Sitosahau nilikiona cha moto urithi wa mali za babu

SEHEMU YA 19

ILIPOISHIA
“Mmmh…! Mganga akaguna. Baada ya kuwaza kidogo aliniambia.
“Nakumbuka kulikuwa na msichana alikuwa akimsumbua sana babu yako. Huyo anaweza kujua siri ya mali ya babu yako. Babu yako alikuwa akimpenda na alifikia kumshirikisha kwenye biashara zake”
Mganga aliponimbia hivyo nilishituka, nikamuuliza.
“Aliwahi kukutajia jina lake?’
“Aliwahi kunitajia lakini muda ni mrefu nimelisahau”
“Sio Ummy?”
“Sawasawa. Ni Ummy Nasri…”
“Lakini huyo msichana si alikufa?”
“Mimi sijui kama alikufa”
Hapo sasa nikaona nimueleze mkasa mzima wa Ummy Nasir.
SASA ENDELEA
Wakati wote nilipokuwa nikimueleza mganga huyo, alikuwa amenikazia macho kama vile nilimueleza kitu kigeni ambacho hakuwahi kukisikia.
Nilipomaliza maelezo yangu aliniambia
“Subiri”
Alichukua kipande cha ubao akauchorachora vistari kwa kutumia chaki. Alichora mara ya kwanza akafuta. Akachora mara ya pili akafuta. Alipofuta mara ya tatu alifungua kitabu akasoma kisha akatikisa kichwa.
“Nikwambie ukweli. Mimi ni mganga na
nimeshafanya kazi hii kwa zaidi ya miaka thelathini sasa, sijawahi kuona ramli yangu ikiwa na kiza kama leo” Mganga akaniambia.
Nilishituka kidogo.
“Sijakuelewa. Unaponiambia ramli yako ina kiza una maanisha nini?” nikamuuliza.
“Ninamaanisha kwamba sina ninachoona. Ramli imefunga. Hapa ninaona kiza kitupu”
“Inapokuwa hivyo inadhihirisha nini?”
“Inadhihirisha kwamba tatizo lako halitambuliki au kwa maneno mengine nimeshindwa kulifumbua”
“Ni kwa sababu gani?”
“Sijui”
“Kwa hiyo huyu msichana atakuwa ni mzuka kama alivyonieleza mwenyewe”
“Inawezekana”
“Sasa kama yeye ni mzuka ni kwanini ananitokea mimi?”
“Hilo jambo liko nje ya elimu yangu. Siwezi kujua”
“Kwa hiyo unanishauri nifanye nini?”
“Kwa tatizo kama hili, mimi ninakushauri nenda polisi. Huyu mwanamke atakamatwa na atajieleza”
“Sidhani kama polisi watashughulikia suala hili”
“Mimi naamini watalishughulikia”
“Basi nitakwenda kuripoti polisi”
Mazungumzo yangu na mganga huyo yakaishia hapo hapo. Wakati niko kwenye gari nikirudi, niliamua nifuate ushauri wa yule mganga wa kwenda polisi kwa sababu sikuwa na mahali pengine pa kwenda kuomba msaada.
Wakati ninakwenda kwa mganga huyo nilikuwa na furaha kutokana na imani kuwa tatizo langu lingepatiwa ufumbuzi. Lakini wakati ule narudi nilikuwa nimepatwa na wasiwasi hasa kutokana na maelezo ya mganga kwamaba anaona kiza kitupu.
Kwanini aniambie anaona kiza kitupu? Tafsiri ya kiza ni kitu gani? Kifo au uzima? Nilikuwa nikijiuliza bila kupata jibu.
Licha ya mganga huyo kutonifumbulia chochote juu ya kitendawili cha Ummy,
jambo mmoja lilikuwa wazi kwamba lile suala lilikuwa gumu na si la mzaha.
Niliamua niende kituo cha ppolisi cha Kinondoni. Nilipofika nilikutana na polisi waliokuwa kaunta ambao baada ya kuwaeleza tatizo langu walinipeleka ofisini kwa Inspekta Amour.
“Una tatizo gani?” Inspekta huyo akaniuliza.
Nikamueleza. Maelezo yangu yalianzia kupigiwa simu na Ummy. Sikutaka kueleza kuhusu ziara yangu ya nchi tatu nilizozitemnbelea ambapo Ummy aliua watu watatu.
Nilimueleza inspekata huyo kwamba nimekuwa nikipigiwa simu na msichana ambaye sikuwa nikimfahamu akinitaka nikutane naye kwa ajili ya kunipa siri ya mali ya babu yangu aliyekuwa amefariki.
Nikaendelea kumueleza kuwa mara ya kwanza aliniita katika hoteli mmoja iliyoko Masaki ambako nilikwenda kumuona na kuzungumza naye.
Hapo pia sikutaka kueleza ukweli wa tukio hilo isipokuwa nilieleza kwamba nilizungumza na msichana huyo na akanitaka niende kwao Mwananyamala ili nikutane naye kwa mazungumzo zaidi.
Nikaeleza kuwa nilipofika Mwananyamala katika nyumba aliyonielekeza, nilitaja jina lake lakini watu walioniambia kuwa ni wazazi wake waliniambia kuwa Ummy alikuwa ameshakufa miaka mitano iliyopita..
Nilimwambia Inspekta huyo kwamba wazazi hao wa Ummy walinionesha picha zake na nikathibitisha kuwa Ummy niliyemuona alikuwa ni yeye lakini la kushangaza ni kuambiwa kuwa alishakufa miaka mitano iliyopita.
Nikaendelea kueleza kuwa baba yake alinipeleka katika kaburi aliloniambia kuwa ni la Ummy na hakutaka kukubaliana na mimi kwamba Ummy yuko hai..
“Lakini namba yake ya simu waliikubali. Mdogo wake Ummy aliniambia namba niliyowaonesha ilikuwa ya Ummy kweli” nikaeleza.
“Huyo msichana alinipigia tena simu akakubali kuwa yeye alikufa na kwamba ni mzuka uliokuwa unataka kunipa taarifa ya mali za babu yangu na la kunishangaza zaidi ameniambia kuwa ananipenda na anataka niwe mume wake. Haya mambo yameitia wasiwasi sana” nikamaliza.
ITAENDELEA
 
SEHEMU YA 20

ILIPOISHIA
“Sasa ulitaka tukusaidieje?” Inspekta huyo akaniuliza baada ya kumaliza maelezo yangu.
“Ninaiomba polisi ichunguze kuhusu huyu msichana na ikiwezekana akamatwe ili ajieleze ni nani. Nimepatwa na wasiwasi sana hasa baada ya kuambiwa kuwa alishakufa”
“Kazi ya jeshi la polisi nni kulinda
usalama wa raia na mali zao. Vile vile tunashughulikia masuala ya jinai. Kwa vile suala hilo linahusu usalama wako na linaweza kuingia pia katika jinai, tutakusaidia kufanya uchunguzi”
“Nitashukuru sana”
“Nipatie namba ya huyo msichana”
Nikampatia kachero huyo namba ambayo Ummy amekuwa akinipigia simu.
Nilipompa namba ya Ummy aliipiga na kuitega simu sikioni. Baada ya kusubiri kwa sekunde kadhaa aliniambia.
“Namba inaita lakini haipokelewi”
Akaiondoa simu sikioni na kuniambia.
“Twende huko nyumbani kwao”
SASA ENDELEA
Dakika chache baadaye, kachero huyo aliyeonekana kuipenda na kuithamini kazi yake alikuwa amenipakia kwenye gari la polisi tukielekea Mwananyamala.
Alilisimamisha gari mbele ya nyumba niliyomuonesha. Mzee Nasri alikuwa amekaa barazani kwenye kiti cha uvivu akisoma gazeti la lugha ya Kiingeza.
Tulishuka kwenye gari hilo tukamsalimia mzee huyo.
Baada ya salamu Inspeketab Amour alijitambulisha kwake kabla ya kumuuliza kama alikuwa anafahamu Ummy Nasri.
“Namfahamu. Ni mwanagu lakini alishakufa” Mzee akamjibu.
“Alikufa lini?”
“Alikufa miaka mitano iliyopita”
Inspekta Amour alinitazama kisha akayarudisha macho yake kwa yule mzee.
“Unamfahamu huyu kijana?” akamuuliza.
“Huyu kijana aliwahi kuja juzi akatuambia kuwa alionana na marehemu lakini hilo jambo tulilipinga sana kwa sababu marehemu alishakufa”
“Ana uhakika kwamba alikutana na binti yako unayedai kuwa amekufa na amekuja kutoa ripoti kituo cha polisi hii leo. Amedai kuwa huyo msichana anamsumbua na kumsababishia hofu kwani kila mara anampigia simu. Hiyo ndiyo sababu tumekuja kwako ili tupate ukweli”
“Ukweli ndio huo niliokueleza kwamba huyo binti alishakufa. Sasa sijui huyo anayemsumbua yeye ni nani”
“Huyo msichana amemwambia kuwa yeye ni mzuka wa Ummy”
Mzee akatikisa kichwa.
“Hakuna kitu kama hicho”
“Namba ya simu anayotumia huyo msichana umewahi kuiona?” Inspekta alimuuliza mzee huyo.
“Alituonesha juzi. Binti yangu alikubali kwamba ilikuwa namba ya marehemu lakini tangu alipokufa hadi leo ni miaka mitano. Mtu mwingine anaweza kupewa namba hiyo”
“Una picha za huyo marehemu??”
“Picha zipo”
“Ningeomba nizione”
Mzee akainuka na kuingia ndani.
Baada ya muda kidogo alitoka akiwa na mke wake pamoja na mdogo wake Ummy.
Mke wake na mdogo wa Ummy walitusalimia wakati yule mzee akituonesha picha za Ummy.
“Ummy mwenyewe ndiye huyu?” Inspekta akauliza.
“Ndiye yeye. Picha zote hizi ni yeye”
“Na mna uhakika kwamba alikufa??”
“Alikufa, naweza hata kwenda kukuonesha kaburi lake”
“Kwanza ningeomba unipatie picha mojawapo kwa ajili ya uchunguzi”
“Unahitaji ipi?”
Inspekata alichagua picha aliyoitaka. Mzee akaichomoa kwenye albamu na kumpa.
“Sasa nipeleke nikalione hilo kaburi lake”
Mzee akatupeleka. Baada ya Inspekata Amour kuliuona kaburi la Ummy alimwambia mzee Nasri.
“Kaburi nimeshaliona, sasa turudi nyumbani”
Tukarudi. Mke wa Mzee Nasri pamoja na binti yao walikuwa wakitusubiri barazani.
“Baba kuna mazingara yanafanyika siku hizi. Unaweza kuambiwa mtu fulani amekufa kumbe yuko hai. Sisi tulikwenda kwa mganga tukaambiwa Ummy yuko hai amechukuliwa msukule lakini baba yake amekataa jambo hilo” Mke wa mzee Nasri akatuambia.
“Tukiingiza imani kama hizo tutaharibu uchunguzi. Lakini vyovyote vitakavyokuwa ukweli utabainika muda si mrefu kwamba Ummy amekufa au amechukuliwa msukule. Tutajua tu….” Ispekta alimwambia.
“Huo uchunguzi utakuwa ni muhimu sana kwa sababu hilo jambo limeshaanza kututia wasiwasi” Mke wa mzee Nasri alisisitiza.
“Sawa. Hivi sasa tunakwenda katika kampuni ya simu ili tujue ni nani anayetumia hii namba ya Ummy”
“Naamini utampata mtu aliyezusha huu utata” Mzee Nasri akatuambia kabla ya kuagana naye.
Tuliondoka na Inspekta Amour hadi katika ofisi ya kampuni ya simu inayomiliki namba ambayo Ummy amekuwa akinipigia.
Baada ya Amour kujitambulisha aliomba aoneshwe usajili wa namba hiyo.
Sekunde chache tu kompyuta ya kampuni hiyo iliutoa usajili wa namba ya Ummy pamoja na picha yake. Kitu ambacho kiliniacha hoi na pengine kilimuacha hoi Inspekta Amour ni kuona kuwa usajili huo ulikuwa na jina la Ummy Nasri na picha ya kitambulisho pia ilikuwa ya Ummy.
Ndipo maswali yalipoanza.
“Hii namba ilisajiliwa lini?” Inspekta Amour akauliza.
“Kwa mara ya kwanza namba hii ilisajiliwa miaka sita iliyopita. Baada ya kutumika kwa mwaka mmoja iliacha kutumiwa kwa karibu miaka mitano, tukaifuta”
“Baada ya kuifuta nani alikuja kuirudisha?”
“Ni mhusika huyo huyo, alikuja mwezi uliopita akaitaka namba yake. Kwa vile hatukuwa tumeiuza kwa mtu mwingine tukampatia na hivyo alifanya usajili upya”
“Huyo huyo Ummy Nasir ndiye aliyefanya usajili upya?”
“Ndiye huyo huyo kama ambavyo picha yake inaonekana”
ITAENDELEA
 
SEHEMU YA 21

ILIPOISHIA
Kitu ambacho kilitushangaza zaidi mimi na Inpekta Amour ni kuwa tarehe ile ile ya usajili wa mara ya pili ndiyo tarehe hiyo hiyo ambayo Ummy alianza kunipigia simu. Kumbukumbu za tarehe zilikuwa bado zipo kwenye simu yangu.
“Sasa tunaomba utupatie namba nyingine ambazo zilimekuwa zikiwasiliana na namba hii” Inspekata Amour akatoa ombi jingine.
Msichana baada ya kuangalia kwa makini alisema.
“Hii namba tangu iliposajiliwa kwa mara ya pili rekodi yake inaonesha kuwa iliwasiliana na namba moja tu”
Alipoitaja namba hiyo ilikuwa ni namba yangu mimi.
Amour akanitazama kwa mshangao kabla ya kuuliza swali jingiine.
“Ilifanya mawasiliano mara ngapi?”
“Mara tano”
SASA ENDELEA
Inspekta Amour akanigeukia mimi.
“Mlifanya mawasiliano mara tano?” akaniuliza.
“Nafikiri inaweza kufika mara tano”
“Inaonekana kama aliifufua namba yake ili kukupigia wewe tu”
“Sasa swali, katika kipindi chote cha miaka mitano alichoacha kutumia hii namba alikuwa wapi?”
“Ndicho hicho kipindi anachodaiwa kuwa alikufa lakini usajili wake unaonesha kuwa hakuwa amekufa miaka mitano iliyopita kwani alikuja mwenyewe kuifufua namba yake”
Wakati tukiwa garini tukirudi kwa mzee Nasri, Amour aliniambia.
“Nina mashaka na madai kuwa Ummy alikufa”
“Kwa hiyo wazo la kuwa ni mzuka kama alivyoniambia yeye halina ukweli?”
“Mimi kama polisi siwezi kukubaliana na wazo kama hilo”
“Pale kwao wanasisitiza kuwa Ummy alishakufa na hata majirani niliowauliza wameniambia kuwa Ummy alikufa kweli”
“Sasa kama Ummy alikufa kweli, yule aliyekwenda kuisajili ile namba ni nani?”
“Ndiyo maana ninaliona wazo la huo mzuka linahitaji kufanyiwa kazi”
“Hivi wewe unaamini kuwa mtu aliyekufa anaweza kuibuka tena na kuwa mzuka?”
“lisemwalo lipo. Ni vizuri jambo hili lichunguzwe”
Tulipofika kwa mzee Nasri tulishuka kwenye gari. Mzee Nasri hakuwepo barazani. Amour akabisha mlango wa nyumba yake.
Mzee Nasri akatoka.
“Karibuni” akatuambia.
Safari hii alitukaribisha sebuleni.
Baada ya kuketi Amour alimwambia.
“Tumekwenda katika kampuni ya simu tumeambiwa kuwa usajili wa ile namba ni wa mwanao Ummy”
“Inawezekana. Ile namba aliisajili yeye mwenyewe”
“Tuliambiwa aliisajili kwa mara ya kwanza miaka sita iliyopita. Baadaye alacha kuitumia kwa miaka mitano. Hivi karibuni alikwenda kuifufua kwa sababu namba yenyewe ilikuwa imefutwa”
“Alikwenda kuifufua nani?” Mzee akauliza akiwa amemkazia macho Inspekta Amour.
“Alikwenda kuifufua Ummy mwenyewe. Tumeoneshwa kitambbulisho chake na siku hiyo hiyo alimppigia huyu kijana”
“Hilo jambo haliwezekanai. Bado nasisitiza kuwa Ummy amekufa… Ummy amekufa…”
“Mzee huwezi kufufua namba ya mtu mwingine. Ni lazima uoneshe kitambulisho chako ili utambulike kuwa wewe ndiye mwenyewe”
Niliona jasho likimtoka yule mzee.
“Sijui niseme nini..!” akajisemea peke yake.
“Itabidi tulifukue kaburi la Ummy” Ispekata akamwambia.
Mzee akamkazia macho tena Inspekta.
“Kwanini?”
“Kwa sababu kuna madai kuwa Ummy hakufa. Na kama itathibitika kuwa Ummy hakufa anaweza kukabiliwa na kosa la jinai”
“Kama italazimika kuwa hivyo, mimi niko tayari kuruhusu kaburi lake lifukuliwe ili mtibitishe kuwa mwannangu alikufa”
Mzee akanitazama kwa kunilaani. Alikuwa kama anayejiambia mimi ndiye niliyeyaleta yote yanayotokea.
Siku ya pili yake kikosi maalum cha polisi kikiongozwa na Inspekta Amour kilipewa kibali na mkuu wa polisi wa wilaya, cha kulifukua kaburi la Ummy kwa madai kuwa Ummy hakuwa amekufa.
Tulifika katika eneo hilo la makaburi saa nne asubuhi. Mzee Nasri na familia yake walikuwa wamesimama pembeni wakiangalia. Uso wa Mzee Nasri ulikuwa umefadhaika. Kitendo cha kufukuliwa
kaburi la mwanawe kilikuwa kimemkera.
Mkewe na mdogo wake Ummy wallikuwa
na mawazo tofauti. Wao walitaka kaburi hilo lifukuliwe ili wathibitishe ukweli wa mambo.
Kulikuwa na daktari kutoka hospitali ya
Muhimbili ambaye aliletwa kwa ajili ya kuuchunguza mwili utakaopatikana ndani ya kaburi hilo.
Kazi ya kulifukua kaburi hillo ilianza saa nee na dakika tano.
Kwa vile wafukuaji walikuwa polisi wawili, baada ya nusu saa tu kaburi hilo likawa wazi.
Makaburi ya kiislkamu yanakuwa na mfereji mwembamba unaolazwa mwili wa marehemu. Mfereji huo unaoitwa mwanandani hufinikwa na ubao wakati marehemu anapozikwa.
Ule ubao ulikuwa umeshaanza kuoza. Lakini sanda ya marehemu ilikuwa bado ipo ingawa ilikuwa imefubaa.
Polisi waliokuwa wamevaa mipira waliutoa mwili huo na kuuweka juu ya kaburi kisha wakaifungua ile sanda upane wa kichwani.
ITAENDELEA
 
SEHEMU YA 22
ILIPOISHIA
Macho ya watu wote yakaelekea kwenye mwili huo. Polisi hao waliufungua uso wa marehemu huyo. Ingawa ngozi yake ilikuwa nyeusi kwa sababu ya kukaa ndani ya kaburi kwa muda mrefu haikuwa imeharibika.
Uso wake ulikuwa mwembamba na uliosinyaa lakini haukunizuia kugundua kuwa ulikuwa na sura ya Ummy.
“Hebu mtazameni, huyu ndiye maiti wenu?” Inapekta Amour akawauliza wazazi wa Ummy.
“Ndiye yeye” Mzee Nasri akajibu haraka.
Polisi mmoja aliyekuwa na kamera ya kuchukua alama za vidole alipiga picha alama za viganja vya Ummy. Polisi mwingine aliupiga picha uso wake. Daktari naye aliuchunguza mwili huo na kukata kipande cha ngozi yake ya mkono.
Baada ya uchunguzi huo kumalizika, mwili huo ulirudishwa kwenye kaburi na kufukiwa tena
Daktari akawambia watu kwamba atakuwa na matokeo kamili ya uchunguzi wake baada ya saa sita. Polisi walioupiga picha mwili huo wakasema watakamilisha uchunguzi wao baada ya saa tatu.
Tukaondoka.
SASA ENDELEA
Inspekta Amour alinirudisha nyumbani kwangu akanitaka nifike kituo cha polisi asubuuhi ya kesho yake ili nionanne naye.
Baada ya kuagana naye, Inspekta huyo aliondoka. Niliridhika sana na hatua alizochukua. Alikuwa ni miongoni mwa makachero wa polisi niliowakubali sana. Alikuwa akitambua wajibu wake kama polisi mpelelezi.
Hata hivyo bado niliona kitu kama ukungu katika uchunguzi huo wa polisi. Dalili kwamba huenda tukajikuta tupo njia panda katika uchunguzi huo ni kule kukuta maiti ya iliyoonekana kuwa ni ya Ummy kwenye kaburi lililofukuliwa.
Nilijiambia kama itathibitika kuwa aliyezikwa ni Ummy Nasir, moja kwa moja yule msichana anayenipigia simu atakuwa ni mzuka wa Ummy na ndio uliokwenda kusajili namba ya simu kwa ajili ya kunipigia mimi.
Na kama itathibitika kwamba yule si Ummy, basi Ummy atakuwa yupo hai na ndiye aliyeuawa watu waliokuwa wakidaiwa na babu yangu, na ndiye
huyo huyo aliyekwenda kusajili namba ya simu.
Kwa vyovyote itakavyokuwa, niliendelea kujiambia, huenda Ummy huyo asiwe na nia njema na mimi. Kama amedai anaijua siri ya mali ya babu yangu huenda anataka kuniua ili aweze kumiliki mali hizo.
Shaka hii ilinijia baada ya kuona ameshaua watu waliokuwa wanadaiwa na babu yangu bila kueleweka dhamiri yake ilikuwa nini.
Lakini kama utakuwa ni mzuka, suala litakuwa zito zaidi.
Usiku wa siku ile sikupata usingzi kwa kuwaza. Niliwaza mengi yaliyonikera moyo wangu lakini hatimae kulikucha salama.
Saa tatu asubuhi nikawasili kituo cha polisi cha Kinondoni na kuonana na Inspekta Amour.
Inspekta Amour alinikaribisha kwenye kiti akaniuliza.
“Yule msichana hajakupigia simu?”
“Hajanipigia”
“Tumeanza kupata utata kuhusu suala lake. Tumefanya uchunguzi wa kutosha jana na leo lakini matokeo yamekuwa ni ya kutia shaka”
“Kwanini?”
“Uchuguzi wa madaktari wa Muhimbili kwa kutumia chembechembe za mwili wa marehemu na vielelezo vingine umebaini kuwa ule ulikuwa mwili wa Ummy…”
Nilikuwa niimemkodolea macho Inspekta huyo kumsikiliza. Akaendelea.
“Sasa utata unakuja kwa sababuni hata uchunguzi tuliofanya sisi unaonesha kuwa mtu anayekupigia simu ni Ummy huyo huyo ambaye ameshakufa. Alama zake za vidole zilizoko katika usajili wake
na alama tulizozichukua jana katika
viganja vyake zinafanana. Hii inaonesha kuwa ni Ummy huyo huyo!”
“Una maana kwamba alama za vidole za watu hazifanani?”
Inspekta Amour akatikisa kichwa.
“Alama za vidole za binaadamu hazifanani kabisa. Kila mtu ana alama zake”
“Hata kama watachunguzwa watu milioni moja, watakutwa na alama za vidole tofauti?”
“Hata watu milioni kumi, wanaweza kufanana sura tu lakini alama zao za vidole hazifanani. Kila binaadamu anakuwa na alama zake mwenyewe”
“Hicho ni kitu cha ajabu sana”
“Ndiyo maumbile yetu binaadamu. Na wataalamu waligundua hilo. Ndiyo maana alama za vidole zimekuwa kielelezo muhimu cha kumkamatisha mhalifu”
“Mungu ni muweza sana”
“Unaiona ile mistari ya pundamilia?”
“Ndiyo, niimeshawahi kuiona”
“Unaweza kuiona kama inafanana lakini ile pia haifanani. Kila punda milia ana
aina yake ya mistari, hata wawepo pundamilia milioni kumi, watakuwa na mistari tofauti”
“Hilo sijawahi kulisikia”
“Ndiyo nakueleza mimi ili uone maajabu ya Mungu, si katika alama za vidole za binaadamu tu bali tofauti zipo hata katika alama za wanyama”
“Nimekuelewa Inspekta. Sasa hili suala la Ummy unalifikiriaje?’
“Ndiyo nilikuwa nataka kukueleza kwamba limekuwa suala lenye utata. Mtu ambaye imethibitika kuwa amekufa na kuzikwa miaka mitano iliyopita lakini kunakuwepo na ushahidi kuwa yuko hai. Hili jambo ni la ajabu sana”
“Niliwahi kukwambia kwamba inawezekana kuwa ni mzuka wa Ummy”
“Suala hilo la kiimani hatuwezi kuliingiza
katika uchunguzi. Kazi yetu haiamini kuwepo kwa mizuka”
“Sasa atakuwa ni nani yule?’
“Siwezi kusema ni nani kwa sababu hatujamthibitisha ila wewe utakuwa ni nguzo muhimu katika uchunguzi wetu wa awamu ya pili. Nisikilize kwa makini”
“Ndiyo”
“Wakati wowote atakapokupigia simu, kubali kukutana naye halafu tupigie simu ili tufike mahali hapo. Pale mtakapokutana tu tunamkamata hapo hapo”
“Nafikiri hilo litakuwa wazo zuri. Hapo mwanzo nilikuwa sitaki kukutana naye kwa sababu ya hofu lakini kama polisi mtakuja nitaweza kukutana naye”
“Tutakuja. Muulize angependa mkutane wapi”
“Mara nyingi anapenda tukutane mahotelini”
“Basi muache ataje yeye hoteli ambayo angependa mkutane”
ITAENDELEA
 
SEHEMU YA 23

ILIPOISHIA
“Alikuambia hivyo?”
“Ndiyo. Kwa kweli nilishangaa sana”
“Wewe ulimjibu nini?”
“Nilinyamaza kimya. Sikuwa na jibu”
“Milizungumzia mahali pa kukutana?”
“Ametaka tukutane Lux Hotel, kule Masaki”
“Saa ngapi?”
Saa nne, asubuhi hii”
“Sasa acha tujiandae tuje huko”
“Lakini Inspekta huu si utakuwa ni mzuka wa Ummy? Amejuaje kuwa tulifukua kaburi lake?”
“Hapo tutakapomkamata kila kitu kitajulikana”
Kama nitakutana naye ni lazima niwe karibu na polisi, nilijiambia kimoyomoyo.
SASA ENDELEA
“Sasa wewe wahi kufika hapo heteli kabla ya saa nne umsubiri yeye” Inspekta aliniambia kwenye simu.
“Mimi ndiyo najiandaa. Nitahakikisha ikifika saa tatu na nusu niko pale”
“Tafadhali usikae katika eneo lililojificha. Tunataka tukifika tukuone. Kama mtakaa katika eneo la wazi la hoteli itakuwa vizuri sana”
“Sawa”
Baada ya kumaliza kuzumngumza na Inspekta Amour. Sikungoja ifike saa tatu na nusu, niliondoka muda ule ule kwa gari langu.
Niliendesha kwa mwendo wa taratibu huku nikiwaza. Niliwaza kwamba endapo polisi watafanikiwa kumkamata yule msichana, kitendo hicho kitafichua mengi yaliyojificha.
Mengi yaliyojificha ni pamoja na mali za babu yangu ambazo zimekuwa ni kitendawili ambacho nimeshindwa kukitegua.
Kingine ambacho kingefichuka ni kuhusu Ummy mwenyewe ambaye mpaka muda ule tulikuwa hatujui kama alikuwa ni mzuka au alikuwa binaadamu.
Wakati niko njiani Inspekata Amour akanipigia simu.
“Umeshakwenda huko Masaki au bado?”
akaniuliza.
“Ndiyo niko njiani, ninakwenda”
“Ukifika tu utanipigia simu kunijulisha kuwa umekaa sehemu gani”
“Lakini na nyie msichelewe sana, msije mkamkosa. Mimi nimekubali kukutana naye kwa sababu yenu”
“Usiwe na wasiwasi. Tayari makachero watatu wameshatangulia huko”
“Sawa”
Inspekta akakata simu.
Haukupita muda mrefu nikaingia Masaki. Niliutafuta ule mtaa uliokuwa na hoteli ya Lux, nilipoupata nikalielekeza gari ilipokuwa hoteli hiyo.
Baada ya dakika tatu tu hoteli hiyo ikawa upande wangu wa kushoto. Wakati
nakata kona kuelekea kushoto, simu yangu ikaita tena. Kwa vile nilikuwa katika mwendo wa taratibu niliichukua na kutazama namba iliyokuwa inanipigia.
Nikaona namba ya Ummy!
Wakati naipokea ile simu nikamuona Ummy mwenyewe amesimama katikati ya njia mita chache tu mbele ya gari langu.
Alikuwa ameshika simu sikioni. Kumuona kwake kukanigutusha. Nikasema “Hello” kwenye simu huku nimemkodolea macho.
Vile alivyokuwa amesimama katikati ya njia, nilihofia kwamba ningeweza kumgonga kwa vile nilikuwa nimeshamkaribia. Nikafunga breki kusimamisha gari.
“Utaona leo! Utaona leo!” nikaisikia sauti yake ikisema kwenye simu.
Kumbe sikuwa nimekanyaga breki. Nilichokanyaga ni pedali ya mafuta. Gari lilifyatuka na kumgonga Ummy. Ummy akatoweka ghafla mbele ya macho yangu. Badala yake nikaona nimegonga nguzo mbili za umeme zilizokuwa zimebeba transfoma.
Mlipuko uliotokea hapo ulinizibua masikio. Nakumbuka kwa mara ya mwisho niliona moto mkali ukiwaka kama umeme. Hapo hapo fahamu zikanipotea.
Sikuweza kujua gari langu lilisesereka na kwenda upande gani lakini nilizisikia kelele za watu waliokuwa wakikimbia huku na huko. Baadaye nilisikia king’ora ambacho ama kilikuwa cha gari la zima moto au cha gari la hospitali kama si cha gari la polisi.
Nilikuja kuzinduka nikiwa katika chumba cha hospitali. Nilikuwa nimefungwa
bendeji sehemu mbali mballiza mwilli wangu kuanzia kichwani hadi miguuni.
Wakati nazinduka wauguzi na daktari, walikuwa wakishughulika na mimi. Karibu yangu niliona polisi mmoja alliyekuwa na bunduki.
“Oh umezinduka!” Daktari alipoona nimefumbua macho aliniuliza.
Sikumjibu kitu. Bado nilikuwa nikjiuliza nimefikaje pale hospitalli.
“Unajisikiaje?” akaendelea kuniuliza.
Nikatikisa kichwa changu.
“Sijisikii vizuri. Mwili wote unaniuma” nikamwambia.
“Maumivu yako sehemu gani zaidi?”
“Hizi sehemu zilizofungwa bendeji zinaniuma sana”
“Kuna baadhi ya sehemu umeshonwa baada ya kukatwa na vioo vya gari na kuna sehemu nyingine hazikushoneka, zina majeraha makubwa ya kukatwa na
vioo” Daktaria akaniambia.
Nikanyamza kimya na kuanza kuitafakari ile ajali.
“Tutakupatia tenbe za kutuliza
maumivu. Utajisikia vizuri” Daktari akaniambia.
“Nitashukuru”
Mara nikamuona Inspekta Amour akiingia katika chumba hicho.
Alipoona namtazama alimuuliza daktari kama angeweza kuongea na mimi.
“Mnaweza kuzungumza” alipata jibu kutoka kwa daktari.
“Pole sana” Inspekta akaniambia.
“Asante”
“Nini kimetokea pale”
“Kwa kweli palitokea kitu kama miujiza….”
ITAENDELEA
 
SEHEMU YA 24

ILIPOISHIA
Mara nikamuona Inspekta Amour akiingia katika chumba hicho.
Alipoona namtazama alimuuliza daktari kama angeweza kuongea na mimi.
“Mnaweza kuzungumza” alipata jibu kutoka kwa daktari.
“Pole sana” Inspekta akaniambia.
“Asante”
“Nini kimetokea pale”
“Kwa kweli palitokea kitu kama miujiza….”
SASA ENDELEA
Nilimueleza inspekta huyo hali iliyotokea pale. Inspekata Amour akashangaa.
“Una uhakika kwamba aliyekupigia simu ni Ummy na alikwambia kwamba utaona?”
“Nina hakika”
“Na una uhakika kwamba ulimuona amesimama mbele yako wakati unafika pale hoteli?”
“Nina uhakika”
“Tangu tulipooanza uchunguzi wa Ummy, namba ya Ummy imetegwa na kila anapopiga au kupigiwa simu inarekodiwa. Tutakwenda kampuni ya simu ili tuhakikishe kwamba ni namba ya Ummy iliyokupigia na pia tuhakikishe wakati alipokuwa anakupigia alikuwa karibu na wewe”
“Nilimuona mbele ya gari akiwa ameshika simu. Nikafunga breki ili nisimgonge. Kumbe nilikanyaga pedeli ya mafuta, nikamgonga. Nilipomgonga alitoweka pale pale, nikaona nimegonga nguzo ya umeme” nikamwambia Inspekta Amour kwa mkazo.
“Ni kitu kisochoeleweka lakini nitakwenda kwenye kampuni ya simu kufanya utafiti. Laiti tungeuona mwili wake uliogongwa tusingepata utata lakini mwili wa Ummy haukuwepo!”
“Alitoweka kimiujiza. Yule kweli si binaadamu, ule ni mzuka. Ulitaka
kuniua!” nikasema kwa jazba.
“Tulia upate matibabu. Tukio lililotokea ni kubwa”
“Nimekuelewa Inspekta”
Inspekta huyo akaniaga na kutoka.
Yule daktari pamoja na wauguzi wake nao waliondoka. Akabaki yule polisi aliyekuwa na bunduki ambaye sikujua alikuwa akisubiri nini.
Baadaye kidogo muuguzi mmoja alikuja na chano cha dawa. Akanipa tembe za kumeza kisha akanipiga sindano na kuondoka.
Tukio lile lililotokea lilikuwa limeushitua moyo wangu na kuniacha katika hali mbaya. Kila wakati ile picha ya kumuona Ummy akiwa amesimama mbele ya gari huku akiniambia.
“Utaona leo...utaona leo!” ilinijia akilini ikifuatiwa na ile picha ya kumgonga kisha ghfla akanipotea na kuona nimegonga nguzo ya umeme.
Zilikuwa picha zilizonisisimua na kunitia hofu ya kufa. Kama nilinusurika kufa pale, nilijua si muda mrefu Ummy ataniua kama alivyowaua wadaiwa wa babu yangu.
Nilijua kikubwa kilichompa hasira ni kugundua kuwa nilishirikiana na polisi kumuwekea mtego wa kumkamata. Bila shaka Ummy aligundua kuwa polisi walitaka kumkamata ndipo akaona
anikomoe.
Sikuweza kujua gari langu liliharibika kiasi gani na lilikuwa wapi. Na pia sikuweza kujua ule moto uliendelea kuwaka hadi muda gani na ulisababisha hasara ya kiasi gani.
Laiti ningejua kuwa tukio lile lingetokea, katu nisingekwenda kule Lux Hotel wala nisingekubali kumuwekea mtego Ummy wakati nikijua fika kuwa alikuwa mzuka.
Lakini nikajiuliza, Mzuka huo ulikuwa
una lengo gani na mimi?
Sikuweza kupata jibu mara moja.
Baada ya muda kidogo niliona polisi watatu wa usalama barabarani ambao walikuja kuchukua maelezo yangu.
Walitaka kujua jinsi ile ajali ilivyotokea, nikawaelezo lakini niliona wazi kuwa polisi hao hawakuamini maelezo yangu yote. Nusu waliyamini lakini nusu hawakuyaamini.
Kwamba yule msichana ambaye nilipanga na Inspekta Amour tumuwekee mtego alitokea mbele ya gari langu na kisha nikafunga breki na yakatokea yaliyotokea, polisi hao hawakuamini.
Lakini walitimiza jukumu lao la kuandikisha maelezo yangu kama
nilivyoyatoa wakaniambia niweke saini,
nikaweka saini.
Walipokuwa wanataka kuondoka niliwauliza hali ilivyokuwa baada ya ajali hiyo. Polisi hao walinieleza kwamba ajali hiyo ilikuwa kubwa na kwamba transfoma iliyokuwa katiika nguzo za umeme ililipuka moto na kusababisha nyaya za umeme kutoa cheche za moto na moto kusambaa katika eneo kubwa.
Walinieleza kuwa baadhi ya nyaya zilikatika kwa mlipuko na kuanguka chini.
Patashika iliyotokea ilisababisha shughuli kusimama kwa muda katika hotelli ya Lux ambapo wateja walikimbia ovyo kwa hofu.
Ile habari nayo ikazidi kunifadhaisha.
Nikajiambia huo mpango ulipangwa na polisi, mimi nilifuatisha tu maelekezo ya polisi.
Baada ya kupita kama saa nne hivi, Inspekta Amour akarudi tena pale hospitali.
“Ni kweli ulivyosema” akaniambia na kuongeza.
“Sauti ya Ummy imenaswa na amesikika akisema “Utaona leo!” Alikuwa akipiga simu kwenye namba yako. Vile vile mionzi ya simu yake ilionesha kuwa ilirushwa katika mnara mmoja na mionzi ya simu yako. Watu wa kampuni ya simu wameniambia hii inaonesha kuwa ni kweli mlikuwa karibu au mllikuwa katika eneo lile lile”
Inspekta huyo aliponiambia hivyo nikamuuliza kwa pupa.
“Umeamini sasa…umeamini sasa….? Yule msichana ni mzuka! Kama alikuwa pale, sasa yuko wapi? Mbona hakuonekana
tena?”
Inspekta Amour akanyamza kimya.
Nilikaa pale hospitali kwa siku tatu. Polisi aliyekuwa na bunduki alikuwa akibadilishana zamu na mwenzake kila baada ya saa nane. Baadaye niligundua kuwa polisi hao walikuwa wakinilinda mimi kwani nilikuwa chini ya ulinzi.
Asubuhi ya siku ya tano nilitolewa hapo hospitali. Nikapelekwa mahakamani moja kwa moja. Huko nilifunguliwa mashitaka ya kuendesha gari kwa uzembe, kugonga nguzo ya umeme na kusababisha hasara ya karibu shilingi milioni hamsini.
ITAENDELEA
 
SEHEMU YA 25
ILIPOISHIA
Kwa kweli nilishangaa kuona polisi wamenigeuka na kunifungulia mashitaka. Maelezo yalikuwa yamegeuzwa. Badala yake nimeshitakiwa kwa kuendesha kwa uzembe wakati
hapakuwa na uzembe wowote. Kilichotokea kilikuwa miujiza tu.
Kadhalika nilikuwa nimemgonga Ummy na polisi wamekwenda kampuni ya simu na kuthibitisha kuwa Ummy alinipigia simu na alikuwa mbele ya gari langu lakini hakutajwa kuwa nilimgonga.
Inspekata Amour sikumuona tena. Kweli polisi hana rafiki. Anakuwa rafiki yako pale anapotaka lake.
Baada ya kusomewa mashitaka hayo na kuyakana, upande wa mashitaka ulisisitiza kuwa nisipewe dhamana kwa sababu ninaweza kuingilia na kuharibu uchunguzi wao kwani uchunguzi wa tukio hilo ulikuwa bado unaendelea.
Nikapelekwa rumande.
Ile kesi iliendelea kuunguruma kwa miezi minne. Wakati wote huo nilikuwa nimewekwa mahabusi. Japokuwa uchunguzi wa polisi ulikuwa umekamilika, nilinyimwa dhamna kwa madai kuwa hasara niliyoisababisha ni kubwa na ningeweza kutoroka kama nitaachiwa kwa dhamana.
SASA ENDELEA
Inspekta Amour alikuwa ndiye shahidi wa kwanza aliyekuja kutoa ushahidi dhidi yangu. Aliieleza mahakama kuwa alinifahamu nilipokwenda katika kituo cha polisi anachofanyia kazi na kuripoti kuhusu msichana anayeitwa Ummy ambaye alikuwa ananisumbua.
Alieleza kuhusu uchunguzi wake na jinsi alivyogundua kuwa msichana huyo alikuwa ameshakufa lakini kulikuwa na vielelezo na ushahidi kuwa alikuwa hai.
“Kwa vile tulitaka kumkamata tulimwambia mshitakiwa kuwa atakapopigiwa simu na msichana huyo apange naye mahali pa kukutana na atuarifu ili twende tukamkamate” Alieleza Inspekata Amour.
Huku akiongozwa na Mwendesha Mashitaka, Amour aliendelea kueleza jinsi nilivyowaarifu kuwa Ummy alinipigia simu na nilipanga kukutana naye katika goteli ya Lux saa nne asubuuhi ambapo Amour aliandaa mtego wa kumkamata msichana huyo.
Lakini wakati polisi wanajiandaa kwenda hukohoteli ya Lux ndipo walipopata taarifa ya ajali ya gari iliyogonga nguzo ya umeme na kusababisha moto mkubwa kuwaka.
“Tulipofika hapo hoteli tulikuta aliyesababisha ajali hiyo alikuwa mshitakiwa. Tulikuta gari lake likiwa pembeni mwa nguzo zilizokuwa zinawaka huku mwenyewe akiwa amezirai. Tukafanya jitihada za kuokoa maisha yake” Inspekta Amour alisema.
Aliendelea kueleza kuwa baada ya kufanikiwa kunitoa kwenye gari na kunipakia kwenye gari la hospitali, kikosi cha zima moto kiliendelea na jitihada ya kuuzima moto huku wafanyakazi wa shirika la umeme wakiwa wameingia kazini kuzima umeme katika eneo hilo.
“Uchunguzi wetu umeonesha kuwa ajali ile ilitokana na uendeshaji wa kizembe wa mshitakiwa ambaye bila kuwa muangalifu na kujali sheria za usalama barabarani aligonga nguzo za umeme zilizokuwa zimebeba transfoma na kusababisha mlipuko wa moto” Inspekta Amour alimalizia hivyo maelezo yake.
Baada ya inspekta Amour, alikuja polisi wa usalama barabarani ambaye alionesha vipimo vya jinsi ajali ilivyotokea na kueleza kwamba niliacha njia sahihi na kwenda kugonga nguzo za umeme.
Shahidi mwingine alikuwa afisa mmoja wa shirika la umeme ambaye alieleza kuwa kugongwa kwa nguzo za umeme kulisababisha transfoma ya shirika hilo kulipuka na kuwaka moto.
Afisa huyo aliendelea kueleza kuwa hasara waliyoipata kutoka na tukio hilo ilifikia shilling milioni hamsini.
Wakati mashahidi hao wakitoa ushahidi wao, kichwa kilikuwa kinaniuma na kilikuwa kizito kwa mawazo yaliyochnaganyika na fadhaa hasa nilipowaza kwamba kesi ile ingenifunga
miaka mingi.
Baada ya mashahidi hao kutoa ushahidi wao, kesi iliahirishwa na kupangiwa tarehe nyingine ya usikilizaji.
Nilirudishwa mahabusi ambako
niliendelea kusota na kuwazia maisha yangu ambayo niliona yalikuwa yameshafikia kikomo kwani nilijjua kuwa nitafia jela.
Tarehe ya kuendelea kwa kesi hiyo ilipowadia nilipelekwa mahakamani nikiwa na hali mbaya ya kiafya kwani nilikuwa nimekonda. Kule mahabusi nilikuwa sili chakula vizuri kutokana na fadhaa.
Vile vile nilikuwa nikimlaani Inspekta Amour aliyekuwa amenigeuka ili kulinda kazi yake. Amour alifahamu fika kuwa ajali ile ilitokea kimiujiza na si mimi niliyeisababisha lakini alitoa maelezo ya kunitia katika hatia.
Kesi iliendelea kwa mashahidi mbalimbali kuja kutoa ushaidi wao. Katika kipindi chote wakati ushahidi unatolewa nilipewa nafasi ya kuuliza maswali kama kulikuwa na kitu sikubaliani nacho. Lakini ukweli ni kwamba nilishindwa kuuliza chochote.
Nilishindwa kwa sababu ya kutojua sheria na pia kupatawa na hofu.
Pale nilielewa ni kwanini hata wanasheria wanapokabiliwa na kesi wanaweka mawakili wa kuwatetea. Ni kwa sababu wao wenyewe licha ya kujua sheria wasingeweza kujitetea vizuri kwa sababu ya hofu.
Baada ya upande wa mashitaka kumaliza kuleta mashahidi wake, hakimu alisoma muhutasari wa kesi na kueleza kuwa nina kesi ya kujibu, kwa hiyo nilitakiwa nijitetee.
Niliulizwa kama nilikuwa na mashahidi, nikajibu kuwa sikuwa na shahidi yeyote.
Baada ya kujibu hivyo nilitakiwa niandae utetezi wangu ili kesi itakapoitishwa tena niweze kujitetea.
Baada ya hapo kesi ikaahirishwa na kupangiwa tarehe nyingine.
Siku hiyo ilipofika nilipelekwa tena mahakamani ambako nilijitetea kwa kuieleza mahakama kuwa tukio lile la ajali lilitokea kimiiujiza na kwamba ajali ile sikuisababisha mimi.
Hakimu aliandika maelezo yangu na kupanga tarehe ya kutoa hukumu.
Usiku wa siku ile ya kutolewa hukumu niliota ndoto mbaya sana. Niliota ninahukumiwa kifungo cha miaka thelathini jela na kutakiwa nililipe shirika la umeme shilingi milioni hamsini.
Nilikuwa sina pesa hizo nikajikuta nimetupwa jela. Baada ya kusota jela
kwa mika thelathini, eti nikaona ninatoka jela nikiwa mzeee ninayetembea kwa mkongojo!
Ndoto ile ilinishitua sana nikajua ndio
mambo yatakavyokuwa.
Asubuhi nilipelekwa mahakamani kwenda kusikiliza hukumu yangu.
Jalada langu lilipoitishwa nilipanda kizimbani na hakimu akanisomea hukumu aliyokuwa ameniandalia.
Alianza kuyataja mashitaka yaliyokuwa
yananikabili na akaeleza kuwa niliyakana mashitaka yote niliyosomewa.
Baada ya hapo akaanza kuuchambua ushahidi uliokuwa umetolewa na upande wa mashitaka. Alianza kuuchambua ushahidi wa Inspekta Amour.
Akaeleza kuwa ushidi huo anaukubali kwa vile mimi kama mshitakiwa nilishindwa kumhoji shahdi huyo chochote ikimaanisha kuwa nilikubaliana nao.
ITAENDELEA
 
SEHEMU YA 26

ILIPOISHIA
Akaja kwenye ushahidi wa polisi wa
usalama barabarani ulioonesha jinsi ajali ilivyotokea. Akaeleza kuwa pia amekubaliana na ushahidi huo uliokuwa na vipimo vya polisi ambao walipima
ajali hiyo.
Ushahidi wa afisa wa shirika la umeme uliotaja tathmini ya hasara iliyotokea nao ulichambuliwa na kukubaliwa.
Wakati wote niliokuwa nikisikiliza hukumu hiyo, moyo wangu ulikuwa ukienda mbio
kama saa. Na mara moja moja miguu yangu ilikuwa ikitetemeka.
Hakimu alipomaliza kuuchambua ushahidi wa mashahidi wote alisema
kuwa mashitaka yote matatu
niliyoshitakiwa yalikuwa yamethibitishwa bila kuacha shaka yoyote.
“Kutokana na ushidi huo, mahakama hii inakutia hatiani kwa makosa yote matatu.…”Hakimu aliniambia huku akinitazama.
SASA ENDELEA
Ingawa nilijua kuwa ningetiwa hatiani, nilishituka. Uso wangu ulionesha wazi kupigwa na butwaa.
Sasa hapo ilikuwa ni kutiwa hatiani tu, bado adhabu. sikujua ningekula miaka mingapi. Nikapatwa na kihoro kilichofanya nimkodolee macho hakimu.
“Adhabu” Hakimu alisema baada ya kuyageuza macho yake kutoka usoni kwangu na kulitazama jalada alilokuwa akilisoma.
“Baada ya kukutia hatiani ninakuhukumu adhabu ya kulipa faini ya shilingi laki tatu au kifungo cha miezi mitatu kwa kosa la kwanza ambalo ni la kuendesha kwa uzembe”
Hakimu alipenua ukurasa mwingine akaendelea kusoma.
“Pia ninakuhukumu kifungo cha miaka miwili kwa kosa la kugonga nguzo za umeme au ulipe faini ya shilingi milioni kumi”
Hakimu alisita akanitazama kabla ya kuendelea.
“Kwa kosa la tatu ambalo ni kulitia hasara ya shilingi milioni hamsini shirika la umeme, ninakuhukumu kifungo cha miaka mitatu jela au ulipe faini ya shilingi milioni kumi na tano pamoja na fidia ya shilingi milioni hamsini ambayo unatakiwa uwalipe shirika la umeme”
Hakimu alimaliza kupigilia msumari kwenye moyo wangu. Msumari huo ulikuwa umenimaliza kabisa.
Ilikuwa hukumu ambayo sikuitarajia kabisa. Nilijiuliza.
“Nitapata wapi pesa hizo za kulipia faini pamoja na fidia ya shilingi milioni hamsini?
Hapo ilikuwa ni kukubali tu kufungwa, hakukuwa na jingine.
“Kama utaweza kulipa faini na kulipa fidia utakuwa umeepukana na adhabu ya kifungo” Hakimu aliendelea kunifahamisha.
“Na kama utatumikia kifungo bado utalazimika kulipa fidia baada ya kifungo chako” hakimu alimaliza hukumu yake.
Nilihisi kijasho chembamba kikinitiririka kwenye uti wa mgongo wangu. Yalikuwa ni matokeo ya joto lililofumka ghafla mwilini mwangu.
Baada ya kusomewa hukumu hiyo nilikuwa kama niliyepatwa na wazimu. Nilikuwa nikisema peke yangu huku nikiwalaumu polisi hususan Inspekta Amour..
“Mshitakiwa utalipa faini na fidia au utatumikia kifungo ambapo utakapomaliza kifungo chako utalazimika kulipa fidia ya shilingi milioni hamsini” Hakimu akaniuliza baada ya kimya kifupi.
Sikuwa na jibu. Akili yangu ilikuwa imeruka. Pakapita ukimya wa karibu sekunde tatu kabla ya kuisikia sauti ya mwanamke ikisema.
“Mheshimiwa nitamlipia fainii pamoja na fidia ili asitumikie kifungo”
Maneno hayo yalinishitua, nikageuza uso wangu kuelekea upande sauti hiyo ilikotokea.
Ilitokea kwenye safu za watu waliokuwa wakisikiliza ile kesi. Kulikuwa na msichana mmoja aliyekuwa amesimama akimtazama hakimu. Nikahisi yeye ndiye aliyesema atanilipia faini pamoja na fidia.
“Hebu tokea hapa mbele” hakimu alimwambia.
Msichana huyo alitoka na kusimama karibu na meza ya mwendesha mashitaka. Nilipomtazama vizuri nilishituka nilipogundua kuwa alikuwa Ummy!
Alikuwa amevaa wigi lililompendeza na alipachika begani mkoba wa ngozi ya pindamilia uliokuwa umeendana na vazi allilokuwa amevaa.
“Hebu rudia ulichosema” hakimu akamwambia.
“Nimesema kwamba nitalipa faini na fidia aliyotozwa mshitakiwa”
“Umeisikiliza kesi vizuri?” hakimu akamuuliza.
“Ndiyo, nimeisikiliza”
“Umeisikia na hukumu niliyoitoa hapa?”
“Nimeisikia”
“Utamlipia faini ya kiasi gani na fidia ya kiasi gani?”
“Kiasi chote kitakachohitajika”
“Fidia peke yake ni shilingi milioni hamsini!”
“Ninajua mheshimiwa”
“Haya nenda kalipe”
Hakimu akamtaka polisi aliyekuwa akinilinda kufuatana na Ummy pamoja na mimi kwenda kulipa faini na fidia.
Sikuamini na sikujua kama Ummy angeweza kulipa kiasi cha pesa kilichohitajika. Lakini katika hali ya kushangaza Ummy alitoa katika mkoba wake maburungutu ya noti nyekundu ambayo aliyakabidhi kwa karani wa mahakama.
Taratibu za kulipa faini na fidia pamoja na kuachiwa huru zilichukua karibu saa moja. Wakati ule Ummy akinilipia pesa hizo nilijikuta nikimheshimu na kumchukulia kama mkombozi wangu ingawa ndiye yeye aliyekuwa ameniangamiza.
Nilipoachiwa huru na kutoka nje ya mahakama nikakutana na Imspekta Amour, akanipa mkono na kunisalimia.
“Pole sana na hongera” akaniambia kwa uso mkavu usio na aibu.
ITAENDELEA
 
SEHEMU YA 27

ENDELEA..
Baada ya kuachiwa huru na mahakama nilimshukuru Sana ummy kwa kuniokoa na kifungo kile japo nilijua wazi msababishaji ni yeye.
Ummy alinitaka tukutane saa 11 jioni ya siku ile japo sikua tayari ila niliogopa kumkatalia.
Naomba tukutane kwa mazungumzo zaidi Leo saa 11 kwenye bustani ya mnazi mmoja.
Nilimwitikia sawa ningefika mahala hapo kwa mda aliopanga.
Niliagana na ummy na kurudi nyumbani.Niliendelea na kazi za nyumbani masaa nayo yalikatika haraka nikifikiria kuhusu kukutana na ummy tena kutokana na visa na makubwa yaliyonikuta kutokana na ummy nilijikuta na kuwa mzito Sana kukubaliana na wazo la kukutana naye tena. Niliamua nipuuzie wito wake wa kukutana naye kwa kuepusha makubwa zaidi. Mda alioutaja tukutane ulifika na ukapita nilitegemea ningepokea hata simu au ujumbe wa simu kuniuliza kwanini sikufika lakini haikua hivyo.Usiku uliingia Niliendelea na mambo mengine ya nyumbani mda wa kulala ukafika nikalala japo nilikua na mfikiria Sana Ummy ila sikuchukua mda nilipitiwa na usingizi wakati nikiwa nimelala kunakitu nilikisikia nje Nikatega masikio yangu kusikiliza vizuri ili nijiridhishe kuwa mlango wa nje
ulikuwa unabishwa. Mlango huo ukabishwa tena.
“Hodi! Hodi!” Sauti ya mwanamke ikasikika.
Nikanyamza kimya huku nikijiuliza ni nani abishaye mlango usiku ule. Ile sauti iliporudia tena kupiga hodi nikaigundua kuwa ilikuwa sauti ya Ummy.
Nikashituka. Ummy ameamua kunifuata nyumbani usiku?
Wakati najiuliza hivyo nikasikia mlango wa nje unafunguliwa. Nikasikia kama viatu vya Ummy vikitembea ukumbini hadi kwenye mlango wa chumba changu. Kitendo hicho kilinishangaza kwa sababu sikujua ule mlango uliwezaje kufunguka wakati hakukuwa na mtu aliyeufungua.
Ndani ya ile nyumba nilikuwa ninaishi peke yangu.
Sasa mlango wa chumbani mwangu nao ukaanza kubishwa!
Nikaisikia sauti ya Ummy ikipiga hodi.
“Hodi! Hodi!”
Hapo ndipo nilipoanza kutetemeka nikijua kuwa sasa Ummy ananiingilia chumbani mwangu.
Nilikuwa nimejifinika shuka shuka gubigubi huku nimetega masikio yangu kwenye mlango. Jinsi nilivyokuwa nikitetemeka sikutofautiana na mgonjwa wa homa ya baridi aliyekuwa amefinikwa shuka.
Licha ya kuisikia waziwazi sauti ya Ummy ikipiga hodi kwenye mlango wa chumbani kwangu sikuthubutu kujibu chochote.
Nilijua kuwa maana ya Ummy kuopiga hodi ni kutaka nimkaribishe chumbani mwangu lakini wakati huo huo alishaingia ndani ya nyumba yangu bila
kumkaribisha.
Nikajiambia hata kama sitamfungulia mlango wa chumbani, ataingia mwenyewe kama alivyoingia ukumbini.
Kunyamza kimya kwangu kusingesaidia kumzuia msichana huyo asiyeeleweka kuniingilia chumbani.
Nikajikuta nikijuta kwa kutotimiza ile ahadi tuliyowekeana ya kukutana saa kumi na moja jioni kwenye bustani ya Mnazi Mmoja. Kama tungekutana, Ummy asingekuja nyumbani kwangu usiku huo. Nilijua kuja kwake kulitokana na mimi
kutotimiza ahadi yangu.
“Hodi! Hodi!” Sauti ya Ummy iliendelea kusikika mbele ya mlango.
Alipoona simjibu aliniambia.
“Kama hunijibu, naingia chummbani mwako!”
Maneno hayo ndiyo yaliyonipasua moyo wangu, nikawa nahema kama niliyemuona Ziraili akiniambia amekuja kuitoa roho yangu.
Mara ile ile nikausikia mlango wa chumbani mwangu ukitoa mlio wa kufunguliwa.
Nikafungua shuka kwenye usawa wa macho yangu na kuchungulia. Nikamuona Ummy Nasri akiingia chumbani. Alikuwa amevaa viatu vya mchcumio vilivyokuwa vikitoa mlio wakati akitembea.
Alipoingia chumbani kwangu macho yake yalikwenda kwenye kitanda nilichokuwa nimelala. Akawa anakisogelea kitanda hicho huku akinitazma jinsi nilivyokuwa nimejifinika shuka. Ili asione kuwa niko macho nilifumba macho yangu niikajifanya nimelala.
Ummy alitembea kwa mwendo wa taratibu akafika kando ya kitanda
changu. Akasimama na kukitupia macho chumba changu kisha akakaa kwenye pembe ya kitanda changu ambapo palikuwa na nafasi ndogo.
Akaniita kwa kulitaja jina langu. Nikanyamaza kimya.
“Mimi najua kuwa uko macho na umesikia wakati naingia ndani ya nyumba hii” akaniambia lakini mimi niliendelea kunyamza.
“Umenyamza lakini mwili wako unatetemeka, inaonesha kuwa uko macho na umeshaniona” Ummy aliendelea kuniambia kwa kunisuta.
Mtetemeko ulikuwa umeniumbua lakini sikuwa na namna ya kujizuia nisitetemeke.
“Inuka tafadhali”
Nikaitenga shuka na kuinuka, nikakaa kitandani.
“Mimi ni Ummy Nasri” Ummy akaniambia mara tu alipoona nimeketi kitandani.
“Nimeamua kuja nyumbani kwako baada ya kuona umekuwa ukinikwepa sana. Kama ungejua usingenikwepa kwani nina habari zenye manufaa kwako wewe” Ummy aliendelea kuniambia.
Ummy akanyamaza kidogo na kunitazama kisha akaendelea.
“Nataka kukupa hadithi fupi kuhusu marehemu babu yako. Babu yako alimpenda sana Ummy Nasri mpaka alimuachia mali zake, lakini Ummy hakumtaka babu yako zaidi ya kutaka kumla pesa zake kwa sababu babu yako alikuwa mzee”
Ummy aliendelea kuniambia.
“Kuna mwanamke wa kijini ambaye alimchunuka babu yako. Mwanamke huyo alitaka aolewe na babu yako na aliahidi kumpa utajiri. Alimfuata babu yako mara kadhaa lakini babu yako hakuwa tayari kukubaliana na jini huyo na sababu kubwa ni kuwa moyo wa babu yako ulikuwa kwa Ummy Nasri.
“Huyo jini akachukua uamuzi wa kumuua Ummy Nasri kisha akavaa sura ya Ummy na hapo akamfuata babu yako na kumwambia yeye ni Ummy anataka waoane. Ndipo babu yako alipooana na jini huyo akijua ameoana na Ummy Nasri. Babu yako akapata utajiri mkubwa sana.
“Jini huyo alimuonesha babu yako mahali ambapo angepata madini ya Tanzanite ambayo aliyauza nje ya nchi na kumpatia pesa nyingi”
Maneno ya Ummy sasa yakaanza kuniingia vizuri kichwani mwangu kwani ni kweli babu yangu alikuwa akiuza madini hayo nje ya nchi na mara kadhaa niliwahi kujiuliza babu yangu alikuwa akiyapata wapi madini hayo.
Ummy aliendelea kuniambia.
“Jini huyo aliendelea kuishi na babu yako. Babu yako alipokufa yule jini alichukua mali yote aliyompa na ndiyo
maana wewe hukupata mali yote ya babu yako na umekuwa ukijiuliza utajiri wa babu yako umekwenda wapi”
Maneno hayo sasa yalianza kuzindua akili yangu. Sasa nikaanza kufahamu asili ya utajiri wa babu yangu na jinsi utajiri huo ulivyotoweka mara tu mwenyewe alipokufa.
“Umekuwa ukinidhania kuwa mimi ni mzuka wa Ummy. Ukweli ni kwamba mimi ndiye huyo jini niliyevaa sura ya Ummy ambaye nilikuwa mke wa babu yako. Mimi ndiye niliyempa utajiri babu
yako na mimi ndiye niliyeupoteza utajiri huo mara tu baada ya babu yako kufa” Ummy aliendelea kuniambia.
Nikainua yangu yangu na kumtazama mwanamke huyo usoni.
“Niangalie vizuri. Mimi ni mwanamke wa kijini” Mwanamke huyo akaniambia na kuongeza.
“Jina langu ninaitwa Maimun. Usilinganishe na Maimuna. Mimi ni Maimun binti Hashhash”
ITAENDELEA
 
SEHEMU YA 28

ENDELEA...
Nikainamisha uso wangu na kuanza kuwaza kwamba kumbe yule mwanamke aliyekuwa akitusumbua alikuwa jinni na si mzuka wa Ummy.
“Nilikuelekeza uende nyumbani kwa kina Ummy uniulizie, lengo langu ni kutaka kukuonesha miujiza. Baada ya Miujiza ile nilitaka tukutane nikueleze ukweli lakini ulikuwa ukinikwepa hadi hii leo nilipofanya uamuzi wa kukufuata nyumbani kwako” Maimun aliniambia.
Akaendelea. “Najua kilichokutisha ni jinsi nilivyowaua wale watu kule Botswana, Zimbabwe na Afrika kusini. Wale watu baada ya kugundua kuwa aliyewapa mali alikuwa amekufa walipanga njama za kukuua. Ndipo nilipochukua uamuzi wa kuwaua wao mmoja baada ya mwingine. Wewe hujui tu lakini mimi nipo na wewe tangu babu yako alipofariki”
Wakati wote huo nilikuwa kimya nikimsikiliza kwa makini mwanamke huyo.
“Nilikwambia kuwa ninaijua siri ya mali ya babu yako, siri yake ndiyo hiyo. Utajiri wa babu yako ninao mimi na ninakusudia kukupa wewe. Lakini nisingekupa mpaka nikutane na wewe kama tulivyokutana hii leo na unirithi mimi”
Nikainua uso wangu na kumtazama mwanamke huyo huku nikimfananisha na jini. Hakuonesha ishara yoyote ya kuwa jini zaidi ya ile miujiza yake alionionesha siku ile katika eneo la hoteli ya Lux. Ile miujiza pekee ilitosha kunipa imani kuwa alikuwa jini kweli.
“Nikurithi kivipi?” nikamuuliza.
“Unirithi kama mke wa babu yako na uendelee kuishi na mimi kama mke wako”
“Mimi sijui mlikuwa mnaishi namna gani?”
“Tulikuwa tunaishi kama mke na mume. Tofauti ilikuwa mimi ni jini, yeye ni binaadamu”
Nilijaribu kuwaza kwamba ninaishi na mwanamke ambaye ni jini nikaona jambo hilo haliwezekani.
Nikatikisa kichwa.
“Naona kama haiwezekani kuishi na mwanamke ambaye ni jini”
“Inawezekana. Mbona babu yako aliweza”
“Sijui alikuwa akitumia mbinu gani kuishi na wewe”
“Haihitaji mbinu. Tunaishi tu kama mke na mume. Vile ambavyo utamtumia mke wako ndivyo ambavyo utanitumia mimi. Na vile ambavyo mimi nitamtumia mume wangu ndivyo ambavyo nitakutumia wewe”
“Unaweza kunipa muda wa kufikiria jambo hilo na kunipa muda wa kujiandaa”
“Ninaweza. Niambie nikupe muda wa siku ngapi?”
“Nipe muda wa wiki moja tu”
“Sawa. Nitakupa muda wa wiki moja. Lakini nitakuwa na masharti yangu
ambayo ni lazima uyafuate”
“Masharti gani?”
“Kwanza sitataka ujihusishe kimapenzi na mwanamke mwingine. Pili kila jambo ambalo utalifanya ni lazima utake ruhusa kutoka kwangu. Na mimi kila jambo ambalo nitalifanya ni lazima nitake ruhusa kutoka kwako”
“Sawa. Na kuhusu huo utajiri nitaupataje?”
“Utaupata wakati tutakapokuwa tumekubalina kuwa wanandoa”
“Sawa”
Pakapita ukimya wa karibu sekunde kumi. Maimun alikuwa akikikodolea macho chumaba changu.
“Sasa mimi nakwenda zangu” akaniambia baada ya sekunde hizo.
“Sawa, tutawasiliana”
Maimun akainuka kutoka kitandani na kuniambia.
“Kwaheri”
“Karibu sana”
Akageuka na kuelekea kwenye mlango. Alifungua mlango akatoka. Nikainuka na kumfuatia ukumbini. Sikumuona tena. Nilikwenda kwenye mlango wa mbele
nikaukuta umefungwa kwa ndani.
Sikuweza kujua alitoka vipi. Nikarudi chumbani mwangu na kufunga mlango.
Nilijitupa kitandani na kuanza kuwaza. Kile kitendawili cha Ummy alikuwa nani, kilikuwa kimeshateguka. Sasa nilikuwa nikifahamu kuwa Ummy ni jini na siye yule Ummy tuliyekuwa tukimdhania aliyekuwa amezikwa kaburini.
Kile kitendo cha kuvaa sura ya Ummy ndicho ambacho kilinichanganya na kumdhania alikuwa mzuka wa Ummy.
Sasa suala la Ummy ni nani lilikuwa limeshapata jibu. Ummy ni jini na jina lake ni Maimun binti Hashhash. Suala sasa ni la kufikiria kuishi na mwanamke huyo kama mke na mume.
Awali sikuwa nikijua kama babu yangu alikuwa na mke wa kijini. Kwa vile nilikuwa nikiishi Morogoro sikuwahi kumuona hata siku moja na babu yangu hakuwahi kuniambia. Jambo hilo alilifanya kuwa siri yake.
Sasa babu ameshakufa, nilijiambia, jini huyo amenifuata mimi na ametaka
nimrithi.
Amenipa siku saba za kufikiria ama kumkubalia ama kumkatalia.
Nikajiuliza endapo nitakubali kumrithi Maimun na kuwa mke wangu faida yake itakuwa ni nini?
Jibu nililipata mara moja. Faida yake ni
moja tu, kupata utajiri ambao kila mwanaadamu katika ulimwengu huu anauwania.
Nikimrithi Maimun nitakuwa tajiri. Nitaishi katika jumba la kifahari na nitakuwa na gari kama sio magari ya gharama. Vile vile nitaishi maisha ya hali ya juu.
Na je kama sitataka kumrihi athari yake itakuwa nini? Nilijiuliza.
Jibu hilo lilipaswa litolewe na Maimun mwenyewe lakini nililijibu mimi kwamba endapo sitamrithi Maimun sitapata utajiri. Nitendelea kuishi katika umasikini. Hilo ndilo jibu la haraka haraka nililolipata.
Usiku ule nilikesha macho nikiwaza hadi asubuhi. Wazo ambalo niliamka nalo ni la kwenda kwa yule mganga wa marehemu babu aliyeko Chanika ili anipe ushauri wake.
Ilipofika saa nne nikaliwasha gari na kwenda Chanika kwa yule mganga.
Nilipofika nyumbani kwake nilimkuta akikatakata vipande vya mzizi.
“Habari za siku nyingi?” akaniuliza.
“Nzuri. Habari za hapa?”
“Hapa ni kwema. Karibu sana”
“Asante. Niimekuja nina tatizo moja. Nataka kupata ushauri wako”
“Tatizo gani hilo?”
Nikamueleza kuhusu yule jini aliyekuwa mke wa babu yangu.
Baada ya kumpa maelezo yangu mganga alishituka na kushngaa. Akaacha kukatakata vipande vya mizizi.
ITAENDELEA
 
SEHEMU YA 29

ENDELEA...
“Kumbe babu yako alikuwa na mke jini, ndiyo maana alipata utajiri ghafla! Lakini hakuwahi kunieleza hata siku moja. Alikuwa msiri sana”
“Huyo jini sasa amejitokeza kwangu na anataka nimrithi ili anipe utajiri aliokuwa nao babu yangu”
“Sasa ulitaka nikupe ushauri gani?”
“Nimkubalie au nimkatalie?”
Mganga baada ya kutafakari aliniambia.
Umefanya vizuri kuja kwangu. Mimi nitakupa ushauri mzuri”
“Nitakushukuru sana”
“Usikubali. Huyo jini atakusumbua sana na pengine atakuja kukuua. Sasa nimeanza kugundua kuwa hata babu yako aliuawa na huyo jini”
Maneno ya mganga huyo yakanishitua.
“Kumbe hivi viumbe vina madhara makubwa?” nikamuuliza
“Wewe hujui tu. Hawa viumbe si wazuri. Uliona wapi jini akaolewa na binaadamu?”
“Sijawahi kuona”
“Sasa ujue kuwa hicho kitu hakiwezekani. Huyo jini anakilazimisha kwa nia mbaya. Amemuua babu yako, sasa anataka kukuua wewe”
Nikabaki nimepigwa na butwaa la mshangao.
“Wewe angalia vituko na miujiza aliyokufanyia ndipo utajua ana madhara ya kiasi gani”
“Sasa nifanye nini ili niweze kuepukana naye?”
“Njoo kesho asubuhi, nitajua jinsi ya kukusaidia. Huyo hawezi kuondoka mwenyewe mpaka nimuondoe mimi”
“Sasa hapo kesho utakuja kumuondoa?”
“Nitamuondoa na utaishi kwa usalama. Wewe ni binaadamu, wajibu wako ni kuoa binaadamu mwenzako mzae watoto na sio jini. Kama utaoana na jini mtazaa watoto gani? Mtazaa binaadamu au majini?”
Mganga aliniuliza swali hilo lakini sikuwa na jibu. Nikaona kweli ushauri wa kumrithi yule jini haukuwa na maana.
“Kama ulivyoniambia nitakuja kesho unishighulikie” nilimwambia mganga huyo kabla ya kuagana naye.
Nilipoondoka nyumbani kwa mganga huyo niliona mawazo yake yalikuwa sahihi. Si tu ningejitafutia matatizo
mimi mwenyewe kwa kukubali kuishi na jinni bali pia sikuwa na uhakika tungezaa watoto wa aina gani.
Kama tungezaa watoto wa kijini wasingekuwa na manufaa kwangu na hata kama watoto hao wangekuwa ni binaadamu bado wasingekuwa binaadamu kamili, wasingeweza kuishi na watu wengine.
Lakini kulikuwa na kitu kilichojificha ambacho nilikuwa sikijui. Nilikuwa sijui
kwamba yale maneno ya yule mganga yalikuwa ni ya roho mbaya. Alikuwa akitia fitina ili mimi nisimrithi yule mwanamke wa kijini kwa kuona kwamba nitaidi utajiri wa bure.
Lengo lake la kuniambia niende kesho lilikuwa ni kutafuta mbinu ili amchukue yeye jini huyo.
Asubihi ya siku ya pili yake nikaenda tena kwa mganga huyo.
“Sasa mwanangu unajua hii kazi haitafanyika hapa. Itafanyika shanbani kwangu. Itabidi twende shamba” akaniambia.
“Sawa. Tunaweza kwenda. Gari lipo”
Mganga akaandaa vifaa vyake. Akawachukua wasaidizi wake wawili ambao bila shaka alishawaeleza tunakwenda shamba kufanya nini.Tukaondoka na gari.
Shamba hilo lilikuwa kule kule Chanika lakini lilikuwa mbali kidogo. Akaniambia tuingize gari ndani ya shamba hilo. Nikaliingiza gari na kulisimamisha mbele ya nyumba yake ya miti na udongo iliyokuwa katikati ya shamba.
Tukashuka na kuingia kwenye ile nyumba.
Kwa jinsi nilivyofahamu baadaye ni kuwa ili aweze kumchukua Maimun alitaka kwanza aniue mimi na ndiyo madhumuni ya kunipeleka huko shamba.
Baada ya kuniua alitaka achukue damu yangu na kuioga mwilini mwake kisha ajipake mafuta ya waridi.
Tulipoingia kwenye ile nyumba nikaambiwa nikae chini. Kwanza kilianza kisomo. Nilisomewa na watu watatu bila
kuambiwa ninasomewa nini.
Baada ya kisomo hicho mganga alikoroga dawa kwenye kikombe akanipa ninywe.
“Kunywa hii dawa” alinaimbia kisha akaongeza.
“Nitakupa na dawa nyingine ya kuoga”
Kumbe ile haikuwa dawa. Ilikuwa sumu! Alitaka niinywe ili nife pale pale na kisha wanitoe damu kabla haijakauka.
Kile kikombe nilikipokea nikakisogeza midomoni mwangu ili ninywe ile dawa niliyoambiwa. Hapo hapo niliona kikombe kinabetwa. Kikanitoka mkononi na kuanguka chini. Sumu iliyokuwamo ikamwagika. Yule mganga na wasaidizi wake walikuwa wameshangaa. Aliyenibeta kikombe hakuonekana!
Ghafla nikasikia mganga anapigwa kibao
cha nguvu na kuanguka chini. Alivyoanguka alinza kutokwa na povu mdomoni. Wale wasaidizi wake walipoona hivyo walitimua mbio.
Nikabaki nimekaa nikiwa sijui kinachoendelea. Ikabidi niinuke na kumtazama yule mganga. Nikaona amekauka. Tukio hilo likanishitua.
Nikatoka nje ya ile nyumba kuwatazama wale waliokimbia lakini sikuwaona.
Nikasikia ninaitwa ndani ya gari langu. Niliposogea kwenye mlango nikamuona Maimun amekaa kwenye siti ya upande wa pili wa dereva.
“Ingia twende zetu” akaniambia.
Nikafungua mlango wa gari na kujipakia.
“Washa gari tuondoke”
Nikawasha gari.
“Umeuona upuuzi wako?” Maimun akaniuliza.
Kwa vile nilikwenda pale kwa ajili ya kumfukuza yeye, sikujibu kitu. Nilihisi pengine upuuzi aliokusudia ulikuwa ni huo.
“Sisi tunakubaliana kitu vizuri halafu wewe unakwenda kwa mganga! Ulikwenda kwa mganga kufanya nini?” Maimun akaniuliza.
Kwa kweli nilitahayari aliponiuliza hivyo. Nikaendelea kubaki kimya.
ITAENDELEA
 
SEHEMU YA 30

ENDELEA...
“Mwenzako amekudanganya. Amekwambia mimi ni mbaya kwa maana yake. Alikuleta huku ili akuue. Ile dawa aliyokupa kwenye kikombe haikuwa dawa. Ilikuwa ni sumu. Kama
ungekunywa ungekufa pale pale! Mimi ndiye niliyekibeta kile kikombe”
Hapo ndipo nilipogutuka.
“Kumbe alikuwa ananipa sumu?”
“Alikuwa anakupa sumu akuue. Ukishakufa alitaka anichukue mimi
niwe mke wake ili apate utajiri”
“Ndiyo maana aliniambia tuje huku shamba!”
“Sasa ndiyo ujue kuwa ulichofanya kilikuwa ni upuuzi. Kwanini ulikuja kumueleza siri ya mimi na wewe?”
“Nilikuja kumtaka ushauri, ndio akaniambia kuwa wewe ndiye uliyemuua babu yangu na utaniua na mimi. Kwa hiyo alitaka akuondoe”
“Shiit…! Mimi nimuue babu yako kwa kosa gani wakati nilimchunuka mwenyewe. Babu yako alikufa kwa sababu alikuwa mzee. Angeendelea kuishi hadi lini?”
“Basi alinaimbia umemuua wewe”
“Yale yalikuwa maneno ya uchochezi yenye lengo la kutaka unichukie mimi na ukatae kunirithi” Maimun aliniambia kwa huzuni kisha akaongeza.
“Ni mganga mwenye roho mbaya sana. Kama mimi ni mbaya mbona alinitaka yeye?”
Nikanyamaza kimya nikifikiria kwamba kama si mwanamke huyo ningekuwa nimeshauawa kwa sumu.
“Unajua hukupaswa kuwaeleza watu kila kitu. Babu yako alikuwa msiri sana. Hakuwa na mtu yeyote aliyejua kama alikuwa na mke jini. Hata yule mganga wake hakumwambia”
“Ni kweli nilikosea”
“Sasa acha tabia ya kuwaeleza watu habari zangu. Utakuja kuuawa bure”
“Yule mganga sitamuamini tena”
“Kwani nani alikwambia kwamba ataamka tena?”
Nikashituka.
“Hataamka tena?”
“Ile ndiyo safari. Nilikubeba wewe kile kikombe kisha nikampiga kibao. Alijiona anapigwa lakini hajui anapigwa na nani. Hataamka tena. Ile ndiyo safari!”
“Niloimuona amekakamaa”
“Hivi ndivyo ninavyomfanya mtu mpumbavu. Kama ni mganga kweli mwenye majini, mbona hawakunizuia nisimpige? Yule hawezi kunichukua mimi. Mimi ni jini wa kweli kweli. Sio vijini vyake ochwara!”
Kikapita kimya cha sekunde kadhaa nikiyawazia maneno ya Maimun.
“Sioni haja ya kusubiri ujiandae au ufikirie. Unajiandaa kwa lipi au unafikiria nini? Leo utanirithi na ninakuwa mke wako. Sasa twende madukani tukanunue nguo kwa ajili ya sherehe yetu ya usiku” Maimun akaniambia ghafla.
“Tutakuwa na sherehe leo usiku” nikamuuliza.
“Ndiyo, sherehe ya kuoana kwetu”
“Itafanyika wapi?”
“Itafanyika nyumbani kwako usiku”
“Itakuwa ni sherehe ya namna gani?”
“Sherehe kama sherehe yoyote ya ndoa. Nitawaalika wageni wangu kutoka kwetu lakini wewe usialike mtu. Itakuwa sherehe ya majini”
“Kwani haitaki maandalizi?”
“Mimi mwenyewe nitaandaa kila kitu”
Nikabaki nimeduwaa. Ningemjibu nini Maimun anayeua watu kwa vibao? Ilibidi nimkubalie kila alichosema.
Nikampitisha katika maduka makubwa ya nguo. Akanunua vitu pamoja na nguo zake na zangu. Alijaza masanduku mawili ya nguo zenye thamani na kuyapakia kwenye gari. Pesa
zilizomtoka zilikuwa karibu shilingi milioni ishirini na tano!
Ile ‘shopping’ ilinitisha hata mimi. Kununu nguo zenye thamani kubwa kiasi kile kwa wakati mmoja halikuwa jambo dogo. Niliamini kuwa kweli yule mwanamke alikuwa na utajiri, si mchezo.
Tulirudi nyumbani kwangu na yale masanduku. Maimun akaniambia siku ile nisiondoke kwenda popote. Nikatii agizo lake nikashinda nyumbani hadi jioni lakini yeye aliondoka. Usiku nilitoka mara moja kwenda kula chakula halafu nikarudi kulala.
Yapata saa nae usiku, mlango wa chumba changu ukabishwa. Nikasikia sauti za watu ukumbini. Sikupata hofu kwa vile Maimun aliniambia sherehe zitafanyika usiku. Nikaamka na kwenda kufungua mlango.
Niliona wasichana wawili waliokuwa mbele ya mlango. Sikuwa na shaka kwamba wasichana hao walikuwa majini kwani walikuwa wazuri sana.
“Wakati umewadia. Unatakiwa uoge uvae joho lako alilokununulia dada, ujifunge na kilemba halafu ujitie manukato” Mmoja wa wasichana hao wakaniambia.
Nikarudi chumbani na kuingia bafuni. Nilioga na nilipomaliza nilitoka nikavaa ‘Panjabi’ aliyoninunulia Maimun kisha nikajitia manukato.
Nikatoka bila kuvaa kilemba kwani nilishindwa kukifunga. Nilikuwa nimekishika mkononi.
Wale wasichana wawili walikuwa bado wako kando ya mlango kama maaskari. Waliponiona ninatoka, mmoja alinishika mkono akanirudisha chumbani.
“Usitoke hivi hivi, dadada atagomba” akaniambia na kunifunga kile kilemba.
Baada ya kufungwa kilemba hicho nilijitazama kwenye kioo. Nilijiona nilikuwa kama ‘Mpakistani’ anayejiandaa kwanda kuswalisha.
Nyumba yangu ilikuwa imepambwa vilivyo. Mapazia yalikuwa yamewekwa mengine. Taa zilikuwa zimebadilishwa na kuwekwa taa za rangi mbalimbali na zisizo na mwanaga mkali.
Niliona watu mbalimbali, wake kwa waume, wakishughulika. Maimun aliniambia mchana kuwa ataalika wageni kutoka kwao. Nikahisi wageni wenyewe ndio wale niliowaona hapo.
Nikapelekwa sebuleni. Sebule ilikuwa imebadilishwa. Makochi yangu yaliondolewa na kuwekwa makochi mengine ya chini chini. Nilikuta watu wawili, mmoja akiwa mzee mwenye ndevu nyeupe ambaye alikuwa amevaa joho na kilemba cheupe.
Pembeni yake palikuwa na chetezo kilichokuwa kinafuka moshi uliokuwa unanukia ubani uliochanganya na udi wa mawaridi, wengine huuita udi wa Unguja.
Sebule nzima ilikuwa ikinukia udi wa mawaridi.
“Kaa hapa” yule mzee aliyekuwa amevaa joho akaniambia akinionesha sehemu iliyokuwa mbele yake.
Nilipokaa tu akaniambia.
“Lete mkono wako”
Nikampa mkono.
“Unaitwa nani?” akaniuliza.
ITAENDELEA
 
SEHEMU YA 31

ILIPOISHIA
Nikamtajia jina langu.
“Nikilitaja jina lako utaitikia labeka”
“Sawa”
Mzee huyo akaniita. Nikamuitikia “labeka”
“Ninakuozesha Maimun binti Hashhash kwa mahari mliyokubaliana. Unakubali?”
“Nimekubali”
“Sema nimekubali kumuoa Maimun binti Hashhash kwa mahari tuliyokubaliana”
Nikasema kama vile alivyonifundisha. Akarudi kunaimbia hivyo mara tatu.
Hapo hapo nikasikia sauti za wanawake waliokuwa wamekaa ukumbini ziking’ara kwa vifijo.
Yule mtu aliyekuwa amenichukua kutoka mlango wa chumbani kwangu, akaniambia niinuke. Nilipoinuka akanirudisha chumbani kwangu. Nilipoingia nilikuta chumba hicho kimebadilishwa.
SASA ENDELEA
Hakikuwa kile chumba changu kabisa. Kitanda kilikuwa kimewekwa kingine. Kabati lilikuwa jingine na mapazia pia
yalikuwa mengine. Kwa kweli kilikuwa kimependeza sana. Hata taa zizokuwa zinawaka zilikuwa ni za rangi mbali mbali.
Nikamkuta Maimun binti Hashhash amekaa kwenye kitanda. Pale kwenye kitannda palikuwa pametandazwa maua ya mawarisi, asmini, vilua, mlangilangi na vitu vingine ambavyo vilikuwa vikitoa
harufu nzuri mle chumbani.
Maimun alikuwa amepambwa na kupendeza kama malkia wa Habesh. Alikuwa akinukia manukato ya kila aina. Mwili wake ulikuwa umejaa mapambo ya dhahabu. Kuanzia kwenye shingo yake ambapo palikuwa na mkufu mzito wa thamani. Masikioni mwake alikuwa amewekwa vipuli vilivyokuwa vikimeremeta. Kwenye mikono yake alikuwa amevaa aina ya bangili za dhahabu.
Kadhalika katika mguu wake wa kulia alikuwa amefungwa mkufu mwembamba uliokuwa ukimeremeta.
Kwa kweli alikuwa amependeza na kutamanisha.
Alikuwa amefunikwa mtandio uliokuwa unaonya. Hivyo niliweza kuyaona macho yake yaliyokuwa yamepakwa wanja mzito mweusi huku yakiwa na kope ndefu mithili ya kope za bandia.
Nyusi zake pia zilikuwa zimeongezewa msitari wa wanja uliopinda juu ya macho yake mithili ya pindi za mvua.
Aliniomba nimfunue ule mtandio, nikaushika kwa uoga na kuufunua. Akaniambia.
“Asalaam alaykum mume wangu” Wakati akinipa salaam hiyo alikuwa akinipa mkono.
“Wa alayka salaam” nikamjibu na kushikana naye mkono.
Mkono wake ulichorwa maua kwa kutumia piku na hina. Ulikuwa umeota malaika marefu yasiyo ya kawaida.
“Salaam yako ina kasoro, sikuipenda” Maimun akaniambia wakati tumeshikana.
“Kwanini?” nikamuuliza.
“Nimekusalimia asalaam alaykum mume wangu. Ulipaswa kujibu wa alayka salaam mke wangu”
“Samahani. Ni kweli nimekosea”
“Sasa nijibu kwa usahihi”
“Wa alayka salaam mke wangu”
Maimun akakibusu kiganja cha mkono wangu kisha akaniambia.
“Karibu chumbani”
“Asante” nikamjibu.
Kusema kweli nilikuwa nimenywea kama vile kile chumba hakikuwa changu.
Yule mtu aliyenisindikiza mle chumbani akaniambia.
“Kama umeshaonana na mke wako, mimi nakwenda zangu”
“Wewe nenda, muache” Maimun akanijibia.
Yule mtu alipotoka Maimun akajilaza kitandani na kuniambia.
“Huu ni wakati wako. Karibu tujipumzishe…..”
**********
Mkono wenye ngozi laini kama ya mtoto mchanga uliokuwa ukipapasa kifua changu ndio ulioniamsha kutoka usingizini.
Nikafumbua macho yangu na kuisikia sauti ya Maimun ikiniambia.
“Amka mume wangu, kumekucha”
Maimun alikuwa amesimama kando ya kitanda mkono wake ukiwa kwenye kifua
changu. Sikuweza kujua alikuwa ameondoka muda gani hapo kitandani lakini wakati ule ananiamsha kulikuwa kumeshakucha.
“Amka ukaoge, nimeshakuandalia kifungua kinywa” akaniambia.
Nikaitenga shuka na kushuka kitandani.
“Utaoga maji ya moto?” Maimun akaniuliza.
“Hapana, ninaoga maji baridi tu”
Niliingia naye bafuni tukaoga pamoja. Baada ya kuoga Maimun akanikaribisha mezani nipate kifungua kinywa alichokuwa ameniamndalia. Ile vurugu pale nyumbani haikuwepo tena.
Nyumba ilikuwa kimya na hakukuwa na mgeni yeyote aliyekuwa amebaki. Sikuweza kujua wageni wale waliokuwepo usiku waliondoka saa ngapi.
Kitu kilichoonesha kuwa usiku uliopita kulikuwa na sherehe ni mapambo yaliyopambwa mle ndani ambayo bado yalikuwepo.
Baada ya kupata kifungua kinywa pamoja na Maimun tulirudi chumbani ambapo Maimun alifungua kabati. Hilo kabati lilikuwa moja ya vitu vilivyoletwa usiku uliopita. Halikuwa lile kabati langu.
Maimun alipolifungua kabati hilo, upende mmoja ulikuwa umepangwa nguo zake, upande mwingine ulipangwa nguo zangu.
Katika sehemu ya chini ya kabati hilo kulikuwa na sanduku la chuma. Maimun akanipa funguo na kuniambia nilifungue
sanduku hilo. Nikalifungua na kupatwa na mshituko.
Sanduku hilo lilikuwa na tabaka tatu. Tabaka ya kwanza ilikuwa imepangwa maburungutu ya noti nyekundu za Kitanzania. Zilikuwa noti nyingi na mpya zilizozonesha kama zilitoka benki kwani bado zilikuwa zimefungwa mfungo ule
ule wa kibenki.
Tabaka la pili lilikuwa limejaa mapambo ya dhahabu, mikufu, bangili, vipuli na vitu vngine.
Tabaka la tatu lilikuwa na maburubgutu
ya noti lakini hazikuwa za Kitanzania. Zilikuwa ni dola za Kimarekani.
Nikamtazama Maimun kwa mshangao.
“Hizo ni za kutumia hapa nyumbani. Zikiisha ninaweka zingine” Maimun akaniambia.
Nikageuza tena uso wangu na kuzitazama zile noti nilizoambiwa kuwa ni za kutumia.
“Bado kuna pesa za miradi ambazo nitakupa” Manuna aliendelea kuniambia.
Akilini mwangu niljiambia kuwa nimeshakuwa tajiri.
“Chukua kiasi unachotaka uweke mfukoni mwako”
“Nichukue dola au hizi za Kitanzania?’
“Chukua unazotaka”
“Kuna miradi mingi ambayo ninataka kuianzisha”
ITAENDELEA
 
SEHEMU YA 32

ILIPOISHIA
“Nimekwambia hizo si za miradi. Hizo ni za kutumia tu. Pesa za miradi nitakupa baadaye”
“Sawa. Ngoja nichukue milioni moja”
“Chukua hata mbili”
Nikatia mkono na kuchukua burungutu moja ya zile noti za Kitanzania.
“Si unataka milioni mbili, chukua mawili”
Nikatia tena mkono na kuchukua burungutu jingine.
“Sasa funga hilo sanduku”
Nikalifunga. Maimun akanipa ufunguo wa sanduku hilo.
“Funguo utakaa nayo mwenyewe” akaniambia.
SASA ENDELEA
Aliponiambia hivyo, kwa bumbuwazi lililonipata kufuatia kuwa na pesa nyingi kiasi kile nikabaki nikimuangalia Maimun.
“Vipi mume wangu, mbona umetulia unaniangalia?”
“Unajua siamini macho yangu. Kwa hiyo pesa zote hizi nizitumie?”
Nilipomuuliza hivyo Maimun alitoa
kicheko laini akaniambia pesa zote zile zilikuwa zangu. Hivyo naweza kuzitumia kununua chochote nitakachotaka.
“Nakushukuru sana mke wangu”
Maimun aliachia tabasamu kabla ya kuniambia kuwa kulikuwa na jambo muhimu alinieleza.
“Sijui kama unalikumbuka?”
“Nimesahau mke wangu ni jambo gani hilo?”
“Mume wangu jamani! Naona furaha yako imepita kiasi mpaka umesahau jambo muhimu nililokueleza. Kweli umesahau au unataka tu nikueleze tena?”
“Siyo hivyo mke wangu, ningekumbuka ningekwambia. Naomba unikumbushe maana umeniacha njia panda mwenzio”
SASA ENDELEA
“Haya njoo hapa kitandani nikueleze tena” Maimun akaniambia. Kidogo nilipatwa na wasiwasi. Nikamfuata.
“Mbona hujafunga kabati?” Maimun akaniuliza na kuongeza.
“Funga kabati kwanza ndio uje”
Nikarudi kunako kabati. Nikalifunga kisha nikaenda pale kitandani ambako
Maimun alikuwa ameketi.
Maimun akauzungusha mkono wake mmoja kwenye shingo yangu, mkono mwingine ukawa unapapasa kifua changu.
“Kassim una manyoya marefu kifuani!” akaniambia halafu akawa anacheka kama mtoto
Aliendelea kunipapapasa huku akiendelea kusema peke yake.
“Utadhani jini…!”
Aliposema hivyo aliangua kicheko kabisa.
“Hivi majini wanakuwa na manyoya marefu?” nikamuuliza.
“Hunioni mimi?” akaniambia huku akinionesha mikono yake ambayo ilikuwa na malaika marefu.
Akaendelea kunionesha miguu yake.
Ingawa alinionesha miguu na mikono lakini kifuani kwake kulikuwa na manyoya zaidi. Niliyaona usiku uliopita.
“Nilidhani ni wewe tu” nikamwambia.
“Hapana, hivi ndivyo tulivyo. Tena mimi ni mafupi lakini majini wenzangu wana manyoya marefu sana”
“Kwa hiyo unapenda malaika marefu?”
“Sana”
Maimun aliposema neno ‘sana’ aliurudisha mkono wake kwenye kifua changu.
Mbona hujaniambia hilo jambo muhimu ulilotaka kunieleza”
“Ni kukukumbusha tu, nilishakwambia jana kwamba sitaki siri yangu uitoe nje. Hizi pesa ninazokupa ziwe siri yako na bado nitakupa nyingi zaidi. Sitaki nikuone unamueleza mtu kwamba mke wako ni jini na anakupa pesa. Umenielewa?”
“Nimekuelewa”
“Siku nikikusikia ukimwambia mtu habari zangu ujue umenivunjia mwiko wangu. Sawa”
“Sawa mke wangu. Sitamueleza mtu.
Kwanza nimueleze mtu ili iweje?”
“Mimi nazijua tabia za binaadamu. Wengine wanapenda sifa sana. Na sifa haifai”
“Ni kweli lakini mimi sina tabia hiyo”
“Nataka nikukumbushe kitu kiingine kwamba usiwe na mahusiano na mwanamke yeyote na kama ulikuwa naye umuache”
Hapo nikanyamaza kidogo. Nikamfikiria msichana wangu mmoja ambaye ndiye niliyekuwa nimepanga kuoana naye.
“Mbona umenyamaza?” Maimun akaniuliza.
“Sikufichi. Kuna msichana mmoja ambaye nilikuwa na uhusiano naye na tulikuwa tumepanga kuoana…”
Nilikuwa sijamaliza sentensi yangu,
nikauona uso wa Maimun ukiwa mwekundu mpaka niliogopa.
“Unasemaje?” akaniuliza huku akiwa amekunja uso.
“Nilikuwa nataka kukueleza kwamba huyo msichana itabidi niachane naye…”
Maimun akabaki kunitazama. Hata hivyo kwa vile nilikuwa nimeshamzoea nikamshika kiuno chake na kumvuta upande wangu. Wakati namvuta alikuwa laini kama si yeye aliyekuwa amekasirika.
“Unakasirika nini” nikapata ujasiri wa kumuuliza nikiwa nimemkumbatia.
“Sitaki shirika. Siku nikikufuma naye ujue ninamuua” akaniambia kwa sauti ya kudeka kama ya mtoto mdogo. Hasira zilikuwa zimeshamtoka.
“Hutonifuma naye ila itabidi nimueleze kuwa sitaoana naye tena”
“Kwa hilo ninakuruhusu”
“Yaani Maimun unafikiri mimi ni mjinga sana, nikupate wewe mrembo ambaye unanipa utajiri halafu nitafute mwanamke mwingine wa kunifilisi!”
Maneno hayo yakamfurahisha Maimun ambaye bado nilikuwa nimemkumbatia.
“Si kukupa utajiri tu, pia nakupa mapenzi adhimu” akaniambia kwa kunilegezea sauti.
“Ni kweli. Sasa baada ya hayo yote nitafute nini tena kwa mwanamke mwingine?”
Sikujua Maimun alipandwa na mori gani, akanipindua kitandani kisha akanikalia juu.
“Hutatoka humu chumbani leo. Nakwambia tutashinda humu humu nikuoneshe mahaba ya kijini” akaniambia.
Ni kweli siku ile siikutooka nje. Kumbe babu yangu alikuwa akifaidi! Majini wanajua mapenzi ya kweli. Kuoana na Maimun kuliniingiza katika enzi mpya katika maisha yangu, enzi ya mapenzi adhimu.
Mapenzi yetu hayakuwa chumbani tu, yalikuwa mahali popote, kwenye chakula, kwenye kuoga na hata kwenye mazungumzo.
Kitu ambacho niliokiona kilikuwa kero ni wivu wa mwanamke huyo. Alikuwa na wivu wa kupindukia. Siku akiamua nisitoke nyumbani, sitoki. Nitashinda naye chumbani mchana kutwa.
Siku ambayo ninapomuudhi anakasirika mchana kutwa. Anakuwa hataki kusema na mimi lakini siku akifurahi atakuenzi mpaka basi.
Saa moja asubuhi Maimun anakuwa ameshanitayarishia kifungua kinywa. Saa sita mchana ameshatayarisha chakula cha mchana. Chakula cha usiku kinakuwa tayari saa mbili.
Vyakula ambavyo Maimun alikuwa akivipenda ni uji uliochanganywa na nyama ya mbuzi, anauita ‘shurba’ Pia hupenda chai ya maziwa, chapatti, mkate wa mchele, pilau ya kuku, biriani na wali kwa maziwa ya mgando.
Vitu ambavyo alipenda kuvinunua kila siku ni aina za manukato. Kwenye kabati letu kulikuwa na chupa karibu ishirini za manukato tofauti tofauti.
Alikuwa akipenda kuoga. Mchana mmoja alioga karibu mara sita na akiingia bafuni huchukua muda mrefu kutoka. Ngozi yake ilikuwa safi na laini kama ngozi ya mtoto mchanga.
Kuna kitu kimoja nilikuja kukigundua kwamba Maimun alikuwa halali usingizi. Ninapolala naye usiku anafanya geresha tu. Ninapopitiwa na usingizi mwenzangu anabaki macho akiwa na kazi ya kuniamgalia tu. Wakati mwingine hushuka kitandani na kwenda kukaa sebuleni usiku kucha.
ITAENDELEA
 
SEHEMU YA 33
ILIPOISHIA
Siku nilipogundua hilo nilimuuliza.
“Hivi wewe Maimun hulali usiku?”
“Sisi majini hatulali, tunakuwa macho tu” akanijibu.
“Kwaninini?”
“Ndiyo maumbile yetu”
“Kumbe usiku nalala peke yangu?”
“Ukilala mimi nakulinda”
Kuna siku moja aliniamsha saa nane usiku akaniambia nichukue shepe kisha nitoe gari. Baada ya kulitia shepe kwenye gari nililitoa gari. Maimun akajipakia na kukaa kando yangu.
“Twende Kigamboni” akaniambia.
“Kuna nini?” nikamuuliza.
“Wewe twende tu”
Nilikwenda kukutana na maajabu ambayo sitayasahau katika maisha yangu.
SASA ENDELEA
Tulifika Kigamboni kama saa nane na nusu hivi. Ilielekea Maimun alikuwa akilijua vizuri eneo hilo kwani aliniongoza hadi sehemu ambayo ilikuwa na pori.
Akaniambia niingize gari katika pori hilo. Sikumuelewa halafu pia nilipata hofu kidogo. Nikafunga breki na kumuuliza.
“Kwani tunakwenda wapi?”
“Wewe twende tu”
“Lakini huku unakoniambia twende hakuna njia”
“Mimi pia nina macho, ninaona kuwa hakuna njia. Ingiza gari hivyo hivyo”
“Unataka tutokee wapi?”
“Kassim mbona mbishi sana?”
“Mahali kuna pori, unaniambia niende! Njoo uendeshe wewe”
“Kumbe huniamini?”
“Ninakuamini. Tatizo nini kuwa siwezi kuendesha gari kwenye pori na pia sijui tunakwenda wapi”
“Kwahiyo turudi?”
“Tusirudi. Nimekwambia njoo uendeshe wewe”
“Inaelekea wewe ni muoga sana!”
Hapo sikumjibu. Nikanyamaza kimya kwani ukweli ni kuwa uoga pia nilikuwa nao.
“Shuka unipishe hapo kwenye sukani” Maimun akaniambia.
Nikafungua mlango na kushuka.
Kulikuwa na gari ambayo ilikuwa nyuma yetu ikatupita na kusimama mbele yetu.
Wakati ule nafungua mlango nikaona ninavamiwa na mtu mmoja miongoni mwa wanne waliotoka kwenye lile gari. Mtu huyo alinishikia bastola na kunitia kabari kwa nyuma. Mtu mwingine alifungua mlango wa upande aliokuwa Maimun akamwambia.
“Shuka haraka!”
Maimun akashuka kwenye gari.
“Mnataka nini?” Maimun akiwauliza.
Mimi nilikuwa nimeshadhibitiwa. Mkono ulionitia kabari ulikuwa ukinikaza na kunifanya nisifurukute hata kidogo. Mdomo wa bastola ulikuwa ukitekenya shavu langu la kulia.
Sikuweza kujua watu wale walikuwa kina nani na walikuwa wanataka nini.
Kulikuwa na watu wengine wawili ambao walikuwa wamefungua milango ya ile gari kama vile walikuwa wakitafuta kitu.
“Mnakwenda wapi?” Yule mtu aliyemtoa Maimun kwenye gari akamuuliza Maimun.
“Nyinyi ni majambazi sio?” Maimun akawauliza.
Yule mtu alitaka kumpiga Maimun kibao, bila shaka kwa vile alivyowambia ni majambazi. Maimun akatoweka ghafla mbele yake. Kibao kikakata hewa. Maimun akaibuka tena mahali pale pale. Nikamsikia akitoa mlio kama wa fataki inayopaa juu huku na yeye akirefuka kwenda juu.
Wakati ule mmojawao, alikuwa ameshajipakia kwenye gari kwenye siti ya dereva. Nikahisi walitaka kutupora lile gari.
Lakini kitendo cha Maimun kurefuka kiliwashitua. Maimun aliendelea kurefuka akafikia kimo cha mnazi!
Nikawasikia wale watu wakisema kwa fadhaa. “Ha! Ha1 Ha!”
Yule aliyenitia kabari aliniachia akakimbilia kwenye gari lao. Yule aliyetaka kuendesha lile gari letu alitoka kwenye gari na kukimbia lakini yule aliyetaka kumpiga Maimun kibao alinata pale pale.
Wale waliokimbilia kwenye gari walikwama baada ya Maimun kupiga hatua moja na kutinga mbele ya gari hilo. Mtu mmoja alianguka hapo hapo. Wengine wakakimbia kwingine na kuliacha gari.
Baada ya tukio hilo nikauona mwili wa Maimun umerudi vile vile kama ulivyokuwa mwanzo.
Akaja kwenye gari letu upande wa dereva na kuniambia.
“Ingia garini twende”
Nikazunguka kwenye mlango wa upande wa pili na kujipakia. Yule mtu aliyenata alikuwa bado amesimama pale pale, mkono wake mmoja akiwa ameunyoosha mbele kama vile anampiga mtu kibao.
Maimun alikuwa ameshaingia kwenye gari akaliondoa na kuliingiza kwenye pori.
Kile kitendo cha Maimun kujirefusha, hata mimi kilinishitua kwani katika maisha yangu sijawahi kuona mtu akirefuka kwenda juu akafikia kimo cha mnazi.
Mpaka wakati ule nilikuwa bado nikitweta.
“Umewaona wapumbavu wale?” Maimun akaanza kuniambia akionekana alikuwa amekasirika.
“Nimewaona lakini sikujua walikuwa ni kina nani”
“Wale ni majambazi, walitaka kulipora hili gari. Walitufuata kuanzia mbali sana. Nilishawaona lakini sikukwambia”
“Kwa hiyo walitaka watuue?”
“Sasa kama walitutolea bastola, unadhani walikuwa wana maana gani nyingine?”
“Lakini wametishika!”
“Walivyonuona ninakuwa mrefu sio?”
“Ndiyo. Hata mimi nimetishika”
“Wewe mume wangu pia unatishika?”
“Sijawahi kukuona ukiwa vile!”
“Acha vile naweza kujirefusha mpaka ukawa hujui nimefikia wapi!”
“Sasa unafanyaje?”
“Ni namna yetu. Naweza pia kujigeuza mnyama kama vile punda au joka kubwa”
“Lakini sitapenda ufanye hivyo mbele yangu”
“Nikifanya mbele yako ndipo utakaponizoea”
“Eh! Nitaogopa sana”
“Utazoea tu. Utaogopa mwanzo, mwisho utakuwa huogopi tena”
“Sasa yule mtu aliyetaka kukupiga kibao, ataendelea kubaki pale hadi lini?”
“Atajua mwenyewe, achana naye”
Maimuna aliendesha gari huku akikata kona ndani ya msitu hadi tukatokea mahali ambapo palikuwa na mawe makubwa sana yaliyotokea ardhini.
Akalisimamisha gari na kuniambia tushuke. Tukashuka. Palikuwa ni mahali panapotisha usiku huo lakini kwa vile nilikuwa na Maimun sikuwa na hofu sana. Nilijua kama kutatokea tatizo atanisaidia.
“Toa lile shepe nyuma ya gari” akaniambia.
ITAENDELEA
 
Back
Top Bottom