Pdidy
JF-Expert Member
- Nov 22, 2007
- 50,720
- 21,779
Na Sadick Mtulya
SPIKA wa Bunge Samuel Sitta amesema hoja za vigogo wa CCM akiwamo Kingunge Ngombale Mwiru kutaka ajiuzulu ni kelele ambazo haziwezi kumnyima usingizi.
Alisema wana-CCM hao ni wale waliopo kwenye kundi ambalo halipendezwi na msimamo wake bungeni kutokana na kuziba mianya yao ya kujipatia riziki kinyume na taratibu.
Spika Sitta aliliambia Mwananchi Jumapili jana kuwa kuondoka kwake madarakani kutatokana tu na mwongozo wa Katiba na sio hila wala fitina za watu.
Spika Sitta alisema hayo siku moja baada ya baadhi ya vigogo wa CCM kudai mbele ya kamati ya Rais Ali Hassan Mwinyi mjini Dodoma wiki hii kuwa mgawanyiko na uhasama uliojengeka miongoni mwa wabunge wa chama hicho tawala, umechochewa na Spika Sitta.
Akizungumza na Mwananchi Jumapili jana katika mahojiano maalumu, Spika Sitta alifafanua kuwa kelele zinazopigwa sasa dhidi yake zinahusu maslahi binafsi ya kundi la watu wachache, akiwemo Kingunge na sio maslahi ya taifa.
“Yote mnayosikia na yatakayoendelea kuzungumzwa, ukiyafuatilia kwa makini utakuta ni kundi la watu wachache akiwemo huyo Kingunge; wanaohisi kuwa mwenendo wa Bunge ulivyo hivi sasa unaziba maslahi yao binafsi,†alisema Sitta.
Spika Sitta alisema pamoja na kelele hizo yeye bado ni Spika mahiri na kamwe hawezi kuyumbishwa na misimamo ya watu hao wachache wasiolitakia taifa mema.
Alisema kwa kuwa vigogo hao wana uhuru wa kidemokrasia wa kutoa hisia zao, hashangazwi na maneno yao ila akayafananisha na kelele.
"Maneno yao yote ni sawa na kelele, hivyo waendelee kupiga kelele tu. Mimi ni Spika ninayependwa na kukubalika na wabunge pamoja na wananchi, hivyo sitishiki na nipo imara kupambana hadi hatua ya mwisho," alisema Sitta.
Spika ambaye mara baada ya kuchaguliwa kukalia kiti hicho na kutangaza kuwa Bunge lake litaongozwa kwa viwango na kasi, alisema hatishiki na lolote kwa kuwa Bunge linakwenda vizuri na kwa viwango vinavyokubalika.
"Kutokana na hilo ndiyo maana Bunge hivi sasa linapendwa na wananchi na hata nchi wahisani wanalithamini," alifahamisha na kuongeza;
“Uimara wangu katika nafasi yangu ya uspika ndio unaolifanya Bunge lipendwe na wananchi hata nchi wahisani".
Jana baadhi ya vigogo wa CCM akiwamo Kingunge Ngombale Mwiru walikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari wakisema kuwa matatizo yanayoikabili CCM ni matokeo ya uongozi mbaya wa Sitta.
Sitta hivi karibuni alinusurika kunyang'anywa uanachama wa CCM katika kikao kilichopita cha NEC baada ya wanachama wanaodaiwa kuwa wafuasi wa watu wanaotuhumiwa kwa ufisadi kumtuhumu kuwa amekuwa akiendesha Bunge kibabe na upendeleo. Pia walidai kuwa staili ya Sitta kuingilia mijadala ndani ya Bunge na kushikamana na kundi moja la wabunge na kuingilia madaraka ya mihimili mingine ya dola, ni uvunjaji mkubwa wa misingi ya mgawanyo wa madaraka na kwamba imechangia kuleta mgawanyiko mkubwa miongoni mwao.