Siyo rahisi kwa mwanamke kuwa kiongozi wa siasa

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,316
33,112


000000000000000000000000000000000000000001ladies.jpg
Jane Omary (kulia) mwanamke aliyepigwa na mumewe kwa sababu ya kujiingiza kwenye masuala ya siasa na kudhoto ni Flora Lucas diwani viti maalum kata ya Ijombe Mbeya vijijini aliyeachwa na mume wake sababu ya masuala ya kisiasa.​
Brandy Nelson
“NI miaka 10 sasa tangu mume wangu aliponiacha mwaka 2002 kwa sababu tu ya kujiingiza katika masuala ya siasa…, alinifukuza nikiwa na watoto watatu na ujauzito wa miezi minne…. na yeye kubaki na mali zote tulizochuma pamoja bila ya kunipa chochote,” haya ni maneno ya Flora Joseph (42), Diwani wa Kata ya Ijombe, wilaya ya Mbeya Vijijini.Flora ni mmoja kati ya wanawake waliotoa ushuhuda katika mafunzo ya uraghibishi ya kuwajengea uwezo yaliyokuwa yakiendeshwa na mtandao wa kijinsia Tanzania (TGNP) wakazi wa kata ya Ijombe Wilaya ya Mbeya vijijini hivi karibuni.
Anaanza kwa kueleza ugumu aliokabiliana nao hadi kufanikiwa kuwa diwani, na kukiri haikuwa rahisi kwake kupata nafasi hiyo.
Anasema mwaka 1998 alikuwa anagombea nafasi ya uenyekiti wa wilaya katika Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) ambapo mume wake alimzuia kugombea nafasi hiyo lakini yeye akaendendelea na msimamo wake huku akikimbilia kwa mkwe wake ambaye ni balozi wa nyumba 10.
“Nilikwenda kwa balozi wa nyumba 10 ambaye ni baba mkwe wangu na kumueleza nia yangu lakini mwanaye ananizuia ndipo baba mkwe akaniambia twende wote kwa mume wangu akamweleze lakini juhudi zote hizo zilikwama aliendelea kunizuia nisigombee nafasi hiyo,” anasema Flora.
Anasema kuwa alichana na uamuzi wa mume wake na kuamua kugombea nafasi hiyo na bahati nzuri alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa UWT wilaya ya Mbeya vijijini na kutumikia nafasi hiyo katika kipindi cha miaka 10.
Anafafanua kuwa mwaka 2002 alimweleza mume wake kuwa anataka kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya udiwani wa viti maalum lakini alimkatalia.
Akisimulia jinsi ndoa yake ilivyovunjika, Flora anasema ilikuwa ni siku alipohudhuria mkutano wa vijana uliokuwa ukiendeshwa na Waziri wa sasa wa Mambo ya Ndani Dk Emmanuel Nchimbi ambapo aliporudi nyumbani akakuta mlango umefungwa.

“Siku hiyo ndiyo ilikuwa mwisho wa ndoa yangu kwani niliporudi usiku ule aliniambia hawezi kunifungulia nirudi nilikokuwa huku nikiwa na mimba ya miezi minne ambapo nililala nje na hakutaka kuniruhusu kuingia ndani,” anasema Flora.

Anasema kuwa tangu siku hiyo alitengana na mume wake na yeye aliendelea na masuala ya siasa ambapo mwaka huo alifanikiwa kugombea nafasi ya udiwani viti maalum ambapo hadi sasa ni diwani viti maalum kata ya Ijombe Wilaya ya Mbeya vijijini.

Flora anaeleza kuwa kupitia nafasi hiyo ameweza kupata mafanikio kwani ameweza kujenga nyumba, kumili mashamba na kufanya biashara ndogondogo ambazo zinamwingizia kipato na kwamba kwa sasa mume wake amefilisika mali zote alizomuachia zimekwisha.

“Nawashauri wanaume waache tabia ya kuwanyanyasa wake zao na kuwanyima haki ya kuingia katika siasa na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwani baadaye wataweza kuwasaidia katika kuendesha maisha ya familia zao.”

Kumekuwapo na mikakati ya kuwahamasisha wanawake kushiriki kwa wingi katika masuala ya siasa nchini. Tofauti na wanaume, wanawake wengi wamekuwa nyuma katika uongozi na nafasi nyeti za maamuzi nchini na sehemu mbalimbali duniani.

Tanzania imeridhia maamuzi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (Sadc) ya kutoa asilimia 30 ya nafasi za uongozi kwa wanawake.

Katika kuhakikisha hilo linafanikiwa ni pale Bunge la Jamhuri ya Muungano kuwa na wabunge wa viti maalum na kwa mabaraza ya madiwani kuwa na madiwani wa viti maalum ambao wote ni wanawake ikiwa ni lengo la kuwajengea uwezo.
Kupitia nafasi hizo wanawake wengi wamefanikiwa katika nafasi zao na hata wale ambao walijitosa katika majimbo nakupambana na Wanaume.

Mbali na Serikali, mashirika yasiyo kiserikali na Wanaharakati mbali mbali wamekuwa wakihamasisha wanawake kujitokeza kugombea nafasi mbali mbali za uongozi ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo ikiwa ni pamoja na kujiamini ili kuondoa woga.

Hata hivyo bado wanawake wengi wanakumbwa na vikwazo vingi hadi kufikia nafasi hizo hasa pale wanapojitokeza kwenye nafasi za siasa.
Kwa upande wake mkazi wa kijiji cha Songwi juu kata ya Ijombe Wilaya ya Mbeya vijijini Jane Omary (26) anasema mume wake alimpiga na

kumuumiza jicho baada ya kusikia kuwa amechaguliwa kuwa katibu wa Tawi la Songwi juu kupitia tiketi ya chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Jane mwenye mtoto mmoja anaeleza kuwa wanawake hasa wa vijijini wamekuwa wakinyanyaswa na waume zao ikiwa ni pamoja na kunyimwa haki zao za msingi na kufanyiwa ukatili kwa kupatiwa kipigo na hata kufikia hatua ya ndoa zao kuvunjika mara pale watakapokuwa wakihitaji kupata haki zao.

Anasema kuwa yeye mume wake wanaitikadi tofauti za kivyama ambapo mume wake ni mwanachama wa CCM na yeye ni mwanachama wa CHADEMA.

“Mei mwaka huu 2012 Chadema walitangaza uchanguzi wa viongozi wa matawi ambapo walihamasisha wanaotaka kugombea nafasi hizo waende kuchukua fomu ambapo mimi nilifanya hivyo nikachukua fomu na kujaza kugombea nafasi ya ukatibu wa tawi la Songwi juu,” anasema.

Anaeleza kuwa baada ya kumueleza mume wake kuwa tayari amechukua fomu ya kugombea nafasi hiyo ya ukatibu wa tawi la Songwe juu na baadaye kuambiwa kupitia kwa rafiki wa mume wake ndipo alipobadilika na kumtaka mke wake asiende kushiriki uchaguzo huo.

“Siku ya uchaguzi mume wangu alinikataza nisiende kwenye uchaguzi na mimi sikuenda wakafanya uchaguzi wakapiga kura ambapo kabla ya kutangaza matokeo kuna kiongozi wa CCM wa kijiji alikuwa kwenye kituo cha kupigia kura akifanya kampeni ya kuzuia watu wasipige kura

na walipotangaza matokeo alisikia jina langu likitangazwa kuwa nimeshinda nafasi ya Katibu Tawi,” anasema Jane na kuongeza;
“Baada ya jina langu kutangazwa kuwa nimeshinda nafasi ya ukatibu tawi, nyumbani walizungumza mengi. Walipotoka kwenye mazungumzo

yao ilikuwa tayari usiku na kunikuta nimelala akaniuliza, wewe umegombea Chadema na kwa nini umeandika jina langu na kwanini usiandike jina la ukoo wenu? Hapo hapo akaanza kunipiga hadi nikapasuka jicho baada ya kudondokea kwenye mbao…”
Jane anasema kuwa siku ya pili mume wake alikwenda kumnunulia dawa na plasta ambapo alikataa kutumia dawa hiyo na kukaa na majeraha hayo kwa muda wa siku tatu.

Jane anaeleza kuwa baada ya hapo alikwenda katika ofisi za Chadema na kuwaeleza kuwa waliondoe jina lake katika nafasi hiyo ya uongozi na kuwaeleza matatizo yaliyompata ambapo walifanya hivyo na kuwaambia kuwa yeye ataendelea kuwa mwanachama wa kawaida wa Chadema.

“Msimamo wangu upo pale pale mimi nitaenelea kuwa Mwanachama wa Chadema lakini uongozi sitaweza kugombea tena na kilichonikera zaidi ni kitendo cha yule kiongozi wa CCM wa kijiji ambaye alichochea ugomvi kwenye familia yangu kwa kwenda kumwambia maneno yaliyosababisha mume wangu achukie kupita kiasi kwani alikuwa anajua kuwa mimi naipenda Chadema na ni mwanachama,” anasema Jane.

Masaibu haya yamekuwa yakiwakumba wanawake wengi nchini licha ya Serikali na wadau wengine kuwahamasisha wanawake kushiriki kwenye uongozi na masuala ya siasa kwa jumla.


Siyo rahisi kwa mwanamke kuwa kiongozi wa siasa
 
kumbe wanaume hawajiamini hivyo......... Maana nyuma ya pazia kuna mwanaume asiyejiamini....
 
Ni kweli ni vigumu sana hasa kwa sababu ya mfumo dume, pamoja na mila na desturi ambazo
zinamkandamiza mwanamke. Lakini kimsingi wanawake wanaweza kufanya vizuri kabisa shughuli za kisiasa.
Tatizo hili halipo Tz pekee. Ikumbukwe kuwa hapo awali wanawake hawakupewa hata nafasi ya kupiga kura katika nchi zingine.
 
Kiukweli kabisa wanawake bado hawawezi uongozi hasa katika masuala ya siasa, wanajilazimisha na kulazimishwa tu.
 
Back
Top Bottom