Simulizi za kusisimua: Vijana wenye msimamo mkali mlimani enzi hizo


M

maggid

Verified Member
Joined
Dec 3, 2006
Messages
1,084
Likes
398
Points
180
M

maggid

Verified Member
Joined Dec 3, 2006
1,084 398 180
- Hawakupenda anasa ya kula nyama kutoka Australia na mayai kutoka Israel!

Ndugu Zangu,

Mwanazuoni Born Again Pagan amepata kusimulia haya kwenye mtandao wa mjengwablog.

"Nilianza masomo ya chuo kikuu hapo Mlimani (1966) katika mazingira hayo ya kusisimua yaliyokuwa yamejijenga au kuendelea kujijenga. Kampasi (Campus) ilipendeza sana, wanafunzi wa kwanza ndio tu walichangia vyumba vya kulala, isipokuwa wale walioishi Hall No. 1 (London Hall). Mashuka yalibadilishwa kila siku ya Jumanne. Chakula kilikuwa ni kizuri sana: mayai kutoka Israel, nyama (ng’ombe na kuku) na apples kutoka Australia, na samaki sijui kutoka wapi! Chai na biskuti kwa wingi saa nne asubuhi na saa kumi alasiri.

Mwanzoni mwa mwaka, tulikipewa pesa za matumizi, ikiwa ni pamoja na
kukopa Wizarani shilingi 500/- (kuzilipa baada ya kuanza kazi). Wanafunzi wengi walikuwa wakikosa kuingia madarasani shauri ya “pesa kibindoni” au kwa msemo wa siku hizo “bumu” (boom)! Wanafunzi wa kiume waliweka hata vimada wa kike hadi “bumu” ilipokauka!
Mwanzo wa mwaka ulikuwa pia ni “bumu” kwa watu wengi wasio wanafunzi. Waliibia kuja kula hadi hapo vitambulisho vilipotolewa na njia nyinginezo za kudhibiti kula mara mbili au tatu zilipotekelezwa kwa wanafunzi!
Najua wakati wa Juma la Kwanza la Kuzoezeshwa (Orientation Week), tulifundwa namna ya kuishi katika mazingira hayo ya ki-elimu na yale ya maudhui ya kufahamiana na kuelewana (social growth), ikiwa ni pamoja na ustaarabu (etiquettes) wa chumba cha mlo: jinsi ya kutumia uma, vijiko na visu na chakula gani kinaanza!

Wenzetu wenye msimamo mkali wakawa wanalalamika, “Eti wanatufundisha kuwa wastaarabu! Ni nani atatupa vyeti vya ustaarabu? Hatukuja hapa kujifunza namna ya kula, tumekuja kupata ma-digrii!”
Nakumbuka mwaka wangu wa kwanza na wa pili, kila baada ya miezi kama mitatu hivi, jioni moja tulikuwa tunaandaliwa Hall of Residence Dinner Evening – kana kwamba tuliishi katika hoteli ya Nyota Nne au Tano – na dansi la kukata shoka! Mwishowe, wenye msimamo mkali wakakataa hayo ya Dinner; tulikuwa na chakula cha jioni ambacho kilikidhi mahitaji ya siha na kutujenga akili.
Wanafunzi wengine waliokuwa na akili za huruma (compassion) kwa maskini na ma-kabwela walishauri, pembeni, hizo pesa za “dinner” zitumike kwa ajili ya maslahi yao. Lakini wanafunzi wenye kupenda ulevi (unywi) walishauri kuwa hizo pesa zitumie kuongezea vinywaji; wakashinda! Baadhi ya wanafunzi “wanywi” wakaanza kukusanya hata makesi ya bia. Hatimaye, ikaamuliwa kuwa kila mmoja apewe vocha tatu kwa ajili ya kupata chupa tatu za bia.

Lakini wapi! Walikuwepo wanafunzi wengine ambao hawakunywa bia. Kwahiyo, wenye kupenda “unywi” zaidi wakawa wanawaomba wapewe hizo vocha zao kiasi cha mmoja kukusanya vocha za bia kumi au zaidi!
(Tuyaache hayo ya unywi!) ... Wengi wetu hatutamsahau Daktari m-Ulaya wa dispensary yetu! Jina lake limenitoka kidogo...tulimwita “Dr. Nyurosisi” (Neurosis) kwa sababu kwake kila tatizo la kuumwa kwa mwanafunzi lilisababishwa na “neurosis”!

Wanafunzi wa ki-Tanzania walikuwa ndio wengi. Kwa bahati mbaya, wenye asili ya ki-Asia walikuwa na ubaguzi wao. Wazazi wao hawakupenda watoto wao, hasa mabinti, waje waishi kwenye mabweni Mlimani. Walitarajia kuwa wanawaleta kutoka majumbani kwa magari kila asubuhi na kuja jioni baada ya masomo kuwarudisha tena kwenye viota vyao vya ubaguzi. Serikali ilikataa maombi yao.
Sisemi kuwa kila m-Tanzania mwenye asili ya ki-Asia alikuwa mbaguzi. La hasha! Vijana wengine, kama akina Issa Shivji, Hirji, Sumra na Meghji walijumuika nasi wa-Matumbi bila ubaguzi wowote. Lakini kulikuwa na fununu kuwa baadhi yao walikuwa wakipata wakati mgumu kutoka kwa “dugu zao” waliowashitaki mbele ya jamii yao huko mjini!

Anasimulia Born Again Pagan kwenye mjengwablog.com
 

Attachments:

  • File size
    10.5 KB
    Views
    107
fdhly

fdhly

Member
Joined
Aug 5, 2013
Messages
22
Likes
26
Points
15
fdhly

fdhly

Member
Joined Aug 5, 2013
22 26 15
aaaaah mlimani bhana..hivi mlikuwa mnalima au mnapanda.. maana hadithi tamu...!
 

Forum statistics

Threads 1,274,224
Members 490,637
Posts 30,505,510