BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,790
- 288,006
- Asema ni biashara ya kipumbavu na wizi mtupu
na Mwandishi wetu
SIKU chache baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, kusajili tuzo ya malipo ya fidia kwa Kampuni ya kufua umeme ya Dowans, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Samuel Sitta, ameibuka na kutoa madai mazito dhidi ya kampuni hiyo, akisema ni ya kikundi cha wezi wachache, wanaopaswa kulaaniwa na kila mzalendo mwenye mapenzi mema kwa taifa hili.
Septemba 28 mwaka huu, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Emilian Mushi, alitupilia mbali pingamizi la baadhi ya wanasiasa na wanaharakati waliotaka kulizuia Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco), lisilipe dola za Marekani milioni 65 (sh bilioni 94) kwa Dowans Tanzania kama ilivyoamuliwa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa migogoro ya Kibiashara (ICC).Tuzo hiyo ilitolewa Novemba 15, mwaka jana na Januari 25 mwaka huu, Dowans iliwasilisha ombi lake la kutaka Mahakama Kuu ya Tanzania iisajili lakini baadhi ya wanasiasa na wanaharakati walifungua kesi Mahakama Kuu kupinga tuzo hiyo isisajiliwe.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili jana kwa njia ya simu, Sitta ambaye ni miongoni mwa makada maarufu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliokuwa mstari wa mbele kutaka Dowans isilipwe mabilioni hayo, alisema kuwa msimamo wake upo pale pale na kwamba atapambana hadi mwisho."Sikiliza kijana, mbona mnakuwa kama hamna uzalendo, Dowans ni biashara ya kipumbavu…nawashangaa hata hao wanaotulaumu sisi kuwa ndio tumeifikisha nchi katika hatua hiyo ya kutakiwa kulipa deni hilo…Dowans ni wizi ambao kila Mtanzania anapaswa kuulaani ushenzi huo badala ya kushangilia," alisema Sitta ambaye ni Spika mstaafu wa Bunge la tisa.
Kada huyo ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Mashariki, alifafanua kuwa Tanzania iliingia mkataba na Kampuni ya Richmond ili ifue na kuzalisha umeme lakini cha ajabu humo humo kukafanyika wizi na mkataba huo hewa wakarithishwa Dowans.
"Nakwambia wazi labda kama na wewe gazeti lako hilo ni la kifisadi…lakini sisi Dowans hatukuwapa mkataba bali walirithi wizi wa kampuni hewa, hivyo hatuwezi kubebesha wananchi matatizo ya majizi halafu tukashangilia kuibiwa," alisema Sitta kwa hasira.
Sitta, maarufu kama Spika wa Kasi na Viwango, katika Bunge lililopita alisimama imara pamoja na baadhi ya wabunge waliojipambanua kama wapambanaji wa ufisadi kupinga Kampuni hewa ya Richmond (sasa Dowans) na kuishinikiza serikali ivunje mkataba huo.
Akifafanua zaidi, alisema kuwa Watanzania wanapaswa kuwa na uzalendo wa kulipigania taifa lao badala ya kukatishwa tamaa kwa kutishwa kuwa Dowans lazima ilipwe. Hivyo, alidai kuwa mapambano ya kupinga malipo hayo yasifanyike bado yanaendelea.
"Kwanza nikuhakikishie huu si mwisho wa mapambano…Dowans kulipwa ni sawa na kuhalalisha ushenzi wa majizi hayo…hatuwezi kushangilia, nitapinga hadi mwisho…unanielewa, hatuwezi kulipa wezi," alisisitiza Sitta na kukata simu.ICC iliitia hatiani Tanesco kwa kosa la kuvunja mkataba na Dowans iliyokuwa ikitetewa na wakili wa kimataifa Kennedy Fungamtama na ikaiamuru iilipe tuzo hiyo na riba ya asilimia 7.5.
Hatua hiyo ya kuchelewesha malipo ya tuzo hiyo itaifanya Tanesco sasa kulipa kiasi kikubwa zaidi, kwani riba imekuwa inaongezeka. Hadi siku hukumu inatolewa na Jaji Mushi, Dowans ilikuwa inastahili kulipwa na Tanesco sh bilioni 113 badala ya sh bilioni 94.