Siri za Siasa; mojawapo ni hii | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Siri za Siasa; mojawapo ni hii

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by George Kahangwa, Jan 4, 2010.

 1. George Kahangwa

  George Kahangwa Verified User

  #1
  Jan 4, 2010
  Joined: Oct 18, 2007
  Messages: 539
  Likes Received: 14
  Trophy Points: 35
  Mara kadhaa nimealikwa katika makongamano ya vijana kuzungumzia kwa mfano nafasi ya vijana katika siasa. Kutokana na yale tuliyofunzwa shululeni kuhusu uandishi wa mada za kuwasilisha (presentation) nilijikuta mara zote nikiingiza ainisho la neno siasa katika utangulizi wa mawasilisho yangu. Nakumbuka mwaka fulani katika ukumbi wa shule ya sekondari ya Perfect Vision ya jijini Dar es Salaam, niliiambia hadhira mbele yangu hivi; Siasa maana yake ni njia azitumiazo mtu au kundi la watu kupata nguvu na madaraka, na ikitokea mtu akapata nguvu hizo huendelea na hatua ya pili ya njia hizo ili kuhahihisha anabaki na nguvu zake au na madaraka yake kwa lengo la kuendelea kufanya kile alichokikusudia. Kinachogomba hapo ni nguvu azipatazo mwanasiasa anazitumia kwa maslahi ya nani.
  Baada ya mawasilisho niliulizwa masawali kadhaa, mengi yakihusu msingi wa mada yaani vijana na nafasi yao katika huo utafutaji na utumiaji wa nguvu. Wakati wa chai, alinifuata kijana mmoja akaniuliza hivi; ‘kumbe mwenzetu uko katika siasa, nini siri ya urembo?’ kwa kuwa aliuliza swali kiutani, niliishia kumjibu (pengine bila kutafakari sana); ‘sio siri, ni kuamua tu’. Tuliishia kucheka na hatimaye chai ikawa imeisha, kuashiria mwisho wa kongamano, maana kabla ya chai vikumbo vya kumwona mwekahazina na wasaidizi wake vilikuwa vimeishapigwa.
  Leo hii ninapotizama nyuma, ninawiwa kutafakari, nini siri ya mtu kuwepo katika siasa, kwa maneno mafupi nini siri ya siasa. Majibu yanaweza kuwa mengi, lakini leo nataka kuwashirikisha jibu hili, ambalo naamini kwa hakika linadokeza siri hasa ya siasa.
  Jamii nyingi duniani zimegawanyika kiuchumi katika makundi mawili, yaani wenye uwezo kiuchumi na wasio na uwezo huo. Yawezekana kukawa na kundi la katikati, lile la wenye uwezo wa wastani. Misemo mingi imekuwa ikitumika kuyaeleza makundi haya, matharani; wenyenacho na wasionacho, au walalaheri na walalahoi. Kila moja la makundi haya lina maslahi yake katika uchumi ambayo hayana budi kulindwa au kutetewa. Wenyenacho wanatamani kisiwaondokee na ikiwezekana wapate zaidi. Wakati huo huo wasionacho wanataka wapate na jitihada zao zisiishie kufyonzwa na wenyenacho. Kwa ufupi hayo ndio maslahi ya makundi haya. Ni katika jitihada za kulinda maslahi, linapojitokeza kundi la watu (yamkini wajanja wajanja hivi) wakiuomba umma uwape nguvu za kutetea maslahi.
  Ukichukulia mfano wa mechi ya mpira wa miguu, timu ya walionacho dhidi ya timu ya wasionacho, marefa, makamisaa na chama cha mpira ndio hao waamuzi wa mechi. Mambo yanaweza kwenda vyema kama waamuzi hawa watahakikisha ‘fair play’ tu ndio inakuwa sheria-mama ya mchezo. Lakini imetokea mara nyingi kwamba marefa wameionea timu fulani na kuipendelea timu nyingine.
  Ninachomaanisha hapa, mwanasiasa ni refa wa kiuchumi katika jamii. Siri yake ni maslahi anayoyapata kutokana na kazi yake hiyo, na ili apate maslahi yake inategemea analinda maslahi ya nani. Mwanasiasa anaweza kuamua kulinda maslahi ya walionacho, mwingine anaweza kuamua kuwa mlinzi wa maslahi ya wasionacho, na mwingine akatetea maslahi ya pande zote mbili (au tuseme pande tatu, maana na yeye ana maslahi yake)
  Tukiziangalia siasa za Afrika (waweza kusema za Tanzania) za wakati huu, kwa mtazamo wangu, wanasiasa walioko madarakani ni watetezi na walinzi wa maslahi ya mwenyenacho. Kwa kufanya hivyo nao wananufaika. Katika utetezi wao huo wamekuwa wakiambatanisha unafiki kwa kujifanya wanatetea maslahi ya wasionacho kwa kuwagawia viperemende ndani ya karatasi za plastiki.
  Wakati huo huo kuna wanasiasa waliopewa jina la wapinzani. Hawa nao kwa kauli zao (nasisitiza; kwa kauli) wanajitahidi kuonekana wanatetea maslahi ya wasionacho, ingawa wengi wa wasinacho wanaelekea kutoelewa bado ni nini hasa hawa watetezi ‘wapya’ wanakimaanisha. Pengine wanajiuliza kwamba, hawa wapinzani kinachowasukuma ni mapenzi yao kwa wasionacho au na wao wanatafuta nafasi ya kuwa karibu na mwenyenacho ili wafaidi? Wasionacho wanaendelea kujiuliza, vipi hao wachache toka upinzani ambao tumewasikiliza, wakapenya hadi kwenye viti vya madaraka na nguvu, wamekuwa watetezi wenye tabia gani?
  Wanasiasa upenda kuoa ushaidi wa utetezi wao wa maslahi kwa alama ya mambo yaliyofanyika kwa jitihada zao, matharani miundombinu iliyojengwa, huduma za jamii na kadhalika. Ndugu msomaji, haijengwi barabara pasina kulengwa maslahi ya kundi. Barabara inaweza kujengwa ili mwenyenacho aufikie mzinga wa asali na kuirina kisawasawa. Lakini mwanasiasa kwa ulaghai wake atasimama na kuwambia wasionacho; jamani nimewajengea barabara ya lami. Wasionacho huenda wasione kwamba hiyo barabara badala ya kunufaika nayo, ndio kwanza inatumika kama mrija wa kufyonza kisima cha raslimali hadi kikauke. Mwigine atasimama na kusema; nipeni muhula wa pili nimejenga au nimepanua ‘intaneshono eapoti’ (uwanja wa ndege). Ni vyema umma ukaacha kushangilia tu upanuzi bila kujiuliza na kutathmini kwa kina upanuzi huo ni kwa maslahi ya nani. Yasije yakawa ni yale yale, ije midege isombe kila samaki na kutuachia mapanki, harafu ushuru wa mijidege uingizwe kwenye akaunti za wanasiasa.
  Mara nyingi hata mimi huwa najiuliza ninaposikia hili neno miundombinu; mbinu za nani? Huwa najiuliza pia, serikali bora ni ipi; inayojenga nyumba za wafanyakazi au inayojenga (inayosaidia kujenga) za wakazi? Mnh, ajengaye za wafanyakazi anataka wawe karibu na eneo la kunyonyewa nguvu kazi zao kwa maslahi ya mwajiri kisha wakistaafu ‘watajiju’, bali ajengaje za wakazi anaitakia jamii maisha bora ujanani na uzeeni.
  Ndugu zangu, kwa siri hii niliyowashirikisha, natoa changamoto ya kuendelea kutafakari sera za kiuchumi za wanasiasa dhidi ya maslahi. Unaposikia sera kama; kuvutia wawekezaji, ubinafsishaji, uchangiaji huduma na nyinginezo, unaona ndaniye maslahi ya nani.
  Siri ya siasa; ulinzi wa maslahi ya kundi ili mwanasiasa naye apate chake. Maslahi ya nani yanalindwa na mwanasiasa husika ndio yanayowatofautisha wanasiasa wetu. Kazi yetu kujua tunamchagua yupi. Angalizo; miongoni mwa wanasiasa, wapo wachache sana ambao wanatoa kafara maslahi yao wenyewe kwa ajili ya kulinda tu maslahi ya kundi wanachagua kulitumikia, yamkini hao ndio walio bora.
   
 2. Waridi

  Waridi JF-Expert Member

  #2
  Jan 4, 2010
  Joined: Mar 30, 2008
  Messages: 1,027
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 135
  Mkuu,
  The beatiful ones are possibly not yet born, Oops labda Mandela.
   
 3. C

  Charuka Member

  #3
  Jan 5, 2010
  Joined: Oct 20, 2009
  Messages: 56
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 0
  Pangekuwa na unafuu kama wangekuwa wanalinda maslahi ya walio nacho wazalendo tu, tatizo wanalinda ya mabwana zao wa kutoka mataifa ya kigeni, ndio maana wakipewa masharti na vyombo kama IMF na World Bank wanayakubali haraka. Ndio maana wawekezaji wa kigeni ndo wameshikiria uchumi wa nchi kwa sasa. Kazi tunayo...!
   
Loading...