Siri ya watoto kumzika baba yao akiwa hai Songea

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,357
8,067
Imani potofu za kishirikina walizonazo baadhi ya vijana wa Kijiji cha Mahanje, mkoani Ruvuma hasa anapokufa kijana mwenzao, zimesababisha vifo na mateso kwa wazee wanaotuhumiwa kuhusika na vifo hivyo.

Mbali na vifo, pia wamekuwa wakiwahusisha wazee na matatizo yao, ikiwemo kuumwa kwa madai wamewaroga.

Tukio la hivi karibuni ni la watoto kushirikiana na vijana wengine kumzika baba yao mzazi, Florence Komba (78) akiwa hai, wakimtuhumu kumuua mwanaye, Severine Komba (34) kwa imani za kishirikina.

Mbali na tukio hilo, Februari mwaka huu, vijana wa kijiji hicho waliwahi kuwacharaza viboko wazee watatu wakiwatuhumu kuhusika na kifo cha kijana mwenzao aliyekufa baada ya kuumwa na nyoka.

Mauaji ya Komba yametokea ikiwa imepita miezi miwili baada ya dunia kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukatili dhidi ya Wazee. Siku ya Wazee Duniani huadhimishwa Juni 15 ya kila mwaka.

Siku hiyo huadhimishwa kufuatia Azimio la Umoja wa Mataifa la Desemba 2011 lililotokana na maombi ya Shirika la Mtandao wa Kimataifa wa Kuzuia Ukatili dhidi ya Wazee.

Sababu za ukatili huo

Mmoja wa wazee wa Kijiji cha Mahanje kilichopo wilayani Songea, Suzo Hunja, alisema kuwa kijiji hicho kimekuwa na historia ya watu kuhusishwa na matukio ya kishirikina mara kwa mara na wazee kuchapwa viboko, kutishiwa na hata kunyanyaswa na watoto wao kwa kushirikiana na baadhi ya makundi ya vijana.

Hunja alisema yeye ni mmoja wa wazee waliokumbwa na msukosuko baada ya kifo cha kijana mmoja kilichotokea Februari mwaka huu.

Hunja alisema yeye na wazee wenzake watatu walipigwa viboko na kunyanyaswa na vijana wa kijiji hicho kwa tuhuma za kumuua Simon Mwinuka, aliyefariki kwa kuumwa na nyoka.

Alisema walinusurika kifo baada ya kuokolewa na polisi kwa kuhifadhiwa kwenye kituo cha Polisi Madaba wakiwa na mwili wa kijana huyo hadi kesho yake ulipokabidhiwa kwa familia kwa ajili ya mazishi.

Naye mzee Odillo Luambano, ambaye ni rafiki wa marehemu mzee Komba, alisema kijiji hicho kimekuwa na matukio mengi ya kutuhumiana ushirikina kutokana na imani za vijana wengi kuwatuhumu wazazi wao wachawi.

Luambano alisema vijana wamekuwa wakiwapiga na kuwatesa wazazi wao, huku akitoa mfano wa watoto wa marehemu Komba kwamba walikuwa na tatizo na baba yao kwa muda mrefu wakimtuhumu ni mchawi, hali ambayo ilikuwa ikileta mgogoro mara kwa mara .

“Watoto hao walipokuwa na tatizo au wakiugua walikuwa wanamtuhumu mhusika wa matatizo yao ni baba yao,” alisema Luambano.

Sababu ya kifo


Akizungumza na gazeti hili kijijini hapo mwanafamilia Agnes Luambano, alisema marehemu Komba ni mjomba wake na alimlea na hakuwahi kusikia anahusika na ushirikina.

Alisema Severine Komba (34) alikuwa na ugonjwa wa kifafa na ndio uliosababisha kifo chake na kwamba kuna ndugu zake wawili walikufa kwa kifafa.

“Wanafamilia walikuwa wakilia na kumtaja muaji ni baba yao ambaye mimi ni mjomba wangu na kuwa anawamaliza kuwaua. Hata hivyo, mtendaji aliwasihi wasiendelee kulia hivyo na kuwakalisha kikao na walikubaliana kuwa yameisha na wapo tayari kwenda kuzika, kumbe walikuwa wanaenda kumzika yeye,” alisema.

Agnes alisema mjomba wake kabla ya kuuawa aliombwa kwenda kuonyesha sehemu ambapo kaburi la Severine litachimbwa na alifanya hivyo.

“Lakini, mara baada ya kurudi nyumbani alifuatwa na vijana na kupakizwa kwenye Toyo ambayo ilikuwa imebeba mwili wa marehemu mwanaye Severine ambapo waombolezaji wengi walikuwa wakitembea kwa miguu.

“Kumbe alipigwa na magogo na kulazimishwa kubeba msalaba wa mwanaye na vijana wake kwa kushirikiana na baadhi ya wananchi wakimtuhumu kuwa ndiye aliyemuua mwanaye ambapo wakamshikilia kwa nguvu na kumtupa kwenye kaburi huku wakimfukia na udongo akiwa hai.

“Nimeumia sana, hasa nilipoambiwa ndugu zangu ndio wamehusika kufanya huo unyama, hata kama kweli kulikuwa na mgogoro huo bora wangemshitaki kuliko walichofanya, amekufa kikatili sana mjomba wangu, hakustahili kabisa hiyo adhabu jamani,” alisema.

Agnes aliiomba Serikali kuwachukulia hatua kali za sheria wote ambao wametenda unyama huo ili haki ya mjomba wake iweze kupatikana.

“Mjomba wangu alikuwa mtu wa watu, hakuna baya alilofanya, amekuwa mhasibu wa kijiji kwa miaka mingi na alipostaafu aliendelea na shughuli za kilimo, hajawahi kuwa na historia za ajabu ajabu ingawa ni kweli wanae saba kwa bi mkubwa wamekufa, ila kwa maradhi na si uchawi.

Ukosefu wa elimu


Mwenyekiti wa kitongoji cha Nguruma, Kijiji Mahanje, Moses Fussi alisema wananchi wa kijiji hicho wamekosa elimu sahihi, kwani kila ikitokea kifo, hasa akifariki dunia kijana tuhuma zote zinawaangukia wazazi kuwa wamemuua kwa ushirikina, inayosababisha chuki kati ya wazee na vijana.

Aliiomba Serikali kuingilia kati kwa kuwa baadhi ya watu wamekimbia kwa hofu na wameshindwa kuvuna mazao yao na wameyatelekeza mashambani.

Kijana wa kijiji hicho, Festo Mahundi alisema tukio hilo linahuzunisha na aliiomba Serikali ielimishe wananchi kuhusu ubaya wa ushirikina, huku akiwataka wazee wakae na vijana wao na kumaliza matatizo yao ili kurudisha amani.

Kiongozi wa dini

Mchungaji Kanisa la Ephata tawi Mahanje, Joachim Lugongo aliwataka wakazi wa kijiji hicho waokoke, kwani wasipokubali kumrudia Mungu wataendelea kuangamia.

Alisema vitendo vya ushirikina vimetawala kwenye kijiji hicho alichoishi kwa miaka mitano na sifa zake huko nje ni ushirikina.

“Nimewasihi sana wasiwahukumu wazee wao kuwa ndio wahusika wa matatizo yao, hata mimi nimeteswa sana na uchawi, lakini nimemshirikisha Mungu kwenye matatizo yangu, japo nilitembea na kuambiwa kuwa wanahusika ila nilimuomba Mungu kibali nisiwachukie wala kufanya jambo baya na nimeweza kuishi kwa amani,” alisema Mchungaji Lugongo.

Mbunge, Mwenyekiti wa kijiji

Mbunge wa Madaba, Dk Joseph Mhagama akizungumza na Mwananchi juu ya tukio hilo, alikemea tabia huku akisema ataendelea kutoa elimu zaidi kwa wananchi kupitia nyumba za ibada na mikutano ya hadhara kuacha kutekeleza vitendo hivyo alivyosema ni vya kikatili kupita kiasi.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Simon Para alisema wanaandaa vikao vya pamoja kati ya wazee na vijana ili kutafuta suluhu ya tatizo hilo.

“Tunataka kutoa elimu kwa wananchi, kwani matukio ya wazee kucharazwa viboko na kutishiwa maisha yanazidi kila kukicha, ikiwamo hili tukio la kwanza mtu kuzikwa akiwa hai” alisema.

Para alisema tukio linalofanana na hilo, nusura litokee Februari 8, mwaka huu, lakini lilizimwa na vyombo vya dola.

Alisema mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Simon Mwinuka alifariki dunia baada ya kuumwa na nyoka, lakini vijana walifanya vurugu wakiwatuhumu wazee watatu kuhusika na kifo hicho, akiwamo baba mzazi wa marehemu (Mzee Sabu Mwinuka).

Alisema wazee hao walifuatwa majumbani mwao na kutandikwa bakora na wengine waliwatandika viboko makaburini.

Mkuu wa wilaya alaani

Mkuu wa Wilaya ya Songea, Pololet Mgema, alisema alipopata taarifa hizo aliambatana na kamati ya ulinzi na usalama hadi eneo la tukio kushuhudia kilichotokea ambako alikemea kitendo hicho cha kikatili na hakipaswi kufumbiwa macho na lazima hatua za kisheria zichukue mkondo wake.

Alisema unyama huo hauwezi kuvumiliwa na alishangaaa kuona wanaotuhumiwa ni watoto waliozaliwa na mzee Komba.

“Binafsi nalaani tukio hili la kinyama lililotekelezwa na watoto wake, hii haikubaliki. Naagiza wote waliohusika kufanya kitendo hiki wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya dola ili hatua stahiki zichukuliwe, sitaki tena tukio kama hili lijirudie,” alisema mkuu huyo wa wilaya.

Alisema Kijiji cha Mahanje kimekuwa na matukio mengi ya ajabu akieleza kuwa miezi miwili iliyopita, alipata taarifa za vijana kutaka kumuua mzazi wao wakimtuhumu kwa imani za kishirikiana tukio alilosema lilidhibitiwa na Jeshi la Polisi waliowahi eneo husika.

Mkuu huyo wa wilaya aliwaonya wananchi aliodai wako mstari wa mbele kuhamasisha vurugu kuacha vitendo hivyo mara moja kwa sababu Serikali haitosita kuwachukulia hatua kali pale watakapobainika.

Chanzo: Mwananchi
 
Hatari sana vijijini watu wamechoka Wana hasira..Bora wangezika watu wengine wanaozingua kina mwiguru...timing unafanyiwa ishu za mirathi nashukuru wote wamekamatwa...afu watoto wakiwa wachache wanachanganya Bora wawe watano au sita
 
Imani potofu za kishirikina walizonazo baadhi ya vijana wa Kijiji cha Mahanje, mkoani Ruvuma hasa anapokufa kijana mwenzao, zimesababisha vifo na mateso kwa wazee wanaotuhumiwa kuhusika na vifo hivyo.

Mbali na vifo, pia wamekuwa wakiwahusisha wazee na matatizo yao, ikiwemo kuumwa kwa madai wamewaroga.
Asante kwa taarifa mkuu

Suala la elimu juu ya hizi imani potofu ni la muhimu sana
 
Pamoja na ukosefu wa Elimu nikisoma kwa makini hivyo vifo vina utata watoto saba wote hawawezi kufa kwa Kifafa. mimi naungana na wanafamili. Uchawi unarudisha nyuma sana maendeleo watu wanateseka kweli kweli ila kama huamini uchawi au hayajawahi kukukuta huwezi kuelewa
Haha mkuu kama mtu unaishi dsm unaweza kuona ao jamaa wakatili sana ila wenyej wa ruvma wanaelewa uhalisia wa ayo mambo kuna watu ata kwao awataki kurudi kuogopa ushirikina
 
Kauli ya mchungaji wa Ephata inaonesha kuwa kanisa hilo linachochea moto wa kuwaaminisha wanakijiji kuwa ushirikina upo hapo kijijini hivyo wanakijiji waokoke, hili ni tatizo lililopo kwenye makanisa ya walokole.
 
Nauliza tena..., hii ni karne ya 21 au 12 ?

Seems wakati tunasonga mbele wengine wanarudi nyuma
 
Wakati umefika wa serikali kuanza kuamini uchawi.
Bila hivyo ni shida sana
 
Kauli ya mchungaji wa Ephata inaonesha kuwa kanisa hilo linachochea moto wa kuwaaminisha wanakijiji kuwa ushirikina upo hapo kijijini hivyo wanakijiji waokoke, hili ni tatizo lililopo kwenye makanisa ya walokole.
Boss hilo halipingiki Kuwa uchawi upo
 
Back
Top Bottom