Sitta awasilisha ombi la kuahirisha bunge April 28, kwa JK

Mwikimbi

JF-Expert Member
Mar 8, 2008
1,762
825
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta, amewasilisha maombi kwa Rais Jakaya Kikwete, kuomba Bunge hilo liahirishwe Aprili 28, mwaka huu.

Kadhalika, Sitta ameomba nyongeza ya muda wa Bunge hilo baada ya siku 70 za kisheria kumalizika.

Aliyasema hayo alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza kikao cha faragha baina yake na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo na Mufti wa Tanzania, Sheikh Mkuu, Issa bin Shaaban Simba, jana.

Sitta alisema juzi alikutana na Rais Kikwete na kupeleka mapendekezo ya kuahirishwa kwa Bunge hilo ili kupisha Bunge la Bajeti na Baraza la Wawakilishi.

"Jana (juzi), nilikutana na Rais na kumueleza hali ilivyo ili atafakari namna ya kuongeza muda wa Bunge hilo baada ya siku 70 kumalizika Aprili 28, lakini iwe baada ya Bunge la Bajeti kumalizika," alisema Sitta.

Kwa mujibu wa Sitta, siku 70 zilizopangwa kisheria kwa Bunge Maalumu la Katiba zinamalizika Aprili, 28 mwaka huu.

Hivyo, alishauri Bunge la Bajeti lianze hadi Juni 30 na wabunge wapewe mwezi mmoja kwenda majimboni na kurudi Agosti, mwaka huu, kuendelea na Bunge Maalumu la Katiba.

Alisema kwa sasa Bunge hilo limegawanyika kwenye kamati 12, ambazo zinajadili sura ya kwanza na sita zinazobeba sehemu kubwa na muhimu ya katiba, hivyo kazi iliyobaki siyo nzito kama iliyopo kwa sasa.

"Matumaini yetu ni kuwa kwa muda, ambao Rais ataongeza kwa mujibu wa sheria, rasimu inayopendekezwa na Bunge itakamilika na baadaye Kamati ya Uandishi itaandika katiba inayopendekezwa na kukabidhiwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar na baadaye kupigiwa kura na wananchi wenye sifa," alisema Sitta.

Alisema kwa jinsi alivyoongea na Rais, uwezekano wa Bunge hilo kuahirishwa kupisha Bunge la Bajeti ni mkubwa ili kuwezesha serikali kutekeleza bajeti na isikumbwe na msukosuko katika utendaji wa kila siku.

"Kama sheria inavyonitaka nimeieleza Ikulu mapendekezo yetu kuwa mchakato upishe Bunge la Bajeti na Rais aangalie uwezekano wa kuongeza muda wa Bunge la Katiba…ameelekea kukubali na tutajua hilo kwenye tangazo kwenye Gazeti la Serikali la nyongeza ya muda," alisema Sitta.

Aidha, sura 15 za Rasimu ya Katiba zilizobaki siyo ngumu hivyo hazitachukua muda mrefu katika majadiliano kwa hivyo uwezekano wa kumaliza kwa haraka ni mkubwa.

MWELEKEO WA BUNGE KWA SASA
Sitta alisema siku ya Alhamisi, wenyeviti wa Kamati 12 zenye wajumbe 52 kila moja watawasilisha taarifa zao kwa mtiririko na mjadala kuanza wiki ijayo.

Alisema katika mjadala huo atajitahidi kuzingatia wajumbe wote kutoa mchango wao kulingana na makundi wanayowakilisha ili kuweza kuwa na maboresho mazuri na mwisho wa siku watapiga kura ya kuamua juu ya sura hizo.

Alisema sura ya kwanza na sita ni muhimu kwa kuwa zimebeba mambo ya msingi wa Taifa ikiwa ni pamoja na muundo wa serikali, utendaji wa mahakama.

SURA HIZO ZINAELEZAJE
Suya ya kwanza ya Katiba ina sehemu za Jina; Mipaka; Alama; Lugha na Tunu za Taifa ikiwa na vipengele vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Eneo la Jamhuri ya Muungano; Alama na sikukuu za Taifa; Lugha ya Taifa na lugha za alama na Tunu za Taifa.

Sehemu ya pili ni mamlaka ya wananchi; Utii na Hifadhi ya Katiba yenye sehemu za Mamlaka ya wananchi; watu na serikali; Ukuu na Utii wa Katiba na Hifadhi ya Utawala wa Katika.

Sura ya sita Rasimu hiyo inazungumzia Muundo wa Jamhuri ya Muungano yenye vipendele vya Muundo wa Muungano ambavyo ni Muundo wa Muungano; Vyombo vya utendaji vya Jamhuri ya Muungano; Mamlaka ya Serikali ya Muungano.

Mengine ni Mambo ya Muungano, Nchi Washirika; Mamlaka ya Nchi Washirika, Mahusiano kati ya Nchi Washirika; Mawaziri Wakaazi; Mamlaka ya wananchi na Wajibu wa kulinda Muungano.

Source: Nipashe
 
Back
Top Bottom