Waziri wa Ujenzi, Miundombinu na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa.
Asilimia 90 ya malalamiko ya bidhaa zilizo chini ya kiwango yanayopokelewa Tume ya Ushindani wa Haki (FCC) yanahusu simu.
Haya yanabainika wakati serikali ikisisitiza kuzifungia simu bandia ifikapo Juni 17, mwaka huu.
Mkuu wa Idara ya Elimu kwa Mlaji kutoka FCC, Magdalena Utouh, aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati wa mafunzo ya Siku ya Haki za Watumiaji wa Huduma Ulimwenguni.
Katika mada yake iliyozungumzia bidhaa bandia na usimamizi wa haki, Utouh alisema bidhaa bandia zimeshamiri na miongoni mwa malalamiko wanayopokea ni ya simu.
“Malalamiko mengine tunayopokea ni ya vifaa vya ujenzi, umeme, kieletroniki, betri, losheni, vipuri, vibiriti, dawa za viatu, dawa za meno na sabuni za kuogea,” alisema.
Alisema bidhaa bandia hufifisha ushindani na humdanganya mlaji kuwa ni halali wakati siyo kweli.
“Wafanyabiashara wanatakiwa kutambua, kukopi bidhaa ya mtu mwingine ni wizi, wewe ni mwizi kama wengine, uwapo wa bidhaa bandia unaleta madhara katika uchumi wa nchi kwa sababu watu hawa hukwepa kodi au wakizilipa huwa kwa kiwango kidogo kutokana na kudanganya,” alisema.
Aliongeza kuwa watu hao wamekuwa hawawajibiki na athari za mlaji hivyo humtwisha mzigo mmiliki halali wa bidhaa husika.
“Madhara mengine kiuchumi ni kuwaogopesha au kuwatorosha wawekezaji wapya, lakini bidhaa hizi muda wake ni mfupi sokoni kwa sababu hawatengenezi za kukaa muda mrefu,” alisema.
Aidha, aliwasisitizia walaji wakati wote wanaponunua bidhaa kudai risiti ambazo ndizo zitakazowawezesha kisheria kupambana na bidhaa bandia.
Waziri wa Ujenzi, Miundombinu na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alisema watazifungia simu hizo lengo likiwa ni kujenga taifa lenye kuthamini ubora wa bidhaa.
Profesa Mbarawa katika taarifa yake iliyosomwa kwa niaba yake na Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Maria Sasabo, aliwataka wananchi kuunga mkono juhudi hizo za serikali.
Kuhusu watumiaji wenye mahitaji muhimu, alisema Mamkala ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imeandaa mwongozo kwa ajili ya kuhimiza matumizi ya huduma za Tehama na kutaka ukabiliane na changamoto za watumiaji wenye ulemavu na mahitaji maalum.
Alisema lengo ni kuwawezesha kutumia huduma kikamilifu na mwongozo uwe na vipengele vya kuwataka watoe huduma kuwa na mipango maalum kwao.
Aidha, alisema matumizi ya simu za mkononi na ujumbe mfupi umeongezeka ndani ya miezi mitatu mwaka jana ambapo Oktoba ulikuwa dakika bilioni 3.9 na Desemba zilifikia dakika bilioni 4.1.
“Meseji zilizotumwa kupitia simu za mkononi mwaka jana zimeongezeka kutoka bilioni 3.8 Oktoba hadi bilioni 4.4 Desemba, wastani wa idadi ya dakika ambazo mtumiaji mmoja mmoja alitumiwa katika kipindi hicho imeongezeka kutoka dakika 101 na kufikia 104,” alisema.
Alisema asilimia 94 wanatumia huduma ya intaneti.
Pia alisema idadi ya laini za simu za mkononi iliongezeka kutoka 2,963,737 na kufikia 39, 808,419.
Aidha, alisema matumizi ya king’amuzi vinavyowezesha kuonekana kwa matangazo ya digitali, yameongezeka kutoka 832,427 na kufikia 1,032,177 mwaka 2013.
Alisema licha ya serikali kuwa na jukumu la kuwalinda wananchi katika huduma za mawasiliano, watumiaji wengi hawana uelewa na elimu ya kutosha na hutegemea maelezo ya watoa huduma.
Aliongeza kuwa watumiaji hawajajipanga na hawana umoja hivyo ni rahisi kurubuniwa na watoa huduma.
“ Baadhi ya wadau kwenye sekta hii kama vile wauzaji na wasambazaji wa simu na vifaa vya mawasiliano na ambao wanasimamiawa na zaidi ya taasisi moja wanaweza kuingiza bidhaa ambazo zinaathiri watumiaji, nawataka wafuate masharti ya leseni zao,” alisema.
Aliongeza kuwa hivi sasa kuna tatizo la baadhi ya wakala wa huduma kuuza laini za simu bila kuzisajili au kuzisajili kwa majina bandia.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Ally Simba, alisema tathmini ya kampeni ya elimu kwa umma kuhusu mfumo wa Rajisi Kuu ya namba tambulishi inaonyesha idadi ya sintofahamu imepungua ambapo Desemba ilikuwa asilimia 38 na Februari imefikia asilimia 18.
Alisema mfumo huo utasaidia kupunguza matukio ya wizi wa simu na hata kama zitaibiwa hazitauzika popote.
Kaimu Mkurugenzi Mawasiliano na Uhusiano Vodacom, Rosalynn Mworia, alitoa rai kwa watumiaji wa simu kutosubiri mpaka simu zao zizimwe badala yake waziangalie mapema ili wazibadilishe.
Mwenyekiti wa Wasioona Wilaya ya Ilala, Alhaj Madebe, alitoa wito kwa TCRA kusajili simu ambazo zitawawezesha wao kusoma ujumbe mfupi.
Chanzo: Nipashe