Kanungila Karim
JF-Expert Member
- Apr 29, 2016
- 20,744
- 25,425
SEHEMU YA 01:
Ninaposema niliolewa na wanaume watatu, nataka nieleweke vizuri kwamba walinioa na niliishi nao kwa miaka kadhaa bila wao wenyewe kujuana. Kwa maneno mengine ni kwamba nilikuwa mke wa wanaume watatu kwa wakati mmoja, wanaume wenyewe wakiwa hawajui.
Sijui niseme ulikuwa uhuni au ni tamaa ya maisha au ulikuwa ni ujinga, sijui.Tukio hilo nililifanya miaka michache iliyopita wakati huo nikiwa bado msichana mwenye matumaini ya maisha.
Kielimu sikuwa nimesoma zaidi ya ile elimu ya kufuta ujinga, yaani kujua kusoma na kuandika. Niliishia darasa la saba tu. Na nilikomea darasa hilo kutokana na utoro wangu shuleni.
Sikuwahi hata kufanya mtihani wa taifa, nilikuwa siendi shule. Baba na mama yangu walikuwa wameshafariki dunia. Mama alifariki dunia nikiwa darasa la tano na baba alimfuata nikiwa darasa la saba ambalo sikulimaliza.
Nilielezwa kuwa nilikuwa na akili lakini sikuwa nikipenda masomo hata kidogo. Wanafunzi wenzangu niliokuwa nao darasa la saba waliniambia laiti ningefanya mtihani wa darasa la saba ningefaulu kwenda sekondari kutokana na akili yangu.
Licha ya kuishia darasa la saba, ujanja wangu uliniwezesha kuzungumza lugha ya kiingereza kwa ufasaha mzuri ila kwenye kuandika ndiyo ilikuwa balaa lakini nilikuwa ninaweza kusoma vitabu na magazeti yaliyoandikwa kwa lugha hiyo.
Watu wengi wasionijua vizuri walikuwa wakinidhania nilikuwa na elimu ya chuo, kumbe ni ya msingi.
Wakati naacha masomo nilikuwa na umri wa miaka kumi na tatu. Nilikuwa nikiishi na shangazi yangu maeneo ya Ilala jijini Dar. Shangazi alinichukua baada ya wazazi wangu wote kufariki dunia.
Jina langu ni Mishi. Baba yangu alikuwa anaitwa Ramadhani Mzaka, Mdigo wa Tanga. Mama yangu ndiye alikuwa Mwarusha. Alikuwa mwanamke mweupe kama Mwarabu. Mimi ndiye nilishabihiana naye kwa sura, weupe na uzuri.
Vile vishawishi vya wanaume ndivyo vilivyoniingiza katika balaa nikiwa na umri mdogo. Kulikuwa na kijana mmoja aliyekuwa akiitwa Sele, maarufu kama Sele Msela. Yeye ndiye aliyeniingiza katika mapenzi.
Nilikuwa nimesoma naye katika shule ya msingi darasa moja. Mimi nilipoacha masomo, yeye aliendelea hadi akafika kidato cha nne.Miaka miwili baadaye alifanikiwa kupata kazi Shirika la Bandari. Nilikuwa nikikutana naye karibu kila siku kwa vile tulikuwa tunaishi mtaa mmoja.
Sele alikuwa kijana wa kwanza kunitamkia kuwa alitaka kunichumbia baada ya kuwa naye kwa muda mrefu. Miezi michache baadaye Sele akakamatwa na vitu vya wizi bandarini. Alikuwa na mchezo wa kukwapua-kwapua vitu na kuja kuviuza mjini.
Ingawa alishinda kesi, alifukuzwa kazi na kurudi kijiweni. Kwa vile alishazoea kushika pesa, maisha yalimshinda akakimbilia Sauzi kutafuta maisha. Siku za kwanza-kwanza tulikuwa tukiwasiliana kwa simu akinipa matumaini kwamba dhamira yake ya kuja kunioa ilikuwa palepale lakini siku zilivyozidi kwenda mawasiliano yetu yakakatika.
Siku zikazidi kwenda. Nikamsahau Sele kwani hatukuwa na mawasiliano tena.Siku moja nilikuwa natoka Kigoma. Basi liliharibika njiani. Tulikaa hadi usiku, basi lilikuwa bado likishughulikiwa. Likapita lori likielekea Dar. Nilikuwa nimesimama peke yangu pembeni mwa barabara.
Dereva wa lori hilo aliponiona alifunga breki akatoa kichwa kwenye dirisha na kuniuliza.
“Unakwenda Dar?”
Nilikuwa kwenye lindi la mawazo yaliyochanganyika na uchovu. Ile sauti ya dereva ikanishitua.
“Unasemaje?” nikamuuliza.
“Unakwenda Dar?” Akaniuliza tena.
“Ndiyo ninakwenda Dar lakini basi letu limeharibika.”
“Uko tayari kusafiri kwa lori?”
“Acha lori, hata kwa trekta niko tayari. Nimechoka sana.”
“Njoo ujipakie twende.”
Kwa vile sikuwa na mzigo wowote zaidi ya mkoba wangu ambao nilikuwa nao begani nikasogea kwenye lori hilo. Taniboi alifungua mlango akashuka na kunipisha. Nikaingia kwenye lori.
Nikawekwa katikati. Kulia kwangu kulikuwa na dereva. Kushoto kulikuwa na taniboi.
Tukaanza safari.
“Unatokea wapi?” Dereva akaniuliza.
“Natoka Kigoma,” nikamjibu na kuongeza:
“Lakini najuta kupanda lile basi, limeharibika njiani mara tatu.”
“Pole sana. Sasa wewe ni mkazi wa Kigoma au Dar?”
“Ni mkazi wa Dar. Kigoma nilienda tu mara moja.”
Wenyewe walikuwa wakitafuna mahindi ya kuchemsha waliyonunua njiani. Wakanipa moja na mimi nikawa natafuna.Ilipofika saa 2:00 usiku. Lori likasimama katika kijiji kimoja. Tukashuka kwa ajili ya kupumzika na kupata maakuli. Mimi nilikataa kula kwa sababu nilikuwa nimechoka na sikuwa nikitamani kula kutokana na ile fadhaa ya safari.
Lakini dereva wa lori hilo alinilazimisha nile.
“Tutafika alfajiri, hutapata chakula tena,” akaniambia.
Nikaamua nile. Nikala kuku mzima na wali. Wakati nataka kulipa dereva akaniambia nisilipe. Akalipa yeye. Nikamshukuru kwa wema wake.
Baada ya kula tulipumzika kwa muda mrefu tukizungumza kile na hiki. Tulipoanza tena safari nililala ndani ya lori. Mpaka nakuja kuzinduka tupo Chalinze.
“Tuko wapi hapa?” Nikamuuliza dereva.
“Tuko Chalinze,” dereva akanijibu.
“Kumbe nimelala sana. Ni saa ngapi sasa?”
“Inakaribia kuwa saa 9:00 usiku.”
Pale Chalinze lori lilisimama tena. Tukashuka. Tuliingia kwenye mgahawa mmoja tukanywa chai. Dereva akamtuma taniboi wake akanunue mirungi.
Sisi tulibaki kwenye mgahawa hadi taniboi alipokuja na bahasha iliyofungwa mirungi. Nikamsikia dereva akimuuliza taniboi huyo.
“Umepata gati au shambarungu?”
“Nimepata gati.”
Dereva akaifungua palepale na kuitazama.
“Hii ni giza halafu ni kilalo,” akasema baada ya kuiangalia.
“Saa hizi huwezi kupata ya leo.”
Vilikuwa vichanga sita. Dereva alichagua vichanga vitatu akachukua yeye, vitatu akampa taniboi wake.“Umenunua bigijii?” Akamuuliza.
“Ndiyo hizi hapa.”
Zilikuwa kwenye mfuko. Taniboi akatia mkono mfukoni na kutoa bigjiii hizo za ubani zipatazo kumi.
Dereva alichukua tano na tano nyingine akamuachia taniboi.
Itaendelea