Simulizi: Scaila Michael

Shunie

JF-Expert Member
Aug 14, 2016
152,886
453,430
Mtunzi Nyemo Chilongani

Sehemu ya 01.

Nilikuwa chumbani kwangu, kichwa changu kilikuwa na mawazo tele. Akili yangu ilichanganyikiwa, kulikuwa na mambo mengi ambayo yalinichanganya kipindi hicho, ila kubwa zaidi ni kuhusu msichana niliyekuwa nikimpenda kwa moyo wangu wote, Shasta Karina.

Naweza kusema kwamba miongoni mwa wasichana ambao nilikuwa nao katika maisha yangu, huyu nilimpenda mno. Alikuwa msichana mrembo ambaye ninaweza kusema alistahili kuwa mke wangu wa ndoa, nimuoe na hatimaye tujenge familia pamoja.

Nilikutana na Shasta miaka miwili iliyopita maeneo ya Victoria, Mikocheni kaika Mgahawa wa KFC. Siku hiyo nilikuwa nikitoka kumtembelea rafiki yangu aliyekuwa akiishi Msasani.

Nakumbuka nilipofika maeneo hayo, nilipaki gari langu na kwenda kwenye mgahawa huo uliokuwa mahali hapo, nikaingia na kukaa kwenye meza moja.

Nilikuwa kimya mno, sikutaka kuwa na presha yoyote ile, humo ndani macho yangu yalikuwa yakiangalia huku na kule kama nilikuwa namtafuta mtu fulani hivi, macho yangu yakatua kwa mhudumu mmoja, aliyevalia nguo zake safi, harakaharaka akaja pale nilipokuwa.

“Karibu!” aliniambia kwa sauti nyembamba, na kwa jinsi alivyokuwa mzuri, nilihisi kama nikipata hali fulani moyoni.

“Ahsante sana!” niliitikia na kumkazia macho, sikutaka kuyatoa kutoka usoni mwake.

Nilibaki nikimwangalia kwa sekunde kadhaa, alikuwa akiangalia pembeni huku akionekana kusikia aibu kupita kawaida. “Karibu!” alinikaribisha tena, akasindikiza na tabasamu fulani pana.

“Nashukuru sana! Ninahitaji chakula kizuri kama ulivyo,” nilimwambia kiutani huku macho yangu yakiendelea kubaki usoni mwake.

“Oh!”
“Ndiyo! Chipsi combo!” nilimwambia.
Msichana huyo akaondoka, nilibaki nikimwangalia, alionekana kuwa miongoni mwa wasichana warembo mno ambao niliwahi kukutana nao katika maisha yangu.

Kipindi hicho nilikuwa singo, niliachana na msichana aliyeitwa kwa jina la Evelyne kwa sababu tu hakuwa na sifa za kuwa mwanamke wa kuishi naye.

Ninapomfuata msichana kuna vitu vingi ninaviangalia, cha kwanza ni uwezo wa akili yake, je, nikiwa naye anaweza kulea watoto wangu kwa staili ninayoitaka?
20190607_134612.jpg
 
Sehemu ya 02

Kuna wanawake wengi, warembo, wanavutia ila unapoishi nao kwenye uhusiano tu unagundua si mtu sahihi kwako, hatoweza kuwalea watoto katika malezi uliyokuwa ukiyahitaji.

Ukiachana na mambo ya malezi pia kuna suala la akili tu ya maisha. Unapotafuta mtu wa kujenga naye maisha unatakiwa umpate mtu ambaye unalingana naye akili ama hata kama umempita basi uwe umempita kwa kidogo sana.

Unapompata mtu ambaye umemzidi akili kwa kiasi kikubwa huwezi kusonga naye popote pale kwa sababu atakifanya kila utakachomwambia hata kama hilo litakuwa baya na kukurudisha nyuma.

Mara nyingi watu wa hivi si wa kupingana na mawazo yako hata kama yatakuwa mabaya. Unaweza kutaka kufanya biashara, ukamwambia nataka tufanye biashara hii, hata kama ni mbaya, anakubaliana na wewe pasipo kukwambia ni changamoto kiasi gani zinaweza kuingilia biashara yako na hatimaye kufa.

Unapokuwa na mwanamke ambaye umemzidi akili kwa kiasi kidogo ama kulingana, nakuhakikishia utakuwa umepata mwanamke sahihi ambaye atayafanya maisha yako yasonge mbele tofauti na mtu ambaye umemzidi kwa kiasi kikubwa, ni lazima ipo siku wote wawili mtaingia porini kwa kuwa wewe ndiye ambaye utakuwa tegemeo la kuanzisha mambo bila kupokea changamoto zozote zile.

Ndivyo ilivyotokea kwa Evelyne, alikuwa mrembo hasa ila hakuwa na sifa hiyo na ndiyo maana niliamua kuachana naye na kutafuta mwanamke mwingine ambaye niliamini angekuwa sahihi kwa ajili ya watoto wangu.

Nilisubiri chakula kwa dakika kadhaa mahali hapo, baada ya dakika kadhaa tangu niingie, ghafla nikawaona wasichana wawili wakiingia humo mgahawani, mmoja alikuwa mweusi na mrefu kidogo na mwingine alikuwa mweupe.

Nilimwangalia msichana huyo mweupe, alinichanganya kwa sababu mimi ni mweusi. Mara zote wanaume weusi wanapenda wanawake weupe na wanawake weupe wanapenda wanaume weusi.

Ipo hivyo! Ni mara chache sana kuona wapenzi wakiwa wote wa rangi moja, hutofautiana na hata wakiwa wanatembea, unaona kabisa wamependeza tofauti na wale wa rangi moja.
 
Sehemu ya 03.

Nilibaki nikimwangalia msichana yule kiasi cha yeye mwenye kujishtukia kwani kila alipogeuza macho na kuniangalia, nilikuwa nikimwangalia yeye, nikawa naachia tabasamu tu.

Baada ya dakika kama kumi, chakula changu kikaletwa na kuanza kula. Pale nilipokuwa na mahali walipokaa wasichana wale hapakuwa mbali, nikapiga moyo konde na kuanza kusogea kule walipokuwa.

Huwa nipo hivyo! Inapotokea kupenda, huwa siangalii nipo sehemu gani, ninapomuona mwanamke mzuri, ninatumia nafasi hiyo hiyo kuzungumza naye kwa sababu hakuna kitu ninachokichukia kama kujuta.

Nilishajuta sana! Nilishajilaumu kupita kawaida. Kuna wakati unakutana na msichana mrembo ambaye unahisi kabisa mngeendana lakini jambo la ajabu, humwambii kitu chochote kile, labda unaogopa na mwisho wa siku ukienda nyumbani, unajuta kwa nini hukuzungumza naye kipindi kile.

Hivyo kwa huyu msichana sikutaka kabisa kuona akiondoka bila kuongea nami na ndiyo maana nikaamua kuwafuata ili tu nizungumze naye, japo kidogo tu.

Nilipofika, nikaweka chakula changu kwenye meza yao, wote wakayainua macho yao na kuniangalia kama watu waliokuwa wakishiangazwa na kile kilichotakiwa kutokea mahali pale.

“Samahani kwa kuwavamia kikomandoo!” nilisema huku nikitoa tabasamu pana ambalo niliamini liliwachanganya wasichana wengi.

Hawakunijibu! Nilikaa na kuanza kuwaangalia. Hawakufanya jambo lolote zaidi ya wao kuniangalia tu, walijiuliza sababu ya mimi kwenda pale, nilihitaji nini lakini hawakuwa na majibu yoyote yale.

“Ninaitwa Nyemo Chilongani!” niliwaambia huku nikiwaangalia kwa zamu.

“Unaitwa nani?” aliniuliza yule mwingine huku akiniangalia na kuweka usikivu zaidi.
“Nyemo Chilongani!” nilijibu.

Huwa ninapenda kuangalia muvi, zinaniathiri sana. Kwa Wazungu, huwa wanasema ni jambo jema kabisa kujitambulisha kabla ya kuanzisha mazungumzo yoyote yale.

Kwenye muvi zao huwa hivyo, kitu cha kwanza unajitambulisha na kisha kuanza kuzungumza mambo mengine, huwa wanaamini unapojitambulisha, inakuwa ni rahisi kwa mtu kukutilia umakini katika mazungumzo yako kuliko kutokukufahamu.

“Oh! Sawa! Karibu! Ila hilo jina bayaaaaa...” aliniambia yule niliyekuwa nikimtaka mno, nikatoa tabasamu pana.
 
Sehemu ya 04.

“Ila utalizoea!”
“Mh! Sidhani! Yaani ni jina baya!” aliniambia huku akiendelea kutabasamu.
Nilianza kuongea nao, kitu cha kwanza kabisa ambacho huwa ninakiamini sana mbele ya mwanamke yeyote yule ni kumfanya agundue kwamba wewe una akili sana, huwa unafuatilia mambo mengi kupita kawaida.

Mwanamke ana kawaida moja, huwa anapenda kuwa na mtu aliyemzidi na si yule ambaye ataonekana kuwa chini yake.

Yaani mwanamke anapenda kuwa na mwanaume mwenye pesa kushinda yeye, mwenye uwezo kushinda yeye, mwenye akili kushinda yeye, mwenye elimu kushinda yeye, huwa hapendi mwanaume ambaye amemzidi, yaani mwanamke huwa hapendi kuwa na mwanaume ambaye hana kipato zaidi ya kile alichokuwanacho yeye.

Kwa hawa wasichana wawili, sikujua uwezo wao wa kifedha ila niliamini ni lazima katika mazungumzo yangu nionekana mtu ‘smart’ sana kwa sababu ndiyo watu ambao huwa wanatamani sana kuwa nao kuliko hao wengine.

“Naomba niongee ukweli kwanza,” niliwaambia huku nikiwaangalia kwa zamu.

“Ongea tu!”
“Huyu dada ni mzuri jamaniiii! Ninamfananisha na Malkia Cleopatra wa Misri,” niliwaambia huku nikimwangalia yule niliyekuwa namtaka sana.
“Uwiiiiii...wewe kaka utanifanya nichanganyikiwe!” aliniambia huku akionekana kuwa na aibu sana.

“Huo ndiyo ukweli! Katika maisha yangu huwa ninapenda kuwa mkweli! Unapokosea, ninakwambia hapo hapo, unapokuwa mzuri huwa ninakwambia bila kumung’unya maneno na ninaamini Mungu anafurahishwa na ukweli wangu,” niliwaambia.

“Kivipi?”
“Ninapokwambia u mzuri, Mungu anajiona yupo sahihi kukuumba jinsi ulivyo, anathamini uwezo wake na kuona yupo juu, ninapokwambia u mzuri inamaana nimemsifu Mungu kwa kazi yake kubwa ya uumbaji,” niliwaambia.

“Na sisi wabaya tusemeje? Aliwakosea?” aliniuliza yule rafiki yake.
“Hakuna binadamu mbaya, kila mtu ni mzuri! Mbaya unayemuona wewe, ni mzuri kama malaika kwa mwingine.

Huyu mwenzako, ninamuona mzuri sana, ila kuna mtu anamuona ni kituko, si mrembo na wakati kwangu mimi, kwa leo nahisi nitamuota usiku kucha,” niliwaambia, akazidi kuhisi aibu.
 
Sehemu ya 05.

“Hebu tell us about Cleopatra! Was she very beautiful?” (tuambie kuhusu Cleopatra! Alikuwa mzuri?) aliniuliza kwa Kiingereza, nikaachia tabasamu.

“Of course she was. Alikuwa mrembo mno kiasi kwamba mpaka kaka yake, Ptolemy wa 13 akashindwa kuvumilia, akaamua kumuoa kwa nyakati tofauti katika kile kipindi cha Utawala wa nguvu wa Mfalme Kaisari...” nilijibu.

“Kaka yake alimuoa?”
“Yaap! Hapo utagundua ni kwa jinsi gani huyu mwanamke alikuwa mzuri! Uzuri wake naufananisha na huu wa rafiki yako!” nilimwambia.

“Jamani we’ kaka...”
Ulikuwa ni muda wa kuzungumza ukweli, sikutaka kung’ata maneno hata kidogo, niliendelea kumwambia kuhusu uzuri wake, jinsi meno yake yalivyopangika vizuri, yalivyokuwa meupe, ngozi yake ya kung’ara, alivyokuwa akitembea na hata nguo zilivyokuwa zikimpendeza kupita kawaida.

Alibaki akishangaa tu, nilionekana kuwa mtu wa tofauti sana. Siri ya wanawake ipo hapa. Mwanamke anapenda kusifiwa, anatamani kujiona yeye ni namba moja duniani.

Watu wengine wanaibiwa wake zao kwa sababu tu wanashindwa kuwasifia ndani ya nyumba.

Mwanamke ananunua nguo nzuri, anajishebendua weeee, anavaa, anajiona amependeza na anapotokeza kwa mume wake, hamsifii hata kidogo, mwisho wa siku akienda mtaani, kuna kajamaa tu kanamwambia ‘Anti umependeza’ mwisho wa siku kajamaa hakohako kanamchukua na kulala naye kwa sababu alimwambia maneno ambayo mume wake alishindwa kumwambia ndani ya nyumba.

Tulikaa kwa zaidi ya saa moja, kile chakula walichokuwa wameagiza, mimi ndiye nililipia, nilionekana kuwa na furaha sana na ndipo msichana yule aliponiambia aliitwa Shasta Karina na alikuwa akiishi maeneo ya Kijitonyama jijini Dar es Salaam.

“Ooh! Ninashukuru kukufahamu!” nilimwambia huku nikimpa mkono.
“Na mimi naitwa Mage...” aliniambia rafiki yake huku akitabasamu.

“Ooh! Na wewe nashukuru kukufahamu!” nilimwambia na wote kuanza kucheka.
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kukutaka na huyu Shasta!

Alikuwa msichana mrembo mno, tulibadilisha namba za simu na kuanza kuwasiliana. Niliendelea kumwambia kuhusu hisia zangu, nilivyokuwa nikimpenda na kumuhitaji kupita kawaida.
 
Sehemu ya 06.

Alifurahi sana, tukawa tunaonana na kufanya mambo mengi kama wapenzi japokuwa siku za mwanzoni alikuwa mgumu mno.

Nilikaa naye kwenye uhusiano wa kimapenzi kwa kipindi kirefu, cha miaka miwili kwenye mahusiano yaliyokuwa imara mno, uhusiano wa kufa na kuzikana, ule wa kujiandaa kuwa mume na mke.

Shasta aliamini ningemuoa, hii ni kwa sababu nilimuonyeshea dalili zote za kufanya hivyo. Nilikubalika na marafki zake wengi, ndugu zake na watu wengine wengi ila baadaye nikagundua kulikuwa na kitu kimoja ambacho kingenifanya kutokuweza kumuoa mwanamke niliyekuwa nikimpenda, kitu hicho kilikuwa dini.

Yeye alikuwa Muislamu na mimi nilikuwa Mkristo. Kwangu, ilikuwa vigumu sana kubadili dini kwa sababu yake. Huwa ipo hivi!

Mwanamke anapoolewa, anaondoka nyumbani kwao na kwenda kuungana na ukoo wa mume wake, hubadilisha jina la ukoo wake na kulichkua jina la ukoo wa mwanaume.

Mwanamke uhama kabisa na kuhamia upande wa pili hivyo wanaume tunaamini ni kosa kubwa sana kubadilisha dini na kumfuata mwanamke ambaye anahamia kwako na kuchukua kila kitu cha huku.
Niliwahi kuzungumza naye sana, nilimwambia jinsi nilivyokuwa radhi kumuoa, nilivyotamani sana kuishi naye.

Alikubaliana nami kwa kila kitu, kwake, dini haikuwa ishu kubwa ila tatizo lilikuwa kwa wazazi wake, hawakutaka kusikia kitu hicho kabisa.

“Wazazi wamekataa!” aliniambia huku akionekana kusikitika kupita kawaida.
“Suala la wewe kubadilisha dini?”
“Ndiyo! Yaani hawataki hata kusikia! Wanakukubali sana, ila kwenye kubadili dini, ni kitu kisichowezekana kabisa,” aliniambia huku machozi yakimlenga.
Hakuna siku ambayo nilijisikia vibaya kama siku hiyo.

Kukataliwa kubadilisha dini kuliniuma kupita kawaida. Nilijaribu kumwambia maneno mengi ya ushawishi ila msimamo wake ulikuwa kwa wazazi wake, asingeweza kufanya jambo lolote lile pasipo wao kukubaliana naye.

“Kwani watakuoa wao?” nilimuuliza, nilionekana kukasirika.
“Nyemo...”
“Shasta! Kwa nini lakini? Hutamani kuolewa?” nilimuuliza huku nikimwangalia.

“Ninatamani!”
“Basi acha nikuoe!”
“Kwa ndoa gani?”
“Kanisani!”
“Haiwezekani Nyemo, serious haiwezekani!” aliniambia huku akiniangalia.
 
Sehemu ya 07.

Kwa jinsi nilivyokuwa nikimwangalia, alionekana kutamani sana ndoa lakini lilionekana kama jambo ambalo halikuwezekana hata kidogo.

Aliumia kupita kawaida lakini hakuwa na jinsi.
Niliendelea kuwa kwenye uhusiano naye lakini niliamini nisingeweza kumpata msichana mrembo, niliyempenda kwa moyo wa dhati kama alivyokuwa.

Hicho ndicho kitu kilichonifanya niumie, niwe na mawazo kupita kawaida. Nilibaki nikifikiria sana maisha yangu, bila Shasta yalionekana kuwa si lolote lile.

Tuliendelea kuwasiliana, kunitembelea lakini kila mmoja alijua kabisa hakuna ndoa mbele yetu.

“Au nikutie mimba tu labda wazazi wataweza kubadilisha mawazo?” nilimuuliza. “Haiwezekani! Dada yangu, Hadija alipewa mimba na Mkristo, na bado wazazi walikataa aolewe naye, hilo halitasaidia,” aliniambia.

Siku zilikwenda kama kawaida! Nakumbuka siku moja nilipigiwa simu na kuambiwa kulikuwa na maofisa wa TRA walifika katika duka langu kubwa lililokuwa maeneo ya Kinondoni Mkwajuni kwa lengo la kulifunga duka hilo kwa kuwa sikuwa nimelipia kodi.

Nilishtuka, hakukuwa na kitu ambacho nilikuwa makini nacho kama kulipa kodi. Niliongea na mfanyakazi wangu na kumwambia awaambie nililipia lakini hawakutaka kukubali hivyo kunitaka mimi niende haraka sana.

Nikatoka ndani, nikaingia ndani ya gari langu na kuanza kuondoka kuelekea huko Kinondoni na kwa kuwa nilikuwa nikiishi Sinza Darajani, njia rahisi ilikuwa ni kupitia katika barabara ya Uzuri.

Niliondoka na kuelekea huko. Njiani nilikuwa na maswali mengi. Suala la Shasta lilinichanganya sana, halafu likaibuka jambo jingine kabisa kuhusu TRA.

Nikapiga gia! Nilipofika maeneo ya Magomeni Fundikira, wakati nakaribia kufika Magomeni Kanisani, mara nikamona dereva wa bodaboda akiwa amempakiza dada fulani mzuri hivi, alitaka kulipita gari moja, ghafla akasukumwa na kuuingia mtaroni.

Nilishtuka, ilikuwa ajali mbaya! Wote wawili walikuwa kwenye mtaro, watu wakajaa, nikasimamisha gari na kuteremka, lile gari lililokuwa limewasukuma, liliondoka kwa mwendo wa kasi.

“Aisee huyu dada ameumia,” alisikika mwanamke mmoja huku akionekana kuogopa.
 
Sehemu ya 08.

Watu walikuwa wakiwaangalia tu pasipo kutoa msaada wwote ule. Nilichokifanya ni kuwaambia watu wanisaidie kumtoa yule dada ambaye alionekana kuzidiwa zaidi na kumpakiza ndani ya gari langu.

Hilo likafanyika, akanyanyuliwa na kuingizwa ndani ya gari na watu wengine wawili na kuanza kuelekea naye hospitalini huku tukimuacha dereva bodaboda ambaye alisema yupo fiti kabisa.

Niliendesha kwa mwendo wa kasi kuelekea Hospitali ya Mwananyamala. Kulikuwa na urahisi wa kumpeleka Hospitali ya Magomeni lakini nilihisi kungekuwa na watu wengi hivyo nikaamua kwenda huko.

Ndani ya gari msichana yule alikuwa akilia tu, mguu wake ulichubuka, alionekana kuwa kwenye maumivu makali na muda mwingi alikuwa akilitaja jina la mama yake tu.

Alibembelezwa lakini hakubembelezeka! Alilia mpaka tulipomfikisha hospitalini na kuchukuliwa na machela na kwenda kupewa huduma huko.

“Jamani naomba niwaache!” niliwaambia wanaume wale.

“Hata sisi tunasepa! Wewe unakwenda wapi?” alijibu mmoja na kuniuliza.
“Nakwenda Kinondoni Mkwajuni!”
“Tunaomba utusogeze,” aliniambia mmoja.

Hapakuwa na tatizo lolote lile, tukaingia ndani ya gari na kuondoka mahali hapo. Niliwafikisha mpaka Magomeni Kanisani, nikageuza na kuelekea Kinondoni.

Nilifika huko kuonana na hao maofisa wa TRA ambao nilizungumza nao, nikawaonyesha risiti, waliporidhika, wakaondoka zao, nikaingia ndani ya gari kujiandaa kurudi nyumbani.

Nikiwa humo, ghafla nikasikia simu ikianza kuita, haikuwa yangu, mlio ulitokea humohumo ndani, nilipoangalia nyuma, chini ya kiti niliiona simu moja aina ya Samsung J7 Neo, nikaichukua na kuanza kuiangalia, mpigaji aliseviwa kama mama.

Nikajipa uhakika kwamba simu hiyo ilikuwa ya yule msichana, aliidondosha na mtu aliyekuwa akipiga alikuwa mama yake. Nikaipokea.
“We’ Scaila!” aliita mama yake.
 
Sehemu ya 09.
|
|

“Samahani mama! Mwenye simu amepata ajali!” nilimwambia bila hata salamu.
“Uwiiiiii...unasemaje?” aliniuliza huku akionekana kupaniki.

“Ameumia kidogo! Nilimsaidia! Yupo Mwanyamala anapatiwa matibabu, hakuumia sana mama usijali,” nilimwambia mama yake, hata kabla hajaniambia kitu kingine, simu ikaishiwa chaji hapohapo, ikazima.

Nilichanganyikiwa ila sikuwa na jinsi, nilichokifanya ni kuondoka na kurudi hospitalini, ilikuwa ni lazima nifanye hivyo kwa sababu ni utu kumsaidia mtu na hata kumjulia hali kutokana na kile kilichokuwa kimetokea lakini pia ilikuwa ni lazima nimpelekee simu yake.

Nilipofika, niliulizia na kuambiwa mahali alipokuwa na hivyo kwenda kule. Aliponiona tu, kwa mbali akaanza kutoa tabasamu, nilishindwa kugundua kama huyo msichana ndiye aliyepata ajali kwani alionekana kuwa mzuri kupita kawaida.

Kama nitaambiwa nimzungumzie sifa zake, zilikuwa nyingi sana, alikuwa mweupe, kama Mpemba fulani hivi, mwembamba kidogo, miguu ya kawaida, alikuwa na vishimo viwili mashavuni ambavyo vilionekana kila alipokuwa akitabsamu, alikuwa na nywele ndefu, yaani kwa jinsi alivyokuwa ilikuwa ni kama nilikutana na jini katika daraja la Salenda.

Nikabaki nikiushangaa uzuri wake. Msichana huyo aliitwa Scaila John ambaye ninataka nianze kukupa stori yake hii ndefu na ya kusisimua mno ambayo itaweza kukufundisha mambo mengi katika maisha yako.

|
|
Je, nini kitaendelea?
 
SEHEMU YA 10.

Katika maisha yangu nimewahi kuwaona wanawake wa kila aina, wale wanene, wembamba, weupe, weusi, warefu na wafupi ila kwa huyu aliyekuwa mbele yangu, alikuwa mzuri kupita kawaida.

Nilimwangalia Scaila huku akinitolea tabasamu pana, lilinichanganya, ngozi yake nzuri, nyeupe kama Mpemba fulani ilinipagawisha mno. Mashavuni mwake niliviona vile vishimo vilivyoonekana kila alipokuwa akicheka ama kutabasamu.

Nilimsogelea pale alipokaa, sikumwambia kitu chochote kile, ni kama nilikuwa nikiuangalia uzuri wake wa ajabu mbele yangu. Nilimpomfikia, nikamsalimia na mimi nikijifanya kutoa tabasamu pana lilelile.

“Bila shaka unaendelea vizuri! Pole sana kwa matatizo,” nilimwambia huku nikiliangalia jeraha lake ambalo wakati huo lilikuwa likifungwa bandeji.

“Nashukuru sana kwa msaada wako!” aliniambia kwa sauti nyembamba kabisa, iliyopenya masikioni mwangu, ikaenda ubongoni na kuvuruga kila kitu.

Mawazo yangu yakaanza kwenda mbali kabisa kuhusu. Alinichanganya kabisa, picha niliyokuwa nikiiona kichwani mwangu, nilisimama kanisani na msichana huyo na kufunga ndoa, baada ya hapo tukaanza kuishi kama mume na mke.

Nilitulia kimya, sikutaka kuongea kitu chochote kile lakini macho yangu yaliganda sana usoni mwake kiasi ambacho hata yeye mwenyewe alikuwa akishangaa kwani alitegemea ningeendelea kuongea jambo lolote lile, lakini nilikuwa kimya kabisa.

“Naitwa Nyemo! Nilikusaidia baada ya kuona umeumia sana, wakati mwingine nilihisi kama ungekufa kutokana na ajali ile kuwa mbaya sana,” nilimwambia maneno hayo lakini nilitoa tabasamu kwa mbali, sikutaka aone nilikuwa siriazi na kile nilichokuwa nikikisema.
“Nashukuru sana! Yaani sijui ilikuwaje!” aliniambia.

“Unaifahamu namba ya mama?” nilimuuliza.
“Mama yangu?”
“Yaap!”
“Naifahamu!”

“Basi mpigie, muondoe hofu, alikupigia kwa namba yako ila simu ilizima,” nilimwambia na kumpa simu yangu.

Akaichukua na kuanza kubonyeza namba za mama yake ambazo zilikuwa kichwani mwake. Baada ya sekunde kadhaa, akaanza kuongea naye.

Kwa jinsi mwanamke huyo alivyokuwa akiongea kutoka upande wa pili, sauti yake ilisikika kama mtu aliyekuwa amechanganyikiwa sana, Scaila alimpoza kwa kumwambia kwamba yupo salama na hakutakiwa kuhofia.
 
SEHEMU YA 11

“Upo wapi?” aliuliza mwanamke huyo.
“Nipo njiani nakuja!” alijibu Scaila.
“Niliambiwa umepata ajali!” alisikika mama yake.

“Haikuwa kubwa, ni kidogo tu mama, ila nipo salama nakuja,” alisema Scaila huku akitoa tabasamu ambalo bado liliendelea kunichanganya kupita kawaida.
“Sawa.”

Baada ya kumaliza kuongea naye, akanipa simu na mimi kumpa simu yake, tukafanya malipo yaliyotakiwa na kuchukua dawa na baada ya hapo kuanza kuondoka hospitalini.
“Naitwa Scaila Michael....” alijitambulisha.
“Una jina zuri.....”
“Nashukuru!”

“Kama jinsi ulivyo...” niliongezea.
Hakuitikia, alibaki akitoa tabasamu pana kuonyesha kufurahishwa na kile nilichokuwa nimemwambia. Nilimuuliza alipokuwa akiishi, akaniambia Tabata Bima hivyo kuanza safari ya kuelekea huko.

Njiani tulikuwa tukiongea mambo mengi, muda mwingi alikuwa akinishukuru kwa kile nilichokuwa nimemfanyia kwani ilikuwa ni vigumu kwa watu wengine kutoa msaada wa dhati kwa mtu ambaye hawakuwa wakifahamiana hata kidogo.

“Msaada ni kitu muhimu sana, huwezi kujua unamsaidia nani muda huo,” nilimwambia huku macho yangu wakati mwingine yakimwangalia.
“Oh! Labda unamsaidia rais wa baadaye!” aliniambia.

“Au labda unamsaidia mke wako wa baadaye...” na mimi nilimwambia.
Kwa jinsi alivyokuwa mzuri sikutaka kujizuia, nilihisi kama baada ya kumfikisha nyumbani kwao basi ndiyo ingekuwa mwisho kati yangu na yake na ndiyo maana nilihakikisha kwenye kila neno ninalomwambia ni lazima niweke ishara fulani hivi ya kumtaka kimapenzi.

Tulichukua nusu saa mpaka kufika kwao. Nikateremka, nikaenda kumfungulia mlango na kugonga hodi getini kwao.

Ni ndani ya sekunde chache, msichana fulani akaja kufungua, tukaingia, tulimkuta mama yake akiwa kibarazani, alipotuona, akasimama na kutusogelea, cha kwanza akaanza kumjua hali binti yake.

“Umeumia sana? Nini kimetokea? Mungu wangu! Scaila, umeumia vibaya sana,” alisema mama yake huku akionekana kutokuwa sawa kabisa.
 
SEHEMU YA 12.

Mwanamke huyo alionekana kuogopa sana lakini Scaila akamtoa hofu kwa kumwambia alikuwa salama kabisa. Tukaingia ndani, muda wote nilikuwa karibu na mrembo huyo kiasi kwamba kama ungetukuta mara ya kwanza ingekuwa ni rahisi kusema tulikuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi.

Tulipofika sebuleni na kukaa kwenye kochi ndipo Scaila akaanza kunitambulisha kwa mama yake. Alimwambia kila kitu kilichokuwa kimetokea, jinsi ajali ilivyokuwa na hata ule wema wangu wa kumsaidia.

Mama yake alinishukuru sana, hakuamini kama ningeacha mambo yangu kwa ajili ya mtu ambaye sikuwa nikimfahamu kabisa. Tuliongea mambo mengi na baada ya kumaliza, nikawaambia ninahitaji kuondoka.
“Haina shida baba! Karibu tena,” alisema mama yake.

Nikasimama, huku Scaila akionekana kuwa na maumivu ya mguu wake, akanishika mkono na kunisindikiza mpaka nje. Wakati amenishika, muda wote mapigo yangu ya moyo yalikuwa yakinidunda kupita kawaida.

Kwa Scaila, sijui aliniroga! Yaani alinichanganya kwa muda mfupi kiasi kwamba nikaanza kumsahau Shasta kabisa. Tulipofika nje, tukaelekea mpaka kulipokuwa na gari langu na kusimama, tukabaki tunaangaliana.

“Unaniangalia sana mpaka nasikia aibu,” aliniambia kwa sauti ya chini.

“Najaribu kuutafakari ukuu wa Mungu na uumbaji wake,” nilimwambia kwa sauti ndogo, nami kama kawaida niliachia tabasamu pana.

“Uumbaji wake umefanyaje?”
“Nadhani alikuumba siku ya wikiendi, yaani ile ambayo alimaliza kazi zake zote, sasa akawa na kazi moja ya kumuumba msichana mmoja mrembo sana,” nilimwambia, maneno hayo yalimfanya kusikia aibu zaidi, akaanza kuangalia chini.

“Scaila! Nimefurahi kuonana na wewe, wakati mwingine hata matukio makubwa na mabaya hutokea kwa sababu Mungu anahitaji kuwaunganisha watu wawili,” nilimwambia, nikamvutia kwangu.
“Unamaanisha nini?”
“Bila ajali nisingeweza kuonana na wewe,” nilimwambia.

“Mh!”
“Ndiyo hivyo! Naomba niondoke, nitakuja kukuona siku nyingine,” nilimwambia kwani sikutaka kuongea mambo mengi sana, nilihisi kama yote ningeyamaliza hapo na wakati kulikuwa na mengi ya kuongea.
 
SEHEMU YA 13.

Nikambusu kwenye paji lake la uso na kisha kuingia ndani ya gari. Kichwa changu ni kama kilivurugika kupita kawaida. Huyu Scaila alinichanganya mno.

Niliondoka Tabata Bima huku nikimfikiria yeyey tu, nilipofika Tabata Mwananchi ndipo nikakumbuka sikuchukua namba ya simu yake, yaani kwenye mambo yote tuliyokuwa tumeongea, eti sikuchukua namba yake!

Nilijilaumu sana lakini sikuwa na tatizo lolote lile kwa kuamini ningeweza kuonana naye siku nyingine, hivyo niliendelea na safari yangu kama kawaida.

Baada ya dakika kadhaa, nikafika nyumbani na kujipumzisha kwenye kochi. Kwa jinsi nilivyokuwa na furaha, nilimwambia dada wa kazi hakutakiwa kupika, nilihitaji nitoke naye na kwenda kula chakula sehemu yoyote ile.

Yeye mwenyewe kwa jinsi alivyoniona, alihisi kulikuwa na kitu upande wa pili kwani nilionekana kuwa na furaha kupita kawaida. Alitamani sana kuniuliza lakini alishindwa kwani hakuona kama ingekuwa sawa kuniuliza mambo binafsi kama hayo.

Alijiandaa na tukatoka kwenda kwenye mgahawa wa Samaki Samaki na kuanza kula chakula hapo. Kwa jinsi nilivyokuwa nikiongea naye, hakuwa na shaka kwamba nilikuwa mmoja wa watu waliokuwa na furaha tele katika dunia hii.

“Kuna nini kaka?” aliniuliza huku akiniangalia, alikuwa na kimuemue cha kutaka kufahamu ni kitu gani ningemwambia.

“Unajua napitia mambo mengi sana Grace,” nilimwambia.

“Mambo hayo ndiyo yanayokufanya kutabasamu muda wote?” aliniuliza.
“Hapana! Ila kuna jingine kubwa,” nilimwambia.
“Au wifi Shasta amekubali muoane?” aliniuliza.

“Hapana!”
“Kumbe je?”
Nikaanza kumwambia kilichokuwa kimetokea, alibaki akinisikiliza kwa makini. Nilimwambia kuhusu huyo Scaila, jinsi alivyokuwa mrembo.

Nilijitahidi kumpamba kupita kawaida. Ni kama pale unapoamua kumwambia mtu fulani kuhusu uzuri wa msichana fulani, unatamani kumuonyeshea ni kwa namna gani mtu huyo alivyokuwa mrembo kwani maneno tu hayakuonekana kutosha hata kidogo.

“Yaani ni mzuri!” nilimwambia, maneno hayo niliyazungumza mara kwa mara.
 
SEHEMU YA 14.

“Una picha zake?”
“Hapana! Lakini ni mzuri..yaani ni mzuri! Grace, duniani kuna wanawake wazuri sana. Yule Scaila, yaani ni mzuri balaa,” nilimwambia kwa msisitizo, yaani yote hiyo nilitaka aamini kwa asilimia mia moja nilichokuwa nikimwambia.

Grace alibaki akicheka tu. Huyu alikuwa mfanyakazi wangu, nililetewa na dada yangu kutoka mkoani Mwanza, alikuwa Msukuma mzuri, mwenye umbo matata sana ila kipindi alichokuwa amekuja jijini Dar es Salaam, hakuwa na muonekano mzuri.

Nilikubali awe dada wa kazi, kwanza kitu cha kwanza nilichokifanya ni kuanza kumbadilisha. Huyu Grace alitakiwa kuwa na muonekano mzuri, msafi kwa sababu pale nyumbani kwangu kulikuwa na marafiki zangu wengi waliokuwa wakifika kunitembelea.

Kipindi cha kwanza walimchukulia kawaida sana ila baada ya kumbadilisha, kila mtu aliyekuwa akifika nyumbani hapo alichanganyikiwa.

Alipendeza mno, wengi waliniambia niwaunganishe naye ila sikutaka kufanya hivyo kwa sababu nilijua ni kwa namna gani marafiki zangu walivyokuwa wahuni, hawakuwa waoaji, na wale waoaji hawakutaka kutulia kwenye ndoa zao kabisa.

“Hebu cheki wezele ile...dah! Nyemo unafaidi sana! Yaani huyu mtoto ukimuweka kwenye kumi na nane zako, usiku mzima wewe unaimba wimbo wa CCM mbele kwa mbele,” aliniambia rafiki yangu, aliitwa Juma Hiza.
“Acha ujinga wako! Dada yangu huyo,” nilimwambia Juma.

“Sasa inakuwaje?”
“Kuhusu nini?”
“Nimeshachanganyikiwa, yaani siambiwi wala sisikii hapa,” aliniambia.
“Tubadilishane basi. Namuomba Amina!” nilimwambia, huyo alikuwa dada yake.
“Hahah! We mjinga sana, nikupe Amina mimi!” aliniambia.

“Kwani kuna ubaya gani! Si mara moja moja unakuja kula kwa shemeji, ukiniona unanipiga mizinga,” nilimwambia kwa utani.

Juma alikuwa na dada yake aliyeitwa Amina, alimpenda mno, alimchunga sana na wanaume hasa sisi marafiki zake kwa kuwa tulikuwa tunajuana ni watu wa aina gani.

Hakutaka kusikia kitu chochote kuhusu Amina, alijitahidi kumlinda na sisi lakini siku ambayo nilikutana naye maeneo ya Mwenge ndipo nilipochukua namba yake na kuisave kama Fundi Bomba.
 
SEHEMU YA 15.

Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa mimi na Amina kuwa pamoja mpaka nilipokamilisha mipango yangu, kuwa wapenzi wa siri pasipo yeyote kufahamu, na hata tulipoachana, bado hapakuwa na yeyote yule aliyekuwa akifahamu chochote kile.

Juma hakuyajua hayo yote kwa kuwa nilikuwa msiri sana. Leo alikuwa akimuhitaji Grace. Hakuwa na ndoto za kuoa, alikataa kuoa kwa hiyo niliamini hata kama angekuwa na Grace, mwisho wa siku binti wa watu angelia tu, asingeweza kumuoa.

Tuliendelea kula na kunywa na Grace, tulipomaliza tukarudi nyumbani. Alilala lakini chumbani kwangu hakukulalika hata kidogo, muda wote nilikuwa nikimfikiria Scaila, nilitamani sana niwe na namba yake, muda huo nimpigie na kuzungumza naye sana.

Nilikuja kupata usingizi majira ya saa nane usiku, na ilipofika saa moja, nikaamka na kuanza kujiandaa. Wakati nikifanya hayo yote, picha ya Scaila ilikuwa kichwani mwangu, ni kama iliganda na haikutaka kutoka kabisa.
“Leo usiniwekee chakula mchana,” nilimwambia Grace.

“Utakuwa wapi?”
“Nataka kuonana na Shasta, kuna ishu anataka tuzungumze,” nilimjibu.
“Sawa kaka!”

Niliondoka na kuelekea kwenye kazi zangu kama kawaida. Siku hiyo sikutaka kabisa kumfikiria mtu mwingine zaidi ya yule Scaila tu.

Nilifanya mambo yangu mengi na ilipofika majira ya saa nane mchana, Shasta akanipigia simu na kutaka kuonana nami kama tulivyopanga.
Tukaonana na kuanza kuzungumza.

Siku hiyo alionekana alikuwa na jambo kubwa alihitaji kuniambia, lilionekana kama kumkaba kooni lakini alishindwa ni mahali gani alitakiwa kuanzia.
“Nyemo...” aliniita kwa sauti ndogo.
“Naam!”
 
SEHEMU YA 16.

“Nataka kuolewa!” aliniambia.
“Ila wazazi wako wamekataa nikuoe!” nilimwambia.

“Simaanishi unioe wewe. Nimempata mwanaume mwingine wa kunioa. Ni Muislamu mwenzangu, anaitwa Karim Kanungila,” aliniambia.

Hata kama kulikuwa na mpango wa kuachana na msichana fulani halafu usikie kwamba alitaka kuolewa na mwanaume mwingine, ilikuwa ni lazima kuumia tu, ndivyo ilivyotokea kwangu kipindi hicho.

Nilimwangalia Shasta mara mbilimbili, sikuamini nilichokisikia, nilianza kumpenda Scaila moyoni mwangu lakini nikiri kwamba huyu niliyekuwanaye kipindi hicho alikaa moyoni mwangu na kutulia.

Moyo wangu ukaanza kudunda kwa nguvu kiasi kwamba kuna wakati nilihisi kama ungeweza kuchoma kutoka mwilini mwangu. Hali ya hewa ilikuwa ni ya kawaida lakini kijasho chembamba kikaanza kunitiririka.

Nilihisi kama kupigwa shoti ya umeme, kitendo cha kusema alitaka kuolewa na mwanaume mwingine kilinipagawisha kupita kawaida.

“Shasta...unasema unataka kuolewa?” nilimuuliza msichana huyo.

“Ndiyo! Barua ililetwa jana! Nadhani mwezi huu nitaolewa. Sikutaka kufanya kimya kimya, ilikuwa ni lazima nikwambie,” aliniambia, alihisi ni kitu kizuri lakini ukweli ni kwamba aliuweka msumali wa moto ndani ya moyo wangu.
“Unaolewa?”

“Ndiyo!”
“Na mwanaume mwingine tofauti na Nyemo?” niliuliza.
“Ndiyo!” alinijibu kwa unyonge alionekana kabisa hata kile alichokuwa akiniambia, hakuwa na furaha nacho.
 

Similar Discussions

14 Reactions
Reply
Back
Top Bottom