Simulizi: Mtoto wa ajabu

MTOTO WA MAAJABU: 37

Muda huo mtoto nae akasogea kwenye maongezi yao na kumuuliza Juma,
“Baba una uhakika gani kama mimi ni mchawi?”
Juma akamuangalia huyu mtoto bila kumjibu kitu na kumfanya mtoto amuulize tena Juma lile swali kisha Juma akamjibu,
“Mimi sijasema kama wewe ni mchawi”
Mtoto akacheka kisha akamuangalia Zayana na kumwambia,
“Mmdogo, achana na huyo mwanaume utajutia maisha yako yote. Achana nae huyo nakwambia”
Zayana akamuangalia huyu mtoto ila hakumwambia kitu na kumfanya huyu mtoto aongee tena,
“Mamdogo, sirudii kukwambia ila huyo mwanaume hakufai, utajuta maisha yako yote nakwambia”
Halafu yule mtoto akaingia chumbani kwake, kwahiyo pale Juma alibaki na shemeji yake Zayana, kisha Juma akamwambia Zayana,
“Hapo sina usemi zaidi shemeji, acha niende kazini tu”
Juma akaondoka kwa muda huo na hata hakusema jambo lingine zaidi.
Zayana alikaa chini huku akitafakari, mama yake nae alitoka chumbani muda huu ambapo Zayana alimsimulia mama yake yale ambayo mtoto ameyasema, basi mama yake akasema,
“Inamaana hako katoto bado kana mambo ya ajabu?”
“Ndio mama”
“Mmmmh halafu unajua nakaogopa eeeh! Sijakaona nikajua hakapo”
“Ila kumbuka Mariam alisema tu kuwa kamelala”
“Sikia mwanangu, tujiandae tuondoke maana mimi hako katoto huwa hata sikaelewi”
Basi wakaenda kujiandaa ili waweze kuondoka kwani mama Mariam hakutaka kabisa kuwa karibu na yule mtoto sababu alikuwa akimuogopa.
Basi wakawa wanajiandaa huku wakijadili,
“Kwahiyo mama niolewe au nisiolewe?”
“Mmmmh sijui ila kama wanakataza mwanangu usiolewe maana hata mimi naogopa usijekupatwa na matatizo”
“Na kuhusu hii mimba je!”
“Hakuna tatizo, itabidi tu uzae mwanangu, usiwe na mawazo sana kuhusu hiyo mimba”
Zayana alikubaliana na mama yake na waliendelea kujiandaa kwaajili ya kuondoka.

Mariam muda huu aliandaa kifungua kinywa kwaajili ya ndugu zake, ila baada ya muda ndugu zake walitoka na kudai kuwa wanaondoka,
“Kheeee mama jamani asubuhi yote hii!”
“Ndio mwanangu, mambo ni mengi na majukumu ni mengi pia. Lazima tuondoke leo tena muda huu”
“Jamani mama jamani! Mnywe basi chai”
“Aaaaah Mariam tunatakiwa kuwahi”
“Hapana mama, nimeandaa chai kwaajili yenu”
Basi ikawabidi tu wakae na kunywa chai ambapo mama Mariam akamuuliza Mariam,
“Una mdada wa kazi siku hizi?”
“Mmmmh! Sina mama, yule mdada aliyepita alinifanyia vitu vya ajabu sana, kwahiyo sina mdada wa kazi”
“Kwahiyo hii chai umeandaa mwenyewe Mariam!”
“Ndio mama, kwanini umeuliza hivyo?”
“Kweli mwanangu umekua jamani, tena umekua sana, najua kawaida yako Mariam ni kuamka saa nne yani hapo hadi tungekuita kukuamsha, ila eti ushaandaa chai hii saa mbili duh! Umebadilika mwanangu”
Mariam akacheka tu na kumwambia mama yake,
“Hata nyumba tayari nimesafisha”
“Kheeee, wewe mwenyewe? Na jana umepika mwenyewe?”
“Ndio mama, kila kitu siku hizi nafanya mwenyewe”
“Duh!! Kweli umebadilika mwanangu ila ndio vizuri hivyo kwnai unafanya mama yako nijivunie uwepo wako, nisiwe na mawazo kabisa”
Mariam akatabasamu tu kwani hajawahi kuambiwa hivi na mama yake, ukizingatia kila siku mama yake alikuwa anamwambia bora umeolewa, ukizingatia mama yake alimwambia wazi mume wa Mariam yani Juma kuwa Mariam ni mvivu sana, kwahiyo Mariam alijisikia vizuri kuambiwa hivi na mama yake.
Walipomaliza kunywa chai sasa wakataka kuondoka ila mtoto akatoka ndani na kusema,
“Bibi, unajua kama hatujakaa hata kidogo kuongea! Sasa unataka kwenda wapi? Hunipendi mjukuu wako?”
Mama Mariam alimuangalia huyu mtoto kisha alimuangalia Mariam halafu alimwambia Mariam,
“Hivi ndio huyu mtoto wa miezi mingapi tu iliyopita tulikuja kukuhudumia kwaajili yake?”
“Ndio ni huyu mama”
“Mbona ananyoosha maneno hivyo?”
“Sababu amekua mama”
“Mmmmh!”
Mama Mariam akaguna halafu akajikuta akishindwa kuongeza neno kwa yule mtoto ila Mariam alielewa kuwa hawa wakilazimisha kuondoka ni kitu gani kitatokea, basi akamuuliza mwanae,
“Unataka waondoke lini?”
“Kesho au kesho kutwa, sana sana kesho kutwa. Nataka wakusaidie kidogo mama na kazi za hapa nyumbani”
Wakaangaliana kwa muda, basi Mariam alimshika mkono mama yake na mdogo wake na kwenda nao chumbani kishia akawaambia,
“Jamani nawaomba muondoke hiyo kesho kutwa, huyu mtoto wangu namfahamu vizuri sana. Nawaomba sana tafadhari”
Yani mama Mariam hakupenda kabisa ila ilibidi tu akubaliane na kile ambacho kimesemwa na Mariam.

Juma akiwa ofisini leo alishangaa kufatwa na Pendo ambaye alikuwa akiongea huku anatetemeka hadi Juma akamuuliza,
“Tatizo ni nini Pendo?”
“Naomba unisamehe Juma, tena nisamehe sana”
“Kivipi? Umefanyeje kwani?”
“Nisamehe kwanza halafu nitakwambia”
“Sawa, nimekusamehe”
“Ni hivi nilikuwa nakulazimisha kumchukua yule mdada wa kazi hata nikakununia na kuchukia kabisa ila ukweli wa hali halisi kuhusu yule mdada sikuufahamu, naomba unisamehe”
“Kwani imekuwaje?”
“Na bora hata hamjamchukua, yani sikujua kama yule mdada ni wa ajabu, kuna rafiki yangu alikuwa anahitaji mdada wa kazi ila alimchukua na kusema siku hizi kuna matukio mengi sana ya wadada wa kazi na yeye huwa akichukua mdada wa kazi cha kwanza anampeleka hospitali kumpima ukimwi na magonjwa ya zinaa kwani kuna watoto wameambukizw amagonjwa na wadada wa kazi, halafu kingine anasema huwa lazima mdada wa kazi ampitishe kwenye maombi kwanza kwani mambo mengi na dunia imeharibika. Sasa alimchukua nyumbani kwangu na moja kwa moja akaenda naye kwenye maombi, duh kilichotokea huko hapana aisee hadi naogopa”
“Mmmmh nini tena?”
“Kumbe yule mdada hakuwa binadamu wa kawaida, alikuwa ni chatu”
“Khaaaa weeee Pendo unazungumzia vuti gani?”
“Yani hapa nilipo natetemeka, yule mdada wangu mpya wa kazi alipogundua unajua amekimbia, naogopa mimi naogopa sana kumbuka siku zote hizi nimelala nao na kuishi nao, jamani naogopa sana”
“Pole sana Pendo”
“Asante, nisamehe sana kwa kukununia sababu ya hawa wadada jamani sikujua mimi naogopa hadi muda huu naogopa kabisa”
“Ndiomana kwasasa mimi na familia yangu tumeamua kutokuwa na mdada wa kazi ndani sababu ya mambo kama hayo. Unamkumbuka yule mdada wa kazi aliyepita alikuwa anafanya mambo ya kichawi ndiomana hatutaki labda tumtambue vizuri”
“Ila mbona mwanzoni ulikubali na badae ukabadili maamuzi, ulishtuka kitu gani tena?”
“Aaaah mke wangu alikataa tu jambo hilo”
Yani Pendo bado alikuwa akitetemeka, ilionyesha wazi kuwa ile habari ilimshtua sana ndiomana alikuwa bado anatetemeka.

Leo kweli kabisa mama yake Mariam alisaidia kufanya baadhi ya kazi mule ndani na kumfanya Mariam afurahi kwa hawa ndugu zake kuambiwa kuwa wabaki hapo nyumbani kwake.
Ila mama Mariam akasema,
“Jamani kuna mboga gani leo Mariam?”
“Kuna maharage mama na mchicha upo”
“Aaaah sitaki kwakweli, mimi nataka nyama tena nyama ya kuku”
Mariam akacheka na kusema,
“Sasa mama kwanini hukumwambia mkwe wako asubuhi!”
“Nimwambie nini kwani tulipanga kukaa mpaka leo? Si mtoto wako tu ndio kalazimisha tukae jamani”
“Sasa itakuwaje mama”
Wakati wanaongea Zayana alikuwa akicheka na kufanya wamuulize,
“Sasa unacheka nini Zayana?”
“Yani nimemwambia huyu baba kijacho wakati mnazungumza hapo, nikamwambia nina hamu ya kuku, eti kanitumia hela kasema nikanunue”
Zayana akaendelea kutabasamu, basi mama yake akasema,
“Yani huyo baba kwenye maswala hayo yupo vizuri sana, anajua kuhudumia hadi kumuacha mtu unajiuliza uliza mara mbili, nimuache huyu niende kwa nani?”
Wote wakacheka, kisha mama Mariam akamwambia Zayana,
“Basi mwanangu, nenda kanunue huyo kuku tule jamani mwanangu”
Zayana akatabasamu na kusema,
“Naenda kununua sasa hivi”
Basi akajiandaa na kuondoka kwahiyo Mariam alibaki na mama yake wakiendelea na mambo mengine ila mama yake alifurahi sana kuhusu swala la kwenda kununuliwa kuku, basi Mariam akamtania mama yake,
“Mama siku hizi unapenda kuku eeeh!!”
“Uzee mwanangu, tunataka vitamu tamu midomo icheze”
Mariam akacheka na kuuliza tena,
“Mwanaume wa Zayana ana hela sana eeeh!!”
“Hamna yupo kawaida ila ni mwanaume anayejali sana”
“Ila ndio mchawi”
“Aaaah hayo mambo tumuachie Mungu ndio anayejua, sisi tunaangalia nje tu. Ila ni maamuzi ya Zayana mwenyewe kama kuolewa nae au la”
“Kweli mama”
Wakawa wanaongea huku wakiendelea kufanya mambo mengine.

Zayana alipoenda sokoni kununua kuku kama alivyokuwa akihitaji, basi alifika moja kwa moja na kwenda kwa wale wauzaji na wanyonyoaji maana alitaka aende na nyama tu, basi alinunua na walianza kumnyonyolea ila kuna mbaba alienda kununua kuku pia akamkuta Zayana pale na kumsalimia pale na kuanza kumchombeza,
“Inaonekana unapenda kuku eeeh!!”
“Napenda sana, yani napenda sana nyama ya kuku kwakweli”
“Kwahiyo umechukua kuku wangapi?”
“Mmoja tu”
“Khaaaa mpo wangapi kwenu?”
“Watatu halafu kuna mtoto wa dada jumla tupo wanne”
“Basi sawa”
Yule mbaba aliinuka na kwenda kuongea na yule muuza kuku kisha akarudi pale alipo Zayana na kumsifia hadi wakabadilishana namba ya simu,
“Yani nimetokea kukupenda sana wewe binti, unaongea vizuri hadi raha jamani!”
“Asante sana”
Basi muda Zayana anachukua kuku alishanga akupewa kuku wanne ambapo yule baba akamwambia kuwa kamuagizia kama idadi ya watu nyumbani kwao, basi Zayana alichekelea na kuona raha sana.
Yule baba alimsindikiza Zayana hadi alipofika halafu yeye ndio aliondoka zake, kwahiyo yule baba alijua Zayana ndio anaishi mahali pale.

Zayana alipoenda kuwapelekea walifurahi sana hadi mama Mariam akasema,
“Khaaa haya ndio mambo ya kuzaa binti mzuri jamani yani hadi raha”
Mariam akasema,
“Mmmmh mama jamani kwani mimi sio mzuri?”
“Sina maana kuwa wewe sio mzuri Mariam, ila wewe ni mke wa mtu kwanza ofa za hivi hazikufai ila huyu mdogo wako bado”
Mariam akacheka na kumwambia mama yake,
“Kumbuka mshakula posa ya watu!”
“Aaaah tuachane na hayo Mariam, tupike kuku tule hapa, tule kuku hadi tujisikie jamani. Kwanza tupike kuku wawili”
Walifurahi pale na moja kwa moja walienda kupika wakisaidiana wote watatu ila mtoto alikuwa ametulia tu chumbani kwake.
Basi muda huu walikaa na kuanza kula, ila kuna mgeni alifika na kufanya Mariam ainuke na kwenda kufungua malngo ila alishangaa sana kwani hakumtegemea mgeni huyu, alikuwa ni mama mkw ewake. Akamkaribisha,
“Karibu mama”
“Asante”
Ila huyu mama alionekana kutokuwa na furaha kabisa, alipoingia aliwakuta ndugu wa Mariam wakiwa wanakula basi Mariam akamwambia mama mkwe wake,
“Umekuja muda mzuri mama, karibu mezani?”
“Mmmh hapana, endeleeni tu”
“Jamani mama, basi karibia hata utie baraka tu mama”
“Mmmmh sina baraka ya kutia hapo”
Basi mama Mariam na yeye alimuangalia na kumsalimia kisha kumkaribisha ila alikataa vile vile na kufanya Mariam aende akaendelee kula tu bila tatizo.
Walipomaliza kula, huyu mama mkwe alisema tu mambo mengine hata hakuongelea kilichompeleka pale wala nini kwahiyo Mariam hakujua kitu gani kilimpeleka mama mkwe wake siku ile.

Juma alipotoka kazini tu siku ya leo, moja kwa moja alienda nyumbani kwake kwani hakuwa na sehemu yoyote ya kupitia, alipofika kwake alimkuta mama yake ambapo yule mama aliaga kwa muda ule ule kuwa anaondoka zake ila alihitaji kusindikizwa na Juma tu maana alihitaji kuongea nae, kwahiyo Juma alimsindikiza mama yake stendi, ila mama yake alianza kumsema,
“Hivi Juma mwanangu ni lini utaamka jamani?”
“Kwanini mama?”
“Hebu angalia, mkeo anachokifanya, wakija ndugu zako hapendi na hawahudumii vizuri ila ndugu zake sasa wanakuja na wanahudumiwa vilivyo”
“Kwani vipi mama?”
“Kwanza si ulisema mkeo hapendi wageni wewe, sijui hata ndugu zake hawafiki pale kwako, kwahiyo wale waliofika pale ni wakina nani?”
“Aaaah mama jamani!!”
“Mama jamani kitu gani? Tena wanalala pale pale, mkeo ana roho mbaya tu. Hapendi ndugu zako, anawapenda ndugu zake”
“Jamani mama, wale wamekuja jana tu ujue na sidhani kama watakaa sana”
“Halafu ona ndugu zake anavyowalisha vizuri”
“Mmmmh mama”
“Guna tu, wakati alikuja babako mdogo pale hujajisumbua kumpikia kuku hata mara moja ila wale nimewakuta wanakula makuku jamani, mbona Juma upo hivyo mwanangu!”
“Mmmmh mama unajua unanipa lawama za bure tu, kwenye upishi mimi sipo halafu mke wangu mboga kubwa huwa anapenda samaki na mboga za majani, mara moja moja huwa tunapika nyama tena nyama ya ng’ombe ila mara nyingi pale huwa tunakula maharage na mchicha”
“Huo ni upuuzi, kwahiyo ndugu zako ndio walishwe maharage na mchicha halafu ndugu zake wale makuku! Huo ni ubaguzi, acha huo ujinga Juma, mwanamke gani anakuendesha kiasi hiko jamani! Mwanamke ana roho mbaya yule sijapata kuona”
“Usiseme hivyo jamani mama”
“Nisiseme hivyo kivipi? Ukoo ndio haumtaki hivyo yule mwanamke, hatumtaki, ukoo mzima hawamtaki tunamtaka yule tuliyekutafutia sisi. Hao wanaondoka lini?”
“Sijui mama”
“Kesho asubuhi nakuja, halafu utaona nakuja kufanya nini”
“Jamani mama”
“Hakuna cha jamani, nimechukia sana. Halafu janamke lako lilivyo choyo, hata kunipa mimi kipande kimoja hakuna, nawaangalia tu wanatafuna manyama ya kuku khaaa ule ukoo una roho mbaya sana sijapata kuona”
Yani Juma akajikuta hadi cha kujibu zaidi hana, basi mama yake akapanda daladala na kuondoka ila alikuwa amechukia sana kiasi kwamba aliondoka bila kumuaga vizuri mtoto wake.

Usiku wakati wa kulala, Juma aliamua kumuuliza mkewe kwa ujanja tu maana hata yeye chakula cha usiku ule alipewa zile nyama za kuku,
“Samahani Mariam leo ulienda kununua kuku?”
Mariam alicheka na kusema,
“Khaaaa sikujua kama ungeuliza hilo swali Juma”
“Kwanini nisiulize? Nimeenda kuangalia ninapoacha hela nimekuta zipo vile vile, umenunua na nini hiyo kuku?”
Basi Mariam alimsimulia mume wake jinsi ilivyokuwa hadi wakapika ile mboga ila tu hakumwambia kama kuna kuku alipewa yani alichomwambia ni kuwa alitumiwa hela na kwenda kununua hao kuku wanne, basi Juma akacheka tu na kusema,
“Ila nyie wanawake akili zenu jamani! Yani mdogo wako hata hajapata wazo la kutunza hela nyingine jamani! Yani kaenda kununua yote kuku khaaaa ila Zayana ana akili mbovu sana”
Mariam akacheka tu, kisha Juma aliuliza kuhusu mama yake na Mariam alimwambia jinsi mama yake alivyoenda pale, yani Juma alisikitika tu kusikia kuwa mama yake ndiye aliyekataa chakula yeye mwenyewe halafu alianza kumlalamikia kuwa mke wake ana roho mbaya, yani Juma alitikisa kichwa tu.
Kisha waliamua kulala kwa muda huo.

Asubuhi na mapema, mlango wa nyumbani kwa Juma uligongwa na kumfanya Juma aende kufungua ila alipofungua tu alimkuta mama yake na kumshangaa,
“Mama!! Muda huu kweli?”
“Kwani tatizo liko wapi? Nakuja kwa mwanangu muda wowote niutakao”
“Haya, karibu”
“Nipo na mgeni”
Kisha mama Juma alimuita yule mgeni ambaye alisogea karibu sasa, alikuwa ndiye mwanamke ambaye wanataka Juma amuoe ila Juma alishtuka sana kumuona yule mwanamke na kujibu pale kwa ukali kabisa,
“Simtaki huyo mwanamke mama”

Itaendelea…..!!!
 
MTOTO WA MAAJABU: 38

Kisha mama Juma alimuita yule mgeni ambaye alisogea karibu sasa, alikuwa ndiye mwanamke ambaye wanataka Juma amuoe ila Juma alishtuka sana kumuona yule mwanamke na kujibu pale kwa ukali kabisa,
“Simtaki huyo mwanamke mama”
Mama Juma anamshangaa Juma na kumuuliza,
“Weee mwana vipi wewe?”
Kisha mama Juma alimshika mkono yule binti ili aingie nae nyumbani kwa Juma ila Juma alibamiza mlango na kufunga huku akisema,
“Ondoka mama na huyo mwanamke, simtaki”
Mama Juma anagonga sana ila Juma hafungui mlango yani yule mama alichukia sana,
“Wewe Juma wewe sio akili yako hiyo, umerogwa wewe, huyo mwanamke kakuroga wewe nakwambia. Una nini Juma lakini, hebu nifungulie mlango huko”
Juma hakufungua na kumfanya yule mama azidi kuongea kwa jazba, Mariam akatoka chumbani maana haelewi na kumuuliza Juma,
“Kwani kuna nini, si sauti ya mama yako hiyo nje lakini?”
“Achana nae”
“Mmmmh Juma, mfungulie bhana”
Yule mama na yeye nje aliendelea kuongea,
“Wewe Mariam hizo dawa ulizompa mwanangu kuna siku zitaisha tu na mwanangu atakuwa huru, linga sasa hivi ila dawa zitaisha tu hizo”
Juma alimshika mkono mkewe Mariam na kwenda nae chumbani kwani hakutaka Mariam asikilize yale ambayo mama yake alikuwa akisema pale nje, yule mama aligonga sana na mwisho wa siku aliamua kuondoka huku akiwa amechukia sana kwa ile hali.

Mariam alikuwa akimshangaa tu Juma kuwa kwanini amefanya kitu cha namna ile kwa mama yake,
“Ila Juma jua yule ni mama yako?”
“Najua ndio”
“Umeshindwa nini kumfungulia mlango tu na kumsikiliza?”
“Sijaona sababu ya kufanya hivyo, hata hivyo mama anajua kosa lake kuwa kwanini sijamsikiliza, huwa sipo hivi ukiona imetokea hivi ujue kuwa kuna sababu”
“Haya, sababu ni nini lakini?”
“Mariam acha tu nijiandae niende kwenye kazi zangu maana sidhani kama nitakuwa na maelezo stahiki kwa muda huu”
Na kweli kabisa Juma alijiandaa na kuondoka zake kwani hata mama yake hakuwepo kwa muda huu.
Basi Mariam alitoka na muda huu aliwakuta mama yake pamoja na Zayana wakiwa sebleni aliwasalimia pale ila mama yake akaanza kumsema,
“Mmmmh Mariam kumbe kuna mambo yanaendelea ila huwa husemi?”
“Mambo gani mama?”
“Wewe tumesikia yote ambayo mama mkwe wako ameyasema hapo nje, kumbe familia haikutaki Mariam na wanadai kuwa wewe ni mchawi unamroga mtoto wao”
“Kheeee makubwa, sasa mimi nimroge Juma kwa lipi jamani! Mbona mambo ya ajabu hayo? Kwahiyo ndio alivyokuwa anasema?”
“Ndio, na inaonekana kwao wakina Juma wamemtafutia mwanamke Juma nadhani ndio mama yake alikuwa amekuja nae”
“Kheeee huyo mama ana wazimu au ni kitu gani? Kweli unaweza kumpelekea mtoto wako mwanamke mwingine wakati yupo kuishi na mwanamke mwingine jamani? Huo ni upuuzi kwakweli sijapata kufikiri kabisa”
“Ila mbona Mariam ulikuwa husemi yote haya?”
“Niseme nini mama wakati nilipojifungua tu uliona, kitu kidogo mama akaongea utadhani nimefanya nini hadi nikamuomba msamaha, sijui aseme nimemfundisha mtoto kukataa jina lake, hadi siku aliposonywa nilicheka sana maana kayataka mwenyewe na akaipata”
Yani Mariam hata hakushtushwa kabisa na kuambiwa kuwa mkwe wake alikuwa akilalamika na kumuita mchawi, hata hakuhangaika ukizingatia yeye na mkwe wake kuna viwango ambavyo hawapatani.

Juma akiwa anaelekea kwenye kazi yake, njiani alikutana na yule jirani yake ambaye alionekana kuna ujumbe anahitaji kumwambia ila Juma alimwambia jirani yake huyu kuwa watazungumza badae.
“Ila namba yako ya simu sina jirani, yani huwa nafanya kukuvizia tu”
Juma akampatia huyu jirani namba yake ya simu kisha akaondoka zake na kuelekea kwenye shughuli zake, ila alimkuta Pendo yupo nje kajiinamia, ikabidi amfate na kumuuliza kuwa ana tatizo gani,
“Vipi Pendo, nini tatizo maana umejiinamia hapa”
“Hivi Juma unajuaga kama mimi nina mume?”
“Mmmmh sijui kumbe uliolewa?”
“Ndio mimi niliolewa, tena ndoa takatifu kabisa tulifunga Kanisani na mume wangu”
“Sasa mbona huwa huishi na huyo mumeo?”
“Chanzo ni mama mkwe, hadi namshangaa yule mama hanipendi jamani tena hanipendi kabisa”
“Kwanini hakupendi?”
“Sijui mwenyewe ana sababu zake zipi, sasa mimi na mume wangu tuna watoto wawili ila kwasasa hao watoto wote wapo kwa huyo mama mkwe wangu sababu mume wangu alitafutiwa mwanamke mwingine ndio anaishi nae”
“Duh!! Pole, kwahiyo imekuwaje sasa”
“Kilichokuwa kinanifanya nimtafute mdada wa kazi ni sababu likizo hii nilikuwa nahitaji kuka na watoto wangu na tumekubaliana vizuri kabisa, ingawa sijapata mdada wa kazi ila bado nahitaji kukaa na watoto wangu japo kidogo, nimeenda kuwafata mama mkwe kanikatalia kabisa yani kabisa kabisa kamavile watoto sio wangu”
“Dah!! Pole sana Pendo kumbe una majanga hivyo eeeh!!”
“Ndio, sina raha wala amani hapa, ni kwanini mama mkwe anifanyie hivi lakini?”
“Ila mama mkwe wako sio wa kumlaumu sana, kwani akili mbovu hapo ni za mume wako, kwanini afanye kitu cha kukuumiza? Mtu kaamua kukupenda na kuishi na wewe, anatakiwa kuwa makini sana kabla hajafanya maamuzi yoyote, kwa hilo ni yeye ndio wa kulaumiwa nakwambia”
“Mmmmh ngoja nikupe namba yake ili hata siku ujaribu kumtafuta huyu baba uwasiliane nae maana ananichanganya hatari”
Basi Pendo alimpa Juma zile namba na pale Juma alimshauri shauri Pendo kisha wakarudi kwenye shughuli zingine.

Muda huu wa mchana, Mariam alikaa na ndugu zake mezani huku wakila na kusifia zile kuku maana na leo walipika, hadi Zayana akawa anasema,
“Jamani vya kuhongwa vitamu”
Na wote wakawa wanacheka huku wakiendelea kula, ila mama Mariam akasema,
“Ila imenoga zaidi na hii pilau”
“Ndio mama, bora Mariam alitoa wazo la kula pilau”
Wakafurahi pale na kuendelea kula mara mlango uligongwa na moja kwa moja Mariam alienda kufungua na kuwakuta mlangoni kaka wa Juma na shangazi wawili wa Juma, basi Mariam aliwakaribisha na wakaingia ndani, ila moja kwa moja shangazi mmoja wa Juma aliongoza hadi mezani ambapo ndugu wa Mariam walikuwa wanakula, yule shangazi akaguna na kusema,
“Mmmmh mnakula minyama tu kwa hela ya mtoto wenu, hebu dada njoo uone”
Shangazi mwingine wa Juma akasogea na kuguna pia huku akisema,
“Ndiomana hakuna maendeleo yoyote ambayo yanafanyika, sababu muda wote mwanamke anawaza kuwashibisha mema ndugu zake tu”
Mariam aliwashangaa na kuwauliza,
“Kwani tatizo lenu ni nini? Kama chakula si make mle pia maana ni kingi hiki, hatumalizi peke yetu”
“Muone vile hata aibu huna unaongea tu kama unatapika”
“Shangazi nakuheshimu, mimi ni chizi zaidi yako naomba kama mmeshindwa kukaa hapa muende tu”
“Kwahiyo unataka kunifanya nini na uchawi wako?”
Mariam akachukia, na mama Mariam akagundua hilo, ila sababu alikuwa anamjua mwanae vizuri aliinuka na kwenda kumpooza huku akimtaka atulie kwani anajua ambacho kingetokea kisha mama Mariam akawaambia,
“Jamani tungekaa na kuzungumza ili tujue tatizo ni nini?”
“Hatuna muda wa kuzungumza na nyie wachawi wakubwa”
Mariam alisonya pale na kuwaambia,
“Wachawi ni nyie mlionifungia mimba kwa miaka mitatu halafu mkajifanya kuniletea dawa ya kuweza kujifungua, wanga wakubwa nyie. Naona mnataka niongee vya rohoni na roho mbaya zenu, mnadhani mtaniweza mimi? Mimi ni kisiki cha mpingo,wamenishindwa wachawi na wachawi ndio mtaniweza nyie? Mna nini nyie hapo mlipo, mbele hamchezi na nyuma hamtikisiki, tena msinitibue mashetani yangu huwa sina mtoto wala mkubwa, mama yangu mwenyewe ananielewa vizuri sana ninavyokuwa nikitibuka, nyie ondokeni zenu”
Wale ndugu wa Juma hapo hawakujibu kitu ila waliondoka tu bila kuaga, halafu Mariam alikaa pale mezani na kuendelea kula yani hakuwa na wasiwasi wala tatizo lolote lile.

Muda huu ndugu wa Mariam walijiandaa na kutaka kuondoka hadi Mariam alisikitika kwakweli kwani hakupenda waondoke siku ile,
“Jamani mama kwanini muondoke leo?”
“Hakuna jinsi mwanangu, yani naona ndugu wa mumeo wanaona tunafaidi sana hapa, bora wasitukute”
“Yani mnababaishwa na wale viumbe mama? Hata wasiwashangaze wale, mimi hata sijali wala nini”
“Hata kama wewe hujali, ila sisi tunajali, hatuwezi kwakweli kuendelea kuishi mahali hapa”
Zayana na yeye akasema,
“Ila dada acha tu tuondoke.afu si unajua kama mama ana presha eeeh!! Basi tusisababishe mambo mengine hapa”
Basi Mariam hakuona sababu ya kuendelea kuwalazimisha kukaa mahali hapo kwani aliwaruhusu tu muda huo kuondoka.
Walipomaliza alitoka na kwenda kuwasindikiza, yani wakati wako njiani ndio wakakumbuka,
“Jamani mtoto? Hatujamuona leo mtoto! Yuko wapi kwani?”
“Nadhani leo hajatoka”
“Kwanini sasa? Usikute ni mgonjwa jamani!”
“Sidhani, atakuwa kaamua tu”
“Hapana Mariam usiseme hivyo, mbona roho imeniuma sana. Twende kumuangalia jamani!”
“Ila mama mmeshafika karibu na stendi ndio mrudi kumuangalia kweli?”
“Ndio, hata kama ana mambo ya ajabu ila bado ni mtoto sidhani kama tunatakiwa kutokumkumbuka”
Basi Mariam alikubaliana na mama yake kisha moja kwa moja alirudi nao nyumbani hadi chumbani kwa mtoto ambapo walimkuta kalala hoi kabisa,
“Sasa kalala mama, nifanyeje?”
“Weeee Mariam, hata kipindi nawalea sijawahi kuwaacha mlale siku nzima, hata kama mnaumwa lazima nitakuamsha na kukuongelesha yani Mariam huna hata habari, mtoto hajaamka toka asubuhi unaona kawaida tu!”
Bibi akajitia ujasiri na kwenda kumuamsha mtoto ambaye aliamka akiwa anausingizi sana ila yule mtoto alikaa na kuongea kwa sauti ya usingizi na kitoto kwa muda huu,
“Asante bibi kwa kuniamsha, njaa inaniuma sana”
“Sawa, amka mjukuu wangu”
Mama Mariam akambeba huyu mtoto hadi sebleni na kumwambia Mariam ampakulie chakula na leo yule mama alimlisha mwenyewe huyu mjukuu wake na baada ya hapo alienda kumuogesha na kisha walimuaga ila huyu mtoto hakuwakatalia kuondoka kama siku ile kwani aliwaaga tu vizuri,
“Wasalimie huko bibi”
“Asante mjukuu wangu, nitawasalimia”
Kwahiyo alimuacha kwenye kochi kisha Mariam alimwambia tu huyu mtoto kuwa anawasindikiza mara moja, na mtoto alikubali ambapo Mariam alienda kuwasindikiza.
Njiani mama Mariam akasema,
“Ila Mariam mtoto wako labda ni kuongea kwake tu ndio kwa ajabu ila mbona ni mtoto wa kawaida tu kama watoto wengine? Leo nimeweza kumuangalia vizuri sana wakati namuogesha, mbona ni mtoto wa kawaida kabisa?”
“Yani mama, tatizo la yule mtoto ni mambo anayoyafanya ndio hapo kuna tatizo zaidi”
“Ila kwasasa Mariam kuwa karibu na mtoto sababu sioni tatizo alilokuwa nalo, ni mtoto wa kawaida tu kama walivyo watoto wengine”
Hapo Mariam hakusema zaidi akaamua tu kuweka mada nyingine kwani mama yake alishamtetea mtoto vya kutosha, aliendelea tu kuwasindikiza.

Juma alivyokuwa anarudi tu alipigiwa simu ila alishangaa sana maana ile namba alikuwa kaitunza kwenye simu yake kama Shemeji, mume wa Pendo. Alishangaa kuwa yule ameipata wapi namba yake hadi kumpigia? Akahisi huenda Pendo kampa huyo mumewe namba yake ya simu, basi Juma akaipokea ile simu,
“Hallow, umesharudi?”
Juma alishangaa kidogo ila akajibu,
“Ndio narudi muda huu”
“Nakukuta wapi sasa?”
“Mmmmh unanifahamu vizuri?”
“Kwani uko wapi muda huu? Nakufahamu ndio ingawa hunifahamu kwa jina ila nikija utanitambua”
“Mmmmh nipo kwenye njia ya kwenda nyumbani kwangu”
“Basi nakuja muda sio mrefu”
Yani Juma alikuwa bado anashangaa na kweli muda sio mrefu alifika yule jirani yake na kumsalimia, bado Juma alikuwa akimshangaa na kuamua kumuuliza,
“Samahani, mkeo anaitwa Pendo?”
Yule jirani alishangaa pia na kumuuliza,
“Kwani unamfahamu Pendo?”
“Ndio namfahamu na leo Pendo amenipa ya mumewe, nimeshangaa wewe umenipigia simu imekuja kwenye ile namba”
“Mmmmmh kwani Pendo unafahamiana nae vipi?”
“Nafanya nae kazi”
Yule alishangaa kidogo na kuuliza tena,
“Inamaana Pendo kakupa namba yangu ya nini?”
“Kwanza nijibu, Pendo ni mke wako?”
“Ni mke wangu ndio ila ni mke wangu wa zamani, kuna historia ndefu hapo naomba tuongee siku nyingine”
Halafu alianza kuondoka, Juma akamuuliza,
“Sasa ulichotaka kuongea na mimi leo?”
“Hapana, tuongee tu siku nyingine”
Aliondoka kabisa yule jirani na kumuacha Juma akaimshangaa tu pale hadi alipoishia kabisa ndipo Juma alipoendelea na safari ya kurudi nyumbani kwake.

Usiku wa leo, Mariam alimsimulia Juma kuhusu kile ambacho ndugu zake wamekifanya kwa siku hiyo yani hadi Juma alichukia sana na kusema,.
“Khaaa ndiomana wanakazana kunipigia simu na kunisisitiza niende kwenye kikao cha familia kumbe kuna ujinga ambao wameufanya tayari!”
“Haya tuachane na hayo Juma, niambie kwanza kumbe mama yako kakutafutia mke mwingine? Mbona hukuniambia?”
“Sikutaka kukwambia Mariam samahani kwa hilo, ila pia siwezi kukubali kuoa mke mwingine hata iweje. Mama ananiletea kibinti kidogo, kwakweli siwezi kumkubali yule binti hata alete mwanamke wa aina gani siwezi kumkubali jamani, nilishasema nampenda mke wangu na hiyo ndio itabaki kuwa kauli yangu hadi mwisho hakuna cha kubali kauli hiyo maana nakupenda sana Mariam”
Kwakweli Mariam alijihisi raha sana na kitu hiki ndio kinamfanya awe ana furahi muda wote na mume wake na ndiomana hata watu wengine walikuwa wakiongea alikuwa akiwajibu atakavyo kwani anajua ni jinsi gani mume wake alikuwa akimpenda.

Leo Juma ndio aliambiwa aende kwenye kikao nyumbani kwao ila alisema kuwa haendi kwenye kikao wala haendi popote, atabaki tu pale pale nyumbani akisaidiana na mke wake katika mambo mbalimbali.
Muda huu Juma alikuwa nje akisafisha uwanja basi mtoto wake alienda na kumuuliza,
“Baba, kwanini unampenda mama?”
Hapo Juma alikaa kimya kwa muda na kumjibu tu yule mtoto,
“Sababu nampenda tu”
Kisha mtoto akamwambia tena,
“Unajua ni kwanini ndugu zako wanamchukia mke wako?”
Juma aliacha kufagia na kumuangalia yule mtoto kisha akamuuliza,
“Kwanini?”
Mtoto yule akachukua kijiti na kuandika maneno chini ambapo Juma aliyasoma na kushangaa sana.

Itaendelea…..!!!
 
MTOTO WA MAAJABU: 39

Kisha mtoto akamwambia tena,
“Unajua ni kwanini ndugu zako wanamchukia mke wako?”
Juma aliacha kufagia na kumuangalia yule mtoto kisha akamuuliza,
“Kwanini?”
Mtoto yule akachukua kijiti na kuandika maneno chini ambapo Juma aliyasoma na kushangaa sana.
Juma alimtazama tena yule mtoto kisha akamuuliza,
“Kwani umeandika nini hapo?”
Yule mtoto akasema,
“Kwani baba huwezi kusoma?”
“Mmmmh siwezi, hebu nisomee”
“Acha utani baba, soma hapo halafu kama hujaelewa niambie nikuelezee”
“Mmmmh!! Umeandika Mishi, sasa hiyo Mishi inahusiana vipi na mke wangu na ndugu zangu?”
Mtoto akacheka na kusema,
“Baba, wewe ulimpenda sana Mishi bila kujali chochote kile kilichokuwepo kwake, na ndugu zako hao hao ndio waliofanya ukaachana na Mishi na ndio hao hao leo hii wanataka wakufanye uachane na mama, ila kitu usichokifahamu vizuri ni kuwa mama na Mishi wanajuana vizuri sana, waliwahi kuwa marafiki wakubwa sana”
Hapa Juma alikaa na chini ili amuulize vizuri huyu mtoto, alipokaa tu akamuuliza,
“Mbona mama yako huwa nikimuuliza habari za huyu Mishi anakataa na huwa hataki kuziongelea?”
“Je wewe umeshawahi kumwambia mama ukweli kuhusu maisha yako na huyu Mishi? Usikute unachokificha wewe ndio hiko hiko anachokificha mama”
“Mmmmh jamani mbona mtoto unanishangaza sana, kwanza yote haya umeyajuaje?”
Mtoto akacheka, muda huu Mariam na yeye akatoka ndani kwenda pale nje ila Juma alifuta yale maandishi ambayo mtoto kayaandika pale chini hadi Mariam akauliza,
“Ni kitu gani umefuta Juma?”
“Aaaah huyu mtoto anajifunza kuandika, kwahiyo aliandika makorokocho”
“Aaaah ndiomana nasema kuwa huyu mtoto tumpeleke shule jamani, aanze shule huyu maana hapa nyumbani hapamfai”
Mtoto akacheka tena na kumwmabia Mariam,
“Mama, mimi sina sababu ya kwenda shule. Kama kusoma najua, kuandika najua na kuhesabu najua sasa shule mnataka niende kufanya nini?”
Mariam alimuangalia Juma na hawakujibu kwa muda huo bali Juma aliinuka na kuendelea kufagia, wakati huo Mariam alirudi kusafisha ndani.

Usiku wa siku ile, Mariam aliongea na mumewe kwani alitamani sana kujua ni kitu gani mumewe alikuwa akiongea na mtoto wakati anafagia uwanja,
“Ni nini ulikuwa unaongea na mtoto Juma?”
“Hata mimi mwenyewe sijui”
“Hujui kivipi Juma? Nilisogea pale ukasema kuwa mtoto alikuwa anajifunza kuandika ila yule mtoto akakukatalia na kusema kuwa yeye anajua kusoma na kuandika hana sababu ya kujifunza”
Ila Mariam alikaa kimya kwa muda hapo, ingawa Juma hakumjibu vile ila alimwambia Juma kitu ambacho alikifikiria kwa muda ule,
“Hivi Juma, ngoja nikuulize mwenzangu. Hivi ule muda huyu mtoto kasema kuwa yeye anaweza kusoma, kuandika na kuhesabu wewe uliwaza kitu gani kwa muda huo?”
“Mmmmh pagumu hapo, yani moja kwa moja mimi nimefikiria kuwa huyu mtoto wetu ni wa ajabu”
“Tena sio kidogo, huyu mtoto ni wa ajabu haswa Juma, yani mtoto mdogo anafanya mambo ya ajabu kiasi hiki kweli? Unajua inaogopesha sana eeeh!!”
“Kweli inaogopesha, hata alivyoongea pale tumeshindwa hata kuongea zaidi tumebaki kuangaliana tu”
“Ndio lazima tuangaliane, unadhani ni kitu cha kawaida hiko! Mtoto mdogo kama yule aweze kufanya vyote hivyo na wala hakuna shule aliyoenda wala nini”
Muda huo simu ya Juma iliita, alipoangalia aliona kuwa ni baba yake mdogo anampigia, basi akapokea ile simu,
“Bamdogo mbona usiku huu jamani!”
“Ndio, sababu nikipiga mchana huwa hupokei simu”
“Hapana baba, hujawahi kunipigia”
“Wengine wote huwa wanakupigia mchana na wala huwa hupokei simu zao ndiomana mimi nimeamua kupiga usiku”
“Sawa, nisamehe kwa hilo baba yangu. Nakusikiliza”
“Fanya hima Juma uje nyumbani, kuna kikao cha ukoo Ijumaa hii”
“Sawa, nitajitahidi”
Juma hakuongea nae sana kwani muda huo huo alikata simu na kuamuangalia mke wake kisha kuanza kumuelezea kuhusu ile simu, Mariam akasema,
“Mmmmh mbona Ijumaa!! Wanataka kwenda kukufungisha ndoa nini?”
“Wamfungishe nani ndoa? Mimi sio mjinga kabisa, kwahiyo wasifikirie kuwa ninaweza kukubali ujinga, kama mwanamke hawamtaki wao basi ni wao ila mimi namtaka, waniache nikae na Mariam wangu”
Mariam alitabasamu yani alikuwa anaona raha sana akiambiwa hivyo na kumwambia Juma,
“Asante sana Juma, nitakupenda hadi pumzi yangu ya mwisho”
“Asante mke wangu”
Walikumbatiana kwa furaha na kulala kwa muda huo.

Kama kawaida, Juma leo alijiandaa na kwenda kwenye kazi zake kwahiyo nyumbani alibaki tu Mariam na mtoto wake, na siku ya leo Mariam hata alikuwa hana hali nzuri kwani alikuwa akijihisi uvivu zaidi kiasi kwamba alitoka tu sebleni na kukaa, ila alipokaa kwa muda bila kumuona mtoto aliamua kwenda kumuangalia chumbani kwake na kumkuta amekaa yani Mariam ilikuwa ni ngumu kwake kumzoea mtoto wake moja kwa moja, kwani alishindwa hata kuongea ni mtoto ndio aligeuka na kumuangalia Mariam,
“Umekuja kuniangalia mama?”
Mariam akatulia kidogo na kujibu,
“Ndio, maana leo hujatoka kabisa”
Basi yule mtoto akashuka kitandani na kutoka sebleni na Mariam, ambapo Mariam alikaa tena kwenye kochi kisha mtoto akamwambia Mariam,
“Pole sana mama”
“Asante”
“Nakuona kuwa umechoka sana leo, usijali nitakusaidia”
Mariam alimuangalia tu huyu mtoto ambae alichukua fagio na kuanza kufagia pale sebleni na kudeki yani Mariam alikuwa akimshangaa kabisa maana alikuwa akijiuliza mbona hakuna kitu cha ajabu ambacho anakiona pindi huyu mtoto akiwa anafanya kazi? Ila alikuwa akimuona ni mtoto mdogo tu akifanya kazi kawaida kwa kitoto ila tu ile kazi ilionekana kama ilifanywa na mtu mzima ndiomana Mariam alikuwa akishangaa sana.
Mtoto alipomaliza kudeki alienda moja kwa moja kupika ambapo kama kawaida alimwambia tu Mariam amuandalie kila kitu na kuanza kupika.

Juma akiwa kwenye shughuli zake, alijikuta ameshasahau mambo ambayo Pendo alimwambia, basi Pendo alimfata na kumuuliza,
“Juma umenifanyia kazi yangu?”
“Kazi gani?”
“Kheee Juma jamani, nilikuomba uwasiliane na mume wangu yani baba wa watoto wangu ili na mimi nipate nafasi ya kukaa na watoto, nimewakumbuka sana jamani!”
“Oooooh nimekumbuka jambo Pendo, kwanza naomba unisamehe nimeshindwa kuifanya kazi yako vile unavyotaka”
“Khaaaa jamani Juma, nimekuona una busara sana, halafu kweli umeshindwa kufanya hiyo kazi jamani Juma?”
Basi Juma akamuelezea Pendo kuwa huyo jamaa ni jirani yake kiasi kwamba kashindwa hata kuongea nae moja kwa moja kwani ilikuwa kama kumshtukiza tu, kisha Juma akamuuliza Pendo,
“Umewahi kumpigia simu?”
“Yani mimi nikipiga simu naongea na ndugu zake tu, nikimpigia yeye anakata. Halafu hata nikimpigia kwa namba nyingine, akipokea na kusikia sauti yangu anakata, kwakweli huyu mwanaume basi jamani!! Nilimpenda sana ila kwasasa hakuna cha upendo tena, ila nimekumbuka sana watoto wangu, nilitamani hata mimi nipate wasaa hata wa wiki moja tu kukaa na watoto wangu”
“Pole sana, hata mimi sijaweza kuongea nae huyo jamaa”
“Hivi umesema ni jirani yako, inamaana unapafahamu nyumbani kwake eeeh!!”
“Ndio napafahamu”
“Basi, Juma usimwambie tena. Ila nakuomba tu unipeleke nyumbani kwake”
“Kheeeee kwanini?”
“Nahitaji tu kumuona, unajua ni miaka mingapi imepita tangu niachane nae bila kumuona? Ni miaka mitatu sasa, naishi kwa masononeko na masikitiko, natamani hata nimuone tu, niongee nae macho kwa macho kuwa nilimkosea hadi akaamua kunifanyia hivi? Alisikiliza ndugu zake na kuona mimi ni takataka, nilimkosea nini?”
Juma akapumua kidogo na kumuuliza Pendo,
“Si kama unataka kufanya ukorofi?”
“Hapana, mimi sitafanya ukorofi wa aina yoyote ile, ila nilihitaji kuonana nae”
Juma alifikiria jambo la haraka haraka na kuona hapo labda awakutanishe tu bila yule jirani yake kujua, yani yeye ajifanye kama anataka kuongea nae halafu awakutanishe na Pendo, aliongea jambo hilo na Pendo alikubali, kwahiyo alikubaliana nae kufanya hivyo kesho yake yani Juma alimuonea huruma pendo kwakweli.

Juma akiwa njiani, alikutana na yule jirani yake mmama ambaye aliahidi kwenda kumchukua mke wake na kumpeleka msibani, ila huyu jirani alimsalimia vizuri leo Juma hadi Juma alimshangaa na kujikuta akisimama kumuangalia,
“Kheeee mbona unaniangalia hivyo?”
“Hapana jirani, leo umenisalimia vizuri sana tofauti na siku zote”
“Sijaona sababu ya kutokukusalimia jirani yangu, moyo wangu umenisuta ingawa mke wako alinifukuza”
Juma akatulia kwanza na kumuuliza huyu mama vizuri,
“Hivi ni kweli mke wangu alikufukuza?”
“Ndio alinifukuza hata nikashangaa maana alinifukuza kabisa”
“Pole sana jirani, nitakaa na mke wangu tutayamaliza hata usijali jirani, kukiwa na jambo usisite kuja kutuambia”
“Nitajitahidi ingawa kiukweli kabisa naogopa kuja kuwaambia jamani”
Juma hata hakuwa na ya kuongea zaidi na huyu jirani yake kwani alimuaga tu muda huu na kuondoka zake kuelekea nyumbani kwake.

Usiku wa leo, bado Mariam alilalamika kuwa hali yake sio nzuri na kumfanya Juma ampe pole tu, huku akimuuliza,
“Kwani tatizo ni nini?”
“Mmmh hujui tatizo kwani? Si hii mimba, mara nyingine uzazi unasumbua ujue”
“Pole mke wangu jamani, sasa kazi za humu ndani anafanya nani?”
“Mtoto ananisaidia”
Hapo Juma hakutaka kuongea zaidi kuhusu mambo ya pale nyumbani kwake, na muda huo walilala tu.
Kulipokucha, Juma alijiandaa na kwenda kwenye shughuli zake, kwahiyo pale nyumbani alibaki Mariam na mtoto kama kawaida ila hata leo mtoto ndiye aliyemsaidia Mariam kuhusu kazi za ndani na chakula.
“Halafu leo mama, tutapika chakula kingine”
“Chakula gani hiko?”
“Chakula kimoja hivi, kizuri sana mama. Nitakipika mwenyewe leo ila tu utaniandalia vifaa vya kupika”
“Sawa, nitakuandalia hakuna tatizo”
Yani Mariam kwenye swala la kusaidiwa kazi na huyu mtoto alikuwa akiona furaha sana, yeye alikuwa haelewani na huyu mtoto sehemu ndogo tu ila kwenye kusaidiwa kazi alikuwa anapenda sana.

Juma kama jinsi ambavyo alipanga siku ya leo kuwa Pendo akutane na yule mume wake ambaye ni jirani yake, basi moja kwa moja aliwasiliana kwanza na yule jirani yake,
“Jamaa, nahitaji kuonana na wewe”
“Tuzungumzie nini tena?”
“Aaaah kuhusu majirani wa hapa, unajua wewe unawafahamu vizuri sana, kuna mambo nahitaji kuyafahamu pia”
“Sawa, uko wapi?”
“Nipo njiani hapa kuelekea kwangu”
“Nakuja, muda sio mrefu”
Kweli kwa muda mfupi kabisa yule jirani alikuwa amefika na kusalimiana na Juma pale ambapo Juma alimgelesha pale kwa kuulizia habari za majirani wengine.
“Hivi yule mama jirani yetu ni mkweli yule?”
Muda huo alimtumia ujumbe Pendo aweze kufika pale,
“Aaaah yule mama ni muongo sana, kuna muda huwa ni mkweli ila kuna muda ni muongo sana, hapatani na mke wangu kabisa yule”
“Aaaah yani hata mke wangu hapatani nae kabisa”
“Tatizo la yule mama ni……”
Muda huo huo Pendo alifika, yani yule kaka alikuwa kama kaona kitu gani vile maana alishtuka sana na kujikuta akisema kwa nguvu,
“Pendo!!!”
Yani ilikuwa kama ni ajabu kwa huyu kaka kumuona Pendo kwani alimfata na kumkumbatia kwa nguvu sana, yani Juma alibaki akicheka tu kisha akawaacha pale na kuondoka zake kurudi nyumbani kwake.

Wakati wakila chakula cha usiku, Juma alihisi ladha tofauti ya chakula na kuuliza maana chakula ambacho mke wake huwa anapika anakielewa vizuri sana,
“Mmmmh chakula kina ladha nyingine hiki, kapika nani?”
“Mmmmh na wewe Juma, yani unamaana siku nisipopika mimi unajua eeeh! Haya kapika mwanao, umekipenda?”
“Ndio nimekipenda ni kizuri ila mbona ladha ya leo ni tofauti kabisa na kile ambacho aliwahi kutupikia?”
“Mmmmh hayo sijui, waswahili husema ukimchunguza sana bata basi hautaweza kumla, na tule tu hiki chakula tuache habari za kukijadili zaidi tutakosa amani ya moyo bure”
“Mmmmh haya”
Waliendelea kula pale na kuongea kidogo tu halafu walienda kulala, ila usiku wa siku hiyo walishtuka kusikia mlango wa chumbani kwao ukigongwa na hapo Juma aliinuka na kwenda kufungua walishangaa kumuona mtoto wao ndio yuko mlangoni, basi wakamuuliza,
“Kuna shida gani?”
“Chumbani kwangu kuna kitu”
Juma na Mariam wakashtuka na kuogopa, Juma alimuuliza,
“Kitu gani?”
“Twende ukaone baba”
Juma aliogopa zaidi hata kwenda kuangalia aliogopa ila Mariam alimshika mkono Juma na moja kwa moja walienda chumbani kwa mtoto kwa uoga sana ila hawakuona kitu chochote kile na kumwambia,
“Mbona hatuoni kitu”
Mtoto akawauliza,
“Jamani hamuoni yule mtu pale dirishani”
Yani hapo Juma na Mariam walijihisi kama miguu inaisha nguvu kabisa, hata hawakuelewa na walikuwa hawaoni kitu chochote kweli, basi mtoto alienda mezani na kuchukua poda yake kisha aliwapulizia Juma na Mariam usoni, hapo hapo walishangaa sana kumuona mjomba wa Juma yupo kwenye dirisha la mtoto wao.

Itaendelea……!!!
 
MTOTO WA MAAJABU: 40

Yani hapo Juma na Mariam walijihisi kama miguu inaisha nguvu kabisa, hata hawakuelewa na walikuwa hawaoni kitu chochote kweli, basi mtoto alienda mezani na kuchukua poda yake kisha aliwapulizia Juma na Mariam usoni, hapo hapo walishangaa sana kumuona mjomba wa Juma yupo kwenye dirisha la mtoto wao.
Kwa pamoja walijikuta wakimtazama mtoto sasa ila Mariam akasema,
“Hivi mtoto unajua kama sisi tunaogopa zaidi? Kama na wewe unaogopa itakuwaje sasa?”
Mtoto akawaangalia na kusema,
“Mimi siogopi ila nimewaita ili muone kinachoendelea, baba hiki ndio kinachoendelea kwenye ukoo wako kwasasa wanahitaji kumtoa mama kwa gharama yoyote ile. Mjomba wako ni mchawi ila hata na uchawi wake hawezi kuwaona kama mmemuona, au nifanye awaone?”
Mariam na Juma walikaa kimya kisha mtoto akawaambia,
“Uoga wenu ndio unafanya make kimya, baba nakuomba kesho uende huko kwenu wanapokuita kwenye kikao cha familia ila kuna madawa tayari wamekuandalia ili uwasikilize kile wanachotaka ukifanye na ukifatilie, lengo lao kubwa ni wewe kumuoa yule binti, tatizo la dunia ya sasa ni kule kumshindwa mtu na kuamini kama yule mtu ni mchawi zaidi yako, na ndicho kinachoendelea kwenye ukoo wako, wanaamini kuwa mama ni mchawi zaidi yao na wanaamini kuwa mimi nipo kwaajili ya kumsaidia mama, ila sipo kwaajili ya kumsaidia yoyote yule. Mnataka awaone?”
Juma akatikisa kichwa kuwa wanahitaji awaone na kweli muda ule ule yule mjomba aliwaona wakina Juma na kuogopa sana huku akionekana kwenye harakati za kujiyeyusha ili aondoke mahali hapo, mtoto akacheka na kumwambia,
“Mpaka mimi niruhusu kuwa uondoke, ukiwa kwenye hali yako hiyo hiyo waambie wazazi wangu kuwa ulikuja kufanya nini? Na kwanini ulianzia chumbani kwangu?”
Yule mjomba alikaa kimya ila gafla alikuwa kama mtu anayewashwa maana alikuwa akijikuna, basi yule mtoto alikuwa akicheka sana yani yule mjomba alijikuna sana hadi alikuwa akitia huruma, kisha yule mtoto akamwambia yule mjomba,
“Ondoka zako mchawi wewe”
Yule mjomba akayeyuka halafu Juma na Mariam walikuwa wakiangaliana huku wakitetemeka ila mtoto wao akawaambia,
“Sasa mnaweza kurudi na kulala”
Kwakweli ile ilikuwa ni ngumu kabisa, walienda kukaa sebleni huku wakiogopa sana na kujiuliza kuwa ni kitu gani kile? Walihisi kama wakienda kulala basi yule mjomba anaweza akawajia chumbani kwao, mwishowe wakajikuta wakilala pale pale sebleni.
Kulipokucha, wakajikuta wapo pale sebleni huku mtoto wao akiwa pembeni yao yani Juma alikaa na kutikisa kichwa sana na leo aliweza kumuuliza huyu mtoto,
“Hivi kile kilichotokea usiku kina maana gani?”
“Baba, nenda kwenye kikao kwenu utajua”
Juma akaenda kujiandaa ila Mariam alitaka kwenda nae sema Juma alimkatalia kwenda nae kwahiyo Juma aliondoka mwenyewe kwenda kwao.

Mariam akiwa na huyu mtoto wake ndani, aliona hakuna namna pale zaidi ya kuendelea tu kumzoea huyu mtoto, kwahiyo alianza kuongea nae pale kwa kumuuliza,
“Samahani mtoto wangu, hivi mimi kwanini umekuja kwenye maisha yangu?”
Mtoto akatabasamu na kumwambia Mariam,
“Kwasababu ya Mishi”
Mariam alishtuka sana na kumuuliza,
“Kuna uhusiano gani kwa wewe kuja kwenye maisha yangu na Mishi?”
“Mama, usijifanye hukumbuki kitu. Mishi alikuwa ni rafiki yako mpendwa sana, kumbuka ni kipi kilichovunja mahusiano yako wewe na Mishi ndio utaelewa ni kwanini mimi nimekuja katika maisha yako.”
Mariam aliguna tu na kubadili mada,
“Mmmmh!! Naweza kwenda kwenye kikao cha ukoo wa baba yako?”
“Unaweza kwenda ndio ukiamua”
“Ndio, nahitaji kwenda na nitafanya maamuzi hayo. Naomba ruhusa yako”
“Nimekuruhusu ila kila unapotembea unatakiwa kufikiria kuhusu Mishi, fikiria kilichotokea baina yako na Mishi, halafu ndio ufikirie ni kwanini mimi nimekuja katika maisha yako.”
Mariam hakusema neno ila moja kwa moja alienda kujiandaa ili aweze kwenda kwenye kikao kwakina Juma.

Juma alifika hadi nyumbani kwao na kumkuta mama yake akiwa anaanika mahindi kwa muda huo, kwakweli Juma alifika na kufoka,
“Yani mama, ndio mkaamua kunitumia uchawi kabisa jamani! Kwanini?”
“Usiwe mkali Juma, unatakiwa kwanza ujue sababu ya kufanya hivyo ni nini?”
“Haya, sababu ni nini?”
“Juma, mkeo yule ni mchawi sana. Yule mtoto ambaye mkeo amemzaa ni mtoto wa kichawi, najua kuwa umemuona mjomba wako, kaja kutusimulia yote, ila ni sababu ya yule mtoto na mjomba wako alikuwa pale kumdhibiti yule mtoto”
“Kwahiyo mama wewe na mjomba ni wachawi eeeh!!”
“Hapana mimi si mchawi na wala uchawi siujui mimi, ila mjomba wako ni mganga wa jadi anashughulika na madawa, tena mjomba wako ndiye aliyetoa dawa za kumuwezesha mke wako kujifungua yule mtoto aliyejifungua, bila ya hivyo mke wako angekuwa na mimba hadi leo. Sio kwamba tunawachukia Juma, tunawapenda sana ila kuna mambo lazima tuyaondoe katika maisha yenu ili muwe sawa”
“Ila mama, kama mna lengo zuri ni kwanini mtake kuniachanisha na mke wangu?”
“Juma naweza kuongea sana ila kama hujaamua kunielewa huwezi kunielewa, ngoja wote wafike hapa tuanze kikao”
Juma alikuwa na jazba na kukaa ila badae akawaza kama mjomba wake alikuwa na lengo baya kwao ni kwanini ndio aliyetoa dawa mkewe aweze kujifungua baada ya kukaa sana na ile mimba? Hapo Juma hakuelewa kabisa, yani hakuna alichokuwa anatambua wala nini.

Muda wa kikao ulifika na ndugu wote walikusanyika pale na kuanza kikao, kila mmoja aliongea kile ambacho alikifahamu kuhusu mke wa Juma na wengi walimshutumu kuwa mchawi,
“Yule mwanamke ndiomana ni mvivu, ule uvivu wake upo sababu ya uchawi yani yule mwanamke ni mchawi sana. Anajiamini na anajua wazi kuwa Juma huwezi kumuacha”
Mwingine akajibu na kusema,
“NI ustaarabu gani huo eeeh! Hebu angalia, baba mkwe wako yupo hapo unamlisha mchicha na maharage halafu ndugu zako unawalisha kuku tena makuku ya maana, halafu mkweo anakuja hata kumkaribisha na kumpatia chakula unashindwa, kama sio uchawi huo! Yule mwanamke wa Juma ni mchawi kupindukia”
Muda huo huo Mariam alifika kwenye mazungumzo yao kwahiyo yale ya mwisho alikuwa ameyasikia vizuri sana, Mariam aliwasonya pale tena bila kuwasalimia na kuwajibu kwa jazba,
“Hivi nyie ni ndugu gani mnaokaa na kuzungumza maneno ya uongo bila kuuliza kwa undani zaidi? Ndugu zangu walikula kuku sababu waliwatafuta wenyewe, muulizeni huyo Juma kama aliacha hela ya kununulia kuku pale? Mdogo wangu kaenda kujineng’enesha huko na kupata wale kuku halafu mpo kuonge hapa bila aibu kuwa ndugu zangu wanakula makuku, halafu kingine huyu mama mkwe naye ana gubu, mimi na ndugu zangu tulimkaribisha hadi basi ila alikataa katakata, kama nadanganya hapa basi nife muda huu. Halafu kitu kingine, kumpa huyo baba maharage na mchicha kila siku sijaona kama ni dhambi sababu hiyo ni lishe, mtu umri ushaenda kwasasa halafu unataka ule vitu gani? Kwanini mtake kula vitu visivyokuwa na faida katika miili yenu? Sijapenda kabisa, huo uchawi mmenipa nyie? Yani mchawi aache kuwa huyo mjomba anayekuja usiku wa manane kwenye vijumba vya watu kuwanga iwe mimi kweli?”
Mama Shamimu alimuangalia Mariam na kusikitika kisha akamwambia,
“Yani wifi ulivyokuja na jazba na kuongea hapo kanakwamba watu wote hapa ni watoto kwako au ni wadogo zangu, huo ni utovu wa nidhamu, ndiomana unaitwa mchawi, ni mtu gani usiyekuwa na heshima? Unashindwa hata kutambua kuwa hawa ni wakwe zangu? Unashindwa kutambua hawa ni wakubwa zangu? Wote tuliokuwepo hapa hakuna hata mmoja unayelingana nae Mariam, unadhani watu watasema unajivunia nini kama sio uchawi? Kwanini umekuwa mwanamke wa ajabu kiasi hiko?”
Mariam alikuwa kimya kwani alijiona ni wazi kuwa kwa stahili ile amefanya makosa, akakumbuka na maneno ambayo aliwahi kuambiwa na mama yake kuwa anatakiwa kuwa na heshima sana kwa wakwe zake, awe anawaona kama vile ni wazazi wake na si vinginevyo.
Basi hapo aliamua kuwa mpole na kupiga magoti kuwaomba msamaha wakwe zake kwani alijiona kuwa hajafanya kitu kinachofaa kabisa.
Kisha yule mjomba ambaye walimuona usiku akaongea sasa ila Mariam alishtuka sana baada ya kumuona yule mjomba, akasema pale,
“Ni kweli nilikuja nyumbani kwenu kama mchawi ila mimi sio mchawi, mimi ni mganga nilichokuja kufanya ni kugundua kuwa yule mtoto ana kitu gani kikubwa ila yule mtoto ananizidi maana haiwezekani mlikuwa mnaniona halafu mimi nilikuwa siwaoni, nimekuja kuwaona badae, ile ni ajabu sana kwangu. Mimi sio mchawi jamani, Mariam ile dawa ambayo ulipewa na kuweza kujifungua ni mimi ambaye niliitafuta na kumpatia dada ambapo alikuletea wewe, ila kiukweli Mariam mmezaa mtoto wa ajabu na mkimshuhudia kwa macho ya ndani mngeshindwa kuishi nae, tatizo lako Mariam ulikosea kutumia dawa ndiomana imekuwa hivyo ila ungetumia dawa kwa jinsi inavyotakiwa basi toka mwanzoni ingekuwa rahisi kumdhibiti yule mtoto katika maisha yenu”
Hapo Mariam akawa mpole zaidi maana ni kweli alikosea masharti katika kutumia ile dawa sababu tu alichoka kukaa na ile mimba na alitamani iwe haraka sana aweze kujifungua, basi Mariam aliongea kwa upole,
“Jamani naomba mtusaidie cha kufanya, sio kumchukua Juma aoe mwanamke mwingine maana mimi bado mnaniacha kwenye wakati mgumu. Nisaidieni na mimi niondokane na hili tatizo”
Yule mjomba akasema tena,
“Laiti mngejua nimtoto wa aina gani mnaishi nae basi nina uhakika msingekubali tena kwenda kuishi na yule mtoto, msingekubali kwenda kulala nyumba moja na yule mtoto maana yule mtoto ni wa ajabu na sijajua ni kwanini amekuja katika maisjha yenu”
Yale maneno yalimfanya Juma na Mariam kushikwa na uoga wa kurudi kwenye familia yao, yani walijikuta wakiogopa kuwa itakuwaje kwa mtoto huyo kwenda kuishi nae tena ndani ya nyumba? Wakajikuta wakiogopa.
Basi familia ilianza kujadili cha kufanya na yule mtoto na wakajadili ili wajue nikitu gani kwa muda huo kitawafaa Juma na Mariam,
“Je tutarudi tena kule nyumbani kwetu jamani? Mbona uoga sasa?”
“Kwa leo hamtarudi maana yule mtoto hafai kabisa katika maisha yenu”
“Kwahiyo leo tutalala hapa hapa?”
“Ndio, hadi tutafute dawa ambayo itawawezesha nyie kwenda kule bila kudhurika chochote toka kwa yule mtoto”
“Asante mjomba”
Basi walikubaliana pale kuwa kwa siku hiyo watalala hapo hapo hadi ambapo dawa itatafutwa na kuwawezesha wao kutokudhurika tena na yule mtoto.

Jioni ya siku hiyo, Mariam na Juma walikuwa wamekaa pamoja wakijadiliana kuhusu yule mtoto ambaye wanaishi nae na ambaye wameambiwa kuwa ni mtoto wa ajabu, basi wakajiuliza pale,
“Kama yule mtoto ni mbaya ni kwanini asitudhuru siku zote hizi ambazo tumaishi nae?”
“Mmmh hapo pagumu kuelewa, pengine leo kaujua ukweli halisi ndio atatudhuru”
“Ila mimi sidhani hiko kitu, unajua kwanini Juma? Yule mtoto tulianza kuwa na mashaka nae toka mwanzoni ila mbona hajawahi kutudhuru? Mbona hajawahi kutuletea tatizo lolote lile? Mmmmh sijui lakini”
Waliongea ila waliamua kwenda ndani ili kuangalia kama chakula kitakuwa tayari ukizingatia siku hiyo toka asubuhi ni hawakula chakula, ila walipofungua malango walishangaa sana kujikuta wakiingia ndani ya nyumba yao na mtoto wao ndio alikuwa mezani na kuwakaribisha,
“Karibuni mezani baba na mama”
Juma na Mariam waliangaliana ila hakuna aliyeweza kukimbia wala nini, badala yake waliamua tu kusogea pale mezani alipo mtoto wao na kukaa, kisha mtoto akawaambia,
“Mbona mmekaa tu, pakueni chakula muweze kula”
Bado hawakujibu kitu, walipakua chakula na kula ila kile chakula ndio kilimfanya Juma aongee,
“Kheee mbona chakula ni kitamu sana?”
Mtoto akacheka na kusema,
“Sababu nimepika mimi ndiomana chakula ni kitamu”
Basi waliendelea kula na walipomaliza sasa mtoto akawaambia,
“Mnataka kurudi kule kule mkapewe dawa ya kuwazuia mimi kuwadhuru au mnataka kubaki hapa hapa nyumbani? Mimi nimewaonea huruma, hamjala tangia asubuhi ndiomana nikawaita kuja kula”
Walijikuta wakiangaliana tu na kuwa kimya, kisha mtoto akasema tena,
“Ila mama mara nyingine unachekesha sana, wewe ni mwanamke umefika ugenini umetulia ili na wewe uitwe kula chakula kama wanaume wanavyoitwa, na leo ungekomeshwa wewe maana ilikuwa ni kipimo cha kukupima akili na ufahamu wako kuwa utafanya nini? Toka asubuhi unaona kabisa hakuna chakula mlichopewa, kama mwanamke umeshindwa kabisa kujiongeza, kuwa jamani mama mkwe, vitu viko wapi nipike? Ungeonekana hatankuwasha moto na kufanya mambo mbalimbali ila ndio kwanza umekaa ukiongea ukisubiri kuitwa kula, halafu mmekaa na kujifikiria kuwa njaa zimewawashika sana, mnataka mwende ndani kuangalia kama kuna chakula, ni mzima kwlei wewe mama? Yanio leo familia nzima ingekubaliana kuwa ni sahihi kabisa kwa baba kutafutiwa mwanamke mwingine maana wewe ungeonekana humfai kabisa, mwanamke mvivu umepitiliza, upo ukweni unasubiri kuitwa ili uandae tumbo na kula tu! Ni hasara kwa mwanaume kuoa mwanamke wa aina yako mama, kwahiyo muda mwingine muwe mnanishukuru nimewaokoa, yani dawa ambazo mngepewa ni za kusahauliana ili baba apate nafasi ya kuoa mwanamke mchapakazi na sio mvivu kama wewe mama!”
Hapo Mariam alikaa chini tu na kuinamisha macho chini, kisha alimwmabia mume wake kuwa waende chumbani tu kulala maana kila alichoambiwa na yule mtoto kilikuwa ni cha kweli kabisa.

Usiku ule hata Juma aliamua kumsema mke wake maana aliona wazi kuwa alichosema yule mtoto kilikuwa ni cha kweli,
“Inawezekana kwa asilimia zote kuwa huyu mtoto ni wa ajabu na anafanya mambo ya ajabu ila kila anachokisema kwako mke wangu ni cha kweli maana Mariam mke wangu sio uvivu huo bali ni balaa maana wewe ni mvivu umepitiliza mke wangu”
“Jamani Juma, nimesikia vizuri alichoniambia mtoto na imeniuma haswa, hivi ni kwnaini mimi ni mvivu kiasi hiki lakini?”
“Hapo unatakiwa kujiuliza kwa makini zaidi, ni kwanini ni mvivu hivyo? Mtu hadi wakati nataka kukuoa mama yako ananiuliza mara mbilimbili utamuweza huyu mwanamke? Namjua vizuri mwanangu huyu ni mvivu kupitiliza, utamuweza? Nikasema namuweza maana nampenda sana. Ila kiukweli Mariam ni mvivu sana mke wangu”
“Ila kadri siku zinavyozidi kwned anajirekebisha Juma, kwasasa sio mvivu kama kipindi kile cha mwanzoni”
“Ndio umebadilika ila bado hujabadilika kile kiwango ambacho mtoto anataka ubadilike, jitahidi mke wangu utoke katika kundi la wavivu, inawezekana ni kweli kabisa ndugu zangu walitaka kukupima leo maana kwanini hakuna chakula kabisa? Unajua sio kawaida kwa pale nyumbani ukizingatia mama yangu anapenda sana kupika, ila tangia asubuhi kweli hakuna msosi jamani! Imenishangaza sana”
Wakajikuta wanajadiliana sana kuhusu lile swala ambalo limetokea na moja kwa moja kaumua kulala tu.

Juma alipoamka leo, hata hakujali kuwa karudi kwake jana kimiujiza wala nini, badala yake alijiandaa vizuri kabisa na kwenda kwenye shughuli zake.
Nyumbani alibaki mtoto pamoja na Mariam ila leo Mariam alipoamka tu, alianza kusafisha nyumba na kisha alipika kifungua kinywa na kukaa na mtoto kuanza kunywa chai, kwakweli mtoto alifurahi na kumwambia Mariam,
“Ndio, huyu ndiye mama ninayemuhitaji mimi na sio mama wa kutia aibu kwa watu, anaenda ughenini huko anatia aibu tu. Mama unatakiwa kuwa hivi, mama unatakiwa kubadilika maana wewe ni mama. Hakuna sifa yoyote ya mwanamke ambayo imeandikwa kuwa mwanamke anatakiwa kuwa mvivu, huwa wanasema kuwa mwanamke ni mchapakazi, jasiri, anajituma, anaihudumia familia sasa ukiwa mwanamke mvivu utaihumia vipi familia? Utajua vipi anachopenda mumeo na watoto wako? Huna muda wa kumuogesha mtoto wako, huna muda wa kuangalia mwanao anasumbuliwa na kitu gani, hapo unakuwa sio mama tena na wala sio mwanamke”
“Nimekusikia mtoto na nitajitahidi kwa kadri ya uwezo wangu kujirekebisha, nitafanya mambo mazuri kuanzia sasa”
“Na uache hiyo tabia mbaya ya kumjibu baba hovyo, na tabia yako ya kuropoka utakacho popote pale, unatakiwa kuwa na staha mama. Tunafanya hivyo tunaojiamini na ndiomana mtu wa hivyo hujulikana kuwa ana kitu kingine cha ziada”
Yani Mariam alikuwa akimsikiliza huyu mtoto wake na akimuangalia kwa makini sana kwa kitu ambacho alikuwa akiongea.

Juma akiwa kwenye shughuli zake leo, alifatwa na Pendo ambapo Pendo alikuwa akimshukuru sana Juma kwa kile alichokitenda,
“Kwakwlei Juma asangte sana”
“Ndio, imekuwaje?”
“Huwezi amini, siku ile pale niliondoka na baba watoto wangu na kurudi nae nyumbani!”
“Kheeee, kwahiyo kwa mke wake yule je?”
“Yule mwanamke alimpa dawa jamani, alimpa dawa mume wangu. Mbona alivyoniona mimi kashtuka sana, kajikuta akikumbuka kila kitu kuhusu mimi na yeye, walinifanyia dhambi sana kunitenganisha na mume wangu, kiukweli nampenda sana mume wangu ila sababu ya hasira ndiomana nilisema kuwa simtaki tena”
“Ila hongera kama amesharudi nyumbani, nitapanga siku nije kuongea nae huko huko”
“Karibu sana, njoo uongee nae. Ila ndugu zake bado hawajui kama naishi nae kwasasa, kuna watu wamenishauri kuwa niende nae kwe nye maombi kwanza, ndio leo nataka kwenda nae maana na yeye amekubali kufanya hivyo sababu haielewi akili yake”
“Dah!! Pole lakini, nakutakia mafanikio huko uendako”
Muda huo huo Pendo alimuaga na kuondoka zake kurudi nyumbani kwake.

Leo Mariam aliamua kwenda sokoni mara moja maana hapakuwa na mboga kwa siku hii nyumbani kwao, halafu alikuwa anatamani samaki, basi moja kwa moja alipotoka sokoni tu aliamua kwenda kwenye samaki na kununua ila wakati anarudi alikutana na jirani yake ambaye alimsalimia na kumuuliza,
“Samahani, huwa nashindwa kujua jina lako ndugu yangu, hivi huwa unaitwa mama nani maana najua kuwa una mtoto”
Mariam alikaa kimya kwa muda na kusema,
“Aaaah usijali, niite tu Mariam nitakuelewa”
Mariam hakuongea sana na huyu jirani ila alimuaga na kuondoka zake, ila aliona kuna umuhimu wa mtoto wake kuwa na jina, aliondoka kurudi nyumbani kwake huku akiwaza jambo hilo.
Alipofika nyumbani kwake, alipika huku akiwaza sana jambo hilo yani swala la kujua jina la mtoto wao lilimpa shida kwa kipindi hiki.
Sasa muda wa kula chakula cha usiku wakati huo wakiwa wote mezani yani Mariam, Juma na mtoto ni hapo ambapo Mariam alijikuta akisema,
“Jamani leo nimekutana na mtu na kaniuliza kuwa naitwa mama nani? Yani imeniuma sana kwa mtoto wangu kutokuwa na jina, natamani nijulikane jina naitwa mama nani ili iwe rahisi kujitambulisha, nisijiite Mariam wakati nina mtoto tayari”
Juma akamuangalia mtoto na kumuangalia mke wake kisha akasema,
“Ni wakati wa kumuuliza mtoto wetu jina lake sasa”
Mariam akamuangalia mtoto na kumuuliza,
“Mtoto wetu, naomba utuambie unaitwa nani?”
Mtoto akacheka na kusema,
“Mimi sitawatajia jina langu ila nitawatajia jina la mdogo wangu huyo ajaye, kwa maana hiyo mtakuwa mnatumia jina hilo kujiita ila mimi endeleeni tu kuniita mtoto”
Mariam na Juma wakaangaliana na kumuuliza tena,
“Haya, jina la huyo mdogo wako ajae ni nani?”
Mtoto akatabasamu na kusema,
“Mtamuita Moza”
Juma na Mariam walishtuka sana.

Itaendelea…..!!!!
 
MTOTO WA MAAJABU: 41

Mariam akamuangalia mtoto na kumuuliza,
“Mtoto wetu, naomba utuambie unaitwa nani?”
Mtoto akacheka na kusema,
“Mimi sitawatajia jina langu ila nitawatajia jina la mdogo wangu huyo ajaye, kwa maana hiyo mtakuwa mnatumia jina hilo kujiita ila mimi endeleeni tu kuniita mtoto”
Mariam na Juma wakaangaliana na kumuuliza tena,
“Haya, jina la huyo mdogo wako ajae ni nani?”
Mtoto akatabasamu na kusema,
“Mtamuita Moza”
Juma na Mariam walishtuka sana.
Yani walijikuta wakiangaliana na kusema kwa pamoja yani kila mmoja alikuwa akimuuliza mwenzie,
“Unamfahamu Moza wewe?”
Mariam akajibu,
“Uwiiii naogopa mimi”
Juma naye akajibu,
“Sitaki hata kumkumbuka huyo mtu”
Mtoto akacheka na kusema,
“Yani nyie hamna tena cha kuchagua, hapo mkubali au mkatae ila uzima wa mtoto wenu huyo ajae unategemea na hili jina mtakalompa, mnatakiwa kumita Moza, kwahiyo kuaniza sana baba na mama mtaitwa baba Moza na mama Moza”
Mariam na Juma walitazamana na hawakuongea neno lolote pale hadi walipomaliza kula na kwenda kulala.

Wakiwa chumbani waliamua kuongelea kuhusu lile swala ambalo liliibuka kwa muda wakiwa wanakula,
“Hivi Mariam umemuelewa huyu mtoto?”
“Mmmh sijamuelewa, ngoja nikuulize. Unamfahamu huyo Moza anayemsema mtoto?”
“Yani mke wangu sijui nikuelezeje, ila hapo kuna stori Fulani imejificha”
“Ipi hiyo? Niambie ili nielewe kuwa kuna kitu gani na tujue kwamba tunaanzia wapi?”
“Mke wangu nitakueleza tu, ila nipe muda. Ngoja na wewe nikuulize, huyo Moza unayemfahamu wewe ni Moza gani maana kama kushtuka na wewe pia umeshtuka”
“Mmmh kweli nimeshtuka ila ni historia ndefu sana”
“Historia ndefu kivipi? Hebu nieleweshe nielewe”
“Siku utakayoamua kuniambia ukweli kuhusu unavyomfahamu wewe na ndivyo mimi nitakavyokwambia ninavyomfahamu”
“Mmmh!! Basi tulale”
Kwa muda huo waliamua kulala tu ila kila mmoja alikuwa na mawazo yake tu.

Leo Juma alikuwepo nyumbani sababu hakuna mahali ambako alienda, basi alikuwa akisafisha safisha nyumba yake. Alipokuwa nje kuna baba mmoja wa makamo kidogo alifika na kumsalimia Juma kisha alimuuliza,
“Samahani, namuulizia Zayana”
“Zayana!! Itakuwa mdogo wake Mariam huyo, haishi hapa”
“Haishi hapa kivipi wakati alinionyesha kuwa anaishi hapa”
“Lini alikuonyesha kuwa anaishi hapa?”
“Kuna siku nilimuona kule kwenye machinjio ya kuku, alikuwa akihitaji kuku na nikamnunulia kuku wa nne, nikamsindikiza hadi hapa, aliniambia kuwa anaishi hapa, basi nilimuacha akiingia ndani na mimi nikaondoka”
“Ooooh basi pole Zayana haishi hapa, kuna dada yake tu hapa ambapo mimi ndio mume wa huyo dada yake, kuna siku kama mbili tatu ndio Zayana alikuwa hapa kusalimia tu lakini haishi hapa”
“Dah!! Kwahiyo kanidanganya, naomba namba yake ya simu”
“Samahani, Zayana ni mchumba wa mtu siwezi kutoa namba yake ya simu”
“Khaaaa kumbe kaniingiza mjini sio!! Poa bhana tutakutana tu”
Yule baba akaondoka zake na kumfanya Juma amshangae tu, kisha Juma alirudi ndani kwa mke wake na kumuelezea, halafu akamwambia,
“Kumbe wale kuku huyo Zayana ni alihongwa?”
“Ndio, mbona niliyasema yote siku ile nimekuja kwenu? Niliongea kila kitu kiwa mdogo wangu kajineng’enesha huko na kupata kuku halafu wanasema kuku umetoa hela wewe!! Ila ndugu zako nao loh!! Wangeuliza basi, hata hivyo hivi wangesema wanataka kuku tusingewapikia? Jamani watu wengine wanapenda maneno”
“Mariam acha kubadili mada, tunaongelea kuhusu mdogo wako hapa. Si mchumba wa mtu yule? Ataanzaje na mwanaume mwingine”
“Juma, kama hakuna cha kujadili basi tunyamaze kimya na tulale maana haiwezekani ukanifanya nijadili mambo ya Zayana, wakati Zayana ni mtu mzima anayejitambua, atajijua mwenyewe, akifanya ujinga na mwanaume wake akajua basi atajijua mwenyewe”
“Sasa Mariam ni muda wa kulala kweli huu?”
“Jamani Juma mbona unapenda marumbano yasiyokuwa na maana? Aarggh unakera sasa”
Juma alishindwa cha kuendelea kuongea, basi kwa muda huo Juma akaamua kuelekea sebleni ambapo Mariam na yeye alitoka ila walivyofika sebleni tu, yule mtoto akawauliza,
“Hivi mmeshawaza kuwa muende mkatembelee nyumba ambayo mmemuacha Anna?”
“Mmmmh!!”
Waliguna na kuangaliana maana hawajawahi kufikiria hilo jambo kabisa, basi Juma ndio akasema,
“Unajua hatujawahi kuwaza kama kuna umuhimu wa kufanya hivyo, itabidi tufanye hivyo”
“Hakuna umuhimu kivipi wakati ile ni nyumba yenu!”
“Ni nyumba yetu ndio lakini ina mambo ya ajabu”
“Unadhani ni nani anayeweza kufanya nyumba yake isiwe na mambo ya ajabu zaidi ya nyie wenyewe, mara nyingine mjifunze kutafakari zaidi”
Mtoto akainuka na kwenda chumbani kwake, na hapo Juma na Mariam wakapanga namna ya kwenda kwenye nyumba ambayo wamemuacha Anna huko.

Usiku ule, Juma na Mariam walipanga kuwa kesho yake waende kutembelea ile nyumba ila wakati wanapanga hayo, simu ya Juma ilianza kuita na kumfanya kuipokea maana aliyekuwa anapiga alikuwa ni mama yake,
“Ndio mama?”
“Ila Juma mwanangu kwanini uko hivyo? Kweli ukaamua kuondoka bila hata ya kuaga kweli?”
“Ila mama jamani, yani toka siku ile ndio unanipigia simu leo? Tulishindwa kukaa maana njaa zilitushika tukaamua kurudi kwetu kula”
“Hivi Juma una akili mwanangu au ni kitu gani kinakusumbua Juma jamani! Mke wako alishindwa kuingia jikoni na kupika kweli? Mbona mambo mengine ni ya ajabu sana mwanangu”
“Sasa mama, Mariam ni mjamzito kwahiyo asingeweza kupika”
“Kheeee Mariam kabeba mimba tena!! Huyo na yeye anayataka jamani!! Haya ngoja nikuulize, inamaana wajawazito wote hawali wala hawafanyi chochote maana hawawezi kupika sababu ya ujauzito”
“Sio hivyo mama, tukiwa nyumbani mbona Mariam anapika, ila hawezi kupika chakula cha watu wengi na hali yake hii aliyokuwa nayo. Hata mimi binafsi siwezi kumruhusu afanye hivyo mama, kwahiyo sio kama alijifanyisha ila ni sababu yupo hivyo”
“Mmmmh!! Laiti kama wanaume wote wangekuwa kama wewe duniani basi wanawake wangekuwa wanajivunia sana, yani Juma huwa hutaki mkeo aonekane kuwa kakosea, utatumia kila njia kumtetea duh!! Haya na kwanini hamjaaga?”
“Mama, naomba utusamehe ni njaa tu”
Mama Juma aliamua kukata ile simu basi Juma akamuangalia Mariam naye Mariam akamuangalia Juma na kusema,
“Kwakweli nina kila sababu ya kushukuru na kujivunia kukupata wewe katika maisha yangu maana umekuwa ni mwanaume wa tofauti sana, kila jambo Juma unanitetea jamani. Naahidi kujirekebisha mume wangu, naahidi kila siku iendayo nitakuwa najirekebisha”
Juma alitabasamu tu na kumkumbatia mke wake, yani Juma alimpenda sana huyu mwanamke kiasi kwamba alimtetea kwa kila kitu.
Kulipokucha leo, walijiandaa maana waliona kuwa safari ya kwanza ni kwenda kumtembelea Anna, basi Mariam alimuuliza mtoto wao,
“Je tutaenda wote au unaacha twende wenyewe?”
“Aaaah nyie nendeni tu mama, mie mtanikuta tu hapa hapa nyumbani”
Kwahiyo Juma na Mariam walijiandaa kwa muda huo na kuondoka zao.

Moja kwa moja walienda mpaka kwenye ile nyumba ambayo anakaa Anna, ila palikuwa ni kimya sana, walipoangalia kwa mbali walimuona kama Anna analima na kupanda vitu kwenye bustani ya pale pale nyumbani, basi Mariam akamuita,
“Anna, Anna”
Basi Anna alienda mpaka pale na kuwasalimia ila kitu walichomshangaa ni kuwa Anna alionekana kupooza sana yani kama kuna kitu kimemkumba, alionekana kutokuwa na raha kabisa, basi Mariam alimuuliza,
“Tatizo ni nini Anna?”
“Dada, nauchukia uchawi, nauchukia uchawi mimi natamani kuacha ila nashindwa sijui nifanyeje”
Mariam na Juma waliangaliana kwa muda, kisha Juma alimuuliza Anna,
“Kitu gani kimekukumbua hadi uuchukie uchawi ikiwa kila siku ulikuwa ukikataa kuwa wewe si mchawi?”
“Jamani, mimi sikupenda kuwa mchawi ila mama yangu alinipa uchawi toka nikiwa mdogo kabisa na uchawi ule ulifanya nimsaidie kufanya mambo yake mengi sana. Sikuwa mtoto mzuri, sikuogopa mkubwa wala mdogo maana wote nilikuwa ninawamuda, shule niliyokuwa nasoma nilisoma kwa kiburi na hakuna mwalimu hata mmoja aliyenibabaisha ila baada ya kufa mama mambo yalibadilika sana, ndio hapo nilishindwa hata kuishi na ndugu zangu, niliwaua kaka zangu kiuchawi yote kutaka kuongeza nguvu ila badae nilijilaumu sana, toka siku ile yule dada yangu hataki kabisa kuniona, ananichukia sana ingawa aliahidi kunitunza baada ya kifo cha mama ila yeye ndiye amekuwa wa kwanza kunifukuza, siwezi kumlaumu sana, kwani ni mimi na uchawi wangu ndio nimesababisha yote yaliyotokea. Ila sasa hapa kwenye mtaa wote hawanitaki wananiita mchawi, siwezi hata kwenda kununua chumvi, ndiomana mnaona napanda ili angalau nipate chakula maana hakuna pa kwenda kununua labda nikachukue kiuchawi, yani nauchukia uchawi kwasasa, hakuna mtu anayetamani kuwa kama mimi wote wananichukia”
Mariam aliamua kukaa kabisa na kumsikiliza kwa makini Anna, kisha akamuuliza,
“Kwahiyo ni wazi kabisa unataka kuacha uchawi?”
“Ndio dada, nimechoka kuwa mchawi”
“Ngoja nikuulize Anna, kwanini mama yako alikufa? Alikuwa anaumwa au ni kitu gani?”
“Hapana, mama yangu hakuwa mgonjwa ila hapo kati kuna historia ya ajabu sana ambayo ilitokea katika maisha yetu na kupelekea mama yangu kufa”
“Historia gani hiyo, hebu tuambie kinagaubaga leo Anna”
“Ni hivi dada, kuna mdada wa kazi alipatikana kwetu na huyo mdada alikuwa na mambo ya ajabu sana, alikuwa ni mbea kupita kiasi, yani kila kitu lazima achunguze hadi mimi nikagombana nae sana sababu ya tabia yake hiyo, hata mama aligombana nae. Ila nahisi mama ndio aliamua kumuua yule mdada, kitu ambacho kilienda vibaya sababu ya dawa ambayo mama alitumia, maana makaburini hali ilibadilika na baada ya hapo yule mdada alikuwa akitutokea ndani na kutusumbua sana hadi mwisho wa siku alimuua mama yangu kwa kumchoma ndani na nyumba, sisi tulinusurika basi tu kwa kutolewa nje kabla ya tukio ila yule dada ndiye aliyemuua mama yetu. Siwezi kusahau ila mama yangu na yeye alikuwa ni mchawi sana”
“Mmmmh hatari, mama yako aliitwa nani?”
“Aliitwa Rose”
Hapo Juma alishangaa kidogo na kuuliza,
“Sasa mbona dada yako kampa mtoto wake jina la mama yako ilihali mama yenu alikuwa ni mchawi sana?”
“Sikatai, ni kweli mama yetu alikuwa ni mchawi sana ila bado inabakia pale pale kuwa mama ni mama hata iweje bado mama atabaki kuwa ni mama. Alikuwa mchawi ila alituzaa na kutulea, na kutusomesha alitusomesha, na maisha mazuri sana tumeishi na uchawi wake ila tumeishi vizuri sana, uchawi wa mama yetu bado hauwezi kubadili jambo kuwa yule ni mama yetu. Mimi sipendi uchawi ila mama nampenda hadi kesho, huwa namkumbuka sana”
“Duh!! Kweli mama ni mama”
“Ila yule mdada wa kazi alikuwa wa ajabu sana, huwa nikikumbuka hata jina lake nasisimka sana”
“Aliitwa nani?”
“Alikuwa anaitwa Moza”
Hapo Juma na Mariam walishtuka sana na kuangaliana kwa makini huku kila mmoja kujikuta akishindwa kusema chochote na hapo hapo walimuaga Anna, huku wakimuahidi kuwa watampelekea mahitaji ila hawakutaka kuongelea tena habari ile.

Njiani walijikuta wakijadiliana sana kuhusu lile swala lililoongelewa na Anna, na haswa hilo swala la moza, basi Mariam alimuuliza mume wake,
“Hivi Juma, mpaka sasa hapo umeelewa kitu gani?”
“Yani kwa haraka haraka nilichoolewa ni kitu huyo Moza ndio anayetusumbua sisi”
“Mmmmh ila sisi tulimfanya nini hadi atusumbue?”
“Hapo, sijui ila moja kwa moja ni yeye ndio yupo katika maisha yetu”
“Yani unajua naongea huku nahisi uoga wa hali ya juu kabisa, najiuliza swali nakosa jibu inamaana huyo Moza ndiye aliyemleta Anna katika maisha yetu maana Anna anamfahamu vizuri sana. Ila kama huyo Moza alishakufa anafanya nini katika maisha yetu? Na kwanini yule mtoto na yeye aseme kuwa huyu mtoto ajae ndio nimuite Moza? Kwanini asijiite yeye na maajabu yake?”
“Hapo ndio pagumu mke wangu, ila naomba nikuulize kwanza. Wewe binafsi Moza unamuelewa kama nani? Leo tuelezane na tusifichane maana ukweli utatufanya tuwe huru”
“Hebu nieleze wewe kwanza maana ninachokumbuka mimi huyo mtu anayeitwa Moza aliwahi kunitokea nikiwa na rafiki yangu”
“Rafiki yako yupi? Huyo Mishi?”
“Mmmmh umemjua haraka sababu alikuwa mke wako eeeh!!”
“Hayo sio maswala maana hata mimi niliwahi kutokewa na huyo mtu wa kuitwa Moza nilipokuwa na huyo Mishi, na hadi sasa nilijua mambo ya huyo mtu yameisha katika maisha yangu”
“Mmmmmh pagumu hapo, alipokutokea alikwambia nini? Inawezekana mimi na wewe ni watu tuliowekewa mtego tangu mwanzo ila tulikuwa hatujijui tu”
“Yani mke wangu habari za huyu mtu naongea hadi nasisimka, sina raha kabisa, nasisimka kwa uoga hapa nilipo. Ukizingatia nishawahi kumuona huyo Moza tena kwa macho haya haya”
Mariam alihisi kuingiwa na hofu zaidi ya pale na kuamua wabadili mada kwanza na warudi nyumbani kwao.

Nyumbani kwao hakuna jambo lolote lile waliloulizwa na mtoto wao kuhusu kule walikokuwa wameenda hadi walipoenda kulala bado mtoto hakuwauliza kitu chochote kile na wenyewe hawakuzungumzia kitu chochote na kuamua tu kulala.
Kulipokucha, Juma leo alijiandaa na kwenda kwenye shughuli zake ambapo alifanya kazi kidogo na kufatwa na Pendo kuwa akamsalimie mume wa Pendo, na kweli Juma aliondoka na Pendo hadi nyumbani kwake na kumkuta yule mwanaume akiwa ndani, basi alikaa nae na kuongea nae,
“Samahani, kwani jirani huwa unaitwa nani?”
“Mimi naitwa Abraham, ila wengi huwa wananiita Abrah”
“Aaaah sawa, maana nilizoea tu kukuita jirani basi. Hebu niambie kwasasa unajihisi vipi?”
“Unajua sijielewi yani, nilikuwa kifungoni mimi hadi wakati huu sijielewi”
“Kivipi ndugu? Kwani ilikuwaje hadi ukamuacha mkeo?”
“Yani sielewi, nakumbuka siku hiyo nilienda kwetu vizuri kabisa kulikuwa na msibani ila tulipotoka pale walinipa maneno mengi sana kuwa mke wangu hafai, sijui mchafu ila nashangaa sijui ilikuwaje nikaondoka na yule mwanamke mwingine na tangia hapo sikuwahi kwenda tena kuonana na mke wangu”
“Duh!! Watoto ulikuwa unawaona lakini?”
“Ndio, sababu watoto walikuwa kwa mama yangu na hata hivyo watoto bado wapo kwa mama yangu yani hapa ndio najifikiria ili nikachukue watoto halafu mimi na mke wangu tukae pamoja tulee watoto wetu pamoja”
“Ooooh huo ni uamuzi mzuri sana, hilo ni swala zuri kabisa kuamua kufanya hivyo. Pendo alinifata ili nije niongee na wewe kidogo”
“Ndio nimemwambia anifanyie hivi maana hata sielewi, sikia jirani yani sitamani tena kurudi kwa yule mwanamke niliyekuwa naishi nae, simtaki wala simuhitaji tena”
“Kwanza pole, ni wazi kuwa yule mwanamke alikupa dawa ila katika maisha dawa zina mwisho wake, na mwisho wa dawa alizokupa umefika na ndiomana akili zako timamu zimekuja, na ndiomana hujataka ujinga tena, umeona ni mambo ya kukukera na hayana nafasi”
“Ndio hivyo, sasa naomba ushauri wa namba ya kwenda kwetu na kuchukua watoto wangu”
“Usiende kwa papara, nenda zako kwa utaratibu kabisa na uongee na mama yako akupatie watoto”
“Sijui lakini naona kama itashindikana”
“Hapana, usiwe na mashaka, amini kuwa itawezekana tu”
Basi Juma alimpa ushauri huyu na kuagana nae, kisha Juma alimua kurudi nyumbani kwake kwa muda huo.

Wakati wakila chakula cha usiku, yule mtoto alipaliwa na kukohoa sana hadi Mariam aliinuka na kumshikilia mtoto wake kifua kwa mara ya kwanza maana hakuwahi kufanya hivyo hata mara moja, kisha alimpa maji ambapo yule mtoto alikunywa kisha akasema,
“Sikutaka kuongea na ndiomana nimepaliwa maana natakiwa kuongea hili”
Mariam na Juma walimtazama na kumsikiliza kuwa anasemaje,
“Ni hivi, baba mpigie simu yule jirani yani yule mume wa Pendo. Mwambie asiende kwao kutaka watoto bali ampigie simu dada yake na akubaliane nae mahali dada yake alete watoto halafu akishawaleta ndio arudi nao nyumbani, halafu kikifanyika kikao cha familia afanye pale pale wanapoishi. Mpigie sasa hivi”
Juma alipumua kisha alichukua simu na kumpigia mume wa Pendo kisha akaongea nae vilevile, hakupunguza neno wala kuongeza kisha waliendelea kula huku wakiwa na mawazo mengi.
Usiku ule wakati wa kulala, Mariam hakuwa na usingizi kabisa, basi alikaa na kumwambia Juma,
“Mume wangu, unajua nini Mishi alikuwa rafiki yangu mkubwa sana ila nilimpeleka kwa mganga”
Juma alishangaa na kumuuliza,
“Mlienda kufanya nini kwa mganga?”
“Mmmmh sijui ila naomba twende kwa yule yule mganga ili nijue ni kitu gani kiliendelea maana hakuna ninachoelewa hapa, usingizi hauji yani kila kitu naona sielewi”
“Ndio huelewi mke wangu, ila sema ukweli kuwa kuna kitu gani kati yako na Mishi?”
“Aaaah, naomba kesho twende kwa huyo mganga”
Juma aliamua kuitikia tu ila kiukweli hakumuelewa kabisa mke wake kwa hilo.

Asubuhi na mapema, Mariama alimka na kujiandaa huku akimtaka Juma na yeye kujiandaa ambapo Juma alijiandaa na kisha kuondoka hapo na kwenda kwa huyo mganga.
Ilikuwa ni safari ndefu maana tangu asubuhi waliyoondoka kwao, walifika mwa huyo mganga saa kumi jioni ila mazingira yalikuwa yamebadilika kiasi hata Mariam asijue pa kuanzia kuuliza ila alimuona kijana mmoja na kumsalimia kisha kumuuliza,
“Eti, babu yupo?”
“Aaaah yule babu mbona alishakufa”
Mariam alishtuka na kuuliza,
“Alikuwa anaumwa au ni kitu gani?”
“Sijui, ila toka amekufa kuna chizi huwa analala kwenye banda la yule mganga kila siku, yani asubuhi, mchana, jioni na usiku yule chizi lazima utamkuta pale”
“Duh!! Hebu tuonyeshe alipo maana mazingira yamebadilika”
Basi yule kijana aliongozana na wakina Mariam hadi kwenye mibanda cha huyo mganga, na kweli walimuona chizi mwanamke yupo nje ya lile banda, walipomuangalia vizuri walishtuka sana.

Itaendelea……!!!
 
MTOTO WA MAAJABU: 42

Basi yule kijana aliongozana na wakina Mariam hadi kwenye mibanda cha huyo mganga, na kweli walimuona chizi mwanamke yupo nje ya lile banda, walipomuangalia vizuri walishtuka sana maana yule chizi alikuwa ni Mishi.
Kila mmoja pale alishindwa hata kuelewa na walishindwa zaidi kumsogelea yule chizi, basi moja kwa moja walimfata mwenyeji mwingine wa pale ili waweze kujua ni kitu gani kilimsibu yule ambaye alionekana ni chizi kwa muda ule.
“Samahani ndugu, hivi imekuwaje hadi huyo dada kuwa chizi?”
“Mmmh hatuelewi chochote ila huyo dada kawa chizi kwa kipindi kirefu sana hadi tunahisi pengine alipewa masharti ambayo alishindwa kuyatelekeza, wengine wanasema huenda alitaka kuwa mganga yani kila mtu anasema lake nakwambia hakuna hata mmoja mwenye jibu la moja kwa moja”
“Duh!! Ila ilikuwaje hadi akawa chizi?”
“Yani kuna siku ambayo alitoka huyu binti na kijana Fulani hivi ila hawakurudi kwa siku hiyo, kesho yake alikuja huyu dada na kukuta kuna msiba wa huyu mganga, basi huyu dada hakuondoka tena hadi tulipozika na baada ya hapo alianza kuwa chizi ndio ni chizi hadi leo”
“Hiyo kali kwakweli, anapiga watu?”
“Ukienda kumuongelesha anaweza kukupiga kwahiyo hakuna mtu ambaye huwa anamuongelesha, huwa tunamuangalia hivyo hivyo analala hapo na kula chakula kilichotupwa”
Mariam na Juma walisikitika sana, kisha walimuaga huyu mama na kuondoka mahali hapo.

Ilibidi Mariam akae na Juma vizuri ili wapate kuongea kuhusu Mishi kwani walihitaji kutambua kwa undani zaidi na kila mmoja alitaka kujua Mishi ni nani kwenye maisha ya mwenzie.
Walitafuta eneo na kuanza kuzungunza,
“Hebu Juma leo naomba tuwe makini na tuambiane ukweli wote ili tuweze kujua kuwa tatizo liko wapi, nieleze vizuri unavyomfahamu Mishi hakuna nitakachofanya kibaya, cha muhimu ni kujua ukweli tu.”
“Sawa mke wangu, nitakwambia ukweli wote pia natumaini kuwa na wewe utaniambia ukweli”
“Sawa, niambie”
Juma alianza kumuelezea mke wake sasa,
“Ni hivi, Mishi ni mwanamke niliyekuwa nampnda sana, kipindi nilipokuwa namfatilia Mishi nilikuwa nakufatilia na wewe yani ni kama nilisema kati ya hawa wawili basi atakayekubali kuwa na mimi ndio nimuoe. Kipindi kabla sijamuoa Mishi nilikutana na yule dada yako wa kwanza ambaye ni marehemu sasa, ingawa si vizuri kumsema marehemu ila nitasema tu kile alichoniambia, aliniambia wazi kuwa hunifai pia aliniambia sifa yako ya uvivu halafu pia alisema kuwa wewe ni malaya na una rafiki yako ambaye anasifika kwao kwa umalaya, kwakweli nikaogopa halafu nyumbani walikuwa wakinikazania sana kuwa niende kuoa ikabidi nikamuoe Mishi sababu nilimpenda pia bila kujua kama sifa ya umalaya basi ndio yake namba moja. Nikamuoa kumbe nilimuoa na mimba ambapo alitaka kunisingizia yani kuja kujua ukweli sikuamini macho yangu na nilitaka kumuacha ila akatokea binti mmoja na kunipa onyo kuwa ole wangu nimuache Mishi na ikitokea nimemuacha Mishi basi atanilaani, yani yule binti alikuwa akinitokea mara kwa mara na kufanya nishindwe kumuacha Mishi. Siku hiyo nilimfumania Mishi chumbani kwangu tena kitandani kwangu, niliumia sana ila sikuweza kumuacha, nilisikitika mno sababu Mishi aliniahidi kurekebishika, sasa kweli kabisa mtu anaenda kukusaliti na mimba kubwa kabisa dah!! Niliumia sana. Ila kesho yake Mishi mwenyewe hakuondoka na hakurudi tena, yani sikumuona tena Mishi hadi leo ambapo tumemuona wote. Baada ya hapo ndio nikaja kukuoa wewe, niliamua maisha yangu yaanze upya kabisa, sikutaka hata ujue kama niliwahi kuoa ndiomana. Nisamehe kwa hilo mke wangu”
“Usijali ila tu nimesikitika kwa dada yangu kukwambia habari za mimi kuwa malaya wakati ni mtu aliyekuwa ananifahamu vizuri sana, hapo pamenisikitisha kwakweli maana hapakuwa na habari ya ukweli, uvivu ndio ilikuwa ni tabia yangu, nasema ilikuwa sababu siku hizi nimejirekebisha sana lakini tabia hiyo nyingine hapana jamani haikuwa tabia yangu”
“Sawa, niambie sasa kuhusu ukaribu wako na Mishi”
“Ni hivi, Mishi alikuwa ni rafiki yangu mkubwa sababu nilisoma nae shule moja, nadhani dada yangu alikwambia kuwa mimi naongozana na rafiki muhuni sababu ya mimi kuongozana na Mishi yani alikuwa ni rafiki yangu sana. Ila cha kusikitisha, Mishi hajawahi kuniambia hata mara moja kuwa anaolewa au aliolewa ndiomana mimi sikupata kukufahamu wewe. Ni mwanaume mmoja tu wa Mishi ambaye nilikuwa namfahamu, alikuwa akiitwa Ommy, huyo mkaka alikuwa na mvuto sana ila sijawahi hata kumtamani, uone kama mimi sikuwa na tabia za Mishi kabisa. Sasa kuna kipindi Mishi alikuwa ni mjamzito, alikuja na kuniomba ushauri kuhusu ile mimba nikamshauri kuwa akatoe maana yeye alisema anataka kuolewa na Ommy halafu kabeba mimba ya mtu mwingine, yani sikumshauri kwa ubaya hata hivyo. Aliniambia kuwa kashajaribu hospitali nyingi sana bila ya mafanikio yoyote, alichokuwa akikitaka kwa muda huo ni mambo ya jadi ambapo napo alijaribu ikashindikana, nakumbuka mara ya mwisho nilimwambia Mishi rafiki yangu naomba uzae tu kama imeshindikana kutoa, huyo Ommy kama anakupenda kweli basi hanabudi kumkubali na mtoto wako pia ila Mishi alikazana kuwa anataka kutoa ile mimba. Mimi nilimuuliza huyo marehemu dada yangu na ndiye aliyenielekeza kwa huyo mganga sababu hata yeye amewahi kwenda kutoa mimba huko, nikapanga siku na kwenda na Mishi kwa huyo mganga, nakumbuka siku ya kwanza alipata dawa, halafu siku ya pili tulienda tena ila ile siku ya pili ndio iliyonifanya nikome kufatana na Mishi tena maana wakati Mishi yupo kwa mganga nilitokewa na mwanamke ambaye nilikuwa simjui ila yule mwanamke aliongea na mimi kwa jazba sana, aliniuliza ni kitu gani kimenifanya kumpeleka Mishi kule? Yule mwanamke alinipa laana na kuniambia kuwa hataki tena niwe na Mishi kisha nikamuona akitoa moto mdomoni jamani nilikimbia uwiiiii ya sehemu ya kwanza kusimama nilianguka kama mzigo basi toka siku hiyo sisemi popote kuwa niliwahi kuwa na urafiki na Mishi”
“Mmmmh pole mke wangu, huyo mwanamke alikupa laana gani?”
“Tutaongea nyumbani mume wangu, ona leo tutafika kweli nyumbani?”
“Labda tukalale kwenye nyumba za kulala wageni maana huku ni mbali sana”
“Na mtoto je peke yake kule nyumbani?”
“Mmmmh tukimfikiria sana mtoto tunaweza kujikuta tunatekwa njiani”
Wakakubaliana na kutafuta nyumba ya kulala wageni kisha wakatafuta chakula na kula na kwenda kulala kwa muda huo.

Kulipokucha, ni Juma ndio alikuwa wa kwanza kabisa kuamka ila alikuwa akishangaa na kumuamsha Mariam ambaye na yeye alivyoamka alishangaa na kumuuliza Juma,
“Mbona tupo nyumbani kwetu?”
“Mmmh hata mimi nashangaa ujue yani sielewi kitu hapa”
Basi wakaamka na kutoka ambapo walimkuta mtoto wao akimaliza kuandaa chakula cha asubuhi halafu akawaambia,
“Baba na mama, karibuni mezani”
Mariam na Juma waliangaliana bila ya swali wala jibu la aina yoyote ila tu walisogea pale mezani na kukaa kisha Juma aliamua kujivika ujasiri na kuuliza,
“Tumerudi vipi hapa wakati tulilala nyumba ya kulala wageni?”
Mtoto akatabasamu na kusema,
“Kheee wakati usiku mlikuja na kugonga mlango ili niwafungulie? Nimeona mlichoka sana ndiomana mapema leo nikaamua niandae kifungua kinywa”
Mariam na Juma wakatazamana tena, basi Juma akamwambia Mariam,
“Tusiulize sana, tuendelee tu kunywa chai Mariam”
Yule mtoto akadakia na kusema,
“Hapana, usimuite Mariam. Muite mama Moza”
Mariam na Juma waliangaliana tena na wakashindwa hata cha kusema wala cha kufanya ila walikunywa tu chai, muda huo Juma alihisi kama akili yake ikizunguka tu. Akamwambia Mariam,
“Mke wangu, naomba nijiandae niende mahali kuna jambo nataka kuligundua zaidi maana linanipa mashaka sana”
“Jambo gani?”
“Ni kuhusu huyo Moza, nahitaji kumfahamu zaidi. Kumbuka Anna alisema kuwa huyo Moza aliwahi kuwa mdada wao wa kazi, ngoja nikamtafute yule dada ambaye ni dada yake na Anna, yule mama Rose ili nimuulize vizuri kuhusu Moza maana yeye atakuwa na maelezo yaliyonyooka”
“Mmmh sawa, naona itakuwa ni vyema sana”
Juma alijiandaa na kuondoka zake, kwahiyo pale nyumbani alimuacha yule mtoto pamoja na Mariam.

Juma alivyoondoka nyumbani kwake, alikutana na yule jirani yake mmama na kusalimiana pale kisha yule jirani akaanza kumwambia Juma,
“Unamjua yule jirani yako anaitwa Abrah?”
“Ndio namjua, vipi tena?”
“Khaaaa kumbe mkewe ni mchawi”
“Kivipi?”
“Kwanza nasikia Abrah kakimbia kwa mke wake, kumbe yule mwanamke ni mchawi. Sasa jana wamekuja marambaramba yani wale watu wanaotoa wachawi, ndio wamefika kwenye nyumba ile na kugota hapo hapo khaaa mama katolewa tungule jamani!! Kumbe kachawi kale kamama hatari”
“Duh!! Basi ni balaa”
“Ndio hivyo, kuweni makini sana na wake zenu”
“Asante kwa ujumbe”
Juma aliachana na huyu na kuendelea na safari yake ya kwenda kukutana na mama Rose ambapo aliwasiliana nae na wakakubaliana mahali ambapo watakutana.

Moja kwa moja Juma aliongoza mpaka pale ambapo alikubaliana kukutana na mama Rose, walikutana na kusalimiana kisha Juma alimuuliza mama Rose,
“Samahani, nilikuwa tu nahitaji kujua historia ya Moza”
Mama Rose alishtuka na kumuuliza Juma,
“Unataka kujua historia ya Moza ninayemjua mimi au Moza gani?”
“Huyo huyo Moza amabye alikuwa ni mdada wenu wa kazi”
“Mmmmh imekuwaje kwani?”
“Nahitaji tu kujua kwani Anna aliniambia kuwa aliwahi kuwa mdada wenu wa kazi halafu nishawahi kufanyiwa na kitu cha ajabu na mtu aliyejitambulisha kwa jina la Moza”
Mama Rose akapumua kidogo na kuanza kuongea,
“Unajua huwa sipendi kuongelea kabisa habari za huyo mtu, huwa najikuta tu sipendi kuzungumzia habari zake”
“Basi mimi nakuomba tu, nakuomba sana nahitaji kujua”
“Ni hivi, huyo Moza alikuwa ni mdada wa kazi ambaye alitafutwa na mama hata sijui alimpatia wapi ila alikuwa ni mdada wetu wa kazi. Sema huyo mdada alikuwa ni mbea sana sijapata kuona yani, alikuwa akigombana sana na mama sababu ya umbea wake. Sasa kuna siku hata sijui ilikuwaje jamani, yule mdada alikufa, na tukaweka msiba sababu Moza hakuwa na ndugu yoyote yule kwahiyo msiba wake aliamua kuubeba mama mwenyewe, ila inasemekana kuwa sababu ya Moza kufa ni yeye mwenyewe na umbea wake sababu mama yetu alikuwa ni mchawi sana, kwahiyo kuna umbea aliufanya hapo hadi kupelekea kifo chake. Baada ya kifo, kila kitu kilifanyika hadi kwenda kuzika, tatizo wakati tunazika kuna mdogo wangu anaitwa Salome, alimpenda sana Moza, basi yule Salome akadumbukia kwenye kaburi la Moza na kuzimia, wakamchukua kumuwaisha hospitali, upepo mkubwa ukapita na hapo mwili wa Moza ukapotea, kifupi ni kuwa Moza hakuwahi kuzikwa hata mara moja. Kitu cha ajabu zaidi ni baada ya Moza kuanza kutumia mwili wa Salome katika kulipa kisasi, yani Salome hadi tulianza kumuogopa ila ni Moza ndio aliyekuwa akitumia mwili wa Salome, kiukweli katutesa na kutusumbua sana mpaka mwisho wa siku mama yetu alikufa kwa moto ndani ya nyumba yetu, na uchawi wake wote uliishia humo. Mama na Moza waliishia kwenye huo moto na tulianza maisha mengine baada ya pale hadi leo”
“Mmmmh hiyo stori inaogopesha halafu mtu unaweza sema ni stori ya kutunga”
“Ndio hivyo, ila walioishuhudia wote wanajua ukweli wa hii stori maana huyo Moza alirudi tena kwa mwili wa mtu mwingine”
“Kwa maana hiyo, kwasasa Moza si binadamu?”
“Ndio, atakuwaje binadamu wakati alishakufa?”
“Mmmmh inaogopesha, kwahiyo Moza anaweza kujivika katika mwili wa mtu mwingine?”
“Ndio maana alijivika kwenye mwili wa Salome, ngoja nije nyumbani kwako na Salome halafu yeye atakueleza vizuri kuhusu Moza maana hata yeye alikuwa ni Moza hapo awali”
Juma alipumua kwanza maana aliona kama ni mambo makubwa sana, kisha akamuuliza tu mama Rose kuwa atafika lini,
“Mmmmh nadhani kesho kutwa, nitakuja na huyo Salome halafu muulize maswali mbalimbali unayotaka kuyajua sababu hata mimi sijawahi kumuuliza maana najikuta nikiogopa vitu vingine sana”
“Pole, mimi tu kuna vitu unanisimulia tu lakini sielewi hata singekuwepo ingekuwaje, muende kumzika halafu mwingine adumbukie kwenye kaburi na kuzimia humo duh!! Hiyo habari”
Basi Juma alimuaga mama Rose halafu yeye alirudi nyumbani kwake.

Usiku wa leo, Juma alikuwa akijadiliana na Mariam kuhusu Moza sasa maana waliona huyu ndio wa kumjadili sasa zaidi ya Mishi ambaye ni chizi.
“Kwanza kabisa mke wangu naomba uniambie huyo aliyekulaani alikuwa ni nani?”
“Yani huyo mtu ilikuwa ndio mara yangu ya kwanza na ya mwisho kumuona, alijitambulisha kwangu kwa jina la Moza”
Juma alishtuka na kusema,
“Hata mtu ambaye alikuwa akinizuia mimi nisimuache Mishi na kunipa laana aliitwa Moza”
“Mmmmh!! Habari ya huyu Moza inaogopesha kidogo, haya nieleze alichokwambia huyo mama Rose”
Juma alimuelezea kila kitu ambacho yeye aliongea na mama Rose kuhusu huyo Moza na hapo Mariam alishtuka na kusema,
“Hivi Juma, huhisi kwamba huyo Moza ndio anafanya kazi kwenye mwili wa mtoto wetu?”
Juma na yeye akashtuka na kusema,
“Mmmmh halafu kweli, inawezekana ikawa hivyo, inawezekana kabisa kuwa huyo Moza ndio anafanya kazi kwenye mwili wa mtoto wetu”
“Ila swali ni kuwa ni kwanini anatufatilia? Mtu alishakufa, kwanini atufatilie?”
“Hapo ndio pagumu mke wangu, ila niambie kwanza laana aliyokupa”
“Aliniambia kuwa sitapata mtoto mpaka yeye apende”
“Khaaaaa kumbe mke wangu kuna kitu kama hiko katika maisha yako? Mbona hukuwahi kuniambia?”
“Niliogopa sana, niliogopa kusema chochote kile maana nilihisi usingetaka tena kunioa na kipindi unanioa nilikuwa nishachoka kukaa nyumbani”
“Aaaah na mimi alinilaani yule ujue, kuwa sitokuja kuoa mpaka apende yeye, ndiomana ulipokubali kuolewa na mimi nikakuoa haraka haraka kwani niliona wazi kuwa laana yake imegonga mwamba”
“Ila sasa kwa hizo laana zake ndio atusumbue kwenye familia yetu? Kwanini aje kwenye maisha ya mtoto wetu?”
“Mmmmh ngoja huyo mama Rose aje na huyo ndugu yake ili tujaribu kumuhoji maswali yote hayo”
Hawakuelewa ila kwa muda huo moja kwa moja walihisi tu kuwa mtoto waliyekuwa nae ndani alikuwa ni mtoto ambaye ndani yake aliishi mtu aliyeitwa Moza.

Leo mapema kabisa, Juma alijiandaa na kutoka kwenda kwenye shughuli zake maana siku zote hizi hakwenda, kwahiyo nyumbani alibaki Mariam na mtoto kwakweli Mariam alikuwa na uoga sana kwa kubaki mwenyewe na yule mtoto ambaye walishamuhisi kuwa Moza anaishi ndani yake hadi mtoto alimuona uoga aliokuwa nao Mariam na kumuuliza,
“Mama, mbona leo unaonekana huna amani kabisa?”
Mariam alikaa kimya tu, kisha huyu mtoto aliendelea kuongea,
“Mama, tangu umenizaa nipo katika maisha yako je kuna kibaya nimewahi kukufanyia hadi uniogope? Kuna siku nimewahi kukutisha? Kuna siku umewahi kuniona nipo tofauti hadi uniogope?”
“Hapana, sijawahi kukuona ukiwa tofauti”
“Sasa kwanini mama uniogope, kwanini unione nipo tofauti wakati mimi sijawahi kukuonyesha chochote cha kukukosesha amani. Ni kitu gani unanihisi mama yangu?”
Yani Mariam alibaki akimuangalia tu huyu mtoto na kukosa majibu yaliyonyooka, kisha aliamua tu kushirikiana nae kwa muda huo kama ambavyo huwa akishirikiana nae kwa siku zote.
Ila kwakweli leo Mariam hakuwa na amani hata kidogo alikuwa akijitahidi tu lakini hakuwa na amani kwa chochote kile walichokifanya na huyu mtoto.

Usiku wa leo Juma alimkumbushia mke wake kuwa mama Rose atafika kesho na huyo mdogo wake, Mariam na yeye alimsimulia Juma kitu kilichoendelea mchana baina yake na mtoto wao basi Juma hakutaka wazungumizie sana hadi huyo mama Rose atakapofika mahali pale.
Waliamua kulala, na kulipokucha tu mama Rose alimpigia simu Juma kuwa kwenye mida ya saa nne asubuhi watakuwa wamefika mahali pale.
Kwahiyo Juma hakwenda kwenye shughuli zake leo, alikuwepo tu nyumbani kwani anajua wazi kuwa mama Rose atafika kwenye mida ya saa nne asubuhi.

Wakiwa wametulia muda huu, mama Rose alifika akiwa ameongoza na huyo mdogo wake Salome, yani Juma alipomuona alipiga kelele na kusema,
“Jamani Moza mwenyewe si ndio huyo!”
Mama Rose akamwambia,
“Hapana, huyu anaitwa Salome ila Moza ndio alikuwa akitumia mwili wa huyu Salome”
Mariam na yeye akasema,
“Huyu Salome namjua jamani, sio Moza huyu maana Moza na yeye namjua vizuri sana”
Ila Juma hakutaka kukubali kabisa na kusema,
“Ni huyu huyu ambaye alinipa laana, huyu ndio Moza huyu”
Mtoto akacheka na kusema,
“Baba, hebu acha wenge wewe. Huyo sio Moza, ngoja Moza mwenyewe aje”
Kila mmoja alibaki kushangaa pale, mara muda kidogo kuna mtu alifungua mlango na kuingia ndani na kufanya wote waogope ila Juma alishtuka sana kwani yule aliyeingia alikuwa ndiye binti ambaye mara nyingi alikutana nae njiani na alimpa dawa mbalimbali.

Itaendelea……!!!
 
MTOTO WA MAAJABU: 43

Kila mmoja alibaki kushangaa pale, mara muda kidogo kuna mtu alifungua mlango na kuingia ndani na kufanya wote waogope ila Juma alishtuka sana kwani yule aliyeingia alikuwa ndiye binti ambaye mara nyingi alikutana nae njiani na alimpa dawa mbalimbali.
Juma alishindwa kuongea jambo lolote kwa muda ule ila walijikuta tu wote wakikaa chini huku wakimuangalia huyu aliyeingia ambapo alisema,
“Mimi ndiye Moza mwenyewe, msifanye kazi ya kubishana hapa, ila hata mimi naweza sema sio yule halisi bali naishi kwenye mwili wake na lengo kuu ni kulipa kisasi. Mnajua kwanini naishi kwenye mwili wa Moza? Nendeni mkafatilie chanzo cha kifo cha Moza hadi Moza kurudi na kuwa mzima tena na hapo mtajua imekuwaje niishi ndani ya Moza. Nilichukizwa sana na mambo aliyokuwa akiyafanya Rose, ila Moza alikuwa na nguvu ambayo ilinishawishi kuwa nae karibu ndiomana ilikuwa ni ngumu kushuhudia Moza akizikwa. Mimi ndiye ninayeishi kama Moza, na mimi ndiye niliyeishi kwenye mwili wa Salome, kwa lengo la Salome kumjua baba yake mzazi na kupata haki yake. Tuachane na hayo, naamini kwasasa swala la kumuwazia vingine Salome litakuwa limewaondoka kabisa, sasa ni hivi, mimi nimeanza kukufatilia Juma tangu ulipomuoa Mishi sababu Mishi nilimpa laana ya matendo yake aliyokuwa akiyafanya ya kuchanganya wanaume, nilikwambia wewe usije kumuacha Mishi kwani akili ya Mishi niliitambua vilivyo, nilitaka wewe ucheze nafasi yako kama mwanaume kwenye maisha ya Mishi ili Mishi abadilike ila badala yake ukasimama kama mume bwege na kuniudhi sana. Nikaanza pale kukufatilia wewe sasa, ila yule Mishi alikuwa na kiburi cha kufanya mambo sababu wewe ulikuwa huwezi kumfatilia, wewe ulikuwa husimami kwenye nafasi yako kama mwanaume, hadi Mishi kaenda kwa mganga na kupewa dawa ya kulala na mwanaume kwenye kitanda chako!! Bila mimi kukushtua kwa hakika usingemfumania Mishi kwa hilo, ulimpa uhuru sana, tena uhuru uliopitiliza na kunifanya nichukie sana kwa hilo Juma. Nilikaa karibu na wewe ila ulipomuoa huyu Mariam niliona ni sawa maana wote nyie wawili nilitaka kuwa karibu na nyie. Ila Mariam, dada yako ni mimi ambaye nilimmaliza…..”
Hapo Mariam akashtuka sana ila huyu Moza akasema,
“Usishtuke ila sikia ilivyokuwa, ni hivi dada yako alienda kwa yule babu na kumwambia kuwa ampe dawa Mishi ya kulala na yule mwanaume aliyelala nae, amwambie kuwa tatizo lingeisha, na kweli mimba ilitoka kwa tatizo lile ila lengo la dada yako lilikuwa ni Mishi aweze kuathirika sababu yule kaka alikuwa ni muathirika. Nikachukia sana, maana alichokifanya dada yako ni roho mbaya, nikammalizia huko na ujinga ujinga wake. Sasa nakuja kwa upande wako wewe Mariam, kitendo cha wewe kumpeleka rafiki yako kwenda kutoa mimba ni kitendo ambacho kilinikera sana na hivyo kufanya nipatwe na jazba na hasira nyingi mno na kufanya nizidi kukufatilia na ile mimba ya Mishi aliyoipata kwa vichaa ndio niliyokuwekea wewe na mtoto ni huyo unayemuona. Kwahiyo toka kipindi kile ulikuwa una mimba ila hukujijua hadi ulipoolewa ndio ikajidhihirisha na kukufanya uhangaike sana, kingene kilichofanya niwe karibu zaidi na wewe ni uvivu wako. Sikutegemea kama wewe ni mvivu kwa kiasi hiko ulichokuwa nacho, sikupenda huo uvivu wako. Haya niulizeni maswali muda huu nawajibu”
Wote waliangaliana na kushindwa hata kupumua vizuri, basi Juma alijivika ujasiri na kumuuliza,
“Kwahiyo wewe Moza ni nani?”
Moza alicheka na kuwaambia,
“Mimi ni msichana wa kazi, niliyetoka kwenye familia duni ambapo katika maisha yangu sikuwahi kuolewa wala kuzaa. Nadhani nimekujibu swali lako”
Juma akauliza tena,
“Samahani, wewe ni binadamu wa kawaida?”
Huyu Moza akacheka tena na kujibu,
“Kwahiyo unadhani mimi ni shetani au ni kitu gani? Mbona nilikuwa nakutana na wewe mara nyingi tu na kukushauri mambo mbalimbali! Swali lingine?”
Juma aliguna tu, muda huu ni Mariam ndio aliuliza swali,
“Samahani, kwani yule mganga alikufa na nini na je ni kwanini Mishi ni chizi?”
Huyu Moza akaangalia juu na kushusha macho chini kisha akasema,
“Yule mganga niliwahi kumwambia kuwa hiyo kazi sitaki uifanye maana huyu mtoto ambaye atakayezaliwa atabeba jina langu, yule mganga hakusikia na kufanya hiyo dawa yake na hapo nikachukia na kummaliza, sasa ilitakiwa huyo Mishi asiende msibani maana pale adhabu yake aliyojipa ni kubwa sana, ila kitendo cha yeye kwenda msibani ndio kitendo kilichomfanya awe chizi hadi leo”
Mariam na Juma waliangaliana na kujikuta wakiuliza,
“Je kuna namna ya kumsaidia?”
Moza akawaangalia na kuwaambia,
“Namna ya kumsaidia ipo ila inatakiwa mfanye nyie wenyewe maana nyie ndio tiba ya yule mtu”
Juma akauliza,
“Tiba ipi hiyo?”
Yule Moza akajibu,
“Mnatakiwa mkamuonyeshe Moza mtoto kwa Mishi na hapo mtamfanya Mishi awe mzima”
Mariam na Juma waliangaliana na kuuliza tena,
“Kivipi?”
“Kivipi nini na wakati huyo mtoto mliyebeba ndio Moza”
Mariam na Juma wakaangaliana tena na kuuliza,
“Kwahiyo huyu mtoto ni wa ajabu?”
Moza alicheka na kujibu,
“Hapana, huyo ni mtoto wa kawaida kama watoto wengine ila nataka aitwe Moza kama ukumbusho wa huyu ambaye ni jasiri wangu Moza”
Mariam akauliza tena,
“Lakini Moza si wewe?”
“Sawa, mimi ni Moza. Kwani kuna tatizo gani la mtoto kurithi jina langu? Ngoja niwaambie hiki, msipompa huyo mtoto jina langu basi sitoacha kuwafatilia, nitawafatilia hadi pumzi zenu za mwisho”
Juma na Mariam wakapumua kwakweli, kisha wakaangaliana na hapo Mariam akajivika ujasiri na kumuuliza Moza,
“Samahani, na huyu mtoto tunayeishi nae ndani ni nani?”
Moza akacheka tena na kuwaambia,
“Huyu mtoto sitawatajia jina lake ila akiondoka mtamkumbuka siku zote za maisha yenu, kwanza huyo mtoto ana nguvu kuliko mimi. Kumbuka Juma siku huyu mtoto alipomzaba kibao Pendo halafu mimi nilikupa mkono wangu wa kwenda kumponya Pendo, kumbuka sikuonekana kwa muda kwenye ile njia unayonikutaga sababu nguvu zilipungua. Huyu mtoto ana nguvu sana, ndiomana Anna alipogundua kuwa hapa kuna mtoto wa namna hii akataka kuja kuishi nae kwani anajua ni kitu gani atapata toka kwa huyu mtoto ila hajapatana nae sababu huyu mtoto hapendi uchawi”
Wote wakabaki wanaangaliana pale ambapo Moza aliwauliza tena,
“Swali lingine la ziada mlilokuwa nalo! Ulizeni”
Yani walijikuta hawana swali lolote kwa muda huo, kisha Moza aliwaaga na kuondoka zake yani alitoka tu mlangoni kawaida na kuondoka.
Ndani walibaki wakishangaa sana huku wakiangaliana bila ya kuwa na swali wala jibu.

Baada ya muda kupita ndipo Salome alipoongea maana alikuwa na maswali yake lakini wakati Moza ametokea alijikuta akishindwa kuuliza,
“Jamani mimi nilitaka kumuuliza kuwa aliingiaje kwenye mwili wangu hadi kuna baadhi ya watu wakajua mimi ni Moza?”
Mama Rose na yeye akaongea,
“Mimi swali langu lilikuwa ni kwanini aliamua kumuua mama yangu na kuchoma nyumba yetu ilihali angeweza tu kumpa mama adhabu?”
Mariam akawaambia,
“Sasa jamani mbona hamkumuuliza wakati yupo hapa?”
Juma na yeye akasema swali jingine alilokuwa nalo,
“Mimi nilitaka kumuuliza kuwa amewezaje kufanya hayo anayoyafanya?”
Mtoto aliwaangalia na kuwauliza,
“Kwahiyo mnamuhitaji tena Moza aje kujibu maswali yenu hayo?”
Wakabaki kimya huku Mariam akitikisa kichwa maana alihisi hata yeye ana maswali mengine ya kumuuliza Moza, yule mtoto alitlia kwa muda na kusema,
“Moza, bado unahitajika kwenye nyumba hii”
Na kweli baada ya muda Moza alifungua mlango na kuingia ndani, kisha alicheka jinsi ambavyo waliogopa sana halafu alianza kuongea,
“Nitajibu hayo maswali yenu mliyouliza sasa, Juma umeuliza kuwa natoa wapi nguvu nilizokuwa nazo. Mimi sio wa kawaida kama unavyofikiria, kwa kawaida mimi ni Moza ila mimi nilikuja kwa Moza baada ya kuona Moza ana malengo kama yangu. Moza hakupenda wachawi, hakupenda watu wenye roho mbaya, Moza hakupenda kuishi maisha mabaya ingawa ilimlazimu sababu ya wazazi wote wote kufa. Wazazi wa Moza hawakufa kawaida maana waliuwawa kichawi ila kwa macho ya kawaida utaona kuwa ni kifo cha kawaida. Ingawa ilikuwa ni kiuchawi ila Moza alishuhudia kifo cha wazazi wake kwa macho yake mwenyewe, na ameishi maisha ya shida sana, na ni Moza ndiye aliyenisaidia mimi nitoke nilipofichwa na yule mjinga Rose maana alinificha chini ya ua, nimewaambia fatilieni kifo cha Moza mtaelewa ni kitu gani kilitokea. Halafu kuhusu kuingia kwenye mwili wa Salome ni kutokana na upendo wa Moza na Salome, walikuwa si ndugu ila walipendana sana na huo ndio ukweli hata mkimuuliza hapo Salome kwa muda wenu atawaeleza jinsi gani anampenda Moza, na katika watu wasioamini katika kifo cha Moza basi Salome ni namba moja. Halafu kuhusu kumuua Rose na sio kumpa adhabu ni sababu hakutaka kuacha uchawi kwa njia ya amani, yani uchawi ulishamuingia kwenye damu yake akaona kuuacha ni kazi na kuamua kushindana na Moza tu. Na sababu iliyofanya nimuue Rose kwa kumchoma ndani ya nyumba yake sababu kile ndio kilikuwa kifo pekee cha Rose cha bila kufa na mtu mwingine ila ningemchagulia kifo kingine basi Rose angekufa na watu wengi sana. Nadhani nimemaliza maswali yenu, mwenye swali lolote tena kabla sijaondoka maana muda huu nikiondoka sitaweza kurudi tena”
Walikuwa wakiangaliana tu bila ya kuuliza swali lolote, basi Moza aliwaambia,
“Kama hamna swali naondoka ila sitaweza kurudi tena, nikiondoka sasa nimeondoka kabisa”
Na baada ya pale Moza aliondoka ila Mama Rose na yeye na Salome waliinuka na kuondoka bila ya kusema chochote kile na kufanya ndani wabakie wenyewe wenye nyumba tu.
Usiku ule Juma hakuzungumzia tena habari za yule mtoto wala Moza hata Mariam na yeye ilikuwa hivyo hivyo, walijikuta tu zile habari wameachana nazo kabisa. Basi wakalala na kuendelea kuishi kwa namna hiyo huku wakimuangalia tu mtoto wao kwa yale mambo aliyokuwa akiyafanya na kuendelea na mambo mengine tu.

Leo, Juma aliamua kwenda kumtembelea Pendo na familia yake, alifurahi sana kumkuta Pendo akiishi na mume wake pamoja na watoto wao, basi aliwasalimia pale na kuongea nao jinsi mambo yanavyoenda ila Pendo alimsimulia kitu kingine kilichofanyika kwenye familia yake,
“Juma nilipata mdada mwingine wa kazi kumbe alikuwa ni mchawi ila nimempeleka kwenye maombi naamini atabadilika tu kama akiamua kumtumikia Mungu”
Basi Juma alimtazama Pendo na kumwambia,
“Kuna mdada wa kazi nilikuwa nae ila ni mchawi mbaya, ila kaniambia kuwa anhitaji sana kuacha uchawi. Utamsaidiaje kama huyo?”
“Nipeleke alipo ili nimchukue na kumpeleka kwenye maombi”
Juma hakuona tatizo kwani muda huo huo aliondoka na Pendo hadi kwenda kwenye nyumba ile ambayo walimuacha Anna, ambaye alipowaona aliwasogelea na kuwasalimia kisha Juma akamwambia Anna,
“Ukombozi wako umekuja, huyu dada anataka kukukomboa ila ukombozi huo una masharti”
“Kheee masharti gani?”
“Nenda nae halafu utajua, si unataka kuacha uchawi wewe na umeamua kabisa?”
“Ndio nimeamua”
“Basi jiandae uongozane na huyu dada uende nae huko anapotaka kukupeleka”
Anna alienda kujiandaa, na hapo walianza safari ambapo Juma aliwaacha waondoke halafu yeye alirudi nyumbani kwake.
Ila njiani Juma alimpigia simu mama Rose ili kumpa ujumbe wa Anna, ambapo mama Roze alishangaa kidogo na kuuliza,
“Anna huyo kakubali kuacha uchawi?”
“Kakubali ndio”
“Huyo Pendo si anampeleka Anna kwenye maombi?”
“Ndio, Pendo kasema hivyo”
“Sasa kule huwa wanaambiwa waache uchawi au waombewe wafe, Anna atakubali?”
“Amekubali sio atakubali”
“Halafu hao wachungaji wajipange kama watakuwa hawajasimama vizuri lazima Anna awaangushe kiimani na kiroho nakwambia, maana Anna ni mdogo wangu namjua vizuri. Imeshindikana kila sehemu Anna kuacha uchawi labda akomeshwe na huyo huyo Moza, namjua Anna vizuri sana”
“Haya, tusiongee mengi tutasikia tu yatakayojili huko”
Basi Juma aliagana na mama Rose na kukata ile simu na kuendelea kurudi nyumbani kwake.

Juma alipofika kwake alimkuta mkewe na mtoto wake wakiwa wanakula kwa muda huo, basi akasema,
“Jamani hata kunisubiria?”
Mariam akajibu,
“Aaaah mimi njaa ilianza kuniuma ndio nikamwambia mtoto tule tu”
“Yani mke wangu hujaacha uchoyo tu?”
Kisha Juma akamuangalia mtoto ila kabla hajaongea kitu mtoto akacheka na kumwambia Juma,
“Baba, umejisumbua tu kumpeleka huyo Anna huko kwenye maombi”
Juma akamuangalia yule mtoto na kumuuliza,
“Kivipi?”
“Hivi nyie mnaamini kabisa Anna ataacha uchawi kirahisi hivyo? Anna alipewa uchawi na mama yake toka amezaliwa tayari alikuwa na uchawi, sio rahisi kwa Anna kukubali kuacha uchawi”
Mariam na yeye alimuangalia mume wake na kumuuliza,
“Kwahiyo Anna umempeleka kwenye maombi?”
“Ndio, Pendo kasema hiyo ndio njia ya kumsaidia”
Mariam akamuangalia mtoto na kumuuliza,
“Sasa ni kitu gani kinachoweza kumsaidia Anna aache uchawi aliopewa toka tumboni kwa mama yake? Anna anaongea kwa hisia kali sana kuwa kachoka uchawi hadi anatia huruma, ni kitu gani kitamfanya aache?”
“Hata huko kumuombea kutamfanya aache ila Anna hawezi kuishi bila kuwa mchawi, na mkitaka kugundua kuwa Anna hawezi kuacha uchawi, subiri ukijifungua mtoto akiwa mchanga kabisa muite Anna amuone halafu utaona atakachokifanya sema tu atashindwa sababu huyu mtoto ataitwa Moza, ila utaona tu atakachotaka kufanya”
Juma na Mariam wakaangaliana kisha Juma alikaa na kuanza kula kile chakula kilichokuwa kimetengwa.
Usiku wa leo, mama yake Juma alimpigia simu Juma na kuongea nae,
“Mwanangu, kwasasa hatuna kinyongo chochote kwako na mke wako, tunawatakia heri tu muishi vizuri na mzidi kupendana maana mapenzi ni ya wawili”
“Asante sana mama yangu, kwahiyo hata bamdogo na mjomba hawana tena kinyongo na mimi?”
“Ndio, wote hawana kinyongo na wewe mwanangu, kwahiyo usiwe na shaka wala tatizo lolote. Tunawapenda sana, naomba mtusamehe popote pale tulipowakosea na sisi tumewasamehe kwa yote mwanangu. Amani tu itawale”
Hili jambo lilimfurahisha sana Juma alijikuta akitabasamu tu, hata alipomueleza Mariam na yeye alifurahi sana kuhusu jambo hili.

Miezi ilikuwa imepita na mimba ya Mariam ilikuwa imekua sasa, mimba ilikuwa inatimiza miezi tisa, basi leo alikuwa amekaa na huyu mtoto wake na kumuuliza,
“Samahani mwanangu, je huyu mdogo wako wa kuitwa Moza na yeye atakaa miezi ishirini na tatu tumboni kwangu?”
Mtoto akacheka na kumwambia,
“Hivi mama ulivyoambiwa kuwa huyo ni mtoto wa kawaida hukuelewa?”
Mariam alimuangalia na kumuuliza tena,
“Kwahiyo leo umekubali kuwa wewe ni mtoto wa ajabu?”
Basi mtoto akamjibu kwa kumuuliza,
“Kwani wewe unanionaje?”
Hapo Mariam hakuwa na jibu ila alikuwa akijikanyaga kanyaga tu, basi yule mtoto akamwambia mama yake,
“Laiti ungemsikiliza kwa makini yule mliyekuwa mnamuuliza maswali basi ungeelewa, yani hadi sasa hujui ni kwanini mimi nipo kwenye maisha yako? Wewe ulisaidia kunitoa toka tumboni kwa mama yangu Mishi, mimi ni mtoto niliyetakiwa kuzaliwa na Mishi ila wewe na kiherehere chako ndio ukanitoa, ila hadi sasa nipo kwaajili ya uvivu wako ingawa umejitahidi kwasasa, nitaondoka pindi mama yangu akipona, licha ya makosa yake yote lakini bado nampenda sana”
“Sikuelewi”
Yani Mariam alikuwa akijibu huku akitetemeka kwani kama kuelewa ni tayari ameshaelewa ila tu alijifanya kuwa hajaelewa, na hapo hapo alianza kujihisi uchungu mkali sana na kuamua kuchukua simu na kumpigia mama yake pamoja na mume wake ili apelekwe hospitali.

Juma alifika mapema kabisa pamoja na mama yake Mariam na moja kwa moja walimpeleka Mariam hospitali ambapo baada ya muda kidogo tu alijifungua mtoto mzuri kabisa wa kike, yani Mariam alitabasamu na kufurahi sana wakati anakabidhiwa mtoto wake mkononi, ila muda ule ule mtoto akatoa haja kubwa na ndogo na kumfanya Mariam aanze kulia hadi nesi akasogea kumuuliza,
“Tatizo ni nini dada?”
“Mtoto kajisaidia nesi, haja ndogo na kubwa”
“Oooh vizuri sana, sasa unalia nini?”
“Mtoto wangu ni mtoto wa maajabu, naogopa sana jamani! Yani nimezaa kwa miezi iliyotimia kabisa na nimezaa mtoto wa ajabu?”
“Mtoto wa ajabu sababu ya kukojoa na kunya au kuna lingine?”
“Hamna lingine ila ni sababu hiyo hiyo”
Nesi akacheka na kumwambia Mariam,
“Yani ukiona mtoto wako kajisaidia baada ya kuzaliwa hii ni njia nzuri ya kujua usalama wa mtoto wako, maana kibofu ni kizima na njia ya haja kubwa haina matatizo. Hujawahi sikia mtoto kazaliwa bila njia ya haja kubwa au ndogo, hujawahi sikia mtoto kazaliwa bila sehemu yoyote ya kujisaidia? Kwahiyo ikitokea kama hivi ni jambo la kumshukuru Mungu Mariam kuwa mtoto umezaa mzima wa afya njema”
Basi Mariam akatabasamu na kusema,
“Mtoto wangu huyu ataitwa Moza”Kale katoto kalitabasamu na kufanya Mariam aogope tena ila nesi alimwambia ni kawaida kwa watoto kutabasamu hata usingizini.
Kidogo Mariam alipata amani kwasasa na kuruhusiwa sasa kutoka hospitali maana mtoto alikuwa salama kabisa.

Walivyorudi tu nyumbani, Juma alikumbuka swala la kwenda kumchukua Anna na kwenda nae pale nyumbani, kwahiyo Juma alifika na Anna wakati Mariam yupo kunywa uji sasa huku kichanga chake kimeshikwa na mama Mariam.
Yani Anna alipofika pale akatamani kumshika yeye mtoto hadi anaomba kwa magoti, yani mama Mariam alimshangaa sana,
“Huyu mtoto bado mdogo yani unaomba kumshika hadi kwa magoti?”
Yule mtoto mwingine akasema,
“Anna, unataka kumshika mtoto. Ipo hivi kama ukimshika huyu mtoto kwa upendo basi utakuwa salama ila ukimshika huyu mtoto kwa uchu basi utazikwa wewe kabla yake, ni mtoto wa kawaida huyu ila analindwa huyu mtoto”
Anna akajibu kwa kujiamini,
“kwanza nimeacha uvchawi, nataka kumshika kwa upendo tu”
Kisha yule mtoto akamwambia mama Mariam,
“Bibi, mpe Anna huyo mtoto amshike”
Basi mama Mariam alimpa mtoto Anna ila Anna hadi alionekana wazi kabisa akimtamani yule mtoto mara hapo hapo Anna alianguka chini na kuwafanya wamdake yule mtoto yani hakuna aliyeelewa pale ila yule mtoto aliwaambia kuwa Anna amekufa na hata Juma alipochukua usafiri na kumpeleka Anna hospitali lilikuja jibu lile lile baada ya vipimo kuwa Anna amekufa.

Juma hata hakujua ni namna gani atumie kuandaa msiba wa Anna, basi aliwaita tu ndugu zake waliokuwepo ili wajadili alimuita pia Pendo ili kujua kilichokuwepo.
Walipofika, Juma alienda kuzungumza na Pendo kwanza,
“Hivi kwani ilikuwaje na Anna huko?”
“Ni hivi, Anna nilimpeleka hadi kwa mchungaji ilia ache uchawi na kwangu alisema ataacha, ila tulivyofika kwa mchungaji aliulizwa na kusema kuwa hawezi kuacha uchawi, tena Mchungaji hadi akamfunulia maandika kuwa mwanamke mchawi hastahili kuishi ila hilo wala halikumpa tatizo Anna na alikataa katakata japo alifundishwa vitu vingi sana. Mchungaji akaniambia kuwa swala la kuacha kitu ni lazima mtu awe na utayari, hivyo nikaamua kumrudisha Anna kule nilikomtoa ila alinipa onyo kuwa ole wangu niseme kama hajaacha uchawi”
“Khaaaa kumbe Anna alikuwa anatuigizia kwa kipindi chote hiki?”
“Ndio hivyo yani”
Basi Juma aliongea pia na mama Rose ambaye alisema kuwa mdogo wake Anna akazikwe kwenye kiwanja chao ambapo nyumba yao ndio ilichomwa na mama yao ndani,
“Hata kaka zangu nao walizikwa hapo, kwahiyo Anna na yeye akazikwe hapo hapo nitakuwa nikiangalia makaburi yao maana sijali kitu bado ni ndugu zangu tu”
Basi wakashirikiana wote kwa mazishi ya Anna halafu marehemu Anna alienda kuzikwa ila wakati wamemaliza swala la mazishi ndipo alipopita Mishi akiwa na ule uchizi wake kama aliokuwa nao, ni hapo mama Rose aliposema,
“Jamani ni Mishi yule, masikini ni chizi kabisa kwasasa”
Basi Juma alimuhurumia na akakumbuka lile swala ambalo yule Moza aliwaambia, na hapo aliamua kumkamata Mishi na kumfunga mikono na miguu kisha kukodi gari na kurudi nae nyumbani kwake.

Mariam alishangaa sana kuona Juma karudi na Mishi pale kwao, akamuuliza mume wake,
“Sasa umemleta Mishi wa nini?”
“Umesahau tuliambiwa kuwa sisi ndio tunauwezo wa kumsaidia Mishi! Anatakiwa kumuona mtoto”
“Mmmh sasa nitamtoa mtoto nje wakati hata hajatimiza siku saba?”
“Naelewa mke wangu ila mtoe tu ili Mishi apate kumuona”
“Kwani bado unampenda Mishi?”
“Mmmmh Mariam, shida yangu ni kumsaidia Mishi”
Basi Mariam alienda kumchukua mtoto ila kabla hajatoka nae nje, yule mtoto wao mwingine akamfata Mariam na kumwambia,
“Mama, kwasasa umejirekebisha, nimependa moyo wako wa sasa. Umekuwa na moyo wa huruma na umekuwa muelewa, pia kwasasa mama yangu umekuwa ni mchapakazi ule uvivu umeuacha kabisa. Mimi ndio mtoto wa Mishi na mimi ndiye mwenye uwezo pekee wa kufanya Mishi aondokane na uchizi aliokuwa nao. Ila nakupenda sana Mariam maana ni mbishi ila ukitishiwa unaogopa, halafu nakupenda sababu unapenda kusema ukweli. Mimi naondoka mama, nakupenda sana”
Haka katoto kalimkumbatia Mariam kisha kalitoka na moja kwa moja kwenda kwa Mishi alipokalishwa na kumkumbatia halafu akaondoka hata alipoelekea zaidi hawakumuona maana alipotea tu, pale kila mmoja alishangaa na akili za Mishi zilirudi muda huo huo
Hawakuelewa kabisa ila walimchukua Mishi na kuingia nae ndani ambapo Mariam alimuwekea maji na kwenda kumsafisha maana Mishi alikuwa mchafu sana na kumpa chakula aweze kula na baada ya hapo Mishi alikuwa akishangaa tu, aliwakumbuka wale watu na alipomuona Mariam kabeba mtoto aliumia zaidi na kusema,
“Mimi na ujinga wangu nilimtoa mwanangu”
Mishi alionekana kutia huruma sana, kisha Juma akafanya jitihada na kumrudisha Mishi kwa ndugu zake ambao walifurahi sana kumuona na kumshukuru sana Juma.

Siku ya leo Mariam alikuwa amekaa huku akilia, hadi Juma alimshangaa na kumfata mke wake kumuuliza kitu kinachomliza,
“Vipi Mariam mke wangu nini tatizo?”
“Nimemkumbuka mtoto”
“Khaaa umemkumbuka mtoto si huyo hapo unae tayari!”
“Ndio ninaye ila nimemkumbuka yule mtoto wangu wa maajabu”
“Khaaaa Mariam una wazimu au ni kitu gani mke wangu?”
“Hapana sina wazimu, ona kama muda huu nimechoka ila natamani chakula kizuri jamani!! Mtoto angekuwepo si angenipikia jamani!”
Juma alicheka tu na kutikisa kichwa.

MWISHO

KWA MAWASILIANO NICHEK WHATSAPP 0629980412........
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom