Simulizi: Soka Lilivyonikutanisha Na Shetani

Sehemu ya 36
Hakuna kitu nilikuwa sipendi kama kwenda Mwanza, sio kwamba mji ule nilikuwa siupendi.
Laa! Ila nafsi yangu ilikuwa haipendi kupata kumbukumbu ya kitendo cha kuitelekeza familia yangu hospitali ya Bugando na kutimkia mjini Tabora kwa Lawalawa.
Tukio hilo lilizidi kunitesa kisaikolojia, kila wakati sauti ya mke wangu Pili ikinisihi nisiwaache ilikuwa ikijirudia. Picha ya mwanangu akiwa anateseka kitandani ikawa inajitengeneza kichwani mwangu.
Tulicheza mchezo wetu na timu ya Kigoma fc, mchezo huo tukashinda mabao matatu kwa bila, wakati magoli mawili nikifunga mwenyewe huku lile moja nikitoa asist.
Siku chache baada ya mchezo huo, kocha akatutaka wachezaji tujitayarishe kwa safari ya Mwanza kwa ajili ya mchezo wa na Igogo fc, siku hiyo kutwa nzima nilikosa raha. Kwa kweli sikupenda kabisa kufika katika jiji lile.
Siku ya pili tuliondoka na treni kuelekea Mwanza, wachezaji tulikuwa kwenye mabehwa ya daraja la kwanza. Wakati wenzangu wakicheza karata na kufurahia pamoja safarini, mimi nilikuwa peke yangu nikiwa nimezama kwenye lindi la mawazo.
“Unamuwa nini?” daktari wa timu aliniuliza.
“Hapana naifikiria mechi tu.” nilimdanganya
“Una presha?”
“Ndio, si unajua ni timu niliyotokea.”daktari yule ambaye pia alikuwa mtaalamu wa mambo ya saikolojia alianza kunijenga kiakili.
Tuliwasili Mwanza asubuhi ya siku iliyofuatia, tulifikia katika lodge moja nzuri tu ambayo kwa kweli jina lake sikumbuki vizuri. Baada ya kupumzika kidogo, niliomba ruhusa ya kutoka.
Kwa kuwa walitambua nilikuwa mwenyeji kwenye mji ule, hilo halikuwa tatizo kwao, viongozi wangu wa timu waliniruhusu.
Nilichukua gari hadi Bugando, nikaelekea hadi katika ofisi ya daktari aliyekuwa akimuuguza mwanangu. Kwa bahati nzuri nilimkuta hana wagonjwa wengi, alinikaribisha kitini na kunisikiliza:
“Unanikumbuka dokta?” nilimuliza.
“Vizuri sana, nakukumbuka. Wewe si baba wa yule mtoto aliyekuwa anaumwa kansa ya damu?”
“Naam!! ndio mimi dokta, tangu kipindi kile ndio narudi Mwanza leo.”
“Kwa hiyo huna taarifa ya kilichomkuta mwanao?” dokta aliuliza huku akiningalia kwa chati.
“Sina dokta. ”
“Yule mtoto alifariki dunia,”dokta aliniambia kwa ufupi.
🗣shunie kuja apa uendelee
 
Mwaaah!!! Swadakta, ngoja nijikusanye nianze kuanzia nambari moja mdogo mdogo
Kuna hii apa pia
 
Sehemu ya 37

Kwa dakika nzima nilibaki nimeduwaa, nimeganda kama niko kwenye theruji. Nilihisi uchungu mkali mno moyoni, nilijiona ni mwanaume mpumbavu, nisiyestahili kuigwa mbele ya jamii.

Kwa kiwango kikubwa nilikuwa nimesababisha kifo cha mwanangu. Nilishusha pumzi ndefu, kisha nikaendelea kumuliza daktari.
“Mazishi ya mwanangu yalifanyikia wapi ili angalau nikalione kaburi lake?” “Nitajuaje!!” dokta alijibu harakaharaka.

Sikuwa na la ziada la kumuuliza dakatri yule. Nilichofanya ni kuondoka nikiwa nimeghafirika vibaya sana, nilirudi hadi kwenye ‘lodge’ tuliyokuwa tumefikia, baada ya kufika nikaingia chumbani mwangu na kutulia humo nikitafakari kifo cha mwanangu.

Kwa mara ya kwanza katika maisha yangu nikagundua nilikuwa nimemfanyia kosa kubwa sana mke wangu Pili, pamoja na kwamba nilikuwa sina mapenzi na mwanamke huyo, ila sikutakiwa kabisa kumtelekeza hospitalini akiwa na mwanangu aliyekuwa mahututi kitandani.

siku hiyo nilishinda chumbani kama mgonjwa wa homa kali, daktari wa timu aliponihoji juu ya hali ile nilimdanganya nilikuwa nahisi homa.

Kwa kuwa nilikuwa mchezaji tegemeo katika timu ile, kila mtu aliguswa na hali niliyokuwa nayo, hata hivyo sikupenda kufungua mdomo na kuwaeleza watu ukweli wa jambo linalonisibu.

Hadi inafika siku ya mechi kwa kweli bado nilikuwa sina utimamu wa mwili na akili, nakumbuka siku hiyo nilimwomba kocha asinipange.

Nilikuwa nasumbuliwa na sana taswira ya mwanangu, kila wakati nilikuwa najutia na kujilaumu mwenyewe.

Mchezo kati ya timu yetu na Igogo Fc, timu yangu ya zamani, ulikuwa mkali sana, nakumbuka hadi dakika ya 20 kipindi cha kwanza tayari tulikuwa tumekwisha fungwa goli mbili kwa bila.
Kutokuwepo kwangu uwanjani pengo lilikuwa kubwa sana, timu yangu ya Reli Tabora ilikuwa imejengwa kunizunguka mimi.

Hadi tunakwenda mapumziko ya kipindi cha kwanza timu ya Igogo fc ilikuwa inaongoza kwa goli tatu kwa bila, naweza nikasema timu yangu ilikuwa imezidiwa vibaya sana.

“Vipi hutaweza kabisa kucheza?” kocha aliniuliza wakati wa mapumziko.
“Hapana kocha, bado sijikisii vizuri.
20190909_084031.jpg
 
Sehemu ya 38

“Timu haina muunganiko kwenye safu ya mbele, tunakuhitaji, umepewa nini wewe.”Kocha alinikoromea kwa ukali kana kwamba mimi ndio nimesababisha hali ile.
Hata hivyo bado sikuwa tayari kucheza siku hiyo, kama nilivyosema awali sikuwa najisikia vizuri kiakili na kimwili.

Timu ziliporudi uwanjani, bado timu yangu ya Reli Tabora iliendelea kunyanyasika mbele ya timu yangu ya zamani ya Igogo Fc.

Dakika 10 za kipindi cha pili jamaa walipata penati. Wakatufunga goli la nne. Katika dakika ya 29 ya mchezo. jamaa wakapata kona, ilipopigwa, mabeki wakachelewa kumfanyia ‘marking’ mshambuliaji mmoja mjanja mjanja akapiga ‘Free heder, wakaandika goli la tano.

Timu yetu ilikuwa imepoteana, imezidiwa kila eneo, dakika ya 45 kabla ya mchezo kumalizika tukapigwa tena goli la sita.
Ilikuwa ni siku mbaya kwa timu yangu. Kilikuwa ni kipigo cha mbwa koko. Haikuwahi kutokea kipigo cha hivyo,tangu timu hiyo ianzishwe, kwa kweli yalikuwa ni matokeo ya kuudhi mno.

Nakumbuka refa wa mchezo aliongeza dakika 4, dakika mbili kabla ya filimbi ya mwisho tukafungwa goli la saba!. Tukoandoka uwanjani tukiwa tumepigwa mabao saba kwa bila, kilikuwa ni kipigo kikubwa kwangu tangu niingie kwenye ulimwengu wa soka.

Tulirudi lodge tukiwa tumeghafirika vibaya sana, kIla mtu alichukizwa na matokeo yale, siku hiyo hiyo viongozi wakatutaka tujiandae kwa ajili ya safari ya kurudi mjini Tabora asubuhi ya siku inayofuatia.

Usiku wa siku hiyo nikiwa chumbani mwangu na rafiki yangu mchezaji mmoja anaitwa Said ingawa yeye alipenda tumwite Side, akaniambia viongozi na makocha walikuwa wakinishutumu kwamba nimeihujumu timu
“Kivipi?” nilimuliza nikiwa nimetoa macho pima.

“Wanasema umepewa hongo na timu yako ya zamani ili usicheze.”
“Mimi!!”
“Wewe hapo ndio.”
“Siwezi kufanya huo ujinga.”
 
Sehemu ya 39

Kwenye soka la bongo kuna mambo mengi, kama jamaa wamefika bei nzuri hata kama mimi siwezi kupiga teke kapu la pesa” Side aliongea katika namna ya kutojali utetezi wangu, hata yeye aliamini nilikuwa nimechukua fedha.

“Side nielewe basi, wakati wote kwenye maisha yangu ya soka siwajawahi kufanya hila ya namna yoyote kuihujumu timu yangu.”

“Unataka kuniambia jamaa wanakusingizia?”
“Mwananipakazia Side, siwez kufanya ujinga huo.”
“Na unataka kunimbia jamaa wa Igogo Fc hawajakufuata kabisa kuongea na wewe.”
“Hajaniafuata mtu.”

“Mmh!!! Mbona inasemekana jana asubuhi ulikwenda kuonana nao?”swali hilo lilinishitua mno. Kwa kweli jamaa walikuwa wamewaza mbali sana.
“Jana sikwenda kuonana na mtu yeytote zaidi ya daktari” nilimwambia nikiwa nimesawikija kwa hasira.

“Unaumwa nini?” swali hili halikujibika. Sio kwamba sikuwa na jibu. Laa! bali niliona kumjibu swali lake ningelazmika kutoa hadithi yote iliyonipeleka Bugando kitu ambacho sikuwa tayari. “Unaumwa nini?” Side aliniuliza tena.

“Ni mambo yangu binafsi, sio lazima kila mtu ajue.” “Basi ndio hivyo comredi Ajibu, inasemekana umepewa mlungura ili usicheze.” Side aliendelea kukazia jambo lile.

“Kwa hiyo Side leo ningecheza tusingefungwa goli saba?”
Nilimuliza. Akabakia amenikodolea macho kama mpumbavu.

Tangu Side aliponiambia mambo hayo, nilikosa kabisa amani ya roho. Sikuitwa kuhojiwa na kiongozi yeyote juu ya jambo hilo ingawa liliendelea kuzungumzwa chini chini.
Siku ya pili, tuliondoka na kurudi mjini Tabora, bado hakuna kiongozi yeyote aliyeniuliza japokuwa walionekana kunichukia.

Kwa kuwa sikuwa nahusika na aina yoyote ya hila dhidi ya timu yangu, na mimi sikujisumbua kabisa kwenda na kuhoji juu ya skendo hiyo, niliendelea na shughuli zangu bila kujali uvumi huo. *****

Wiki tatu zilipita. Nikiwa mjini Tabora, angalau kidogo nafsi yangu ilipata ahuni juu ya kifo cha mtoto wangu. Kwa kuwa kilichokuwa kinaniunganisha na mke wangu ni mtoto ambaye naye amekwisha fariki. Niliweka nadhiri ya kutorudi kabisa kijijini kwetu.
 
Sehemu ya 40

Mipango yangu katika maisha, ilikuwa ni juu ya mwanamke mzuri wa kiarabu, Lawalawa. Maisha yangu ya soka yaliendelea kwenye klabu ya Reli ingawa ukweli ni kwamba sikuwa mtu mwenye furaha mahali hapo.

Tangu tukio la kufungwa goli saba na Igogo Fc sikuwa mchezaji ninayeaminika kabisa, unahodha nilipewa siku chache baada ya kusajiliwa na timu hiyo nikapokonywa.

Vituko na lawama za kila aina zikawa nyingi, timu ile ikaanza kupoteza michezo mara kwa mara, kwa kuwa na mimi sikuwa na furaha mahali pale, sikujitoa kwa asilimia mia moja.

Mwezi Decemba wakati wa dirisha dogo, timu mbili za ligi kuu zilikuwa zinanitaka, timu ya kwanza ilikuwa inatoka mkoani Dodoma, na nyingine ilikuwa ya mkoani Dar es salam.

Kwa kuwa moja ya ndoto zangu ilikuwa ni kuishi jijini Dar es salam, nikiamini kwa kuishi Dar ingekuwa rahisi kuzifikia ndoto zangu. Hivyo nilizungumza na maskauti wa timu ya Mzizima Fc, nikawaeleza niko tayari kujiunga na timu yao.

Japokuwa nilikuwa bado nina mkataba wa mwaka mmoja na klabu yangu, lakini nililazimika kununua mkataba ule ilimradi tu niondoke Reli Tabora.

Kupitia mpenzi wangu Lawalawa alinipataia kiasi cha fedha nilichokitaka, nikanunua sehemu ya mkataba ule, kisha nikasajiriwa na timu kutoka Dar, Mzizima Fc.

Mambo yote hayo niliyafanya bila kumshirikisha mpenzi wangu Lawalawa, nilitambua kama ningemweleza nahitaji kuhamia Dar lazima angenikatalia, hivyo baada ya kumaliza mambo yote ndipo nikamwambia:

“Ajibu laiti kama ungeniambia pesa niliyokupa ni kwa ajili ya mchakato wa kutimkia Dar nisingekubali kukupa fedha zangu.”

“Usijali siku moja utanielewa mpenzi”
“Kwa hiyo utahamia Dar kabisa?”
“Ndio Lawalawa, itanibidi nihamie Dar, hata hivyo nitakuwa nakuja Tabora mara kwa mara.”

Lawalawa alinikumbatia na kunipiga mabusu mengi. Siku chache badaye nikatimkia zangu Dar es salam rasmi kwa kucheza ligi kuu Tanzania bara.

Huo ulikuwa ni mwaka 2004. **** Maisha yalikuwa mazuri jijini Dar, angalau nilikuwa nimekwisha sahau kila kitu cha nyuma, sio wazazi wangu, wala mke wangu, Pili, aliyekuwa ndani ya kichwa changu.

Kitu pekee nilichokua nakiwaza kwa wakati huo ni kukamilisha ndoto zangu. Kuwa mchezaji maarufu wa kiwango cha kimataifa.
 
Sehemu ya 41

Dar, nilikuwa naishi Sinza sehemu mmoja maalufu inatwa Sinza kwa Remi. Hapo ndipo klabu yangu ya Mzizima ilipokuwa imenipangia nyumba.

Nyumba hiyo nilikuwa siishi peke yangu, nilikuwa nakaa na mchezaji mwingine aliyesajiriliwa kutokea visiwani Pemba katika moja ya timu za huko. Huyu jamaa alitwa Cholo Abdulahman, na nafasi yake uwanjani alikuwa ni kipa.

Alikuwa ni jamaa mpole lakini mkalimu na alipeda kufanya ibada mara kwa mara. Kwa muda mfupi sana, mimi na Cholo tukajikuta tumeshibana mno.

Kila siku tulikwenda mazoezini pamoja.Katika timu ya Mzizima kulikuwa na wachezaji wenye vipaji vikubwa. Timu hiyo ilikuwa na kikosi kipana sana, hivyo hata ushindani wa namba ulikuwa mkubwa.

Katika nafasi niliyokuwa nacheza uwanjani, kulikuwa na wachezaji wengine kama wawili ambao walikuwa ni moto wa kuotea mbali. Mmoja alikuwa anatokea nchini Kongo mwingine alikuwa ni mwenyeji wa Mbeya.

Hata wakati wa kutambulishwa kwangu, haikuwa habari kubwa kwa kuwa tu ‘plofile yangu haikufanana na washambuliaji waliokuwepo, ambao walitokea katika klabu zenye majina makubwa Afrika.

Hali ya ushindani wa namba uwanjani,haikuwa kwangu tu, bali hata kwa rafiki yangu Cholo ambaye naye alikuwa ni kipa namba tatu, mara nyingi sana tulisota benchi tukingojea wachezaji wanaotumaniwa aidha waumie au wachoke, ndipo sisi tulipata nafasi!. Mara nyingi mimi nilikuwa naingia dakika za mwishoni mwa mchezo tena hapo labda timu imekwisha pata matokeo ndipo kocha mzungu alikuwa akinipa nafasi.

Na japokuwa nilipata nafasi finyu ya kucheza, lakini kila ilipotekea nilikuwa nikionyesha uwezo, kila nilipopata nafasi moja ya kufunga, nilifunga au kutoa asisti.
Maisha yangu ndani ya Mzizima Fc yalikuwa hayo:

Kama kijana mwenye kiu na mafanikio, kwa kweli sikuvutiwa kabisa na maisha hayo, nilikazana na kukazana, lakini wapi, sikuweza kabisa kumshawishi kocha mzungu kuanza kwenye kikosi cha kwanza mbele ya mshambuliaji Mkongamani Didir Bukungu na Felex Kisu, pande la mtu kutoka mkoani Mbeya ambaye pia aliwahi kucheza soka ulaya na timu nyingine kama Al ahal, na Tasker ya Kenya.Sikufua dafu.

“Ipo njia moja tu ya kupata nafasi ya kucheza.” Siku moja cholo aliniambia.
“Njia ipi?”
 
Sehemu ya 42

“Kuwapiga misumari hao mabwege.”
“Kupiga misumari ndio nini” nilimuliza.
“Kuwaroga.”
Eeh!!” “Ndio, njia pakee ya kupata nafasi ni kuwaroga hao jamaa” Cholo alisistiza.

JAMBO alilonieleza Cholo sio kwamba lilikuwa jipya masikioni mwangu. Laa! Nilikwisha wahi kusikia mambo ya wachezaji kurogana, achilia mbali timu kuwanga ili ipate ushindi.

Sikuwa nayamini mambo ya kichawi kwenye soka. Lakini kwa kuwa nilikuwa nahitaji niingie kwenye kikosi cha kwanza kwenye timu yangu ya Mzizima, ilinibidi nimsikilize Cholo kwa makini.

“Yupo mtaalamu anaitwa Majeed Mapaka, ni mganga mzuri, aliwahi kunisaidia kipindi cha nyuma, naamini hii kazi anaiweza,” Cholo alisema.

Alionekana alikuwa na shauku ya kuaminiwa na kuingia kwenye kikosi cha kwanza, alichoshwa kuwa kipa namba tatu. “Hivi kweli uchawi unaweza kutusadia kwenye hili?”
“Nina asilimia mia moja, hiii ndio njia pekee ya kutusadia...”alisema. Akaendelea.

“Unadhani hao jamaa wanaotuweka benchi wao wamekaa tu kibwege kama sisi, nao wanatembea kila mara.”
“Unataka kuniambia nao wanaroga?”
“Sana, tena kama wachezaji kutoka Kongo, wanaroga usiku na mchana.”

“Kwa hiyo kama wao wanaroga tutaweza vipi kupambana nao?” niliendelea kumuuliza Cholo. “Uchawi unatofautiana, mfano huyu mganga niliyekwambia anaitwa Majeed Mapaka ni moto wa kuotea mbali, uchawi wake si mchezo.”
“Yuko wapi huyo Majeed Mapaka?”
“Anaishi Unguja, huko Zanzibar.”
“Lini twende?” nilimuliza.

Nilikuwa na shauku ya kuonana na huyo mganga Majeed Mapaka, ili aweze kunisaidia kupata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza cha timu yetu. “Nakusikiliza wewe.” “Unaonaje tukiomba ruhusa tukaondoka hata Kesho?” “Ni sawa tu, sisi sio wachezaji wa kutegemewa kwenye timu, hatuwezi kunyimwa ruhusa.”

Siku hiyo hiyo tuliomba ruhusa kwa viongozi wa timu. Kila mmoja alitoa udhuru kwa uongo wake. Mfano mimi nilisema mke wangu alikuwa amejifungua huko mkoani Tabora, hivyo nilitakiwa kwenda kumwona. Wakati Cholo yeye alidanganya kwamba amefiwa na shangazi yake.

Kwa kuwa hatukuwa wachezaji tegemeo kwenye timu, wala haikuwa tabu kukubaliwa. Tulipewa ruhusa siku hiyo hiyo.
 
Sehemu ya 43

Kwenye nyumba tuliyokuwa tunaishi tulianza maandalizi ya safari ya kwenda Unguja kwa mganga wa kienyeji. **** SIKU YA PILI saa sita mchana, tulikuwa kwenye boti ya MV Kilimanjaro tukikata mawimbi kuelekea visiwani Zanzibar kuwaroga wachezaji wenzetu ili sisi tupate namba kwenye kikosi cha kwanza.

Baada ya lisaa limoja badaye, tuliwasili Unguja . Ilikuwa ni mara yangu ya kwanza, kufika kisiwani humo, baada ya kutoka bandarini, tuliingia mtaani.

Mji wa Zanzibar mitaa yake kidogo inafanana mno kama huna mwenyeji ni rahisi kupotea hasa sehemu moja panaitwa Malindi.

Kwa kuwa nilikuwa na mwenyeji wangu Cholo, sikuwa na wasiwasi. Tulitembea tukipita hapo mjini Malindi, Mji mkongwe kisha Darajani. Tukapanda daladala ya Kiembe Samaki.

Baada ya kuteremka tulitembea tukizipita nyumba kadhaa, kisha safari yetu ikaishia kwenye nyumba moja iliyo onekana kuwa ya kizamani na ilichakaa kwa kukosa ukarabati wa muda mrefu.
“Tumefika. ” Cholo aliniambia. “Uliwahi kufika hapa?”

“Huku mimi ndio kwetu, naishi sehemu moja inaitwa Jitimai kata ya Fuoni.” Alinijibu.
Tulibisha hodi kwenye nyumba hiyo ambayo ilikuwa imetawaliwa na ukimya mkubwa.
“Kuna mtu kweli hapa?”nilimuliza Cholo kwa sauti ya chini.

Cholo akaendelea kugonga mlango na baada ya dakika kadhaa akaja msichana mrefu mrembo, alikuwa amevaa hijabu.
“Asalam aleykum,” binti alitusalimu kwa sauti yenye lafadhi ya Kizanzibari, pia alikuwa ananukia manukato ya kiarabu.
“Waleykum salam, hujambo?” Cholo akamuitikia.

“Sijambo.”
“Shekh Majeed Mapaka, tumemkuta?”
“Ametoka ila atarejea muda si mrefu.”
“Basi twa’mngoja.”
Binti akatutolea jamvi, akalitandika koridoni, kisha akatukaribisha tupumzike. Tuliketi jamvini kumngoja huyo mtaalamu.

Baada ya kama nusu saa, Majeed Mapaka akawasili. Kwa kumuangalia usingeweza kudhani kwamba alikuwa mganga wa kienyeji. Alikuwa ni kijana mzuri, mweupe, alikuwa amevaa shati zuri na suruali ya kitambaa. Kwa kweli alionekana kuwa tofauti na waganga ambao niliwahi kuwaona.

“Karibuni jamani.”
“Tumekwisha karibia.” “Asalam aleykum, naona leo umenikumbuka bwana Cholo.”
 
Sehemu ya 44

“Waleykum salam, kila siku nakukumbuka ndugu yangu.”
Cholo na yule mganga, walionakena ni watu wanaofahamiana. “Naona umeniletea mgeni kutoka bara.” Mganga alimwambia Cholo.

“Ndio. Anahitaji kuijua dunia kiundani huyu bwana.” Cholo alimjibu.
“Umejuaje natokea bara?” niliuliza.
“Nimeona ukaaji wako tu kwenye jamvi, unaonekana wewe sio mwenyeji wa huku.” Mganga yule alinijibu. Akaendelea kutusaili.

“ Tatizo ni nani hasa?”
“Shekhe Majeed, sisi sote tuna tatizo, na kwa bahati nzuri tatizo letu ni la aina moja. ” “Ni nini hasa shida?”
“Si unajua niko timu ya Mzizima Fc ya huko Dar es salam.”

“Naam! Najua.”
“Basi kupata namba ya kucheza imekuwa mtihani shekh.”
“Poleni sana, kwa nini hampati namba?”
“Kuna wachezaji wanaodhaniwa kwamba wanauwezo zaidi yetu, sababu ni hiyo tu.” Cholo alimwambia.

Mganga yule alipiga kimya kidogo, ni kama alikuwa akifikiria jambo fulani kisha akasema: “Haya simameni twendeni huku. Niangalie ukubwa wa tatizo lenu.”
Akatuiingiza kwenye moja ya chumba katika nyumba ile. Ilikuwa ni chumba cha uani. Ndani ya hiko chumba kulikuwa na tunguri, hirizi na vyungu. Chumba kilikuwa kinanukia harufu ya ubani na udi.

Ukutani kulikuwa na ngozi ya mnyama mbaye hadi leo sijui alikuwa ni kiumbe gani. Kulikuwa na kioo kikubwa pamoja na mkia ambao bila shaka ulikuwa ni wa Simba. Kadhalika, kulikuwa na chupa za dawa zisizo hesabika.
 
Sehemu ya 45

Nilihisi mwili wote ukinisisimka wakati nipo ndani ya chumba kile, jamaa alichukua ile ngozi ya mnyama na kuitandika, akatutaka tukae juu ngozi hiyo.

Akachukua mkia ule mkia wa Simba na kutupiga nao kidogo kichwani. Akawasha ubani, moshi ulipoanza kufuka, akajivisha kitambaa cheusi kichwani, kile kitambaa kilifunika uso na kichwa chote, halafu akaketi kwenye kinu cha kutwangia.

Mimi na Cholo tuliendelea kuketi juu ya ile ngozi, tukiangalia kile kilichokuwa kinajiri. Dakikla moja badaye jamaa akapandwa na Majini. “Mnataka kupata nafasi ya kucheza kwenye timu yenu?” sauti moja ya mkwaruzu iliuliza. Yalikuwa ni majini ya yule bwana.

“Ndio....ndio,”tulijibu kwa pamoja. “Hao wachezaji mnao shindana nao, wametumia uchawi mkubwa kujikinga, inabidi utumike nguvu kubwa kuua zindiko lao.”

“Sawa....sawa” tuliendelea kuitikia. “Leteni kuku weusi wa kienyeji na sanda za maiti, sawa?”
“Ndio. ”Cholo aliitikia. Mimi nilishindwa kuitikia, niliona kama tulikuwa tunatumwa vitu vigumu.
Baada ya dakika mbili tatu, majini yale yakaondoka, mganga Majeed akarudi kwenye hali yake.

“Wamesemaje?” akatuuliza.
Moyoni nikajiuliza inamaana huyu jamaa anatuuuliza majini yake yanasemaje, yeye alikuwa hayasikii? Lakini nikakumbuka niliwahi kuambiwa kuwa mtu akiwa amepandwa na majini anakuwa hana fahamu. “Wamesema watu tunaotaka kushindana nao, wamejikinga sana, hivyo sharti tutumie nguvu kubwa kuua zindiko lao. Wameagiza kuku na sanda.”

“Sawa, nishajua kinachotakiwa kufanyika,” Mganga Majeed alisema. Akaendelea.
“Mnaweza kupata hao kuku na hizo sanda ama muache pesa nikatafute mimi hivyo vitu?”

“Nadhani heri tukupe pesa ukatafute mwenyewe.”
“Basi acheni pesa.”
“Shilingi ngapi?”
“Kama elfu arobaini itatosha.” Kwa kuwa fedha haikuwa tatizo kwetu, tulimpa hiyo pesa mara moja. Akatutaka turudi kesho yake ili tumalize kazi kabisa.

Tuliondoka na kwenda nyumbani kwao Cholo huko Fuoni Jitimai. Cholo alikuwa anatokea kwenye familia ya maisha ya kati na ya dini sana, alikuwa akiishi na mama yake mzazi na nduguze wa kike, alimdanganya mama yake tulikuja Zenji kwa mambo binafsi na ndani ya siku mbili tungerudi Dar es salam. Mama yake hakuwa na tatizo.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom