Sitokaa niwasamehe wazazi wangu kwa kunikatalia kumuoa binti niliyempenda kisa tofauti zetu za Dini

LICHADI

JF-Expert Member
Feb 4, 2015
4,133
11,126
Mimi ni kijana wa kitanzania na umri wangu ni miaka 33, na dini yangu ni Mkristo, Pia ningependa kuelezea mkasa huu ulionikuta ili kila mwenye kujifunza ajifunze kwani Jamii forums kuna wazee na vijana pia ambao wanatarajia kuowa au kuolewa siku za usoni.


•Mahusiano yangu na huyu binti na kisa chenyewe

Huyu ni binti ambaye nlifahamiana nae chuoni wakati mimi nipo mwaka wa kwanza nikisomea fani ya Civil Engineering ,yeye alikuwa mwaka wa tatu akisomea Business Administration ,Alikuwa ni binti mwenye asili ya Pemba na Arab kwa mbali.

Baada ya kufahamiana nae ndipo mda uliposogea tukajikuta ni wapenzi na kitu nlichobahatika ni kuwa yule binti alikuwa ni mtu mwenye malengo na msimamo, anayejiheshim sana pia alikuwa ameishika sana dini na hakuwa mbaguzi, tuliishi kwa mapenzi ya dhati hadi kipindi yeye anakaribia kumaliza mimi ndio nlikuwa nakaribia kuingia mwaka wa pili pale chuoni.

Baada ya yeye kumaliza chuo akasafiri kuelekea zanzibar kwa wazazi wake kipindi hicho hakubahatika kupata kazi hivyo akawa anasaidia kuendesha biashara za wazazi wake, wakati huo mimi nilikuwa mwaka wa pili pale chuoni na kipindi hicho sikubahatika kupata mkopo hivyo nliikuwa napambana kivyangu sababu mzee wangu kuhusu hela ya matumizi alikuwa anantumia siku anayojiskia yeye na siku nyingine alikuwa kimya tu.

Hivyo huyu binti ndio alikuwa kila kitu kwangu, alikuwa akinipa msaada mkubwa sana kila nlipokuwa nakwama alikuwa akinisaidia sababu baba yangu alishakuwa kama kanisahau hivyo mimi nikachukulia kama ni changamoto tu za maisha na mzazi atabakia kuwa mzazi tu.

Alinisaidia katika mambo mengi kila nlipokuwa nakwama, hakuniacha peke yangu japo tulikuwa mbali lakini mapenzi yake kwangu hayakupungua bali yaliongezea kila siku na ahadi yangu mimi na yeye ilikuwa ni kuja kuwa mke na mme panapo majaaliwa.

Huyu biti nlikuwa nlikuwa nimemzidi kiumri kwa miaka miwili lakini alikuwa ana karama ya pekee aliyojaaliwa ambayo ni akili ya kipekee na mbinu za kupambana na maisha, alikuwa ni mtu mwenye maono ya mbali na mwenye uwezo mkubwa kiakili.

Baada ya kunisaidia kwa kipindi kirefu wakati mimi nipo chuoni ,kuna siku aliniuliza hivii "Nitakusaidia mpaka lini?, je ukimaliza chuo na usipopata kazi bado utahitaji msaada wagu tu? " ,Nikamwambia naomba anisamehe kama nimemsumbua na nlijihisi kama mapenzi yameanza kupungua. Lakini haikuwa hivyo

Yeye aliniambia tu baada ya kutoka chuo nitakapofika mtaani sababu nilikuwa nimepanga chumba sehem moja hivi uswazi, akaniambia kuwa nifanye research ni biashara gani nzuri naweza nikaifanya na ikanisaidia kunisogeza kimaisha hadi mambo yatakapokuja kukaa vizuri

Akaniambia kuwa nijaribu kuchunguza biashara ya chakula au duka dogo kwa maeneo yale ni biashara ipi haina watu wengi. Hivyo baada ya kufanya uchunguzi nikagundua kuwa biashara ya chakula kwenye ule mtaa haijachangamka sana na watu wa pale kama wamelala hivi, so akaniambia nitafute frem kwanza ambayo ipo barabarani na yenye eneo la kutosha kwa ndani na nnje pia, pili akaniambia eneo lisiwe na vumbi au uchafu sana yaani iwe sehem safi inayovutia.

Baada ya kuzunguka nikapata frem moja hivi ilikuwa barabarani karibia na maeneo ya pale pale, na kodi yake kwa kipindi kile ilikuwa ni sh 40,000 kwa mwezi, hivyo baada ya kumtaarifu ikabidi ajitoe mhanga kuchukua Milioni moja na nusu(1,500,000)benki pesa ambazo zilikuwa ni za biashara ya wazazi wake kisha akanitumia ili nianzishe hiyo biashara na faida ntakayokuwa napata ntakuwa nazirudisha kidogo kidogo cz hela zilikuwa sio zake .

240,000 -Nikalipia kodi ya miezi 6
500,000-Nikanunulia friji
300,000-Nikanunulia meza na viti
150,000-Nikanunulia vyombo
70,000 -Feni la ukutani
200,000- Nikaitumia kununulia vyakula vyote kwa ajili ya biashara.

Baada ya hapo nikabahatika kuwapata wadada wawili ambao ndio walikuwa wapishi kwenye ile biashara, mimi nikawa asubuhi nikienda chuo jioni naporudi nakuwa nao pale nikiwapa usaidizi, Biashara ikaanza rasmi kwa shida za hapa na pale, ndani ya mwezi bado wateja walikuwa sio wengi sana.

Ila baada ya mwezi kupita ndio mambo yakaanza kunyooka watu wakaanza kupazoea pale kutokana na chakula kilikuwa ni kizuri na usafi ulikuwa wa hali ya juu, hivyo asubuhi ilikuwepo chai kama kawaida na mchana chakula cha uhakika kilipatikana, na baada ya wateja kuongezeka ikabidi nimuongeze tena mtu mmoja asaidiane nao.

Na mwezi uliofuatia nikaongeza huduma nyingine ya mchemsho wa kongoro na chapati, kitu ambacho kilivuta wateja wengi sana na kiliongeza faida ikawa kubwa kwenye ile biashara na nikaongeza wahudumu jumla wakafikia watano, kwa ile ile biashara, so kila siku baada ya kuwalipa wale wadada hela yao mimi nilikuwa naondoka na faida ya 30 hadi 50 kwa siku, kutokana na kuongeza mchemsho mida ya jioni, ilinipatia pesa sana.

Hivyo ndani ya miezi mitatu tu nilifanikiwa kumrudishia yule binti 1,000,000 pesa ya wazazi wake ambayo aliichukua benki bila wao kujua hivyo ikabakia laki tano tu, kiukweli niliona baraka kubwa sana kuwa na mwanamke mwenye akili kiasi kile, nilikuwa nikimshukuru mungu kila siku sababu ya kutikutanisha na mtu aliyebadilisha maisha yangu.

Hivyo baada ya kumaliza chuo sikukaa sana, nikabahatika kupata kazi kwenye kampuni moja ya wazungu ya ujenzi, kampuni ambayo nilikuwa nafanyia field mara kwa mara, hivyo wakanichukua moja kwa moja na wakanipa mkataba wa miaka miwili.

Nlijihisi mtu mwenye bahati ya ajabu kwani niliona matendo makuu ya mungu ndani ya maisha yangu, hivyo mshahara ukawa unaingia hivyo mapato yangu yote kwa mwezi ya biashara na mshahara wangu nlikuwa sikosi milioni tatu kwa mwezi tu.

Hivyo mapema nikaanza taratibu za kujenga huku nikijiandaa kwenda kutoa taarifa kwa wazazi wangu juu ya nia yangu ya kutaka kuowa kisha niende nikamtambulishe msichana wa maisha yangu kwa wazazi wangu ili wamjue na watoe baraka zote ili tuweze kufunga ndoa hata ya bomani sawa tu kwani tulishakubaliana kila kitu na tukiamini kuwa mungu wetu ni mmoja hivyo dini haitokuwa chanzo cha sisi kutengana.

Hivyo nlipopata nafasi nikasafiri hadi kilimanjaro kwa wazee wangu ili niwape taarifa za mimi kuoa na wao wanipe baraka zote pamoja na ruhusa ya kumleta mpenzi wangu ili wamjue na taratibu nyingine zifuate, lakini kipindi hichi sikugusia dini yake wala kabila mimi niliwaambia tu nimepata mchumba na ni mwenyeji wa Zanzibar

Baada ya kurudi Dar nilikaa kama mwezi na nikamjulisha Ilham(mpenzi wangu) kila kitu na tarehe ya kwenda Nyumbani kilimanjaro ili wazazi wangu wamjue, baada ya kumpa hizo Taarifa alizipokea kwa furaha sana na kwa mikono miwili na tukapanga tarehe ya safari

Siku ilipofika tukasafiri hadi kilimanjaro, tukafika salama na tulipofika nyumbani wote tulipokelewa vizuri bila shida yoyote tena tulipokewa kwa furaha wakiwemo wazazi wangu, shangazi zangu ba baba zangu wadogo wote walikuwepo siku hiyo

Baada ya kumtambulisha kikaandaliwa chakula pale na vinywaji kama katafrija kadogo, shangazi zangu wakampokea Ilham vizuri na dada zangu pia walimpokea vizuri na nikajua kuwa mambo yameenda vizuri .

Siku niyomtambulisha Ilham kwa wazazi na Ndugu zangu nakumbuka moyo wangu ulijawa na amani na furaha ya kipekee na nikadhani maisha yangu yanaenda kubadilika kwa sababu ya kumpata mschana mwenye Upendo wa dhati na akili ya kipekee, Nilifarijika sana na nlijiona mwenye bahati kwani ni watu wachache wanaoweza kubahatika kupata wenzi wa maisha wenye mapenzi ya kweli namna ile.

Baada ya tafrija ile ya utambulisho kuisha na huku nikijua kuwa mambo yameenda vizuri, ilipofika mida ya jioni baba yangu aliniita faragha na kunieleza kuwa kesho asubuhi yeye pamoja na mama na baba zangu wadogo watakuwa na kikao cha siri na mimi hivyo nisiondoke kuelekea Dar hadi kikao hicho kifanyike ndio mambo mengine yaendelee.

Sikuwa na jinsi ikanibidi niahirishe safari ila ilipofika asubuhi ikanibidi nimuwahishe Ilham ,ili apate basi la mapema kwani jioni alitakiwa kupanda boti moja kwa moja kuelekea zanzibar, nakumbuka siku hiyo ilinyesha mvua kubwa lakini tulibahatika kupata basi la mapema na akaondoka huku akiwa na furaha akijua kuwa ahadi yetu ya kufunga pingu za maisha inaenda kutimia na kilichobakia ni upande wa wazazi wake tu kunipokea.

Baada ya Ilham kuondoka mimi ikanibidi nirudi nyumbani ili nikawaskilize wazee wangu ni kipi walichotaka kuniambia, nilipofika nyumbani baada ya chai ya Asubuhi baba akawapigia sim baba zangu wadogo akiwajulisha kuwa wao ndio wanaosubiriwa ili kikao kianze.

Baada ya baba zangu wadogo kufika na mama pia akiwepo kikao kikaanza rasmi huku mzee wangu akibadilika na kuwa kama mtu ambae hakuwa na furaha usoni mwake, akionyesha dalili za kuchukizwa na jambo fulani. Pale pale nilianza kuwa na wasiwasi nikaona kuwa kuna jambo halipo sawa lakini nikakaa kimya tu ili nisikilize nini wanachotaka kuniambia.

Baba akawaambia baba zangu wadogo kuwa hatokaa aruhusu tena yaliyomkuta marehem kaka yake(baba yangu mkubwa) yajirudie, akasema kuwa familia ilipitia mtihani mzito sababu ya kaka yake, kubadili dini kisa mwanamke, akasema kuwa "Nadhani mnamkumbuka kaka yetu Minja nini kilimkuta baada ya kubadili dini na kumuowa mwanamke wa kiislam"

"kaka yetu alibadilika na kuwa kama mtu aliyechananyikiwa, pesa na mali zote zilipukutika na kupotea sababu ya yule mwanamke, Kuacha dini yake na kuhamia kwingine ndio alijichimbia kaburi lake mwenyewe, Kaka yetu alikufa kifo cha mateso makali na nadhani mnajua kabisa familia hii ni jinsi gani iliteseka nae na kuumizwa na yaliyomtokea" Akaendelea kusema kuwa " Baada ya kaka yetu na wazazi wetu kufariki mimi ndie baba niliyeachiwa uangalizi wa familia hii na sitoyaruhusu makosa yaliyotuumiza huko nyuma yajirudie tena, Na asiyenisikiliza afanye maamuzi yake yeye mwenyewe asinishirikishe. "

Kisha akasema kuwa Mwanangu Richard(Mimi) ,Maamuzi niliyoyachukua kumleta mchumba wangu hapa nyumbani kumtambulisha ni mazuri sana na ni ishara kuwa nimekuwa mtu mzima, lakini hatoniruhusu kamwe kuowa binti wa kiislam kwa imani ya mambo mazito yaliyomkuta marehem baba yangu mkubwa.

Mzee akasema kuwa familia hii haitoruhusu tena kumpokea mwanamke wa kiislam au mwanafamilia yoyote kuowa au kuolewa kwenye familia ya kiislam, na akasema Kuwa yoyote atakayethubutu asimshirikishe na yatakayokuja kumkuta atajijua yeye mwenyewe.

Baada ya kumaliza kuongea akatoa nafasi kwa kaka zake(Baba zangu wadogo), na Mama yangu pia nao waseme ya kwao ya moyoni ili isije ikaonekana kuwa naonewa, na kitu kilichoniumiza zaidi ni kuwaona baba zangu wadogo nao wakisapoti maneno aliyoyasema baba yangu kuwa wanawake wa kiislam sio wa kuowa na nikijiingiza huko ni kujitafutia mikosi.

Na kilichonitoa machozi kabisa mbele yao ni Mama yangu mzazi ambae nilitegemea atanitetea nae alizidi kumwagia petroli kwenye moto uliokuwa unawaka, akisema kuwa hata yeye hawezi kuniona nafia mikononi mwake sababu ya mikosi, akasema kuwa mateso aliyoyapata kumuuguza marehem shemeji yake (Baba yangu mkubwa) ni makubwa na hataki kisa hicho kijirudie tena kwani mimi ndio tegemeo la familia.

Baada ya kikao nilijihisi kama ni mtoto yatima kwani wale nliotegemea kunitia moyo ndio walikuwa mstari wa mbele kuniumiza. Machozi yalikuwa yakinitiririka kama mtoto kwani sikuamini kilichotokea mbele ya macho yangu, kiukweli kuanzia siku hiyo niliingiwa na chuki kuu ndani ya moyo wangu juu ya wazazi wangu kwa waliyonitendea kwani sikutegemea hata kidogo kama ni wao wamediriki kuchukua maamuzi kama yale.

Haikuwa rahisi kwangu kumuacha mwanamke aliyebadili maisha gangu kwasababu ya wazazi wangu. Niliumia moyo kwa kiasi kikubwa huku nikijiuliza maswali mengi iweje huyu huyu baba aliyenitelekeza kipindi nipo chuoni leo hii mwanamke aliyeniinua wakati wa shida na kunifanya nibadilike kiamaisha ndio aje amkatae kipindi hichi nna maendeleo?.

Usiku mzima nilikuwa nikilia lakini sikuwa na lakufanya, ila nilichoamua niliamka asubuhi ya saa kumi Alfajiri na kuondoka kimya kimya pale nyumbani bila kuaga kwani nilijawa na hasira kuu moyoni mwangu, nlijiisi sina ndugu tena kwani nliowategemea kunipa moyo ndio walioniumiza, niliona kumuacha mwanamke aliyepigania maisha yangu kipindi wazazi hawanikumbuki ndio itaniletea laana ya maisha.

Baada ya kufika Dar nilikuwa kama mtu nliyechanganyikiwa na mwenye majonzi, nilijiuliza maswali mengi kuwa leo hii nitaenda kumueleza nini Ilham, Niliona ni aibu kuu Mwanamke aliyeniongoza kimaisha hadi kupata mafanikio kukataliwa na wazazi wangu kisa dini tu.

Chuki zidi ya wazazi wangu na ndugu zangu iliongezeka hadi nikafikia hatua ya kukata kabisa mawasiliano nao na namba za sim nikabalilisha isipokuwa niliendelea kuwa na mawasiliano ya kimya kimya na mdogo wangu wa mwisho tu ambae nilikuwa namsomesha wakati huo alikuwa kidato cha tano, na ndie ndugu wa pekee ambae nilimuona kuwa hana hatia na alikuwa akinitia moyo kwa kila jambo.

Kitendo walichonifanyia ndugu zangu ilinibidi nikate mawasiliano nao kabisa hata misaada ambayo nilikuwa nawapa pale walipopatwa na shida niliikata kabisa kwa sababu sikuona faida yao na niliwaona ndio maadui zangu wakuu ambao kila siku walinifanya niwe mtu wa huzuni.

Hata bidii yangu ya kazi kazini ilipungua hadi wafanyakazi wenzangu wakawa wananishangaa ni kitu gani kilichonisibu, lakini ilibaki kuwa siri yangu tu pale kazini hivyo ikanibidi niombe mapumziko ya siku saba kwa kisingizio kuwa naumwa, ili nipate mda wa kuyaweka mambo sawa kwani hata Ilham mwenyewe nilikuwa bado sijaonana nae na alikuwa hajui nini kinaendelea kati yangu mimi na wazazi wangu.

Siku ya tarehe 15 june 2014, nakumbuka ilikuwa ni siku ya jumapili ,Ndio ilikuwa siku niliyosafiri kuelekea Zanzibar kwa ajili ya kuonana na Mwanamke niliyempenda Ilham, Niliondoka majira ya saa sita mchana huku nikiwa bado ni mtu mwenye huzuni iliyojaa moyoni mwangu.

Ndani ya boti nilikuwa nikiwaza mengi sana kwamba nitaenda kumueleza nini Ilham, nilijiuliza kama nikimwambia kuwa nyumbani wamemkataa atajiskia vipi wakati alipokelewa vizuri na ndugu zangu bila ya kuambiawa chochote kibaya, Nilihisi kuwa nikimwambia ukweli ndio nitaharibu kabisa na nitamfanya anione mimi ndiye niliyemkataa na sio ndugu zangu.

Lakini wazo lingine likanijia kuwa mwanamke unayempenda kweli huwezi kumficha kitu ili hapo baadae uwe huru, ili lolote litakalotokea liwe zuri au baya muwe tayari mmeshajipanga kulikabili, hivyo ikanibidi nibadili mawazo na nikapanga nikifika tu nimweleze ukweli wa kilichotokea baada ya yeye kuondoka kule nyumbani Moshi, Sikutaka kumficha chochote.

Boti iliwasili Zanzibar majira yaa saa saba na Nusu mchana na nilikuwa na begi dogo tu lenye nguo chache, Na wakati huo aliyekuja kunipokea alikuwa ni Ilham sababu ndio ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kufika Zanzibar.

Baada ya kuniona tu alinikumbatia kwa furaha sana na kuniambia, "karibu sana baby jiskie upo nyumbani " , lakini wakati huo akinikumbatia na kunichangamkia kwa furaha nilikuwa sipo kawaida kama alivyonizoea na macho yangu yalikuwa yamevimba kwa mbali kama mtu aliyetoka kulia hivi, hivyo ikabidi ashtuke na kuniuliza "Richard are you okay? "

Ghafla machozi yakaanza kunitoka nikajikuta nimeinama huku nikilia kwa uchungu hadi watu wakaanza kuhisi kuna kitu hakipo sawa kati yetu, Lakini nikajikaza kiume ikanibidi nivumilie tu na nimdamganye kuwa nna maumivu ya kichwa tu hivyo asijali tukifika hotelini nitameza dawa na everything will be ok.

Tukachukua bajaji eneo lile ikatupeleka hadi hoteli ambayo ilikuwa karibu na eneo lile, hivyo kutokana na sheria za kule na mambo ya maadili Ilham sikuingia nae hotelini bali ilinibidi nilipie tu room kwa siku mbili ambazo ntakuwa pale then nkamwambia Ilham kuwa tutafute sehem nzuri ya wazi iliyotulia nikamwambia kuwa kuna jambo nataka kuongea nae.

Lakini Ilham bado aliendelea kuwa na wasiwasi na aliona dalili zote kuwa kuna kitu hakipo sawa hata kwa muonekano tu nilipungua mwili kwa kiasi kikubwa kutokana na msongo wa mawazo na akili yangu haikuwa sawa kabisa. Hivyo akanimbia niende nae nyumbani kwao nikamsalimie mama yake akaniambia kuwa alishamtaarifu mama yake kuwa amepata mchumba ambae anataka kumuowa ambae ndio mimi.

Baada ya Ilham kuniambia kuwa anataka niende nae tukamsalimu mama yake, kwani alikuwa anataka kuniona nilijikuta kwa mara nyingine tena natokwa na machozi huku nikilia kwa uchungu ikabidi Ilham atoe kitambaa chake na kunifuta machozi huku akiniambia kuwa ni kipi kilichonisibu.

Ilham akaniambia kuwa kama nna tatizo lolote nimwambie kuliko kuendelea kulia bila yeye kujua tatizo lililokuwa linanisibu ni nini, akaniambia kama ni kweli nnalia kwasababu ya kuumwa basi anipeleke hospitali kwani haikuwa mbali na maeneo yale.

Baada ya kutulia kidogo nikamwambia Ilham kuwa mimi ni mzima wa Afya lakini kuna jambo lililo moyoni mwangu na ndilo linalonitatiza na ndio lililonileta hapa Zanzibar siku ya leo, Nikamwambia kuwa siwezi kwenda kwa mama yake hadi nimuambie ukweli nini kilichotokea baada ya mimi kumtambulisha kwa wazazi wangu.

Nikamwambia ni heri nimueleze ukweli tu ili ajue mapema, asije na yeye akanipeleka kwa wazazi wake wakanipokea vizuri wakati kwangu mimi hakupo sawa,

Baada ya Ilham kusikia maneno yale akaniambia kwa sauti ya upole kuwa "Richard pleasee usije ukaniambia maneno ambayo yatauumiza moyo wangu, kumbuka nimeyatoa maisha yangu kwa ajili yako na ukiniacha mimi sitoweza kuishi tena,ni heri nikuambie ukweli mapema ".

Nikamwambia kuwa hata mimi siwezi kumuacha hata iweje hivyo aondoe wasiwasi, kisha ikanibidi nimuhadithie kila kitu kilichotokea baada ya yeye kuondoka, kuhusu kukataliwa na wazazi wangu kisa Dini zetu kuwa tofauti, ikanibidi nimueleze kila kitu bila kumficha chochote huku nikitokwa na machozi.

Ilham nae akashindwa kujizuia akaanza kulia kwa sauti ya chini huku akijifuta machozi kwa kitambaa chake, hakuyaamimi maneno niliyomwambia ,alihisi nimebadili mawazo hivyo nataka kuwa na mwingine .

Nikamwambia kuwa mimi siwezi kumuacha na tayari nimeshagombana na ndugu zangu kwa ajili yake, nikamwambia kuwa ni heri nife tu lakini sio kuishi bila yeye.

Nikamwambia kuwa yeye na mdogo wangu nliekuwa namsomesha ndio ndugu wa pekee waliobakia kwa sasa katika maisha yangu wenye uwezo wa kunipa faraja.

Nikamwambia kuwa bila yeye ni heri nife tu kwani sikuona sababu ya kuishi tena , kisha Ilham akaniambia kuwa "Naskitika sana kwa hayo yaliyotokea kwa wazazi wako lakini nakuomba Richard usije ukawachukia wazazi wako kwani ndio waliokuleta duniani bila wao usingekuwepo, endelea kuwaheshimu usiwachukie", akaniambia kuwa sisi ndio tumependana na mapenzi hayajali Dini wala kabila hivyo isiwe chanzo cha sisi kuachana .

Akaniambia kuwa hata ndoa ya kiserikali tutafunga tu, Dini zetu tuziweke pembeni kwani mungu wetu ni mmoja tu, kisha tukaondoka hadi nyumbani kwao kwa ajili ya kumsalimu mama yake mzazi.

Nilipofika nyumbani kwao nilipokelewa na mama yake vizuri sana na Dada zake pia walikuwepo kasoro baba yao tu ndio hakuwepo nyumbani alikuwa amesafiri, Mama yake Ilham alikuwa ni mama mchangamfu sana na mwenye upendo mkubwa.

Alifurahi sana kuniona kisha akaniandalia chakula na baada ya kula nikajitambulisha kwake na jinsi nlivyokutana na Ilham chuoni hadi leo hapa tulipofikia kuwa wapenzi.

Na kitu kilichonishangaza ni jinsi Mama yake Ilham na dada zake pia hawakushangazwa wala kushtuka kwa kuwa mimi ni Mkristo, mda wote walikuwa ni watu wenye furaha tu kuniona, mama yake alisema kuwa "Nimefarijika sana kukuona mwanangu,karibu sana na jiskie upo nyumbani" kisha akatania kuwa "Ila nasikitika mwanangu Ilham mda sio mrefu ataniacha mwenyewe hapa na sijui nani atanisaidia kazi zangu na mimi nishakuwa mzee sasa" aliongea huku akitabasam.

Pia akaniasa kuwa kama kweli nimempenda binti yake basi niwe serious, akaniambia kuwa hata tofauti zetu za dini tuweke pembeni, Akaniasa kuwa nisimchezee binti yake bali kama nna nia ya kweli ya kumuowa basi nimuowe na akaniambia kuwa wao hawana tatizo lolote na wala hawanilazimishi mimi kubadili dini,

Akasisitiza kuwa Allah atoae baraka na aliyetuumba ni mmoja tu hivyo Familia yake haina shida yoyote ,akaniambia kuwa hata kaka yake wa kwanza alimuowa binti kutoka Tanzania bara ambaye alikuwa ni Mkristo.

Akasema kuwa familia yao haikuwa na neno lolote juu yao bali walimuachia kaka aamue yeye mwenyewe mwanamke anaempenda na tulimpokea vizuri, kisha walifunga ndoa ya bomani nakumbuka ilikuwa ni mwaka 1982, na leo hii mwaka 2014 ndoa yao ina miaka 32 wakiwa pamoja na wana watoto watatu.

Akaniambia kuwa kama kweli tumependana basi tuonyeshe upendo wa kweli, akaniasa kuwa dunia ya sasa ina mengi yakiwemo maradhi, akaniambia kuwa asije akaja kusikia baada ya miaka mitatu tumeachana, akasema kuwa ndoa ni kifungo cha watu wawili ni hadi kifo kitakapowatenganisha, hivyo tujitafakari kwanza kabla hatujaamua hilo.

Akasema kuwa amefurahi sana kuniona na pia atamtaarifu baba yake na Ilham, na atakaporudi natakiwa nirudi tena Zanzibar ili anione na apate kunifaham, akaniambia kuwa nisiwe na wasiwasi wowote pia nijiskie nipo nyumbani.

Baada ya mama yake ilham kuongea maneno yale nilijikuta machozi yananilengalenga hadi nikaomba kwenda uwani, na nilipofika nilijifungia uwani nikaanza kulia kwa uchungu iweje huku nikubalike tena familia ya kiislam na kule kwetu Ilham akataliwe, kimya kikazidi hadi Ilham akanifuata kisha akanipa maji nikanawa uso, akaniambia kuwa nijikaze ili mama asije akashtukia kama kuna tatizo.

Hivyo ikanibidi nirudi ndani pale na niliporudi mama alishtuka akaniuliza vipi mwanangu macho mbona kama yamevimba?, nikamwambia kuwa nilisahau miwani ya macho ndio maana yanauma hivyo asijali, kisha nikamuaga kuwa natakiwa niondoke na boti ya saa mbili usiku ili niwahi kesho kazini, yote hayo ilibidi nidanganye ili niondoke mapema nisije nikaendelea kukaa pale mambo yakaharibika.

Kisha nikaondoka mida ya saa kumi na mbili jioni, wakaniaga huku wakipiga vigelegele nakumbuka hadi majirani pia walikuja akawatambulisha kuwa mimi ndie mme mtarajiwa wa Ilham hivyo ikawa ni furaha tu.

Nikaondoka jioni ile hadi hoteli niliyofikia kisha nikalala hadi ilipofika asubuhi nikampigia Ilham sim aje mida ya saa nne ili nimuage kwani nilitakiwa kuondoka na boti ya saa tano asubuhi, akaja na tukaagana huku akinibusu kwa furaha, nikaondoka kuelekea Dar.

Ilipofika Mwaka 2015 mwanzoni, nilifanikiwa kumtafutia Ilham kazi katika kampuni moja ya wajarumani na kampuni hiyo ilikuwa inadeal na uuzaji wa vifaa vya ujenzi, hivyo kuna mtu nikamuunganisha nae akaitwa kwenye interview na akafanikiwa kupata kazi.

Baada ya kupata kazi ikabidi aje Dar, wakati huo nilikuwa nishamalizia nyumba yangu hivyo tukaamia moja kwa moja na maisha yakaanza huku tukisubiria kufunga ndoa rasmi.

Tuliendelea kupambana na maisha na kila tulichokipata kwenye mishahara yetu lilikiweka sehem moja kwaajili ya kufanya mambo ya maendeleo, na kitu kizuri Ilham alikuwa ni mwanamke mwenye akili sana, akanishauri kuwa tufungue duka vifaa vya ujenzi maeneo yale.

Tukajichanga mimi na yeye tukapata frem tukafungua duka dogo la vifaa vya ujenzi kisha, nikamchukua yule mdogo wangu nliyekuwa namsomesha nikamuweka pale asimamie ile biashara kwani kipindi hicho alikuwa ameshamaliza kidato cha sita hivyo alikuwa anasubiria matokeo tu akijiandaa kwenda chuo.

Maisha yakaendelea na ilipofika mwaka 2016 mwezi wa nane ilham akapata ujauzito, na tulivyoenda kupima ikaonekana ni ujauzito wa watoto mapacha , hivyo doctor akatuambia tutarajie watoto mapacha.

Nililipuka kwa furaha na nikaona hii ndio itakuwa ni njia nzuri ya Ilham kukubalika kwetu hivyo moja kwa moja nikasafiri kwenda nyumbani moshi kuwataarifu wazazi juu ya ujauzito wa Ilham.

Nilipofika tu Mzee wangu alinifukuza kama mbwa akaniambia kuwa tokea mwaka 2014 nlipoondoka pale nyumbani leo hii ndio nimekumbuka kama nna wazazi, mzee akasema "Leo ndio umejua kama una wazazi sio?, toka hapa mshenzi mkubwa wewe na nnakwambia nikija kufa utapata tabu sana wewe" .

Kwa hasira akachukua ndoo ya maji kisha akanimwagia nikiwa pale nnje akiniamuru niondoke kisha akaniambia kuwa hataki kuniona na nisirudi tena na siku akifa nisilisogelee hata jeneza lake, na siku akifa nisipewe urithi wowote kisha akafunga mlango, akarudi ndani.

Nikabaki pale nnje nikiwa nalia tu nikiwa sina cha kufanya ikanibidi nigeuze kisha nikapanda gari hadi moshi mjini, kisha nikachukua room lodge moja iliyo maeneo ya pale ili nilale hadi asubuhi ndio niondoke kuelekea Dar.

Kesho yake safari ilianza na nikafika salama, baada ya kufika Ilham aliniuliza kuhusu hali za wazazi wangu machozi yalikuwa yakinitoka tu,kisha nikamwambia "Ilham mke wangu, wewe sasa ndio baba na mama yangu uliyebakia, wewe na mdogo wangu ndio ndugu zangu mliobakia, nimeshatengwa na familia yangu mimi na sina pakukimbilia ila yote namuachia Mungu tu".

Ilham akaniambia kuwa niache kulia kisha akanifuta machozi akiniambia kuwa yupo kwa ajili yangu na amejitoa maisha yake kwa ajili yangu hivyo tumuombe mungu ipo siku atabadilisha mawazo ya wazazi wangu na watabadilika tu.

Hivyo maisha yakaendelelea, Ilipofika mwezi wa tatu mwaka 2017 ilham alifanikiwa kujifungua salama watoto wawili mapacha, mwenyezi mungu alitujaalia kupata watoto wote wakike.
Nilimshukuru sana mungu na niliona ni zawadi ya pekee kutoka kwake, niliona maisha yetu yanaenda kubadilika kwani watoto siku zote ni huwa ni baraka ndani ya familia.

Furaha yangu ilikuwa ni kubwa sana kwani kuwa na watoto ilikuwa ni ndoto yangu ya mda mrefu na nilijua watoto ndio watakaotuunganisha mimi na Ilham kwa lazima.

Na kitu kilichonisikitisha zaidi ni kitendo cha wazazi wangu pamoja na ndugu zangu kutokanyaga kabisa Hospitalini alipokuwa amelazwa Ilham baada ya kujifungua, waliofi kapale Hospitalini walikuwa ni Wazazi wake Ilham pamoja na ndugu zake wengine wengi wakikuja huku wakiwa na nyuso za furaha machoni mwao.

Baba yake Ilham pamoja na mama yake walijawa na furaha baada ya binti yao kujifungua na wakasema kuwa kwa kipindi kirefu walikuwa wakisubiria kuapata wajukuu kabla siku zao za kuishi hapa duniani hazijaisha, wakasema kuwa dada zake ilhma bado hawajajaaliwa kupata watoto japo washaolewa hivyo hawa wa Ilham ndio wajukuu wao wa kwanza.

Baba yake ilham na mama yake wote tukiwa pale hospitali walituwekea mikono yao vichwani mwetu na kutupa baraka wakisema kuwa, Mwenyezi mungu atujaalie baraka na mafanikio tele katika hatua hii mpya ya maisha yetu pia wakatuasa kuwa tusichelewe katika jambo muhim la kufunga ndoa kisha baba yake Ilham akaondoka kuelekea Zanzibar huku mama yake na dada yake mmoja wakibaki kwaajili ya kumuangalia Ilham hadi atakapokuwa sawa.

Maisha yakaendelea huku nikiona baraka na mafanikio tele yakiongezeka maishani mwangu, nikaendelea kusonga mbele huku nikimuomba mungu aniepushe na laanza zote zilizojuu yangu.

Ilipofika Tarehe 16 mwezi wa pili mwaka huu 2018, nilipigiwa sim mmoja wa wale baba zangu wadogo akinijulisha taharifa mbaya kuwa baba yangu ni mgonjwa miezi mitatu sasa na akaniambia kuwa alipelekwa KCMC hospital ba baada ya kupimwa alikutwa na Kansa ya Koo, akaniambia kuwa iligundulika kuwa ipo kwenye stage ya pili hivyo wamempa transfer hadi Ocean road Dar kwa ajili ya matibabu zaidi.

Akaniambia kuwa nyumbani kwa sasa wana hali mbaya na hata hela ya matibabu imekosekana na dawa zake zina gharama kubwa na wameshindwa kuzimudu na hali ya kaka(baba yangu) ni mbaya kwa sasa.

Hivyo baada ya kuzipata zile taarifa nikamtaarifu ilham, na baada ya kumtaarifu alisikitika sana then akasema kuwa hamna namna hawa ni wazazi wetu hivyo nilazima mimi na wewe tujichangishe tulichonacho ili aweze kuja dar kwanza kwaajili ya matibabu mengine.

Ilham akatoa laki saba (700,000) na mimi nikatoa Milioni moja (1,000,000) kisha nikawasiliana na mama wafungue account ya benki kisha nikawaingizia Milioni moja na laki saba kwa ajili ya kulipa deni la kule KCMC na hela itakayobaki watumie kwa ajili ya kulipia usafiri wa ndege ili waje hadi dar matibabu yaendelee.

Baada ya kufika dar nikaenda na gari hadi Airport kwa ajili ya kuwapokea, lakini nilipofika tu mzee baada ya kuniona akasema kuwa hataki kuniona na nipotee mbele yake, akasema ni heri afe kuliko kuniona mbele yake.

Nikajiuliza maswali mengi kuwa inamaana mzee hakuambiwa kuwa mimi ndie nliefanikisha hadi yeye kuja hapa Dar kwa matibabu?, nikajiuliza kwa nini aseme maneno kama hayo baada ya kufika, kosa langu lipo wapi?,

kwa kuwa mzee alishabadilika Ikanibidi nimtafute ndugu yangu mmoja ambaye ni mtoto wa shangazi yangu ili aje pale airport afanye yeye kumchukua mzee wangu pamoja na mama hadi kwake ili akae kwani mimi ilishindikana kutokana na chuki kubwa aliyoionyesha mzee wangu hivyo nikakosa la kufanya.

kibaya zaidi mzee wangu alikataa kwenda kukaa kwangu sehem ambayo kuna nyumba kubwa tu na huduma nzuri kutokana na hali yake kuwa mbaya yeye akaamua kwenda kukaa kwa binam yangu ilimradi tu anikomoe, lakini mimi Nilimuachia mungu tu.

Binam yangu akawachukua hadi kwake kitunda alipokuwa amejenga na nyumba yenyewe ilikuwa bado hata haijamaliziwa , ikanibidi sasa niweke chuki pembeni nimpiganie mzee wangu afya yake kimya kimya bila yeye kujua.

Cha kwanza niliwatuma mafundi waende wakaangalie nyumba yake ni sehem gani alikuwa hajamalizia, hivyo nikawapa na hela wakaimalizia ile nyumba na umeme pia nikampa hela ukafungwa.

Hayo yote nlikuwa nafanya ili mzee akae sehem nzuri isiyokuwa na shida kutokana na hali yake ilishakuwa mbaya , kisha nikampa Gari yangu binam yangu ikae pale kwake ili awe anampeleka nayo Mzee wangu hospitalini na hela ya matibabu matumizi mengine yote yaliyokuwa yakitakiwa nilikuwa natoa mimi, na mama watoto wangu Ilham pia alikuwa akiichangia kwa kiasi kikubwa .

Ndani ya miezi mitatu ya matibabu tulitumia karibia milioni 12,000,000 na hali bado ikawa ni mbaya, na mwanzoni mwa mwezi huu tumepewa taarifa na madokta kuwa Cancer yake ipo kwenye stage ya Mwisho hivyo hana mieazi zaidi ya mitatu kuishi na matibabu hayawezekani tena, hivyo tumuombe mungu tu au apelekwe nyumbani asubirie siku yake tu.

Na yote hayo yakiendelea mzee wangu naona kifo kinamjia na anaondoka na kauli nzito, na sasa amefunga kauli bila ya kunitamkia neno lolote la heri, mzee anaondoka na kinyongo chake moyoni mwake, na alisema hata jeneza lake nisilisogelee na akifa maisha yangu yatakuwa ni ya tabu.

Lakini namshukuru mungu kwa yote kuwa kazi yangu mimi kama mtoto kumsaidia nimeitimiza na sitarajii kupata laana yoyote, japo mwanzoni niliweka kisasi lakini kwa sasa nimemuachia mungu

Lakini baba yangu ameniacha Dilema, namuona anaenda kaburini huku akiwa na kinyongo pasipo mimi kujua kosa langu ni nini, nitaendelea kumpenda mke wangu Ilham na yote namuachia mungu.

===========******=============


MWISHO
 
Last edited:
Tatizo lako ni kwamba ulikwenda kuwaomba ruhusa wazazi wako ya kuoa huyo binti ndio maana walipata legitimacy ya kukukatalia. Ungeenda kuwa taarifu kuwa unaoa wasingekukatalia.
Mkuu kuwa mtulivu na wala story haijaisha soma vizuri kwanza
 
Kuna watu wanaishi maisha ya tabu na matatizo kisa mashinikizo ya wazazi wao.

Tatizo ni kukaririshwa na vitabu vya dini kuwa Wazazi ni Mungu wa pili, kwamba sikiliza kila uambiwacho nao.

Lkn kwa upande wangu, mimi nakuona wewe ndie dhaifu, kwa elimu uliyofikia hupaswi kushinikizwa, bali kushauriwa.

Ushauri waweza kuukataa au kuukubali baada ya kufikiri na kutafakari kama inafaa kwako na yenye maslai.

Pole sana
 
Kuna watu wanaishi maisha ya tabu na matatizo kisa mashinikizo ya wazazi wao.

Tatizo ni kukaririshwa na vitabu vya dini kuwa Wazazi ni Mungu wa pili, kwamba sikiliza kila uambiwacho nao.

Lkn kwa upande wangu, mimi nakuona wewe ndie dhaifu, kwa elimu uliyofikia hupaswi kushinikizwa, bali kushauriwa.

Ushauri waweza kuukataa au kuukubali baada ya kufikiri na kutafakari kama inafaa kwako na yenye maslai.

Pole sana
Mkuu umeongea kitu cha ukweli na hili jambo sitokaa nisamehe na limeniwekea kisasi moyoni mwangu
 
Back
Top Bottom