Simulizi: Nyumba Iliyojaa Dhambi

NYEMO CHILONGANI.
NYUMBA ILIYOJAA DHAMBI
0718069269

Sehemu ya Pili.

Nilichanganyikiwa, sikujua ni kitu gani nilitakiwa kufanya ili niingize pesa kabla ya siku husika kufika. Niliumiza kichwa changu kwani kiasi cha shilingi elfu tano kwa siku kilikuwa kidogo sana kiasi kwamba kisingeweza kunisaidia kwa lolote lile.
Wakati nikifikiria sana ndipo nikakumbuka kwamba hapo katika Mtaa wa Kongo kulikuwa na uhaba wa walinzi wa kulinda eneo hilo, wale wachache waliokuwa wakilinda walilipwa kiasi cha shilingi elfu kumi kila siku asubuhi.
Nakumbuka niliwahi kuulizwa kama niliitaka kazi hiyo kipindi cha nyuma, niliikataa kwa kuwa niliamini ningekuwa nachoka sana, ila kwa sababu huyo Aisha nilimwambia Ijumaa ilikuwa ni siku ya kuonana na kwenda kula pizza, basi niliona hiyo kazi ilinifaa sana.
Nikaelekea katika ofisi moja iliyokuwa hapohapo ambayo ilikuwa chini ya mzee Juma, nilizungumza naye na kumwambia kwamba niliitaka kazi hiyo. Kuipata haikuwa kazi kwani alinifahamu, nilikuwa mtu wa hapohapo hivyo akanipa nafasi hiyo na kuniambia nianze siku hiyo.
Moyo wangu ukafarijika, na mpango wa kwanza kabisa kabla ya kupanga maisha ilikuwa ni kwenda mtoko huo na Aisha, ilikuwa ni lazima nimuonyeshe kwamba nilikuwa na uwezo mkubwa wa kumchukua msichana na kwenda naye sehemu.
Siku zilikwenda taratibu sana, kwa kuanzia Jumatatu mpaka Alhamisi ilimaanisha kwamba ningepata kama shilingi elfu arobaini kupitia kazi ya ulinzi lakini pia ningepata shilingi elfu ishirini kwa kazi ya usafi, kwa maana hiyo mpaka Ijumaa nilitegemea kuwa na shilingi elfu sitini mfukoni.
Kwa mwaka huo wa 2016 zilikuwa pesa nyingi kutokana na hali ya uchumi, maisha kubana hivyo niliamini kwamba siku hiyo ningefaidi sana na Aisha na kubwa zaidi ni kwamba ningeonekana kwamba nilikuwa na pesa na hakukuwa na chochote cha kunibabaisha.
Wakati nikifikiria kuhusu Aisha, kichwa changu kilikuwa kinaniuma mno kila nilipofikiria kuhusu Issa, niliamini kwamba alinizunguka na kutembea na msichana huyo kwani lisingekuwa jambo jepesi kumuona akichangamkiana naye na wakati niliamini hawakuwa wameonana kabla.
Hilo sikutakiwa kuhofu sana kwa kuwa niliamini kabisa kwamba mara baada ya kuwa naye faragha basi huyo Issa asingemfikiria kabisa kwa sababu nilijiamini kupita kawaida.
“Ila subiri! Cha msingi ni kumuonyeshea mapenzi makubwa,” nilijisemea.
Wakati hayo yote yakiendelea bado sikuacha shobo zangu kwa wanawake wengine waliokuwa wakija hapo Kariakoo kufanya manunuzi yao mbalimbali, nadhani nilikuwa mtu niliyeongoza kusalimia kuliko watu wengine Tanzania. Macho yangu yalikuwa magumu kuvumilia kila nilipokuwa nikiwaona wanawake wazuri ilikuwa ni lazima niwafuate na kuanza kuongea nao kidogo.
Hayo ndiyo yalikuwa maisha yangu kabla ya kufanikiwa. Mpaka leo ninapokaa na kukumbuka miaka miwili nyuma, maisha yalivyobadilika na kuwa hivi yalivyo, huwa ninaamini kabisa Watanzania tunabaki masikini kwa sababu tu hatuna mitaji, hatuna pesa za kuanzia biashara na ndiyo maana tupo hivi.
Sikuacha kumfuata Issa na kumuomba simu yake kuzungumza na Aisha, alinipa na kuongea naye sana na hata siku ya Ijumaa ilipofika, akaja palepale alipokuwa akinikuta, nilimchukua na kuondoka naye.
Njiani nilikuwa nikiongea naye, mfukoni nilikuwa na shilingi elfu arobaini kwani nyingine nilitumia kwenye matumizi yangu mengine.
Hatukuchukua muda mrefu tukafika sehemu ya kununulia pizza na kununua kisha kuondoka, tulikula huku tukitembea, siku hiyo nilijiamini kuliko siku nyingine na nilichokihitaji kilikuwa kulala na Aisha tu.
Kwa Kariakoo nisingeweza kupata chumba kwa kuwa ilikuwa ni gharama sana hivyo kama kweli nilihitaji kufanya naye basi haikuwa na jinsi kuondoka kuelekea Magomeni au Manzese.
Sikutaka kujificha, mwili wangu ulikuwa ni kama umewaka na hakukuwa na kitu cha kunizuia kufanya mambo yangu, nilimwambia ukweli kwamba network ilikuwa ikisoma na nilichohitaji ni kulala naye.
Aisha alinizoea sana, akaniambia kwamba hakuna tatizo, kama nilikuwa na hela ya kumtoa basi hakukuwa na shida. Hapo nilipata swali moja, huyu Aisha alikuwa akijiuza ama kwa sababu kwa msichana wa kawaida angeniacha mimi nifanye naye halafu mambo ya kupeana pesa yangekuja baadaye.
“Kiasi gani unataka?” nilimuuliza huku nikimwangalia usoni.
“Yoyote ile, isiwe elfu kumi, isiwe chini ya elfu kumi,” aliniambia huku akitoa tabasamu lililonimaliza kabisa.
Mfukoni nilikuwa na shilingi elfu ishirini na tano hivyo hakukuwa na tatizo, nikamchukua na kwenda Mburahati ambapo kulikuwa na nyumba ya wageni ya bei rahisi na kumalizia mambo yetu humo.
Wanawake wa mjini wanapenda pesa, kama hauna pesa, huwezi kumpata msichana yeyote yule. Hebu fikiria, mwanamke kama Aisha nilitumia kiasi cha pesa ambacho kwangu kilikuwa kikubwa mno, hii inamaana kwamba unapokuwa na pesa basi una uwezo wa kufanya mapenzi na msichana yeyote uliyekuwa ukimtaka.
Hilo likanifanya kuendelea kuuchukia umasikini, sikuamini kwenye kufanya kazi kwa bidii ndipo ufanikiwe, siku zote niliamini kwamba utajiri ni bahati tu, mtu anaweza leo akawa masikini na kesho akaamka na kuwa tajiri mkubwa.
Niliamini kwamba kuna siku ningetajirika sikujua ni siku gani lakini niliamini kwamba kuna siku tu ingetokea ningefanikiwa na kuwa tajiri mkubwa.
Niliporudi Kariakoo nikaanza kumwambia Issa kwamba nilifanikiwa kumalizana na Aisha, kwa jinsi alivyoonekana tu niliamini kwamba hakuwa mtu mzuri, hakuitikia kwa furaha, alionekana kama kuchomwa na kitu chenye ncha kali moyoni mwake.
Hilo likanipa uhakika kwamba Issa alitembea na Aisha, nilikasirika sana, kwa jinsi tulivyokuwa marafiki sikuamini kama angeweza kufanya kitu kama hicho.
Aliniumiza, wakati yeye akicheka, moyoni mwangu kulikuwa na majonzi makubwa, sikutaka kukubali, kama yeye alitembea na msichana ambaye alijua kwamba alikuwa wangu, akaniumiza basi na mimi ilikuwa ni lazima nimuumize.
“Nitamuumiza, kuna siku nitatembea na dada zake wawili, halafu nitatembea na demu wake,” nilijisemea.
Urafiki wetu ukaendelea lakini haukuwa kama kipindi cha nyuma, yaani siku ambayo nilikwenda kulala na Aisha ndiyo ilikuwa siku iliyobadilisha kila kitu.
Niliendelea kufanya kazi, sikuwasiliana tena na Aisha kwa sababu hata simu Issa hakutaka kunipa kwa kuniambia kwamba alikuwa bize nayo. Kwani simu shilingi ngapi bhana? Nilijidunduliza na kununua yangu, tena ilikuwa ile ya kupangusa.
Huko, nikafanikiwa kuwasiliana na Aisha kwa WhatsApp, tulikuwa tunaongea mengi, aliniambia kuhusu Issa kwamba alikuwa akimfuatilia sana kiasi kwamba mpaka ikawa kero.
“Ikawaje?” nilimuuliza.
“Ikawa hivyohivyo...yaani alikuwa kero,” aliniambia.
“Ikawaje? Yaani namaanisha baada ya kero zake, nini kilifuata?” nilimuuliza.
“Nilifanya naye mapenzi, alinishawishi sana, aliniambia kwamba wewe ni masikini, huna pa kulala, unalala kwenye maduka, unapenda kujipendekeza kwa kila mtu ili upate pesa,” aliniambia.
“Yaani Issa alikwambia yote hayo?”
“Ndiyo! Nadhani hiyo ilikuwa sababu ya kulala naye. Naomba unisamehe,” aliniambia, nilishikwa na hasira mno lakini sikuwa na la kufanya.
Sikumlaumu Aisha, alikuwa msichana aliyekuwa akitafuta mwanaume mwenye pesa, mimi sikuwa nazo, nilikuwa masikini hivyo kama kulikuwa na mwanaume alimfuata kwa kisingizio cha pesa niliamini mwanamke yeyote yule angeweza kudanganyika.
“Ila huyu Issa, ni lazima nitadili naye,” nilijisemea huku nikionekana kuwa na hasira.
Niliona kama nachelewa kupata mafanikio, mtu wa kwanza ambaye nilitakiwa kufanya mikakati ya kuwa naye alikuwa Shamila. Huyu ndiye yule mdogo wake na Issa ambaye nilimtamani sana kwa kuwa niliamini baada ya Issa kugundua kwamba nimelala naye basi angenichukia maisha yake yote. Hiyo ndiyo ilikuwa maana ya kisasi.
Nikaanza kupiga ndogondogo, nikaanza kuzungumza naye kila siku kwa furaha, nilichangamka kiasi kwamba mpaka yeye mwenyewe alinishangaa.
“Mkeka wako umetiki nini?” aliniuliza huku akiniangalia.
“Kwa nini?”
“Unaonekana una furaha sana!”
“We’ acha tu. Ila Shamila wewe mzuri sana,” nilimwambia huku nikimwangalia.
Alichukia, hiyo ndiyo ilikuwa kawaida yake. Shamila alijua kabisa kwamba nilimpenda tangu zamani ila hakutaka kunikubalia kwa sababu tu alijua sikuwa na pesa, sikuwa na makali yoyote yale ya kumfanya mtoto wa kike anikubali.
Bila kunificha akaniambia kwamba hanipendi, tena nisifikirie kuwa naye hata kidogo. Unadhani niliumia, walaaa! Shamila alikuwa msichana mrembo, kusema kwamba sikustahili hata kutembea naye kwangu mimi ilimaanisha kuwa nitafute pesa, nikipata nimtafute.
Kulipa kisasi kwa Issa ilihitaji nguvu kubwa, haikuwa kirahisi kama ilivyokuwa ikionekana, ilikuwa ni lazima nipambane kuhakikisha napata maisha mazuri kama watu wengine, halafu ndiyo nimfuate.
Wanawake waliendelea kufurika Kariakoo, walikuwa wengi mno tena waliokuwa wakipendeza kupit kawaida. Sikuacha kuwasalimia, kila siku niliamini kwamba ili uwapate wanawake wazuri basi hukutakiwa kuwahofia hata kidogo.
Siku ziliendelea kukatika, niliendelea kuwasiliana na Aisha na kuonana naye sana. Alinipenda, si kwamba nilikuwa mzuri ni kwa sababu niliwahi kufanya naye mapenzi.
Nilimzoea, kikafika kipindi akayajua maisha yangu, hata alipokuwa akija na kumwambia kwamba sina pesa, hakuwa akilalamika kwani nilimwambia kila kitu na akatokea kunikubali kwa maisha niliyokuwanayo.
Mishemishe zangu za kumtafuta Shamila hazikukoma, kila siku nilimwambia maneno yale yale kwamba nilimpenda lakini hakutaka kunielewa hata kidogo.
Nilipoona nimeshindwa, nikasema si kesi kama nikiamua kumfuatilia mdogo wake Halima ambaye alikuwa akifika hapo mara chache sana.
Nilijipanga na kusema kwamba ni lazima nimfuate msichana huyo kama tu angekuja Kariakoo kutembea kama alivyofanya. Nikawa mzee wa kucheza karibu, sikutoka maeneo husika kwa kuwa niliamini muda wowote ule Halima angeweza kufika mahali hapo.
Baada ya wiki ndiyo akafika, nilimsalimia na kuendelea na mambo yangu. Sikuwa na presha, nilijua ningemkamatia wapi hivyo nikaanza kupiga misele lakini macho yangu yalikuwa pale dukani.
Ilipofika majira ya saa nane mchana nikamuona akitoka, sikutaka kumfuata moja kwa moja, alikuwa akienda kwenye kituo cha daladala za Kimara hivyo nikapitia kule Big Bon na kwenda kumsubiri kwa mbele.
Nilimuona akija, nikasimama sehemu wanapouza magazeti na kutulia hapo, alipopita tu nikamsogelea na kumshika mkono, alishtuka, akageuka na kuniangalia.
“Edward...” aliniita huku akiachia tabasamu.
“Pole kwa kukushtua jamaniiii!” nilimwambia huku nami nikiachia tabasamu.
“Usijali!”
“Leo mbona mapema?”
“Nawahi chuo, nimeanza jana na ndiyo maana naondoka mapema!”
“Ooh! Msomi wangu! Ningependa nikusindikize!” nilimjaribu.
“Wapi?”
“Chuo! Au sisi ambao hatujasoma hatutakiwi kuingia huko?” nilimuuliza kimatani.
“Hahaha! Acha utani! Nashukuru Edward!” aliniambia.
“Kushukuru kwako kunamaanisha nini? Kwamba naruhusiwa?” nilimuuliza.
“Noooo! Hauruhusiwi! Shemeji yako atakuona!”
“Kwani mimi si joka la kibisa, ananiogopea nini?” nilimuuliza.
“Hahaha! Una maneno wewe!”
“Basi sawa. Nashukuru kwa kuniruhusu kukuleta mpaka hapa kituoni, uwe na masomo mema,” nilimwambia.
“Nashukuru!”
Akaingia ndani ya daladala na kuondoka zake. Alionekana kufurahia pasipo kujua kwamba kwenye zile hatua kumi za kumuumiza Issa hiyo ilikuwa hatua ya kwanza. Nikarudi kuendelea na ishu zangu kama kawaida.
***
“Paaa! Paaa! Paaa...” nilisikia milio ya bunduki kutoka mbali kidogo na mahali nilipokuwa.
Ilikuwa ni majira ya saa kumi alfajiri, kila mlinz aliyekuwa mahali hapo alikuwa akiogopa, milio ile ya risasi ilionekana kabisa kuwa bunduki nzito, japokuwa tulitakiwa kulinda mahali hapo, walinzi wakaanza kukimbia.
Mimi sikukimbia, haimaanishi kwamba nilikuwa na nguvu, hapa, ni kwa sababu sehemu ambayo nilikuwa ilionekana kuwa salama zaidi.
Wote walikimbia na kubaki peke yangu na kilrungu changu. Kwa mbali nikaanza kumuona mzee fulani akikimbia, alivalia kanzu huku mkononi akiwa na mfuko wa nailoni.
Niliogopa, kwa jinsi alivyokuwa akikimbia ilionekana kama mtu aliyekuwa akiogopa kitu fulani na nyuma yake kulikuwa na watu waliokuwa wakimfuatilia.
Nilitoka nilipokuwa na kusogea kule alipokuwa. Mara milio ya risasi ikaanza kusikika tena, mzee yule akaanguka na kutulia.
Nilitetemeka, sikujua kilichokuwa kikiendelea. Ghafla nikawaona wanaume wawili, sikuweza kuaona vizuri usoni kwa sababu ilikuwa usiku na hata hivyo walivalia vinyago usoni ambavyo niliviona baada ya kupita sehemu iliyokuwa na taa.
Wakamsogelea yule mzee ambaye alikuwa akiugulia maumivu pale chini, kitu cha kwanza kilikuwa ni kuuchukua mfuko wake alioushika lakini cha pili kilikuwa ni kutaka kumpiga risasi.
“Wewe simamemi hapohapo,” nilisema kwa sauti kubwa.
Sikujua niliupata wapi ujasiri wangu, saut ile ambayo niliitumia kusema maneno hayo ilikuwa na utisho mkubwa na kuwafanya wale vijana kuogopa, hivyo kuanza kukimbia na ule mfuko huku wakimwacha mzee huyo akiwa chini akilia.
Nikamsogelea, mzee huyo alikuwa ni wa Kihindi, ilikuwa ni lazima niyaokoe maisha yake. Niliogopa kwani sikutaka kujiaminisha kwamba wale watu waliondoka moja kwa moja, niliamini kwamba wanaweza kurudi tena kumalizia kazi yao.
Mzee yule alikuwa akilia kwa maumivu makali, alipoteza damu nyingi, pale chini alipokuwa hakuwa na msaada mwingine zaidi yangu. Roho yangu iliniuma sana kiasi cha kusema kwamba ni lazima nimsaidie kwa nguvu zote.
“Nisaidieee....nakufaaaa....nakufaaaa....” aliniambia mzee huyo huku akilia.
Nikambeba na kumpeleka pembeni, nilipofika kwenye kibaraza kimoja, nikalishika shati lake kwa lengo la kulichana ili nimfunge kwenye kidonda kilichokuwa kimesababishwa na risasi.
Wakati nimemvua shati hilo na kulichana, nikasikia kitu kimetokea kwenye mfuko wa shati na kuanguka. Sikujua ni nini, nilikichukua harakaharaka na kukiweka kwenye mfuko wangu wa suruali na kuendelea kumfunga.
Baada kama ya dakika ishirini ndipo walinzi wenzangu wakafika hapo ambapo tukambeba na kumpeleka katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
“Nyie ni akina nani?” alituuliza nesi mmoja huku akiniangalia hasa mimi ambaye nguo zangu zilikuwa na damu nyingi.
“Wasamaria wema dada!”
“Mmemuokota wapi huyu?”
“Sisi ni walinzi, tulisikia milio ya risasi, kuna watu wakataka kumuua, tukamsaidia!”
“Sawa. Muacheni, njooni asubuhi tena mkiwa mmetoa taarifa kituo cha polisi,” alituambia na sisi kuondoka.
Tuliondoka huku tukisimuliana kile kilichotokea, kila mmoja alinishangaa, nilionekana kuwa mtu wa ajabu sana, iliwezekanaje niende kumsaidia yule mzee na wakati nilisikia milio ya risasi?
Sikuwa na jibu la kuwapa zaidi ya kuwaambia kwamba mimi mwenyewe nilishangaa. Tulilinda siku hiyo kwa kujificha sana, nakumbuka tulikuwa kama wanne hivi.
Ilipofika asubuhi, nikaondoka na kuelekea kwenye kichumba changu nilichopewa kwa ajili ya kukaa huko na kujilaza kitandani, siku hiyo nilichoka kupita kawaida.
Wakati nikiwa nimevua suruali na kubaki na boksa ndipo nikakumbua kuhusu kile kitu nilichokiokota na kukiweka mfukoni.
Haraka sana nikaichukua surualia yangu, nilipokitoa kitu hicho, nilipigwa na mshangao baada ya macho yangu kugongana na almasi iliyokuwa na ukubwa kama mfuniko wa kisoda.
“Hii nini? Almasi au kipande cha chupa?” nilijiuliza na kukiangalia vizuri, ni baada ya sekunde kadhaa nikapata jibu kwamba kile kilikuwa ni kipande cha almasi, mapigo yangu ya moyo yakaanza kudunda kwa nguvu, sikuamini kile nilichokuwa nikikiona. Hii ilimaanisha umasikini ndiyo basi tena ama nini? Kila nilichojiuliza, nikakosa jibu.
2
 
Nimesoma story nyingi humu jf ila hii imekuwa moja ya story Bora kabisa kuanzia namna ya usimuliaji mpaka uhalisia.Kudos mwandishi!
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom