Someni hii, iko safi.......

Tasia I

JF-Expert Member
Apr 21, 2010
1,223
193
Waziri Kombani, ameshindwa kabla hajaanza

Samson Mwigamba

amka2.gif
NIMEKUWA nikijitahidi sana kutoa ushauri kwa watawala (si viongozi) wa nchi hii kutokana na kile ninachokiona huko mbeleni. Ushauri wangu wa bure ni kwa manufaa yao na taifa pia.
Nina wasiwasi kwamba huko tuendako taifa litalazimika kuongeza maradufu bajeti ya mahakama ili kuhimili kesi nyingi za ubadhirifu wa mali ya umma, matumizi mabaya ya madaraka, kuwa chanzo cha uvunjikaji wa amani ya nchi, kuiingiza nchi kwenye machafuko, kushiriki ama kusababisha mauaji ya halaiki, uhujumu uchumi, na kadhalika.
Kwa manufaa ya taifa na kwa manufaa ya watawala binafsi nawasihi wasome alama za nyakati na kubadilika. Nakuwa na wasiwasi na ongezeko la wagonjwa wa shinikizo la damu litakalotokea siku watawala walioko madarakani watakapopoteza madaraka.
Ugonjwa ni ugonjwa, hakuna anayependa ugonjwa na matokeo ya ugonjwa yako katikati ya kupona ama kifo. Nawasihi Celina Kombani na vigogo wenzake wote walioko madarakani wanisikilize japo kwa taabu sana na kuyatafakari maneno yangu.
Nawatakia mema, nawatakia kustaafu kwema baadaye ili wale pensheni yao kwa raha ile ile ya mzee Nyerere na mzee Mwinyi. Sitaki wapate shida wala kuipatisha shida serikali ijayo kila wiki kuwe na kiongozi mstaafu anayekwenda kutibiwa nje ya nchi.
Na mimi si mnajimu lakini nashawishika kwamba serikali ijayo baada ya kuanguka kwa ‘watawala’ wetu yaweza kuwa serikali ya wabana matumizi ya serikali kwa hiyo ikaweka hata masharti magumu kwa kiongozi kutibiwa nje ya nchi.

Celina Kombani, Waziri wa Sheria na Katiba, ni miongoni mwa viongozi ambao miaka michache ijayo wanaweza kuugua shinikizo la damu kwa kutoamini kilichotokea. Nasema hivyo kwa sababu ya matamshi aliyoyatoa hivi karibuni kwenye vyombo vya habari.
Waziri Kombani kwanza alisema hakuna haja ya Katiba Mpya eti iliyopo inatosha isipokuwa kama kuna watu wanalalamikia maeneo fulani fulani ya Katiba hiyo basi wapeleke malalamiko yao mezani kwake ili Katiba ifanyiwe marekebisho.
Akaenda mbali zaidi aliposema eti madai ya katiba si ya serikali wala Chama cha Mapinduzi wala wananchi wa taifa hili. Eti madai ya katiba mpya ni ya akina Tundu Lissu na CHADEMA. Akahitimisha kwa kusema serikali haina pesa za kuandika Katiba mpya.
Tatizo la hawa watawala ni kufikiri na kutenda kama Laurent Gbagbo wa Ivory Coast. Siku zote watawala wenye chama kinachoitwa cha mapinduzi wanafikiria mambo matatu makubwa. Kwanza wanafikiria kushinda na kushika dola. Kwao bila kushika dola hakuna CCM na hivyo CCM ni dola na dola ni CCM.
Ndiyo maana hata kauli mbiu zao za uchaguzi zaweza kuwa za aina ile ya “Ushindi ni Lazima”. Pili hufikiria kwamba lolote lenye maslahi na chama chao (maslahi yana maana kukisaidia CCM kubaki madarakani), lazima kienziwe jua liwake ama mvua inyeshe, wananchi watake ama wasitake, kiwe kina maslahi kwa taifa ama hakina maslahi kwa taifa.
Ni kwa sababu hiyo, katiba mbovu, tume nyonge ya uchaguzi, mfumo mbovu wa utawala, na mengineyo watayang’ang’ania hata kama taifa zima linalia. Mwisho siku zote CCM wanafikiri Watanzania ni majuha, wajinga na wasioelewa mambo ya uraia hivyo unaweza kuwapeleka utakavyo.
Nampa pole sana Waziri Kombani. Kwani amelewa mvinyo huo wa chama chake na wala hahitaji kujipa muda wa kufungua masikio asikilize kilio cha Watanzania. Na kilio kisitafsiriwe kama unyonge usio na mwisho.
Paka ni mnyama mpole sana anayeishi na mwanadamu kirafiki mno. Lakini jaribu kumkamata paka halafu ushike ule mkia wake uwe kama unauvunja halafu atafute chance uone atakavyokung’ata na meno na kukujeruhi vibaya. Namshauri Waziri Kombani ajiangalie upya na kuuangalia upya umma wa Watanzania anaowazungumzia.
Anaweza kudhani ni paka marafiki kumbe wameshashikwa mkia na wanatafuta upenyo wa kujinasua na watakapoamua kucharuka si Kombani wala rais wake watakaokuwa salama.
Hoja za Kombani zote ni za ‘kizushi’. Lengo lake kubwa ni kulinda maslahi ya CCM kwa sababu anajua Katiba Mpya ikiandikwa utawala wa kijanja kijanja wa CCM utakuwa hatarini. Anajua kama mwenyekiti wake taifa anavyojua na viongozi wote wakuu wa chama chao wanavyojua kwamba CCM haina mvuto tena kwa wananchi bali inaendelea kuwa madarakani kwa ‘uchakachuaji’ unaowezeshwa na ubovu wa katiba na ubovu mkubwa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Anasemaje kwamba taifa halihitaji katiba mpya wakati akijua kwamba mabadiliko ya katiba ya Zanzibar tu yameiathiri Katiba ya Jamhuri ya Muungano kwa kiwango ambacho haifai tena kuwekewa viraka. Na hapo sijazungumzia mabadiliko ya kisiasa na kijamii achilia mbali suala la wakati linalotusukuma kuwa na katiba mpya.

Katiba ya Jamhuri imefanyiwa mabadiliko karibu mara 15 na sasa Kombani anadai mabadiliko mengine. Wakati wa kuingia vyama vingi Katiba ibara mbili za katiba yetu (namba 80 na 82) zilifutwa na leo Katiba ina kilema maana ukiisoma ukifika kwenye hizo ibara imeandikwa tu 80. (Imefutwa na sheria namba 4 ya mwaka 1992). Vivyo hivyo kwa ibara namba 82.
Leo Kombani anataka ibara ya kwanza tu ya Katiba iandikwe 1.(Imefutwa 2010 na mabadiliko ya katiba ya Zanzibar ). Ibara ya pili hivyo hivyo. Sasa ni Katiba ya nchi gani ambayo unaifungua tu unakuta ibara ya kwanza na ya pili hazipo eti zimefanyiwa marekebisho. Ibara ya kwanza inasema: “ Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano” lakini Katiba ya Zanzibar kwa sasa inasomeka: “Zanzibar ni miongoni mwa nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

Viraka vitaendelea mpaka ibara ya pili kubadilisha maneno yanayodai kwamba rais wa jamhuri atagawa Zanzibar kwenye mikoa baada ya kushauriana na rais wa Zanzibar kwa kuwa katiba ya Zanzibar sasa inamruhusu rais wa Zanzibar kuigawa ‘nchi’ yake kwenye mikoa bila kushauriana na rais wa jamhuri. Bado hatujazungumzia kwenye ibara hiyo hiyo kuondoka kwa maneno “ Tanzania ni nchi ya kijamaa ya vyama vingi” wakati kiuhalisia nchi haiendeshwi kijamaa bali kibepari tena kwa kufuata soko ‘holela’ wala hata si soko huria. Tutalazimika kubadilisha aidha ibara ya 41 inayotamka: “Iwapo mgombea ametangazwa na Tume ya Uchaguzi kwamba amechaguliwa kuwa Rais kwa mujibu wa ibara hii, basi.

“Hakuna Mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza kuchaguliwa kwake”.
Ama tubadilishe ibara ya 107A inayotamka: “Mamlaka ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano itakuwa mikononi mwa Idara ya Mahakama na Idara ya Mahakama ya Zanzibar na kwa hiyo hakuna chombo cha Serikali wala cha Bunge au Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kitakachokuwa na kauli ya mwisho katika utoaji haki.” Kasoro nyingine kubwa ya Katiba ni ile inayoihusu Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inazungumziwa na ibara ya 116 hadi 123. Mahakama hiyo sasa haitambuliwi na Katiba ya Zanzibar.
Mimi si mwanasheria, naweza kukiri kwamba ni mbumbumbu wa sheria kama alivyo Waziri wangu wa Sheria na Katiba Celina Kombani. Pengine waziri wa sheria angekuwa mwanasheria mahiri kama Samwel Sitta ama Harrison Mwakyembe asingetoa kauli ya namna hii.
Mimi ni mtaalam masuala ya uhasibu niliyosomea Chuo Kikuu cha Arusha labda na masuala ya uhandisi ambayo niliyasomea kwenye Taasisi ya Teknolojia ya Dar es salaam. Waziri wangu Kombani ni mtalaam wa masuala ya utawala wa umma (Public Administration) kutoka Chuo cha Mzumbe. Na kimsingi hatuna tofauti kwenye Katiba maana hata yeye anajua kwamba Katiba ina matatizo na ni kikwazo kikubwa cha maendeleo ya kiuchumi, utawala na demokrasia katika nchi yetu.
Tofauti na yeye ni kwamba yeye anajali zaidi maslahi ya watawala wakati mimi naangalia maslahi ya umma mzima wa Tanzania.
Hapa nimegusia tu mambo machache yanayoonyesha matatizo makubwa ndani ya katiba yetu. Sijagusia masuala mengine kama madaraka makubwa ya rais, mgawanyo makini wa madaraka kati ya mihimili mitatu ya dola, na mengineyo mengi.

Nina uhakika kwamba wanasheria wameshaanza na wataendelea kuichambua katiba yetu kama karanga na kutuonyesha kasoro nyingi ambazo zisipofanyiwa kazi sasa huko tuendako inaweza kuleta kasheshe kubwa. Chukulia mfano mdogo tu wa namna mgombea wa upinzani kupitia CHADEMA Dk. Willbrod Slaa alivyojizolea wafuasi nchi nzima halafu mwisho wa uchaguzi akaeleza wazi wazi tena kwa vielelezo kwamba kura zake zimeibiwa na kupewa mgombea aliyetangazwa mshindi na tume ya uchaguzi. Nini kingetokea kama angeamua kuwatangazia wafuasi wake kwamba hakubaliani na matokeo na kwa kuwa katiba haimpi nafasi ya kwenda mahakamani basi tuandamane kama Kenya ama Zimbabwe na kudai haki yetu. Ni nini leo kingeendelea?
Kombani amekalia shangingi ndilo analozunguka nalo wala hajui huku Uswahilini wananchi wanasema nini. Nilibahatika kukaa na Dk. Slaa baada ya mkutano wake wa kampeni pale Karatu. Tulikaa kwenye hoteli moja tukiwa tunazungumzia mchakato wa kampeni za uchaguzi.
Ingawa hatukukaa zaidi ya saa moja, lakini kwa muda huo tayari alishapokea simu nyingi na ujumbe mfupi wa simu kutoka kila pembe ya Tanzania kutoka kwa wafuasi wake. Nyingi zilitoka mkoani Mwanza kwa wafuasi wake na zilisisitiza:“Tumeshapigwa mabomu ya machozi, sasa tumeapa na tunakuambia tuko tayari kutoa damu yetu kwa ajili yako.”
Maneno kama haya ya Kombani wala Kikwete hawayajui. Hawajui kwamba vijana wengi waliochoshwa na utawala wa kina Kombani wako tayari kwa lolote liwalo. Hawa wangeambiwa na Dk. Slaa daini haki yenu, wangepambana na askari wenye bunduki kwa mapanga na marungu. Ingekuwaje?
Ndiyo maana wakati fulani nilimpongeza Dk. Slaa na CHADEMA kwa ustaarabu waliouonyesha wa kudai haki yao kwa njia za kiistaarabu kabisa. Kombani amka sasa na uwaamshe watawala wenzio waliolala. Mtakuja kuumia huko mbeleni.
Mtaugua presha na mnaweza kupoteza hata maisha baadhi yenu kwa uzembe wenu wa kutosoma alama za nyakati. Acha siasa za zamani zimepitwa na wakati. Nakumbuka mwaka jana wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji, ulimhamisha ghafla Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu katikati ya mchakato wa uchaguzi.
Habari zikasambaa kwamba ulipata taarifa kutoka kwa vigogo wa chama chako kwamba hatawasaidia kushinda. Habari hizo ziwe ni za kweli ama uwongo hatua yako hiyo ilijaa utata. Na utakumbuka kwamba hata baada ya kuja huyo mpya uliyemleta bado chama chako kiligalagazwa vibaya katika uchaguzi ule.
Mwaka huu katikati ya kampeni za uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani, ukiwa bado ni Waziri wa TAMISEMI ukamhamisha ghafla Mkurugenzi wa Manispaa ya Arusha. Habari zikavuma vile vile kwamba ni kwa sababu amekataa kukipendelea chama chako.
Ukaleta mpya, akaanza kwa makeke ya kumpiga faini mgombea ubunge kupitia CHADEMA Godbless Lema, lakini mwisho wa siku Lema alishinda ubunge na halmashauri iko mbioni kwenda CHADEMA. Hayo yakufunue macho kwamba umma ukifika mahali ukashikwa ‘mkia’ huwa kama paka niliyemwelezea huko nyuma. Mbinu za kimafia na tekniki alizopata kuzisema mzee Malecela hazitafua dafu.
Kama ulikuwa ukifuatilia televisheni jikumbushe umma wa wananchi uliosheheni nje ya geti za halmashauri katika maeneo mbalimbali ambako inasemekana mlitaka kuchakachua matokeo kama Arusha, Mwanza, na kwingineko. Tafakari, chukua hatua!
Kisingizio cha serikali kutokuwa na fedha hakiingii akilini. Watanzania wanaomba uwaeleze jambo moja tu: Kuandika Katiba mpya inahitaji shilingi bilioni ngapi na mabilioni yaliyopotezwa na serikali kupitia Dowans, Richmond , IPTL, Meremeta, Deep Green Finance, na ndugu zao wote ni mangapi?

Hivi unapozungumzia katiba unajua unachokizungumzia? Usicheze na roho ya taifa. Katiba ni roho ya taifa lolote duniani. Angalia nchi zote zilizoendelea huko kwa wenzetu ukatazame katiba zao zinavyowatiisha raia wote akiwemo rais ama mfalme ama malkia chini ya amri moja ya kuweka mbele maslahi ya taifa.
Kwenye nchi za wenzetu rais asingeamka tu asubuhi na kukutangaza wewe kuwa waziri wa wizara nyeti kiasi hicho bila kukupitisha bungeni, wabunge wakuchambue kama karanga, waulizie ulikotoka, waangalie CV yako, wachunguze umahiri wako katika mambo ya sheria, waone uadilifu wako na ujasiri wa kutetea maslahi ya taifa na kutekeleza Katiba ya nchi, na mambo mengi kama hayo. Vivyo hivyo kwa waziri wa fedha, mambo ya nje, ulinzi na usalama, ulinzi wa ndani na nyinginezo.

Katika nchi hizo rais hawezi kuteua mwanasheria mahiri mithili ya Samwel Sitta ama Dk. Harrison Mwakyembe kuwa Waziri wa Afrika Mashariki ama Naibu Waziri wa Ujenzi halafu akawaleta bungeni wapitishwe halafu hapo hapo mtu wa utawala wa umma awe waziri wa sheria na katiba. Katika nchi hizo rais hawezi kujipangia baraza la mawaziri anavyotaka. Kila siku kuna idadi ya mawaziri na manaibu wao. Mara 61, mara 47 mara 50.
Iko siku rais mmoja atalazimika kupoza makovu ya uchaguzi ndani ya CCM na kuteua mawaziri 80 kama si 90. Katiba ndiyo tiba ya yote haya. Ni katiba itakayotupatia mwongozo wa kuseti sera zetu za mambo ya nje, biashara za kimataifa, elimu, huduma za jamii na kadhalika, sera hizo zikabaki kuwa za kitaifa bila kujali anatawala CCM ama CHADEMA. Katiba ikifikia hapo itakuwa imetusaidia sana kuweka dira ya maendeleo na kutukimbiza wakati wengine wanatembea.
Nashauri tusikusikie tena Watanzania ukitueleza habari ya serikali na CCM hawataki Katiba mpya kwa kuwa nchi hii si ya serikali na CCM.
Na wanaodai katiba si CHADEMA tu, ni Watanzania wote wakiwemo wana CCM wa kawaida (achilia mbali ‘wenye’ chama). Tumewasikia majaji wastaafu, Jaji Mkuu aliyepo, rais mstaafu, viongozi wa dini, wasomi na wanazuoni mbalimbali, wanaharakati, na wengineo wengi; wote hao ni CHADEMA? Wote hao ni Tundu Lissu? Pole waziri wangu, umeshindwa kazi kabla ya kuanza!


h.sep3.gif

Nitumie ujumbe kwenye: smwigamba@yahoo.com au 0713953761 au 0767953761
juu
blank.gif
blank.gif
blank.gif
Habari Mpya | Matangazo | Bei zetu | Wasiliana nasi | Tuma habari | Webmaster
Copyright 2010 © FreeMedia Ltd. Wasomaji
counter
hit counter


© free media limited 2010
mtaa wa Mkwepu na Makunganya, jengo la Bilicanas, gorofa ya kwanza, SLP 15261, Dar es salaam, Tanzania
simu
• faksi +255-22-2126234 • selula 0713 296570


Source ni kama inavyoonekana hapo.

blank.gif
 
Mi binafsi nashindwa kuelewa kama hawa watawala huwa wanashauriana kwanza kabla ya kuongea..
N'wayz, kwa kuwa washatuchukulia sie Watz ka Babu/Bibi zao so wanatuchezea watakavyo, but watambue kuwa UVUMILIVU UNA KIKOMO.
Yangu hayo tu, ngoja nikimbie Class now..!
 
Big up kaka kwa uandishi wako uliotulia, Upole na ujinga wa watz ndio amani na utulivu wa serikali ya CCM lkn days are numbered, they will never last any longer tumeshamka kama wanafikiri bado tumelala. G'DAY WANAJF!!
 
Chukulia mfano mdogo tu wa namna mgombea wa upinzani kupitia CHADEMA Dk. Willbrod Slaa alivyojizolea wafuasi nchi nzima halafu mwisho wa uchaguzi akaeleza wazi wazi tena kwa vielelezo kwamba kura zake zimeibiwa na kupewa mgombea aliyetangazwa mshindi na tume ya uchaguzi. Nini kingetokea kama angeamua kuwatangazia wafuasi wake kwamba hakubaliani na matokeo na kwa kuwa katiba haimpi nafasi ya kwenda mahakamani basi tuandamane kama Kenya ama Zimbabwe na kudai haki yetu. Ni nini leo kingeendelea?

Angeramba u PM kama odinga na tshavungarai
 
Angeramba u PM kama odinga na tshavungarai

sasa we unadhani hatua hyo ingefikiwa baada ya nini kua kimetokea?? halaf kuna k2 watu hawaelew, jamani vita ya panz furaha ya kunguru, zilipoibuka fujo kenya odinga alidhurika? kibaki je? wao wapo hadi leo.wazimaaa, ila wakina mimi na wewe ndo walionusurika ila wakiwa maskin zaidi, vilema na ndugu zao wakapoteza livin zao.

Mind u!!! simaanish kutopigania haki. tafsiri vizuri
 
Keli hii imekaa safi sana. Huyu jamaa kweli ameonyesha mapenzi na nchi yake na amebainisha wazi kwa wale wenye kuongoza kwa maslahi minafsi!!
 
Nampongeza sana mwandishii.....Cellina Kombani asome kwa makini sana hii itampa upeo mpana sana na kumsaidia usoni.....asifikirie amekaa pale kulinda watu fulani amewasahau wananchi wake..kule mahenge/ulanga wenye shida zote zile.....leo anaogopa mabadiliko na katiba ambayo ndio mama wa kila kitu katika nchi na taifa??????nafikiri amewekwa pale kimakosa kabisa.....wanalipana fadhila kwenye chama..sababu alipita bila kupingwa.....chama kinamlipa fadhila....licha kuboronga mbaya kwenye tamisemi
 
Back
Top Bottom