St. Joseph Dar, Askofu Eusebius atoa tamko zito - Katiba, Mkulanga nako Pengo atoa onyo

Candid Scope

JF-Expert Member
Nov 8, 2010
11,883
6,883
Naye Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa, ameelezea wasiwasi wake juu ya uundwaji wa Katiba mpya kutokana na kuendeshwa kwa misingi ya kichama badala ya maslahi ya taifa.

Akihubiri katika misa maalum ya Sikukuu ya Pasaka katika Kanisa la Mtakatifu Joseph, alisema uudwaji wake umeonyesha shaka na wasiwasi mkubwa kutokana na kuanza kwenye misingi mibovu.

"Katiba mpya ni sheria mama ya nchi, hivyo haina budi kumgusa kila mtu nchini, kanisani na hata ndani ya jamii inayotuzunguka, lakini naona tayari imeanza kutawaliwa na itikadi za kisiasa," alisema Nzigilwa.

Akihubiri huku akisikilizwa kwa makini na waumini waliofurika katika ibada hiyo, alisema Katiba ni jambo kubwa lenye kuonyesha mustakabali wa nchi: kutetea wanyonge, kuleta haki na usawa, hivyo isiandaliwe kwa misingi ya chama fulani cha siasa.

Alisema endapo Katiba inataendeshwa kama ilani ya chama fulani cha siasa ni wazi kwamba taifa litakuwa njia panda na kuelekea mahali pabaya zaidi.

"Endapo chama tawala kinaandaa Katiba mpya kwa ilani yao, ni wazi chama hicho kitaweka vipengele vya kujipendelea chenyewe ili kibaki madarakani, na upinzani kadhalika, utaleta vipengele kwa maslahi yake binafsi yakiwemo ya kumwondoa aliye madarakani. Hatutaki hili litokee sasa.

"Iandikwe katiba yenye kuweka mbele maslahi ya taifa, inayogusa maisha ya wananchi wa mijini na vijijini, na kila mwananchi lazima ashiriki katika jambo hilo," alisema.

Askofu huyo alisema Katiba mpya itakayoundwa lazima iwe yenye uwazi kwa watu wa rika zote na isiyomlinda mtu au kundi fulani la watu na chama.

Alisema hakuna ubishi kwamba baadhi ya vipengele vilivyopo kwenye katiba ya sasa havistahili kunyofolewa, lakini yale yasiyofaa lazima yaondolewa kwa ajili ya maslahi ya watu wote.

Askofu huo pia alitumia muda huo kuonya juu ya baadhi ya watu walioko katika jamii kutumia pesa kwa ajili ya kuficha ukweli.

Akinukuu kifungu katika Biblia kinachosema ‘walinzi walitumia pesa kwa ajili ya kuficha ukweli wa ufufuko wa Yesu', alisema ni jambo la hatari kwa jamii na taifa kwa ujumla, kwani iko siku ukweli wa mambo utawekwa wazi.

Alisema watendaji wa serikali wanapaswa kujihoji ni kwa kiasi gani wanatimiza mapenzi ya Mungu katika kuwatendea wenzao haki.

Aidha, aliwataka waumini wa Kikristo na Watanzania kwa ujumla kuitumia Sikukuu ya Pasaka kurejea matendo mema ikiwa ni pamoja na kuheshimiana na kudumisha amani.

Akizungumzia kudumishwa kwa amani, alisema taifa kwa sasa linakabiliwa na hofu mbalimbali na kuongeza kuwa hofu hizo zinatokana na wananchi na viongozi walioko madarakani kutomtii Mungu ipasavyo.

Alisema hofu hizo ndizo zinasababisha kutoweka kwa amani ya utulivu wa nchi, kutokana na Mungu kuwa mbali na wanadamu wake.

Alifafanua juu ya hilo, alisema Pasaka maana yake ni upatanisho kati ya makundi mbalimbali yanayopingana ndani ya jamii.

Pengo atoa onyo
• Ataka wanasiasa kutohusisha dini na siasa
ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo, amevitaka vyama vya siasa na serikali kwa ujumla kuacha mara moja kuwazuia watu wanaodaiwa kuwa mafisadi kwenda kupata huduma za kiroho.

Pengo alitoa rai hiyo jana alipozungumza na Tanzania Daima baada ya kuhitimisha ibada ya misa takatifu ya sikukuu ya Pasaka katika Kanisa la Mt Vinsent wa Paulo, wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani.

Alisema Kanisa Katoliki kamwe halitamfukuza mtu yeyote anayedaiwa kuwa ni fisadi ili mradi ni muumini wa kanisa hilo na kuwa kanisa litampokea iwapo atahitaji huduma zozote za kiroho.

"Kanisa Katoliki halitamfukuza mtu yeyote yule anayedaiwa na serikali au chama kuwa ni fisadi eti asipate huduma zinazomstahili! Kanisa litampokea iwapo ni muumini mzuri na amekwenda kwa ajili ya kupata huduma za kiroho," alisema.

Alisema vyombo vya dini viko kwa ajili ya kutoa huduma za kiroho, hivyo visihusishwe na vyama vya kisiasa na kuwa Yesu alikuja duniani kwa ajili ya wenye dhambi na ndio maana alikufa msalabani, ili kuwaokoa.

"Natoa wito kwa serikali na vyama vyote vya siasa kutohusisha dini na siasa kama kuna mtu anayedaiwa kuwa ni fisadi na anataka kujisafisha kwa lengo la kutubu au anahitaji huduma nyingine yoyote ya kanisa huku akiwa ni muumini wamuache aende kupata huduma kwa sababu Yesu alikufa kwa ajili ya dhambi, hivyo kutubu ni kuacha kutenda ufisadi na kuwa mtu safi; wasiwazuie!" alisema Kardinali Pengo.

Kadinali Pengo alisema kumtenga mtu ambaye ni muumini kwa sababu za kile kinachoitwa ufisadi ni kosa ikiwa kanisa ni chombo kinachopaswa kumsaidia aweze kuwa mtu mwema.

"Kumtenga mtu ni kosa. Mbona Yesu hakumkataa Maria Madgalena na Zakayo mtoza ushuru sasa iweje leo kanisa liwatenge watu wanaodaiwa kuwa ni mafisadi huku wakiwa ni waumini wa kanisa?

"Kamwe kanisa halikubaliani na hilo, kanisa hutoa huduma za kiroho na lengo ni kumfanya mtu awe mwema sasa tutamkataaje mwenye dhanbi ikiwa Yesu mwenyewe aliwapokea na kuwafundisha kisha wakawa watu wema iweje leo tuwakatae?" alihoji Kadinali Pengo.

Aidha, alisema iwapo mtu hakubaliki katika chama si kweli kuwa na katika kanisa hakubaliki kwa kuwa chama na kanisa ni vitu viwili tofauti.

Alisema vyama vinahitaji watu wasafi, lakini kanisa linahitaji wenye dhambi (watu wachafu) ili wapate kutubu na kumrudia Mungu ndio maana Yesu alikuja kwa ajili ya watu wagonjwa na si wazima.

"Ikiwa Yesu alikuja kwa ajili ya wagonjwa na si watu walio wazima na tena wenye afya ambao hawahitaji tabibu itakuwaje mwenye dhambi asimrudie Mungu? Inawezekana kweli mtu akawa mbaya kwenye chama lakini akawa mzuri kanisani. Je utaweza kumtenga mtu huyo na je utamjuaje kama kweli kule alikotoka alitenda kosa hilo? Zaweza kuwa njama tu za watu serikalini au katika siasa. Hapana Kanisa Katoliki lisihusishwe na hilo," alisema.

Kauli ya Kardinari Pengo imekuja siku chache baada ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, kusema mafisadi walioenguliwa na chama hicho wanataka kuwatumia viongozi wa dini ili kujisafisha.

Katika ibada aliyoiongoza Kardinari Pengo aliwataka waumini wa dhehebu Katoliki kuliombea taifa liwe na amani pamoja na machafuko ya kisiasa yanayozidi kutokea katika bara la Afrika na duniani kosa sanjari na majanga yanayotokea.

Chanzo: Tanzania Daima
 
  • Thanks
Reactions: LAT
"Endapo chama tawala kinaandaa Katiba mpya kwa ilani yao, ni wazi chama hicho kitaweka vipengele vya kujipendelea chenyewe ili kibaki madarakani, na upinzani kadhalika, utaleta vipengele kwa maslahi yake binafsi yakiwemo ya kumwondoa aliye madarakani. Hatutaki hili litokee sasa.

"Iandikwe katiba yenye kuweka mbele maslahi ya taifa, inayogusa maisha ya wananchi wa mijini na vijijini, na kila mwananchi lazima ashiriki katika jambo hilo," alisema.

Askofu huyo alisema Katiba mpya itakayoundwa lazima iwe yenye uwazi kwa watu wa rika zote na isiyomlinda mtu au kundi fulani la watu na chama.
[/I][/SIZE]

Hii imetulia:A S 465:
 
Back
Top Bottom