Simulizi: Mimi na Mwanangu Juu ya Kaburi la Mke Wangu

Codeboy Breezy

Senior Member
Nov 8, 2018
194
323
Mtunzi: Iddi Makengo

BABA JOAN; MIMI NA MWANANGU JUU YA KABURI LA MKE WANGU!—SEHEMU YA KWANZA

“Baba kwani na Mimi ni mchawi kama Mama?” Joan aliniuliza tena, wakati huo tulikua tunaweka mchanga juu ya jeneza la mke wangu.

“Hapana mwanangu, wewe si mchawi, hata Mama yako hakuwa mchawi.” Nilijitahidi kujibu ili kumpa moyo, pamoja na tofauti nilizokua nazo na mke wangu, kamwe sikuwahi kutaka amchukie Mama yake.

“Lakini Baba ulikua unasema Mama anakuloga, sasa kama si mchawi alikua anakulogaje?” Miguu ilishikwa na ganzi, kwa muda nilishindwa kutembea, nilikua kama nimesimamishwa, kwa watu walioniona pale kaburini walidhani ni kwasababu nina uchungu wa kufiwa na mke wangu, lakini swali la mwanangu lilinikumbusha maneno mengi.

“Shangazi naye alisema mimi na Mama ni wachawi, alisema kuwa tutakufa tuzikwe pamoja eti Mama anataka kukuua, akasema Mama akikuua basi atatulazimisha tule nyama yako, mimi sitaki kula nyama yako Baba? Baba mimi si mchawi!” Aliniambia, niliendelea kusimama, maneno aliyokua akiongea hayakua mageni kwangu, sikushangaa kwani ni mara nyingi tu ndugu zangu walishaongea wakimuambia mke wangu kuwa ni mchawi, anataka kuniua na kama akiniua basi atakula nyama yangu. Lakini katika kipindi choe hicho sikuwahi kufikiria kama mwanangu katika umri mdogo kama ule atasikia.

Nilijitahidi kutembea taratibu mpaka kuondoka pale makaburini kabisa, sikua na nguvu ya kuendelea kusimama, nilijisikia vibaya hasa ndugu wa mke wangu walivyokua ananiangalia, ni kama walikua wananiambia “Acha unafiki umemuua Dada yetu.” Sikuweza hata kusubiri kuweka maua, niliondoka na kurudi mpaka kwenye gari nikaa na Joan. Mwaangu alionekana kuwa na wasiwasi sana, alikua akiniuliza maswali mengi ambayo sikua na majibu nayo.

“Baba Jack (si jina halisi, mtoto wa dada yangu mkubwa) alisema kuwa Mama yangu akifa mimi nitaenda kuishi kwao na Mama yao ndiyo atakua Mama yangu, mimi sitaki kuishi huko, Mama yake ananipigaga anasema mimi ndiyo nampa Mama kiburi na wote tutaondoka hatutaki…”

Mwanangu aliendelea kuongea, alinikumbusha namna nilivyokutana na marehemu mke wangu, jinsi ambavyo tulianza kuhangaika wote hatuna kazi baada ya kumaliza chuo, tukafungua duka letu la kwanza. Mke wangu akitengeneza Icecream na mimi kuzizungusha mjini, kipindi hicho tulikua tumemaliza chuo na mke angu alikua na ujauzito hivyo kwao walimfukuza na kwakua kwetu hali ya maisha ilikua ngumu sana basi sikua na namna zaidi ya kupangisha chumba na kuanza maisha.

Friji tulilokua tukitumia lilikua ni la mke wangu, alikua kanunuliwa na Baba yake kipindi bado yuko chuo, alikua akitengeneza Icecrem na mabarafu pamoja na maji ya kufunga, tuliuza mpaka tukapata fremu, mimi ndiyo nilikua nikizungusha. Kwa bahati mbaya wakati mke wangu anajifungua mtoto alifia tumboni. Baada ya hapo ndugu zake walimsihi sana kuachana na mimi kwani nilikua masikini lakini alikataa katakata, walikataa kushirikiana na mimi, hata nilipopeleka mahari kwao walikataa, lakini mke wangu alikua ananipenda sana, alilazimisha mpaka tukafunga ndoa ya serikali bila ndugu yake hata mmoja kuhudhuria.

Ndugu zangu wote walikuepo na walikua wanampenda mke wangu kama pesa, tulianza kwa shida na kweli baada ya ndoa milango ilifunguka. Mwaka mmoja tu baadaye mke wangu alifanikiwa kupata kazi, wakati huo mimi bado nahangaika na duka, alifanya kazi kidogo akachukua mkopo na kunipa, tuliachana na duka la vitu vya nyumbani na kufungua duka la vifaa vya spea za pikipiki. Kipindi hicho ndiyo bodaboda zilikua zinaanza kupamba moto, ndani ya mwaka mwingine mke wangu alikua na ujauzito mwingine wa mtoto wetu Joan, tulishajenga na hapo ndugu zake ndiyo walinikubali.

Walikubali tukafunga ndoa ya kanisani, baada ya hapo tulinunua gari na wakati Joan anazaliwa tulikua na magari mawili na duka lilikua kubwa nikawa naenda china kuchukua mzigo mwenyewe. Kwakua ndugu zangu wengi walikua hawana kazi na mke wangu ndugu zake wana uwezo mkubwa nilianza kuwaweka ndugu zangu katika biashara zangu, mimi nilikua mtu wa kusafiri sana hivyo sikua na muda wa kusimamia. Hapo ndipo kila kitu kilibadilika, kila nikirudi au wakati mwingine nikiwa huko nilianza kusikia malalamiko.

Ndugu zangu walianza kumlalamikia mke wangu, maneno yalikua mengi kuwa anawachukia, anaringa kwakua ana kazi, anaringa kwakua wana uwezo. Mimi nilikua nasikiliza pande zote, mke wangu ananiambia labda waligombana kwakua alipita dukani kukagua, mwanzo mahesabu mimi na mke wangu tulikua tunapiga pamoja, lakini baada ya kuingiza ndugu zangu wakaanza maneno kuwa mke wangu kanikalia, nilijikuta nawaamini nikaanza kupiga mwenyewe na pesa kama ni kupeleka benki basi nampa mdogo wangu anapeleka.

Nilimpa uhuru sana dada yangu mkubwa, yeye ndiyo alikua kama kichwa cha familia, alikua akipanga kila kitu na kila jioni alikua akichukua pesa anapeleka benki, wakati mwingine alikua akichukua bila kumuambia mtu yeyote kitu ambacho kilimkasirisha mke wangu. Alipokua akiniambia nilihisi anawachukia ndugu zangu, niliona kama anawadharau na kuwaona wezi kwakua sisi ni masikini. Mke wangu alipata ujauzito ulimsumbua sana nikamuambia aache kazi, mwanzo alikataa lakini tulisumbuana sana mpaka akaacha, alibaki na kuwa Mama wa nyumbani.

Kwa bahati mbaya mtoto pia alifia tumboni, alifia ujauzito ukiwa na miezi saba, iliniuma sana kwani alikua ni mtoto wa kiume na mimi nilikua na hamu sana ya kupata mtoto wa kiume. Baada ya hapo sasa ndipo yaliibuka mambo ya uchawi, ndugu zangu walianza kumshutumu mke wangu kuwa ni mchawi na anaua watoto kwasababu ya mali. Siku moja Mama alinipeleka kwa mtaalamu mmoja, aliniambia kila kitu kuwa hata mimba ya kwanza ambayo iliharibika ilitokana na mke wangu kumtoa sadaka mtoto wetu.

Aliniambia mambo mengi pamoja na kusema kuwa, hata familia yake inajua kwani utajiri wao ni wa kishirikina. Nilipewa dawa flani ya kutumia ili kujikinga na nguvu za giza za mke wangu. Kweli nilitumia lakini cha ajabu nilijikuta namchukia mke wangu, katika maisha yangu nilikua sijawahi kumpiga mke wangu lakini baada ya hapo kila siku ilikua ni kumpiga, akinikosea kidogo nampiga na kumtukana matusi ya nguoni, kumuambia mchawi na kumuambia kuwa anatakiwa kuondoka katika nyumba yangu.

Mke wangu kazi yake kubwa ilikua ni kuomba na kusali, alikua ni mtu wa kufunga, kupiga magoti kila siku. Lakini hali ilikua mbaya, alipata ujauzito mwingine, Mama yangu akaniambia kuwa haukua wa kwangu, kuna kijana mmoja wa dukani ambaye alikua karibu sana na mke wangu, nikaambiwa kuwa ndiyo mwenye ujauzito. Nilikasirika sana, kwa hasira niliondoka nyumbani, nikahamia kwenye nyumba yetu nyingine kwani mbali na kumfukuza lakini mke wangu aligoma kuondoka akaniambia kama nataka nimpe talaka, sikutaka mambo ya talaka kwani nilijua kuwa tutagawana mali.

Nilishapanga kumaucha, niliondoka na kwenda kushi nyumba nyingine na mwanamke ambaye nilitafutiwa na ndugu zangu. Nilifanya hivyo huku nikianza mchakato wa kubadilisha majina ya mali zangu zote ili kama ikitokea tukiachana na mke wangu basi asiondoke na chochote. Lakini siku moja nilikua safarini, nilikua nimeenda Kigoma kikazi, simu yangu iliita, nilipoangalia ilikua ni namba ya mke wangu. Ni muda sana nilikua sijaongea naye, ni muda mrefu nilikua sipokei simu zake.

Hata nilipotaka kujua hali ya mtoto nilikua nikimpigia dada wa kazi na kumtumja dereva kwenda kumchukua kucheza naye. Lakini siku hiyo kuna kitu kiliniambia pokea msikilize mkeo mmetoka mbali. Nilipokea simu yake na kuiweka sikioni, sikuongea chochote nilinyamaza tu kwani sikua na kitu cha kuongea.

“Naomba usikate mume wangu…” Alianza kuongea, sauti yake ilikua inakwaruzakwaruza, alikua akuongea kwa shida kama mtu ambaye yupo kwenye maumivu makali.

“Mpaka leo sijajua nimekukosea nini kwani ningejua ningekuomba msamaha. Ila haina maana sana kwa sasa, najua sitaishi sana, ila nisingependa niondoke namna hii. Naumwa sana mume wangu, hujui tu lakini nadhani safari hii hutu mtoto ataniondoa.”

Alikua anatia huruma, nilitamani kuongea kumuuliza lakini mdomo haukunyanyuka, nilibaki kimya kumsikiliza.

“Naomba tu ujue kuwa sijawahi kukuloga, najua umejazwa maneno mengi na ndugu zako ila kumbuka hapa duniani hatuishi milele. Najua nitatangulia mimi na utakuja kuujua ukweli, mimi nimekusamehe ila naomba sana mume wangu, mlinde mwanao. Ndugu zako wananichukia si kwasababu mimi mbaya bali kwaua sasa hivi tuna mali, najua unajaribu kubadilisha kila kitu kiwa na majina yako, sijapinga kwakua sikukupendea mali, wewe mwenyewe unajua, familia yangu ina pesa.

Mali ambazo niarithi kwetu zingeweza kunitosha, nilikupenda ukiwa huna kitu sasa kwanini nihangaike kukuloga wakati najua kila kitu ulichonacho kimetoka wapi? Mimi nitakufa lakini wewe mlinde mtoto wetu, ndugu zako wakifanikiwa kuniondoa kikwazo pekee cha wao kuchukua mali zako ni mtoto wetu, mlienda sana asije kuteseka.” Alikaa kimya kidogo kisha akaanza.

“Halooo! Haloo! Haloo mume wangu… ongea basi hata kidogo nisikie sauti yako, nataka nijue kama umenielewa.” Mimi bado niliendelea kubaki kimya, maneno yake yalinichoma sana.

Kweli mke wangu hakunipendea pesa, alinikuta masikini nakula chakula mlo mmoja chuoni tena mchana tu akawa akanisaidia mpaka ananipa pesa ya matumizi, photocopy ananitolea yeye, alikua ananinunulia nguo nzuri na kunipa kila kitu na hata siku moja alikua hajawahi kuninyanyasa, nilijisikia vibaya sana na kutamani kumuomba msamaha. Lakini kuna kitu kama kilikua kinanikataza, saut ya Mama yangu ikiniambia kuwa huyo si mwanamke ana dharau atakuendesha ilinijia kichwani, ilikua haitaki kabisa kuondoka, nilinyamaza kimya lakini mke wangu aliendela.

“Kama una muda naomba tu unisikikilize, nimekua mpweke sana mume wangu, sina mtu wa kuongea naye nimekata tamaa na mara nyingi natamani kufa, kuna wakati nilitamani kumeza hata vidonge lakini nikimfiikiria Joan bado alikua ananihitaji, ila sasa hivi siwezi tena mume wangu. Hata kama ningetaka basi siwezi, naumwa sana mume wangu, presha ipo chini sana na mtoto tangu jana hajacheza, wameniambiam niko hospitalini na ndugu zangu lakini najiona kama niko peke yangu nimekukumbuka sana mume wangu. Muangalie Joan naogopa atateseka sana…”

Ghafla mke wangu alinyamaza, ulitanda ukimya wa kama dakika tano nikidhani kuwa ataongea tena lakini hakuongea. Nilianza kuongea mimi “Haloo! Haloo! Haloo! Mama Joan! Mama Joan!” Niliita sana lakini hakuitikia, nilipata wasiwasi, nikakata simu na kupiga tena kuona kama atapokea. Nilipiga sana lakini iliita tu bila kupokelewa. Nilikaa kama nusu saa hivi na kuanza kupiga tena simu ya mke wangu, ilikua haipatikani kama imezimika, nilimpigia Dada wa kazi, baada ya salamu nilimuulizia kuhusu mke wangu.

Kwanza alishangaa kwakua kwa kipindi chote hicho sikuwahi kumuulizia, mara nyingi nilikua nikipiga simu namuulizia mtoto basi. Aliniambia hajui chochote kwani yeye yupo nyumbani na mtoto na mke wangu alikua hospitalini. Nilikata simu na kumpigia mdogo wake na mke wangu ambaye nilikua na namba yake, aliipokea, alionekana kutokuwa na namba yangu, nilijitambulisha, lakini sauti yake ilionekana kama mtu anayelia. Nilimuuliza hali ya mke wangu alinijibu kwa mkato.

“Mmeshamuua Dada yangu mnataka nini tena? Umepiga kuhakikisha kama kafa kweli?” Alijibu kisha akakata simu. Nilijaribu kumpigia tena simu lakini hakupokea, kweli nilichanganyikiwa, nilipigia baadhi ya ndugu zake wengine lakini hawakupokea simu zangu. Nilitulia kidogo nikiwaza nini chakufanya, lakini kabla ya kufanya chochote simu yangu iliita, alikua ni Mama yangu mzazi nilipokea kabla haya ya kumsalimia alinianza.

“Umesikia yule mchawi amekufa, uchawi wake umemrudia, wamzike huko huko sitaki kabisa maiti yake nyumbani kwangu! Kwani uko wapi, urudi kabisa nyumbani kwako ndugu zake wasijeenda kuchukua vitu vyetu….” Nilijikuta naishiwa nguvu na kushindwa kabisa hata kumjibu Mama.

Bila kudhamiria nilijikuta na kata simu, Mama alipiga tena lakini sikupokea, nilikua na hasira sana.

“Kweli mke wangu kafariki Mama yangu mzazi anawaza mali! Hivi anajua kuwa hizi mali ni mke wangu alinipa nilikua sina kitu kabisa!” Niliwaza kwa hasira, lakini kabla sijafanya chochote simu yangu iliita tena. Alikua ni Dada yangu mkubwa, niliipokea baada ya salamu naye alianza.

“Nimesikia habari, ila usiwe na wasiwasi, nimekua wa kwanza kufika hapa nyumbani kwako, hakuna ndugu yake yeyote ambaye amefika, kama kuna nyaraka zozote ambazo uliziweka humu niambie niziondoe mapema kabla ndugu zake hawajafika maana hatujui wamepanga nini?” Aliniuliza, Dada naye alikua anawaza mali.

Nimeshindwa kuvumilia na kuamua kuandika hiki kisa kabla ya kile kingine

BABA JOAN; MIMI NA MWANANGU JUU YA KABURI LA MKE WANGU!—SEHEMU YA PILI

Nilishindwa kufanya kitu chochote baada ya habari zile, akili ilikua haifanyi kazi sawasawa, kulikua na mambo mengo ambayp yananichanganya. Kitu cha kwanza nilichokua nikikifikiria ni Joan.

“Atakua anaishije huyu mtoto? Atakua yuko katika hali gani baada ya kujua kuwa Mama yake amefariki dunia.” Pamoja na kugombana na mke wangu lakini nilikua nikimpenda mwanangu kuliko kitu chochote kile na nilijua Joan anampenda Mama yake kuliko ananivyonipenda mimi. Kwanza ni kwasababu ya ukaribu wake na Mama yake, kutokana na kazi zangu mimi nilikua mtu wa kusafiri ukichanganya na ile mimi kuondoka nyumbani na kukimbia familia ilinifanya kuwa mbali sana na mwanangu.

Jambo la pili ambalo lilimfanya Joan kuwa karibu na Mama yake ni ndugu zangu ambao mara nyingi walikua ni watu wa kumtukana Mama yake, hali hiyo ilimfanya mke wangu kuwa mtu wa kulia mara kwa mara, mwanzo sikujua kama ni tatizo, lakini baadaye niliona kile kitu kinamfanya Mwanangu kumpenda sana Mama yake. Alikua kama anambembeleza na mara nyingi aliniona nikimgombeza Mama yake na hata kumnunia.

“Dada mwanangu anaendeleaje?” Nilichukua simu na kumpigia dada yangu ambaye aliniambia kuwa yuko nyumbani kwangu.

“Mwanao, kivipi?” Dada aliniuliza, ni kama alikua hajui kama nina mtoto. Niliwaza hivi huyu ni mtu wa namna gani, anasikia mke wangu kafariki kitu cha kwanza ni kuwaza mali bila kuwaza kama mtoto atatunzwaje?

“Kamuangalie Joan kuona kama ameshajua kama Mama yake amefariki dunia, sitaki watu wamuambie ambie tu!” Niliongea kwa hasira, hapo ndipo Dada yangu alikua kama kashtuka flani.

“Aaaa hsngazi yangu, yupo kalikua kanacheza hapo nnje…” Aliongea, nilikua na hasira lakini nilikua mbali, ilikua ni lazima kuongea kwa utaratibu ili mwanangu asije kuzipata taarifa za kifo cha Mama yake kutoka kwa mtu ambaye hajui kuongea na mtoto.

“Joan, shangazi yangu, njoo uongee na Baba yako.” Nilisikia Dada akiongea, joan aliingia chumbani kwa Mama yake wakati naongea na dada yangu kwani alikua kaingia kule kutafuta nyaraka ili afiche.

“Ongea na Baba yako, hii ni damu yako, Mama yako kafa sasa umebaki na Baba mwanangu, lakini usijali, mimi nitakulea kama Mama yako, onge….” Hasira zilinipanda, nilitamani hata kuruka ili kumpiga dad ayangu makofi. Alikua anamuambia mwanangu kuwa Mama yake kafa kwa namna ile.

“Dada! Dada! Dada!” niliita kwa kupiga kelele lakini hakunisikia, alikua kashamkabidhi mwanangu simu.

“Nani kakuambia umuambie mtoto kuwa Mama yake amekufa, unamaana gani kumuambia mtoto mdogo namna hiyo kuwa Mama yake amekufa, hivi una akili kweli?” Niliuliza nikujua kuwa naongea na dada yangu.

“Baba unasema Mama amekufa, mbona Bibi alisema kaenda hospitalini kuniletea mdogo wangu?”

Sauti ya Joan ilinifanya kuwa kama mtu aliyepigwa na shoti ya umeme, kwa muda niliganda, sikujua kama yeye ndiyo alikua ameshikilia simu wakati namuonya dada yangu.

“Kwahiyo na mimi nitakufa Baba?” Aliniuliza, nilibaki kimya, nilishindwa cha kumuambia.

“Shangazi alisema mimi na Mama yangu ni wachawi na Mama yangu atakufa kwa uchawi wake, kwahiyo na mimi nitakufa?” Aliuliza lakini kabla sijamjibu, dad ayangu alimnyang’anya simu.

“Kaka huyu mtoto anataka kutuchonganisha, Mama yake amemjaza maneno ya ujinga. Nilisema mke wako ndiyo mchawi lakini sijawhai kusema kuwa mwanao ni mchawi, hii ni damu yetu na nampenda sana, Mama yake kafa lakini mimi shangazi yake nitabeba jukumu la Mama yake, nitamle katika maadili huna haja ya kuwa na wasiwasi na hilo…”

Aliongea lakini nilishachefukwa, nilikata simu, nilikua sina namna, nilitoka hapo, kwakua nilijua kuwa ndugu wa mke wangu hawawezi kupokea simu zangu nilitoka na kuazima simu ya mtu mwingine. Nilishajua kuwa mwanangu hawezi kuwa katioka mikono salama mbele ya ndugu zangu, nilimpigia shemeji yangu mdogo wake na marehemu mke wangu, alipopokea hata sikusema haloo.

“Joan hayuko katika mikono salama, nenda nyumbani kwa dada yako mchukue mwanangu na mkae naye nyinyi, najua mananichukia lakini yule mtoto akikaa na ndugu zangu watamuua, wala si watu kabisa, kama unampenda dada yako kamchukue yule mtoto, dada zangu washafi…”

Sikumalizia kuongea simu ilikatwa, nilijaribu kupiga tena na tena lakini haikuipatikana. Niliona isiwe shida, nilimpigia binti wangu wa kazi na kumuuliza hali ya Joan, hakua na sababu ya kunijibu kwani alikua akilia nayeye akimbembeleza.

“Analia, hataki kunyamaza!” Aliongea huku nayeye akionekana kuwa alikua Analia, alishajua kuwa mke wangu kafariki.

“Mchukue na ondoka naye, kaa naye nnje, usiruhusu mtu mwingine kukaa naye, hata kama ni Mama yangu mkatalia. Mama yake mdogo atakuja kumhukua muache aende naye, shangazi yake akitaka kumchukua kataa kabisa!” Nilimuambia, sikumuambia sababu lakini alionekana kunielewa kabisa, hata yeye alishawachoka ndugu zangu hivyo alijua ni kwanini sitaki wakae na mtoto.

Alikubali kufanya hivyo, siku ileile nilitafuta ndege na kurudi nyumbani. Pamoja na yote yaliyotokea lakini ndugu wa mke wangu waliniruhusu kumzika mke wangu, Babu yake na mke wangu ndiyo alikua ni kiongozi wa familia, alikua kazeeka lakini bado alikua na busara za kizamani. Alisema mwanamke akishaolewa basi ni wa mume na haruhusiwi kurudi tena nyumbani kwao. Hwakua na namna Zaidi ya kukubaliana na kila kitu ingawa kwa shingo upande, watu walihudhuria mazishi kwa shingo upande, vinyongo na hasira. Ingawa kila mmoja alijaribu kuficha hisia zake lakini ilikua ngumu sana, majirani waliona na watu waliongea.

****

Baada ya mazishi ya mke wangu ndipo niligundua kuwa nampenda mke wangu, nilianza kuona kama siwezi kuendelea kuishi bila yeye. Ingawa nilishahama nyumbani na kwenda kuishi na mwanamke mwingine lakini sikurudi kwake, nilitoa kisingizia kuwa siwezi kumuacha mwanangu peke yake. Nilikaa pale nyumbani kwa miezi mwilili, yule mwanamke mwingine alipoona namna nilivyobadilika aliondoka zake kwani tulikua hatujafunga ndoa bado, pamoja na ndugu zangu kumsihi kuwa hiyo ndiyo ilikua nafasi ya yeye kufunga ndoa na mimi lakini hakujali, aliondoka bila kugeuka nyuma.

Nilikua na mali, nyumba zangu tatu kubwa tu mbili nilipangisha na moja nilikua nikiishi, nilikua na magari matano, moja la kutembelea na manne ya Biashara, nilikua na kazi nzuri na kipato kizuri, lakini sikua na furaha, sikua na mke na kusema kweli nilikua mpweke sana. Katika bishara zangu niliwakeka wadogo zangu kusimamia, kwakua sikua na mtu wa kukaa naye, mdogo wangu wakiek ambaye alikua chuo nilimuambia ahamie kwangu ili kukaa na mwanangu kwani nilikua ni mtu wa kusafiri safari.

Lakini naye hakukaa sana, ilishindikana kwani ilikua ngumu sana kwake kusoma, sikua na namna, nililazimika kummepekla mtoto wangu nyumbani kwa Mama yangu, nikalazimika kuwa na wafanyakazi wawili mmoja wa nyumbani kwangu akawa kama analinda nyumba na mwingine wa kukaa na mtoto kwa Mama. Lakini baada ya kama miezi miwili Mama alianza kuumwa, sikua na namna, dada yangu mkubwa alimchukua mwanangu na kuanza kuishi naye, kusema kweli sikupenda lakini sikua na namna maneno ya mwanangu kuwa walimuamba Mama yake akifa watamlea yalijirudia kichwani kwangu.

“Wakikifanyia kitu chochote unaniambia? Usiogope, mimi ndiyo Baba yako, hakuna mtu wa kukutesa hapa!” Kila mara nikirudi kutoka safari nilikua namuambia mwanangu. Wakati huo alikua darasa la kwanza, alikua na miaka mitano na alikua na akili sana darasani. Lakini alikosa uchangamfu, alikua ni mkimya sana, kila mara alikua mtu wa kujitengatena, kila mara ninapokua sijasafiri nilikua na mwanangu, nilijitahidi kumuuliza maswali ya mtego ili aniambie kama ananyanyaswa laini hapana hakusema, alikua mkimya siku hadi siku.

Maisha yaliendelea, ndugu walikua wakiniambia kuwa nioe, lakini sikuona kama ni kitu cha haraka sana, bdao nilikua sijamsahau mke wangu hivyo niliona kuoa mapema haitsaidia, sanasana nitamsumbua tu binti wa watu ambaye ningemuoa.

“Baba eti mii nina nyumba?” Siku moja Joan aliniuliza. Nakumbuka tulikua Mlimani City, nilimpelaka kula icecream tu na kuzurura.

“Una nyumba, kivipi?” nilishindwa kumuelewa kwanini anaongea habari za nyumba.

“Betty (Mtoto wa Dada yangu, si jina lake halisi) anasema mimi nikifa kama Mama nyumba zangu zote zinakua za kwao kwakua wewe huna mtoto mwingine. Nilijikuta naishiwa pozi, lakini kabla ya kumjibu swali lake aliniuliza swali jingine.

“Eti Baba kwani mtu akifa kinauma? Ni kama sindano?” nilishangaa tena haya mambo ya kufakufa yabnakujaje.

“Mbona unaongea habari za kufa, ni nani kakuambia hayo mambo ya kufa, wewe ni mtoto mdogo hutakufa!” Nilijikuta namdanganya, nilipaniki na sikujua nini kinaendelea.

“Lakini Betty anasema shuleni kwao kuna mtoto mdogo alikufa, alisema eti na mimi wadogo zangu wote wamekufa, Mama ndiyo aliwaua kwakua ni mchawi na mimi eti Mama taniua.” Aliniambia, niliishiwa pozi kabisa.

“Hakuna kitu kama hicho, Mama yako hakua mchawi na wadogo zako hawakuuliwa!”

“Lakini Baba wewe ulimuambia Mama kuwa ni mchawi, kipindi kiel unampigaga si ulikua unamuambia anataka kukua?” Aliniuliza, nilitamani kunyanyuka na kujipiga makofi, kwa mara ya kwanza katika maisha yangu nilitamani kuzaa mtoto taahira, mtoto asiye na akili, mtoto ambaye hakumbuki mambo.

“Hapana! Mama yako hakua mchawi! Mama yako anakupenda hawezi kukuua!” Nilijikuta nafoka.

“Betty anasema kuwa mama yangui alikua mchawi na uchawi wake ndiyo umemuua. Kila mtu anasema Mama mchawi, Bibi alisema, Baba mdogo alisema, Shangazi anasema kila mtu anasema Mama mchawi?”

Nilishindwa hata kumjibu nini, maneno aliyokua anaongea yalikua ni ya kweli, sikutaka kumlaumu dada yangu wala watoto wake kwani maneno mengi aliyasikia kwangu, ilikua inakaribia maiaka miwili tangu Mama yake kufariki lakini abdo alikua anakumbuka kila kitu, ni kama ilikua jana tu na mbaya Zaidi alikua anakumbuka mimi Baba yake nikimpiga Mama yake na kumuita mchawi kuwa anataka kumuua.

“Mimi nilikosea kumuita Mama yako, mchawi, Mama yako si mchawi na hawezi kuwa mchawi, nataka uelewe hilo kuwa Mama yako si mchawi. Naomba unisamehe na kama kuna mtu mwingine atakuambia hivyo niambie, naomba unisamehe!” Nilijikuta naongea mpaka natokwa na machozi, akili ilikua haifanyi kazi. Kuna kitu kiliniambia kuwa huyu mtoto anatakiwa kwenda kwa ndugu wa Mama yake, si salama kuishi kwangu, hata mimi naweza kumjaribu. Niliwaza sana lakini sikupata majibu, akili ilikua haifanyi kazi, nilipotoka hapo nilimuita dada yangu na kumuambia, sikumlaumu kwani hata mimi nilikosea.

“Hayo mambo yalikua ya zamani Kaka, sasa hivi hakuna hayo mambo, wale ni watoto wanataniana, lakini kumpeleka kwa hao ndugu zake si suluhisho, atakaa huko mpaka lini? Akifundishwa maneno mabaya na kukuchukia? Najua tulikosea, tulimkosea wifi sana lakini niwakati wa kurekebisha, tumlee huyu mtoto kwa upendo atakuja kusahau, lakini akiondoka sasa ni kama sisi tumeshindwa kumlea mtoto. Kaka unatakiwa kuoa mwanamke mwingine, huna sababu ya kusubiri, huyu mtoto anahitaji Mama anahitaji mwanamke wa kumlea, mimi najitahidi lakini na wewe uantakiwa uwe na mtu muishi kama Baba na Mama mtoto apate malezi ya pande zote.”

Sikumsikiliza dada yangu kuhusu suala la kuoa laini nilimuelewa kuhusu kuendelea kubaki na mwanangu, niliona kweli kwa jinsi ndugu za mke wangu walivyokua wakinichukia basi wangemjaza manano mwanangu nayeye akazidi kunichukia. Maisha yaliendelea, siku moja nikiwa nimesafiri nilipigiwa simu na Dada yangu mkubwa ambaye alikua anaishi na Joan, Joan alikua kadondoka shuleni na kuvunjika mkono, kilikua kama kitu cha ajabu, alikua kasimama tu peke yake akadondoka na kupoteza fahamu, kufika hospitalini wanasema kavunjika mkono, kila mtu alishangaa, nilikua nnje kikazi na sikuweza kurudi siku hiyo.

Waliniambia anaendeela vizuri lakini niliporudi baada ya wiki moja hali ya mwanangu ilikua tofauti sana, mkono ulikua umeshindikana kufungta POP kwani ulikua umevimba sana, ingawa wakati anadondoka hakua na kidonda lakini kutokana na kuvimba mkono ulipasuka, kuliota kitu kama jipu kubwa ambalo lilitoa usaha sana, nilikasirika kwani mwanangu alikua hoi kitandani lakini hawakuniambia, nilipouliza waliniambia hawakutaka nipaniki.

“Kaka huyu ni mtoto wako?” Nesi mmoja aliniuliza. Ilikua ni jioni, ndugu zangu walishaondoka hospitalini nilibaki mimi na mwanangu nikimuuguza, ilinibidi kumpa uangalizi maalum na kumhamishia katika chumba cha peke yake.

“Ndiyo kwanini?” Nilimuuliza yule dada, alionekana kama mtu mwenye wasiwasi sana lakini ule wa kujali.

“Mbona unaonekana una pesa sana lakini umekuja kumelekeza mwanao hapa, huyu mtoto usipocheza mkono utakatwa, kabinti bado kadogo kana akili sana.” Aliongea, nilishangaa na kumuuliza alikua anamaanisha nini kusama tunamtelekeza mtoto.

“Unajua mwanzo nilikua namhudumia tu hivyo hivyo najua kuwa hana ndugu, lakini ulipokuja na kumhamishia hapa mpaka nimeshangaa. Mtoto ana Zaidi ya wiki hapa, kaletwa na walimu katupwa hapa, hao ndugu zako wamekuja mara moja tu ile siku ya kwanza, hivi kweli Kaka unafikiri hizi shule zinajali, kama huhudumii mtoto wako unafikiri nani atakusaidia?”

Aliongea kwa hasira kidogo, mwanzo nilitaka nisema anadanganya, ndugu zangu hawawezi kufanya kitu kama hicho, lakini nakumbuka ni Zaidi ya mara sita nilitaka kuongea na mwanangu ila dada yangu aliniambia kuwa mara kalala, mara daktari wa zamu, mara hawaruhusu simu.

“Unasema nini dada?” Nilijikuta nawaka.

“Mimi sijui kuhusu familia yenu ila kama wale ndiyo umewaachia mtoto basi na wewe Kaka huna akili, mtoto analia kila siku lakini hakuna ndugu hata mmoja. Kila siku mimi ndiyo nashinda naye, hembu fikiria mtoto mdogo kama huyo anawaza kufa kila saa, kua makini Kaka pesa hizi zinatafutwa ile mtoto utamjutia milele!” Aliongea yule dada na kuondoka zake.

Sihdani kama nina haja ya kukuambia, je Baba Joan ataachana na ndugu zake na kufanya maisha yake, je nini kimempata Joan, basi

BABA JOAN; MIMI NA MWANANGU JUU YA KABURI LA MKE WANGU!—SEHEMU YA TATU

Nilishindwa kuamini maneno niliyokua nikiambiwa, mwanangu alkua ndiyo kila kitu kwangu, baada ya kifo cha mke wangu nilizidisha upendo na ukaribu kwa mwanangu kuliko kitu chochote kile. Nilikua natoa pesa nyingi kwaajili ya kumhudumia na mtu niliyekua nikimpa ni dada yangu ambaye alikua kama Mama yake. Nilikasirika lakini sikutaka kuonyesha pale kama kuna tatizo, niliingia ndani na kukaa na mwanangu.

“Baba nikuambie kitu?” Joan aliniambia. Nilimsogelea na kukaa pembeni yake huku nikikaangalia kamkono kake kadogo ambako kalikua kamefungwa POP.

“Baba Mama alikuja, jana Mama alikuja na kuniambia kuwa nisiogope atanilinda.” Aliongea.

Nilimsikiliza alivyokua anaongea, sikua na jibu la kumpa zaidi ya kumuambia kuwa Mama anatulinda sisi wote kwani yupo mbinguni kapumzika.

“Hapana Baba, Mama hakulindi wewe, wewe huna tatizo, mimi ndiyi wanataka kuniua, Baba mimi sitaki mali zako, kila mtu ananichukia kwakua wewe una pesa, mimi sitaki pesa zako, nataka ukamuambia Shangazi kuwa mimi sitaki pesa zako asije kuniua.” Aliniambia, nilimuangalia na kukumbuka siku ya msiba wa mke wangu namna ambavyo mwanangu alikua akiongea kuhusu mambo ya kufa. Niliona kuna tatizo lakini sikutaka kumuambia kitu, nilinyamaza tu na kumuambia asiogope hakuna mtu wa kumuua.

Jioni ndugu zangu walikuja hosipitalini, walijifanya kumpenda na kumnyenyekea mtoto wangu lakini nilihisi kama kuna kitu. Sikutaka kukaa mbali na mwanangu kwani nilihisi kama kuna kitu kibaya wanataka kumfanyia.

“Kaka unaweza kuondoka, mimi nitabaki na mtoto.” Mdogo wangu wakike aliniambia, nilimkatalia na kumuambia nimemmiss sana mwanangu hivyo siwezi kuondoka. Walinisisitiza sana lakini sikukubali, kuna kitu kibaya nilikihisi, nilikaa mpaka asubuhi. Nikiwa nimechoka asubuhi niliondoka na kurudi nyumbani, nilijua kabisa hawawezi kumfanyia kitu chochote mwanangu, lakini kabla ya kuondoka, nilimfuata yule nes wa jana nikampa laki moja na kumuambia amuangalie mwanangu vizuri.

Nyumbani nilikuta ndugu zangu wote wapo, walishahamia kwangu, walikua kama wamekuja msibani, kwa namna nilivyowaona nilikumbuka siku ambayo mke wangu alifariki dunia, sikua nyumbani lakini niliporudi wote walikua nyumbani wananisubiri kama wanataka kuniambia kitu. Baada ya kusalimiana waliniulizia hali ya mtoto, nikawaambia kuwa anaendelea vizuri, walionekana kama vile wameshangaa lakini mimi hata sikujali. Niliingia ndani na kuoga kisha nikajiandaaa kutoka tena, nilitamani kupumzika lakini kuna kitu kiliniambia hapana, rudi kwa mwanao, nilitoka kutaka kuondoka, wakati nataka kuondoka mtoto wa mdogo wangu wa kike alinifuata.

Derric (si jina lake halisi) alikua ni umri sawa na Joan wangu na alikua anampenda sana, wakati anakua nilimchukua kuishi naye mpaka mke wangu tulipoanza kukorofishana ndipo nilimrudisha na sababu ya kumrudisha nikuwa Mama alikua akisema kuwa mke wangu anamloga, anamtesa na kumnyanyasa.

“Baba, mimi nataka kwenda kumuona Joan.” Aliniambia wakat natoka, kutokana na kumlea tangu akiwa mdogo alikua akiniita Baba, alikua akifahamu kuwa mimi ndiyo Baba yake, hata baada ya kuondoka kwangu alikua akijua hivyo.

“Hapana, muache Baba yako ana mambo yake kwani nani kakuambia kuwa anataka kwenda hospitalini? Haendi huko ndiyo katoka huko!” Dada yangu mkubwa aliongea huku akimshika Derrick na kumrudisha ndani kana kwamba kafanya kitu kibaya.

“Hapana, muache, siendi hospitalini lakini jioni nitapitia huko, ngoja nikazunguke naye mjini, unajua kuwa hawa watoto sijakaa nao muda mrefu, twende.” Nilimjibu kwa mkato, niliongea kwa kufanya maamuzi kana kwamba sihitaji kujibishana na mtu, sijui kwanini lakini niliona kama ninahitaji kuondoka naye, nilimshika mkono na kutoka naye bila hata kutaka abadilishe nguo.

Nilimchukua Derrick na kupanda naye kwenye gari, alikua ni mchangamfu, kama watoto wengine aliuliza uliza maswali mengi mengi na mimi kumjibvu, alikua anaongea sana mpaka ile unaboreka na kupandwa na hasira lakini unakua huna namna, ni mtoto tu utafanyaje.

“Baba, hivi Mama atarudi tena?” Aliniuliza, swali lake lilinikera lakini utafanyaje, ni mtoto na ni mimi niling’ng’ania kuenda naye.

“Hapana, yuko mbinguni amepumzika, sisi ndiyo tutamfuana yeye.” Nilimjibu kwa kifupi tu, alinyamaza kwa muda kama anafikiria kitu kisha aliniuliza swali ambalo lilinichekesha.

“Baba wewe si ni mwanaume kama mim?” Nilimuangalia na kucheka.

“Ndiyo kwanini?” Nilimjibu huku nikicheka, aliniangalia kuanzia chini mpaka juu kisha akaniambia.

“Nakuambia wewe kwaka ni mwanaume, Joan ni rafiki yangu lakini hana kifua, yule ni mwanamke hawezi kuficha siri, ila wewe mwanaume utaficha.” Nilitingisha kichwa tena na kucheka.

“Watoto wana mambo hawa!” Kichwani nilihisi kama labda kashajifunza mapenzi ndiyo anataka kuniambia mambo yake.

“Shangazi alikua hataki niongozane na wewe kwani anaogopa kuwa nitakuambia?” Alianza kuniambia.

“Anaogopa kuwa utaniambia nini?”

“Wanataka kumuua Joan kwani wanasema wewe ukifa yeye ndiyo atachukua mali zako.” Aliongea kwa kujiamini, huku akiniangalia kisha akamalizia.

“Wewe u mwanaume, lazima uvumilie, kuna mambo makubwa sana.” Aliniambia, sikushtuka sana, nilimsikiliza kwa makini.

“Kila siku Shangazi analeta waganga, walikua wanataka umchukie Mama lakini sasa hivi Mama amekufa, wanataka kumuua Joan kwani wanajua unampenda sana na kila kitu umeandika jina lake. Wewe ukifa ndiyo ataridhi mali zake zote, lazima wamuue.” Aliniambia, alikua ni mtoto mdogo lakini alikua anaongea maneno makubwa.

“Wewe ulijuaje?” Nilimuuliza.

“Baba, kila mtu anajua kuwa mimi ni mtoto, wanaongea mambo yao mimi nawasikia, hawajui nimeshakua mwanaume. Mwanzo nilikua namuambia Joan ajilinde lakini naona kashindwa, Imani yake ndogo. Mimi namlinda lakini yeye kanisani hasikilizi vizuri.” Aliniambia.

“Baba, hata wewe Imani yako n indigo, unajua mimi ndiyo nakulinda na wewe?” Aliniuliza. Nilishangaa na kumuuliza ananilindaje, akafungu mkanda wa fari, akanyanyuka na kupita mpaka siti ya nyuma, alifungua chini ya siti ya dereva na kutoa chupa ncogo ya maji kisha akarudi.

“Angalia, haya ni maji ya Baraka, niliiba kanisani na kuja kuweka kwenye gari yako, Mama alikua anasali sana ndiyo maana hawakumuweza, Mama hajauliwa, emekufa kifo cha kawaida, aliniambia nikulinde wewe na Joan kwakua hamna imani. Maji ya Baraka aliyonipa yaliisha, nikaenda kuiba kanisani, najua ni dhami lakini Mungu anajua kuwa mimi ni mtoto nisingepewa maji ya Baraka. Joan wanataka kumuua kwaku hana Imani, wanataka mali zako Baba.”

Nilimuangalia Derrick bila kumpatia majibu, alikua akiongea kwa kujiamini, hapo alikua na miaka nane tu lakini alijua kila kitu. Sijui alipata wapi huo ujasiri nahisi mke wangu, alikua akiongea kama mke wangu ambaye kila wakati alikua akimuita mama.

“Mimi kila siku nawasikia, mipango yao yote, naman Bibi alivyokua akimchukia Mama, namna ambavyo wanasema unalogwa, vitu vyote walivyokufanyia mimi najua. Baba wewe ulimfukuza Mama, hazikua akili zako, silikua ni akili za Shangazi, waliona kuwa Mama ndiyo kikwazo, kama ukifa mali zaote atachukua yeye na wao kubaki hawana kitu. Najua unaniona mtoto lakini chunguza, Joan haumwi, lakini asipopata maji ya Baraka atakufa, ndiyo maana mimi nataka kwenda hospitalini, nimejaribu kipindi chote lakini hawakuniruhusu, kama huniamini Baba nipeleke, nitamuombea, atapona, asipopona Baba usiniamini mimi, Mungu wangu ana nguvu zana kuliko mizimu yao!”

Aliongea sasa kwa kujiamini mpaka nikaogopa, nilianza kupata hofu mtoto kama yule kuongea maneno yale. Ni kama alikua ananisoma, alijua kuwa naogopa akanitoa hofu.

“Baba usiogope, mimi nina Imani, hate wewe ukiwa na Imani ukamjua Mungu vizuri hakuna mtu atakayekusumbua. Uchawi wote ni mambo ya shetani ambaye hamuwezi kabisa Mungu.” Nilikua nimepanga kuzunguka mjini lakini niliamua kumpeleka hospitalini, ingwa sikuwa na imani lakini nilitaka tu kuona kama anachosema ni sawa. Tulifika na akashuka na maji yake ya Baraka. Tuliingia mpaka chumbani, Joan kumuona Derrick alifurahia sana, wakasalimiana kisha Derrick akaniambia.

“Baba wewe toka, Imani yako ni ndogo sana, bado unaamini katika wachawi ndiyo maana ulimuacha Mama, Mungu hajaribiwi, jina la Mungu halitajwitawji bure mbele ya wanafiki, ondoka!”

Aliniambia, sikua na namna niliondoka, kweli nilikua kama mnafiki, sikua na imani na pale sikuenda kuangalia kama atamuombea atapona, nilitaka kupima kama anaongea ukweli, nilikua kama namjaribu Mungu kuwa anaweza kweli au la. Lakini Derrick alikua na Imani. Namna alivyokua anaongea niliogopa na kutoka. Nilikaa nnje kwa nusu saa, kisha nilimuona Derrick akitoka na Joan, alinifuiata na kuniambia.

“Waambie wamtoe haya matambala, Mungu ameshamtbu hana haja ya kuvaa haya makitu.” Aliongea, nilishindwa kumuelewa lakini Joan alikua anarusha mikono kama vile hajaumia huku akilalamika kuwa lile POP ni zito na linamchoma.

Nilimuita Nesi ambaye naye alishangaa, akamuita Daktari, ambaye pia alishangaa, waligoma kumfungua lakini nililazimishia, walimfungua ila kw akujiridhisha walimpiga X-ray nyingine, huwezi amini hawakukuta kitu. Hakuna aliyeamini walilazimika kunionyesha na ile X-ray ya kwanza na kweli mwanangu alikua kavunjika mfupa.

“Hapana, hii haiwezekani, hawezi kupona kirahisi namna hii?” Daktari aliongea akiwa haamini.

“Huamini nini, kama uliamini kuwa mtu anaweza kusimama na kudondoka akavunjika mkono bila hata kusukumwa au kuangukia kitu kwanini usiamini kuwa mtu anaweza kusimama na mkono ukajiunga bila kufungwa popote.”

BABA JOAN; MIMI NA MWANANGU JUU YA KABURI LA MKE WANGU!—SEHEMU YA NNE

Nilimuona Derrick kama malaika, lakini nilimuangalia kwa uoga kwani alikua ni mtoto mdogo lakini alikua akiongea na kufanya mambo makubwa. Tuliruhusiwa kutoka hospitalini baada ya vipimo vyote kuonyesha kuwa mwanangu yuko sawa, tuliondoka lakini sikutaka kabisa kurudi nyumbani, nilizunguka tu na gari mjini nikiwaza namna ya kurudi nyumbani wakati ndugu zangu wote walikua pale.

“Hawezi kuku yeye hana nguvu ya kuua, Mungu tu ndiyo ana nguvu ya kuua, Mama aliniambia.” Joan na Derrick walikua wamekaa nyuma kwenye gari, mimi nilikua mbele naendesha lakini mawazo yangu hayakua barabarani kabisa, ni kwa kudra za mwenyezi Mungu tu nilipona, walikua wakiongea.

“Leah (Mtoto wa dada yangu) alishaema nitakufa kama Mama yangu kwakua sisi ni wachawi, Peter (mtoto mwingine wa ndugu yangu) anasema hivyo hivyo, wote wananichukia.” Joan alilalamika.

“Mama hakua mchawi, alikua mtu wa Mungu na ameenda mbinguni.”

“Hapana, wewe unasema kwakua si Mama yako, mimi najua tu wananichukia na nitakufa!”

Nililazimika kusimamisha gari sehemu na kukaa nao, walikua wananichanganya, walikua watoto wadogo lakini walikua wanaongea maneno makubwa ambayo hata mimi sikuyaelewa. Nilitafuta sehemu tukakaa na kuwanunulia Icecrem kisha nikaanza kuwahoji, Joan yeye alikua angopa lakini Derrick alikua haogopi, aliongea kila kitu, alikaa kwangu muda mrefu kama mwanangu na kuondoka hakurudi kwa Baba yake bali alienda kwa Dada yangu kwani wakati huo Baba yake alikua hajaoa (Mtoto wa kabla ya ndoa) hivyo sisi ndugu wenye ndoa ndiyo tulikua tunamlea.

Ndugu zangu walikua na wasiwasi kuhusiana na mke wangu, waliona kama atachukua mali zangu, katika familia yetu mimi ndiyo nilikua wakwanza kupata pesa hivyo kila mtu alikua akiniangalia kwa jicho la tamaa.

“Kila siku wakija walikua wanasema kuwa Mama ni mchawi, anakuloga wewe ili uwachukie wao, walikua wakimchukia wakisema kuwa wewe ukifa Mama ndiyo atachukua kila kitu…” Alianza kunielezea.

“Mimi mdogo, hawakujua kama nawasikiliza, nilimuambia Mama yeye ndyo akanipeleka kanisani, aliniambia niwe ninaomba kwani mbele ya Mungu hakuna wa kushindana naye.” Aliniambia.

Nilitoka pale na kurudi nyumbani, nilikutya ndugu zangu wakinisubiri, kwa namna walivyokua wananiangalia ni kama walikua wakisiburi habari mbaya, walishangaa kuniona niko na Joan. Mimi sikusema chochote, walinipongeza kinafiki na kuongea maneno maneno yao lakini wala hata sikuwasikiliza. Niliamua kuwa bize na mambo yangu, niliingia chumbani na mwanangu, sikutaka alale chumba kingine, nilitaka niwe namuona. Mdogo wangu Baba yake na Derrick alikuja, alitaka kumchukua Derrick lakini nilimuambia hapana, ngoja abaki hapa kwani nataka acheze na Joan kwani wamezoeana.

Kwakua nilikua kama bosi alinisikiliza. Kurudi kwangu na Joan akiwa salama kuliwaumiza sana, sikuongea chochote, sikuonyesha kuwajali, walijongeza na wote kuondoka, pale nyumbani nilibaki mimi, na wanangu wawili pamoja na binti wa kazi. Kwa wiki nzima nilikua kama mtu aliyechanganyikiwa, akili yangu ilikua kwa mke wangu, mwanamke ambaye nilihangaika naye kipindi cha shida, kipindi sina kitu kabisa. Kwa mambo niliyoyaona kama ningesimuliwa na mtu nisingeamini lakini niliona mwenyewe kwa macho yangu, sikuamini kuwa ndugu zangu niliokua nawapenda sana na kuwaona kama washirika wangu wakuu wangeweza kujaribu kumuua mwanangu kisa mali.

Nilikaa wiki nzima bila kuenda kazini, pamoja na kuwa na kazi nyingi, kuhitajika sana lakini niliacha tu kwenda kazini tena bila kutoa taarifa, nilijisikia vibaya na nilikua kama mtu aliyekata tamaa na maisha. Derrick alishondoka kwangu na kurudi kwa Baba yake, nilibaki na mwanangu Joan ambaye kwa wakati huo hata sikutaka aende popote kwani nilihisi kama wanataka kumfanyia kitu kibaya. Mawasiliano na ndugu, kila walipokua wananipigia simu nilitafuta sbabau tu ya kuwakwepa, walihisi kitu, dada yangu mkubwa ambaye ndiyo tulikua tunamuamini kwa kila kitu ndiyo alikua na ujasiri wa kunipigia na kunisalimia.

Siku moja linipigia na kuniambia kuwa natakiwa tukutane nyumbani kwa Mama, nilikaaa na kumuambia kuwa nipo bize kidogo, lakini jioni yake Mama yangu mkubwa alinipigia simu na kuniambia kuwa natakiwa kwenda nyumbani kwani anataka kuongea na mimi. Pamoja na chuki niliyokua na ndugu zangu wengine lakini Mama yangu mkubwa nilikua nikimheshimu sana, mara nyingi alikua ni mtu wa busara hata kipindi namtukana mke wangu kipindi nawaambia ndugu zangu wengine wote wanamchukia mke wangu yeye alikua bega kwabega na mke wangu.

Nilimchukia kwa kipindi hicho, lakini mara nyingi alikua mtu wa kuniambia, mwanangu ndoa hii ni yako, wewe na mke wako si wewe na dada zako. Yeye ni mtu wa dini sana, na si mtu wa kuficha ficha mambo, kama umekosea kitu anakuambia kabisa kuwa umekosea. Nilienda nikijua labda kaniitia mambo yake, lakini nilipofika nilimkuta dada yangu, nilikasirika kwani niliona kama Mama naye kanisaliti yupo upande wao.

“Dada yako kaniambia kuwa hutaki kuonana naye? Kwani kakukosea nini, nyie ni ndugu hembu ongeeni yaishe…” Alianza kuongea, kwa wakati huo mimi sikua tayari kabisa kuongea chochote, bado nilikua na hasira, nilikua sijamuambia mtu yeyeote mambo niliyoambiwa na Derrick na sikua tayari kufanya hivyo kwa wakati huo.

“Mbona mimi sina tatizo Mama, mimi niko sawa, labda dada ndiyo aseme kuwa kuna tatizo gani, aliniambia leo tuonane nikamuambia nitakua bize, lakini uliponiita wewe kwakua ni Mama basi nikaamua kuja. Nimekuja labda aseme kama mimi nina tatizo au la?” Niliongea huku nikimuangalia, aliniangalia kwa jicho la aibu kisha akasimama na kuniambia kuwa hakuna kitu.

“Nilijua labda una hasira na mimi ndiyo maana nikaja kumuambia Mama mkubwa kwakua unampenda sana utamsikiliza. Lakini kama hamana kitu basi mimi naondoka.” Aliongea harakaharaka na kuondoka kama vile anakimbia, nilishtuka kidogo, nilimuangalia Mama lakini naye alishangaa.

“Nilishakuambia, hawa ni ndugu zako lakini kuwa makini nao. Walikufukuzia mke na kila siku nilikua nakuambia, kua makini nao, kuna kiwanja nasikia wanauza, kuwa makini na nyaraka zako, kuwa makini sana!” Aliniambia, nilimuambia kuwa mimi niko makini sana na nyaraka zangu na tangu kifo cha mke wangu kila kitu niemchukua mimi. Hawna kitu changu hata kimoja.” Nilimuambia.

“Ndiyo maana naona wanahaha haha, naona wanataka kunitumia mimi kukurudisha, hawa si watu wazuri, watu wanaokuja kwako ukiwa ndiyo umepata basi jua kuwa wanaweza kufanya chochote. Kuwa makini mwanangu, uwe unaendaga na kanisani kwani kuna majaribu mengi.” Mama mkubwa aliniambia, nilimuambia niaanza kwenda.

Kutokana na kazi zangu nilikua si mtu wa kanisani kabisa, sikua na mambo ya Imani, mke wangu alikua hivyo na yeye ndiyo alimlea Derrick na Joan kuwa watu wa Imani, mimi hata kwenda kanisani ilikua shida. Nilitoka na kuagana na Mama yangu nikiahidi kwenda kumtembelea kwani yeye peeke ndiyo nilimuona kama ndugu, alikua ananiambia ukweli kila nikikosea, alikua si mtu wa kuzungukazunguka, alikua hajali kama nina pesa wala nini mimi kwake nilikua mtoto ndiyo maana kipindi namtukana mke wangu alikua ananisema na kunigombeza kama mtoto, alikua akimpasha Mama yangu mzazi na kumuambia anaharibua ndoa yangu, mara kadhaa alimtukana na kumuambia anapenda sana pesa an anaharibu watoto, hakuogopa maneno ya watu.

Nilitoka, wakati naingia kwenye gari niliona kitu kimedondoka pembeni ya gari yangu, niliangalia na kuona kama pochi, nilikumbuka kuwa nilimuona dada yangu akiwa na ile pochi wakati yuko kule ndani kwa Mama. Niliiokota, ilikua na pesa kidogo, nilitaka kuirudisha ili Mama mkubwa ndiyo ampe dada lakini niliona kama atahisi kuwa kuna tatizo kwani mimi nilikua narudi mjini na ingekua rahisi kwangu kuonana na Dada yangu kuliko yeye pale nyumbani, nilishamuambia kuwa hakuna shida hivyo sikutaka aone kama nina kinyongo, niliichukua ile pochi ya dada yangu na kuingia nayo kwenye gari yangu.

Nilianza safari ya kurudi nyumbani, lakini nikiwa njiani nilianza kujihisi kama nakosa pumzi, nilipata shida sana kupumua, hewa ndani ya hgari ilianza kuwa nzito na kuanza kujihisi kizunguzungu, hali ilikua mbaya nikwa kama napandwa na presha, nguvu ziliniishia nikajikuta nashindwa kuendelea na safari. Gari ilipoteza uelekeo, niligongana na Lori lililokua linakuja upande mwingine, mimi ndiyo nililifuata, wakati nalifuata nilikua naliona kabisa, naiona ajali inatokea mbele yangu lakini sikuweza kusogeza hata mkono kukwepesha, baada ya hapo sikusikia chochote.

Nilikuja kuzinduka baada ya siku tatu baadaye nikiwa sina miguu yote miwili, ilikua imekatwa juu kidogo ya magoti. Waliniambia nilipata ajali mbaya ni Mungu tu nimepona, hakuna aliyeamini kuwa naweza kuzinduka. Ndugu zangu walikua wanapeana zamu kuniuguza, lakini kwa kuwaangalia niliona kabisa wanafanya unafiki kwani mtu anakuhudumia lakini kwa kinyaa. Nilikaa hospitalini mwa miezi mitatu ndipo niliporuhusiwa kutoka, nilirudi nyumbani na kukuta kama ninaanza upya, maisha yalikua magumu sana, uzuri nilikua nabima, nilikua natibiwa na bima hivyo sikua na madeni mengi.

Kazini niliondolewa na kulipwa kiinua mgongo changu cha ulemavu wa kudumu kwani nisingeweza kufanya kazi tena kutokana na ulemavu wangu. Niliruhusiwa lakini nilikaa nyumbani bila kufanya chochote kwa mwaka mzima nahudumiwa tu mpaka nilipopata nguvu. Niliuza karibu kila kitu, nilibaki na nyumba yangu mmoja ambaye nilikua nikiishi, Biashara nzao ambazo nilikabidhi ndugu zilikufa bila maelezo ila niliona wao wakifungua Biashara zao wenyewe bila kunishirikisha. Nilipitia kipindi kigumu sana, nakumbuka hata mototo wangu alilazimika kurudi kusoma shule ya serikali.

Lakini nimejitahidi sasa hivi nina duka langu kubwa tu linanisaidia kuendesha maisha yangu, mimi na mwanangu. Nimepona na namshukuru Mungu kwa kila siku kuna kauli ambayo hainitoki kichwani kwangu, siku niliporoka hospitalini Derrick aliniambia “Baba una Mungu, ulipopata ajali nilimsikia Shangazi akisema kuwa alitaka kukumaliza, ulikua ufe Baba, una Mungu.” Sikujua kama mali zinaweza kumfanya mtu kuwa na roho mbaya namna hii lakini baada ya kupitia yote haya nimeamini kuwa kuna watu wanaweza kuua kwasababau ya pesa na kusahau utu.

MWISHO
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom