Simulizi : Nguvu ya Mapenzi

SEHEMU YA 415 ......... MWISHO


Usiku wa siku hii waliitumia kama familia kwaajili ya kumuaga Erick, ila baba Angel alikuwa na mashaka sana kuwa kama mwanae wamemtangaza basi itakuwa ni ngumu sana kuweza kutoroka hapo nchini, Erica alimuangalia baba yake na kumuuliza,
“Baba, una mashaka na safari ya Erick?”
“Kiukweli sina raha kabisa”
“Hapana kuwa na amani tu, ataondoka salama”
Basi Erick kusikia vile, alimvuta Erica pembeni na kuongea nae,
“Ila je nitaweza kuishi bila kukuona wewe kabisa kwa siku zote?”
“Kwani umeambiwa kuwa hutoniona siku zote? Kuna siku utaniona tu hata usijali, nenda tu huko kwa usalama wako Erick. Mimi mwenyewe binafsi sitaki upatwe na matatizo yoyote yale”
“Sawa nimekuelewa, ila nitakukumbuka sana”
“Najua hilo Erick, ila jiokoe kwanza kwa haya yaliyopo”
Basi wakarudi na kula kwa pamoja na kuagana nae maana kesho yake ndio alikuwa akianza safari yake, kwa siku hii Sarah na Erica walilala nae pamoja tena.

Muda wa safari tu ulipofika, baba Angel aliondoka na Erick mpaka uwanja wa ndege na kukutana huko na Jack, kisha akaongea na Jack pale jinsi ya kumsaidia mtoto wake ambapo kuna namba za mtu wa kumsaidia ambazo Jack alimpa kisha muda ulipofika moja kwa moja Jack na Erick walimuaga vizuri baba Angel na wenyewe wakaondoka.
Baba Angel alikaa pale akiangalia angalia na muda ulipofika aliamua kuondoka ambapo moja kwa moja alienda kukutana na mtu ambaye alipewa namba na Jack, basi alikutana na yule mtu ambaye aliwasiliana nae, basi yule mtu alimsalimia baba Angel na kujitambulisha jina lake,
“Mimi naitwa Ayubu au baba Yusra, karibu sana”
“Asante, mimi naitwa Erick au baba Angel. Nashukuru sana kukufahamu”
“Jack alinieleza mambo mengi tu kuhusu yanayokusibu”
Kidogo simu ya yule Ayubu ilianza kuita, basi baada ya kuongea nayo ndio akamuangalia baba Angel na kumwambia,
“Oooh kuna jirani yangu mahali Fulani nasikia ameuwawa, leo wamenikumbuka na wanahitaji nifanye uchunguzi wa hiyo kesi ili mtuhumiwa akamatwe”
“Ooooh sasa itakuwaje?”
“Hapo pagumu kidogo, ila unaonaje twende nyumbani kwangu ili ukapafahamu”
Baba Angel alikubali na kwenda pamoja na huyu Ayubu ili apafahamu nyumbani kwake.
Kufika nyumbani kwa Ayubu alishangaa kuona binti wa Ayubu akimfahamu yeye vizuri sana,
“Nakufahamu ndio, wewe si baba yake Angel!!”
“Ooooh kumbe unamfahamu Angel?”
“Ndio namfahamu nilisoma nae yule”
“Aaaah, nafurahi kujua hilo. Nitamwambia basi”
Kisha baba Angel aliagana pale na Ayubu huku wakitegemea tena kuonana kwani Ayubu ndio alikuwa anataka kwenda kwenye huo msiba.

Baba Angel alirudi nyumbani kwake lakini moja kwa moja alijua wazi kuwa yule Ayubu ameitiwa msiba wa Moses ila hakutaka kumuonyesha mshangao mapema, alitaka tu akimaliza hayo mambo ndio aweze kuongea nae.
Usiku wa siku ile baba Angel alipigiwa simu na Ayubu kisha kuanza kuongea nae,
“Jirani yangu anaitwa Moses, mazingira ya kesi yake yanafanana na ambayo amenielezea Jack, je ndio kesi ambayo mwanao anahusika”
“Mmmmh tuonane kwanza ili tuongee vizuri”
“Usijali, nataka niweke sawa haya mambo, kama ni yeye niambie ili nijue jinsi nitakavyowajibu kuhusu ushahidi wangu”
“Ngoja basi nimuulize vizuri halafu nitakujulisha”
Baba Angel alikata ile simu huku akiwaza kwa muda na kuamua kumpigia Jack ila kwa muda huo Jack hakupatikana hewani, aliamua kumtafuta kwenye mtandao wa kijamii na kumpata kisha akamuuliza,
“Yule Ayubu kaniuliza swali ambalo ni kweli kabisa muhusika ni Erick, je nikubali? Haiwezi kuwa tatizo badae yani labda watumie kama ushahidi?”
“Hapana usijali, yule ni ndugu yangu kabisa hawezi kukufanyia kitu kibaya, nishamueleza kuhusu mimi na wewe, hawezi kufanya ubaya, wewe mueleze tu kila kitu naye atajua namna ya kukuepusha na hilo janga”
Ndipo baba Angel alipopata ujasiri wa kuwasiliana tena na yule mtu na kumwambia kuwa mwanae ni kweli ingawa hana uhakika kama kahusika kwa asilimia mia moja,
“Basi ngoja nitajua jinsi ya kufanya, usijali kitu chochote. Kuwa na amani tu”
Basi baba Angel alikata ile simu, ila kiukweli hakuwa na raha kabisa yani mambo hyote alikuwa akiyafanya ilimradi tu.

Wakati mitihani ilipokaribia, ilibidi baba Angel ampeleke Erica akaishi kwa dada yake yaani Tumaini ili iwe rahisi maana kule kwa mama yake ni mbali sana, ingekuwa ngumu kwa Erica kwenda shule na kufanya mtihani.
Basi waliongea kidogo pale na dada yake,
“Hayo mambo yataishia wapi?”
“Sijui dada yangu kwakweli ila Mungu anisaidie tu”
Kisha baba Angel aliondoka kwa dada yake, ila njiani alikutana na Sia na kuanza kuongea nae kwani anajua fika kuwa Sia anafahamu vitu vingi sana, kwanza Sia alianza kumuuliza baba Angel,
“mbona hewani hupatikani?”
“Simu yangu ilipotea”
“Halafu nyumbani kwako hampo familia nzima!”
“Aaaah matatizo tu, nipe khabari maana najua wewe huwa hupitwi”
“Na kweli sipitwi, nilikutana na Manka, yupo kama mtu aliyechanganyikiwa vile. Nasikia Moses amekufa, halafu mke wa Moses nae kachanganyikiwa sana”
“Duh!! Dokta Jimmy anaendeleaje maana simpati hewani”
“Huyo ndio hajulikani kabisa, ni wa kufa leo au kesho, hali yake ni mbaya sana kupita maelezo ya kawaida”
“Duh!!”
Hapa baba Angel ndio aligundua kuwa Erick hakumuua siku ile dokta Jimmy bali ameenda kummaliza Moses na shahidi wa mambo yote yale ni Manka tu ndiomana yupo kama kachanganyikiwa basi baba Angel aliona ni vyema kuongea na Manka pia huku akisaidiana na Ayubu katika kumsafisha mwanae.

Baada ya miezi miwili, baba Angel alimtafuta Manka ambaye alikuwa kama watu waliopungukiwa na akili, hata yeye mwenyewe binafsi alimuhurumia sana, ila alikaa chini na kuongea nae,
“Unajua sina amani, sina furaha moyoni, siwezi kuishi tena na Sarah maana kawapenda sana halafu pia siwezi kuishi na Elly, najihisi vibaya sana katika moyo wangu. Natamani ingetokea kitu moja kikubwa kifanyike hata niweze kuishi pamoja na wanangu hata niwe nawaona tu”
“Usijali, lazima tuhakikishe kuwa tutafanya kitu. Ngoja nikuulize, kesi ya kifo cha Moses imeishia wapi?”
“Ni wazi aliyeua ni mwanao, ila ulichokifanya Erick unakijua mwenyewe, leo hii inasemekana kuwa Moses kajiua mwenyewe, halafu dokta Jimmy alipata ajali eti ajali ndio imemuweka kitandani hadi umauti!!”
“Khaaa dokta Jimmy amekufa?”
“Ndio, dokta Jimmy amekufa, tumetoka kumzika kama wiki mbili zilizopita, hakuna mwenye amani ya moyo kabisa.”
“Yule mtoto ambaye dokta Jimmy alikuwa akimlea, yule wa madam Oliva kaishia wapi?”
“Yule mtoto kachukuliwa na Oliva mwenyewe, kwanza unajua kama huyo Oliva alishajifungua tayari!!”
“Kumbe!!”
“Ndio, amepata mtoto wa kike, na yule mtoto wake ameenda kuishi nae. Yule mtoto anaitwa Jimmy. Ila mimi na yule anaitwa Sia ndio hatuna bahati kwakweli, mimi sijui naishia wapi najiona kabisa nimefikia ukingoni”
“Pole sana”
“Kuna shamba kubwa sana, Sarah alipewa na mzee Jimmy ila Sarah hajawahi kuliona shamba hilo, siwezi kumdhurumu, nashukuru nimekutana nawe twende nikakuonyeshe shamba hilo”
Baba Angel alikubali tu na muda huo huo waliondoka na kuelekea kwenye hilo shamba huku wakiongea vitu mbalimbali,
“Ila kwanini ulitaka kuniua Manka?”
“Nisamehe ila nilikuwa natumwa tu kufanya vile, nilijua hawa watu niko nao pamoja kumbe wananing’onga na kunicheka”
Walifika kwenye lile shamba na baba Angel alipata kuliona, kwakweli lilikuwa kubwa sana na kumfanya baba Angel afikirie kitu cha kufanya na lile shamba.
Aliongea nae kidogo tu na kuahidi kumtafuta tena.

Baba Angel, leo alihama na familia yake kutoka kwenye nyumba ya mama yake maana kulikuwa na nyumba yake nyingine ambayo ndio aliimalizia kuijenga, basi walifurahi na kwa pamoja waliondoka na kuhamia huko, ila sehemu waliyohamia walikuta na baba Emma nae na familia yake ndio wamehamia sehemu hiyo hiyo.
Basi siku hiyo alikutana nae huku baba Emma akilalamika,
“Yani yule dokta Jimmy amekufa bila mimi kujua ukweli wa watoto wangu walipo!! Roho inaniuma sana”
“Pole sana, ila Mungu akitaka ukweli uujue basi utaujua tu maana hakuna marefu yasiyokuwa na ncha”
“Ila naumia sana, huyu dokta Jimmy nitamchukia hadi naingia kaburini”
Baba Angel alijaribu kumpa moyo pale kisha kuendelea kuwa majirani wazuri pale kwao.
Baba Angel aliamua kutimiza lile wazo la Jack na kuamua pia kuishi sehemu moja Derrick na Samir maana alijenga sehemu nyingine ya kuweza kuishi hawa watoto wa kiume ili pale pale maeneo ya nyumbani kwake. Alifanya hivi ili asiwe nao mbali na hawa ukizingatia Jack ndio alikuwa akiishi na Erick.
Pia baba Angel alimwambia mama Sarah arudi kwenye nyumba yake ambapo mara moja moja Sarah alikuwa akimtembelea maana bado ni mlezi wake ila mama Sarah alikuwa kama mtu aliyechanganyikiwa haswaa kwa swala la Elly kutokumkubali huku akizamia kwa baba yake Derrick.

Miaka mitano inapita na kufanya waanze kusahau yale machungu ambayo yalitokea baina yao, leo ilikuwa ni siku ya furaha sana kwenye familia yao kwani ilikuwa ni siku ambayo Erick alirudi kutoka Afrika Kusini akiwa ameongozana na Jack, yani ilikuwa ni furaha sana kwa familia hii na wote walikuwepo nyumbani kwaajili ya kumkaribisha Erick tena katika maisha yao.
Siku hii Angel alikaa na Samir na kuanza kuongea nae,
“Angel, sikia nikwambie kitu yani mimi naona kabisa sitaweza bila wewe kuwa mke wangu. Ila nafasi ya mimi na wewe kufunga ndoa ipo wazi kabisa, sababu wewe ni mtoto wa Rahim na mimi ni mtoto wa Erick, mama zetu ni tofauti kabisa, je kwanini tusiweze kuoana?”
“Mmmmh ngoja tumuombe baba, anaweza akakubali”
Walijipanga na siku hii Angel aliweka ombi hili kwa baba yake kuwa anaomba yeye na Samir wafunge ndoa,
“Hapana haiwezekani Angel”
“Baba, inamaana mimi sitaolewa miaka yote maana mtu ninayempenda ni Samir halafu hakuna kizuizi kati yangu na Samir, kwanini isiwezekane?”
“Ngoja nikajadiliane hayo maswala na mama yenu”
Baada ya shughuli ya siku ile baba Angel alienda kumwambia mama Angel kuhusu watoto wao ila mama Angel alikubali kiurahisi kabisa, kisha kesho yake wakamtaka Angel na Samir waende kuongea na Rahim kuhusu swala lao la hiyo ndoa.

Angel alimuomba Erick aweze kumsindikiza katika kumpa ujumbe Rahim juu ya ndoa yake na Samir maana Samir aliogopa kwenda kusema ukizingatia alikuwa akimuogopa sana Rahim toka siku aliyotaka kumuua.
Angel alikutana njiani na Rahim na kuanza kumwambia kuhusu dhamira yake,
“Naomba mimi na Samir tuweze kufunga ndoa, nampenda na yeye ananipenda”
“Haiwezekani, aibu niliyoipata kwa Derrick inatosha msije kuniletea na nyie aibu”
“Aibu kivipi? Baba kule amekubali ukizingatia mimi na Samir sio ndugu”
“Nitolee balaa Angel, Samir nimemlea kama yeye haoni undugu wenu basi alete masikhara kwangu nitamfanyia kitu kibaya asiweze kusahau maisha yote”
Mara Erick akamwambia Rahim,
“Unasemaje wewe?”
Rahim alimuangalia Erick na kumuona kabadilika sura huku mishipa ikiwa imemsimama yani Rahim aliogopa sana alikumbuka siku aliyokabwa na Erick, kwahiyo kwa kujihami akajikuta akianza kukimbia, ila kwa bahati mbaya hakuangalia upande wa pili wakati anavuka barabara kwa kukimbia hadi akagongwa na gari.


Rahim alimuangalia Erick na kumuona kabadilika sura huku mishipa ikiwa imemsimama yani Rahim aliogopa sana alikumbuka siku aliyokabwa na Erick, kwahiyo kwa kujihami akajikuta akianza kukimbia, ila kwa bahati mbaya hakuangalia upande wa pili wakati anavuka barabara kwa kukimbia hadi akagongwa na gari.
Kilikuwa ni kitendo cha gafla sana, ikabidi Angel na Erick wasogee pale alipokuwa Rahim na kuomba msaada wa kupelekwa hospitali ila haikuchukua muda kwani majibu yalipatikana pale pale kuwa Rahim ameaga dunia, basi Angel alianza kupigia simu watu mbalimbalikuwapa ile taarifa huku akimwambia Erick,
“Na wewe umezidi na misuli yako, kwa stahili hii jamani si utaua wengi wewe!”
“Aaaah sikutaka ila sikupenda ile kauli yake”
“Hata kama, uwe unajitahidi kujizuia, Erick umerudi jana tu halafu leo umezua balaa jamani loh!!”
Wakaenda nyumbani ambapo baba Angel na mama Angel walielezewa na Angel ilivyokuwa na moja kwa moja walijua kuwa uoga wa Rahim kwa Erick ndio umesababisha yote yale ila hawakuwa na cha kufanya maana tayari msiba ulishatokea.

Ikawa ni majonzi ya kifo cha Rahim lakini kilichosababishwa na Erick, huku ikisemekana kuwa ni ajali ndio iliyomuua Rahim, hapo walilia sana hasa watoto wa Rahim na baba Angel kuzidi kuona madhara yaliyopo kwa Erick, kiukweli hakujua cha kufanya na Erick.
Siku ya mazishi ya Rahim, na Manka alikuwepo kwahiyo baada ya mazishi tu baba Angel aliamua kwenda kuongea na Manka kuhusu Erick, alikuwa akihisi huenda hata dokta Jimmy alikuwa amemuachia siri ya kufanya Erick apate nafuu, ila Manka alimwambia kuwa dawa ni moja tu yani Erick alale na Erica ndio nguvu za Erick zitakuwa sawa, kwakweli baba Angel bado roho ilimuuma sana kwa kuweza kufikiria jinsi Erick na Erica walale kimapenzi wakati ni watoto wake wote wawili.
Ila wakati anataka kuondoka, Manka alimpa ujumbe ambao alipewa na Sarah,
“Sarah kaniambia kuwa kapata mchumba, atakuja kukutambulisha ili aolewe”
“Kheee watoto wa siku hizi wanawahi”
“Mwache awahi tu, huyu mtoto alianza mapepe mapema sana, bora tu aolewe ila mimi najitolea kuishi nao yeye na mchumba wake nyumbani kwangu”
“Kama wakiamua kuishi kwao je?”
“Basi nitahamia huko, mimi ni mpweke sana. Halafu ngoja nikwambie kitu kingine ambacho hujui kuhusu mimi”
“Kitu gani hiko?”
“Mimi ni mwathirika”
Hili baba Angel alilijua vizuri kabisa maana huyu alitembea na Rahim ambaye alishaathirika kitambo sana ila tu alijifanya kushangaa kanakwamba hakujua kitu,
“Oooh pole na hongera kwa ujasiri wako wa kusema, kuwa muathirika sio mwisho wa maisha, bado unanafasi kubwa sana ya kusonga mbele”
“Asante ila najua aliyeniambukiza”
“Nani huyo?”
“Huyu huyu marehemu Rahim, alijifanya ananipenda kumbe yupo kwaajili ya kunipa maradhi tu, ila Mungu alivyosasa ona yeye kafa kwa ajali tena ya kujitakia mwenyewe maana alikuwa anakimbilia wapi sijui”
“Mmmmh haya yaishe, tutaonana tena siku nyingine”
Siku hizi Manka alikuwa mpole sana, kwanza alionekana kama mtu ambaye akili zake hazifanyi kazi vizuri na hakuona tatizo kuongea lolote na sehemu yoyote ile.

Baba Angel alirudi nyumbani kwake huku akikuna kichwa chake kwa mawazo aliyokuwa nayo, basi aliongea na mke wake kile ambacho aliambiwa na Manka,
“Unajua Manka anasema tatizo la Erick linaweza kumalizwa na Erica tu”
“Hivi kwa mfano tukamtafutia Erick msichana mwingine itakuwaje?”
“Mmmh unatafuta balaa mama Angel, tutamsafirisha wapi tena akiharibu? Anaweza kuua huyu mtoto ujue. Tujifunze kutokana na makosa”
“Sasa itakuwaje? Tutakubali watoto wetu walale pamoja kimapenzi?”
“Aaaah hiyo ngumu ila ngoja tutafakari”
Waliamua tu kulala kwa muda huo.
Kulivyokucha tu, Sarah aliwafata na kuwapa taarifa kuwa anataka kwenda kumtambulisha mchumba wake kwao, walikubali tu hawakuwa na pingamizi juu ya hilo.
Kisha baba Angel alienda kumfata Erick ambaye hana siku nyimgi toka arudi, aliongea nae kirafiki tu amsikie majibu yake,
“Erick, hebu niambie kitu. Leo ndugu yako Sarah amesema kuwa analeta mchumba wake kumtambulisha, je wa kwako utamleta lini?”
“Kwani na Erica kashamleta wa kwake?”
“Hapana”
“Nitamleta pindi Erica akimleta mtu”
Baba Angel aliitikia tu ila alijaribu kusoma kitu na kwenda kuongea na mke wake kisha wakapanga mpango.

Kwenye mida ya jioni, Sarah alileta mchumba wake nyumbani kwao na walimkaribisha vizuri sana, huyu alikuwa ni mtoto aliyelelewa na madam Oliva, ila ni mtoto wa Sia na Steve yani Paul.
Baba Angel na mama Angel hawakuwa na pingamizi kabisa juu ya mapenzi ya hawa watu.
Kisha baada ya Paul kuondoka, baba Angel aliondoka pia ili kwenda kujaribu kile anachoona kinafaa zaidi, alienda hadi nyumbani kwa Bahati na Fetty na kuongea nao juu ya kijana wao Bahati aje kwake kujitambulisha kama mchumba wa Erica, alimuahidi kumlipa ila hakumwambia kwanini anataka iwe hivyo, hilo lilikuwa swala rahisi sana kwa Bahati mdogo kwani alikubali kiurahisi ukizingatia anampenda sana Erica.
Baba Angel alipomaliza hapo alirudi nyumbani na kumpa ule ujumbe mke wake, ambaye aliafikiana nae na wakapanga kesho yake kuwa wampange Erica aweze kukubali wakati Bahati anaenda kujitambulisha maana hawakutaka kuchelewesha mambo.
Halafu wakapanga lingine sasa,
“Hili likifanikiwa tu, basi moja kwa moja tutaenda kuongea na baba Emma ili tumchukue yule Emmanah awe na Erick au unasemaje?”
“Hapo sawa kabisa baba Angel, yani yule Emmanah umelenga haswaaa, tujitahidi Erick aweze kumkubali kwakweli”
Basi walipanga mpango wao kwa namna hiyo.

Kulipokucha tu, mama Angel akamuita Erica na kumpanga ila Erica alikuwa akipinga vikali kuhusu swala hilo,
“Kwanini mmefikia huko mama?”
“Tunataka kumuokoa kaka yako”
“Nadhani mnataka kumuangamiza, mnajua madhara ya hiko mnachokitaka?”
“Usiwe mkaidi Erica, naomba ukubali”
Erica alikubali lakini kishingo upande.
Jioni ya siku hii, alikuja Bahari kama mchumba wa Erica yani alikuja kujitambulisha na baba Angel aliwaita watoto wake wote ili wamshuhudie mchumba wa Erica, basi baba Angel alianza kutoa ule utambulisho, kitu cha kushangaza Erick aliinuka huku akiwa na gadhabu kali sana, alimkunja Bahati na kumtwika ngumi ambayo ilimpeleka Bahati chini yani ilibidi tu Erica ndio aende kuingilia kati ila Bahati alikuwa na hali mbaya sana ikabidi wamkimbizie hospitali kwa tiba ya haraka yani kila kitu hapo nyumbani kwao kilivurugika.

Wakati baba Angel yupo hospitali kwaajili ya matibabu ya Bahati, ndipo alipokutana na mke wa Moses ambaye alidai kuwa mwanae yupo hapo hospitali pia,
“Kheee pole sana, kafanyaje kwani?”
“Kapata ajali, kapoteza damu nyingi sana yani sijui nifanyeje na anatakiwa kuongezwa damu”
Baba Angel alijitolea kufanya hivyo, ila walienda kumchukua damu yake na kukuta na damu ya yule kijana haziendani, ila mara baba Emma nae alionekana pale akisema kachanganyikiwa maana mwanae kapata ajali pia na anatakiwa kuongezwa damu ila yeye haendani nae damu yake, ila daktari akawaita wote wawili maana kila mmoja damu ilionekana kuonda kwa mwingine, yani baba Emma alifanana damu na mtoto wa Moses halafu baba Angel alifanana damu na Emmanuel, basi waliwaongezea damu na watoto wakendelea vizuri.
Ikawa kila wanapoenda hospitali wanakutana, huku wakina Bahati na mkewe Fetty nao wakienda kumtazama mtoto wao.

Siku hii, Erica alimuita baba yake na mama yake na kuanza kuongea nao,
“Kwani baba na mama tatizo lenu ni nini?”
“Tatizo letu ni kuwa tunaogopa wewe na Erick kuwa pamoja kimapenzi, ndiomana tunafanya jitihada zote kuweza kuweka mambo sawa”
“Ila kabla hamjaendelea na hiso jitihada zenu, nakuomba baba nenda kamtafute yule rafiki yako dokta Noah mwambie akwambie ukweli”
Baba Angel alishangaa sana ila alikubali kufanya vile, na kweli siku ile ile aliamua kumtafuta dokta Noah na kuanza kuongea nae, hata dokta Noah alimshangaa baba Angel na kumuuliza,
“Nani kakwambia kuwa mimi nina ukweli?”
“Binti yangu Erica”
“Dah!! Ila naogopa”
“Hapana, niambie tu.”
“Ngoja nitapanga siku nitakuita mahali utakutana na wengine, na hapo nitasema ukweli ila mnilinde maana sina cha kufanya”
“Nitakulinda, nahitaji tu ukweli”
Baba Angel alimuahidi dokta Noah kuwa atamlinda maana alimwambia kuwa atausema ukweli wote ulivyo.

Siku hiyo dokta Noah alimuita baba Angel na mama Angel, walijiandaa na kwenda alipowaita ila walishangaa sana kufika kule kumkuta baba Emma, mama Emma, mke wa Moses pamoja na Juli, kisha dokta Noah alianza kuongea,
“Samahani sana kwa hiki nitakachowaambia”
“Bila samahani, sisi tutakusikiliza”
“Miaka ya nyumba iliyopita wakati Erica akiwa mjamzito, nilimsikia mkwe wake na dokta mwenzangu wakipanga mipango mibaya juu ya wale watoto, kwanza walipanga mipango ya kuwabadilisha na badae walipanga mipango ya kuwachoma sindano, roho iliniuma sana kwani nilijua wazi hao watoto wakiwa wakubwa watakuwa ni mwiba kwa wazazi wao. Naomba mnisamhe hiki ambacho nitakachowaambia, kuna huyu dada anaitwa Juli, enzi hizo alikuwa na maisha magumu sana na alikuwa akitaka atoe mimba, ila badae alipanga akijifungua atupe mtoto, ila alijifungua watoto mapacha mmoja wakike na mwingine wa kiume, nilimuomba asiwatupe, nikaenda kuwahifadhi na ndipo muda naenda kuwahifadhi nilikuta Erica ameshajifungua wale watoto wake, ila alijifungua mapacha watatu tofauti na tulivyojua mwanzo, yani hata sikufikiria mara mbili bali nilimbadili yule mtoto wa kiume na mtoto wa Erica muda huo huo. Ila sikutaka mtoto wa Erick aende kuishi maisha ya shida, na hivyo nikawaweka pembeni na kupewa mgonjwa wa kujifungua ambaye alikuwa ni wewe Neema, kiukweli hukujifungua mapacha ila ulijifungua mtoto mmoja, nami nikamchukua mtoto wako na kukuwekea wale wawili ambapo mmoja ni mtoto wa Juli na mwingine ni mtoto wa Erica, nikaondoka na mtoto wako ambaye sikutaka apate shida pia, basi mke wa Moses alipojifungua nikamuongezea na mtoto mwingine ambapo na yeye alionekana kuwa kajifungua mapacha, hii kitu imenitesa kwa miaka yote hii. Niliandika hadi kwenye Kitabu changu cha kumbukumbu, kila siku nilitamani kusema ukweli ila niliogopa. Nilijua kuwa wote mngenichukia, sikufanya kwa nia mbaya ila kitendo changu cha kubadilisha mtoto wa Erica ndio kimezaa yote haya. Naomba mnisamehe sana”
Baba Angel alipumua kiasi na kumuuliza,
“Inamaana hata dokta Jimmy na mzee Jimmy hawajui hiki ulichokifanya?”
“Hakuna aliyekuwa anajua zaidi yangu”
“Yani kumbe wengine wanabadilisha huku watoto na wewe unabadilisha huku, mnajua nyie mnaweza fanya wazazi wakawa machizi!”
“Nisamehe Erick, ila nilifanya kwaajili ya kukomboa kizazi chako”
“Kwahiyo Erick sio mwanangu?”
“Ndio, Erick na Emmanah ni mapacha, ni watoto wa Juli ambaye alishindwa kuwalea”
“Duh!!”
Baba Emma nae aliuliza vizuri,
“Kwahiyo na mimi mwanangu ni nani?”
“Ni mtoto wa Moses, anaitwa Abraham ndio mtoto wako wewe”
Mke wa Moses nae alikuwa akishangaa na kuuliza,
“Kwahiyo sikujifungua mapacha?”
“Ndio, ulijifungua mtoto mmoja tu”
“Ile hospitali ndiomana mnapenda kutufanyia upasuaji kumbe mnayenu mnayoyajua nyie”
“Ishafungwa ile hospitali kwa ujinga wao”
“Naomba mnisamehe maana nilitaka kuokoa watoto wa Erick”
“Aaaah hata kama, ila kwanini uingilie na kubadilisha watoto wa wengine? Hapo ndio sijakupenda”
Basi mama Angel alimuangalia Juli na kumuuliza,
“Na wewe kulikoni kutaka kutupa watoto? Ulizaa na nani kwanza?”
“jamani maisha dah!! Najua hata hivyo watoto wenyewe hawawezi kunikubali. Nilizaa na mtu mmoja anaitwa Yuda”
“Khaaa alipokea kichapo toka kwa Erick huyo loh!! Ni halali yake kumbe, alikataa mimba eeeh!!”
“Ndio alikataa ndio chanzo cha mimi kuanza kutangatanga”
Ila wote walijikuta wakimjadili vibaya dokta Noah, kasoro baba Angel, mama Angel na Juli. Ila sababu dokta Noah alisema ukweli baba Angel aliamua kuchukua hatua pale pale na kurudi nyumbani kwake huku akiruhusu Erica na Erick kuwa pamoja maana aliona Erick atazidi kuharibu na kuharibikiwa.
Ila Erica bado alishikilia msimamo wake ule ule kuwa hakuna kitu mpaka ndoa ifanyike, kwakweli hili swala lilikuwa ni jambo la aibu kwa baba Angel ila alikubaliana nao wote kufunga ndoa na kufanya sherehe ya kifamilia.

Na kweli walifunga ndoa na kufanya sherehe ya kifamilia, yani baba Angel alikuwa akiona aibu sana ila siku aliyofunga ndoa Angel na Samir, ndio siku aliyofunga ndoa Sarah na Paul halafu Erica na Erick nao walifunga ndoa siku hiyo. Baba Angel hakutaka wengi wajue, ila habari ilimfikia Sia ambaye alifika na kuongea na baba Angel,
“Unajua kuna vitu mtu unaweza kuvizuia weee ukajikuta unashindwa ila badae mapenzi yakachukua nafasi yake, unaamini kuwa mapenzi yana nguvu sana?”
“Ndio ninaamini, hata kwa madam Oliva na Steve ilikuwa hivi hivi, tulijua ni dawa tu kumbe na mapenzi nayo yalikuwa na nguvu zake hadi mtu kajikuta anatengeneza dawa”
“Umeona kwa watoto, umewalea siku zote katika misingi ya dini sijui ikawaje ukateleza kumbe nguvu ya mapenzi inataka kuchukua nafasi yake”
Baba Angel akacheka na kumwambia Sia,
“Mjinga wewe, saivi na mke wangu tunarudi tena kwenye maombi”
“Mungu hakutaka mumsumbue kwa maombi yenu ya kuombea watoto watengane wakati kuna nguvu ya mapenzi kati yao”
“Mjinga sana wewe”
“Ila tuache masikhara Erick, kwakweli mapenzi yana nguvu”
Baba Angel alicheka tu, ila zile sherehe zilipoisha aliwapatia wote watoto wake nyumba za kuishi halafu yeye nyumbani kwake alibakia na mke wake pamoja na mtoto wao Ester.

Leo, baba Angel alienda kumtembelea Erick pamoja na Erica huku akiwa ameongozana na dokta Noah, ambapo alikaa na kuongea nao ukweli wote ila ilikuwa ni ajabu sana kwani Erick hakuchukia kama siku zote jinsi anavyofanya ila tu alimpongeza huyu dokta kwa kile alichokifanya kwao, huku akimsifia sana Erica,
“Licha ya dawa tulizopewa ila bado Erica ni mwanamke jasiri sana, kwani ameweza kunitoa katika hali hii mara nyingi sana. Kwakweli Erica anahaki ya kupewa sifa ya kuwa mke mwema”
Basi baba Angel alimuuliza mwanae kwa masikhara,
“Eti Erick, mapenzi yana nguvu?”
“Ndio baba yana nguvu sana, yani wao walipanga vile halafu mapenzi yakapanga vingine. Unafikiri kwanini huyu dokta alitubadilisha! Ni sababu ya nguvu ya mapenzi, hakubadilisha kwa akili yake ila nguvu ya mapenzi ilimsukuma, alihisi uchungu kwa rafiki yake kufanyiwa fedheha”
“Ila bado Erick utabaki kuwa mwanangu wa pekee”
“Hata wewe baba utabaki kuwa baba yangu wa pekee”
Erick na baba Angel walikumbatiana pale.

MWISHO
Safi sana... Bonge la story...

Chapter closed...


Cc: mahondaw
 
Hii tamthilia ndefu Sana lakini ni Kiboko.Nipo likizo imenitoa upweke yaani nilikuwa naanza asubuhi Hadi usiku mrefu!
Hongera sana mkuu Abdalahking
 
Hii tamthilia ndefu Sana lakini ni Kiboko.Nipo likizo imenitoa upweke yaani nilikuwa naanza asubuhi Hadi usiku mrefu!
Hongera sana mkuu Abdalahking
Tuko pamoja mkuu, endelea kufutalia nyingine nyingi
 

Similar Discussions

6 Reactions
Reply
Back
Top Bottom