Ngongo
JF-Expert Member
- Sep 20, 2008
- 18,921
- 31,161
2008-12-04 10:26:57
Na Mashaka Mgeta
Na Mashaka Mgeta
SOURCE: NipasheSpika wa Bunge la Jamhuri ya Tanzania, Samuel Sitta, amesema hakuna mantiki kwa waziri kusaini mkataba wa uchumi na biashara nje ya nchi na kufanya kuwa siri kwa umma.
Ingawa Spika Sitta hakumtaja moja kwa moja waziri aliyefanya hivyo, lakini kauli yake hiyo imekuja huku kukiwa na shutuma dhidi ya aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi kusaini kwa siri mkataba wa uwekezaji katika mgodi wa Buzwagi ambao unamilikiwa na kampuni ya Barrick, nchini Uingereza.
Sitta alisema hayo jana jioni katika ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam wakati akizindua Mfuko Maalum wa kusaidia kujenga uwezo kwa wanahabari na vyombo wanavyofanyia kazi.
Alisema usiri unaofanyika katika kusaini mikataba hiyo, hautoi fursa iwapo umefanyika kwa maslahi ya umma au kwa kuiuza nchi.
``Kuna mantiki gani kwa waziri anakwenda ughaibuni kutuambia kuwa anakwenda kusaini mkataba wenye maslahi yetu wananchi na baadaye akirejea atuambie kuwa walichokubaliana ni siri, hata kwa wawakilishi wetu yaani wabunge,`` alisema Spika na kuhoji.
``Tutapimaje basi ikiwa maslahi ya nchi yamezingatiwa au mhusika kaenda kuiuza nchi,`` alizidi kuhoji.
Mwanzoni mwa mwaka huu, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, aliibua mjadala mkubwa nchini baada ya kutoa siri za Karamagi kusaini mkataba nje ya nchi.
Zitto alitoa shutuma hizo katika hoja binafsi aliyowasilisha bungeni ambapo alidai kuwa, Karamagi alitumia madaraka vibaya kwa kusaini mkataba kinyume na agizo la Rais kwamba sheria za madini zipitiwe upya.
Hatua hiyo ya Zitto kutoa hoja hiyo bungeni, ilisababisha mbunge huyo kusimamishwa.
Hata hivyo, watu wa kada mbalimbali, walilaani kitendo cha kumsimamisha mbunge huyo kijana na machachari.
Spika alisema kuna makubaliano na serikali kwa waziri kumpatia Katibu wa Bunge mikataba yote ya maendeleo ambayo hivi sasa imetengewa masijala mahususi kwa ajili ya wabunge.
``Wanaoendeleza dhana ya usiri dhidi ya mwenye mali (mwananchi), wanalo jambo, wasakamwe ili waache mizengwe hiyo,`` alisema. Alisema usiri wa namna hiyo, ndio unasababisha wanahabari kuandika habari za kuhisi au kile wanachokiamini kuwa ni sahihi.
``Nawashauri wenzetu serikali kuweka utaratibu ulio wazi kwa kila wizara kuwa na dawati la taarifa ambapo wanahabari na wananchi wanaweza kupata habari za uhakika kuhusu utekelezaji wa majukumu yaliyo chini ya wizara hizo,`` alisema.
Alisema kumekuwapo na mvutano kati ya serikali na vyombo vya habari, hali iliyoko katika nchi nyingine zilizoendelea.
``Mivutano hii inatokana na haja ya wanahabari kufichua mambo ya hovyo yanayofanywa na serikali, na serikali kutokuwa tayari mambo yake kuanikwa kwa umma,`` alisema.
Alisema vyombo vinasaidia kufichua vitendo vinavyokwamisha maendeleo ya nchi kama vile ufisadi, rushwa katika utawala, matumizi mabaya ya madaraka, huduma mbovu kwa wananchi na ubadhirifu wa mali ya umma.
Alisema katika nchi nyingi masikini ikiwamo Tanzania, zina mifumo na sheria ambayo inakandamiza uhuru wa vyombo vya habari.
Alitoa mfano wa sheria ya magazeti ya mwaka 1976 ya hapa nchini kwamba imepitwa na wakati.
``Natoa wito kwa serikali ya Tanzania kuharakisha kufikisha bungeni muswada wa sheria mpya ya habari itakayolingana na hali ya sasa,`` alisema.
Alisema katika miaka ya hivi karibuni kumekuwapo na vitendo, kauli na mitazamo ya baadhi ya watu inayoashiria mwelekeo wenye nia ya kuibomoa misingi iliyojengwa na Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere kupitia baadhi ya vyombo vya habari.
Spika Sitta alisema vyombo vya habari hivyo vinaandika habari za uchonganishi, uzushi na hisia za chuki na utabaka.
``Hii ni tabia moja mbovu ambayo hutumiwa na waandishi wasio waadilifu kwa lengo la upotoshaji ili kujenga hoja juu ya upotoshaji wanaoufanya,``alisema Sitta.
Alisisitiza juu ya kauli yake aliyowahi kuitoa bungeni kwamba haki za binadamu za mtu mmoja mmoja ambaye kwa vitendo vyake anahujumu watu mamilioni, haziwezi kutazamwa bila kuzingatia haki za hao mamilioni.
Alisema ni wajibu wa nchi yoyote kuzingatia kwa haki za binadamu hazitoi mwanya wa kujenga tabaka la watu maalum ambao utaratibu wa kuwashughulikia unakuwa tofauti na watu wengine, ama walarushwa wakubwa wanaohujumu uchumi wa taifa kujisikia wana uhuru mpana wa kuendeleza maovu yao huku hali ya wengi ikididimia.
``Hali hii isipodhibitiwa mapema itauvunja umoja na utengemano wetu na kutuingiza kwenye migawanyiko, machafuko na hatimaye hata vita vya wenyewe kwa wenyewe,`` alisema Sitta.
Last edited by a moderator: