Siri kuu ya mafanikio; fanya kazi yako na wawezeshe wengine kufanya kazi zao

Makirita Amani

JF-Expert Member
Jun 6, 2012
1,781
3,074
Rafiki yangu mpendwa,

Hakuna kitu kimekuwa kinatafutwa kwa muda mrefu kama siri za mafanikio.

Mamilioni ya vitabu yameandikwa kuhusu siri za mafanikio.

Lakini siri hizo hazijafichwa kwa namna yoyote ile, ziko wazi kabisa.

Ambacho watu wamekuwa wanatafuta kwenye siri za mafanikio ni njia ya mkato ya kufanikiwa, kupata mafanikio ya haraka bila ya kuweka kazi. Hicho ni kitu ambacho hakijawahi kuwepo na wala hakitakuja kuwepo.

Dunia inaendeshwa kwa sheria za asili ambazo hakuna mwenye ujanja au uwezo wa kuzivunja. Huwezi kukusanya kuni na kuziambia nipe moto halafu zikakupa, lazima wewe uzipe moto kwanza.

Kanuni kuu ya asili kwenye eneo la mafanikio ni sheria ya kisababisho na matokeo. Kwamba kwa kila matokeo unayoyaona, kuna kisababisho chake. Kama shamba lina mahindi, ni kwa sababu kuna mbegu za mahindi ziliwekwa pale. Mambo hayatokei tu kimiujiza, bali yanasababishwa.

Kutokana na kanuni hii kuu ya asili kwenye mafanikio, tunaipata siri kuu ya mafanikio, ambayo iko wazi kabisa lakini tutaendelea kuiita siri kwa kuwa wengi bado hawaielewi.

huwezi-kuwaridhisha98.png
Siri kuu ya mafanikio ni kutoa thamani kubwa sana kwa wengine, kuwapa kile wanachokihitaji sana na wako tayari kukilipia, kuwafikia wenye uhitaji wa thamani unayotoa na kuwapatia. Sentensi hiyo ndiyo imebeba kila kitu kuhusu mafanikio.

Kwanza ni kujua kipi ambacho wengine wanakihitaji zaidi na wapo tayari kulipia ili kukipata. Mbili ni kuweka kazi katika kukifanya kitu hicho kwa ubora wa hali ya juu sana. Tatu ni uwe na njia za kuwafikia wote wenye uhitaji wa kile unachofanya. Na nne ni kuweza kuwashawishi watu hao wakipate na kukulipa.

Kipi sahihi kwako kufanya?

Watu wengi wamekuwa wakiuliza wafanye kazi au biashara gani ambayo itawalipa. Wengine wamekuwa wakihangaika na kila fursa mpya wanayoiona, lakini wanashindwa kupata mafanikio.

Ukweli ni kwamba, kila kazi na biashara inalipa, lakini hazilipi sawa kwa watu wote. Ulipaji wa kitu unategemea yule anayekifanya, kwa namna anavyokifanya kwa utofauti na viwango vya juu kabisa.

Fanya kazi yako.

Sehemu sahihi kwako kuanzia safari ya mafanikio makubwa ni kuijua kazi yako na kuifanya. Na hapo lazima ujue kusudi la wewe kuwa hapa duniani, uwezo mkubwa ulio ndani yako na vipaji ulivyonavyo. Hayo kwa pamoja yanakuwezesha kujua ni kipi uko vizuri zaidi kwenye kufanya.

Ukishajua kile ambacho uko vizuri kwenye kufanya, na watu wapo tayari kukulipa kwa kukifanya, hicho ndiyo unapaswa kukifanya.
Weka juhudi zako zote kwenye kufanya kazi yako. Achana na mengine yote ambayo hayana mchango kwako kufanikiwa kwenye kazi yako.

Ona ni wajibu wako kabisa kufanya kazi yako, kwani usipoifanya unawanyima wengine kile wanachotegemea kutoka kwako.

Uko vizuri kwenye kufanya kile ulichochagua kufanya, usipokifanya umechagua kuwadhulumu wengine, umeamua kuipunja dunia mchango wako ambao ni wa muhimu sana.

Wawezeshe wengine wafanye kazi zao.

Kama ambavyo wewe uko vizuri kwenye kile unachofanya, kuna wengine wengi wako vizuri kwenye yale wanayofanya.
Na wewe una mahitaji ambayo wengine wako vizuri kwenye kuyatatua.

Ni wajibu wako pia kuwawezesha wengine kufanya kazi zao kwa ubora, kwa kulipia kile ambacho wanafanya na una uhitaji nacho.
Hivyo ndivyo jamii bora ya binadamu inavyojengwa, kwa kila mtu kutoa thamani kubwa kwa ajili ya wengine.

Kutokufanya kazi yako vizuri ni ubinafsi. Kutokuwa tayari kulipia kazi nzuri wanayofanya wengine na unayohitaji pia ni ubinafsi.
Fanya kazi yako vizuri na kwa viwango vya juu sana na wawezeshe wengine nao wafanye kazi zao vizuri.

Unawezaje kuwafikia wengi kwa unachofanya?

Hili ni swali ambalo wengi hujiuliza, na msukumo wa swali hili unatokana na tamaa ya watu kutaka mafanikio ya haraka kwa njia za mkato.

Kila mtu anataka aanzishe biashara na ndani ya muda mfupi iwe na wateja wengi. Au afanye kazi na kila mtu aweze kuielewa haraka.
Hivyo sivyo siri hii kuu ya mafanikio inavyofanya kazi.

Unaweza kuwafikia wengi kwa kile unachofanya, lakini lazima uanze na wachache, uwape thamani kubwa mno na wao ndiyo wawe mabalozi wazuri kwa wengine. Wapate thamani ambayo hawakuitegemea kiasi cha kuwa tayari kuwaambia wengine namna wanavyonufaika kupitia wewe.

Ni zoezi hilo ndiyo litakuwezesha kuwafikia wengi zaidi, kwa sababu maneno ya watu kuambiana yana nguvu kuliko mbinu yoyote ile ya masoko.

Anza na watu wachache, wape thamani kubwa mno, hawatakaa kimya na thamani wanayoipata kwako, watawaeleza wengine ambao watakuja kwako ili wapate thamani kubwa zaidi.
Kidogo kidogo, kwa kuweka kazi na kujipa muda, unajenga watu wa uhakika wanaokutegemea kwenye kile unachofanya.

Simamia ubora na thamani.

Unapotoa thamani kubwa kama ambavyo tumejifunza hapa, wengi watasikia kuhusu wewe na watakuja wakitaka wapate thamani hiyo.

Kadiri muda unavyokwenda, ndivyo watu wanaokuja kwako kutaka wapate thamani unayotoa wanavyokuwa wengi.
Inafika hatua ambapo unakuwa na watu wengi kuliko unavyoweza kuwahudumia.

Hapo ndipo penye hatari nyingine kubwa, kwa sababu utatamani kuendelea kupokea wengi zaidi, lakini huwezi tena kuwahudumia wote kwa ubora wa hali ya juu.

Hapa ndipo unapaswa kujiwekea msimamo wa kuzingatia ubora na thamani.
Unapaswa kuhakikisha unaendelea kutoa thamani kubwa sana.
Na kuwapa wateja wako ubora wa hali ya juu mno.
Hivyo ni vitu ambavyo hupaswi kuruhusu viathiriwe na chochote kile.

Unapokuwa umefika kwenye ngazi hiyo ya kuwa na wengi kuliko uwezo wako wa kuwahudumia, lazima utumie kila gharama kuhakikisha kwamba thamani na ubora haviathiriwi.

Kama utatanua kile unachofanya ili uweze kuhudumia wengi zaidi, fanya hivyo ila linda sana ubora na thamani unayotoa.
Usikubali kwa namna yoyote ile kuathiri ubora na thamani.

Unaweza pia kuboresha vigezo vyako vya watu utakaokubali kufanya nao kazi na kuwakatalia wengine ambao hawafikii vigezo hivyo.
Na moja ya vigezo unapaswa kutumia ni uwezo wa kulipia.

Kama umeshaweza kutoa thamani ambayo watu wameielewa na wengi wanakuja kwako kuipata, basi anza kutoza gharama kubwa zaidi. Na waeleze watu wazi kwamba watalipa gharama kubwa zaidi ya wanavyoweza kulipa pengine, lakini watapata thamani ambayo hawawezi kuipata pengine, na kisha timiza hilo.

Kwa kufanya hivyo utapunguza wengi wasumbufu na ambao hawajajitoa kweli kwenye thamani unayotoa na kubaki na wale wanaoielewa na kuithamini.

Kuwa muwazi na mwaminifu sana kwenye kile unachofanya. Waeleze watu wazi nini wategemee kutoka kwako na timiza kila unachoahidi.

Usikubali mafanikio unayopata yawe kikwazo cha mafanikio zaidi, bali yafanye yawe mlango wa kupata mafanikio makubwa zaidi.

Hatua hii ni muhimu na wengi huwa hawaizingatii. Ndiyo maana unaweza kuona biashara inaanza vizuri mwanzoni, inakuwa na wateja wengi lakini baada ya muda inapoteza wateja wake wengi. Ni kwa sababu thamani na ubora havizingatiwi sana. Wewe pambana navyo kila siku.

Kadiri unavyojijengea sifa zaidi, endelea kutunza thamani na ubora unaotoa.

ngvu-ya-miujiza-na-elimu-ya-biashara-2.jpeg

Usijichukulie poa.

Haijalishi wewe ni nani na uko wapi sasa,
Una uwezo mkubwa na wa kipekee sana ndani yako,
Kuna vitu unaweza kuvifanya vizuri mno kuliko watu wengine wote.
Ukivijua vitu hivyo na kuvifanya, dunia inanufaika kwa kupata mchango wako,
Na wewe pia unanufaika kwa kupata kile unachotaka.

Nikusihi sana usiendelee kuchezea na kupoteza uwezo wako mkubwa kwa kuhangaika na mambo ambayo hayana tija kwako.
Kuzurura kwenye mitandao ya kijamii,
Kufuatilia maisha ya wengine,
Na kujaza uchafu kwenye mwili wako,
Vyote hivyo havina mchango kwako kuacha alama hapa duniani kwa kutumia uwezo wako.

Achana navyo, peleka nguvu zako kwenye kile unachoweza kufanya vizuri, toa thamani kubwa na wafikie watu sahihi na hivyo ndivyo utakavyoweza kuacha alama kubwa hapa duniani.
Weka vipaumbele vyako vizuri, jua muda ni rasilimali adimu ambayo ukishaipoteza hairudi tena.

Usijichukulie poa, wewe ni zaidi ya unavyojijua na kujitumia kwa sasa, jijue zaidi na jitumie kwa viwango vikubwa ili uweze kufanya makubwa hapa duniani.

Kama ungependa kupata usimamizi wa karibu kabisa kwenye kulijua kusudi la maisha yako na kuliishi karibu kwenye KISIMA CHA MAARIFA. Hii ni jamii ya tofauti na ya kipekee kabisa ambayo inakusukuma kufanya makubwa kwenye maisha yako.
Kujiunga tuma ujumbe kwa wasap kwenda namba 0717 396 253.

Ni imani yangu umejifunza kitu muhimu hapa, ila kujifunza pekee haitoshi, nenda kachukue hatua mara moja.
Kaa chini na ujitafakari, ujijue mwenyewe na ujue kile ambacho uko vizuri kwenye kukifanya, kisha weka akili na nguvu zako zote kukifanya kwa viwango vya hali ya juu sana.

Rafiki yako anayekupenda sana,
Kocha Dr Makirita Amani.
 
Me nakomenti kutokana na heading, huko kwingine watosoma wengine na kukomenti.

Iko hivi, issue ya kuwawezesha wengine wafanye kazi ili nifanikiwe nadhani si kwa Afrika, maybe umekusudia bara lingine.

Unafiki, kutokupendana nk hivi ndivyo vinamfanya mtu mweusi kutoweza kufikia viwango vya juu.

👉🏾I still learn to live with people.
 
Me nakomenti kutokana na heading, huko kwingine watosoma wengine na kukomenti.

Iko hivi, issue ya kuwawezesha wengine wafanye kazi ili nifanikiwe nadhani si kwa Afrika, maybe umekusudia bara lingine.

Unafiki, kutokupendana nk hivi ndivyo vinamfanya mtu mweusi kutoweza kufikia viwango vya juu.

👉🏾I still learn to live with people.
Mkuu,
Ungejitahidi usome kabla ya kucoment.
Dhana ya kuwawezesha wengine wafanye kazi yao niliyozungumzia siyo kwa kuwasaidia.
Soma utaelewa vizuri.
Ni kitu ambacho tayari kinafanyika kwa sababu jamii haiwezi kwenda hivyo, ila sasa unachagua kukifanya kwa makusudi kabisa.
 
Nikijaribu kuangalia asilimia kubwa ya waliofanikiwa , iwe kitaaluma kiuchumi, kijamii ama kifedha ni dhahiri wanaangukia ndani ya hizo principal mbili.

Ni either wamesucrifice kwaajili ya wazazi wao masikini, au watoto wao wawapendao kwa dhati.

Hii inatosha kabisa kusema, hili andiko ni Sahihi Sana.
 
Utoe tu utoe tuu wewe utabaki na nini.
Naona wengi wanaifanikiwa ni wenye roho mbaya.
 
Back
Top Bottom