Mtambuzi
Platinum Member
- Oct 29, 2008
- 8,810
- 15,398
Wiki kadhaa zilizopita kwa bahati mbaya au kwa kusudi, mke wangu alifungua ujumbe ulio kwenye simu yangu. Aliposoma alikutana na ujumbe wenye neno Dear. Bila shaka neno hilo likiwa limeandikwa na mwanamke, lilimfanya kuuliza maana ya neno lile. Hakujali ujumbe ulisema kitu gani, bali alijali neno Dear. Kidogo lilitutikisa. Lakini mambo yaliisha.
Lakini walisema muonja asali haonji mara moja. Nadhani aliona kusoma ujumbe unaotumwa kwenye simu yangu kunamfanya apate nguvu au kuthibitisha anachotaka kuthibitisha, Siku nyingine tena kwa kile kinachoitwa bahati mbaya, alisoma tena ujumbe kwenye simu yangu.
Ujumbe huu sasa ulikuwa na neno Darling, sio Dear tena. Pamoja na neno hilo kulikuwa na maneno yenye kuonesha kwamba, aliyeniandikia anataka tuwe wapenzi na tushiriki tendo na kwamba, angependa anipeleke mahali kwa siku mbili na nisije nikaanza kumkumbuka mke wangu.
Kwa kweli nadhani ujumbe huu na hasa neno Darling, ulimvunja nguvu mke wangu kiasi kwamba, alilia kwa muda mrefu wa usiku. Nilihuzunika kwa hilo. Lakini nilijiambia na kujiuliza, alikuwa na haki gani kukagua ujumbe kwenye simu yangu? Ukweli ni kwamba, simu ni yangu na watu ninao wasiliana nao , nawajua mimi na najua ni kwa nini nawasiliana nao kwa namna fulani. Yeye akisoma ujumbe wa aina yoyote, atafanya majumuisho yake na sio ya hali halisi.
Kwa mfano, mwanamke huyu ambaye, mke wangu alisoma ujumbe wake alianza kuniita Darling, baada ya siku moja kimzaha kuniuliza, ningependa kuitwa nani na yeye, bosi, mheshimiwa, baba fulani, au jina langu. Nilimuuliza, mbona umesahau kutaja neno Darling? Kwa utani, kuanzia siku hapo akawa ananiita Darling.
Ujumbe aliousoma mke wangu, ulikuwa ni utani, ambapo alikuwa anasema, akija kunitembelea atanipeleka mahali na kwa sababu mimi najifanya naaminika, nimwombe mke wangu ruhusa ya siku mbili kwamba naenda semina. Tulijibizana kwa muda mrefu kwa ujumbe katika mzaha kama tulivyokuwa tumezoea.
Bila shaka kila mmoja kati yetu alikuwa huru, kwani kila mmoja alijua kuwa anachokifanya ni mzaha. Lakini hata kama mtu mwingine angetulia, ujumbe ule ulikuwa unaonesha utani wa wazi kabisa. Lakini kwa mke wangu ingekuwa vigumu kuona mzaha ndani ya ujumbe ule. Siyo kwake tu, bali hata kwako na kwa mwingine, ingekuwa hivyo. Kwa nini?
Hapa ndipo panawaumiza wengi kwenye suala la ujumbe kwenye simu. Hadi mtu achukue simu ya mpenzi wake na kuanza kukagua ujumbe uliotumwa humo au majina ya watu walio kwenye orodha ndani ya simu hiyo, ni lazima ana wasiwasi na mwenzake. Kwa sababu ya wasi wasi huo, chochote atakachokiona ambacho kinaonesha dalili za kukosa uaminifu, hatatumia akili kukipima, bali ataendeshwa na mihemko.
Kuna mazingira mengi ambapo mtu anaweza kuamini kabisa kwamba, mwenzake anatoka nje. Hata anapowasimulia wenzake nao watampambisha moto kwa kumwambia, haiwezekani, ni lazima wana uhusiano, wakati hakuna jambo kama hilo. Tunaona sana mambo haya kwenye sinema zinazooneshwa kwenye televisheni zetu.
Nikipi kinasema kweli, ni tabia ya mtu kama tunavyoijua au ujumbe tuliouona kwenye simu? Nafikiri kuwa unamjua vipi mume au mke wako, ndilo jambo la msingi kwanza. Kama humwamini, ni lazima utapata mazingira ya kuthibitisha wasiwasi wako. Utachakura kwenye simu yake, utapekua mkoba wake, utakagua mifuko ya nguo zake na hata diary yake utaikagua kila wakati. Kwa sababu lengo ni kuthibitisha kwamba siyo mwaminifu, ni lazima utathibitisha.
Kushindwa kujua kwamba, simu kila mmoja ni yake na yaliyomo ndani ya simu ni yake na yeye ndiye mwenye kujua maana yake, hilo huwaumiza wengi. Niliwahi kupokea ujumbe kwenye simu ambao unasema, kumbe umeshikwa na mkeo, wewe mpumbavu kweli. Kumbe umekuwa unapoteza bure muda wangu. Kabla sijakaa sawa, nikatumiwa ujumbe mwingine na mtu huyo huyo akisema, Kama unaona vipi tuachie hapahapa kabla hatujafika mbali, tusije kuumizana bure.
Ilibidi nimpigie simu huyo aliyetuma ujumbe huo. Nilipomwambia kwamba huenda amekosea namba , alikiri. Lakini alisema kuna mtu ameanza kufanya naye biashara na amegundua kuwa kila kitu ni hadi mke wa huyo jamaa aamue. Hivyo ameamua kumwonya, kwani kwa sababu hiyo tayari wameshapata hasara.
Je mke wa huyo jamaa angeuona ujumbe ule kwenye simu ya mumewe angeelewa hivyo? Sio rahisi, angeelewa kwamba huyo mwanamke ni hawara wa mumewe na anataka wavunje uhusiano kwa sababu hampi anachokitaka, yaani kuwa naye muda mwingi au wote.
Ubaya wa ujumbe ni kwamba huwezi kuzuia usiingie, tofauti na kupigiwa,ambapo unaweza kukata simu au unaweza kuacha mtu azungumze wakati simu umeiweka mbali. Hapo hakuna ushahidi unaoachwa, Ujumbe huacha ushahidi ambao ni dhaifu sana, hata hivyo. Kama nilivyosema awali, kuna kuvunjika kwa ndoa kwingi sana, kutokana na simu za mkononi.
Lakini bahati mbaya ni kwamba, kuna kuuana au kujiua au kuuawa ambapo chanzo ni simu za mkononi. Ni kwa nini binadamu awe kipofu kirahisi kiasi hicho?Kwa nini simu ndio imfundishe kuhusu mwenzake, badala ya mwenyewe kumjua mwenzake?