Sitta mmoja akiuawa kisiasa, Sitta 16 wapya huzaliwa!

Pdidy

JF-Expert Member
Nov 22, 2007
50,906
22,052
Nakala chapishi
Mtumie mwenzio
Jiandikishe utaarifiwe



Sitta mmoja akiuawa kisiasa, Sitta 16 wapya huzaliwa!

Johnson Mbwambo Agosti 26, 2009




HUWA najiuliza mara kwa mara: Mwalimu Nyerere angekuwa hai angeichukuliaje hali ya sasa ya chama chake CCM? Je, angekuwa bado ni mwanachama wa chama hicho au angekuwa ameachana nacho?

Najiuliza maswali haya kwa sababu si siri kwamba Mwalimu Nyerere hakuwa na furaha na chama chake hicho miaka ya mwisho ya uhai wake.

Kwa hakika, Mwalimu alishaanza kuchukizwa na mienendo ya CCM wakati wa utawala wa awamu ya pili wa Rais Ali Hassan Mwinyi.

Ni wakati huo ambapo si tu ‘Mzee Ruksa’ aliugeuza uchumi wetu kuwa wa soko huria, lakini pia ni kipindi hicho hicho ambapo wafanyabiashara wa Kihindi walianza kuizoea Ikulu ya Tanzania kama vile nyumbani kwao.

Ni kipindi hicho hicho ambapo wafanyabiashara hao wa Kihindi walianza kununua picha za Rais Mwinyi kwa Sh. kati ya milioni tatu hadi tano katika hafla mbalimbali za kuchangisha fedha. Ni katika kipindi hicho ambapo baadhi yao walifikia hata hatua ya kumwita ‘shemeji’ mke wa ‘Mzee Ruksa’, Mama Sitti.

Ni kipindi hicho hicho cha utawala wa Mwinyi ambapo baadhi ya wafanyabiashara hao, ambao leo baadhi yao wanatuhumiwa kwa ufisadi, walianza kupanda chati na kukubalika kama wafadhili wa CCM. Nazungumzia wafanyabiashara kama vile Chavda, Jeetu Patel na wengine kadhaa.

Mwanzoni walikuwa ni wachache –tena Wahindi, lakini baadaye wazawa nao wakadandia behewa la treni la mafisadi. Wote kwa pamoja wakaiteka CCM. Chama kikaanza sasa kutetemekea wenye pesa au wanaoungwa mkono na wenye pesa. Mwenye pesa au anayeungwa mkono na mwenye pesa sasa akawa ndiye hushinda uchaguzi na ndiye husikilizwa na Chama!

Mambo hayo ndiyo yaliyoanza kumkosesha raha Mwalimu Nyerere; kwani aliiona mapema hatari iliyo mbeleni. Aliziona mapema ishara za CCM kuwakumbatia wafanyabiashara matajiri na kuwasahau wanyonge.

Ni katika kipindi hicho Mwalimu alianza kutoa kauli mbalimbali za kuitahadharisha CCM ikiwemo ile kwamba amani haiwezi kuwemo nchini kama pengo kati ya matajiri na masikini litazidi kuachiwa liongezeke. Alifikia hata hatua ya kusema kwamba CCM si mama yake, na kwamba angeweza kuachana nayo.

Kipindi cha utawala wa Mzee Mwinyi kilipomalizika, Mwalimu akahamishia matumaini yake ya kuiona CCM inarejea katika misingi yake ya awali, kwa Benjamin Mkapa. Pamoja na afya yake kutokuwa nzuri, Mwalimu alizunguka nchi nzima kumpigia kampeni Mkapa; kwa matumaini kwamba ndiye angekiokoa chama hicho kutoka kwa wafanyabiashara hao.

Lakini dalili kwamba Mwalimu alikuwa amekosea kuweka matumaini yake hayo kwa Mkapa zilianza kuonekana miezi michache tu ya mwanzo ya utawala wa mtu huyo aliyepata kuitwa “Bwana Msafi”.

Dalili zilianza kuonekana pale “Bwana Msafi” alipopuuza ushauri wa wengi (akiwemo Mwalimu) kwamba asiiuze NBC kwa makaburu wa Afrika Kusini. Mkapa alikaidi, na kilichotokea baada ya hapo sasa ni historia; ila yatosha tu kukumbusha kwamba muda mfupi tu baada ya kuingia Ikulu, Mkapa aliomba na kupewa mkopo mkubwa na benki hiyo hiyo! Alianza kufanya biashara Ikulu miezi ya mwanzo tu ya utawala wake!

Ilinisikitisha kusoma kwenye gazeti moja, hivi karibuni, makala ya mwandishi mmoja wa kundi linalojaribu kuwasafisha mafisadi inayomsifu Mkapa; kwamba alikuwa kiongozi wa kiwango cha hali ya juu!

Ukweli ni kwamba uchafu huu wa ufisadi ambao, mpaka sasa, unaendelea kuitingisha nchi ulianzia kwenye utawala wa Mkapa; japo uliibuliwa kwenye utawala huu wa sasa wa Jakaya Kikwete. EPA, Kagoda, Meremeta, Rada, uuzaji nyumba za serikali nk, zote ni skandali zilizoanzia kwenye utawala wa Mkapa wakati huo akiwa na swahiba wake mkuu BOT, Daudi Balali (marehemu).

Niishie tu kueleza hapa kwamba matumaini ya Mwalimu Nyerere kwamba Mkapa angeirekebisha CCM kwa kuitoa kwa wafanyabiashara matajiri na kuirejesha kwa wakulima na wafanyakazi, yalitoweka haraka. Nina hakika mpaka mauti yanamfika, Oktoba 14, 1999, mjini London, alikuwa tayari ameshakata tamaa kabisa na CCM.

Leo hii, Mkapa hayupo madarakani na badala yake tunaye Jakaya Kikwete. Pamoja na mabadiliko hayo ya uongozi, hali ya CCM imezidi kuwa mbaya mwaka hadi mwaka. “Mdudu” yule yule aliyeanza kuitafuna CCM enzi za Mwinyi ndiye huyo huyo aliyeendelea kuitafuna CCM chini ya Mkapa, na ndiye huyo huyo anayeendelea kuitafuna CCM, hivi sasa, chini ya Jakaya Kikwete.

Ni ‘mdudu’ gani huyo? ‘Mdudu’ huyo ni wafanyabiashara mafisadi ambao wameingia katika siasa na wengine kufanikiwa kushika nafasi za uongozi serikalini, na ambao yaelekea wamefanikiwa kuiteka CCM; kiasi kwamba sasa nguvu yao ndani ya chama hicho ni kubwa, kama tulivyoshuhudia katika kikao cha NEC kilichomalizika hivi karibuni mjini Dodoma.

Katika kikao hicho, wafanyabiashara hao ambao ni kama genge la Mafia walitumia ushawishi mkubwa wa kipesa walionao kuwarubuni baadhi ya wajumbe wa NEC kumsulubu Spika Samuel Sitta wakilenga kumwondoa uspika, na ikiwezekana hata kumfukuza uanachama. Na ‘kosa’ la Spika Sitta ni nini? ‘Kosa’ pekee la Spika Sitta (kama unaweza kuliita kosa) ni kuivalia njuga, bungeni, vita dhidi ya ufisadi!

NEC ya CCM ya enzi za Mwalimu Nyerere ingekutana Dodoma si kwa lengo la kumsulubu spika anayepambana na ufisadi; bali kwa lengo la kuwajadili viongozi wote wanaotuhumiwa kwa ufisadi kama vile Andrew Chenge nk.

NEC ya CCM ya enzi za Nyerere ingempongeza Spika Sitta na si kumsulubu au kumtisha kumpokonya kadi ya chama!

Ndugu zangu, kama NEC ya CCM inakutana si kwa lengo la kujadiliana namna ya kuukomesha ufisadi serikalini; bali kwa lengo la kuwanyooshea vidole wanaopigana kuukomesha ufisadi huo, basi, mjue chama hicho kinaishi siku zake za mwisho madarakani; kama ilivyokuwa KANU kwa Kenya au UNIP kwa Zambia!

Yamesemwa na kuandikwa mengi kuhusu kilichotokea Dodoma kwenye mkutano huo wa NEC. Wako wanaosema kwamba Sitta alilazimishwa na Kikwete kuomba radhi, na kwamba alifanya hivyo. Lakini wako wengine wanaosema kwamba Sitta hakuomba radhi.

Sina uhakika ukweli ni upo katika jambo hilo, lakini natamani ukweli uwe ni kwamba Sitta hakuomba radhi. Aombe radhi kwa lipi ovu alilolifanya?



Nelson Mandela
Natamani Spika Sitta angemuiga Nelson Mandela katika kesi ile maarufu ya Revonia ambapo aliposimama mahakamani kuanza utetezi wake, Aprili 20, 1964, Madiba alimalizia utetezi wake kwa kusema hivi: “I have cherished the ideal of a democratic and free society in which all person live together in harmony and with equal opportunity. It is an ideal which I hope to live for and to achieve. But if needs be, it is an ideal for which Iam prepared to die.”

Kwa tafsiri ya Kiswahili isiyo rasmi, Madiba alisema hivi: “Nimekuwa muumini wa dhana ya jamii huru inayoishi kwa kufuata misingi ya kidemokrasia ambako wananchi wote huishi kwa amani wakiwa na fursa sawa. Ni imani ambayo natarajia nitaendelea kuishi nayo na kuifanikisha. Lakini ikibidi, ni imani ambayo kwayo niko tayari kuifia.”

Maneno hayo ya Madiba ya mwaka 1964 ndiyo yanayonichochea nitamani ndani ya kikao hicho cha NEC, kilichofanyika Dodoma, ingetokea hivi: Baada ya kushambuliwa na wajumbe wengi ambao ni mawakala wa mafisadi, Spika Sitta naye angesimama kujitetea na kumalizia utetezi wake hivi: “Maisha yangu yote nimepigania haki na usawa. Ninapambana na ufisadi nchini nikiamini kwamba ustawi wa taifa letu unahatarishwa na kukithiri kwa ufisadi nchini. Nitaendelea kuamini hivyo, na ni imani ambayo, ikibidi, niko tayari kufa nikiipigania.”

Maneno hayo yangekuwa si ya kuomba radhi; bali ni ya kuthibitisha kutotetereka katika imani yake ya kutetea haki na usawa, ya kutetea wanyonge.



Spika Samwel Sitta
Nimalizie safu yangu kwa kusema kwamba alichokifanya au anachokifanya Spika Sitta na wabunge wenzake wanaopambana na ufisadi, ni kuisaidia CCM ijione ilivyo na ijirekebishe.

Ni bahati mbaya tu kwamba walio wengi ndani ya chama hicho hawazisomi alama za nyakati, kwa sababu ya kulewa fedha za mafisadi!

Kwa maneno mengine, ufumbuzi si kumsulubu Spika Sitta na kumfukuza uanachama. Ufumbuzi ni CCM na Serikali yake kujitazama upya na kujisafisha kwa kuwaweka mafisadi wote pembeni. Kwa sababu tatizo si Sitta, tatizo ni chama kutekwa na mafisadi.

Naambiwa kwamba mkakati wa kummaliza Sitta kisiasa haujaishia Dodoma ulikokwama kwenye kikao hicho cha NEC; bali sasa unaelekezwa katika jimbo lake la uchaguzi ili asishinde ubunge mwakani.

Vyovyote vile; kwa nguvu yao ya pesa, mafisadi wanaweza kufanikiwa katika hilo, na yawezekana Sitta asirejee bungeni mwakani. Hata hivyo, jambo moja ni dhahiri. Jambo hilo ni kwamba, kwa jinsi ambavyo ufisadi na dhuluma vimekithiri nchini, kuuawa kisiasa kwa Sitta mmoja kutazaa Sitta wengine 16!

Kutazaa sita wengine 16, kwa sababu siku zote binadamu huusaka ukweli na siku zote ukweli hushinda.

Rais wa zamani wa Marekani, Abraham Lincoln alipata kueleza hivi, kwa njia ya swali, kuhusu ukweli: “Je, mbwa ana miguu mingapi kama utaamua kuuita mkia wake kuwa ni mguu? Jibu lake ni miguu minne; kwani mkia hauwi mguu kwavile tu umeamua kuuita hivyo”.

Ndugu zangu, CCM itafanya kila jaribio la kuwasafisha mafisadi, lakini hawatasafishika kwavile tu CCM inataka wasafishwe! Kumbuka na tafakari maneno yangu haya!
 
Back
Top Bottom