Simulizi ya mama aliyekalia maji ya chumvi kutibu fistula

Juma Issihaka

New Member
Sep 25, 2019
3
3
Na MWANDISHI WETU

YUNIS Simon (50) si jina halisi mama wa watoto watatu mkazi wa Mkoa wa Simiyu , ambaye alitaabika na tatizo la kutokwa na haja ndogo na kubwa sehemu ya haja ndogo hali inayotajwa na wataalamu kuwa tatizo la fistula ya uzazi.

Mama huyo anabainisha tatizo la kutokwa na haja ndogo mfululizo lilimpata katika uzao wake wa kwanza mwaka 1994.

“Sikujua kama hili janga lilinipata,nilisikia uchungu na kukesha nao nikiwa na mama yangu mzazi , kituo cha afya kilikuwa mbali na nilipokuwa nikiishi,uchungu uliendelea mpaka asubuhi ilipotimu saa tano nakujifungua kwa usaidizi kutoka kwa ndugu zangu,

Nilipomaliza kujifungua nilisikia sauti ikiniambia muangalie mtoto na baada ya muda mfupi nilipoteza fahamu, huo ukiwa ni uzao wangu wa kwanza,”anasema.

Anasema wazazi wake walijitahidi kumwagia maji apate fahamu, lakini hali haikuwa hivyo walivyotarajia, hali ile ilidumu hadi saa 11 jioni alipopata fahamu na kujikuta katika eneo lililotapakaa maji mengi, akihisi maji hayo yalitokana na mvua.

“Sikujua kama nilipata tatizo cha kushangaza kwa takribani siku tatu sikupata haja kubwa , na siku ya nne niliona haja kubwa ikitoka eneo la haja ndogo na nilipomweleza mama aliniambia tatizo langu ni la kawaida hivyo napaswa kuvumilia kwani litaisha, “anasema.

Yunis anasema alivumilia tatizo hilo na baada ya miezi mitano baadae alirejea kwa mumewe, ambaye alikaa naye muda mfupi na kumtelekeza.

“Sikujua aligundua tatizo langu kwa kuwa sikumweleza chochote, nilikuwa makini sikuwa na uwezo na kukabiliana na changamoto za maisha nikiwa peke yangu,

Mtoto alipofikisha miaka mitatu nilimuacha na kurudi nyumbani ambapo nilipitia unyanyapaa mkubwa kutokana na harufu mbaya iliyonitoka sehemu za siri,

Nilikaa nyumbani ,mama yangu pekee ndiye aliyenitia moyo kwamba tatizo lingeisha, lakini baadae nilimuomba niondoke nyumbani kwani sikuwa na uwezo wa kutoka ndani kwenda kwa wanawake wenzangu, kutokana na harufu sehemu zangu za siri, “anasema

Yunis anasema baadae alitafuta eneo la kuishi,kufikia mwaka 2003 alimpata mwanaume ambaye hakufahamu kwamba ana tatizo hilo na kumzalisha mtoto wa pili ambaye ujauzito wake ulitoka.

Anasema mtoto wa pili alijifungulia nyumbani, kutokana na kutokuumwa uchungu kwani wakati ulipofika alihisi kubanwa na haja ndogo.

“Maisha yaliendelea na mwaka 2006 nilipata ujauzito mwingine, ambao haukutoka lakini baada ya muda kupita mumewangu wa pili alinitelekeza .

Huku nikiendelea na maisha ya tabu kutokana na ugonjwa huo mwaka 2011 mume wangu wa pili aliyenikimbia alirejea na kunizalisha mtoto wa pili na jumla nikawa na watoto watatu,

Mwaka 2014 mama yangu akapoteza maisha na ndio kipindi mwanangu wa kike anaolewa,”anasema.

Yunis anasema watoto wake walianza kuhisi utofauti na mara nying walimuuliza tatizo linalomsumbua na kuwaeleza anasumbuliwa na uvimbe tumboni.

“Mtoto wangu alinipeleka Hospitali ya jeshi mkoani Mwanza, lakini tatizo halikugundulika kutokana na namna nilivyodanganya na vipimo kutokuonyesha hali hiyo,

Nilielezwa kwa daktari mwingine ndani ya hospitali hiyo ambaye aliponiona kwa mara ya kwanza aliniambia nivue nguo zote, nilipata hofu kwani ungekuwa mwanzo wa ugonjwa unaonisumbua kugundulika,”anasema.

Yunis anasema licha ya kumshawishi daktari kutokufanya hivyo, hakuelewa na ikalazimu kuvua nguo hizo na ndipo alipogundulika kusumbuliwa na fistula.

“Sikujua kama nilichanika sehemu zangu za siri kutokana na namna mama alivyokuwa akinieleza nikalie maji ya chumvi ambapo nilifanya hivyo kwa zaidi ya miezi mitatu nikiamini nitapona ,daktari alinieleza tatizo na kuniambia ningetakiwa kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu,”anasema.

Yunis anasema, mwanae wa kwanza alitafuta usaidizi kutoka kwa wataalamu Hospitali ya Rufaa Bugando, ambapo alionana na daktari bingwa wa wanawake ambaye mara baada ya kuona mwenendo wa afya yake alimwandikia apatiwe matibabu akiwa ndani ya hospitali (yaani mgonjwa wa kulazwa)

“Nilimwomba daktari kwanza niende kuieleza familia yangu matatizo niliyonayo na baada ya siku mbili nilirejea hospitali na kulazwa.

Hiyo ilikuwa mwaka 2015 nililazwa na kufanyiwa vipimo na kuwekwa katika kundi la wagonjwa wa upasuaji,sikujua kilichoendelea nilikaa hospitalini na tukaanza kupatiwa mafunzo mara bada ya matibabu kwa njia ya upasuaji ,

“Nikiwa na wenzangu tulianza kupatiwa mafunzo ya ujasiriamali ndani ya hospitali namna ya kushona vitambaa chini ya Shirika la Utafiti na Tiba Barani Afrika(Amref),

Siku nimeruhusiwa kutoka hospitali nilipewa khanga mbili, chupa ya chai na sahani nilirudi na kukaa kwa mwanangu kwa mwaka mmoja ambapo shirika lisilo la kiserikali la kutetea haki za wazee (MAPERECE) lilinifuata nyumbani wakielezwa ninapokaa na Hospitali ya Bugando lengo kusaidia wahanga wa fistula,”anasema.

Mwaka 2017 anasema, kupitia shirika hilo na shirika la Amref alipata mafunzo ya namna ya kuwasiliana kufanya biashara na kupatiwa mtaji .

“Nilikuwa mwanamke wa kukaa ndani lakini sasa huwezi kunikuta ndani,nafanya ujasiriamali na biashara mbali mbali ikiwemo uuzaji wa chai na vitafunwa ,barafu ,mkaa hivyo naishukuru Amref kwani isingekuwa shirika hili bado nisingethubutu kutoka nje na sasa tumekutanishwa kupitia vikundi vya ujasiriamali,”anasema.

UNYANYAPAA

Yunis anasema baada ya mama yake kufariki kila alipokanyaga watu walionekana kutamka hadharani kuwa anasambaza kinyesi jambo ambalo lilimfanya kuishi kwa majonzi.

“Naiomba jamii hata mtu akiwa na hali ya fistula watoe msada kwani changamoto niliyoipitia hakuna mtu mwenye uwezo wakupitia na nimenusurika kuoteza maisha kwa neeema za mungu,lengo nimetibiwa na nimepona kutokana na biashara zangu sasa huwezi kuamini kama niliugua fistula,

Nawashauri wanawake wenzangu wanaopitia hali kama yangu wasiwe na hofu kwani ugonjwa unatibika na wasiogope kujishughulisha na biashara,biashara haihitaji mtaji mkubwa,hata sh 5,000 usisubiri kuanza na mtaji mkubwa ,pia niwaombe kina baba wawanaotukimbia tunapopitia hali wawe karibu na wake zao kwani anapomtelekeza na kumuacha humsababishia msongo wa mawazo,”anasema.
Yunis anasema maisha yote ya unyanyapaa aliyoyapitia na kukimbiwa na wanaume mwaka 2016, mumewe alirejea kwa mara nyingine na kumuomba radhi , lakini haikupita muda alitoweka kwa mara nyingine na mpaka sasa bado anaishi kwa misaada.
MTAALAMU
Daktari Bingwa wa Upasuaji CCBRT Dk.James Chapa anaufafanua ugonjwa wa fistula ni shimo kubwa kati ya njia ya uzazi na njia ya mkojo unatokana na mama kuwa na uchungu wa muda mrefu bila matibabu.
“Ili mwanamke apone ugonjwa huu ni vyema akatibiwe hospitali kwani hakuna eneo mmbadala ambalo tiba inapatikana,
Matibabu yakifanyika mapema na kwa ufasaha majibu huwa mazuri kwa zaidi ya asilimia 90, hivyo kama yupo mwenye tatizo hili na bado hajafika hospitali afike CCBRT kwa ajili ya matibabu”anasema.
Mwakilishi kutoka shirika la AMREF, Dk. Magdalena Dhalla anasema baadhi ya dalili za mgonjwa mwenye Fistula ni kutokwa na haja ndogo au kubwa usiku na mchana bila kujitambua, vidonda sehemu ya siri, harufu mbaya ya mkojo au kinyeesi na kuchechemea kwa sababu ya kuumiza mguu kutokana na uchungu pingamizi.

“Madhara mengine yanayoambatana na ugonjwa wa fistula ya uzazi ni kupoteza uwezo wa kupata mtoto tena, kukosekana kwa kushiriki tendo la ndoa, kuporomoka kiuchumi,
Hivyo ni vema wagonjwa wakafika hospitali kwa matibabu na ugonjwa huu unatibiwa bure ikiwa ni pamoja na operesheni katika Hospitali ya Bugando au CCBRT,”
anasema.

HALI YA FISTULA NCHINI
Kwa mwaka 2020 idadi ya Wanawake waliojitokeza kutibiwa Fistula CCBRT, Bugando, Nkinga na Kuvulini Maternity Center ilipungua kwa zaidi ya asilimia 30 kwa mujibu wa Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Takwimu hiyo ni ikilinganishwa na mwaka 2015 na 2019 ambapo mwaka 2015, wanawake 1,337 walipatiwa matibabu ya Fistula,
Mwaka 2016 wanawake wenye fistula walikuwa 1,356, 2017 idadi hiyo ikashuka na kufikia 1060,
Pia 2018 ikashuka na kufikia idadi ya wanawake 900, na 2019 ikafikia wanawake 852.
Hii imetokana na kuimarika kwa upatikanaji wa huduma za upasuaji wa dharura nchini.

Kwa mujibu wa wizara ya afya serikali imeimarisha huduma kwa wajawazito, hatua ambayo imesaidia kupunguza matatizo ya fistula kwa wanawake wengi nchini.
Wajawazito waliotimiza mahudhurio manne au zaidi (ANC4+) mwaka 2019/20 walifikia asilimia 77 ikilinganishwa na asilimia 41 kwa kipindi kama hicho mwaka 2015/2016,

Kina mama wanaojifungulia vituo vya kutolea huduma imeendelea kuongezeka hadi kufikia asilimia 83 mwezi Machi 2020 ikilinganishwa na asilimia 64 kwa kipindi kama hicho mwaka 2015/16.

Idadi ya vituo vya afya vinavyotoa huduma ya dharura kwa wajawazito (CEMONC) imeongezeka na kufikia vituo 352 mwezi Machi mwaka 2020 ikilinganishwa na vituo 115 mwaka 2015.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2018 zinaonyesha kuna wanawake takribani milioni mbili wanaoishi na fistula duniani.

Inakadiriwa wagonjwa wapya kati ya 50,000 na 100,000 hupatikana kila mwaka, wakati juhudi za kutibu fistula duniani huishia kutibu wagonjwa 20,000 tu.
 
Back
Top Bottom