Sitta atema cheche Jumuiya Afrika Mashariki

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, amependekeza kuwepo kwa mfumo wa kugawana nafasi sawa za ajira (quota system) katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Akizungumza katika Baraza la Mawaziri jijini hapa juzi, Sitta alisema wazo hilo ni utekelezaji wa miongozo ya kikao cha 19 cha Baraza la Mawaziri.
Alisema wakati wa mkutano sekretariati ya EAC ilipewa jukumu la kutayarisha mchanganuo kabambe kuhusu ugawanaji wa nafasi ikiwemo mapendekezo ya kutumia quota system wakati wa mchakato wa kuajira wafanyakazi.
Sitta ambaye ni mwenyekiti anayemaliza muda wake wa Baraza la Mawaziri la EAC, alisema mkakati huo ni sehemu ya suluhisho la muda mrefu katika changamoto zinazoikabili jumuiya hiyo.
Alisema jumuiya hiyo imekuwa ikikua kwa kasi na kusababisha hitaji kubwa la raslimali watu kuratibu na kufanikisha michakato ya ushirikiano.
“Ili kulitafutia ufumbuzi suala hili, inatakiwa kufanyika mapitio kamilifu kama ilivyoelekezwa na baraza,” alisema Waziri Sitta.
Alizungumzia haja ya sekretariati kuharakisha utekelezaji wa maamuzi ili kuruhusu Baraza la Mawaziri kujikita katika mikakati na masuala ya sera ili kuwezesha maendeleo ya jamii kasi inayotarajiwa pamoja na kuhakikisha matokeo yake.
Kauli yake imekuja wakati kukiwa na malalamiko kwamba baadhi ya nafasi nyeti katika sekretariati hiyo ya Afrika Mashariki zikiwa zimeshikwa na Wakenya, wakifuatiwa Waganda, wakati nafasi za ngazi za chini zikiwa zinashiliwa na wafanyakazi kutoka nchi nyingine.
Hata hivyo, Waziri Sitta, alisema jumuiya hiyo imekuwa ikitekeleza miradi kadhaa kama vile mipango ya ujenzi wa barabara, reli na umeme ili kuhakikisha kwamba jamii wanajikwamua kutokana na matatizo hayo.
Kwa mujibu wa Sitta, ufinyu wa bajeti ni changamoto nyingine inayozuia utekelezaji wa mipango ya miradi mbalimbali ya maendeleo.
Alisisitiza umuhimu wa kuangalia mfumo mzima wa bajeti kuwa unahitajika katika kukabiliana na baadhi ya changamoto katika ukanda huo wa jumuiya.
Pia aliipongeza EAC kwa kufanikiwa kutekeleza Mkataba wa Soko la Pamoja ulioanza Julai mwaka huu.
Ujumbe wa ngazi ya juu wa jumuiya hiyo unatarajiwa kuanza mazungumzo kuhusu kuwa na mkataba wa sarafu moja unatarajiwa kuanza Januari mwakani.
Alielezea kufurahishwa kwake kuhusu maendeleo ya miradi ya pamoja ya jumuiya kama vile ujenzi wa barabara ya Arusha – Namanga hadi Arthi, ambao alisema unaendelea vizuri ukitarajiwa kukamilika Machi mwakani kwa upande wa Kenya na Julai mwakani kwa upande wa Tanzania.
 
Back
Top Bottom