Sirro: Lissu atahakikishiwa usalama wake atakaporejea nyumbani

Amesemei kurejea kwake kutakasaidia kukamilisha upelelezi na kufahahamu waliohusika na shambuli lake.

Kamanda Sirro amesema kurejea kwa Lissu kutasaidia kukamilisha uchunguzi na kufahamu waliohusika na shambulio lake.

Akizungumza na Nipashe jana, Sirro alisema kama raia wengine wa Tanzania, anahakikishiwa usalama wake kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.

“Kwanza tunashukuru kuwa amepona na sasa anarejea… tutaweza kufahamu zaidi waliohusika na shambulio dhidi yake, lakini pili usalama wake ni jambo la muhimu kama raia mwingine yeyote wa nchi hii,” alisema na kuongeza: “Ndio maana hata wewe upo salama, kwa hiyo tutahakikisha anakuwa salama.”

Jumatano, mbunge huyo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alitaja tarehe rasmi ya kurejea nchini kuwa ni Septemba 7, mwaka huu.

Lissu ambaye kwa sasa anatembea kwa msaada wa gongo moja, amepanga kurejea siku hiyo tarehe ambayo mwaka 2017, alishambuliwa kwa kupigwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana.

Septemba 7, mwaka juzi, Lissu alishambuliwa kwa kupigwa risasi akiwa ndani ya gari nyumbani kwake Area ‘D’ jijini Dodoma na watu hao wakati akitoka bungeni.

Akizungumza na gazeti hili Jumatano, Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Patrick Ole Sosopi, alisema Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe, aliwapa taarifa kuwa Lissu amemwambia kuwa atawasili nchini tarehe hiyo.

“Tuliambiwa na mwenyekiti wetu kuwa Lissu amesema atarejea Tanzania Septemba 7, mwaka huu na atakuwapo kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa,” alisema.

Katika ukurasa wa Bavicha Instagram, waliandika: “Lissu atawasili nchini Septemba 7, mwaka huu na mapokezi yake yatatangazwa kitaifa.”

Awali taarifa za kurudi kwa mbunge huyo zilianza kusambaa kupitia video fupi ikumuonyesha Mbowe akiwataarifu wanachama wa chama hicho kuhusu kurejea kwa Lissu.

Baada ya shambulio hilo la risasi, Lissu ambaye ni Mnadhimu Mkuu wa Upinzani Tanzania alipelekwa Hospitali ya Rufani ya Dodoma kwa matibabu ya awali na siku hiyo hiyo usiku alihamishiwa katika hospitali moja mjini Nairobi, Kenya.

Lissu ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema, alikaa siku 121 hospitali ya Kenya hadi Januari 6, mwaka jana, alipohamishiwa hospitali nyingine nchini Ubelgiji ambako Desemba 31, alimaliza matibabu yake ya awali na kuanza ziara nchi mbalimbali.

Januari 19, mwaka huu, Lissu alihojiwa katika kipindi cha Dira ya Dunia cha Idhaa ya Kiswahili ya BBC na kuonyesha nia ya kugombea urais mwaka 2020 kama wanachama na viongozi wenzake wa Chadema watampa ridhaa hiyo.

Januari 21, Lissu alihojiwa kwenye kipindi cha HardTalk kwenye Televisheni ya BBC na mtangazaji maarufu Stephen Sackur, kipindi ambacho kilizua mjadala mkubwa kutokana na namna alivyojibu maswali.

Februari 20, mwaka huu, Lissu alifanyiwa upasuaji wa 23 wa mwisho kwenye goti la mguu wa kulia katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Leuven, Gasthuisberg nchini Ubelgiji, na alisema baada ya hapo atarejea Tanzania.


CC: Petro E. Mselewa
 
Back
Top Bottom