Simulizi: Kazi ya Kutengeneza Majeneza

Sehemu ya 91.

Wakati tunarudi, njiani nilimwambia mdogo wangu kuwa, huenda wale watu waliagizia majeneza mawili, kwangu moja, kwa fundi mwingine moja. Sasa walikuja kulichukua hilo jingine na kulipeleka kisha watalirudia jingine ambalo liko kwangu.

"Mh! Huenda kaka, lakini si ulisea maeneo haya hakuna sehemu wanakouza majeneza?" aliniuliza.

"Labda walichukua mahali wakaliteremsha pale, halafu saa zile ndiyo walikuwa wakilipakiza garini," nilimjibu kwa kujigongagonga ili mradi tu.

"Lakini walipokuwa wanaondoka si walikuaga kwamba wanakwenda kuangalia uwezekano wa usafiri kaka. Sasa kama ni hivyo unavyoongea walikuwa na maana gani wakati usafiri walikuwa nao?" mdogo wangu aliniuliza kwa sauti iliyojaa wasiwasi.

Kuna uwezekano mkubwa kwamba, muda ulivyozidi kwenda na yeye kwa vile ana akili timamu alikuwa anapata picha tofauti na ile ya hali aliyoiona tayari.

Mpaka giza linaingia wale watu walikuwa hawajaja kulichukua jeneza lao licha ya kwamba lilikuwa limekwisha lote mpaka kulipaka vanishi.

Nilimwambia mdogo wangu tuliingize ndani sisi tuondoke lolote litakalotokea sisi hatutahusika kwa namna yoyote ile.
Alikubali, tukafungafunga kazi na kuondoka zetu hadi nyumbani. Tulipofika tu, mdogo wangu alikwenda kuoga, alipotoka alichukua sigara yake na kutoka nje akiniambia kuwa, anarudi muda si mrefu, lakinu akirudi atakuwa na mazungumzo makubwa na mimi. Nikamjibu sawa.

Dakika tano tu, alirudi akionekana alitoka kuvuta sigara.

"Kaka," alianza kusema mdogo wangu huku akikaa juu ya kitanda.

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 92.

"Mimi naona nirudi nyumbani Tanga," mdogo wangu aliniambia kisha akaniangalia usoni kwa kunichunguza nimepokeaje ombi lake hilo.

Badala ya kumjibu nilibaki namwangalia tu usoni, kwani sikujua kwanini aliniomba kurudi nyumbani.
"Je, ni kwa sababu ya haya maajabu anayoyashuhudia kwa mbali au?" nilijiuliza mwenyewe bila kutoa sauti.

"Au amekumbuka nyumbani, maana hata mimi siku za kwanza nilipokuja Dar nilikuwa nakumbuka sana nyumbani," niliendelea kujisemea moyoni mwenyewe.
Nilimkazia macho zaidi huku nikitafuta kumsoma usoni ambako kulionekana kabisa kwamba alichokuwa akikiongea kilikuwa cha dhati na cha kutoka moyoni mwake.
"Kuna nini?" ndiyo swali la kwanza kumuuliza baada ya kutoa ombi lake.

"Wapi?" naye aliniuliza. Ilionekana muda ulivyopita baada ya yeye kusema akawa amepoteza muungano wa ombi lake na swali langu.

"Si huko nyumbani," nilimjibu.
"Nataka kwenda tu," naye alinijibu.
"Kwenda tu! Kwenda tu," nilijikuta mimi nayarudia maneno hayo.

"Ndiyo kwenda, kuna matatizo au umeona nini wewe kuwepo hapa Dar? Si tulishakubaliana toka tunakuja, tukiwa kule nyumbani kwamba utakaa huku ujifunze kazi kama yangu halafu utafute maisha yako?" nilimuuliza kwa kumsuta na kumbana.
Niliamua kumbana kwa kujua kwamba kwa vyovyote vile lazima atasema kwanini anataka kurudi nyumbani.
"Ni kweli kaka, lakini naomba sana niende tu."

Aliponijibu hivyo nilijua kwamba hakuna njia nyingine itakayomfanya asiendelee kuniambia kwamba anataka kurudi nyumbani.

Nilimuuliza alitaka kuondoka lini, akajibu hata kesho yake. Nilimpa pesa ili aondoke hiyo kesho yake. Na mimi kutotaka kumwona tena nyumbani kwangu.
***

Usiku nikiwa nimelala, nilijikuta nikishikwa mguu wa kulia na kuvutwa. Kwa mbali sana nilianza kufumbua macho ili kuangalia nini kilikuwa kikifanyika mle chumbani mwangu.
Sikuyafumbua macho kabisa kama inavyokuwa, bali nilikuwa kama nusu nimelala, nusu niko macho.

Mwanamke yule yule aliyekuwa amenitokea siku moja nyuma akiwa amejifunika ushungi, alikuwa amesimama mbele yangu huku akiniangalia kwa umakini na akiendelea kunishika mguu kunivuta taratibu sana.

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 93.

Sikutaka kupiga kelele kuomba msaada. Kwa jinsi nikivyofumbua macho niliweza kumwona mdogo wangu amelala pembeni yangu kama ilivyo kawaida.

Sikuwa nachezesha kichwa wala shingo ili yule mwanamke asije akashituka. Lengo la kutulia sana lilikuwa ni kutaka kumwona vizuri sura ili nimtambue ni nani.
Aliendelea kunivuta taratibu nikiwa nakitoka kitanda kwenda chini.

Ilipofila wakati miguu mpaka kiuononi vinaning'inia, halafu nusu ya kiuno hadi kichwani viko kitandani, aliniacha akasimama katikati ya chumba.
Nilimuona akianza kuvua nguo. Hapo nilimshukuru sana Mungu. Alianza kwa kuvua kitenge alichokuwa amejifunga kuzunguka kiuno.

Akaja alichokuwa amejifunga kwa kuzunguka mabega kisha akabaki na kaptura kwa ndani. Lakini ushungi ilikuwa bado umemziba kichwa.
Akanisogelea na kuniinua ili nikae. Nikakaa akiwa amenishika kwamba nisianguke akaniacha.

Lakini ukweli ni kwamba nilikuwa na uwezo wa kukaa mwenyewe pale kitandani hata kama yeye asingenishikilia.
Nikapata bahati moja kubwa sanaz kwamba uso wangu ukawa unaangalia chini aliposimama. Niliweza kuona miguu yake yote miwili. Lakini sasa sikuwa naifahamu ni miguu ya nani.

"Mwache aende! Mwanchie mdogo wako aende zake," yule mwanamke aliniambia akiwa bado amenishika.
Sasa alinishika mabegani kwa mikono yake yote miwili.

Sauti yenyewe ilikuwa ikitoka kwa chini sana kama vile mtu anavyonong'ona. Nadhani lengo lake lilikuwa mimi nisiweze kumtambua yeye ni nani ingawa kwake yeye alinifahamu mimi ni nani.

Katika kuangalia miguu vizuri niliweza kuona kovu moja kubwa ambalo lilikuwa kidonda zamani.

Lilikuwa kovu la duara. Hapo nilibaini kuwa, mguu ule niliwahi kuuona sehemu, lakini sikukumbuka niliuonea wapi.
Niliumiza kichwa ili kukumbuka lakini sikufanikiwa. Moyoni nikaazimia kwamba, kuanzia kesho yake asubuhi kufanya uchunguzi wa kina kwa kila mwanamke ninayemfahamu ili kuona mguu wenye kovu kwa juu ni wa nani.

Nitakayemuona ndiye mbaya wangu wa siku zote.

Aliponiachia alinisukuma nikaangukia kitandani na kulala usingizi wa moja kwa moja mpaka asubuhi mdogo wangu aliponiamsha na kuniambia yeye yupo tayari kwa safari ya kwenda nyumbani, Tanga.

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 94.

Niliamka kama naweweseka nikaangalia huku na kule, kisha nikamuuliza ameamka saa ngapi.
"Nilikuwa macho usiku wote," alinijibu.
Niliogopa nikasikia aibu.

Niliwaza kuwa, kama ni kweli ina maana kwamba yote yaliyokuwa yakifanyika usiku aliyashuhudia ila alibana kama mimi mwenyewe niliyekuwa nafanyiwa nilivyobana.

Nilitaka kumuuliza aliona nini na nini usiku, lakini moyo wangu kama kawaida yake ukawa unaogopa.

Nilitoka kitandani, nikamchukulia pesa ya nauli na ya matumizi ya siku mbili tatu. Kisha nikampa na pesa ya kumpa baba na mama. Nikamwambia anisalimie wote nikarudi kitandani kulala.

***
Saa mbili na nusu nikiwa naingia kazini kwangu, kwanza kabisa hata kabla sijafungua yule mama jirani aliniita akiwa amesimama nje ya nyumba yake.

"Hujambo lakini?"
"Sijambo, shikamoo!"
"Marhaba! Eti, kuna watu walikuja kwangu usiku wakasema wanataka jeneza lao, nikawajibu umeshaondoka wakasema wanakufuata nyumbani kwako ili uje uwape jeneza lao, sijui ulikuja kuwapa?"

Niliguna kwanza kisha nikamuuliza kama hao watu wanapafahamu nyumbani kwangu.
"Walisema wanapafahamu, kwa bibi nani sijui walitaja na jina," yule mama alinijibu hivyo.

Nilimwambia anipe muda ningemjibu huku nikifungua geti kubwa kuingia ndani ili kuangalia kama jeneza lipo au la!

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 95.

Hakukuwa na jeneza wala mfano wake. Ukweli ni kwamba wale watu walilichukua jeneza lao baada ya mimi kuondoka au ndiyo vile tena, huenda walinifuata nyumbani kimauzauza na kunichukua kimauzauza hivyo hivyo kwenda kuwatolea jeneza lao kazini kwangu.

Wakati nawaza hayo, niliendelea nilibaki nimesimama getini nikikodolea macho mle ndani huku nikishangaa ni maajabu gani yananitokea kiasi kile?
Kwa nini mimi?
"Kwa nini mimi?" nilimuuliza kwa sauti ya juu nikiwa na hasira.

"Kwa sababu ni wewe," niliisikia sauti nyingine ikinijibu kwa kutokea ndani mimi nikiwa bado nimesimama mlangoni.
Badala ya kutoka nje niliingia ndani na kulifunga geti mimi nikiwa ndani sikujali ile sauti iliyotoka ndani.

"Mimi ndiyo ninastahili kufanyiwa hivyo?" nilifoka sana. Moyo wangu kama ulikufa ganzi sasa. Sikuona sababu wala faida ya kuendelea kuishi duniani.

Faida yake nini? Mbona kila kukicha ni presha tu. Hakuna siku hata moja ambayo niliwahi kuona nitafika kesho. Ni Mungu mwenyewe tu.

"Nyamaza," ile sauti iliniambia.
Ilikuwa ni sauti ya mwanamke. Lakini kwa kusikiliza kwa mbali ilifanana na ya yule bibi mwenye nyumba wangu.
"Sinyamazi," nilijibu kwa ule ule ujasiri wa mwanzo.

"Tutakuonesha wewe na sisi nani zaidi?" hilo lilijirudia akilini mwangu.
Neno "tuta" na neno "sisi" yalimaanisha ni zaidi ya mmoja.
Ghafla! Woga uliniingia nikafungua geti na kutoka nje.

Halafu kule nje pia sikukaa, nilikwenda mpaka barabarani na kujikuta nazungukazunguka bila ya kufanya kitu cha maana. Niliingia duka la kwanza. Nikaenda duka la pili, la tatu. Mwisho nikajikuta niko kwenye magenge ya akina mama ntilie.
Lakini pia sikuwa na la kufanya nikarudi kazini kwangu.

Nilipofika nikaanza kutoa zana za kazi. Nilitoa zote lakini huku mapigo ya moyo yakienda mbio, sababu hasa ni kwamba nilihisi wale wateja au wafiwa wangefika tena kulitaka jeneza lao. Tukio kama hilo liliwahi kunitokea siku za nyuma. Wapo wanajeshi walifanya hivyo. Waliacha jeneza lao wakati walisema wangekuja kulifuata siku hiyo hiyo.

Ili kuwasaidia nililiacha nje wakati naondoka kurudi nyumbani. Nilimwachia maagizo yule mama jirani. Lakini kesho yake wakadai hawakutokea lakini cha ajabu jeneza nalo halikuwepo.

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 96.

Baadaye walipokuja wenyewe na kuingia ndani lilikuwepo wakalichukua.
Wakati nawaza hivyo yule mama jirani alitokea akiwa ameshika gazeti. Nilihisi kuna kitu kipo kwenye gazeti sasa anakuja kunionesha lakini haikuwa hivyo.
"Za muda huu?" aliniambia. Nikajua anakuja kuchukua majibu niliyomwahidi kwamba nitampa.

"Enhe? Walikuja kwako wale watu?" aliniuliza, uso wake ukionekana kuwa na shauku sana.
"Walikuja, nikaja nao kuwapa jeneza lao," nilimjibu.

Niliposema tu walikuja yule mama alionekana kushtuka kitu. Lakini akajipotezea ghafla!
Labda baada ya kujua ningehisi kitu kutoka kwake.
"Kwani wanapafahamu nyumbani kwako?" aliniuliza.

"Wao walipokwambia wanakuja kwangu walikujibuje?" nilimuuliza badala ya kumjibu.
"Walisema wanapajua."

Nikiwa naendelea kuwaza niendelee kumjibuje yule mama, ghafla kuna wazo lilinijia. Kwamba usiku uliotangulia yule mwanamke aliyeniingilia chumbani kwangu alikuwa na kovu la jeraha lililopona juu ya mguu wake. Nikapata wazo nimwangalie yule mama jirani, huenda ningepata ukweli zaidi.

Nilipoteremsha macho nilikumbana na raba. Miguu yote alivaa raba nyeusi. Wakati hata siku moja mimi sijawahi kumwona amevaa raba, ndiyo siku hiyo.

"Mbona unaniangalia miguuni?" aliniuliza.
"Kuna kitu nataka kuhakikisha kwako," nilimjibu bila kuogopa huku nikimkazia macho.

"Kitu gani? Unafikiri miguu yangu ina makovu makovu?" aliniuliza huku akitabasamu. Niliogopa, nikashtuka.

"Unashtuka nini?" aliniuliza.
"Sijashtuka," nilimjibu.
"Umeshtuka," alisisitiza.
"Umeniangalia vibaya," nilimjibu.

"Nilikuangalia vizuri sana," alinihakikishia.
"Jamani habari za leo?" sauti ilisalimia kwa nyuma yangu. Niligeuka haraka sana ili kumwona mtu huyo aliyetusalimia,kwani sauti niliyoisikia ilionekana haikiwa ngeni masikioni mwangu.

Ni kweli kabisa walikuwa wale wateja wa jeneza. Walivaa vile vile kama walivyokuwa wamevaa jana yake, wengine kanzu wengine kawaida.

Je nini kitaendelea?
Tukutane kesho kwenye muendelezo...
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom