Simulizi ya kweli: Niliishi kuzimu siku saba

Kanungila Karim

JF-Expert Member
Apr 29, 2016
20,744
25,425
8d6685ca573429266a7b4d25310950a2.jpg

SEHEMU YA 01:

Damu nyingi zilikuwa zinanitoka upande wa kushoto wa kifua changu kiasi cha kunifanya nilowe chapachapa. Nilijitahidi kuinuka pale nilipokuwa nimelala huku damu nyingi zikiendelea kunitoka lakini maumivu makali yalinirudisha chini.
Kwa kutumia mikono yangu miwili, nilijaribu kuminya pale kwenye jeraha kubwa ili kuzuia damu isiendelee kunimwagika lakini nilijikuta mikono ikikosa nguvu, kadiri muda ulivyokuwa unasonga mbele ndivyo nilivyokuwa nazidi kuishiwa nguvu.
Watu wengi walianza kukimbilia pale nilipokuwa nimeanguka na kunizunguka, niliwasikia wengine wakishindwa kuficha hisia zao na kuanza kuangua vilio wakilitaja jina langu. Nadhani hali waliyoniona nayo iliwafanya waamini kwamba siwezi kabisa kupona kutokana na damu zilivyokuwa zinaendelea kunimwagika mithili ya bomba lililopasuka.
Nikiwa kwenye maumivu makali, nilijigeuza na kuanza kutazama angani, upeo wa macho yangu ukagota kwenye mawingu meupe na ya bluu yaliyokuwa yakilipendezesha anga, nikabaki nimetulia nikiwa kwenye hali hiyo.
Kelele za watu wengi waliokuwa wanazidi kuongezeka eneo la tukio kunishangaa, zilianza kupungua taratibu masikioni mwangu, zikazidi kupungua na baadaye nikawa nasikia kama watu wananong’ona. Kwa mbali nilisikia mlio wa ving’ora ambavyo hata hivyo sikujua ni vya nini.
Nikiwa naendelea kutazama angani, taswira ndani ya mboni za macho yangu ilianza kufifia taratibu na kadiri muda ulivyokuwa unazidi kusonga mbele ndivyo nayo ilivyozidi kufifia, japokuwa ilikuwa ni mchana, kigiza kikaanza kutanda kwenye macho yangu.
Nakumbuka neno la mwisho nililofanikiwa kulisema, ingawa ilikuwa ni kwa taabu kubwa kutokanana midomo yangu kuwa mizito, ilikuwa ni: Mungu nisaidie! Nikafumba macho na giza totoro likatawala kila sehemu, sikuelewa tena kilichoendelea baada ya hapo!
Katika hali ambayo sikuitegemea na ambayo mpaka leo huwa siwezi kuifafanua, muda mfupi baadaye nilijikuta nikizinduka lakini nikiwa kwenye hali ya tofauti kabisa. Nilizinduka nikiwa palepale nilipokuwa nimelala awali lakini katika hali ya ajabu, nilikuwa mwepesi sana.
Nikajikuta nikianza kupaa taratibu kuelekea juu. Nikiwa juu kidogo, niligeuka na kutazama pale nilipokuwa nimeangukia, nikashangaa kuona bado mwili wangu ulikuwa umelala palepale, damu nyingi zikiendelea kutoka kwenye jeraha la kifuani, tena safari hii zikitoka kwa mabongemabonge.
“Mungu wangu! Hiki ni kitu gani tena?” nilijikuta nikisema kwa sauti ya chini, ungeweza kudhani nilikuwa kwenye ndoto lakini haikuwa hivyo. Nilijiuliza kama mwili wangu bado ulikuwa pale chini, mimi niliyekuwa napaa nilikuwa ni nani?Sikupata majibu.
Niliendelea kupaa kuelekea juu mpaka nikafikia umbali wa mita kadhaa, ulioniwezesha kuona vizuri kila kitu kilichokuwa kinaendelea eneo la tukio. Niliwaona watuwakizidi kumiminika kwa wingi eneo la tukio, wengine wakishika vichwa vyao baada ya kuuona mwili wangu ukiwa kwenye hali ile.
Niliwaona watu kadhaa ambao nilikuwa nikiwafahamu wakiwa na nyuso za huzuni kali, wengine wakiangua vilio kwa nguvu. Nilimuona rafiki yangu na mfanyakazi mwenzangu ambaye muda mfupi kabla ya tukio nilikuwa naye, Justice akiwa analia kwa uchungu mno huku akilitaja jina langu.
Nilimuona pia Raya, msichana ambaye naye tulikuwa tukifanya naye kazi na ambaye alikuwa anapenda sana kuwa karibu na mimi ingawa mara kwa mara nilikuwa nikimkwepa (nitaeleza zaidi kuhusu msichana huyu baadaye), naweza kusema yeye ndiye aliyekuwa na hali mbaya kuliko watu wengine wote kwani alikuwa akilia kwa sauti ya juu huku akilitaja jina langu kiasi cha kusababisha muda mfupi baadaye aanguke na kupoteza fahamu.
Niliwaona pia baadhi ya watu wakiupiga picha mwili wangu kwa kutumia simu zao za mikononi, niliwaona pia waandishi kadhaa wa habari ambao nao walikuwa wakipiga picha nyingi eneo la tukio, za mnato na za video.
Muda mfupi baadaye, walifika askari wanne waliokuwa wamepakizana kwenye pikipiki mbili, maarufu kama tigo ambao niliwaona wakianza kuwarudisha watu nyuma kutoka pale mwili wangu ulipokuwa umelala.
Mmoja wao alisogea jirani kabisa, nikamuona akiuchunguza mwili wangu kisha akaugusa shingoni kama anayesikiliza mapigo ya moyo, nikamuona akiinuka na kuwasogelea wenzake, wakawa wanazungumza jambo ambalo sikuelewa ni nini. Mmoja akatoa simu ya upepo (radio call) na akawa anazungumza na upande wa pili.
Nikiwa bado naendelea kushangaa kwani kila kitu kilikuwa kigeni kwangu, nilianza kusikia ving’ora kwa mbali, nikakumbuka kwamba kabla sijapoteza fahamu kutokana na kutokwa na damu nyingi, nilivisikia tena ving’ora hivyo lakini tofauti yake ni kwamba sasa nilikuwa na uwezo wa kuona kila kilichokuwa kinaendelea.
Lilikuwa ni gari la kubebea wagonjwa (ambulance) ambalo lilikuwa likija kwa kasi eneo lile mwili wangu ulipokuwepo. Nyuma yake lilikuwa limeongozana na difenda ya polisi ambayo niliitambua kwa urahisi kutokana na namba zake za usajili na maandishi yaliyokuwa ubavuni yaliyosomeka ‘Police’.
Wale askari waliokuwepo eneo la tukio waliwatawanya watu upande ule ile ambulance ilikokuwa inatokea, gari likasogea mpaka jirani kabisa na pale mwili wangu ulipokuwepo.
Likasimama ambapo manesi wanne waliovalia nguo nyeupe waliteremka wakiwa na machela, sambamba na askari kadhaa waliokuwa kwenye ile difenda, wote wakasogea na kuuzunguka mwili wangu.
Wakasaidiana kuuinua mwili wangu pale chini na kuulaza kwenye machela kisha wakauingiza kwenye ambulance. Nilimuona Justice naye akipanda. Raya yeye alipakizwa kwenye lile gari la polisi akiwa hajitambui.
Gari likaondoka kwa kasi kubwa likifuatiwa na difenda kwa nyuma, wale askari wa pikipiki waliendelea kuwepo pale eneo la tukio kwa dakika kadhaa wakiwa makini kuwasikiliza watu walichokuwa wanakisema huku wakiwahoji wengine kadhaa.
Kwa muda wote huo, bado nilikuwa najiuliza kilichotokea bila kupata majibu, sikuelewa nipo kwenye hali gani kwa sababu kama ni mwili wangu, tayari ulishapakizwa kwenye ambulance na kukimbizwa hospitali lakini nilishangaa mimi bado nipo eneo lile nikielea angani.
Nilijiuliza ule mwili wangu unapelekwa wapi lakini pia sikupata majibu. Ghafla nilipata wazo la kuifukuzia ile ambulance ili nijue wanaupeleka wapi mwili wangu. Wazo nililoona linafaa, ilikuwa ni kushuka chini na kuchukua bodaboda kwani niliamini kutokana na foleni iliyokuwepo na kasi ya ambulance, ni usafiri huo pekee ndiyo unaoweza kuniwahisha.
Nilishuka jirani kabisa na pale mwili wangu ulipokuwepo muda mfupi uliopita, watu wakawa wameshaanza kutawanyika huku wengine wakijikusanya vikundivikundi pembeni na kujadiliana kuhusu kilichotokea. Nilimsikia mzee mmoja akiwaambia wenzake: “Kwa hali aliyonayo, hawezi kupona, lazima afe.”
Nikashtuka sana kusikia kauli hiyo kwa sababu sikujua wanamzungumzia nani kwamba lazima afe wakati mimi bado nilikuwa hai na nilikuwa nawasikia wanachokisema.
Sikutaka kupoteza muda, harakaharaka nilisogea pembeni ya barabara na kupunga mkono kusimamisha bodaboda, japokuwa dereva alikuwa akija upande wangu, nilishangaa akinipita kama hajaniona. Akaja wa pili naye licha ya kumpungia mkono kwa nguvu hakusimama, akanipita kwa kasi.
Nilijitazama vizuri mwilini kwani nilihisi huenda wanaogopa kusimama kutokana na mwili wangu kulowa damu lakini kituambacho pia nilishindwa kukielewa, shati nililokuwa nimevaa halikuwa na hata tone la damu. Lilikuwa ni shati lilelile ambalo mwili wangu wakati unatolewa eneo lile lilikuwa halitamaniki kwa damu.
Nilishindwa kuelewa ni nini hasa kimetokea, nikajitazama vizuri mwili wangu na kugundua kwamba ulikuwa na hali fulani kama ya kung’aa kusiko kwa kawaida, nilijishika pale kifuani lakini hapakuwa na alama kwamba nilikuwa nimejeruhiwa vibaya, nikazidi kuchanganyikiwa.
Ilibidi nisogee mpaka kwenye maegesho ya bodaboda nikiamini pale itakuwa rahisi kuzungumza na dereva yoyote ili aniwahishe kabla ile ambulance haijapotea kabisa. Nilipopiga hatua moja nilijiona kuwa mwepesi sana halafu tambo lilikuwa refu sana tofauti na kawaida. Sehemu ambayo ningetembea hata hatua ishirini, nilipiga hatua mbili tu, nikawa nimeshafika pale kwenye bodaboda.
Je, nini kitafuatia?
 
SEHEMU YA 02:


ILIBIDI nisogee mpaka kwenye maegesho ya bodaboda nikiamini pale itakuwa rahisi kuzungumza na dereva yeyote ili aniwahishe kabla ile ‘ambulance’ haijapotea kabisa. Nilipopiga hatua moja, nilijiona kuwa mwepesi sana halafu tambo lilikuwa refu sana tofauti na kawaida.
Sehemu ambayo ningetembea hata hatua ishirini, nilipiga hatua mbili tu, nikawa nimeshafika pale kwenye bodaboda.
SASA ENDELEA…
“OYA mambo vipi mkubwa!” nilimsalimu dereva wa bodaboda aliyekuwa pembeni yangu kwa bashasha kubwa lakini hakuniitikia, akawa anaendelea kuifutafuta bodaboda yake.
Nilirudia kumsalimu lakini bado hakunijibu chochote na wala hakuonyesha kama ananisikia. Nilimgusa begani lakini bado ilikuwa ni kazi bure, aliendelea kufutafuta bodaboda yake, nikabaki nimepigwa na butwaa.
Ilibidi nimsogelee dereva mwingine wa bodaboda, naye nikamsalimia kwa bashasha lakini hakunijibu, nikarudia tena na tena lakini bado hali ilikuwa ileile, nikaenda kwa watatu ambaye alikuwa akipiga stori na wenzake, naye akaonyesha kutonisikia.
“Kwani imekuwaje? Mbona sielewi kinachoendelea?” nilijisemea huku nikianza kutetemeka kwa hofu kubwa, mwisho niliamua kufanya jambo moja, nilipaza sauti kwa nguvu nikiita ‘bodabodaaa!’ niliamini yeyote ambaye atakuwa wa kwanza kuniona basi nitamchukua huyohuyo lakini wapi! Kila mmoja aliendelea na mambo yake.
Ni hapo ndipo nilipogundua kwamba huenda nilikuwa sionekani kwa macho ya kawaida wala sauti yangu haisikiki licha ya ukweli kwamba mwenyewe nilikuwa najisikia vizuri tu.
“Sasa nitafanyaje?” nilisema huku nikigeuka kuitazama ile ‘ambulance’, tayari ilishapotea kwenye upeo wa macho yangu lakini akili zangu zilinituma kuamini kwamba lazima itakuwa imeupeleka mwili wangu Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
“Nataka nikashuhudie kila kitu kinachoendelea,” nilisema huku nikianza kutafuta mbinu nyingine ya kunifikisha hospitalini hapo. Sijui nilipata wapi akili hizo lakini nilijikuta tu nikiamua kuanza kutimua mbio kuelekea kule ile ambulance ilikoelekea.
Nilipopiga hatua chache tu, nilijikuta nikiwa napaa angani kwa kasi kubwa, nikawa naitazama mitaa ya jiji kutokea angani. Kuna wakati akili zangu zilinituma kuamini kabisa kwamba nilikuwa kwenye ndoto ya kutisha ambayo muda wowote itaisha lakini akili nyingine zikawa zinaniambia kwamba siyo ndoto, kila kitu kilikuwa kikitokea kwa uhalisia.
Wakati ambulance ikiwasili kwenye geti kuu la kuingilia Muhimbili, na mimi tayari nilikuwa nimeshafika eneo hilo, geti likafunguliwa na likaingia moja kwa moja mpaka kwenye eneo la ‘emergency’ ambalo wagonjwa wenye hali mbaya ndipo walipokuwa wanafikia.
Milango ya ambulance ilifunguliwa, manesi waliokuwa ndani ya ile ambulance pamoja na wengine waliokuwa pale mapokezi, walisaidiana kuushusha mwili wangu na kukimbizwa mpaka ndani, nikawa nashuhudia kila kitu kilichokuwa kinaendelea.
Harakaharaka nilianza kupewa huduma ya kwanza, nikamuona nesi mmoja akichukua mkasi na kukata shati nililokuwa nimevaa, nilipoliona jeraha lililokuwa kifuani wangu, nilisisimka mno. Nilijiuliza iweje mtu anifanyie ukatili mkubwa kiasi hicho, tena bila sababu ya msingi?
Japokuwa vitabu vya dini vinakataza kulipa kisasi, nilijikuta nikipandwa na ari kubwa ya kulipa kisasi, nilikuwa nimejeruhiwa sana. Niliwaona hata wale manesi akitetemeka kila walipokuwa wanalitazama jeraha langu.
Kwa bahati nzuri, madaktari wa kiume waliingia, huwa naamini siku zote kwamba sisi wanaume Mungu ametuumba na ujasiri mkubwa kuliko wanawake. Wakaanza kunifanyia kile ambacho
kitaalamu huwa kinaitwa ‘dressing’, yaani kusafisha jeraha kabla ya kuanza kutibiwa. Muda mfupi baadaye, tayari nilikuwa nimesafishwa jeraha hilo, nikahamishwa na kupelekwa chumba cha wagonjwa mahututi nikiwa bado sijitambui huku madaktari na manesi wakiendelea kuhangaika kudhibiti damu zilizokuwa zinaendelea kunitoka kwa wingi.
Nilipoingizwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi, harakaharaka niliunganishwa kwenye mashine ya kunisaidia kupumua huku dripu ikitiririka kwa kasi kuingia kwenye mishipa yangu.
“He has lost a great deal of blood, he need an urgent transfusion,” (Amepoteza damu nyingi sana, anahitaji kuongezewa damu haraka iwezekanavyo) alisema daktari mmoja kwa Kiingereza, kwa kuwa na mimi shule ilikuwepo kiasi chake kichwani, nilimuelewa vizuri.
Niendelee kusisitiza kwamba wakati haya yote yakitokea, katika ulimwengu wa kawaida sikuwa na fahamu hata kidogo, nilikuwa nimefumba macho na kulala pale kitandani kama maiti, nikiwa nimeunganishwa na mashine ya kunisaidia kupumua lakini katika ulimwengu mwingine ambao hata sijui niuiteje, nilikuwa nimesimama kwenye pembe moja ya ile wodi, nikishuhudia kila kilichokuwa kinaendelea.
Kazi ya kuokoa maisha yangu iliendelea, madaktari na manesi wakawa wanapishana huku na kule, huyu kabeba dawa, huyu kabeba chupa ya damu, huyu mikasi na sindano, ilimradi kila mmoja alikuwa bize.
Nilijisikia ahueni kubwa ndani ya moyo wangu kuona watu ambao pengine hata hawakuwa wakinijua, wakipigana kuokoa maisha yangu. Niliendelea kuwatazama wanavyohangaika, kuna wakati machozi ya uchungu yalikuwa yakinitoka kwa sababu ya kilichotokea, nikawa naendelea kujiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu.
Nilivuta kumbukumbu ya jinsi mambo yote yalivyoanza kutokea.
***
Januari 16, 2012
Mikocheni, Dar es Salaam.
“Haloo!”
“Haloo, nani mwenzangu.”
“Mh! Kwani namba yangu hujaisevu Moses, mbona una visa wewe.”
“Samahani, utakuwa umekosea namba, mimi siitwi Moses wala sikufahamu.”
“Ooh! Basi samahani kaka yangu nitakuwa nimechanganya namba. Samahani sana.”
“Usijali, kuwa makini,” yalikuwa ni mazungumzo kati yangu na mtu aliyepiga simu na kunifananisha.
Nilikata simu na kubonyeza kitufe kwenye rimoti ya runinga yangu kubwa (flat screen) niliyokuwa nimekata sauti (mute) baada ya kuona simu yangu inaita. Nikawa naendelea kutazama muvi kwani miongoni mwa vitu nilivyokuwa navipenda, ilikuwa ni kutazama muvi, kuangalia mpira na kusikiliza muziki, hasa muda ninaokuwa nyumbani baada ya kutoka kazini.
Haukupita muda mrefu, simu yangu ikawa inaita tena, nilikasirika kwa sababu muvi ilikuwa imefika sehemu nzuri na sikutaka inipite hata sehemu moja, safari hii nilibonyeza kitufe cha ‘pause’ kuisimamisha ili isiendelee, nilipotazama namba ya mpigaji, ilikuwa ni ileile ya yule mtu aliyedai kukosea namba.
“Samahani mpendwa najua nakusumbua, nimeangalia vizuri simu yangu na kugundua kuwa ni kweli nilikosea namba wakati nakupigia.”
“Usijali dada, tufanye yameisha.”
“Ahsante kwa kunisamehe kaka yangu, japo sikujui lakini unaonekana mstaarabu sana. Mimi naitwa Shenaiza sijui mwenzangu unaitwa nani.”
“Naitwa Jamal au kwa kifupi Jay,” nilimjibu kwa kifupi kwa sababu niliona kama ananiletea stori zisizo na kichwa wala miguu.
“Ooh! Nimefurahi kukufahamu kaka Jamal. Unaishi wapi vile?”
“Mikocheni,” nilimjibu na safari hii niliamua kubonyeza tena rimoti, muvi ikaendelea kwani niliona hana chochote cha maana cha kuniambia, nikawa nimeiweka simu sikioni huku nikiendelea kuangalia muvi.
“Mbona kuna kelele kwani uko wapi?” alihoji msichana huyo lakini sikumjibu chochote, naona baadaye alijishtukia mwenyewe, akaamua kukata simu. Nikaiweka simu pembeni na kuendelea kutazama muvi.
Baadaye ilipoisha, nilichukua simu yangu na kugundua kuwa kulikuwa na meseji nyingi zimeingia bila mwenyewe kushtukia, nikaanza kuzisoma moja baada ya nyingine.
Nilishangaa kugundua kwamba ukiachilia mbali meseji mbili za rafiki zangu, Justice na Prosper, nyingine zote zilikuwa zimetoka kwa yule msichana aliyekosea namba ya simu, nikashusha pumzi ndefu na kuanza kuzisoma, moja baada ya nyingine nikiwa
na shauku kubwa ya kutaka kuona ameandika nini.
Je, nini kitafuatia? Meseji zinahusu nini?
 
SEHEMU YA 03:

NILISHANGAA kugundua kwamba ukiachilia mbali meseji mbili za rafiki zangu, Justice na Prosper, nyingine zote zilikuwa zimetoka kwa yule msichana aliyekosea namba ya simu, nikashusha pumzi ndefu na kuanza kuzisoma, moja baada ya nyingine nikiwa na shauku kubwa ya kutaka kuona ameandika nini.
SASA ENDELEA…
YA kwanza ilisomeka: “Samahani kaka Jamal naomba tuchati kama hutajali.” Nikaisoma na kuirudia zaidi ya mara mbili, sikuelewa maana ya yeye kuomba tuchati ni nini kwa sababu tayari nilishamwambia amekosea namba na mwenyewe akakiri hilo.
Hakuishia hapo, meseji nyingine ikasomeka: “Nina tatizo kubwa nilikuwa nahitaji mtu wa kumshirikisha ndiyo maana nikawa nimempigia simu ndugu yangu mmoja aitwaye Moses lakini baada ya kusikia sauti yako, naamini na wewe unaweza kuwa na busara na kunisaidia nini cha kufanya.”
“Mbona hunijibu?” ilisomeka meseji nyingine, nikawa naendelea kuzisoma moja baada ya nyingine ambapo msichana huyo alianza kulalamika kwamba nimemdharau ndiyo maana nilikuwa sitaki kujibu meseji zake, mwisho akaniambia nisimfikirie vibaya na kama ameniudhi anaomba nimsamehe.
Nilishusha pumzi ndefu baada ya kumaliza kusoma meseji zote, nikatafakari kwa kina nikiwa sijui lengo la msichana huyo ni nini hasa. Sina desturi ya kumdharau mtu hata mara moja, hasa anaponiambia ana matatizo. Huwa naamini kwamba hata kama huwezi kumsaidia mtu kwa namna nyingine, ushauri wa kimawazo unaweza kuwa msaada tosha kwake.
Ilibidi nichukue simu yangu na kupiga namba ya yule dada aliyeniambia kwamba anaitwa Shenaiza. Ilipoanza kuita tu, harakaharaka alipokea, nikamueleza kwa nini nilichelewa kujibu meseji zake.
“Nilikuwa na kazi naifanya ndiyo maana sijakujibu, nisamehe kwa hilo,” nilimwambia, harakaharaka akaniambia nisijali na anashukuru kwa kuwa nimempigia kwani tayari alishaanza kujisikia vibaya ndani ya nafsi yake. “Umeniambia una tatizo, naweza kukusikiliza tafadhali,” nilimuuliza kwa sauti ya kiungwana, nikamsikia akishusha pumzi ndefu kisha akaniuliza mahali nilipo.
“Nipo nyumbani, Mikocheni.”
“Mimi nipo Ilala, tunaweza kuonana tafadhali kama hutajali.”
“Mh!” niliguna, nilishindwa kuelewa msichana huyo anataka nini. Haikuwa kawaida yangu kuonana na watu nisiowajua, yaani dakika chache zilizopita mtu anakupigia simu na kukueleza kwamba amekosea namba, muda mfupi tena baadaye anakueleza kwamba ana shida muhimu na anataka kuonana na wewe? Nilijiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu.
Nimewahi kusikia visa vya watu wengi hasa jijini Dar es Salaam ambao walitekwa na kwenda kufanyiwa vitu vibaya baada ya kutegeshewa wanawake. Wengi wanaamini ni wanaume wachache sana wanaoweza kuepuka kishawishi cha mwanamke anayekupigia simu na kuomba kuonana na wewe, hata kama hamfahamiani.
“Hapana, haitawezekana dada’angu, tuzungumze tu kwa simu, leo nina kazi sana,” nilimkatalia kijanja. Msichana huyo aliendelea kung’ang’ania akitaka kuonana na mimi lakini kwa sababu za kiusalama, niliendelea kushikilia msimamo wangu.
Alipoona nimekuwa mgumu, aliniomba basi nipange siku na mahali ambapo tutaonana kwa sababu anahisi kwamba huenda nina wasiwasi naye, nikamwambia asiwe na wasiwasi siku nitakayokuwa na nafasi nitamtaarifu.
“Ila naomba iwe haraka, nina tatizo kubwa mwenzio,” alisema huku sauti yake ikionyesha kwamba alikuwa na huzuni kali ndani ya moyo wake. Nilikata simu na kujilaza kitandani, nikashusha pumzi ndefu na kuendelea kujiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu.
Kwa muda mfupi tu niliozungumza naye, tayari tulikuwa kama watu ambao tumefahamiana miaka mingi iliyopita. Sauti yake ilionyesha alikuwa na jambo zito ndani ya moyo wake lakini sikutaka kuwa mwepesi na kujiingiza kichwakichwa, nilikuwa tayari kutoa msaada wowote ambao angeuhitaji lakini pia nilihitaji kuwa na uhakika na maisha yangu.
Muda uliendelea kuyoyoma, kwa kuwa siku hiyo nilikuwa mapumziko nyumbani baada ya kazi za wiki nzima, niliutumia muda wangu mwingi kufanya usafi ndani kwangu, kufua nguo za kazini pamoja na za kushindia na baada ya kumaliza, nilirudi na kuendelea kutazama muvi. Jioni nilitoka na kwenda kwenye mgahawa uliokuwa jirani na pale nilipokuwa naishi, japokuwa nilikuwa nimekamilika kimaisha, nilikuwa mvivu sana kwenye suala zima la kupika kama walivyo vijana wengi ambao hawajaoa.
Kwa hiyo shughuli nyingine zote nilikuwa nikizifanya kwa mikono yangu isipokuwa jambo moja tu; kupika. Japokuwa nilikuwa na umri ambao ningeweza kuwa na msichana wa kunisaidia majukumu madogomadogo ya nyumbani, namaanisha mpenzi lakini nilikuwa nimeamua kuishi ‘single’ hasa kutokana na maumivu makubwa ya moyo niliyoyapata katika uhusiano wangu uliopita.
Tangu nilipoanza kuwa na akili za kikubwa, nilikuwa nimetoka na wasichana wawili tu, tena kwa nyakati tofauti lakini mambo niliyokutana nayo, yalinifanya nisitamani tena kuwa na mpenzi. Nikaamua kutuliza moyo mpaka umri wa kuoa utakapofika na huo ndiyo ulikuwa msimamo wangu.
Baada ya kupata chakula cha jioni, nilirudi nyumbani kwangu na kuendelea na mapumziko yangu. Majira ya kama saa tatu za usiku, yule msichana alinitumia tena ujumbe akinitakia usiku mwema, nami nikamjibu na tukawa tumeishia hapo kwa siku hiyo.
Kesho yake asubuhi, niliwahi kuamka na kuanza kujiandaa kuelekea kazini kama kawaida. Mahali nilipokuwa nafanya kazi, hapakuwa mbali sana na nyumbani kwangu kwa hiyo nilikuwa nikipanda daladala au wakati mwingine nikiwa na fedha za ziada, nakodi Bajaj au bodaboda.
Nilikuwa nikifanya kazi kwenye kampuni ya ukandarasi ya Collins Constructors & Civil Engineering, Mbezi Beach nikiwa kwenye kitengo cha usanifu wa ramani za majengo au kwa Kiingereza Architecture.
Sikuwa nimeanza kazi muda mrefu kwa sababu ndiyo kwanza nilikuwa nimehitimu masomo yangu ya chuo kikuu. Nikiwa kazini, niliendelea na majukumu yangu kama kawaida, ilipofika majira ya kama saa nne, muda ambao kwa kawaida huwa tunapumzika dakika chache kwa ajili ya kifungua kinywa, Shenaiza alinipigia simu kwa lengo la kunijulia hali, tukazungumza kawaida tu kisha akakata simu.
Niliendelea na kazi na kutokana na ubize wangu, sikushika tena simu mpaka saa kumi na moja jioni, muda ambao kwa kawaida huwa tunatoka kazini. Niliposhika simu yangu, nilikutana na ‘missed calls’ nyingi za Shenaiza na ujumbe mmoja ulionishtua sana moyo wangu. Aliniambia kwamba anahisi anakaribia kufa.
Ujumbe uliishia hivyo tu, nikashindwa kuelewa alikuwa anamaanisha nini? Ilibidi nimpigie, simu yake ikawa inaita tu bila kupokelewa. Nilipiga tena na tena lakini hakukuwa na majibu, nikapatwa na wasiwasi mkubwa ndani ya moyo wangu.
Sikujua msichana huyo amepatwa na nini, nikajihisi kuwa na hatia kwa sababu pengine kama ningekubali kuonana naye jana yake alipotaka nifanye hivyo, ningeweza kuelewa nini kinachomsumbua na pengine ningeweza kumsaidia.
Niliondoka kazini nikiwa ni kama nimechanganyikiwa, sikuwa namjua Shenaiza lakini sijui kwa nini nilihisi kama matatizo yake yalikuwa yakinihusu sana. Nikiwa kwenye kituo cha daladala nikiendelea kusubiri usafiri, ujumbe mfupi uliingia kwenye simu yangu, ulisomeka:
“Mwenye simu hii amelazwa Hospitali ya Amana, Ilala. Hali yake ni mbaya, hawezi kuzungumza.”
Je, nini kitafuatia?
 
SEHEMU YA 04:

Niliondoka kazini nikiwa ni kama nimechanganyikiwa, sikuwa namjua Shenaiza lakini sijui kwa nini nilihisi kama matatizo yake yalikuwa yakinihusu sana. Nikiwa kwenye kituo cha daladala nikiendelea kusubiri usafiri, ujumbe mfupi uliingia kwenye simu yangu, ulisomeka:
“Mwenye simu hii amelazwa Hospitali ya Amana, Ilala. Hali yake ni mbaya, hawezi kuzungumza.”
SASA ENDELEA…
“Mungu wangu,” nilisema baada ya kumaliza kuusoma ujumbe huo. Nilijaribu kuipiga tena namba hiyo, ikapokelewa lakini sauti haikuwa ya Shenaiza, akaniambia yeye ni Rozina, nesi katika hospitali ya Amana na kwamba yeye ndiye aliyekuwa akimhudumia msichana huyo.
Nilimuomba anitajie wodi aliyolazwa msichana huyo, akaniambia niende tu nikifika hospitalini hapo nipige kupitia namba hiyohiyo atakuja kunipokea. Niliita bodaboda na kumuelekeza kukimbia kadiri awezavyo kuelekea Amana. Abiria wengine waliokuwa pale kituoni wakisubiri daladala, walibaki kunishangaa lakini mwenyewe sikujali.
Nikaondoka na bodaboda huku nikimhimiza kuongeza mwendo ili tuwahi kufika. Baada ya kuhangaika sana kwenye foleni, kama ujuavyo Jiji la Dar es Salaam nyakati za jioni, hatimaye tuliwasili Amana. Nikapiga namba ya Shenaiza ambapo yule nesi alipokea tena, nikamweleza kwamba tayari nilikuwa nimefika, akaniambia nimsubiri mapokezi.
Sikuwa hata naijua sura ya huyo Shenaiza mwenyewe kwa sababu hatukuwahi kuonana zaidi ya kusikia sauti yake tu kwenye simu.
Muda mfupi baadaye, alitoka nesi mmoja, mwembamba, mrefu mwenye rangi ya weusi wa asili, akaniuliza kama mimi ndiye niliyekuwa nawasiliana naye kwenye simu. Nilipomjibu kwamba ni mimi, aliniuliza nilikuwa na uhusiano gani na mgonjwa?
Nikamjibu kwamba mimi ni kaka yake, nikamuona akiguna huku akinitazama kwa macho ya udadisi. Sikuelewa kwa nini ananitazama hivyo, nikajikaza kiume na kuonyesha kutobabaika.
“Nifuate!” alisema huku akianza kutembea kuelekea wodini, na mimi nikawa namfuata. Tulipita kwenye korido na kutokezea kwenye wodi za wanawake, nikawa naangaza macho huku na kule wakati tukipita pembeni ya vitanda walivyolazwa wanawake wengi, tukapita na kwenda kwenye wodi iliyokuwa imejitenga peke yake. Yule nesi akafungua mlango na kunipa ishara kwamba niingie.
Japokuwa kulikuwa na vitanda vinne ndani ya wodi hiyo, ni kimoja tu kilichokuwa kimelaliwa na mgonjwa aliyeonesha kutokuwa na fahamu. Yule nesi alinipa ishara kwamba yule ndiyo mgonjwa mwenyewe, nilimtazama kwa mshangao nikiwa kama siamini macho yangu.
Hakuwa Shenaiza yule ambaye nilimjengea picha kichwani mwangu, alikuwa mtu mwingine tofauti kabisa kiasi cha kunifanya nihisi huenda nesi amekosea kunipeleka au hatukuelewana katika mazungumzo yetu.
Hakuwa msichana wa Kitanzania kama nilivyokuwa nimemfikiria, alikuwa na mchanganyiko ambao siwezi kueleza moja kwa moja kama ni Mzungu au ni Mwarabu lakini alikuwa katikati ya jamii hizo mbili. Kiumri alionesha kuwa bado ni binti mdogo tofauti na nilivyomfikiria kwamba anaweza kuwa ni mwanamke mwenye kati ya miaka 25 hadi 30.
Alikuwa amelala tuli kitandani huku akiwa amefungwa bandeji kubwa kichwani, huku jicho lake moja likiwa limebadilika rangi na kuwa na weusi na wekundu kwenye ngozi inayolizunguka jicho kuonesha kwamba damu zilikuwa zimevilia kwa ndani. Pia mkono wake mmoja ulikuwa umezungushiwa bandeji kubwa kuanzia juu kidogo ya kiganja mpaka kwenye kiwiko cha mkono.
Dripu moja sambamba na chupa ya damu vilikuwa vikitiririka kwa kasi kuingia kwenye mishipa yake ya damu, nikajikuta nikipatwa na hali ambayo siwezi kuielezea kwa urahisi. Kwa kifupi, japokuwa bado sikuwa na uhakika kwamba yule ndiye Shenaiza tuliyekuwa tukiwasiliana naye, nilijikuta nikimuonea huruma sana kutokana na hali aliyokuwa nayo.
Nilitamani kujua nini kimemfika mpaka akawa kwenye hali hiyo. Nilitamani pia nimjue yeye ni nani na asili yake ni wapi hasa kwani hakuonesha kuwa Mtanzania japokuwa alikuwa akizungumza vizuri Kiswahili.
“Mbona unamshangaa sana? Kwani mlikuwa mnafahamiana kabla?” yule nesi aliniuliza baada ya kuniona hali niliyokuwa nayo, nilishusha pumzi ndefu na kuzugazuga, nikasogea pembeni ya kitanda cha Shenaiza na kumpa ishara kwamba tusogee pembeni ili tuzungumze zaidi.
“Samahani nesi, hebu nieleze nini kimetokea?”
“Nitakueleza lakini nataka na wewe unieleze ukweli, usije ukanisababishia matatizo kwenye kazi yangu, huyu ni nani kwako?”
“Nimeshakwambia kwamba ni dada yangu.”
“Hapana, siyo kweli! Hebu ngoja kwanza,” alisema huku akienda kuchukua simu iliyokuwa pembeni ya kitanda cha Shenaiza, akanifuata na kuniuliza kama simu yangu nilikuwa nayo, nikamjibu kwamba ninayo, akaniambia nipige namba ya Shenaiza. Nikatoa simu yangu na kutafuta namba yake kisha nikampigia.
“Unaona amekusevu vipi?” aliniuliza yule nesi huku akinionesha jina lililotokea kwenye simu yake, nikabaki nimepigwa na butwaa kutokana na jinsi alivyokuwa amenisevu.
Sikutaka kuendelea kumbishia yule nesi kwa sababu angeweza kupata sababu ya kukataa kunipa ushirikiano baada ya kuamini kwamba nilikuwa nikimdanganya, nikaamua kukubali yaishe, nikamuacha aamini kile mwenyewe alichotaka kukiamini (nitafafanua zaidi baadaye jinsi alivyokuwa amenisevu).
Baada ya kuelewana na nesi huyo, alianza kunieleza kwamba walimpokea mgonjwa huyo majira ya saa tisa za jioni baada ya kuletwa na wasamaria wema ambao walidai wamemkuta amepigwa na kujeruhiwa vibaya nje ya nyumba yao.
“Alikuwa akitokwa na damu nyingi huku pia akiwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake, ikabidi tumpokee hivyohivyo na kuanza kumpatia matibabu lakini mpaka sasa hakuna anayejua jina lake, ametokea wapi na nini kilichomsibu, tunasubiri labda akirejewa na fahamu au ndugu zake wakija ndiyo watueleze kilichotokea,” alisema yule nesi, nikashusha pumzi ndefu na kugeuka kumtazama Shenaiza pale kitandani.
Baada ya kumaliza kuzungumza na nesi, nilimuomba niende kukaa pembeni ya Shenaiza mpaka atakaporejewa na fahamu zake lakini aliniambia kuwa ni kinyume na taratibu za hospitali hiyo, akanitaka nikakae nje ya wodi na kama kuna chochote, atanipa taarifa lakini akasisitiza kwamba mgonjwa alikuwa anahitaji damu zaidi kwa sababu amepoteza nyingi, akanitaka kama nipo tayari kumchangia anielekeze nini cha kufanya.
Sikuwa na kipingamizi, nilikubali kumchangia damu, yule nesi akanichukua mpaka kwenye wodi nyingine ambapo alinitambulisha kwa madaktari wenzake na kuwaeleza kwamba nilikuwa nataka kumtolea damu mgonjwa wangu Shenaiza. Nikachukuliwa vipimo vya awali na baada ya kuonekana nilikuwa fiti, niliingizwa kwenye chumba kingine na kuanza kutolewa damu.
Nikiwa naendelea kutoa damu, niliendelea kujiuliza maswali mengi kuhusu Shenaiza yaliyokosa majibu. Kuna wakati nilijilaumu sana kukataa kuonana naye mapema kwani niliamini pengine ningeweza kumsaidia asipatwe na kilichomtokea. Hata hivyo nilijipa moyo kwamba sikuwa nimechelewa, nikawa namuombea kwa Mungu apone na kurudi kwenye hali yake ya kawaida.
Baada ya kumaliza kutolewa damu, nilirudi pale nje ya wodi na kukaa huku nikiendelea kutafakari mambo mengi. Tayari kigiza cha jioni kilishaanza kuingia lakini moyo wangu haukuwa radhi kuondoka hospitalini hapo, nilijiapiza kwamba hata ikibidi kukesha usiku kucha, nitafanya hivyo mpaka nifahamu kilichomsibu Shenaiza.
Ilipofika majira ya kama saa moja za jioni, yule nesi, Rozina alinifuata na kunipa habari ambazo zilinifanya mapigo ya moyo yanilipuke kuliko kawaida. Aliniambia Shenaiza amerejewa na fahamu na jambo la kwanza alilouliza ni kama nilikuwa nimempigia simu.
“Nimemwambia kwamba upo hapa nje, akaniomba sana akuone, lakini anazungumza kwa shida sana,” alisema nesi huyo, nikainuka na kuanza kumfuata harakaharaka kuelekea wodini.
Je, nini kitafuatia?
 
SEHEMU YA 05:

ILIPOISHIA:
Aliniambia Shenaiza amerejewa na fahamu na jambo la kwanza alilouliza ni kama nilikuwa nimempigia simu.
“Nimemwambia kwamba upo hapa nje, akaniomba sana akuone, lakini anazungumza kwa shida sana,” alisema nesi huyo, nikainuka na kuanza kumfuata harakaharaka kuelekea wodini.
SASA ENDELEA…
Muda mfupi baadaye, tulikuwa pembeni ya kitanda alichokuwa amelazwa msichana huyo, nesi Rozina akaniambia ananipa dakika chache za kuzungumza na mgonjwa, akatoka na kufunga mlango wa wodi hiyo. Kwa muda wote huo, macho yangu yalikuwa juu ya uso wa msichana huyo ambaye naye alikuwa akinitazama, tukawa tunatazamana.
Tofauti na nilivyofika mara ya kwanza hospitalini hapo, safari hii niliweza kumuona vizuri msichana huyo. Kitu ambacho naomba nikiseme wazi, japokuwa alikuwa kwenye maumivu makali, akiwa amefungwa bandeji kubwa kichwani na jicho lake moja likiwa limevilia damu na kuwa jekundu, Shenaiza alikuwa na sura nzuri mno.
Nilijikuta nikivutiwa naye na kuendelea kumtazama, naye akawa ananitazama bila kusema kitu chochote mpaka nilipoamua kuvunja ukimya.
“Pole dada Shenaiza! Pole sana,” nilisema kwa sauti ya upole, kauli yangu ikawa kama mkuki ndani ya moyo wake kwani badala ya kujibu, alianza kuangua kilio kikali cha kwikwi, machozi mengi yakawa yanachirizika kupitia kwenye pembe za macho yake na kuishia kwenye shuka jeupe alilokuwa amelala juu yake.
Ikabidi nimsogelee zaidi na kumuinamia pale kitandani, kwa kutumia mkono wangu mmoja nikawa namfuta machozi huku nikiendelea kumpa maneno ya kumfariji, nikamuona naye akitoa mkono wake mmoja kwenye shuka na kuushika mkono wangu huku akiendelea kulia, akauvutia kifuani kwake huku akinitazama usoni.
Macho yake ni kama yalikuwa na sumaku kwani katika mazingira ambayo sikuyategemea, na mimi nilijikuta nikianza kulengwalengwa na machozi. Nilijikuta nikimuonea mno huruma msichana huyo na kuwa na shauku kubwa ya kutaka kusikia nini kilichomtokea.
Mpaka muda huo, hakuwa amefumbua mdomo wake na kuzungumza neno hata moja zaidi ya kuendelea kulia tu huku akinitazama kwa macho yaliyobeba ujumbe. Japokuwa na mimi nilijisikia uchungu sana, nilijitahidi kujikaza kiume na kuendelea kumbembeleza.
“Nashukuru kwa upendo wako ulionionesha, kumbe nilivyokuwa nimekutafsiri baada ya kusikia sauti yako mara ya kwanza nilipokosea namba yako ya simu nilikuwa sahihi kabisa,” alisema Shenaiza kwa sauti ya chini mno lakini iliyosikika vizuri kabisa masikioni mwangu.
“Usijali Shenaiza, nipo kwa ajili yako na nitaendelea kuwepo pembeni yako kwa shida na raha,” nilimwambia, kauli ambayo ilimfanya aachie tabasamu hafifu, akaubusu mkono wangu ambao muda wote alikuwa bado ameung’ang’ania.
Kilichonishangaza kwa Shenaiza, japokuwa ndiyo kwanza tulikuwa tunakutana kwa mara ya kwanza, tena akiwa kwenye maumivu makali, alionesha kama ana hisia fulani juu yangu kwa sababu siyo rahisi kumshika mkono kisha ukaubusu kwa mtu ambaye wala hujawahi kumuwazia akilini mwako.
“Halafu kumbe wewe ni kijana mzuri namna hiyo, kwa nini hujaoa mpaka leo,” alisema Shenaiza kwa lafudhi nzuri japo alionesha kuwa na maumivu, nikajikuta nikitabasamu na kukosa cha kumjibu.
“Kwani nini kimekutokea dada’angu?”
“Ni stori ndefu, ngoja nitakusimulia kila kitu nikipata nafuu lakini naomba umwambie na nesi kwamba sihitaji mtu yeyote ajue kwamba nimelazwa hapa, naweza kupata matatizo mengine bure. Naomba wewe ndiyo uwe mtu pekee wa kunisimamia mpaka nitakapopona,” alisema msichana huyo kwa sauti ya chini iliyoonesha bado yupo kwenye maumivu, nikawa natingisha kichwa kuonesha kukubaliana naye.
Kwa muda mfupi niliozungumza na Shenaiza, niligundua kwamba huenda ana jambo zito sana lililokuwa likiusumbua moyo wake na kweli alikuwa akihitaji mtu wa kumsaidia ingawa bado sikuwa najua ni nini kilichokuwa kinamsumbua.
“Nikuulize swali jingine?” nilimhoji, akatingisha kichwa kuonesha kukubali. Nilitaka kumuuliza kuhusu jinsi alivyokuwa amenisevu kwenye simu yake lakini nikahisi huenda nikam-boa kwa swali hilo.
“Uliza tu,” alinisisitiza baada ya kuona nasitasita.
“Kwa nini umenisevu vile kwenye simu yako?”
“Simu yangu? Mungu wangu, we umeonaje wakati hata simu yangu huijui,” alisema msichana huyo huku aibu za kikekike zikiwa zimetawala kwenye uso wake, akawa anakwepesha macho yake ili yasigongane na yangu, tabasamu hafifu likiwa limechanua kwenye uso wake.
Aliendelea kulikwepakwepa swali hilo lakini na mimi niliendelea kumbana hapohapo. Nilichokifanya, niliamua kuipiga namba yake na kwa kuwa simu yake ilikuwa pembeni ya kitanda chake ingawa mwenyewe hakuiona, muda mfupi baadaye ilianza kuita, namba yangu ikiwa imeseviwa ‘My Husband’! Akazidi kujisikia aibu za kikekike na mwisho akafunguka:
“Niliamua kukusevu hivyo kwa sababu ya matatizo yanayonikabili, naomba suala hilo tusilizungumze leo, ipo siku utanielewa,” alisema na kugeukia pembeni kuonesha hakuwa akitaka tuendelee kuzungumzia suala hilo, nikabadilisha mada haraka.
Kingine kilichonishangaza kwa Shenaiza, kila nilichokuwa namuuliza alikuwa akikwepa kunijibu, hakuna jambo hata moja ambalo nilitaka kulijua na akanijibu bila wasiwasi, nilipomuuliza anaishi wapi na anakaa na nani, alikwepa swali hilo kwa maelezo kwamba tutazungumza siku nyingine akiwa amepona.
Nilipomuuliza pia nini kilichomtokea mpaka akaumia hivyo mpaka kulazwa hospitalini hapo, bado hakuwa tayari kunieleza, kisingizio kikawa kilekile kwamba mpaka atakapopona ndiyo atanieleza kila kitu.
Kwa kuwa bado mwili wake haukuwa na nguvu hasa baada ya kupoteza damu nyingi kama alivyonieleza nesi Rozina, nilikubaliana naye. Nilipomuuliza kama angehitaji nini usiku huo kwa ajili ya chakula kwa sababu nilikuwa na uhakika kwamba hajala chochote, aliiambia nikamtafutie juisi tu, inamtosha.
Tayari nesi alishaingia na kunitaka nitoke kwani mgonjwa alikuwa akihitaji mapumziko ya kutosha, nikamwambia kwamba kuna vitu ameniagiza naenda kumnunulia nitarejea baada ya muda mfupi, nesi akaniruhusu huku akisisitiza niwahi kwani kuna muda ukishafika, watu wa kawaida hawaruhusiwi tena kuingia wodini.
Nilitoka haraka na kwenda kwenye maduka yaliyokuwa jirani na hospitali hiyo, nikamnunulia juisi maboksi mawili na keki laini ambazo niliamini atazipenda. Nikarudi wodini na muda mfupi baadaye niliruhusiwa tena kuingia wodini, nikamkuta Shenaiza ametulia pale kitandani, akionesha kuanza kupata ahueni kubwa. Aliponiona tu, tabasamu pana lilichanua kwenye uso wake, nikamsogelea mpaka pale kitandani, nikatoa maboksi ya juisi na keki na kuweka kwenye droo ya pembeni ya kitanda na kumtaka akijisikia ahueni ajitahidi kunywa.
Kwa kuwa muda nao ulikuwa umeyoyoma, nilimuaga kwamba narudi nyumbani lakini nitakuja kumtembelea asubuhi lakini alionesha kuwa mgumu kukubaliana na hilo.
Mara simu yake ilianza kuita mfululizo, akaishika na kutazama namba ya mpigaji lakini katika hali ambayo sikuielewa, aliiachia simu hiyo, ikadondoka chini na kufunguka betri ikaangukia kivyake, mfuniko kivyake na simu nayo kivyake. Akaanza kuangua kilio kwa uchungu huku akiniomba nimsaidie, nilibaki nimepigwa na butwaa.
Je, nini kitafuatia? Usikose
 
SEHEMU YA 06:

ILIPOISHIA:
Mara simu yake ilianza kuita mfululizo, akaishika na kutazama namba ya mpigaji lakini katika hali ambayo sikuielewa, aliiachia simu hiyo, ikadondoka chini na kufunguka betri ikaangukia kivyake, mfuniko kivyake na simu nayo kivyake. Akaanza kuangua kilio kwa uchungu huku akiniomba nimsaidie, nilibaki nimepigwa na butwaa.
SASA ENDELEA…
“Nikusaidie nini Shenaiza?” nilimuuliza huku nikiiokota ile simu na kuiunganisha upya.
“Nakuomba usiniache, fanya kila kinachowezekana unitoroshe hapa hospitalini usiku huuhuu, watakuja kunimalizia,” alisema msichana huyo na kuzidi kunichanganya.
“Watakuja kukumalizia? Akina nani? Na Kwa nini tutoroke wakati hali yako bado siyo nzuri?”
“Naomba ufanye nilichokuomba mengine utaenda kuyajua mbele ya safari,” alisema msichana huyo huku akiendelea kulia.
Nikiwa bado nimeduwaa, nikiwa sijui cha kufanya, nilishtuka kumuona akichomoa sindano ya dripu aliyokuwa amechomwa mkononi mwake na kusababisha damu zianze kumtoka mkononi, akajikongoja huku akionesha kuwa na maumivu makali, akanitaka nimpe bega langu ili apate balansi ya kutembea.
Sikuwa na cha kufanya zaidi ya kukubaliana na matakwa yake, japokuwa nilikuwa najua kwamba ninachokifanya ni hatari sana lakini sikuwa na namna zaidi ya kumsaidia msichana huyo ingawa mpaka muda huo sikuwa najua nini kinachomsumbua.
Huku damu zikimvuja na kudondokea sakafuni, nilimsaidia kutembea, tukatoka mpaka nje ya wodi hiyo huku mara kwa mara nikigeuka nyuma kutazama kama hakuna mtu aliyekuwa akitufuatilia.
Kwa bahati nzuri, kwa kuwa muda ulikuwa umeenda sana, madaktari wengi walishaondoka sambamba na manesi ambapo waliosalia walikuwa ni wale wenye ‘shift’ ya usiku ambao nao hawakuwa wengi.
“Heeei! Mnakwenda wapi usiku wote huu,” mwanaume wa makamo ambaye bila hata kuuliza tulijua ni mlinzi wa hospitali hiyo kutokana na kuvalia sare huku mkononi akiwa na kirungu, alituuliza huku akifunga geti la kutokea nje.
Ilibidi nimdanganye kwamba nilimleta mgonjwa wangu kutibiwa majeraha aliyoyapata kwenye ajali lakini hatukumkuta daktari kwa kuwa alishaondoka, nikamdanganya kwamba tunaenda kujaribu kwenye hospitali nyingine lakini hakutaka kuelewa. Akasema hawezi kuturuhusu kutoka mpaka tupate kibali kutoka kwa daktari aliyekuwa zamu usiku huo.
Shenaiza ni kama alijua kilichokuwa ndani ya akili yangu kwani alianza kuugulia kama anayesikia maumivu makali, nikatumia kigezo hicho kuendelea kumshawishi yule mlinzi aturuhusu na alipozidi kukomaa, nilichomoa noti moja ya shilingi elfu kumi na kumshikisha, nikamuona akiachia tabasamu na kututaka kuwa makini.
Akafungua geti ambapo breki ya kwanza ilikuwa ni kwenye kituo cha teksi kilichokuwa nje ya hospitali hiyo, tukaingia kwenye teksi moja na kuondoka huku nikimuelekeza dereva kutupeleka nyumbani kwangu, Mikocheni.
Kwa kuwa ulikuwa ni usiku na hakukuwa na foleni, haikutuchukua muda mrefu tukawa tayari tumeshawasili Mikocheni, nilipotaka kumlipa dereva teksi fedha zake tulizokubaliana, Shenaiza ambaye muda wote alikuwa amejilaza huku kichwa chake akiwa amekiweka kwenye mapaja yangu, aliniambia nisilipe.
“Nina fedha za akiba kwenye pochi yangu ndogo, hebu fungua,” aliniambia, kweli nikafungua pochi yake ndogo aliyokuwa ameiweka kwenye mfuko wa gauni refu alilokuwa amelivaa. Nilipoifungua, nilishangaa kukuta kuna noti kadhaa za dola miamia za Kimarekani na noti mbili za shilingi elfu kumi, zote mpya.
Nikatoa na kumpa dereva na kutaka kurudisha pochi mahali pale lakini aliniambia kwamba nikae nayo mimi, nikakubali na kuiweka kwenye mfuko wa suruali niliyokuwa nimeivaa.
Wakati wa kushuka, kama ilivyokuwa wakati wa kupanda, ilibidi yule dereva teksi anisaidie kumtoa Shenaiza ambaye bado alikuwa akiugulia maumivu makali, akapitisha mkono wake kwenye bega langu na nikawa namsaidia kutembea kuelekea ndani kwangu.
Nilifungua mlango na kumkaribisha ndani, japokuwa alikuwa kwenye maumivu makali, nilimuona akiachia tabasamu hafifu kisha akanisifia: ”Mh! Jamani wewe msafi hadi raha, inatakiwa umpate mwanamke msafi kama wewe ndiyo awe mke wako ndiyo mtaendana,” alisema huku akikodolea macho huku na kule ndani ya sebule yangu.
Japokuwa sikuwa nimeoa lakini hakuna kitu nilichokuwa nakipenda kama kuiweka nyumba yangu katika hali ya usafi, kuanzia sebuleni mpaka chumbani huku nikinunua vitu vingi vya kisasa.
Nilimsaidia Shenaiza kukaa pale sebuleni kwenye sofa kisha nikamvua viatu alivyokuwa amevaa pamoja na koti alilovaa juu ya gauni lake na mtandio aliokuwa amejizibia lile jeraha la kichwani.
“Shenaiza mwenzio naogopa kulala na wewe ukiwa kwenye hali hiyo, ukizidiwa usiku itakuwaje? Kwa nini tusiende hospitali nyingine? Hapa siyo mbali na Hospitali ya Kairuki,” nilimwambia lakini alikataa katakata na kuniambia kwamba hospitalini haikuwa sehemu salama kwake kwa wakati huo.
“Basi kuna rafiki yangu anaishi hapo mtaa wa pili ni daktari lakini bado hajaajiriwa, anafanya ‘field’ hapo Kairuki, unaonaje nikamuite aje kutusaidia?”
“Hapana usijali, nitakuwa sawa kwa sababu kama ni damu nimeshaongezewa ya kutosha, ondoa hofu,” alisema huku akiinua mkono wake taratibu na kunigusa kwenye shavu langu la upande wa kushoto, akawa ananivutia pale alipokuwa amekaa.
Kwa tahadhari kubwa nikiogopa nisije nikamtonesha majeraha yake, niliulanisha mwili wangu, akanivutia mpaka nilipomsogelea kabisa, akanibusu kwenye shavu langu na kuninong’oneza.
“Ahsante sana kwa msaada wako, ni Mungu pekee ndiye atakayekulipa, upo tofauti sana,” nilitabasamu na kumtazama, macho yetu yakagongana, naye akaachia tabasamu hafifu.
Kwa kuwa sikuwa nimekula chochote, ilibidi nimuage kwamba naenda kubahatisha kama nitapa chipsi kwenye banda lililokuwa mtaa wa pili kutoka pale nilipokuwa naishi. Nilitoka huku Shenaiza akinisisitiza niwahi kurudi pia nifunge mlango kwa nje ikiwa ni pamoja na kuzima taa zote. Sikujua kwa sababu gani bado alikuwa na hofu kubwa kiasi hicho. Nilifanya kama alivyoniambia na kutoka, nikafunga mlango kisha nikafunga na geti la chuma kwa nje na kuondoka kuelekea mtaa wa pili.
Kwa bahati nzuri nilikuta bado hawajafunga, nikaagiza chipsi sahani mbili na vipande vya kuku kwani nilitaka nikambembeleze Shenaiza naye ale japo kidogo. Dakika kadhaa baadaye chakula changu kilikuwa tayari, nikalipa na kuanza kuondoka huku nikijitahidi kutembea haraka kwani nilipoteza muda mwingi pale kusubiria chakula.
Katika hali ambayo sikuitegemea, nilipotokeza kwenye uchochoro wa kuelekea kwangu, kwa mbali niliwaona wanaume kama watatu hivi wakiwa wamesimama mlangoni kwangu, mmoja akiwa anagonga mlango kwa nguvu.
“Mungu wangu, akina nani tena hao usiku wote huu?” nilijiuliza huku nikirudi nyuma na kujibanza pale uchochoroni, nikawaona wale wanaume wakiendelea kugonga mlango kwa nguvu. Ugongaji wao ulionesha dhahiri kwamba hawakuwa wamekuja kwa heri, nikawa natetemeka nikiwa sijui nitafanya nini.
Je, nini kitafuatia? Usikose
 

Similar Discussions

23 Reactions
Reply
Back
Top Bottom