Simiyu: Ng'ombe zaidi ya 1484 wadaiwa kufa mikononi mwa Maafisa wa Pori, huku wengine wakiuzwa kwa Shilingi laki moja

Suley2019

JF-Expert Member
Oct 7, 2019
1,813
4,545
Zaidi ya ng’ombe 1, 400 wa wafugaji wa Wilaya za Itilima na Meatu mkoani Simiyu wamekufa mikononi mwa Maafisa wa Pori la Akiba la Maswa baada ya kushikiliwa hifadhini kwa kipindi cha miaka mitatu bila kupatiwa huduma muhimu za chanjo, dawa, maji na malisho licha ya Mahakama kutoa hukumu kwa wamiliki kurejeshewa mifugo yao.

Wafugaji hao wamesema tangu mwaka 2017 ng’ombe 1, 484 walikamatwa kwa madai kuwa walikuwa ndani ya pori hilo na kwamba licha Mahakama kuamuru warudishiwe ng’ombe wao bado waliendelea kushikiliwa na kuendelea kufa na kubaki 72 na kuwasababishia umasikini mkubwa.

Wafugaji hao walifikisha kilio hicho kwenye mikutano wa hadhara ilioitishwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina aliyefika katika vijiji vya Laini A na Laini B wilayani Itilima, Mwangudo na Malwilo Wilayani Meatu mkoani Simiyu ambapo walisema licha ya Mahakama kutoa uamuzi wafugaji hao warejeshewe mifugo bado hawajarudishiwa mifugo yao hadi sasa na kwamba inadaiwa kuwa mifugo hiyo imekufa.

Baadhi ya Wamiliki wa mifugo hiyo ni walioshinda kesi kwa upande wa Itilima ni Malimi Sendama, Ngasa Mbeho, Kongwa Tulutu na Maduhu Mbuli ambapo walimkabidhi Waziri Mpina risiti mbalimbali zinazoonesha mifugo hiyo kuuzwa kwa bei ya kutupa huku ngombe anayetakiwa kuuzwa laki 4 hadi 5 akiuzwa sh laki 1.

Wafugaji wengine kwa upande wa Meatu waliodhulumiwa ng’ombe 345 ni Subi Maduhu, Masunga Muhamali, Zengo Kusekelwa, Kija Badila ambapo mifugo yao inadaiwa kufa huku mfugaji mwingine akidai ngombe wake 55 ambao Mahakama iliamuru alipe faini ya shilingi milioni 1.4 ili arudishiwe mifugo yake na alilipa faini hiyo lakini mifugo yake haijarudishwa hadi sasa.

Akiwasilisha kilio kwa niaba ya wafugaji hao, Katibu wa Mbunge wa Itilima, Alex Ngulukulu alisema wahifadhi hao walitoa maelezo kuwa ng’ombe 289 wamekufa jambo ambalo sio la kweli kwani askari wa hifadhi walikuwa wanaendesha minada ya kuuza mifugo hiyo.

“Ng’ombe walikuwa wanauzwa kwenye minada wakati kesi ikiendelea mahakamani na tuna ushahidi wa kutosha wa risiti zote walizokuwa wanatoa kwa wanunuzi wa mifugo hiyo” alisema Alex.

Diwani wa Kata ya Tindabuligi, Tabu Maghembe alisema maelezo yaliyotolewa kwamba mifugo hiyo imekufa hawakubaliani nayo kwani hakuna mlipuko wowote wa magonjwa ulioripotiwa katika kipindi hicho na hivyo kumuomba Waziri Mpina kufikisha kilio hicho cha wafugaji wa Itilima na Meatu kwa Rais Dk. John Pombe Magufuli ili aingile kati waweze kupata haki yao kwani kwa muda mrefu amekuwa akipigania haki za wanyonge.

Mbali na malalamiko hayo pia wafugaji hao walilalamikia kitendo Maofisa wa Pori la Akiba Maswa kutanua mpaka bila kuwashirikisha wananchi na hivyo kuendelea kupunguza eneo la malisho na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wafugaji. Pia wananchi wa Wilaya za Wilaya za Maswa na Meatu wamelalamikia mgogoro wa mpaka katika Ziwa Kitangiri na kwamba wamekuwa wakizuiliwa kuvua na kukamatwa kwamba wameingia wilaya ya Iramba Mkoa wa Singida.

Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Juma Mpina amshukuru Rais Dk. John Magufuli kwa kuruhusu matumizi ya mita 500 kutoka kwenye Pori la Akiba la Maswa yatumike kwa shughuli za kulishia mifugo sambamba na kuruhusu matumizi ya mita 60 kutoka kwenye mto kutumika kwa shughuli za akunyesha maji mifugo yao jambo ambalo hapo kabla wananchi walikuwa wakizuiliwa na kusababisha mifugo mingi kufa kwa kukosa maji na malisho.

Akizungumza baada ya malalamiko hayo Waziri Mpina aliwaagiza Wakuu wa Wilaya za Itilima na Meatu kuitisha kikao cha pamoja kitakacho mhusisha Mhifadhi Mkuu wa Pori la Maswa, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Tanzania na Mwanasheria wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wafugaji wanaolalamikia kudhulumiwa mifugo yao na kupitia vielelezo vyote vilivyotumika kukamata, kutunza na kuuza mifugo pamoja na kupitia hukumu ya Mahakama ili haki iweze kutendeka .

Pia ameagiza Kamishna wa Ardhi, Mkurugenzi wa Uvuvi Tanzania, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meatu na Mkurugenzi wa Iramba ili kupitia upya mipaka hiyo na kumaliza kabisa mgogoro huo kuhusu uvuvi katika Ziwa Kitangiri

Kuhusu suala la kutanua mpaka kiholela, Waziri Mpina

meagiza timu ya Wataalamu kutoka Wizara nane kupita kwenye maeneo yanayolalamikiwa na kupima upya mipaka hiyo kwa uwazi na kwamba wananchi watashiriki katika zoezi hilo. Aidha kuhusu upungufu wa maeneo ya malisho vijiji saba vinavyounda WMA ya Makao, Waziri Mpina aliagiza wafanye tathmini ya mahitaji ya ardhi ya wananchi kwa sasa na kuandaa GMP itakayoruhusu baadhi ya maeneo kutumika kwa ajili ya kulishia mifugo.

Hivyo Waziri Mpina ameagiza wafugaji wote mkoani Simiyu walioshinda kesi mahakamani na kutakiwa kurejeshewa mifugo yao kuwasilisha vielelezo vya hukumu za kesi hizo kwenye ofisi za Wakuu wa Wilaya za Itilima na Meatu ili haki iweze kutendeka. Mbali na hayo Serikali imetenga zaidi ya shilingi milioni 400 kwa ajili ya kuangamiza wadudu aina ya mbung’o katika vijiji vyote vinavyopakana na WMA Makao na maeneo mengine nchini ili kutokomeza kabisa mdudu huyo hatari kwa mifugo.
 
Back
Top Bottom