Simulizi: Soka Lilivyonikutanisha Na Shetani

Shunie

JF-Expert Member
Aug 14, 2016
152,959
453,698
Mtunzi Ally Katalambula

Sehemu ya 01

SIKUJUA kama nina kipaji cha mpira wa miguu, hadi watu wa pembeni walipoanza kunieleza hivyo. Mtu wa kwanza kuniambia nina kitu miguuni mwangu, alikuwa ni mwalimu wangu wa michezo. Mwalimu Keneth Edson.

Kipindi hicho nilikuwa nina miaka 13 na nilikuwa darasa la tano. Mchezo wa mpira wa miguu kwetu tulicheza kama sehemu ya kujifurahisha. Faida pekee iliyoujaza moyo wangu katika mchezo huo ni SIFA.

Nilipokuwa nikisifiwa kwa umahiri nichezapo mchezo wa soka, ilitosha kabisa kuyafurahia maisha, hakukuwa na la ziada lenye thamani katika kipindi hicho cha utoto zaidi ya sifa kemkem nilizo mwagiwa niwapo uwanjani.

Sikuwa na matarajio yoyote kwenye mchezo wa soka. Sio kwa kutojua tija inayopatikana katika mchezo huo bali hata kuamini.

Nani angeniona huku kijijini Nyamakobiti? Kijijini. Makalioni mwa Tanzania. Kiongozi gani wa soka angesadiki, eti mimi nina kipaji zaidi ya vijana wa Dar es salam?

Fikra hizi zilinifanya nione na kuamini, ukomo wa soka langu ni pale nitakapomaliza shule. Kwa kuwa mchezo huo hakuwa kipaumbele changu maishani, nilikazana na masomo ili niweze kufauli kwenda sekondari. Mara chache sana nilipopata nafasi nililisakata kabumbu barabara.

kiasili mimi ni msukuma wa Bariadi, na ninatokea au niseme nilikuwa natoka katika familia ya wafugaji. Wazazi wangu walilowea mkoa wa mara wilaya ya Serengeti katika kijiji cha Nyamakobiti nje kidogo ya mji wa Maji moto.

Pamoja na kwamba baba yangu alisifika kwa utajiri wa idadi kuwa ya ng’ombe, lakini hatukuwa tunaishi maisha bora. Kwa kweli hatukutofautiana na watoto wa wakulima na masikini wengine pale kijijini!. Nitaeleza kwa nini nasema kauli hiyo.

Kwa milongo miwili iliyopita, watu wengi waliokuwa mashuhuri katika vijiji vya wafugaji, walijisikia fahari kusifiwa kwa utajiri wa idadi kubwa ya mifugo, hususasani Ng’ombe. Ilikuwa haijalishi makazi, mavazi na chakula unachokula.

Baba yangu alikuwa ni moja ya matajiri wa aina hiyo, pamoja na kuwa na idadi kubwa ya mifugo, lakini kula yetu na lala yetu ilikuwa ni duni mno, mavazi yangu yalikuwa yamechanika chanika na kujaa viraka
 
Sehemu ya 02

Robo tatu ya wanafunzi katika shule niliyokuwa nasoma, walikuwa hawana viatu, mimi nikiwa miongoni mwao. Nyumba yetu ilikuwa ya nyasi na makuti ambapo ukuta wake ulikandikwa kwa tope na kinyesi cha ng’ombe.

Tulizaliwa saba katika familia na mimi ndiye nilikuwa mtoto wa mwisho na wa kwanza wa kiume, ndugu zangu wote walikuwa wanawake ambao hadi nyakati hizo nikiwa na miaka 13 wengi wao walikwishaolewa.

Kwa kuzaliwa mtoto wa kiume, baba yangu alinitizama kama mrithi wake wa pekee. Elimu haikuwa kipaumbele chake, alinipeleka shule kama kutimiza wajibu tu. Wakati wote aliamini elimu sio kila kitu kwenye maisha ya binadamu.

Sambamba na hilo, suala la kucheza mpira, lilikuwa likimuudhi mno mzee wangu, wakati wote alinisihi niachane na michezo isiyokuwa na faida yoyote maishani mwangu. Kuliko kucheza mpira baba yangu alinisihi heri nichunge ng’ombe kuliko kupoteza muda uwanjani nikivuja jasho bila faida yoyote.

Niliendelea kuwa nacheza mpira kisiri siri na jina langu likiendeelea kupata umaarufu kwa kasi kubwa, miaka miwili badaye nilihitimu darasa la saba na kwa bahati mbaya sikuchaguliwa kujiunga na masomo ya sekondari. “Ajibu mwanangu.” Baba yangu aliiniita siku chache baada ya matokeo ya la saba kutoka.

“Nam baba.”
“Ni muda sahihi wa wewe kuwa na familia,”alisema hali akinitizama usoni. Akaendelea kuongea.

“Utalazimika kuoa mke, na sehemu ya mifugo mali zangu nikugawie urithi mapema tu.”
“Ndio kwanza nina miaka 15!!”
“Kwani hujabalehe?” baba aliuliza.

“Nimekwisha balehe”
“Kwa hiyo unajiona bado mtoto?”
Alihoji. Macho yake makali akiwa ameyatumbua usoni kwangu. Katika umri ule, niliogopa majukumu ya familia.
 
Sehemu ya 03

Kilikuwa ni kipindi cha mvua za alumino. Mvua kali za upepo zilikuwa zikinyesha na kusababisha mafuriko na maafa makubwa katika kila pembe ya nchi. Mazao mengi yalikwenda na maji, nchi ikaingia katika hali ya baa la njaa.

Ni katika Kipindi hicho ndipo nilipo oa.
Nakumbuka ilikuwa imepita miezi mitatu tangu nimwoe mwanamke mmoja jina lake aliitwa Pili Maendeka. Alikuwa ni mwanamke ambaye labda naweza kusema alikuwa mrembo kwenye macho ya mwanaume mwingine, Ila Kwangu kuna kitu kilipungua.

Alikuwa binti mweusi, mrefu, amejazia kwa nyuma, uso wake mpana na macho makubwa ya kurembua yangeweza kumzuzua rijali yeyote mkware.

Pili alikuwa na nywele nyingi na nyeusi tii. Kifua chake kilibeba matiti yenye ukubwa kama embe dodo. Miguu ya bia na kiuno chembamba kama kinu. Kilihitimisha mwonekano halisi wa mwanamke wa kibantu.

Pamoja na sifa hizo, moyo wangu hakuwa kwakwe! Sikuwa na hisia na mwanadada huyo. Kuna kitu ambacho Pili alikosa, ambacho mimi ndio huwa ugonjwa wangu mkubwa.

Rangi!.
Moyo wangu unahusudu mno wanawake weupe, katika umri ule wa miaka 15 niliyokuwa nayo. Japo sikuwahi kujihusisha kimapenzi na mwanamke yeyote lakini nilikuwa sijiwezi mbele ya mabinti weupe niliosoma nao.

Kitendo cha kuozeshwa Pili Maendeka, mwanamke mwenye sifa za kibantu, kilififiza mapenzi yangu kwakwe. Ningefanya nini? ndio baba alikwisha nichagulia mwanamke huyo.

Ushamba katika mambo ya kiutu uzima, sambamba na kutokuwa na hisia na mwanamke yule, nakumbuka tulikaa karibu wiki nzima tangu tuoane bila kushiriki tendo la ndoa. Mwili wangu ulikuwa wa baridi hata aliponikumbatia. Kwa kuogopa aibu kijijini, nikajitahidi tahidi kuweka hisia hatimaye siku ya nane, nikafanya naye tendo la ndoa.

Rasimi nikaayanza maisha ya ndoa mimi na mke wangu nikiwa na umri wa miaka 15 tu. Mke wangu alikuwa mtu mpole na mchapakazi. Pamoja na ukweli kwamba nilikuwa naishi na mke nisiyempenda, hata hivyo ktika maisha ya ndoa, nilivutiwa na kitu kimoja tu. Kitu ambacho nilikikosa kipindi niko chini ya wazazi.
Uhuru.
20190907_191717.jpg
 
Sehemu ya 04

Nilikuwa nina uhuru mkubwa wa kufanya mambo yangu binafsi ukilinganisha na kipindi cha nyuma.

Hali ile niliipenda sana, katika hali isiyotarajiwa nikajikuta narudi kwenye mchezo wa soka.

Mchezo niliokuwa nikiuuhusudu mno. Kila siku baada ya kazi za mchana kutwa, vijana wengi tulikutana kwenye kiwanja cha kijiji na kulisakata kabumbu.

Kwa uwezo wangu mkubwa wa soka, nikajikuta naingia moja kwa moja kwenye timu ya kijiji, nilikuwa ndiye mchezaji mwenye umri mdogo kuliko yeyote yule.

Wachezaji wengi wa timu ya kijiji umri wao ulianzia miaka 30 na kuendelea. Ilikuwa ni mibaba iliyoshiba.
Baba yangu hakuweza tena kunizua, wala kunipangia jambo lolote, nilikuwa mtu mzima sasa.

Siku moja, timu inayoshiriki ligi daraja la pili itwayo ‘Home Boys’ ya wilayani Bunda, walikuwa katika ‘tour’ ya maandalizi ya msimu mpya wa ligi, walikuja kijijini kwetu kufanya utalii.

Hapa kuna kitu nimesahau kukielezea, katika kijiji chetu kulikuwa na kivutio kimoja kikubwa, ambacho watu wengi ulimwenguni walikuwa wakija kwa ajili ya kufanya utalii. Kulikuwa na chemichemi itoayo maji ya moto miaka yote.

Chemi chemi hiyo huwa haikauki, na ndiyo iliyobeba jina la kijiji chetu yanii kijiji cha maji moto. Kwa kweli huwa ni kivutio kikubwa kwa wageni wa ndani na nje ya nchi.

Timu ya Home Boys ilipofika kijijini kwetu walikaa kwa siku tatu, wakiwa pale wakaomba mechi ya kirafiki na timu yetu ya kijiji. “Timu kutoka mjini iitwayo ‘Home Boys ipo hapa kijijini...” jioni moja baada ya mazoezi mwalimu kuu wa shule ya Maji moto ambaye ndiye alikuwa kama kocha wa timu yetu ya kijiji alituambia.
 
Sehemu ya 05

“Wameomba mechi ya kirafiki na timu yetu kabla ya kurudi Bunda, hii ni fahari kwetu kucheza na timu kama Home Boys,” alisema.

Kimoyomoyo nikaona hii ndio fursa na daraja la kwanza la kunitoa kisoka. Nikashangilia moyoni.

“Mchezo utakuwa lini kocha?” niliuliza “Swali zuri...” alisema kisha akaendelea.
“Jamaa wamependekeza mchezo uwe jumapili ya wiki hii. Binafsi nimekubaliana nao maana siku hiyo watu wengi wanakuwa katika mapumziko...

Tumeelewana?”
“Ndiooo!” wachezaji wote tukaitikia kwa pamoja.
Nilirudi nyumbani nikiwa na matarajio makubwa sana maishani. Angalau katika nyakati zile za ujana, nilikwisha tambua tija inayopatikana kwenye mchezo wa soka.

**** Nilipofika nyumbani nikamkuta mke wangu Pili akiwa amekamata shoka anakata kata kuni za kupikia. Ilikuwa ni jioni, na muda wa kutayarisha chakula ulikuwa ndio umewadia.
Nuru ya jua la jioni ilikuwa inaishilizia na giza kuchukua hatamu.

Nilisimama katika kona ya ukuta ambapo mke wangu Pili hakuniona. Nikawa namwangalia kiumbe yule namna anavyo nyanyua shoka hewani na kulishusha katika kipande cha gogo.

Tendo lile likawa linamfanya atikisike. Nikawa naangalia wowo lake na kifua chake kilichobeba embe dodo vikiwa vinatikisika katika namna ya kuvutia.

Labda angekuwa mwanaume mwingine anayependa sampuli ya wanawake wa vile, angefaidi sana. Bahati mbaya mwanamke yule alikosa sifa igusayo moyo wangu, kama ambavyo nimekwisha eleza hapo nyuma.

Msichana yule ni kama tulikuwa tunalingana kiumri, unaweza pia kusema, sote tulikuwa tumeingizwa katika ndoa za utotoni. Angalau yeye alikuwa na umbo kubwa ambalo hata angesema anamiaka 18 usingekataliwa.

Mimi nilikuwa na kamwili kadogo dogo, tungesimama pamoja ungedhani ni mtu na mama yake mdogo. Kwa upande wake, binti yule alinipenda sana, japokuwa alikuwa ni msichana mdogo, ila alinionesha mahaba makubwa aliyofunzwa unyagoni.

Jambo hilo lilinifanya nimwonyeshe tabasamu bandia. Isingekuwa ungwana kutomwonyesha kicheko na tabasamu ilihali yeye alinipa mahaba na upendo mkubwa.

Siri ya kutompenda ilibaki moyoni mwangu. Sikuwa na matarajio naye yoyote. Niliamini siku moja nitakuwa na familia niitakayo. Naye ningemwacha tu.
 
Sehemu ya 06

Nikiwa nimesimama pale gizani, mambo mengi niliyafikiria harakaharaka. Miongoni mwa mengi yaliyopita kichwani, kubwa ni lile la kumtoroka.

Nilijisema moyoni: Endapo timu ya Home boys ikinihitaji, lazima ningemwacha tu.

Kamwe nisingekuwa tayari kuongozana na Pili mjini, kwa kuwa nitakuwa nakwenda kuanza maisha mapya. Vilevile familia yangu, hususani baba yangu, asingekuwa tayari kuona naiacha familia yangu eti kisa nakwenda kucheza soka Bunda.

Nikiwa pale gizani nafsi yangu ikajaribu kupima mambo: Kati ya familia na soka kipi kimeujaza moyo wangu!. jibu lilikuja haraka haraka. Nilikuwa nalipenda soka kuliko Pili.

Sauti moja kichwani ikanihoji: “Huoni kama Pili anaweza kuwa kikwazo kwa soka lako?” Kwa mara nyingine nikajikuta nachukia ile ndoa yangu, nikajikuta namchukia Pili kwa kumwona kama kikwazo kikubwa kwenye harakati zangu.
“Au nimuue ili niwe huru?” Nilinong’ona taratibu. Nilikuwa nimefika mbali sana. Kwa umri wangu nilikuwa nimefikiria jambo kubwa na baya mno kisa soka.

NILIZIFUTILIA mbali fikra za kumzuru mke wangu kisa mpira, hasa ukizingatia hata nafasi ya kusajiliwa na timu ya Home Boys kutoka mjini nilikuwa sijapata!. Kadhalika, halikuwa hilo tu, hata mchezo wa kirafiki ambao ndio nilitegemea nionekane ulikuwa haujachezwa.

Nilijitokeza pale gizani nilipokuwa nimejibanza na kusimama mbele ya mke wangu.

“Wajionaje mume wangu,” mke wangu Pili alinilaki baada ya kujitokeza mbele yake.
Uso wake ulionesha mapenzi makubwa kwangu, nilirejesha tabasamu bandia, akanipokea viatu vyangu vya mpira na kupeleka ndani.

“Ukitoka nje, njoo na redio yangu ndogo” nilimwagiza.
“Ondoa shaka Ajibu.”
Aliniitikia kwa utii na adabu, kama nilivyosema awali, mke wangu alikuwa ni mwanamke mwenye heshima kubwa kwangu.

Alirejea na redio yangu ndogo, kisha akaendelea na maandalizi ya chakula cha usiku. Huwa ni ratiba yangu ya kila siku jioni kufuatilia vipindi vya michezo. Nilipenda sana kusoma na kusikiliza habari za michezo hasa mchezo wa soka katika redio na magazeti.

Kila niliposikia habari mbalimbali za wachezaji mashuhuri wa mpira hapa nchini, nilishikwa misisimko ya ajabu sana. Kuna wakati nilikuwa nikijiona kama mimi ndio wao,
 
Sehemu ya 07

ikawa naishi katika dunia ya umaarufu kwa hisia tu.
Tamaa yangu ilikuwa ni siku moja na mimi niwe miongoni mwa wachezaji mashuhuri wa mpira wa miguu. Ambaye nitapamba vichwa vya habari kwenye magazeti na redio.

Nilikuwa ni binadamu ninayehusudu mno umaarufu, hulka na ushamba wa kupenda sifa ulifunika utashi wangu.
Giza lilikuwa limekwisha ingia. Mke wangu naye alikwisha maliza kupika, akanifuata:
“Mume wangu utakwenda kuoga ama utakula kwanza.”
“Nitaoga kwanza.”

Akanikaribisha kwa kunipigia magoti. Baada ya kuuoga, nikarudi mezani kwenye chakula. Dakika chache tu nikazitumia kukishambulia chakula kile kitamu alichopika Pili, mke wangu.
Masaa mawili badaye nilikuwa kitandani mke wangu Pili akiwa upande wa pili:
“Ajibu...” aliniita kwa sauti itakeayo puani, mikono yake alikuwa anapapasa kifua changu.

Kwa dalili tu, nilitambua ni kitu gani mke wangu alikuwa akitaka. Penzi. Ita yake ilikuwa ya mahaba. Alikuwa mtupu. Mkono wake ulikuwa ukipapasa kifua changu. Joto la mwili wake liliingia kwenye ngozi yangu. Matiti yake yaliyo wima, ncha ya chuchu zilinichoma ubavuni.

Nilionekana kama ananihitaji kimwili. Tulikuwa tuna kama wiki mbili au tatu hatuja ‘duu’ pamoja na yote lakini hisia zangu kwa kiumbe yule zilikuwa maili nyingi sana. Nilifaya naye tu kwakuwa alinisisimua kwa muda mfupi, lakini sikuwa na na japo chembe ya upendo moyoni mwangu.

“Nimechoka Pili, leo tulikuwa na mazoezi makali mwili wote nahisi kama umepondwa pondwa,” nilimjibu huku nikigeukia upande wa pili, sikuwa na hamu ya kufanya mapenzi na binti yule mweusi mwenye wowo kubwa.

“Hutaki tuzungumze mume wangu?” akaniuliza kwa sauti ya upole.
“Unataka tufanye mapenzi? Au unataka mazungumzo ya kawaida.” Nilihoji kwa ukali.

Kauli hiyo ni haikuwa nzuri kwa mke wangu. Nilimsikia akivuta pumzi na kuzitoa kwa mkupuo, akapiga kimya kidogo kisha akaniambia:

“Nina mimba Ajibu.” Nilishtuka.Ilikuwa ni shambulio la ghafla. Sikutegemea kabisa kusikia taarifa ya namna ile. Nikagueka upande wake na kumtizama usoni mrembo yule.
“Mimba ya nani?” nikauliza swali la kipumbavu.

“Swali gani hilo unauliza?”
“Ina miezi mingapi?” badala ya kujibu nikapandisha swali jingine.
“Miezi mitatu kasoro.”
 
Sehemu ya 08

Ukimya mfupi ukapita kati yetu, kisha nikamwambia:
“Kwa nini ulishika mimba bila kunishirikisha?”

“Wewe ni mume wangu halali. Ni lini nawe umekaa nami ukazungumza kuhusu mapenzi yetu?”
“Ndio ukaaona ujichukulie maamuzi peke yako?”
“Hapana.”
“Kumbe?”

“Imetokea tu bila mwenyewe kutarajia.” Mke wangu, Pili, alisema. Uso wake ulionesha wasiwasi mkubwa.
Ukimya mwingine ukapita tena baina yetu, kisha nikamwambia:

“Hongera....Hongera sana mke wangu?” Nilimwonesha tabasamu bandia. Ukweli ulibaki moyoni mwangu. Sikufurahishwa na jambo lile hata kidogo.

Niliamini hali ile inaweza kuwa moja ya kizuizi cha harakati zangu za soka.

ningetakiwa kuwa karibu na familia kwa namna yoyote ile. Niliamini ili niweze kuzifikia ndoto zangu kwa urahisi ni kujitenga na familia yangu.
Sasa mimba hii vipi tena? Nilikosa amani, sikuwa na furaha hata kidogo.

*****
ILIKUWA ni jumamosi tulivu. Anga lilikuwa na ubuluu wake. Hakukua na dalili zozote za mvua kama ilivyokuwa kawaida. Ni aghalabu katika kipindi kile cha mwezi wa nne, mvua kutonyesha nyakati za jioni.

Angalau siku hiyo hali ilikuwa shwari. Watu walikuwa wamefurika katika kiwanja cha mpira cha shule ya msingi.
Siku ya mechi ya kirafiki kati ya timu yetu ya kijiji na timu ya Home Boys kutoka Bunda ilikuwa imewadia.

Tulipokuwa uwanjani tukiwafanya mazoezi madogo madogo kabla ya mchezo, tofauti kubwa ya timu yetu na timu ya Home boys ilionekana.

Kwanza, sisi jezi zetu zilichakaa, kuanzia nguo hadi viatu. Pili, timu ya Home boys walikuwa ni vijana wenye umri mdogo ambao kwa kiasi fulani walionekana kuwa wa rika langu, huku sisi tukijaza mibaba.

Kimwonekano wachezaji wa Home boys walikuwa ni vijana wa mjini waliokwenda na wakati. Ukiachilia mbali jezi zao nzuri nyeupe zilizo nakshiwa na mistari myekundu, wachezaji hao baadhi yao walikuwa katika mitindo ya nywele ya vijana wa kileo.

Wengine walijichora ‘tatoo’ miliini mwao. Ongea yao ilikuwa nzuri, hata mazoezi yao yalikuwa ya ya kuvutia. Kwa kweli niliwaonea wivu wale jamaa. Baada ya itifaki za kimpira kuzingatiwa, refa aliweka mpira kati tayari kwa kuanza.
 
Sehemu ya 09

Mwili ulinisisimka, niliamini huo ndio wakati wa kuonyesha vitu vyangu na kusajiliwa na timu ile. Sikutaka kabisa kuendelea kuishi kijijini baada ya mchezo ule.

Mpira ulianza. Kwa kasi, jamaa walikuwa na kipaji asikwambie mtu, kwa dakika mbili nzima, walikuwa wakipigiana pasi kwa umahiri mkubwa. Walinonekana ni wachezaji wanaoelewa kile wanachofundishwa.

Kila kitu ambacho jamaa walikuwa wanafanya kilikuwa cha ajabu kwetu, hata mashabiki wetu walianza kuwashangilia. Tulikuwa tunakimbia huku na kule kuusaka mpira kama wendawazimu.

Mimi, ambaye nilikuwa nacheza nafasi ya mbele, kama mshambuliaji wa mwisho, kwa dakika za mwanzoni nilikosa kabisa mtu wa kunilisha mipira kama tukicheza na timu nyingine za vijijini. Jamaa walituzidi kila kitu.

Mpira mmoja ulipigwa, kwa bahati ukambabatiza, mchezaji wetu mmoja, tukacheza pasi mbili, tatu kisha tukapiga shambulizi la ghafla (Counter attack)
Nikakimbia kwa kasi , kuufuata mpira.

Bahati nzuri nilimzidi kasi beki wa pembeni wa Home Boys. Niliumiliki mpira miguuni mwangu, alitokeza beki wa kati ambaye alikuja kwa nia ya kunifanyia madhambi nje ya 18

Kwa weledi mkubwa, nilichota mpira, nikampiga kanzu, jamaa akapitiliza kama mwendawazimu. Uwanja ukalipuka. Wakati anarudi kusahihisha makosa, alikwisha chelewa. tayari nilikuwa namwangalia kipa wao.

Mlinda mlango alikuja kwa kasi ili ikiwezekana aubabatize mpira na kukoa hatari langoni kwake, lakini kwa kuwa nilikwisha mwangalia anavyokuja, na namna alivyokaa, nikausukuma mpira katikati ya miguu yake, nikawa nimempiga tobo moja ya dharau. Mpira ukajaa wavuni. Tukaandika bao la kwanza.
Uwanja ulilipuka.

Watoto wale wa mjini wakabaki wameshika vichwa, hawamini kilichotokea. Nilishangilia bao langu kwa mambo mawili, kwanza kabisa kwa kuonesha kiwango bora kabisa mbele ya viongozi wa timu ya Home boys. Jambo la pili ni kuifungia timu yangu bao.

Mpira uliwekwa kati, timu ya Home Boys wakaanza tena. Nilikuwa katika hali kubwa ya kujiamni, kama kawaida, jamaa walipiga pasi nyingi kama Barcelona.

Tulipigwa chenga na kanzu za maudhi. Bahati nzuri mabeki wa timu yetu walikuwa makini na nguvu kubwa.
 
Sehemu ya 10

Mipira yote iliyopigwa na timu pinzani iliishia miguuni mwa mabeki wetu au mikononi mwa kipa. Kwa kweli japo jamaa walikuwa wanatuzidi kila kitu ila timu yetu ya kijiji tulicheza kwa nidhamu kubwa.

Kila tulipokuwa nao sisi mpira, hatukuweza kuumiliki japo kwa sekunde 10 tu, ila angalau kila tulipoupata Mpira tulitengeneza nafasi za mabao japokuwa mashuti mengi yaliishia kugonga nguzo ya goli mengine kuokelewa.

Kipindi cha kwanza kilimalizika, kila timu ikaenda kupata maelekezo ya kiufundi kwa makocha.

Tuliporudi uwanjani jamaa waliwatoa wachezaji wao wote. Kumbe wale walioanza kipindi cha kwanza ilikuwa ni timu yao namba mbili.

Moyoni nikasema sasa wale wachezaji walikuwa timu namba mbili wametusumbua vile. Je hii ya kikosi cha kwanza si tutautafuta mpira kwa tochi?.

Mpenzi msomaji, baada ya refa kupuliza kipenga cha kipindi cha pili, jamaa wale walicheza mpira wa kiwango ambacho sijawahi kukutana nacho. Ndani ya dakika tatu tu tangu mpira uanze wakapata bao la kusawazisha.

Dakika tano zingine tukapigwa bao la pili. Dakika nne tena, tukapigwa bao la tatu. Ilikuwa ni mvua ya magoli. Jamaa wakawa wanacheza kwa kupigiana pasi na kumiliki mpira kwa weledi mkubwa.

Dakika tano kabla ya mpira kuisha tukapigwa goli la tano, mpira ukawekwa kati, tukaanzisha sisi, tukapigiana pasi mbili tatu kisha ikapigwa ndefu kwangu.

Nikakimbiza. akaja beki mmoja kwa kasi lakini akiwa na tahadhari kubwa ya kuadhirika kwani walikwisha nijua, aliponifikia nikamdeshi kama napita, ile anakuja tu, nikampiga chenga moja ya maudhi. Uwanja ukalipuka.

Akaja beki mwingine. Naye nikamkimbiza kwa nguvu, akanifuata kwa kasi lengo lake acheze ‘tackling’ lakini ile anafika tu, nikamfinya kwa nyuma jamaa akapitiliza na kufyatua hewa.
Uwanja ukalipuka tena.

Wakati huo kipa aliyeingia kipindi cha pili, alionekan ni mwenye utulivu kuliko yule wa mwanzo. Akiwa katika namna ya kuokoa shambuilizi, nilichofanya ni kupiga mpira kwa kasi ndogo lakini kiufundi.

Mpira uliambaa na kuingia kupitia katika ukingo wa goli, yule kipa aliruka lakini hakuweza, nikaandika bao la pili kwa timu yetu. Matokeo yakawa, wao tano sisi mbili.
Watu huko nje walipagawa.
 
Sehemu ya 11

Nilikuwa naonyesha kiwango ambacho sijawahi kukionyesha hata siku moja pale kijijini.

Mpira ukawekwa kati na kuanza tena. Hata hivyo, hadi refa anapuliza kipyenga cha mwisho tulifungwa bao sita kwa mbili.
Niliamini kwa kiwango nilicho kionesha, bila kujali kufungwa kwa timu yetu, lazima wale jamaa wangenitafuta na kuzungumza na mimi.

Ajabu ni kwamba, baada ya mchezo kumalizika hapakuwa na hata mmoja wapo aliyeniuliza jina langu naitwa nani. Wale jamaa walionesha kutobabaishwa na kiwango changu baada ya mchezo.

Walirudi katika lodge waliokuwa wamefikia bila hata kuniuliza jina langu naitwa nani.

Nilirudi nyumbani nikiamini inawezekana watazungumza na mwalimu Keneth ambaye alikuwa kocha wetu na mwenyeji wao pale kijijini.

Siku ya pili baada ya mchezo ule, nilipata taarifa zilizovunja moyo wangu. Nilitamani iwe ndoto. Zilikuwa ni taarifa mbaya. Niliambiwa eti ile timu ilikuwa imeondoka kijijini na kurudi kwao Bunda. Bila kuzungumza na mimi!!!!.
Niliumia sana. Nilikata tamaa.

KWA mara ya kwanza katika siku za ujana wangu, nikabubujikwa na machozi kwa kuililia timu kutoka mjini, Home boys. Nilikuwa ni mvulana mwenye matarajio makubwa mno dhidi ya klabu ile.

Niliamini timu hiyo ingekuwa ni daraja la kunivusha katika safari ya ndoto yangu. Lakini kila kitu kilikuwa kimepeperuka kama tiara. Jamaa hawakuwa wameona chochote miguuni mwangu.

“Mbona unalia?” mwalimu Keneth alinihoji baada ya kuona machozi yamejikusanya machoni mwangu. “Nilidhani wangenichukua...” niliongea kwa uchungu sana, sikuweza kutamka maneno mengine zaidi ya hayo.

Machozi yaliyokuwa yamejikusanya machoni mwangu yalinifanya nione ukungu na uvulivuli, nikazifumba kope za macho, ikawa kama nimeyakamua machozi, yakanitiririka hadi mashavuni mwangu.
 
Sehemu ya 12

Kwa kweli sikupenda mwalimu Keneth aione huzuni yangu, hata hivyo bahati mbaya, nilishindwa kabisa kuificha.

Uso wa mwalimu Keneth ulisawijika kwa mshangao, kwanza baada ya kusikia natamka maneno yale, pili kububujikwa na machozi. Hakutegema kama ningeweza kuwa katika hali ile kwa sababu ya soka. “Una uhakika ni hilo ndilo linakufanya uwe hivyo?”

Sikujibu swali lake, nilichofanya ni kuanza kutembea kuondoka nyumbani kwakwe. Nilielewa Swali lake lilibeba mantiki ya kuona nalizwa kwa jambo la kitoto. “Hebu ngoja kwanzaa, subiri kwanza Ajibu...” alinizuia nisiondoke. Akanimbia:

“Ajibu, najua uwezo wako katika mchezo wa mpira wa miguu, ila sikudhani kama ulikuwa na matarajio fulani kwenye mchezo huu.”

“Ninazo ndoto kubwa mwalimu.” Nilimjibu.
“Mbona hukuwahi kunieleza? usingekuwa hapa kijijini Ajibu.” Kauli yake ilionyesha nimechelewa, sikupenda kukubali hilo kirahisi, nikawambia:

“Nisaidie mwalimu Keneth, nisaidie tafadhali, nahitaji niwe mchezaji wa kulipwa, sitaki tena kuishi hapa kijijini.”
“Una uhakika ajibu?” “Kabisa.” Mwalimu Keneth aliniangalia kwa dakika nzima, ni kama vile alikuwa akisoma kitu fulani machoni mwangu. Akaniuliza.

“Una mke?” Swali hilo halikunivutia, nilijua kivyovyote kitendo cha kuwa na mke ingeweza kuwa kikwazo kwa namna moja ama nyingine. “Ndio, nina mke.” Nilimjibu kinyonge.

“Hilo linaweza kuwa tatizo.”
“Kivipi mwalimu?”
“Kama nilivyo kwambia huwezi kutoka kisoka ukiwa huku kijijini, kijiji ambacho watu wake hawajapevuka kiutashi, lazima usogee katika mazingira ambayo yanaweza kukuvusha na kwenda unapopataka.

Nikiamua ‘kukuconect’ na jamaa zangu waliopo huko Mwanza utaishije na mkeo hasa ukizingatia huko utakuwa mgeni? Au utamwacha mkeo hapa kijijini?”
“Ndio nitamwacha...Atabakia hapa kijijini.” Niliitikia harakaharaka, nilikuwa na shauku kubwa juu ya fursa ambayo mwalimu Keneth angenipa.

Baada ya jibu langu, mwalimu alinitizama tena usoni kwa macho yake madogo lakini makali kama ya paka. Alikuwa ni mwalimu mpole lakini mkali sana pale anapochukizwa.
 
Sehemu ya 13

Wakati nasoma, wanafunzi walimpachika jina la utani, walimwita ‘chui’ Aliogopwa na wanafunzi wengi watukutu. Wachache tuliokuwa marafiki zake, hatukuwa na tatizo naye kabisa.

Hii ilitokana na mambo mawili. Kwanza tulikuwa tukitii maelekezo yake yote aliyoyataka. Pili alikuwa ni mwalimu, rafiki yangu kwa kuwa mara nyingi tulikutana naye uwanjani katika michezo mbalimbali hasa soka.

“Sikiliza mwanangu...”alisema huku akinishika bega, macho yake kama ya paka yakiwa bado usoni mwangu.
“Nakupa muda utafakari juu ya hatima ya familia yako, kisha njoo baada ya siku mbili.”

Maneno ya mwalimu Keneth sio tu yalinifurahisha lakini pia, yalinipa tumaini jipya. Nilirudi nyumbani kwa ajili ya kutafakari juu ya fursa ambayo mwalimu Keneth alitaka kunipa.

Kama kawaida nilimkuta mke wangu anaendelea na shughuli za nyumbani. Nilimwita chumbani kwa ajili ya kuzungumza naye. “Kuna mambo ambayo unatakiwa uyatambue mke wangu.” nilianza kuzungumza. “Nahitaji kwenda mjini kwa muda kidogo.”

“Kuna nini Ajibu?”
“Nimepata timu huko. Nimesajiliwa.” Nilimdanganya.

Sikutaka kumwambia kwamba ndio nakwenda kutafuta timu, niliamini lazima angenitia uchuro kwenye wazo langu lile.
Hata hivyo, pamoja na hilo, uso wa mke wangu, Pili ulionekana kusawijika kwa wasiwasi. Akaniuliza:

“Ni timu gani na mjini wapi huko Ajibu?” swali hili lilikuwa gumu, kwani hapakuwa na ukweli wowote katika maelezo ya awali niliyompa. Hivyo inabidi niuendeleze uongo wangu.
“Ni mwanza, timu inaitwa....inaitwa, Home Boys”

“Mwanza!! Home boys!!.. Mbona uliniambia hiyo timu maskani yake ni Bunda?” Nilikuwa nimejichanganya vibaya sana, kila mtu kijijini aliitambua timu ya Home Boys ilitokea Bunda, kitendo cha kumwambia mke wangu nilitaka kwenda Mwanza badala ya Bunda kucheza katika timu ya Home Boys ulikuwa ni uongo wa kitoto sana.

“Nimeghafilika tu, ni Bunda mke wangu. Nakwenda Bunda katika timu ya Home boys ” nilisahihisha uongo wangu.
Pili aliniangalia kwa macho yenye mashaka na wasiwasi, akaniuliza tena.
“Kwa hiyo?”

“Itabidi nitangulie kutengeneza mazingira, kisha nitakuijia kabla ya hujajifungua mtoto wetu.”
 
Sehemu ya 14

Alinisogelea akanikumbatia kisha akaning’oneza:
“Mume wangu Ajibu, nakuomba usije nisahau mimi na mwanangu aliyetumboni, wewe ndiye dereva wa maisha yetu, nakuamini mume wangu mpenzi.” Maneno yake yaliniingia akilini. Pamoja na ukweli kwamba nilikuwa sina mapenzi ya dhati kwakwe.

“Usijali mke wangu, kila kitu kitakwenda sawa, siwezi kuwaacha, ila jambo moja naomba uniahidi?” “Lipi?”
“Hili suala liwe siri kati yangu na wewe?”
“Itawezekanaje ajibu na kwa nini iwe siri?”

“Baba hawezi kukubali nikacheze mpira mjini Pili, nawe unajua matamanio yangu ni siku moja kuwa mchezaji mkubwa, hata wewe unatamani siku moja tukaishi pamoja miji kama Dar, Mwanza, au sivyo?”

“Ndivyo Ajibu. Lakini lazima nitaandamwa na maswali mume wangu.”
“Utasema pale itakapobidi ila iwe siri yako?”

“Nimekuelewa mume wangu.” mke wangu, Pili, alijibu, ilikuwa rahisi kumshawishi mke wangu, kwa upendo mkubwa aliokuwa nao asingekuwa na ubavu wa kuniletea ukinzani kwa jambo nisilolitaka.

Kadhalika, sikuwa na wasiwasi na maisha ya mke wangu Pili baada tu ya kuondoka na kutokomea mjini. Nilikuwa nina ng’ombe wa kutosha ambao baba yangu alinigawia nilipo oa.
Biashara ya kuuza maziwa.

Niliamini ingeweza kuendesha maisha ya mwanamke yule kwa muda mrefu sana.
Siku mbili badaye, nilirudi kwa mwalimu Keneth na kumweleza kila kitu nilichozungumza na mke wangu, kitu pekee ambacho sikumwambia ni juu ya uongo niliomweleza Pili, kuwa nimekwisha sajiliwa na timu ya Home Boys ya mjini Bunda.

“Kwa hiyo uko tayari kwenda mjini?”
“Ndio.” Nilimjibu. Nilitamani nijue mjini alikokuengelea ni mjini ipi ya mkoa gani. Naye kama vile alijua shauku yangu, akaniambia:

“Kuna timu ipo Mwanza mjini inashiriki ligi daraja la nne nimekutafutia nafasi huko, naamini kwa uwezo wako hutodumu japo kwa nusu msimu tu utakuwa ushapata timu nyingine kubwa.”
“Inaitwaje?” nikamuliza kwa kiherehere.
“Igogo FC.”

“Kwa hiyo mipango ikoje mwalimu?” “Ukitaka kuondoka hata leo ni wewe tu. Alisema, akaniangalia usoni kwa yale macho yake makali, kisha akaendelea.
Nimekwisha wasiliana Gideon Nkisi, huyu ni kocha wa timu hiyo, ambaye pia ni rafiki yangu mkubwa, amesema atakupokea kilabuni.”
 
Sehemu ya 15

Nilifurahi sana, sikuwa na cha kumlipa mwalimu Keneth, alikuwa amenisapoti kwa kiwango kikubwa mno. Angalau njia ya kuelekea kwenye safari ya matumaini niliiona.

Alinipa mwongozo namna nitakavyoweza kumpata Gideon Nkisi pale nitakapofika jijini Mwanza. Nilirudi nyumbani ili kuweka sawa mazingira ya safari ya Mwanza. *****

Alfajiri na mapema ya siku ya pili, nilikuwa stendi nikiagana na mke wangu, nilimwahidi nisingekawia kurudi kumchukua, nilimdanganya wakati wote wa maisha yangu nitapambana nikijua nina watu wawili wanaonitegea. Yeye na mwanangu.

Maneno yangu yalimfariji mke wangu, Pili, akaniombea dua. Akanishika kiganja cha mkono wangu akaking’angania kwa nguvu, halafu akaninong’oneza.

“Nakupenda Ajibu” “hata mimi”nilimjibu, ingawa moyo wangu ulikuwa mtupu kwakwe. Akaniachia mkono wangu.
Uso wake ulijaa upendo mkubwa juu yangu. “Kwa heri mpenzi.”

“Kwa heri.”
Nilijitoma katika gari, halikuwa basi, lilikuwa gari aina ya Pajero, toleo la zamani lililochoka. ndani, lilijaa vumbi, vyuma vilionekana kuwa vilishachomelewa kwa idadi isiyo hesabika.

Viti vyake vilikuwa chakavu. Vitambaa vilivyofunika viti vilichanika na kuacha sehemu ya kuegemea zikiwa wazi. Mvunguni mwa kila kiti kulikuwa na gogo ambalo lilishikilia kiti. Baadhi ya sehemu viti viling’oka pakawekwa vigoda vya mbao.

Msafiri kafiri, sikuwa na chaguo. Ulipofika muda wa kuondoka, gari liling’oa nanga baada ya wanaume kadhaa kulisukuma. Wakati wa kuliwasha lilitoa moshi mzito mweusi. Lilitoa kelele ya mkwaruzo iliyokuwa kero masikioni.

Vyuma vilisikika kulalamika kwa kugonganagongana. Potelea mbali, nilikuwa nikitaka gari linifikishe Musoma kisha Mwanza maana uzuri wa gari si fahari ya msafiri.

Gari lilipokuwa likichanja mbuga, liliegama kushoto marakulia. Wakati fulani lilikwenda juu na kutua kwenye makorongo likiacha vumbi kwa nyuma.
Tuliingia Musoma saa sita mchana, ilikuwa ni mara yangu ya kwanza katika maisha kufika mjini. Nilivutiwa na kila kitu nilichokiona.

Nilipanda basi jingine liitwalo Mombasa Raha, Hili lilikuwa ni basi zuri mno ambalo liliendana na dunia ya sasa. Safari ya Mwanza ikaendelea.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom