Simulizi: Penzi ama kaburi?

Shunie

JF-Expert Member
Aug 14, 2016
152,886
453,430
Mtunzi Nyemo Chilongani

Sehemu ya 01

“Shadya! Wewe ni msichana mzuri sana, mrembo, msichana ambaye ninajisikia fahari sana kuwa nae,” ilisikika sauti ya mwanaume mmoja aliyekuwa amejibanza kwenye ukuta wa chuo cha madrasa ya Al Munira Siraja kilichokuwa katika Mtaa wa Michenzani huko Zanzibar.

Shadya alikuwa kimya, macho yake aliyatuliza usoni mwa kijana aliyesimama mbele yake. Alivalia kanzu ndefu nyeupe, kichwani alikuwa na kofia aina ya baghalashia na mkononi mwake alishika tasbih, chini alikuwa peku.

Hapo waliposimama ilikuwa ni rahisi kusikia sauti za wanafunzi waliokuwa wakijifunza koran ndani ya madrasa hiyo.

Kijana aliyekuwa akizungumza aliitwa kwa jina la Ngwali Shangali, alikuwa mwalimu wa madrasa hiyo ambaye alipewa jukumu la kuwafundisha watoto wadogo waliotakiwa kuishi katika misingi ya kumtumikia Mungu.

Shadya alikuwa kimya, alimwangalia kijana huyo, maneno aliyokuwa akiyazungumza yalimgusa kupita kawaida. Alimpenda, alimthamini, katika maisha yake hapakuwa na mwanaume aliyekuwa akimpenda kama huyo.

Kwa kumwangalia, Shadya alikuwa msichana mrembo mno, alivutia, alikuwa na asili ya Pemba, mweupe, macho ya goroli na kila alipokuwa akicheka ama kutabasamu ilikuwa ni rahisi sana kuviona vishimo vidogo mashavuni mwake.

Weupe wake ulimfanya kuvutia, sura ya kitoto ilimfanya kupendwa na kila mtu katika mtaa huo wa uswahili.

Wanaume wengi walimfuata tangu alipokuwa na miaka kumi na tatu, walihitaji nafasi ndani ya moyo wake, alikuwa mdogo lakini urefu wake ulimfanya kila mmoja kuhisi alikua, alifaa kulalishwa kitandani na kuvuliwa nguo.

Wengi walimmendea, walimtolea macho huku wakitamani hata kuiona miguu yake, ilifananaje, ule weupe uliokuwa ukionekana usoni ulikwenda mpaka miguuni na mapajani, tumboni ama la.

Japokuwa hapo Unguja lilikuwa jambo gumu kwa mwanaume kumsimamisha mwanamke waziwazi na kuongea naye stori za kimapenzi lakini kwa Shadya walishindwa kuvumilia kabisa, hivyo wakajikuta wakianza kufanya hivyo.

Mpaka anafikisha umri wa miaka ishirini na moja Shadya alimvulia nguo mwanaume mmoja tu, naye alikuwa Ngwali ambaye alisimama mbele yake muda huo.
 
SEHEMU YA 02

Kukutana kwao ilikuwa ni humohumo chuoni, wakati Shadya alipokwenda kujiunga na madrasa hiyo, Ngwali alichanganyikiwa, alijitahidi kuwa naye karibu, kumsaidia na mwisho wa siku kuingia kwenye uhusiano wa kimapenzi.

Sheria za dini hazikuruhusu, hata sheria za madrasa hiyo hazikuruhusu hivyo walifanya mambo yote kwa siri huku wakiwa makini kwenye kuepuka siku za hatari kwa msichana huyo.

Japokuwa watu wengi wa huko hawakuamini kama msichana alitakiwa kusoma kipindi hicho lakini mzee Hamduni alikuwa na jukumu la kumsomesha binti yake ili siku moja aje kuwa na maisha yake, apate kazi nzuri na kulipwa mshahara mnono.

Alimkazania kila siku, alitumia pesa zake kuhakikisha anasoma, tena kwa kufaulu vizuri huku wakati mwingine hata wao wenyewe kama wazazi wakijinyima.
Mbali na huyo Shadya pia kulikuwa na kijana wao mwingine, alikuwa pacha wa Shadya, kijana huyo aliitwa Rahim.

Kwa kumwangalia harakaharaka, Rahim alifanana sana na Shadya, alibarikiwa kuwa na uzuri, wasichana wengi walimpenda, wakatamani kulala naye lakini hakukuwa na kitu alichokuwa akikiogopa kama kulala na mwanamke, kama ni kidume basi aliitwa ‘Joka la Kibisa.’

Pamoja na kuwa na umri wa miaka ishirini na moja lakini Rahim aliogopa wanawake waliokuwa wakijipeleka kwake kimahaba, hakutaka kusikia lolote kuhusu wanawake hao na hata walipokuwa wakimwambia kuwa walimpenda, hilo halikumuingia kabisa akilini.

“Rahim niangalie kwanza,” alisema mwanamke mmoja huku akimwangalia Rahim aliyekuwa kwenye kochi. Siku hiyo alishindwa kuvumilia, alimpenda sana kijana huyo kiasi kwamba alikuwa tayari hata kuvunja ndoa yake lakini mwisho wa siku alale naye.

Alivizia muda ambao mume wake alikwenda kazini ndipo akamleta kijana huyo ndani na kumuweka kwenye kochi. Alivua juba lake na kubaki na sketi fupi laini iliyoifanya miguu yake kuonekana mpaka juu ya magoti kidogo na kumwangalia Rahim ambaye hata kusisimka hakusisimka.
20190918_175553.jpg
 
Sehemu ya 03

“Naomba unipoze kiu,” alisema mwanamke huyo ambaye alikuwa kwenye ndoa kwa miezi sita, hata kifua chake kilionekana kichanga, yaani kilisimama dede.

“Allah hapendi!” alijibu Rahim huku akitetemeka.
Mwanamke huyo hakutaka kukubali, akamsogelea pale kwenye kochi na kumshika mkono, Rahim akahisi kama amepigwa shoti ya umeme, kijasho kilikuwa kikimtoka.

“Kwani unaogopa nini jamani?” aliuliza mwanamke huyo huku akianza kuitoa nguo yake ya juu, sasa akabaki kifua wazi.

Japokuwa alikuwa na mvuto wa aina yake lakini kwa Rahim ulikuwa si kitu, hakutamani, hakusisimka, hakuwehuka, hakudata, yaani alipokuwa akimwangalia mwanamke huyo, ni kama alikuwa akimwangalia mwanaume mwenzake, yaani hata suruali yake maeneo ya zipu haikupanda juu.

“Rahim...” aliita mwanamke huyo kwa sauti ya mahaba tele lakini ilikuwa ni sawa na kumpigia mbuzi gitaa acheze na wakati hata kukata viuno hakujua.
“Naomba niondoke!” alisema Rahim.

“Kwa hiyo hutaki kula?”
“Naomba niondoke nitapiga kelele!” alisema mwanaume huyo.
Ilishangaza, ikamshtua sana lakini hakuwa na la kufanya, hivyo akakubaliana naye, akavaa nguo na Rahim kuondoka zake.

Haikuwa kwa mwanamke huyo tu, kwa wengi walifanya kama hivyo lakini hawakuambulia kitu, hawakujua kama Rahim alikuwa na tatizo, jogoo wake hakuwa akiwika na taratibu hisia zake zilianza kuhama, kuhamia upande mwingine kabisa.

Kila alipokuwa akipiga stori na wanaume wenzake walikuwa wakimtania kwamba alifanana na Shadya, alikuwa mwanamke kwa asilimia tisini na tisa ila Mungu alijisahau na kumuumba akiwa mwanaume, hakutakiwa kuwa hivyo.

Walimtania lakini maneno yale yakawa yanajijenga kichwani mwake, akayaamini kwamba kweli Mungu alikosea, alitakiwa kuwa mwanamke kama dada yake.

Hilo likawa kosa, akabadilika na kuanza kuwatamani wanaume wenzake. Lilikuwa jambo baya mno, lilikuwa siri lakini baada ya kupita kipindi fulani, wale ambao walifanikiwa kuwa naye wakatoa siri na hivyo kila mmoja kugundua hilo.

“Umeanza lini?” aliuliza mzee Hamduni kwa ukali.
“Baba nisamehe!”
“Sawa! Ila umeanza lini?”
 
Sehemu ya 04

“Zamani! Walianza kuniambia eti mimi ni mwanamke kama Shadya!” alijibu Rahim huku akionekana kuogopa.

Mzee huyo hakuwa na jinsi, aliumia moyoni mwake, alijua hata kama angemwadhibu Rahim asingeweza kumbadilisha hivyo kuonana na madaktari na kuanza kumpa matibabu na hata ushauri.

Ilisaidia kidogo, alianza kubadilika lakini kila alipokuwa chumbani peke yake alitamani kuwa na mwanaume, ilikuwa dhambi kubwa iliyokuwa ikimtafuna kila siku.

Japokuwa alikuwa katika hali hiyo lakini Rahim alikuwa kijana mwenye akiili mno, alikuwa na uwezo mkubwa darasani. Tangu alipoanza darasa la kwanza mpaka kidato cha sita alikuwa akishika nafasi ya kwanza na dada yake kushika nafasi ya pili.

Na muda huo wawili hao walifaulu vizuri hivyo wazazi wao kuomba uhamisho ili wapelekwe jijini Dar es Salaam na kusoma katika Chuo Kikuu.

Uhamisho ulikubaliwa kwa haraka sana mpaka wakashangaa. Siku chache kabla ya kuondoka kuelekea huko ndipo Shadya akaonana na Ngwali na kumuaga, alimwambia alikuwa akienda Dar es Salaam kusoma.

“Nitakupenda maisha yangu yote,” alisema Ngwali.
“Nitakupenda pia!”
“Naomba usinisaliti!”
“Sitokusaliti! Ninakuahidi hilo!” alisema Shadya huku akiwa na uhakika wa kutokumsaliti mpenzi wake hata kama angetokea mwanaume mzuri kiasi gani.
“Una uhakika?”

“Mbona unaogopa hivyo mpenzi?”
“Dar es Salaam! Jiji la maovu, jiji la ngono! Nalichukia sana. Liliwahi kuniharibia dada yangu, wakamtia mimba, wakamuacha,” alisema Ngwali huku akionekana kuwa na majonzi tele.

Ni kweli alikuwa na hofu, Dar es Salaam ilikuwa Dar es Salaam kweli. Watu walikuwa bize kutafuta pesa ila kwa upande mwingine walikuwa bize kutafuta mapenzi.

Wanaume walipokuwa wakimfuatilia msichana fulani walimfuata kwa uwezo wao wote, walifuatilia kana kwamba walifuatilia kazi TRA, kwa wasichana waliokuwa wakitoka Zanzibar na mikoani wengi waliishia mikononi mwa watu hao, walifanya walichokuwa wakitaka kufanya.

“Sitokusaliti!” alisema Shadya kwa sauti ya chini, iliyomaanisha alichokuwa akikisema.
“Kabisa mpenzi?”
 
Sehemu ya 05

“Niamini! Kama nilivyokuwa bega kwa bega na wewe, nilivyokuwa muaminifu nina hakika nitakuwa hivyo mpaka huko!” alisema.
“Ila ile ni Dar es Salaam baby!”

“Hata ingekuwa Marekani! Shadya na Ngwali milele!” alisema msichana huyo, moyo wa Ngwali ukawa na amani, sasa akaanza kuamini kama kweli mpenzi wake angekuwa mwaminifu katika kipindi chote cha miaka mitatu kusomea masomo ya Uandishi wa Habari.

Baada ya kuzungumza na mpenzi wake, Shadya akaondoka kuelekea nyumbani. Alipofika huko akajifungia chumbani na kuanza kuifikiria safari yake.

Hakuamini kama alikuwa akienda Dar es Salaam, yaani kwenda kusoma huko. Wakati mwingine alihisi kama alikuwa akiota na muda mfupi angeamka na kujikuta akiwa kitandani.

Alitamani kwenda kuishi huko. Ni mara chache kipindi cha likizo alikuwa akielekea kwa shangazi yake aliyekuwa akiishi Ilala hukohuko Dar.

Aliyapenda mazingira ya huko, alipenda kila kitu, mpaka vyakula ambavyo vilipikwa tofauti na watu wa Zanzibar.
“Eti nimsaliti Ngwali! Haiwezekani! Yaani hata kwa dawa,” alijisemea.

“Ila kumbuka ile Dar! Kule kuna watu wenye uwezo wa ajabu sana,” aliisikia sauti yake ikimwambia moyoni.

“Hata kama siwezi!”
“Una moyo huo?” Iliendelea kuuliza.
“Utaona!”
“Si unakumbuka Nusrat alipata mimba!”
“Ni yeye! Ila si mimi.”

“Kweli?”
“Kabisa. Wewe subiri utaona. Hizo siku elfu moja ni chache sana. Nitabaki hivihivi mpaka nitakaporudi Zanzibar na kufunga ndoa na Ngwali!” aliijibu sauti ile.

Na baada ya siku mbili, Shadya na Rahim wakaanza safari kuelekea jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuanza maisha mapya, kusoma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, moja ya sehemu kulipokusanya watu wa kila aina.

Wapole, wababaishaji, mabishoo, masista duu na hata wanaume waliokuwa tayari kuachana na vipindi darasani ila mwisho wa siku wafanikishe misheni zao za kumnasa msichana fulani.
 
Sehemu ya 06

Ndani ya boti Shadya alionekana kuwa na mawazo tele, alikuwa akimfikiria mpenzi wake, Ngwali ambaye alimuacha huko Unguja. Moyo wake ulimpenda kijana huyo kwa asilimia mia moja na muda wote ambao alikuwa humo kwenye boti, alijiambia ilikuwa ni vigumu kumsaliti mwanaume kama huyo.

Mbali na kumfikiria Ngwali, pia alikuwa akifikiria masomo yake, alitamani mno kuwa mwandishi wa habari, alikuwa akijisikia wivu sana kila alipokuwa akiwaona waandishi wadogo wa kike kama yeye wakitangaza kwenye televisheni na redio, kupata umaarufu na kuingiza pesa nyingi.

Alitamani kuwa kama wao, hakutaka kuona akiendelea kuishi kwa wazazi, kwa kipaji cha utangazaji ambacho aliamini alikuwanacho, ilikuwa ni lazima apambane mpaka kuona akitimiza ndoto zake na kuwa mwandishi mkubwa.

“Nitatimiza ndoto zangu halafu nitafunga ndoa na Ngwali,” alijisemea kipindi hicho boti ilikuwa ikiendelea na safari zake.

Baada ya saa tatu, yaani saa tisa alasiri tayari boti ya Azam Marine ilifika katika bandari ndogo ya jijini Dar es Salaam na watu kuanza kuteremka. Hali ya hewa haikuwa na mabadiliko yoyote yale, ilikuwa ni joto kama ilivyokuwa huko walipotoka.

Hapo walipokewa na mjomba wao ambaye aliwachukua na kuanza kuondoka nao kuelekea Ilala alipokuwa akiishi. Mazingira yalikuwa vilevile, hapakuwa na mabadiliko yoyote yale, ilikuwa ni kama walivyokuwa wakija katika siku za nyuma.

Japokuwa Unguja ilikuwa kwao lakini moyo wake ulikuwa na mapenzi ya dhati na Dar es Salaam, alilipenda jiji hilo kwa kuwa aliamini mara unapokuwa humo, mzunguko mkubwa wa pesa unakufanya na wewe kuwa mchakarikaji kama watu wengine.

Kulikuwa na watu wengi waliokuwa wakitoka mikoani na kuelekea Dar es Salaam, walipofika huko, walifanikiwa kwa sababu kulikuwa na idadi kubwa ya watu, kulikuwa na nafasi nyingi za kazi, maeneo ya kufanya biashara zako na mambo mengine mengi, yaani kwa kifupi, Tanzania nzima ilikuwa ikipatikana jiji hapo.
 
Sehemu ya 07

“Mbona shangazi hajaja kutupokea?” aliuliza Shadya huku akimwangalia mjomba wake aliyekuwa mbele akiendesha gari.
“Nimemuacha akifanya baadhi ya kazi nyumbani, ila alitamani sana aje,” alijibu mjomba.

“Nimemkumbuka!” alisema Rahim.
“Amewakumbuka pia! Kwanza hongereni kwa kufanya vizuri kwenye masomo yenu,” alisema mjomba huku uso wake ukiwa na tabasamu pana.

“Tunashukuru! Allah ndiye kila kitu!”
“Ila someni sana, mnajua kwamba nyie ndiyo vichwa vyetu vilivyobaki, yaani sisi hatujasoma, nadhani mnajua hilo, shangazi, baba zenu wadogo kwa wakubwa wote hawajasoma, tunaomba msituangushe,” alisema mjomba huyo.
“Sisi tutasoma sana, tena sana yaani!” alisema Shadya.

Walikuwa wakizungumza haya na yale na baada ya nusu saa wakafika Ilala ambapo wakateremka na kwenda ndani. Siku hiyo ilikuwa ni ya furaha tele, kila mmoja alipenda kuwaona mahali hapo.

Hiyo ndiyo ilikuwa siku ya kwanza kufika hapo Ilala baada ya kumaliza masomo yao, walionekana kuwa na furaha mno, kwa uzuri wa Shadya, wanaume waliokuwa mtaani hapo hawakuacha kumwangalia kwa macho ya matamanio, walimpenda na waliamini alikuwa mmoja wa wasichana waliokuwa warembo mno.

Japokuwa alipenda sana kuvaa mavazi makubwa na marefu kama dela, mabaibui lakini hayo yote hayakulifanya umbo lake zuri kuonekana, alivutia, kiwowowo chake kilikuwa kama pembe la ng’ombe, yaani hata kama kilifunikwa vipi ilikuwa ni lazima kionekane tu.

Wanaume hao hawakuacha kumuita, alivutia lakini Shadya hakuwa na habari nao, alifika Dar es Salaam kwa ajili ya kusoma tu, ukiachana na hivyo, alikuwa na mpenzi wake ambaye hakutaka kabisa kuona akimsaliti, alikuwa tayari kujitoa uhai lakini si kumvulia nguo mwanaume yeyote yule.

“Nimekwishakukumbuka mpenzi,” alisema Ngwali kwenye simu. Pumzi zake zilikuwa zikisikika masikioni mwa Shadya.
“Nimekukumbuka pia!” alisema Shadya.
“Umekumbuka nini kutoka kwangu?” aliuliza Ngwali.

“Sauti yako!”
“Kingine?”
“Muonekano wako!”
“Kingine?”
“Tabasamu lako!”
“Kingine?”
“Jinsi unavyojua kuuchezea ulimi wako mwilini mwangu,” alisikika Shadya.
 
Sehemu ya 08

“Kweli?”
“Kabisa! Huwa ninahisi kuweweseka sana kila ninapokuona mpenzi! Nilikwishasema kwamba huu mwili ni wako, peke yako na hapatotokea mwanaume mwingine wa kuweza kuushika kama ulivyokuwa ukiushika!” alisema Shadya.

“Ila upo Dar kumbuka!”
“Hata ningekuwa Marekani! Bado msimamo wangu utabaki kuwa hivyo,” alisema Shadya.

Walikuwa wakizungumza kila siku, ilikuwa ni lazima kwa wawili hao kuongea usiku, walikuwa wakiambiana jinsi walivyokumbukana, jinsi uhusiano wao huo ambavyo ungedumu na mwisho wa siku kuja kufunga ndoa na kuwa mume na mke.

Siku zilikatika na baada ya kukamilisha kila kitu kwenda kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, hatimaye wakaenda huko na kuanza masomo katika chuo hicho.

Hawakutakiwa kurudi Ilala kwanza, walichukua mabweni ya huko, ndani ya chuo hivyo kama walitaka kurudi Ilala walitakiwa kusubiri mpaka wikiendi.

Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam kilikuwa na wasichana warembo mno, waliokuwa wakijua kuvaa, wasichana ambao mara unapokutana nao kwa mara ya kwanza basi ingekuwa ni rahisi kuhisi umekutana na msichana mrembo kuliko wote katika dunia hii.

Walijua kuvaa, kutembea, kuongea kwa sauti ya kumuibia mwanaume, walijua kumgusa mwanaume, kumpapasa, kumrembua macho na kufanya ujinga wote ambao hata kama angefanyiwa mwanaume aliyejiita kuwa mgumu, mwisho wa siku angeingiza mkono mfukoni na kutoa pochi yake iliyokuwa na pesa.

Wengi wao hawakufikiria masomo, walifika hapo huku wakiwa na mambo mengine kabisa, walifikiria vitu vingine lakini si hasa kile kilichokuwa kimewapeleka mahali hapo.
“Wewe ni wa mwaka wa kwanza?” alisikika msichana mmoja akimuuliza Shadya, walikuwa katika sehemu ya kulia chakula.
“Ndiyo!”

“Oh! Nimejua tu!” alisema msichana huyo huku akiachia tabasamu pana.
“Umejuaje?”
“Unavyovaa!”
“Kwani vibaya?” aliuliza Shadya huku akijiangalia.
 
Sehemu ya 09

“Si vibaya! Ila kama unakwenda kuswali!”
“Eh! Jamani!!!”
“Usijali! Hata mimi nilikuwa hivyo mwaka wa kwanza. Ukifika wa pili, au hata wa kwanza mwishoni utaona mabadiliko makubwa sana,” alisema msichana huyo aliyekuwa akimwangalia Shadya, naye msichana huyo akamwangalia, alivalia sketi fupi na kuyaacha mapaja yake wazi, kwa juu alivaa kiblauzi fulani ambacho kilionyesha nyamanyama za matiti yake.

“Kama yapi?” aliuliza.
Msichana huyo hakumjibu, alikuwa na mambo mengi ya kumwambia lakini hakutaka kufanya hivyo kwa sababu aliamini raha ya ngoma, ingia mwenyewe uicheze.

Masomo yalikuwa yakiendelea, uzuri wa Shadya ulionekana wazi, kila mwanaume aliyekuwa akimwangalia, alipenda sana kuyaweka macho yake kwake tu.

Alikuwa na urembo wa asili, alivutia, alikuwa akinukia vizuri, mikono laini na kila alipokuwa akiangalia na mwanaume yeyote na kugonganisha macho, alijisikia aibu, hivyo kuangalia chini.

Wanaume aliokuwa akisoma nao hawakuacha kumfuata, walitamani sana kuzungumza naye, walihitaji kuisikia sauti yake kwani kwa jinsi alivyokuwa mrembo, waliamini alikuwa na sauti ya kumtoa nyoka pangoni.

Alipokuwa akifuatwa, hakukataa, alijumuika nao na kuongea nao mambo mengi, hasa masomo waliyokuwa wakifundishwa.

Shadya akamuona kila mwanaume ni rafiki yake, hapakuwa na yeyote ambaye alimwambia jambo lolote la mapenzi, walikuwa wakijadili kuhusu masomo kana kwamba wanaume wote hao walikuwa majoka ya kibisa.

Hilo likampa amani, akahisi kabisa kweli watu walikuwa bize kusoma kumbe upande wa pili wanaume walikuwa wakitafuta nafasi nzuri ya kumuingia, mahesabu yao hayakutaka kuishia hapo, walihitaji hata kumpeleka mitaani walipokuwa wakiishi, kwa jinsi Shadya alivyoonekana kuwa mrembo, waliamini hata majirani ambao wangediriki kumuona msichana huyo, wangeshangazwa na uzuri wake.

Hapo chuo akafanikiwa kupata marafiki kadhaa wa kike ila rafiki yake mkubwa akatokea kuwa Diana. Alikuwa mmoja wa wasichana wakimya, alikuwa mwaka wa kwanza lakini alifanya kosa moja kubwa ambalo kwa kipindi hicho hakuona kuwa kosa, pale alipoanza urafiki na msichana aliyeitwa kwa jina la Bupe aliyekuwa mwaka wa pili.
 
Sehemu ya 10

“Ila wewe ni mzuri sana,” alisema Diana huku akimwangalia Shadya.

“Nani?”
“Wewe hapo! Yaani u mzuri mpaka unaboa!” alisema msichana huyo huku akicheka, macho yake yalionyesha kumaanisha alichokuwa akikizungumza.
“Mbona nipo kawaida!”

“Yeah! Hata Malkia Cleopatra naye alikuwa akijiona kuwa kawaida, ni jambo la kawaida pia,” alisema Diana huku akimwangalia Shadya.

“Nashukuru jamani! Ila hujafika Unguja, kuna wanawake wazuri kuliko mimi,” alisema Shadya, akaachia tabasamu la aibu.

Huo ulikuwa ni mwezi wa kwanza chuoni hapo. Mambo yalikuwa moto! Alikipenda sana chuo hicho kwa kuwa kilimchangamsha na kumfanya kuonekana kuwa tofauti kabisa.

Wakati yeye akipata marafiki wapya hata ndugu yake, Rahim naye alipata marafiki wapya kila siku. Alijitahidi sana kujizuia, hakutaka watu wajue kama alikuwa mshirika mzuri wa mapenzi ya jinsia moja.

Alijikaza, kila alipokuwa akitembea, alitembea kiume na wakati mwingine alijilazimisha kuongea sauti nzito.

Yalikuwa ni kama mateso kwake, hakuzoea lakini ilikuwa ni lazima kujikaza ili watu wasijue kama alikuwa na tabia zipi. Siku zikakatika, mpaka mwezi wa pili unaingia, Rahim alijikaza kuonyesha uanaume wake na Shadya alionyesha umwamba wake wa kuwa muaminifu kwa Ngwali aliyekuwa huko Unguja.

“Shadya...” alisikika mwanaume mmoja akiita kwa nyuma kwa sauti ya taratibu.
Shadya aliyekuwa amekaa katika Ukumbi wa Nkurumah, akageuka na kumwangalia mtu aliyemuita.

Alikuwa ni rafiki wake, waliyekuwa kwenye kundi moja la kujisomea, mwanaume mweusi, aliyenyoa kwa staili ya panki kwa mbali, aliyevalia mavazi nadhifu, kijana aliyejua mno kutabasamu, mwenye sura ya upole, aliitwa Gibson.

“Oh! Gibson...” aliita Shadya, akasimama na kumkaribisha mwanaume huyo.
“Mzima lakini?”
“Nipo poa!”
“Nimekupigia sana simu, hupatikani!”

“Mimi?”
“Yaap!”
“Mbona napatikana!”
“Hapana! Hupatikani!” alisema Gibson, hapohapo Shadya akatoa simu yake na kuangalia, ilikuwa imejizima kwa kuishiwa chaji.

“Oh! Kumbe ilizima!”
“Bado unatumia hiyo simu?” aliuliza Gibson huku akiachia tabasamu.
 
Sehemu ya 11

“Gibson sipendi! Ushaanza utani wako!”
“Sasa huoni jinsi hizo simu watu wanavyozikashifu mitandaoni jamani! Kweli msichana mrembo kama wewe unatumia hiyo simu! Kweli jamani!” alisema Gibson huku akianza kutoa kicheko cha chini.

“Kwani kuna tatizo gani?”
“Inashusha hadhi yako! Yaani ni sawa na kumuoa mwanamke mzuri halafu hazai!” alisema.

“Jamaniiiiiiiiiii.....” “Ndiyo! Hebu fikiria umealikwa na rais, halafu kwenye kuchukua namba yako ukatoa simu hiyo! Hahaha...”

“Jamaniiiii! Hebu usitutanie!”
Baada ya utani huo wakaanza kuzungumza mambo mengi, Gibson alionekana kuwa kama kijana safi ambaye hakuwa na papara zozote zile, na alionekana kutokuwa na lengo lolote baya kwa msichana huyo.

Baada ya kuongea kwa robo saa nzima, hatimaye Gibson akaamua kumwambia kitu fulani Shadya ili ampe kazi ya kumanya kutafakari siku nzima.
“Nikwambie kitu Shadya....” aliuliza Gibson, akautoa uso wa masihara na kuuweka ule wa usiriazi.

“Kitu gani!”
“Unazijua gari fulani zinaitwa Range?”
“Ndiyo! Zile za hela nyingi?”
“Yaap! Unaonaje siku moja ukaliona Range kaliiii halafu lina matairi ya Vitz?”

“Unamaanisha nini?”
“Hujajibu! Utaonaje?”
“Nitashangaa....”
“Basi ndivyo ambavyo hata sisi tunashangaa!” alisema Gibson, akasimama kutoka kwenye kiti.
“Unamaanisha nini?”

“Naomba niondoke, tutaonana siku nyingine,” alisema na kuanza kuondoka.
“Gibson! Unamaanisha nini?”
“Nitakwambia next time.....” alisema kijana huyo na kupotea zake.

Shadya akabaki na maswali mengi, hakujua kijana huyo alifikiria vipi, alijiuliza maana halisi ya maneno yale lakini hakuambulia kitu.

Cha kushangaza! Akaanza kuwa na hamu ya kuonana na mwanaume huyo tena na kumwambia maana halisi ya maneno yale.
Alitamani kumpigia simu lakini haikuwa na chaji, alichanganyikiwa, kufuata chaji mpaka bwenini alihisi ni mbali mno.

Hakusoma tena, kila alipojitahidi kufanya hivyo, alishindwa kwani ni Gibson tu ndiye aliyekuwa kichwani mwake, alifikiria zaidi kile alichokuwa amemwambia.
 
Sehemu ya 12

Alipomaliza kusoma, akatoka na kuelekea bwenini, alipofika huko, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuchaji simu yake, halafu kuanza kuitafuta namba ya Gibson, kitu cha ajabu, hakuweza kuiona.
“Ilikuwa humu! Eeh! Imefutika?” alijiuliza.

Hakutaka kukubali, akampigia simu Diana na kumuomba namba ya Gibson kwani alikuwa na uhitaji nayo sana.
“Wewe ya nini tena?” aliuliza Diana.

“Nataka nizungumze naye!”
“Are you guys in love?” (mpo kwenye mapenzi?)
“Nope! I wanna talk to him, pleaseeee...” (Tafadhali...nataka kuzungumza naye)
“What is it about?” (kuhusu nini?)
“About something...” (kitu fulani)
“Is it love?” (ni mapenzi?)

“I said no! Something else...” Nilisema hapana! Kitu kingine) “Sawa mama! Ila kuwa makini na moyo wa Gibson, nilichokisikia juu yake, kinasikitisha mno,” alisema Diana, wakati Shadya alipotaka kuuliza kuhusu hicho alichokisikia rafiki yake kuhusu huyo Gibson, simu ikakatwa na baada ya sekunde chache meseji iliyokuwa na namba ya Gibson ikaingia kwenye simu yake.

Sasa kukawa na vitu viwili alivyokuwa navyo, na alitamani sana kuvisikia. Kitu cha kwanza kilikuwa ni kuhusu yale maneno aliyomwambia kule kwenye ukumbi lakini kitu cha pili kilikuwa ni kutaka kufahamu kwa undani kile alichoambiwa na Diana.

Akabaki katikati, hakujua ni kitu gani hasa alitakiwa kuuliza. “Labda nianze na hili la Gibson kuhusu ule msemo wake, halafu nitamuuliza Diana kuhusu huyu kijana! Kuna mambo gani hapo?”

alijisema huku akionekana kuingia kwenye dimbwi la mawazo kwa vitu ambavyo havikumuhusu kabisa, na hapakuwa na ulazima wa kuyajua.

Hapo akaanza kukaribishwa jijini Dar es Salaam, kwa watu waliokuwa na mbinu za kila namna pale walipokuwa wakihakikisha msichana fulani ilikuwa ni lazima walale nae.

“Gibson! Upo wapi?” aliuliza Diana.
“Nyumbani!”
“Kwani unaishi kwenu?”
“Ndiyo! Si unajua nafanya kazi!” alisikika mwanaume huyo.

“Unafanya kazi?”
“Ndiyo! Huku nasoma!”
“Mwaka wa kwanza?”
“Ndiyo! Kwani ni ajabu Shadya?”
“Hapana! Si ajabu.”
“Kwanza namba yangu umeitoa wapi?” “Nilikuwa nayo!”
 
Sehemu ya 13

“Haiwezekani hata kidogo!”
“Kwa sababu gani?”
“Namba yangu huwa haichukuliwi na watu wanaotumia simu zenu,” alisikika mwanaume huyo.

“Jamaniiii! Yaani bado unatuponda tu!”
“Ndiyo! Nitafanya hivyo mpaka nitakapokuona unabadilika na kununua simu nyingine!” alisema mwanaume huyo.
“Sasa wewe unataka nitumie simu gani?”
“iPhone!”

“Mh! Nitaweza kuwa nayo?”
“Kwa nini ushindwe! Umeingia chuo kumbuka, kuna mikopo kama yote!”
“Najua! Ila si natakiwa nifanyie mambo mengine!” “Kama yapi?”
“Tuachane na hayo! Niambie kuhusu kile ulichokuwa umeniambia darasani....”
“Kipi?”

“Ule mfano wa gari na matairi, ulikuwa unamaanisha nini?” aliuliza Shadya huku akitoa tabasamu.

“Halooooo...” alisikika Gibson akiita.
“Halo! Nasema niambie sasa...”
“Halooo...Shadya...halooo...”

“Gibson....”
“Haloooo...”
Mara simu ikakatwa, alipojaribu kumpigia, haikuwa ikipatikana.
“Shiiiiiiiit....” alijikuta akisema Shadya kwa hasira, akagundua kwamba Gibson alimfanyia makusudi, alimsikia ila akajifanya kama hakuwa akimsikia vile.
 
Sehemu ya 14

“Diana, niambie kitu kimoja!”
“Kitu gani?”
“Kuhusu rafiki yako!”
“Yupi? Ninao wengi!”
“Namaanisha yule kipenzi kabisa!”
“Shadya?”

“Ndiyo!”
“Amefanya nini?”
“Hivi unauonaje ule uzuri wake?”
“Kwani upoje?”

“Yaani nyie wanawake hamuwaonagi wenzenu walivyokuwa wazuri ama kiburi cha uzima tu? Hahaha!” “Mtoto wa Kipemba yule!”

“Ni mashallah! Nataka nipite!”
“Unamaanisha nini?”
Yalikuwa ni mazungumzo ya watu wawili, Gibson aliyekuwa akizungumza na Diana, rafiki yake na Shadya.

Walikuwa wamekaa sehemu fulani na kuanza kumzungumzia msichana huyo mrembo, alikuwa na mvuto wa aina yake, kila wanaume walipokuwa wakimwangalia, walimpenda na kumuona kuwa msichana wa aina yake kabisa.

Wanaume walimfuatilia, na miongoni mwa wanaume hao alikuwa Gibson. Alimpenda, alivutiwa naye lakini aliona kuna ugumu mkubwa wa kumpata kwani endapo angemuingia kichwa kichwa, asingefanikiwa kumpata hata kidogo.

Alitakiwa kuwa na akili ya aina yake, kumfuatilia kwa mtindo ambao kusingekuwa na mtu yeyote ambaye angegundua, si hao tu bali hata Shadya mwenyewe asingegundua kama alikuwa na lengo hilo.

Kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuuteka umakini wake. Kumtia hamu na kumfanya kuwa na hamu ya kuonana naye.

Huo ndiyo mtihani wa kwanza ambao wanaume wengi walifeli, waliwafuatilia wanawake kihovyohovyo na mwisho wa siku kuambuliwa kukataliwa, kama mwanaume unayejitambua, unapomtaka msichana fulani ni lazima uwe na mipango yako madhubuti na kufanikiwa kukaa naye chumbani, tena kitandani.

Silaha ya kwanza ilikuwa ni kulijua jina la mwanamke, kumuonyesha kwamba alikuwa maarufu, alijulikana kila kona, ni njia nzuri ambayo kama akifuatwa msichana yeyote yule na mwanaume asiyemjua, ilikuwa ni lazima ampate hata kama ni mgumu kama chuma.

Alimfahamu Shadya, walikuwa wakijuana, hivyo njia hiyo haikuwa sababu ya kumfanya kuwa wake, kulikuwa na plan B ambayo alitakiwa kuifanya kuhakikisha anampata, na hiyo ilikuwa ni kumuwekea umakini, hamu ya kuonana naye kutokana na maswali aliyokuwanayo juu yake.
“Hii ni njia nzuri sana,” alijisemea huku akimwangalia Diana.
 
Sehemu ya 15

“Njia gani?”
“Kumpata Shadya!”
“Sasa kuna ugumu gani kwani?”
“Wewe uliniambiaje mwanzo?”
“Kwamba ana mtu wake!”

“Yaap! Kuna njia za kuwafuata wasichana waliokuwa na watu wao, wale waliokuwa singo, walioolewa, wanaofanya kazi benki na sehemu nyingine, na pia kuna njia za kuwafuata hata wale wanaofanya kazi ya mama ntilie!” alisema Gibson maneno yaliyomfanya Diana kunyamaza kwanza.

“Mh!” akaguna.
“Unaguna nini?”
“Hayo unayoyasema! Kwa maana hiyo kuna njia mpaka ya kunipata mimi?” aliuliza Diana.

“Ndiyo! Tena wewe ni kesho tu tungekuwa gheto tunafanya yetu...Hahaha...” alisema Gibson na kuanza kuchak.
“Hebu nitolee ujinga wako!”
“Diana! Ninamtaka Shadya! Ninataka kuiteka akili yake kwa kitu kimoja tu!”
“Kipi?”

“Kuipa maswali ya jambo fulani, awe na hamu ya kunitafuta kila siku,” alisema Gibson.

“Ipi?”
“Hebu naomba namba yake,” alisema Gibson, Shadya akashangaa kwani walikuwa kundi moja chuoni, sasa kwa nini hakuwa na namba yake.

“Kwani wewe huna?”
“Acha uswahili! Unadhani ningekuwa nayo ningekuomba?” aliuliza Gibson, Shadya akampa namba hiyo.

Gibson akaichukua na kuondoka zake, kichwa chake kilikuwa na jambo moja, ilikuwa ni lazima amtafute Shadya na kuanza kumfuatilia kwa njia ambayo alikuwa ameipanga.

Hakuona ugumu kabisa, alimtafuta na alipompata ndipo akampa suala la gari la Range kuwa na tairi la Vitz.

Hilo likaanza kumsumba Shadya kichwani, akahisi kabisa kijana huyo kulikuwa na kitu cha umuhimu alichokimaanisha hivyo kuanza kumtafuta ili amwambie alimaanisha nini.

Huo ulikuwa mtego namba moja, ilikuwa ni lazima atafutwe kwanza, kwa kipindi fulani, aanze kuleta mapozi, amringie lakini mwisho wa siku amuite sehemu ambayo hata kwa dawa asingeweza kuchomoka.

“Gibson! Hivi unaniona mimi bibi yako!” alisema Shadya, alijifanya kukasirika, walikuwa wakiongea kwenye simu.
“Kwa sababu gani?”

“Kwa nini hutaki kuniambia!”
“Siwezi kwa sababu kila mwanaume chuoni atanishangaa wakijua nimekwambia!” alisema Gibson, maneno hayo yakazidi kumpagawisha Shadya.
“Wanaume wa chuo?”
 
Sehemu ya 16

“Ndiyo! Wote wanajua, na wanakushangaa sana! Aiseee! Hivi ni kweli Shadya?” aliuliza Gibson, ili kumtia presha, akakata simu.

Moyo wa msichana huyo ukawa na presha kubwa zaidi, alihisi kulikuwa na jambo kubwa lililokuwa likiendelea ambalo Gibson hakutaka kumwambia hata kidogo, akaanza kuogopa na kuanzia siku hiyo akaanza kukosa amani, kila alipomuona mwanaume hapo chuo, akahisi naye huyu alikuwa akijua.

Hilo likamfanya kila siku alipokuwa akitoka darasani tu, alikimbilia bwenini na kujifungia, hakutaka kutoka, hakutaka kuonekana kwani tayari moyo wake ulionekana kuwa na hofu.

Alikaa chuo, alimsubiri Gibson ili aje kumwambia ukweli lakini kijana huyo hakutokea. Kichwa kikawa na mawazo, sasa akawa hamfikirii sana Ngwali, mtu aliyekuwa akimfikiria alikuwa Gibson, na mbaya zaidi alitamani sana kupokea simu ya kijana huyo kuliko hata ya yule mpenzi wake.

“Gibson! Why?” alijiuliza kila siku.
Baada ya siku tatu, Gibson akatokea hapo chuo, Shadya alipomuona tu, akamkimbilia, siku hakutaka kabisa kumuacha kijana huyo, ilikuwa ni lazima aambatane naye na kumwambia alichokuwa akikimaanisha ambacho kilimpa maswali mengi.

“Niambie!”
“Sina muda. Nimekuja mara moja tu, ni jambo kubwa, si la kuzungumza kwa dakika moja ama kumi,” alijibu Gibson, tena alijifanya kuwa bize mno.
“Mbona unaonekana una haraka?”
“Nataka kuondoka! Nimekuja mara moja tu!”

“Sasa ndiyo hutaki kuniambia?”
“Nitakwambia hata kesho!”
“Hapana! Ninataka leo!”
“Basi ngoja niende sinema kuna muvi mpya imetoka, nitakwambia!”
“Hapana! Twende wote, ninataka mpaka uniambie,” alisema Shadya.

Gibson akabaki kimya, hicho ndicho alichokuwa na hamu ya kukisikia, hapakuwa na tatizo, akamchukua na kwenda naye Mlimani City ambapo hapo akakata tiketi ya muvi ya saa kumi na mbili na kungia.

Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa msichana huyo kuingia humo, alishangaa, hakuzoea kuona mambo hayo alipotoka, aliburudika, aliona kama ameonyeshwa ulimwengu mwingine wa maisha ya binadamu.
 
Sehemu ya 17

Waliangalia mpaka saa mbili na nusu, Gibson akaongezea na kuangalia nyingine mpaka mishale ya saa nne, walipomaliza, wakatoka.

Shadya akamzoea Gibson, na hata mpenzi wake alipokuwa akipiga simu, hakutaka kupokea, alihitaji kuambiwa kile alichohitaji kuambiwa na kijana huyo lakini pia la zaidi lilikuwa ni kutamani sana kuendelea kuwa naye kwani alimuonyesha ulimwengu mwingine kabisa.

“Twende Sinza!” alisema Gibson.
“Kufanya nini?”
“Kula! Au umekula?”
“Bado!”
“Basi twende!”

Wakaondoka na kuelekea huko, walikuwa wakizungumza mambo mengi. Kwenye maneno yote hayo Gibson hakutaka kumficha Shadya, alimwambia jinsi alivyokuwa mzuri, alivyovutia na kuonekana kuwa mwanamke mwingine wa tofauti kabisa.

“Shadya! Nimeona wanawake wengi, ila wewe ni wa tofauti kabisa,” alisema Gibson huku akitembea na msichana huyo.

“Kwani mimi nipoje?”
“U mzuri, mtanashati, unajua kuvaa, unapendeza sana,” alijibu Gibson maneno ambayo yalimfanya Shadya kujisikia mtu wa tofauti.

“Hebu toka huko!”
“Shadya! Ninakwambia ukweli! Hebu jiangalia ulivyo! Kila mwanaume anajisikia raha kuwa na mwanamke kama wewe. U mrembo sana, unaongea vizuri, lipsi zako zinavyochezacheza, hakika hakuna mwanaume ambaye anaweza kuthubutu kutoa macho yake kuangalia pembeni!” alisema, alizidi kuongeza sifa.

“Ndivyo unavyojidanganya!”
“Shadya! Unajua kwa nini nimekuomba tukaangalie muvi?” aliuliza.

“Sikukuomba! Nilitaka mwenyewe!”
‘Sawa! Kwa nini kwako nimekuwa mwepesi sana kukubali?” aliuliza.
“Mh! Sijajua!”
“Ni kwa sababu ya jinsi ulivyo!”
“Nipoje?”

“Nimekwishakwambia kwamba u mzuri sana. Uliona watu walivyokuwa wakikuangalia pale tulipokuwa kwenye viti kusubiri kuingia ndani?” aliuliza, kiukweli hapakuwa na watu waliokuwa wakimwangalia, ila aliongeza chumvi kwa kuwa alijua msichana huyo hakuwa makini.

“Walikuwa wakiniangalia?”
“Ndiyo! Sikufanya makosa kwenda na wewe. Shadya! Unajua kuvaa, sura nzuri, hutumii make up, unajijali, una mvuto wa aina yake, hakika hata siku nikiambia niwe na msichana mrembo, hakika nitakuchagua wewe,” alisema Gibson.
“Shindwa!”

“Shadya! U mzuri mno mno mno....” alisema Gibson.
 
Sehemu ya 18

Japokuwa alijifanya kukaza lakini moyo wake ulijisikia tofauti kabisa. Alimzoea Ngwali, alikuwa mpenzi wake lakini hakuwahi kumsifia kama alivyokuwa akimsifia Gibson muda huo.

Maneno ya mwanaume huyo yalibadilisha kila kitu na kujiona mtu mpya, aliyezaliwa kwa mara ya pili na kuhisi katika dunia hii hapakuwa na msichana aliyekuwa mzuri kama yeye, hapakuwa na msichana aliyekuwa akijua kuvaa kama alivyokuwa akivaa.

Gibson alikuwa akimsikilizia pumzi zake tu, alitamani kusikia ni kitu gani angesema msichana huyo, alipoona maneno hayo yamemuingia, sasa ukawa muda wa kutaka kufanya jambo moja kuona kama angemkatalia, akaupeleka mkono wake na kuushika mkono wa msichana huyo, hakugoma.

“Una mikono lakini sana, laini mno!” alisema Gibson.
“Mbona kawaida!”
“Na inanukia mno! Unatumia mafuta gani?”

“Ya nazi!”
“Oh! Ni mazuri sana! Sijawahi kumshika mwanamke mwenye mikono laini kama yako!” alisema Gibson, Shadya akajikuta akichekacheka tu.

Wakafika mpaka Sinza, kila mmoja aliona kama wamewahi kufika, wakaingia kwenye mgawa mmoja na kuanza kula chakula. Muda wote huo kazi ya Gibson ilikuwa ni kumsifia Shadya tu, jinsi alivyokuwa mrembo, alivyokuwa na mvuto wa aina yake.

Msichana huyo alijisikia furaha mno moyoni mwake, hakuamini kama sifa zote hizo alikuwa akisifiwa yeye, wakati mwingine alijiona mrembo zaidi ya Alicia Keys ama Mila Kunis.

“Gibson! Unaniangalia sana mpaka naona aibu!” alisema Shadya wakati alipogundua kijana huyo alikuwa akimwangalia kwa zaidi ya dakika tatu nzima..

“Najaribu kuuangalia utaalamu wa Mungu! Alikuumba akiwa kwenye utulivu wa hali ya juu,” alisema kijana huyo.
“Unajua unanifanya nisikie aibu!”
“Shadya!”
“Abeee...”
“Nakupenda!” alisema Gibson! Msichana huyo akabaki kimya.

“Umenisikia?”
“Ndiyo! Ila nina mtu wangu!”
“Sijakwambia umuache, ni mwanaume mwenye bahati sana, endelea naye tu! Ila jua kuna mtu anakupenda!” alisema.
Hiyo ilikuwa njia ya pili aliyokuwa ameitumia.

Kwa mwanaume hakutakiwa kuonyesha chuki kwa mwanaume aliyekuwa na mwanamke aliyekuwa akimpenda, bali alitakiwa kumpongeza kwa kumuona mtu aliyekuwa na bahati sana.
 
Sehemu ya 19

Hilo likamfanya Shadya kuona kama mtu huyo hakuwa na lengo lolote kwake, yaani alikuwa innocent kabisa. Sasa moyo wake ukaanza kuwa tayari kwa lolote kwa kijana huyo.

“Kila mwanaume anapenda kuwa na mwanamke mzuri, kama jinsi ulivyokuwa,” alisema Gibson, akajiona kule alipokaa kuwa mbali, akamsogelea karibu, miguu yao ikaanza kugusana.

“Unamaanisha nini?”
“Jiangalie jinsi ulivyo, ulivyokuwa na ngozi laini,” alisema Gibson, akauchukua mkono wake na kuupeleka kwenye upaja wa Shadya, alivalia baibui kubwa jeusi.
“Oh! Unafika mbali sasa!”

“Hapana! Ninatamani kukugusa kila kona, una ngozi laini sana, unanukia vizuri mno! Shadya! Ninakupenda mno! Sijajua ni kwa namna gani natakiwa kukwambia hili,” alisema Gibson, akaanza kuupeleka mkono huku na kule kwenye paja lile, halafu akamuachia.

“Unanipa majaribu sana! Hebu niambie kuhusu mfano wa gari!”
“Nitakwambia tu! Shadya! Wewe ni msichana mzuri! Jua hilo!”
“Umeniambia tayari!”

“Wewe ni gari la kifahari, wakati mwingine unatakiwa kutumia vitu ambavyo vinadhihirisha uzuri wako!” alisema Gibson.

“Kama vipi?”
“Simu na vitu vingine!”
“Gibson!”

“Simaanishi kwa ubaya! Shadya! Unapendwa na wengi sana chuoni, yote ni kwa sababu ya uzuri wako! Naomba umalize haraka nikurudishe!” alisema Gibson.

“Chuo?”
“Ndiyo!”
“Nimechelewa sana!”
“Unataka kwenda wapi?”
“Popote ila si chuo!”

Gibson akakaa kimya kwa sekunde kadhaa. Hapo kukaja kitu kingine kichwani mwake, ulikuwa ni muda wa kumuonyesha Shadya kwamba alikuwa gentleman, hakutakiwa kuwa na haraka.
 
Sehemu ya 20

Alikuwa na uwezo wa kumchukua na kumpeleka nyumbani kwao, lakini akajiuliza kama lingekuwa jambo jepesi ama la, kwani kwa mwanaume kuvumilia usiku mzima ilikuwa ni kazi kubwa.

“Au nifanye naye? Ila akikataa? Nitaanza kuona noma na mwisho wa siku nitaomba nisionane naye! Ngoja nivumilie,” alijisemea.

“Basi twende nyumbani!”
“Kwenu?”
“Yaap!”
“Kuna chumba cha wageni?”
“Hapana!”
“Sasa nitalala wapi? Sebuleni?”
“Hapana! Chumbani kwangu!”
“Na wewe?”

“Humohumo!”
“Hapana!”
“Shadya! Kuna mengi huwa yanatokea, ila naomba uchukue saa ishirini na nne tu katika maisha yako uniamini,” alisema Gibson.

“Mh!”
“Pleaseeee...”
“Nimwamini mwanaume?”
“Ikiwezekana! Hata kama wote huwaamini! Mwamini Gibson basi!” alisema.

Shadya akajifikiria kwa dakika kadhaa, akakubali na hivyo kuondoka mpaka alipokuwa akiishi kijana huyo, wakaingia ndani, akaandaliwa maji ya kuoga, akaoga, akakaribishwa kitandani na kulala.

Hakupata usingizi, muda wote mawazo yake yalikuwa yakimfikiria huyo mwanaume, ni kwa namna gani angeweza kuvumilia kulala naye mpaka asubuhi pasipo kumgusa, lakini hakuamini mpaka asubihi ilipofika, hakuguswa, akaamshwa, akaelekea bafuni, akaoga na baadaye kurudi chuoni, kila alipomfikiria Gibson, hakumpatia majibu, hakujua kama mwanaume huyo alikuwa na hesabu zake, na kwa kifupi, kabla ya kumuonyeshea madhara, alitakiwa kumwamini.

Hiyo ilikuwa njia ya tatu kumnasa msichana. Ufanye moyo wake uingie na imani kubwa juu yako.


Je, nini kitaendelea?
 

Similar Discussions

7 Reactions
Reply
Back
Top Bottom