SOKO LA SAMAKI FERI:Kichaka cha samaki kutokana uvuvi haramu

Yericko Nyerere

JF-Expert Member
Dec 22, 2010
16,977
20,244
Mbali na kuuzwa kwa samaki hao wanaotokana na uvuvi haramu wa kutumia baruti, katika eneo la Zoni Namba Nane pia kunadaiwa kufanyika vitendo vingine vya uvunjaji wa sheria vikiwamo uuzaji wa dawa za kulevya na pombe haramu ya gongo, uvutaji bangi, wizi na ukabaji.

Zoni Namba Nane imepewa jina la Lebanon kutokana na kuwapo kwa vitendo hivyo na vingine vya vurugu za hapa na pale na hivyo kufananishwa na nchi hiyo ya Mashariki mwa Asia iliyokumbwa na vita ya wenyewe kwa wenyewe kati ya mwaka 1975 na 1990.

Vyanzo vyetu vinasema mnada huo hufanyika nyakati za usiku kinyume cha sheria na taratibu za Soko la Feri ili kutoa fursa ya kuuzwa kwa samaki wanaovuliwa kwa baruti wakiwa wamechanganywa na samaki wengine.

“Wanavunja sheria na kanuni za soko, taratibu za soko ni kufunguliwa saa 12:00 asubuhi na kufungwa saa 1:00 usiku, lakini wavuvi hao wana mnada wao ambao unaanza saa 1:00 mpaka saa 4:00 au saa 5:00 usiku,” kilisema chanzo chetu na kuongeza:

“Wanaponadi samaki wao huwa kuna watu maalumu wanaowalinda, baadhi yao ni polisi wana maji na askari wa Jeshi la Wananchi (Navy), Kigamboni, kama hawa hawahusiki, hivi haya mabomu (baruti) yanapopigwa huwa wanakuwa wapi?”

Mmoja wa wafanyabiashara wa samaki katika soko hilo alisema: “Tulishawahi kumwuliza, Naibu Waziri, kipindi hicho wizara ilikuwa chini ya Dk Magufuli (John) kama Serikali haina vyombo vya kuangalia usalama wa baharini, lakini mpaka leo hatujapata jibu.”

Wafanyabiashara wengi wa samaki Feri waliohojiwa wanawatuhumu askari polisi na wale wa Kikosi cha Maji cha JWTZ kuwa wanahusika. Wanadai kwamba vitendo hivyo hufanyika mbele yao huku baadhi yao wakishirikiana na wahalifu.

“Wengi wao wakija hapa huwa tunawapa samaki, huo ndiyo ujira wao, maana usipowapa basi ujue uko matatani, lazima ukamatwe. Hivyo ukitaka biashara yako iendelee utoe, hilo ni jambo la kawaida,” alisema mmoja wa waliobobea katika biashara hiyo.

JWTZ kupitia kwa Msemaji wake, Kanali Kapambala Mgawe na Ofisa Mnadhimu wa Polisi Kikosi cha Majini, Ahmed Kinyunyu kwa nyakati tofauti walikiri kufahamu kuwapo wa uvuvi haramu wa kutumia baruti, lakini wote wanasema hawafahamu chochote kuhusu uhusika wa askari wao katika kulinda uhalifu huo.

Yanayofanyika ‘Lebanon’
Mbali na kuwa kituo cha kuuzia samaki wa baruti, Lebanon, pombe haramu ya gongo na dawa za kulevya pia ni miongoni mwa biashara zinazofanywa usiku sambamba na mnada wa samaki hao.

Mashuhuda wanadai kuwa biashara hiyo imekuwa ikifanywa kwa ushirikiano wanaopewa na mama lishe ndani ya eneo kwani wao si rahisi kukamatwa.

“Hivi vifurushi vya dawa za kulevya huhifadhiwa na mama lishe pembeni mwa majiko yao na uvunguni mwa meza zao,” alisema mmoja wa mashuhuda hao.

Kadhalika, nje kidogo ya soko hilo, nyuma ya Ikulu vimekuwa vikiripotiwa vitendo vya ukabaji na wizi na kwamba waathirika wa matuko hayo wengi ni watembea kwa miguu, hususan watalii ambao ni raia wa kigeni.

“Hapa wazungu huwa wanakiona cha moto, wakati mwingine huwa wanaporwa vitu vyao mchana kweupe, wakitokea kule baharini, lakini kagiza (giza) kidogo kakishaingia hali inakuwa mbaya zaidi, hapa huwa hapapitiki kabisa,” anasimulia mfanyabiashara mwingine katika eneo hilo.

Kaimu Mkuu wa soko hilo, ambaye pia ni Ofisa Uvuvi Manispaa ya Ilala, Fidelis Ntima alikiri kuwapo kwa taarifa za vitendo vya uvuvi haramu, lakini akasema mnada wake umekuwa ukifanyika nje ya soko hilo.

“Taarifa za uvuvi haramu zipo na tulishawaambia* polisi, hilo waulize, lakini ni kweli kuwa uvuvi wa baruti upo na mnada upo unafanyika nje ya soko,” alisema Ntima na kuongeza: “Wanaojihusisha na uvuvi haramu ndiyo hao, wanaojihusisha na mnada na hilo eneo liko nje ya ofisi zetu za soko.”

Polisi na JWTZ
Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali Abdulrahaman Shimbo alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema: “Kama wiki mbili hivi zilizopita, mimi mwenyewe* nilipigiwa simu na mtu wa Sea Cleaf (Hoteli) akaniambia kuna vijana wameonekana wakiwa kwenye boti wanavua kwa kutumia baruti.”

“Nikachukua vijana wangu tukaenda tukawakamata tukawafikisha kwa wenzetu Polisi Wanamaji, lakini kama unavyojua mfumo wa mahakama zetu, unakamatwa unalipishwa faini asubuhi uko uraiani.”

Luteni Jenerali Shimbo alisema JWTZ wanafanya kazi kwa kushirikiana na polisi wanamaji lakini akaomba ushiriki wa umma ili kukabiliana na uvuvi haramu ambao alisema: “Ni tatizo na ni jambo baya sana.”
“Ulinzi si jukumu letu peke yetu, lazima tusaidiane na wananchi, tungependa sote tushirikiane tulipige vita ni suala baya si zuri hata kidogo,” alisisitiza Shimbo.

Kwa upande ke, Kanali Mgawe alisema hawana taarifa iwapo askari wao wanashiriki katika uhalifu wa mnada wa kuuza samaki wanaovuliwa kwa baruti.

Kauli kma hiyo pia ilitolewa na Kinyunyu ambaye alisema hafahamu kuhusu mnada wa usiku unaofanyika kuuza samaki wanaotokana na uvuvi huo haramu.

“Hilo la uvuvi wa baruti lipo nani asiyejua kwamba kuna uvuvi wa baruti? Hao ni wavuvi wasiotii sheria sijui wanazipata wapi baruti hizi, tumewakamata mara nyingi tumewafikisha mahakamani wanalipa faini, wanahukumiwa, kazi imekwisha,” alisema Kinyunyu.

Kuhusu tuhuma kwamba baadhi ya polisi wa Kikosi cha Maji wanahusika, Kinyunyu alisema kazi ya askari wake ni kulinda usalama katika eneo la Kivukoni na kwamba kama wanakwenda kwenye mnada huo, watakuwa wamejituma wenyewe.

Chimbuko la Mnada
Uchunguzi umebaini kuwa chimbuko la mnada huo wa usiku ni dharura ambayo iliruhusiwa na uongozi wa Manispaa ya Ilala kuruhusu uuzwaji wa wa samaki ambo huletwa ufukweni na boti ambazo hufika kwa kuchelewa.

Ofisa Masoko wa Halmashauri hiyo, Athuman Mbelwa anasema taarifa ya mnada wa usiku anayo lakini akadai kwamba mnada hufanyika mara chache tu pale kunapokuwa na dharura ya samaki kufikishwa ufukweni kwa kuchelewa.

Mbelwa anasema pale samaki hao wanapochelewa, hulazimika kufanyika kwa mnada usiku kutokana na soko kukosa majokofu ya kuhifadhia samaki.

“Nina taarifa chache za huo mnada kufanyika usiku, siyo kinyume na utaratibu, bali ni utaratibu unaotambuliwa na soko, tunafanya hivyo kuokoa samaki wanaochelewa kufikishwa ufukweni wasiharibike maana hatuna mahali pa kuwahifadhi, lakini huwa inatokea mara chache,” alisema Mbelwa.

Mbelwa alisema si rahisi mnada huo kufanyika kila siku na kwamba hana taarifa iwapo samaki wanaouzwa huwa wanavuliwa kwa kutumia baruti.

*“Unajua mtu anaposema mnada unafanyika kwa siri ina maana uongozi hauna taarifa, hilo si kweli, maana sisi tuna taarifa za kila mnada,” alisema Mbelwa.
Itaendelea wiki ijayo.....
 
Haya ndo mapato yanayofadhiri ustawi wa chama tawala, black money, money loundering- ni fedha za hatari sana, wahusika wanafedha nyingi: wanapata samaki wengi kwa mda mfupi, hawatoi kodi, wanauza madawa ya kulevya....................... Harafu Manispaa ya ilala haina mapato ya kutosha kuwapa huduma wananchi...................
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom