SoC01 Simu imekuwa kama Nyoka kwenye Mahusiano, Mapenzi na Urafiki. Sumu yake ni hatari sana

Stories of Change - 2021 Competition

TheDealer

JF-Expert Member
Nov 19, 2012
2,424
1,129
Wana JF, salaam nyingi.


SUMU YA SIMU NA SUMU YA NYOKA:

“Naongea na simu”.

Siku hizi simu zinatoa sumu kali sana, hadi kuua zinaua. Hebu tulia kidogo, kisha fananisha kidogo simu yako na nyoka. Vipi, simu yako mara ya mwisho kutoa sumu ni lini?

Nyoka asipotoa sumu hana madhara, lakini akitoa sumu itakayompata mtu basi anakuwa na madhara yawe madogo ama makubwa. Simu nayo isipotoa sumu haina madhara, lakini ikitoa sumu inakuwa na madhara iwe kwenye mahusiano, mapenzi ama urafiki. Madhara yanaweza kuwa makubwa ama madogo sawa na sumu ya nyoka.

Mara nyingine unaweza kujikuta umelala na nyoka ndani tena kitandani, lakini maadam nyoka huyo hajatoa sumu ya kumdhuru mtu basi nyoka huyo hana madhara.

Kuna kampuni zingine wanatumia nyoka kuingiza kipato hata kodi wanalipa, na zaidi huajiri na watu wengine pia.

Kwa maneno mafupi sana, nyoka ana madhara akitoa sumu lakini asipotoa sumu hana madhara bali ana faida. Sumu hiyo ikiwa imempata mtu huweza kumuadhiri na pengine kumuua kabisa.

Kama ilivyo kwa nyoka mtoa sumu hivyo ndivyo ilivyo kwa simu itoayo sumu.

Kwa miaka ya hivi karibu kumekuwa na matumizi makubwa sana ya simu. Lengo kuu la simu ni kwa ajili ya mawasiliano baina ya mtu na mtu ama watu na watu.

Kwa msaada mkubwa wa intaneti simu imeweza kutumika kwa manufaa mapana sana kiuchumi, kiafya, kijamii, kidini, kisiasa na kwa namna mbali mbali.

Kwa mfano, simu inatumika kufanya kazi za ki benki, simu inatumika kufanya kazi za ki usalama, simu inatumika kufundishia, simu inatumika kujisomea, simu inatumika kuelimisha, na kadhalika. Nina uhakika mtu asiye na simu hujihisi mnyonge na kuna kitu cha muhimu sana atahisi kapungukiwa. Kwa ujumla simu ni nzuri sana kwa ustawi wa maisha ya watu, lakini ikitoa sumu ni hatari sana sawa na nyoka aliye na sumu atoapo sumu yake.

SASA NAJUAJE SIMU INATOA SUMU?

Sumu ya simu inaanza kutoka pale simu inapoanza kutoa ujumbe wa kusaidia katika kufarakanisha watu, kugombanisha watu, kutenganisha watu, kutisha watu, kuogopesha watu, kulumbanisha watu, kunyima haki watu, kupora watu, kuua watu, kuvunja udugu, kuua urafiki, kuvunja mahusiano, kuua mapenzi na mengine mengi yanayofanana na haya.

Kwa ujumla sumu ya simu inaanza kutoka pale ambapo kinachoendelea kwenye simu hiyo ni angamizo kwa mtu mwingine, ama ni mfadhaiko kwa mtu mwingine kwa namna moja ama nyingine.

Nina uhakika kwenye maisha yetu ya kila siku ya kimahusiano, ya kimapenzi ama ya kirafiki tumewahi kupigwa na sumu ya simu. Wengine hadi wameponea chupu chupu kupoteza uhai wao.

Simu ina namna nyingi sana ya kutoa sumu yake. Lakini ki vyovyote vile sumu ya simu haijawahi kuwa salama. Angalia kwa mfano:
  • Sumu ya simu imeua mahusiano machanga na hata yaliyodumu kwa muda mrefu, imeua mapenzi, imeua urafiki wa watu wengi sana
  • Sumu ya simu inawafukuzisha watu kazi kwa namna mbali mbali
  • Sumu ya simu inazalisha watoto wa mtaani kwa namna mbali mbali kila kukicha. Wapendanao hutengana, hufarakana na hata kuuana.
  • Sumu ya simu inazalisha watoto yatima kwa namna nyingi sana
  • Sumu ya simu imefanya malezi ya watoto kuwa magumu. Watu wapo karibu zaidi na simu zao kuliko na watoto wao.
  • Sumu ya simu imefanya jamii kupotoshwa mara kwa mara kuhusu masuala mbali mbali yanayojiri kwenye Duniani
  • Sumu ya simu imewafanya watu kutapeli na kutapeliwa
  • Sumu ya simu inazalisha wajane na wagane kwa namna tofauti tofauti kwa wivu wa kimapenzi
  • Sumu ya simu imewafilisi watu kiuchumi kwa namna nyingi sana
  • Sumu ya simu inasababisha ajali mbali mbali barabarani na maeneo mbali mbali ya kazi
Hatuwezi kumaliza mifano ya sumu ya simu. Lakini, kubwa kuliko ni kwamba sumu ya simu inaua mahusiano, inaua mapenzi, inaua urafiki, inaua uchumi, inaua imani, inaua afya, inaua ndoa za wapendanao kwa namna mbali mbali kila kukicha.

Kufa kwa mahusiano, kufa kwa mapenzi na kufa kwa urafiki huleta mfadhaiko mkubwa sana na pengine huleta angamizo kwa jamii pana ya watu kiuchumi, kisiasa na hata kiimani. Simu ikitoa sumu ni hatari zaidi ya hatari yenyewe.

Ni ndoa ngapi kwa muda huu tunaposoma uzi huu yanapumulia oksijeni kwa sababu ya sumu ya simu?

Ni watu wangapi wanalaani sumu ya simu kwa kuwavunjia mahusiano yao, mapenzi yao ama urafiki wao?

Ni watu wangapi kwa muda huu ajira zao zipo mashakani kwa sababu ya sumu ya simu?

Watu husema watu wa zamani walikuwa wanadumu sana kwenye mahusiano. Ni kweli. Lakini nina uhakika pia kuwa kama kipindi hicho kungekuwa na matumizi makubwa ya simu kama ilivyo sasa nadhali hali ingekuwa tofauti kidogo.

Wewe unayesoma uzi huu:

Je, sumu ya simu imewahi kukuacha salama ?

Je, sumu ya simu imemuacha salama jirani yako ?

Je, sumu ya simu imemuacha salama ndugu yako ?

Je, sumu ya simu imemuacha salama nani unayemfahamu?

Tujuzane.

SULUHU NI NINI?

Bahati nzuri ni kwamba, si ngumu kubaini kuwa sasa simu yako inatoa sumu. Ni rahisi sana kubaini, sawa na ilivyo rahisi kubaini kuwa sasa una njaa na hata kiu hivyo kuhitajika kula ama kunywa maji.

Pindi utakapobaini kuwa simu yako inatoa sumu basi acha mara moja kutumia simu yako kutoa sumu, badala yake tumia simu yako kuboresha zaidi maisha yako na ya wapendwa wako.

Usikubali simu yako itoe sumu ya kugombanisha, usikubali simu yako itoe sumu ya kutapeli, usikubali simu yako itoe sumu ya kuvunja ndoa za wengine, usikubali simu yako itoe sumu ya kuharibu mahusiano na mapenzi ya watu wengine. Usikubali simu yako itoe sumu ya namna yeyote ile, bali tumia simu yako kwa ajili ya ujenzi bora wa maisha yako na wapendwa wako.

TheDealer.
 
TheDealer dah umepiga mwingi sana pale kati.

Simu imevunja mahusiano mengi haswa.

Wengine hadi wanachoma wapenzi wao moto mbali na wale wanaochoma visu.

Kinacho trend sasa hv ni mwamba kuchomwa moto kisa wivu wa mapenzi. Bila shaka simu itakuwa imehusika hapo kumwaga sumu yake.

Kudos bro' endelea kupambana.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom