Simulizi: Penzi lisilo Na Mwisho

Sehemu ya 21

Hapo ndipo akapata jibu sababu iliyomfanya Sharifu kuchelewa kuufungua mlango alipokuwa akipiga hodi.

Akahisi moyo wake ukiwaka kwa hasira, hakuweza kuvumilia pale ukutani alipojificha, kwa kasi ya ajabu akachomoka, akawafuata kule walipokuwa, hawakuwa wamemuona, ile ghafla, msichana Nusrat akashtukia akikabwa roba kali na kuanza kushambuliwa kwa ngumi mpaka kuanguka chini.

“Sabrinaaa....” alijikuta akiita Sharifu, hata kumtoa Sabrina alishindwa kwani alikuwa na nguvu mno, alimkalia Nusrat juu huku akimpiga mfululizo.
*****
Mapenzi yakawa motomoto, kila walipokuwa, walikuwa pamoja, hakukuwa na kitu ambacho kingeweza kuwatenganisha kutoka katika penzi zito walilokuwa nalo zaidi ya kifo tu.

Kila mmoja alichanganyikiwa, kwa Aisha, hakuamini kama kweli maisha yote aliyoishi kipindi cha nyuma yalibaki na kuwa historia, yaani asingeweza kurudi tena mitaani, kuombaomba na kutafuta mabaki ya chakula katika hoteli mbalimbali zilizokuwa Kariakoo.

Maisha yake yalikuwa mapya kabisa, alitakiwa kusahau kila kitu, alitakiwa kujua kwamba kwa kipindi hicho yeye alikuwa mpenzi wa mtoto wa bilionea, hivyo shida zote alizokuwa nazo kipindi cha nyuma alitakiwa kuzisahau.

Aisha hakutaka kuwaacha mapacha ambao ndiyo walionekana kuwa sababu ya yeye kukutana na Razak, alihakikisha nao wanapata maisha bora kama aliyokuwa akipata, hilo, kwa Razak wala halikuwa tatizo, kwa sababu umri wao haukuwa mkubwa sana, akawahamisha katika nyumba hiyo na kuwapeleka katika nyumba nyingine nzuri iliyokuwa Sinza, walitakiwa kuishi huko, wakawekewa mfanyakazi na kupewa kila kitu walichokihitaji.

Yote hayo aliyafanya kwa kuwa alitaka kumuona mpenzi wake akiwa na furaha tele, hakutaka ayakumbuke maisha aliyopitia kipindi cha nyuma, kila kitu kilichopita, alitaka kiwe historia ambayo isingeweza kujirudia tena maishani mwake.

“Unapenda nikufanyie nini katika maisha yako?” aliuliza Razak huku akiwa amemlaza Aisha miguuni mwake.
“Ninataka unioe...” alijibu Aisha huku akiachia tabasamu pana.
“Hilo tu?”

“Yapo mengi, ila hilo ndilo la kwanza!”
“Usijali mpenzi, nitahakikisha nakuoa haraka iwezekanavyo...” alisema Razak huku akiachia tabasamu pana.

Razak alikuwa na fedha, hilo kwake halikuwa tatizo hata kidogo, mara kwa mara walikuwa wakitoka na kuelekea sehemu mbalimbali kula maisha, walikwenda Zanzibar, katika Visiwa vya Komoro na Shelisheli, kote huko alitaka kumuonyesha Aisha jinsi maisha ya kuwa na fedha yalivyokuwa.

Kwa jinsi walivyopendana, kusikilizana na kujaliana, hakukuwa na aliyefikiri kwamba wakati mwingine kwenye mapenzi kuna kugombana na kufarakana, kwao, mapenzi yalikuwa motomoto.
Razak hakutaka kumkumbuka Sabrina, alitaka kumfuta kabisa kwenye akili yake.

Moyoni mwake alihisi kwamba kuna kitu kingeweza kutokea, hivyo alichokifanya ni kujihami mapema kabisa.
Akamwambia Aisha kuhusu msichana huyo, jinsi alivyokuwa naye na mapenzi kuja kuyumba na hatimae kuachana kabisa.

Kwa Aisha, hilo halikuwa tatizo, alifurahi kupewa taarifa na hivyo akajiandaa kwa lolote ambalo lingeweza kutokea.

Je nini kitaendelea....
 
Sehemu ya 22

Siku zikakatika, alichokifanya Razak ni kuanza mikakati ya kufunga ndoa na Aisha. Hakutaka kuchelewa, alitamani kumfanya mpenzi wake kuwa na furaha zaidi ya mwanamke yeyote chini ya jua.

Hakutaka kuchelewa, kwa kuwa yeye mwenyewe alianza kusimamia biashara mbalimbali za baba yake, akamnunulia Aisha gari la kifahari kwa ajili ya kufanyia mizunguko yake ya huku na kule.

Yule msichana mchafumchafu, aliyekuwa akiomba mitaani, hakuwa huyu wa kipindi hiki, huyu alikuwa Aisha mwingine kabisa, aliyependwa na kupendeka, aliyepanda thamani ambaye kila alipokanyaga, alipewa heshima na watu wengine.
“Hili ndinga kakununulia?” aliuliza Mohammed huku akionekana kulishangaa gari la Aisha.

“Ndiyo! Ni zuri au baya?”
“Ni zuri sana, aiseee...una bahati sana Aisha...”
“Bahati ya nini?”

“Kuwa na huyu Razak, anakupenda kweli...sasa itakuwaje? Mwambie basi na sisi atufanyie mchongo tupate ndinga...” alisema Mohammed huku macho yake yakiliangalia gari lile.

“Hakuna tatizo...kwanza mnahitaji nini katika maisha yenu?” aliuliza Aisha.
“Kwanza tuwe na hela za kula bata tu,” alijibu Mohammed.

“Hapana! Bata za nini kwanza? Cha kwanza tufanye biashara...” aliingilia Ahmed ambaye alikuwa kimya kwa kipindi kirefu.

“Hapo umeongea Ahmed....”
“Cha kwanza ni biashara, fedha zitapatikana tu, bata haziishi Moody, ni lazima tufanye kitu,” alisema Ahmed.

Hakukuwa na kipingamizi, kwa sababu Ahmed alishauri kwamba ni lazima wapewe hela ya kufanya biashara, hilo halikuwa tatizo, kesho yake tu Aisha akarudi mahali hapo huku akiwa na zaidi ya milioni kumi na kuwakabidhi, ilikuwa ni lazima wafanye biashara.

Biashara ambayo waliichagua ni kununua nafaka mikoani na kuyapeleka jijini Dar es Salaam. Hiyo ilionekana kuwa biashara nzuri ambayo iliwafanya kutokutulia jijini Dar.

Mara kwa mara walikuwa watu wa kusafiri, walikuwa vijana wadogo lakini maisha waliyoishi hapo kabla yalizifanya hata akili zao kukomaa na kufanya mambo kama watu wazima.

Huku Dar, bado mipango ilikuwa ikiendelea, watu wakapewa taarifa kwamba miezi miwili ijayo kungekuwa na harusi kubwa kati ya mtoto wa bilionea, Razak na msichana mrembo, Aisha.

Kutokana na baba yake Razak kujulikana sana na wafanyabiashara kutoka sehemu mbalimbali katika nchi za Kiarabu, watu wengi wakaahidi kuhudhuria harusi hiyo ambayo ilitarajiwa kutikisa kuliko harusi zote zilizowahi kutoka nchini Tanzania.
“Hivi kweli unanioa?” aliuliza Aisha huku akionekana kutokuamini.

“Ninakuoa mpenzi...unakwenda kuwa mke wangu...” alisema Razak huku akitoa tabasamu pana lililokuwa na matumaini kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima harusi ifungwe.
****

Ulikuwa usiku sana, sehemu kubwa ilikuwa kimya lakini katika nyumba moja tu ndiyo kelele kubwa zilikuwa zikisikika, wanawake wawili walikuwa wakipigana huku mwanaume mmoja akiwa pembeni, alijaribu kuwagombelezea lakini hawakuachiana.

Sabrina alionekana kuwa na hasira kali, hakutaka kukubali hata mara moja kuona mwanaume wake aliyempenda akichukuliwa na mwanamke mwingine, hasira zilimpanda na kila alivyomwangalia Nusrat, alijikuta akiendelea kumshambulia pale chini.

Japokuwa Nusrat ndiye aliyefumaniwa na kuleta upole mwingi, alishindwa kuvumilia, hakutaka kuona akishambuliwa pasipo kurudisha mapigo, naye akaanza kumshambulia Sabrina.

Ulikuwa ugomvi mkubwa, uliosababisha kelele nyingi, hakukuwa na aliyekuwa radhi kumuachia mwenzake na hata Sharifu aliyekuwa pembeni alishindwa kabisa kuwagombelezea.
“Hebu achianeni kwanza....” alisema Sharifu huku akijaribu kuwatenganisha.

“Simuachiiii...yeye si anajifanya bingwa wa kuchukua wanaume za watu, simuachiii...” alisema Sabrina huku akiendelea kumng’ang’ania Nusrat.
“Wewe Sabrina hebu muachie mwenzako...nitakupiga...”

“Unipige mimi...wewe wa kunipiga mimi...kwa nini usimpige malaya wako?” aliuliza Sabrina, hasira zilimpanda kichwani, hakutaka kusikia lolote lile.

Je nini kitaendelea....
 
Sehemu ya 23

“Unipige mimi...wewe wa kunipiga mimi...kwa nini usimpige malaya wako?” aliuliza Sabrina, hasira zilimpanda kichwani, hakutaka kusikia lolote lile.
Alichokifanya Sharifu ni kutumia nguvu kumvuta Sabrina na kumuweka pembeni kisha kumsogelea Nusrat na kuanza kumpeleka nje ya nyumba hiyo.

Sabrina hakuwa na cha kufanya, alibaki akiwa amesimama, machozi yalilowanisha mashavu yake, hakuamini kile alichokiona, yaani mwanaume aliyekuwa akimpenda, aliyempa moyo wake, leo hii aliamua kuingiza mwanamke mwingine.

“Sharifu...kwa nini unanifanyia hivi?” aliuliza Sabrina huku akilia, Sharifu hakujibu kitu, alipohakikisha Nusrat ameingia ndani ya gari lake na kuondoka, akaingia ndani huku akimwacha Sabrina pale nje.

Moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali, hakuamini kile alichokiona, mwanaume yuleyule ambaye rafiki yake, Minah alimfuata na kumwambia kwamba alikuwa akimpenda na ndiye mwanaume huyohuyo ambaye leo hii aliamua kumuingiza mwanamke mwingine, alipouliza, hakujibiwa zaidi ya kuingia ndani.

Hakutaka kubaki pale nje, alihisi moyo wake ukiwa kwenye hasira kali, hakutaka kukubali kabisa, alichokifanya ni kuingia ndani, moja kwa moja akamfuata Sharifu aliyekuwa chumbani na kuanza kumuuliza maswali kwa sauti kali.

“Sikiliza Sabrina, sipendi kelele kabisa, tena unyamaze....nitakubabua...” alisema Sharifu huku akionekana kumaanisha alichokisema.

“Sharifu...kwa nini unanifanyia hivi?”
“Nimekufanyaje? Yaani unamvamia mtu na kugombana naye, humjui yeye ni nani, hujauliza, unaanza kumpiga, hivi unajua yule ni nani?” aliuliza Sharifu huku akionekana kukasirka.
“Unanifanyia hivi Sharifu...kweli unanifanyia hivi?”

“Unajua yule ni nani? Unajifanya una hasira sana, unajifanya una wivu sana, unadhani wewe ndiye mwenye hasira peke yako humu duniani? Unafikiri wewe ndiye mwenye wivu kuliko watu wote humu duniani?” aliuliza Sharifu huku akiendelea kumkaripia Sabrina.

Kilichofuata ni Sabrina kuanza kuongea maneno yake huku akimlaumu sana Sharifu lakini mwanaume huyo hakutaka kuzungumza tena, alibaki kimya huku akigeukia upande wa pili wa kitanda chake.

Sabrina alijuta, mwanaume ambaye alijitolea moyo wake wote kumpenda ndiye aliyeamua kumuumiza kwa kumuingiza mwanamke ndani ya chumba chake.

Hakulala usiku mzima, alibaki akilia pembeni ya kitanda cha Sharifu. Mwanaume huyo alipoamka asubuhi, akabaki akimwangalia Sabrina, hakumuonea huruma, kwake, alimuona mwanamke mpumbavu ambaye alifanya jambo la kipumbavu kumvamia msichana na kumshambulia pasipo kuhoji alikuwa nani.

“Naomba unisamehe mpenzi...” alianza kuomba msamaha Sabrina.
“Kwa lipi?”
“Kumpiga mtu pasipo kujua alikuwa nani...”

“Wewe si umejifanya mjanja...”
“Hapanna! Sikujua mpenzi, naomba unisamehe, ni hasira na wivu tu ndiyo vimeniponza....” alisema Sabrina.

Hicho ndicho alichokuwa akikitaka Sharifu, alijua kwamba yeye ndiye alikuwa na makosa lakini kamwe hakutaka kuonyesha kwamba kweli alikosea, hakutaka kujishusha kwa kuona kwamba msichana huyo alikuwa akimpenda, hivyo yeye ndiye aliyetakiwa kumuomba msamaha.

Sabrina hakuwa na jinsi, hakutaka kumuacha Sharifu, alimpenda hivyo hata kumuomba msamaha ilikuwa ni sehemu ya mapenzi mazito aliyokuwa nayo kwake.
“Usirudie tena, umesikia?” alisema Sharifu huku akimwangalia Sabrina kidharau.

“Nimesikia, sitorudia mpenzi...” alisema Sabrina huku akitokwa na machozi tu, moyo wake ulikuwe kwenye maumivu makali ambayo hakuhisi kama kuna siku angeweza kuumia namna hiyo.
*****
Je nini kitaendelea.....
 
Sehemu ya 24

Shamsiaa Othman: Huyu alikuwa msichana mrembo, kwa kumwangalia, ungehisi kwamba umekutana na malaika.

Alivutia machoni na hata umbo lake lilikuwa zuri, kila mwanaume aliyemwangalia, alitokea kumpenda mno.
Nilimpa moyo wangu wote, anipende kama nilivyompenda, pamoja na mapenzi yote niliyompa, akaondoka Dubai na kuniachia upweke.

Alikwenda nchini Oman, aliporudi, akaniambia kwamba amepata mwanaume mwingine, mzuri zaidi yangu na hivyo angeolewa na huyo.

Niliumia sana, kuanzia siku hiyo, nikajiapiza kwamba nisingependa tena, yaani ningekuwa natembea na wanawake na kuwaacha kwenye maumivu makali kama alivyonifanyia Shamsiaa.

Khadija Rahman: Baada ya Shamsiaa, nikaona ni bora nitafute kimbilio hukohuko Dubai. Moyo wangu ukaangukia kwa msichana huyu mrembo mwenye asili ya Yemen.

Kwa kumwangalia, alikuwa mrembo lakini kitendo cha mimi kwenda kwake, hakikuwa mapenzi, bali nilitaka nilipe kisasi kile nilichofanyiwa na mwanamke mwenzao.

Kweli akanipenda sana, alinipa nilichotaka lakini sikutaka kumpa mapenzi kwa asilimia mia moja, baada ya kutembea naye ndani ya mwezi mmoja, nikaachana naye.

Je nini kitaendelea.....
 
Sehemu ya 25

Catherine Gozbert: Huyu alikuwa Mkristo safi. Mara ya kwanza kukutana naye alikuwa akitoka kanisani. Alikuwa msichana mrembo, mkononi alishika Biblia, nikaamua kumfuata na kumuomba nimpe lifti.

Alikuwa na usafiri wake, ilikuwa vigumu sana lakini nikahitaji nimsindikize, kweli akanikubalia, gari lake likawa mbele, langu nyuma. Alipofika kwao, akaliingiza gari kisha mwenyewe kuja nje.
Nilizungumza naye, alionekana kuwa mchangamfu.

Nilikuwa nikimuogopa ila baada ya kuona kwamba alikuwa mtu wa kawaida, nikazoeana naye, akanipenda, nikampenda ila kama kawaida yangu, sikuwa na moyo wa kupenda, moyo huo aliondoka nao Shamsia, hivyo nikamuacha, alilia na kulia, ila sikuweza kurudi kwake.

Farha Majeed: Nilisoma naye kitambo, baada ya kupotezana naye kwa kipindi kirefu, hatimaye nikaonana naye na ghafla tukatokea kuwa wapenzi.

Nilidumu naye kwa kipindi cha mwezi mmoja kama kawaida yangu, baada ya hapo, nikamuacha katika maumivu makali kwa kuamini kwamba ningempenda mpaka ndoa.

Sikuwa na historia ya kupenda na kufa kwa msichana, hivyo nilivyomtumia, nikamtupa kama ilivyokuwa kwa wengine. Akalia, akajuta kuwa na mimi ila sikutaka kusikia. Baada ya hapo, nikaamua kuelekea nchini Tanzania.

Je nini kitaendelea.....
 
Sehemu ya 26

Nusrat Twaha: Tulikutana katika Ukumbi wa Maisha Basement, akatokea kunipenda sana lakini hakujua ni kwa namna gani angenipata, hivyo akamtumia rafiki yangu wa kike, Minah ambaye naye nilimkosakosa.

Minah akanifuata na kuniambia kwamba nilikuwa napendwa, nikakubali, nikawa na Nusrat, tukafanya mengi, akapagawa nami ila ndiyo hivyo, muda wangu wa mwezi mmoja umetimia, hivyo nitammwaga kama wengine.

Sabrina Seif: Nilipomuona kwa mara ya kwanza, nilimpenda kidogo, nilimtaka niwe naye katika miezi yangu miwili ya kuwa hapa Tanzania kabla sijarudi Dubai. Sikujua ningempata vipi hivyo nikamtumia Minah, akanirekebishia na hivyo nipo naye.

Kama kumpenda, nampenda ila kwa asilimia tano tu. Nimemchezea kama wengine, nimemfanya ninachotaka kumfanya na sasa hivi nimemchoka, kama ilivyokuwa kwa wasichana wengine, hata naye huyu Sabrina nitamwaga japokuwa anapenda sana ndoa, kila nikikaa naye, anazungumzia ndoa tu.

Kashanifumania na Nusrat, nimemzugazuga tu, hivyo nammwaga kama kawaida kisha kurudi zangu Dubai. Kwa kifupi, siwezi kupenda, yule Shamsia ndiye aliyeharibu kila kitu. Baada ya kummwaga huyu, mwingine atakuja tu. Nafanya haya yote kama kisasi cha kuumizwa zamani.

Je nini kitaendelea.....
 
Sehemu ya 26

Nusrat Twaha: Tulikutana katika Ukumbi wa Maisha Basement, akatokea kunipenda sana lakini hakujua ni kwa namna gani angenipata, hivyo akamtumia rafiki yangu wa kike, Minah ambaye naye nilimkosakosa.

Minah akanifuata na kuniambia kwamba nilikuwa napendwa, nikakubali, nikawa na Nusrat, tukafanya mengi, akapagawa nami ila ndiyo hivyo, muda wangu wa mwezi mmoja umetimia, hivyo nitammwaga kama wengine.

Sabrina Seif: Nilipomuona kwa mara ya kwanza, nilimpenda kidogo, nilimtaka niwe naye katika miezi yangu miwili ya kuwa hapa Tanzania kabla sijarudi Dubai. Sikujua ningempata vipi hivyo nikamtumia Minah, akanirekebishia na hivyo nipo naye.

Kama kumpenda, nampenda ila kwa asilimia tano tu. Nimemchezea kama wengine, nimemfanya ninachotaka kumfanya na sasa hivi nimemchoka, kama ilivyokuwa kwa wasichana wengine, hata naye huyu Sabrina nitamwaga japokuwa anapenda sana ndoa, kila nikikaa naye, anazungumzia ndoa tu.

Kashanifumania na Nusrat, nimemzugazuga tu, hivyo nammwaga kama kawaida kisha kurudi zangu Dubai. Kwa kifupi, siwezi kupenda, yule Shamsia ndiye aliyeharibu kila kitu. Baada ya kummwaga huyu, mwingine atakuja tu. Nafanya haya yote kama kisasi cha kuumizwa zamani.

Je nini kitaendelea.....
Wakule tu baba,hasa mtafune zaidi sabrina

Sent using Jamii Forums mobile app
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom