Soko la Maua la Dounan, lililoko Wilaya ya Chenggong, mji wa Kunming, Mkoa wa Yunnan, ni soko kubwa zaidi la biashara ya maua barani Asia. Soko hili lenye shughuli nyingi huvutia wageni kutoka nchi mbalimbali kutokana na aina zake nyingi na za kustaajabisha za maua. Wakati huohuo soko hili linapambwa kwa rangi tofauti za kuvutia, harufu nzuri, na sanaa yake ya maua.
Soko hili linalojulikana kama mahali pa kujua "uhuru wa maua," linawapatia uzoefu mkubwa wapenzi wa maua na watu wanaotembelea na kutaka kujua zaidi kuhusu maua. Sifa kemkem za soko hili zilinifanya nami nitamani sana kutembelea na kujionea kwa macho yangu, kwani kama tunavyofahamu kuwa kwa baadhi ya wanawake maua huwa yanatupatia utulivu wa moyo na kuondoa msongo wa mawazo pale tunapoyanusa ama hata kuyaona tu.
Katika safari yangu mjini Kunming mkoani Yunnan nilihisi kwamba matembezi yangu hayatakamilika kama sikufika kwenye soko hili. Naam, wakati tunakaribia kufika tu kwenye soko harufu nzuri ilitanda hewani na kunifanya nikumbuke nyumbani kwetu Zanzibar visiwa vya karafuu.
Ndani ya soko la Dounan lenye pirikapirika nyingi za kuuza na kununua, kuna maua ya aina tofauti ninayoyajua na nisiyoyajua ambayo yametengenezwa vikuba, mataji ya kichwani na mashada makubwa na madogo. Hivyo nilipoingia tu, kwanza nilinunua kikuba ambacho kilinikumbusha sana harusi za kwetu, pia nikanunua taji na kuvaa vyote viwili kikuba na taji, baada ya hapo nikajihisi sasa na mimi ni miongoni mwa watu waliofika hapo kuangalia shughuli za biashara na kununua maua.
Ukienda Dounan si tu kwamba unapata kununua maua bali pia ni mahali pa unapopata uzoefu mzuri wa kuona mandhari, kusikia sauti mbalimbali, na harufu nzuri za kuvutia. Asubuhi na mapema soko hili huwa na shughuli nyingi zaidi, kwani muda huu wauzaji wa jumla na rejareja hupatana bei na kuchagua maua freshi kabisa kwa ajili ya kusafirisha au kuuza. Mazungumzo ya wachuuzi, mchanganyiko wa petali za maua, na rangi angavu huleta mazingira changamfu ambayo huwavutia wageni wafikao hapo.
Kwa kuwa Yunnan inazalisha maua kwa kiasi kikubwa bei za maua ya soko la Dounan ni za chini kiasi, ambapo maua haya yanasafirishwa kwenda Japani, Singapore, nchi za Asia ya Kusini-mashariki, na maeneo mengine mengi jirani. Maua yana umuhimu mkubwa wa kitamaduni katika mkoa wa Yunnan na China kwa ujumla, kwani yanaashiria uzuri, ustawi, na sherehe. Utamaduni huu wa jadi unaelezwa kwa njia za kisasa kwenye Soko la Maua la Dounan, ambalo linadumisha sehemu muhimu ya uchumi wa ndani na kutambulisha utamaduni wa China.
Kwa wakulima na wafanyabiashara, soko hili huwapatia riziki muhimu, pia husaidia jamii za vijijini na kuhifadhi maarifa ya kilimo. Na kwa wateja, linatoa njia nzuri ya kuwa karibu na uzuri wa asili na urithi uliosheheni wa bustani za maua za mkoa huo. Soko hili sio tu kwamba linauza maua, bali hata bidhaa zinazotokana na maua kama vile sabuni za maua, manukato ya maua, majagi ya kuwekea maua, picha za kubandika ukutani za maua makavu pia zinapatikana hapa.
Mbali na soko la maua linaloendeshwa na wachuuzi binafsi, Donan pia kuna Kituo cha Mnada wa Maua cha Kimataifa cha Kunming, ambacho huunganisha taarifa, kufanya biashara, kuhifadhi maua, kufanya miamala, kusafirisha maua kwa njia ya anga, kutoa ushauri wa kiufundi, na kuweka mfumo madhubuti wa biashara ya maua.
Ili kujua shughuli kamili za soko hilo, ilibidi nikae hadi jioni wakati ambao mnada ndio unafanyika. Ulipofika muda wa mnada nami nikajiunga na wenzangu wengi waliokuwa wakisubiri kununua maua kwa njia ya mnada. Kwa kuwa wateja wengi wanakuwa online hivyo mnada huendeshwa kwa njia ya mtandao. Baada ya kufahamishwa namna ya kununua maua kwa kutumia simu yangu, mnada ulipoanza nilifanikiwa kununua maua kadhaa na kisha kituo kinashughulikia kuyasafirisha mahali nilipoamua yaende. Kwenye mnada huo wastani wa maua yanayouzwa kwa siku ni karibu mashina milioni sita.
Cha kufurahisha ni kwamba hata wateja wa kawaida wanaonunua maua au bidhaa za maua nao pia wanapatiwa huduma ya kusafirishiwa maua yao mahali popote wanapotaka yaende hapa nchini na nje ya nchi.
Mkoa wa Yunnan kupitia soko la Dounan limeunda mnyororo kamili wa viwanda unaojumuisha utafiti na maendeleo ya aina mbalimbali za maua, upandaji na usindikaji, ufungashaji na usafirishaji, biashara na usambazaji, na utamaduni wa utalii, na kuvutia idadi kubwa ya makampuni kuanzisha shughuli zao hapa Yunnan.
Kama nilivyosema awali soko hili mbali na maua, pia wanatengeneza bidhaa zinazotokana na maua kama vile bidhaa za kitamaduni na vyakula vinavyotengenezwa kwa maua pia zinapatikana. Wakati huo huo, biashara za matangazo ya moja kwa moja mtandaoni zinakua kwa kasi, na kupanua zaidi njia za mauzo ya maua ya soko la Dounan.