtawala wa rasilimali-watu, fedha na vitendea-kazi. Hili lisipoheshimiwa, kila siku kunakuwa na migongano kati ya mawaziri, makatibu wakuu na wanataaluma wa wizara.

Katika hayo yote, ambayo tayari ni magumu, tunaongeza utamaduni wa kutaka kuonekana tunatoa maelekezo na kuwapangia maofisa walete majibu mnamo siku saba au mnamo wiki mbili. Aidha wakubwa wanapenda sana kutoa maelekezo na maagizo hayo mbele ya kamera za televisheni, ili watu wamuone kwamba ?anachapa kazi?. Huu ni upuuzi mtupu, na ni tabia ya kujipatia umaarufu wa bei nafuu kwa watu wasiojua serikali hufanya kazi kwa njia gani.

Kazi ya serikali na maamuzi yote ya serikali ni budi yatiwe katika maandishi, la sivyo ni hewa tupu. Kusubiri kamera za televisheni kabla ya kuanza ?kuchapa kazi? ni upuuzi ambao umedumu kwa muda mrefu sasa, na hauna budi kukomeshwa. Iwapo mawaziri wa Magufuli watafanya kazi kwa staili hiyo, lazima tujue kwamba hakuna jambo la maana wataloweza kulifanya.
Tumekuwa na wakuu waliokuwa wakitoa amri na watu wanatetemeka. Leo najiuliza amri hizo ambazo tuliambiwa kwamba zimetekelezwa wakati ule, zimeishia wapi na ni kwa nini hatuoni dalili zake? Najua kwamba kutoa amri za papo kwa hapo huibua shangwe ya wananchi ambao wanaona kama vile wamepata mkombozi dhidi ya mifumo inayowakandamiza na kuwanyima haki zao. Lakini hiyo si dawa. Dawa mujarrab ni kuweka misingi inayoeleweka na kutabirika, na kujenga mifumo imara na inayoaminika ya utekelezaji na utoaji wa taarifa.

Iwapo kuna tatizo Ilala au Kinondoni na waziri anakimbia kwenda ?saiti? kutoa maagizo, je linapokuwa tatizo kama hilo hilo limejitokeza Bukoba au Sumbawanga, au Masasi, au Ulanga, anafanyaje? Hawa si mawaziri wa Dar es Salaam, kama nimeelewa vyema, ni mawaziri wa nchi nzima. Kote nchini, ikiwa ni pamoja na Ilala na Kinondoni kuna wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya, kama wale wa Bukoba, Sumbawanga, Masasi na Ulanga. Kwa nini hawatumiki?

Katika mambo ninayoyajua kwamba yanatukwamisha na yataendelea kutukwamisha hata kama Magufuli atatoa amri 100 kila siku, ni ubovu wa taarifa za utekelezaji zinazofuatia maelekezo yaliyotolewa na wakubwa kuelekea ngazi za chini. Binafsi kutokana na uzoefu mdogo nilio nao katika utendaji nchini hapa, siamini kwamba zaidi ya asilimia 30 ya taarifa za utekelezaji wa mipango ya serikali ni za ukweli.

Nyingi miongoni mwa taarifa hizo ni za kubuni na kutunga, na maofisa wa ngazi mbalimbali wamejenga uwezo mkubwa wa kuandika taarifa zilizosheheni takwimu za mafanikio ya utekelezaji, majina ya vijiji na tarehe za kuanza kwa mradi na idadi ya watu walionufaishwa na mradi au programu bila hata siku moja kukanyaga katika sehemu inayotajwa. Ni uongo mtupu.

Nimekwisha kuzungumzia umuhimu wa katiba mpya, na sichoki kulijadili hili, kwa sababu ni la umuhimu mkubwa kuliko jambo lolote jingine. Katiba ndiyo inaweza kutuelekeza ni namna gani iliyo bora ya kuiendesha nchi yetu, kuwapa wote wanaohusika majukumu mahsusi ya kutekeleza na kuainisha mifumo ya utawala.
 
Staili za "zimamoto" na "ziara za kushitukiza" haziendeshi serikali

.... inaelekea mawaziri walioteuliwa walikuwa wamedurusu bosi wao mpya na kubaini kwamba staili yake pamoja na waziri mkuu wake ni kwenda kwenye maeneo yenye matatizo na kutoa maelekezo ya papo kwa hapo, na baadhi yao wakaanza kuiga staili hiyo... Huu ni upuuzi mtupu....

Mwandishi mzoefu, Mr. Ulimwengu, ameandika makala nzuri katika gazeti la Rai, na sasa naiona hapa, lakini makala hii inazo dosari kadhaa. Nitaziongelea kwa ufupi hapa.

Ni kweli kwamba Staili ya "zimamoto" haiendeshi serikali, lakini sio madai ya kweli kusema kwamba Staili ya "ziara za kushitukiza" haiendeshi serikali. Mfumo ya utawala anaouongelea lazima utahusisha monitorning and evaluation framework.

Na kazi hii hufanyika ka njia tatu. Kitaalam njia hizo ni ex-ante control mecanisms, ex-post control mechanisms, and on-the-spot control mechanisms. Hii njia ya tatu ndio sababu ya kuwa na vitaasisi kama vile Kamati za Kudumu za Bunge. Ni njia inayohusiana na ziara za kushtukiza. Huu sio "upuuzi mtupu" kama alivyodai.

Nimeona hata Nyaronyo Kicheere anafanya kosa kama hili la Ulimwengu. Nawashauri wajielimishe kuhusu mambo haya kwa kusoma zaidi juu ya "Principal-Agent Theory" na kisha wanyooshe hoja zao katika makala zao zitakazofuata.... Watwambie kwa mujibu wa uzoefu wao ni wapi hakuna ex-ante control mecanisms, ex-post control mechanisms, au on-the-spot control mechanisms, na namna ya kuboresha.

Naamini maboresh haya yanaweza kufanyika sasa hivi hata bila kusubiri ujio wa Katiba Mpya au Marekebisho ya Katiba ya sasa. Marekebisho katika Regional Administration Act, Local Government Authorities Acts, Public Service Act, etc yanatosha kuweka mazngira mazuri zaidi kuliko ilivyo sasa.

Mr. Ulimwengu kama ex-DC anaweza kueleza vizuri mambo haya. Lakini aboreshe style, approach, na tone katika uandishi waki. VIjembe, kejeli, na maneno makali ni aina mojawapo ya communication barriers. (NB:Nimefanya kazi kama mhadhiri wa mawasiliano sanifu).

Nikipata muda nitachangia kwa kirefu kuhusu mada hii kupitia gazetini....
 
Back
Top Bottom