Siwaungi mkono madaktari kwa sasa, lakini tujenge utamaduni wa kujiuzulu | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Siwaungi mkono madaktari kwa sasa, lakini tujenge utamaduni wa kujiuzulu

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by sulphadoxine, Mar 9, 2012.

 1. sulphadoxine

  sulphadoxine JF-Expert Member

  #1
  Mar 9, 2012
  Joined: Nov 1, 2010
  Messages: 2,264
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 135
  NCHI hii ina kansa ya watu wanaofanya makosa, ama hata kutuhumiwa kwa makosa, kutochukua hatua ya kuwajibika. Ninavyojua mimi, si lazima anayewajibika awe ndiye ametenda kosa kwa mkono wake, bali hata kama ni watendaji walio chini yake ambao hakuwasimamia ipasavyo.


  Kadhalika, kuwajibika, hakuna maana siku zote kwamba ni adhabu kwa mhusika ama kumaanisha kwamba mhusika amekiri kosa, bali ni njia nzuri ya kuonesha uugwana. Edward Lowassa, mpaka kesho anakana kuhusika katika tuhuma za kampuni tata ya ufuaji umeme wa dharura ya Richmond, lakini aliamua kujiuzulu nafasi hiyo kubwa ili kuondoa kiwingu.

  Huwa ninashaangaa kusikia, kwa mfano, kumetokea tatizo sehemu lililosababisha kuundwa kwa tume, lakini utakuta wanaochunguzwa ama anayechunguzwa bado yuko ofisini akidai eti aliyemteua hajamuondoa katika nafasi hiyo au waliohusika ni watu wa chini yake. Unapochuguza mahala kama hapa kweli matunda yanayotarajiwa yatapatikana?

  Viongozi ama watendaji wetu siku hizi wanaamini kwamba ofisi za umma ni zao, ni milki yao; hivyo basi, hata kama wakiiba, wakifanya makosa, wakisababisha maafa ama kingine chenye ukakasi, suala la kuwajibika haliwahusu kabisa.

  Mimi kwa kweli nilishangaa sana namna ambavyo Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi ‘alivyogoma’ kujiuzulu baada ya milipuko miwili katika kambi za jeshi jijini Dar es Salaam, iliyosababisha vifo vya Watanzania kadhaa na hasara nyingine nyingi.

  Juzi nilimsikia bwana mmoja akiwashangaa wanaharakati waliokuwa wakimshinikiza Dk. Mwinyi kipindi kile ajiuzulu hata kabla ya uchunguzi kufanyika, lakini mimi nikawa ninamshangaa yeye. Utamchunguzaje mtu kwa uwazi wakati yuko ofisini? Hata kama, kwa mujibu wa bwana huyu, matokeo ya uchunguzi yalionesha kwamba wananchi nao walikuwa na makosa kwa kujenga makazi karibu na makambi ya jeshi eti yaliyochangia joto na mabomu kulipuka, kwa nini kosa hilo lisiihusu wizara husika kwa kulifumbia macho? Yaani wananchi walijenga kwenye maeneo ya jeshi wizara ikiwa imelala wapi? Na kwa nini, kama ilijisahau kwa kulala hadi wananchi wakazunguka kambi, kwa nini wizara isiihamishie kambi hiyo mahala salama kuliko kusubiri maafa?

  Tunaosema sema, tungeweza tusiseme sana kama mlipuko ule wa mabomu ungeliishia Mbagala pekee ambao mimi siamini kabisa kwamba hakuna uzembe wa mtu, na ambao Watanzania tuliaminishwa kwamba hakutatokea tena kitu kama hicho.

  Lakini tukashangaa likatokea tukio lingine la mlipuko Gogo la mboto ambalo halikutofautiana sana na lile la Mbagala. Hata hivyo, kwa vile waziri aliona hahusiki, labda kwa vile yeye si mwanajeshi, hakujiuzulu. Si yeye wala si maofisa wa jeshi katika milipuko hiyo ya mabomu ambao tumesikia wakiwajibika wenyewe ama kuwajibishwa.

  Hatari ya hii, ni kwamba tunasubiri mabomu mengine kulipuka kwa sababu wahusika wataendelea na mazoea na mazingira yale yale.

  Wakati meli ya MV Bukoba ilipozama Mei 21mwaka 1996, serikali iliunda tume ya kuchunguza sababu za maafa yale ikiongozwa na Jaji Robert Kisanga. Kumbukumbu zangu zinaonesha kwamba Tume iligundua kwamba uzembe mkubwa ulisababisha maafa yale ya Watanzania takriban 1000. Kwamba licha ya meli ile kutofanyiwa matengenezo ya mara kwa mara kama ilivyokuwa inastahili, siku ya tukio ilibeba abiria na mizigo mingi kuliko uwezo wake.

  Pamoja na hayo, hatukusikia kiongozi yoyote anawajibika hususan waziri mwenye dhamana ya mawasiliano na uchukuzi, zaidi ya aliyekuwa nahodha wa meli hiyo, Jumanne Rume- Mwiru kushitakiwa. Ukiuliza kisa atakwambia mimi binafsi sihusiki. Hahusiki vipi wakati uzembe uliosababisha maafa umetokea kwenye wizara yake? Kwa nini meli ikawa haifanyiwi matengenezo, kwa nini kabeba kupita uwezo wake?

  Pengine kutokana na hali hii ya watu wanaofanya makosa kutowajibika ama kuwajibishwa na mamlaka za juu, zipo taarifa zinazoonesha kwamba ajali nyingi za majini nchini mwetu zimekuwa zikisababishwa na uzembe kama ule ule wa MV Bukoba.

  Vyombo vya majini vimekuwa vikibeba abiria kuliko uwezo wake, vimekuwa havifanyiwi matengenezo ya mara kwa mara kama inavyostahili na hata idadi ya abiria wanaobebwa na vyombo hivi; kuanzia mitumbwi, ngalawa, boti hadi meli imekuwa haifahamiki vyema. Wala hakuna anayezingatia katika kuhakikisha kwamba vyombo hivi vinakuwa na vifaa vya kujiokolea vya kutosha.

  Mwishoni mwa mwaka jana sote tunakumbuka ajali mbaya ya MV Spice Islanders ambayo haina tofauti sana na ajali ya MV Bukoba. Sababu za ajali zinatajwa kwamba ni zilezile; kubeba sana kuliko uwezo meli. Meli hii pia inadaiwa ilikuwa chakavu sana kwani ilitengenezwa mwaka 1967 na kukataliwa na nchi kadhaa kwa uchakavu kaba ya kuuzwa Tanzania. Kwa lugha sahihi, licha ya kupoteza fedha na kuunda tume ya Jaji Kisanga hatuna ambacho Tanzania tulijifunza kutokana na ajali ile. Lakini mimi ninaamini kama watu wangewajibika ama kuwajibishwa baada ya ajali ya MV Bukoba, kungekuwa na ujumbe mkali kwa wengine kuliko taarifa ya Tume ya Jaji Kisanga.

  Matukio ya wizi, ubadhirifu na matumizi mabaya ya ofisi yamekuwa yakitokea kila kukicha lakini hakuna anayewajibika ipasavyo. Tuchukulie kwenye Wizara moja tu ya Maliasi na Utalii kama mfano. Wiki kadhaa zilizopita, kulikuwa na habari kuhusu Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali Kuu (PAC) kubaini utata wa matumizi ya zaidi ya Sh. 25 bilioni katika Wizara ya Maliasili na Utalii.

  Hii ni wizara ambayo si siku nyingi ilikumbwa na kashfa nyingine ya utoroshaji nje twiga wakiwa hai, kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

  Mimi ninaamini kwamba, pamoja na watu kadhaa kuchukuliwa hatua stahili, kufuatia sakata la usafurishaji wa Twiga, waziri anayehusika alitakiwa kujiuzulu pia

  Hayo tuyaache. Jumanne ya wiki hii wakati ninaandika makala haya, kulikuwa na habari za mawaziri wawili; mtu na naibu wake, Dk. Haji Mponda na, Dk. Lucy Nkya, ambao wamekuwa wakitakiwa na madaktari kujiuzulu kwa kuwa tatizo kwenye Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii wanaoiongoza. Lakini wao wakawa wanasema kuwa suala lao liko kwa mamalaka zinazohusika, kwa maana ya Rais Jakaya Kikwete.

  Mapema Jumatatu baada ya madaktari kusisitiza kwamba walikuwa tayari kukutana na serikali kwa mazungumzo lakini kwa sharti la viongozi hao wa wizara kuondoka kwenye nafasi zao, waandishi wa habari walijaribu kuwatafuta mawaziri hao kueleza lolote, lakini wakagoma kukutana nao.

  Dk. Mponda alisema kupitia kwa msemaji wa wizara hiyo kwamba suala la yeye kijiuzulu ama kutojiuzulu, liko mikononi mwa mamlaka zilizomteua kushika nafasi hiyo.

  Naye Dk. Nkya aliepuka kujibu swali la moja kwa moja kama atawajibika kwa kujiuzulu nafasi hiyo ama la, akisema kwamba suala hilo kwa sasa liko mikononi mwa rais.

  Lakini Jumanne juzi, Waziri Mkuu Pinda akawashangaa madaktari wale kwa kitendo chao cha kumpa Rais siku awe ametimiza matakwa yao ya kuwafukuza mawaziri wa wizara hiyo, vinginevyo wangelianza mgomo.

  Niweke wazi mapema kwamba sipendi kuona mgomo wa madaktari ukitokea tena kutokana na madhara yake kwa hiyo ninaupinga tofauti na pale mwanzoni nilipouunga mkono. Pamoja na kuupinga, ninaungana na madai yao kwamba ni ya msingi. Ninapenda pia kuwakumbusha kwamba kwa mujibu wa maadili yao hawatakiwi kugoma, ingawa pia sipendi kuona serikali inayoshindwa kutekeleza majukumu yake ikiachiwa hivi hivi bila kutikiswa kwa njia ya mbalimbali ikiwemo migomo.


  Nina sababu kama moja ya kutounga mkono mgomo wa madaktari ulioanza Jumatano nayo ni kwamba bado walikuwa na nafasi ya kukaa mezani na serikali. Kama serikali haijatekekeleza kwa wakati madai yao, walipaswa waiambie na kutuambia pia sisi wananchi, kisha wavute subira na si kukimbilia kugoma, kitu kinachoanza kuonekana kama ‘fasheni’. Walitakuwa wavumilie kama walimu ambavyo huwa wanavumilia na kwa kufanya hivyo wangeendelea kuungwa mkono na sisi wananchi na watapata mafanikio. Lakini walivyoishiwa subira, ingawa tunaunga mkono madai yao lakini wanachi nikiwemo mimi, tumejitenga nao kwa sababu si mwafaka kugoma kwa sasa. Ninaamini kama wananchi hawatokuwa nyuma yao, mgomo wao wa sasa hautazaa matunda na serikali itaibuka mshindi!


  Lakini, kama nilivyoanza kusema hapo juu, nimeandika haya ninayoandika ili kuwashangaa mawaziri, Dk. Mponda na naibu wake Nkya kwa kutoachia ngazi mapema.

  Sisemi kwamba wana makosa katika sakata hili, la hasha isipokuwa ukweli kwamba kama mgomo ulitokea mikononi mwao, ukasababisha maafa, madaktari wakaonesha hawana imani nao, hawakuwa na lingine zaidi ya kuachia ngazi.

  Kwanza nini wanachoongoza kikubwa pale wizarani kwao? Bila shaka ni huduma za afya. Sasa kama watendaji muhimu (madaktari) hawawakubali wanaweza kweli kuendelea kung’ang’ania kuwaongoza watu wa aina hiyo kwa ufanisi?

  Kusema kweli, mawaziri hawa walitakiwa wawe wamewajibika muda mrefu hususanm pale madaktari walipogoma hata baada ya Waziri Mkuu Pinda kuwaamuru warudi kazini, vinginevyo wangelifukuzwa kazi.

  Siku ile Pinda aliporudiwa ‘hekima’ na kuongea na madaktari huku katika kauli zake zikionesha pia kwamba mawaziri hao wangechukuliwa pia hatua, wao wangeondoka ofisini siku hiyo hiyo kwa vile walikuwa wameshachelewa! Lakini wameendelea kukalia ofisi hadi Jumanne ya wiki hii nilipokuwa naandika makala haya wakisukumia mpira kwa mamlaka zilizowateua, yaani Rais Jakaya Kikwete.

  Kwa mtazamo wangu, kuna ugumu sana kwa Kikwete kuchukua hatua za kuwaondoa mawaziri hao kwenye wizara hiyo kwa sasa, kwa shinikizo la madaktari. Atakuwa anajenga utamaduni ambao nina wasiwasi nao kwamba si mzuri kwani sasa kila anayegoma atataka kwanza watu fulani waondoke madarakani ndipo yawepo mazungumzo.

  Ninataka kusema kwamba mawaziri hawa walitakuwa kumsaidia rais kwa kujiondoa wenyewe ingawa rais naye, kama bado anawaamini, angeliwabadilisha mapema kwa kuwapeleka katika wizara nyingine kabla ya kusubiri mashinikizo.

  Sina hakika, lakini nimesikia kwamba Dk. Mponda alishaandika barua ya kuachia nagzi lakini bosi wake hakuijibu. Ingawa sijui hekima ya rais ya kukataa kumkubalia Dk.Mponda kama habari hizi ni za kweli, lakini ningelimshauri Rais akubali na kuwaambia Watazania kwamba yeye alikuwa bado anamhitaji lakini Waziri Mponda kapima na kuamua mwenyewe kuondoka wizarani baada ya kuona hakubaliki.

  Nimalizie makala hii kwa kusema kwamba katika katiba tunayotarajia kuiandika, lazima tuungane na Wakenya ambao kwa sasa Katiba yao inatamka wazi kwamba kiongozi wa umma anapokuwa na tuhuma anatakiwa kupisha ofisi. Ndio maana tumewaona Naibu Waziri Mkuu wa Kenya, Uhuru Kenyata na aliyekuwa Waziri wa Kilimo, William Ruto wakijiuzulu nyadhifa zao baada ya mahakama ya uhalifu ya kimataifa (ICC) kuwaona wana kesi ya kujibu kuhusu mauaji yalioikumba nchi hiyo baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2007. Ukweli ni kwamba Ruto alikuwa keshawajibika baada ya kutuhumiwa kwa rushwa kwenye wizara yake hata kabla ya ICC kumuona ana kesi ya kujibu.


  Kwa vile mawaziri wetu wameshindwa kuwajibika wenyewe wanapokuwa na tuhuma ama kukataliwa na wananchi wanaotakiwa kuwaongoza, basi heri tutumie katiba tutakayoiandika kama ilivyo kwa Kenya, kuwawajibisha.
   
Loading...