Soka yetu inapokuwa ni zaidi ya 'komedi'!

Mbonea

JF-Expert Member
Jul 14, 2009
640
20
mpilipili.jpg

lC.gif
Chesi Mpilipili​

rC.jpg

KILA mtu ana namna yake ya kujiliwaza baada ya kazi ngumu za siku au wiki nzima. Kuna wanaopenda kwenda kwenye kumbi za sinema ama za starehe kusikiliza na kucheza muziki huku 'wakimwagilia' makoo yao yaliyokauka baada ya kazi ngumu za siku au wiki nzima.
Kuna wanaopenda kutazama vipindi vyetu vya kuchekesha vinavyorushwa na vituo vyetu vya televisheni kama vile 'Orijino Komedi', Futuhi, Vimbwanga Time na kadhalika.
Zipo pia 'komedi' za aina nyingine kabisa zinazoletwa kwetu kupitia vyombo vyetu vya habari kwa hisani ya wanaoitwa watu wa mpira, klabu zetu kubwa za soka nchini na wadau wengine wa soka wanaodhani kuwa bila matamshi ama matendo yao hakuna mpira wa miguu nchini.
Kwa hakika, matamshi na matendo ya watu wetu hawa wa mpira si tu kwamba ni burudani ya kutosha pengine hata kuzidi akina Futuhi na vimbwanga Time, bali pia yanamfanya mpenzi wa soka kujiuliza kama kandanda letu linaweza kufika popote!
Kwa bahati mbaya, vyombo vyetu vya habari vimekuwa mstari wa mbele kuendeleza komedi hizi kwenye soka letu kwa kutumia kurasa za magazeti na 'airtime' ya vituo vya televisheni kutangaza majibishano na vituko vya watu wetu wa soka na zinazoitwa kuwa ni klabu zetu mbili kubwa za soka nchini!
Katika hili, pengine hata makala yangu hii inaingia kwenye mkumbo huo wa kupoteza kurasa za magazeti kuandika vituko vya watu wetu wa mpira na klabu zetu kubwa za soka! Pengine. Tuvumiliane.
Siku chache zilizopita kwa mfano, Katibu mkuu wa Simba, Mwina 'Simba wa Yuda' Kaduguda alinukuliwa na gazeti moja nchini akisema uongozi wake umegundua njama za watu fulani kutaka kuuvuruga uongozi wa klabu hiyo kutokana na mafanikio wanayopata kwenye ligi ya Vodacom. Hakuna jina lililotajwa.
Huyu alikuwa ni kiongozi ambaye timu yake ilikuwa inashikilia usukani wa Ligi Kuu ya nchi. Tulitarajia atuzungumzie kuhusu mikakati ya timu yake kuhakikisha kuwa inabaki katika nafasi hiyo lakini badala yake akaweka kipaumbele katika kuzungumzia maadui wasiokuwa na majina waliokuwa wanataka kuvuruga maendeleo ya klabu hiyo!
Katika kipindi hicho hicho, kule kwa watani zao wa jadi nako katibu mkuu mpya wa kuajiriwa wa Yanga, Lawrence Mwalusako alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa timu yake ilikuwa imegundua njama za watu fulani za kutaka kipa nambari moja wa timu hiyo afungiwe ili klabu yake ikose kipa! Taarifa hii pia haikuandamana na jina la 'wabaya' hao lililotajwa!
Pengine kilichosikitisha zaidi katika hili ni kile cha katibu mkuu huyo mpya Mwalusako ambaye ni miongoni mwa mabeki wazuri sana ambao Tanzania imepata kutoa, akilazimika kuanza kazi na 'fitna' za kutafuta mchawi wa chanzo cha Yanga kuanza vibaya kwenye ligi hiyo kubwa ya soka nchini!
Kwa hakika, ligi yetu inaelekea kuwa ndio ligi pekee duniani ambayo timu inayoongoza ligi inadai kuwa kuna watu wanaifanyia mtimanyongo hali kadhalika kwa timu inayoshika nafasi ya tano ya ligi hiyo!
Uzoefu unatuambia kuwa hii huwa ni mbinu ya kawaida inayotumiwa na viongozi wa timu zetu kubwa kuwaweka sawa wanachama na mashabiki wao kwa kipigo chochote kitakachoipata timu yao. Ni mbinu ambayo kwa namna moja ama nyingine inaonyesha jinsi viongozi wetu wa soka wasivyojiamini.
Hilo ni moja. Mwishoni mwa wiki iliyopita timu ya Yanga ilipata ushindi mkubwa walipoifunga Mtibwa mjini Morogoro mabao 2-1 baada ya kuwa imesuasua katika mechi za mwanzo za ligi hiyo na kujikuta ikishika nafasi ya tano.
Katika kusuasua huko, viongozi wa Yanga walijikuta wakichanganyikiwa na kuanza kutupiana lawama na kocha wa timu hiyo kiasi cha kusababisha wapenzi wa michezo nchini kujiuliza kama watu hao hawakuwa na ofisi ambako wangeweza kukaa na kutafuta chanzo cha timu yao kuanza ligi vibaya badala ya 'kumwaga mtama' kwenye kuku wengi kupitia kurasa za michezo za vyombo vya habari!
Taarifa za baadhi ya vyombo vya habari kufuatia ushindi wa Yanga dhidi ya Mtibwa zililenga katika kutuaminisha kuwa hayo yalikuwa ni matokeo ya mfadhili wa timu hiyo, Yussuf Manji ambaye alikuwa safarini Uingereza kurejea na 'kuongea' na wachezaji!
Kwamba kabla ya hapo viongozi, wachezaji, wanachama na mashabiki wa timu hiyo walikuwa wameshindwa kuwa na mikakati ya kuhakikisha kuwa timu yao inapata ushindi unaotakiwa hadi mfadhili aliyekuwa safari aliporudi.
Nimejiuliza ingekuwaje iwapo safari ya mfadhili huyo ingechukua kipindi kizima cha mzunguko wa kwanza wa ligi?
Kwa mpenzi wa kawaida wa soka anaweza kujiuliza: Je, uwajibikaji na utii wa wachezaji wetu viwanjani unatokana na mikataba na ajira zao katika klabu hizo ama unatokana na mazungumzo wanayofanya na mfadhili wa timu?
Kila mpenzi wa timu angetaka timu yake kupata ushindi lakini ni vizuri tukaliangalia kwa mapana yake hili la inapotokea timu kufanya vibaya kwenye ligi basi mfadhili wa timu anafanya mazungumzo binafsi na wachezaji na ghafla timu inakuwa moto wa kuotea mbali!
Tukumbuke pia kwamba hili la timu kufanya vibaya wakati mfadhili wa timu amesafiri na kisha timu kufanya vizuri baada ya mfadhili kurejea na kuongea na wachezaji limeshapata kutokea mara nyingi tu huko nyuma.
Viongozi, wanachama na wapenzi wa vilabu vyetu vya soka nchini wanapaswa kujiuliza ni kwa nini suala hili liwe linajirudia rudia na kisha watafute dawa yake ambayo si zaidi ya kuondoa utegemezi kwa wafadhili wa timu.
Sio kwa nia mbaya lakini kwa hakika kutokana na jinsi vyombo vyetu vya habari vilivyouhusisha ushindi wa Yanga na kurejea kwa Manji. Mpenzi wa kawaida wa soka anatamani katika mchezo unaofuata timu hiyo ifungwe ili tuone tu vyombo hivyo vitaandika nini!
Ndio, haiwezekani siri ya ushindi kwa timu kubwa ya karne ya 21 kama Yanga iwe ni mfadhili wa timu kuzungumza na wachezaji wa timu! Mfadhili akiwa safarini basi na ushindi unakuwa pia safarini hivyo kuwa bidhaa adimu!
Cha kushangaza ni kwamba wakati ushindi wa Yanga angalau kwa mechi ya Mtibwa unaoanishwa zaidi na kurejea nchini kwa mfadhili wao na kufanya mazungumzo na wachezaji, kule kwa mtani wao wa jadi Simba mambo ni tofauti kidogo.
Wekundu wa Msimbazi wameweza kuongoza ligi bila ya kuwa na 'Manji' wa kueleweka zaidi ya kile alichosema Kaduguda kuwa ni 'mshikamano miongoni mwa viongozi, wachezaji na wapenzi wa klabu hiyo'!
Simba imeweza kuthibitisha, angalau mpaka sasa, kwamba timu inaweza kufanya vizuri kutokana na mshikamano na mikakati inayohusisha viongozi, wachezaji, wanachama na mashabiki wa timu bila mfadhili wa timu kulazimika kufanya mazungumzo binafsi na wachezaji.
Kwa bahati mbaya, pamoja na kuongoza ligi viongozi wake badol wana mambo yale yale ya mwaka 47 ya kuogopa vivuli vyao wenyewe na kuweka akiba ya maneno kwa kudai kuwapo kwa maadui hewa wanaofanya njama za kuvuruga mafanikio yao.
Yote haya yanafanya wapenzi wa soka nchini kujiuliza, je yataisha pale timu zetu zitakapoanza kushinda mataji ya kimataifa ama tutaendelea na 'komedi' zetu na kuzifanya kuwa za kimataifa zaidi?

hs3.gif

 

Similar Discussions

Back
Top Bottom