Simba SC 2 - 1 Yanga SC: Shiza Kichuya aibuka shujaa wa Simba

Na msimamo wa ligi mpaka sasa uko hivi

98ff51224bf5762899b1e806a03c259a.jpg
 
Hatimaye joto, tambo na majigambo ya nani mbabe kati ya mahasimu wa soka la Bongo Simba a.k.a mnyama, na Yanga limeshuka rasmi na hali hii ikiendana na hali ya hewa ya Dar es Salaam ambapo joto pia limeshuka. Wakati Wanamsimbazi wakifurahia baraka hii ya mvua na hewa safi, Wanajangwani wanajikuta wakihisi ubaridi mkubwa sio mwilini tu bali hata kihisia.

Kwa takribani miaka minne hivi iliyopita, Simba imekuwa ikionekana machoni pa wengi kama ‘second best’ kwa Yanga. Na hata pale ambapo ilijitutumua lakini sehemu kubwa ya wadau wa soka waliamini Yanga ni bora zaidi na changamoto pekee ilikuwa ni Azam.

Na hii haikuwa imani tu, bali takwimu pia zinathibitisha hilo. Yanga ilikuwa na kikosi ghali zaidi nchini, na benchi lililokamilika zaidi na huku Simba ikiwa na mabadiliko ya mara kwa mara kwa benchi na hata kikosi cha wachezaji. Hali hii imeifanya Yanga iwe imechukua mataji karibu yote makubwa ktk kipindi hiki ukiacha yale ya ngazi ya CAF. Kuanzia kombe la CECAFA, VPL, FA, na hata Ngao ya hisani huku pia ikiwakilisha nchi mfululizo ktk mashindano ya klabu barani Afrika. Simba wameishia kujifariji na Kombe la Mapinduzi na tuzo ya Mtani Jembe. Bila shaka yoyote, kitu ambacho hakiwezi kuvumilika tena na Wanamsimbazi.

Lakini mtanage wa juzi baina ya timu hizi na Simba kushinda umehitimisha rasmi ukaka-mkubwa wa Yanga wa miaka takribani minne na italazimika kufanya kazi ya ziada kuirudisha hadhi hii. Kwa taarifa yako, Simba imethibitisha ubabe wake kwa Yanga ktk mechi 3 mfululizo za hivi karibuni dhidi ya Yanga.

Pasina shaka wala wasiwasi wowote naweza kuitangaza Simba kama bingwa mtarajiwa wa Tanzania japo ligi haijaisha. Na sio hivyo tu Simba inazidi kuimarika na muda si mrefu itakuwa timu bora zaidi hapa Tanzania na ukanda huu wa Afrika.

Kutoa kauli na namna hii ni kujilipua kwa kiwango kikubwa lakini kwa mtu anayeweza kusoma alama za nyakati hawezi kupata shida kuelewa ninachokimaanisha. Zipo sababu na dalili kadhaa za kuonesha hilo ninalozungumzia.

Kama Yanga hawakuona au kushtuka kwa matokeo ya sare ya Oktoba 1, 2016 dhidi ya Simba pungufu, na kufungwa kwa penati katika kombe la Mapinduzi mapema mwaka huu 2017 mjini Zanzibar, basi ushindi mujarabu wa juzi wa Simba dhidi ya Yanga, ni hitimisho la kile nilichokuwa nikikiona kama mpambano wa kugombania ufalme wa soka katika ardhi ya Tanzania, na Yanga inapaswa kustuka!

Simba imefanikiwa kukusanya pointi 7 kati ya 12 ilizopaswa kuzinyakua toka kwa timu pinzani za uzito wake ambazo ni Yanga na Azam. Imechota 4 kwa Yanga na 3 kwa Azam, huku Yanga ikifanikiwa kuchukua pointi 2 tu hadi sasa kutoka Kwa Simba na Azam ambayo hawajarudiana nayo, na inaweza kufikisha pointi 5 au kubaki na hizi hizi 2. Yanga ana deni na Azam, ana deni na Mtibwa ugenini. Simba ana deni kanda ya Ziwa. Lakini Yanga haijaifunga Azam ktk VPL kwa takribani misimu mitatu, huku ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kucharazwa bakora 4 bila majibu na matajiri hao wa Chamazi, ktk kombe la Mapinduzi.

Vyovyote iwavyo Simba inaonekana inaenda kuwa mfalme mpya katika soka la Tanzania. Sababu ni nyingi lakini chache kati ya hizo ni;

1. UCHOVU WA YANGA

Moja, Yanga imechoka. Imechoka kimwili kutokana na ushiriki mfululizo wa makombe mbalimbali iliokuwa nao hasa kuanzia mwaka 2015. Tulisema tangu mwanzo Yanga watakumbana na tatizo la fatigue, lkn wanazi wa timu hii hawakuelewa! Viongozi hawakuelewa japo nataka kuamini makocha hasa Hans na Mwambuzi wanaelewa vzr.

Yanga wamechoka pia kisaikolojia, lkn pia uchovu mwingine ni wa sehemu kubwa ya kikosi kuundwa na wachezaji wenye umri mkubwa ambao hawana warithi au wasaidizi wazuri wa kuwacompliment!

Matokeo ya mkusanyiko wa uchovu wote huu ni kuumia-umia kwa wachezaji tegemezi kama Ngoma na Kamusoko ambaye habari za mitaani inasemekana chanzo cha kuumia kwake ni chenga kali aliyopigwa na Mohamed Ibrahimu ‘Mo” mwishoni mwa kipindi cha kwanza. Sina uhakika na hili lkn huwezi kupuuza kwa kuwa ilikuwa chenga ya ghafla na kali mno. Lakini pia uchovu umesababisha Yanga kushindwa kuhimili kasi ya Simba kipindi cha pili japo Simba walikuwa pungufu. Wastani wa umri wa wachezaji wa Simba ktk mechi ya juzi ilikuwa ni miaka 24 dhidi ya 29 ya wachezaji wa Yanga.


2. SIMBA INA SAIKOLOJIA YA KIBINGWA

Simba wana njaa ya ubingwa na uwakilishi wan nchi. Hamu hii ilionekana tangu mwanzo wa msimu. Wanazungumza lugha moja, kuanzia, viongozi, wachezaji na mashabiki. Kila mara unasikia Simba wakisema ‘we want to reclaim our lost glory’. Hiyo imetengeneza morali ya ushindi. Kitendo cha kutokukubali kufa kirahisi ktk mechi hizi mbili dhidi ya Yanga tena huku wakiwa pungufu na kucheza ktk mazingira yasiyorafiki kwao, ni kuonyesha ni morali ya aina gani waliyonayo wana msimbazi. Huoni njaa hii katika Yanga. Of course hata mazingira ya hivi karibuni kuelekea ktk mechi hiyo hayakuwa rafiki sana kwa Yanga. Madai ya malimbikizo ya mishahara, misukosuko ya Mwenyekiti wao Manji, habari za kudekadeka na Ngoma na Bosou na mambo ya namna hiyo yameongeza kitu katika hali ya udhaifu wa kisaikolojia uliokuwepo kabla na hali hii itaendelea kuila Yanga hadi mwisho wa msimu.

Lakini morali ya Simba imeendelea kuwa juu hata katika kipindi mambo yalikuwa yakiiendea kombo sio tu katika mechi bali ilipokuwa ikipoteza pointi muhimu. Hii ndio saikolojia ya kibingwa yaani cup winning mentality. Kuhimili mitikisiko no matter what.

Nilipata kumwambia rafiki yangu mmoja kuwa Simba atatwaa ubingwa kwa staili ya staa wa filamu za kihindi. Hii ilikuwa ni ktk kipindi Simba ilipoanza kudondosha pointi huku Yanga akitumia muda huo kukata gap. Staa wa movie yoyote na hasa za kihindi huonekana kuzidiwa sana hadi kufikia watazamaji kukata tamaa lakini ghafla huibuka na kushinda upinzani iwe ni ngumi, au kesi mahakamani. Simba ilifikia pointi mbaya na kilele kilikuwa walipopoteza mechi dhidi ya Azam

3. OMOG NA UDHIBITI WA KIUFUNDI

Kama kuna silaha kubwa waliyonayo Simba msimu huu ni uwepo wa kocha Joseph Omog. Kocha huyu mpole raia wa Cameroun ameonekana kuituliza Simba hasa ktk vyumba vya kubadilishia nguo. Ni dhahiri anaonekana kuwa na utawala wa kikosi bila kuwa misuguano mikubwa dhidi ya makomandoo na viongozi wa aina ya timu hizi wanaoshinikiza upangwaji wa kikosi wapendavyo wao. Omog pia ameonekana kuwa mzuri ktk kusoma mchezo na kufanya mabadiliko sahihi. Uwezo huu umeipatia Simba ushindi au sare za ‘usiku’ katika mechi nyingi muhimu. Pointi nne ilizopata Simba kutoka Yanga msimu huu ni kazi nzuri ya Omog.

Licha ya kufanya makosa kwa kukipanga kikosi vibaya ktk mwanzoni mwa mechi ya juzi, kwa ujumla Omog ameonesha uwezo mkubwa wa kufundisha, na kuituliza timu kipindi inapokuwa katika hali mbaya ya kimchezo. Mara mbili dhidi ya Yanga ameirudisha timu mchezoni huku ktk mchezo wa mzunguko wa kwanza akiwarudisha wachezaji uwanjani na mchezoni baada ya wote kuonekana kupaniki na goli la mkono la Tambwe na kadi nyekundu ya Mkude. Hakuna zawadi nzuri ambayo wachezaji waSimba wanaweza kuitoa kwa Omog zaidi ya ubingwa. Na nimesikia wamemwahidi hili.

Jackson Mayanja aliishindwa kazi hii mwaka jana baada ya kujikuta akiwa na malumbano na wachezaji wake waandamizi wakati msimu unaelekea ukingoni licha ya kushinda mechi 8 mfululizo kabla ya kupoteza udhibiti wa chumba cha kubadilishia nguo.

Kwa upande wa mkufunzi wa Yanga George Lwandamina, bado hajawa na utawala wa moja kwa moja. Kwanza, anafanya kazi chini ya kivuli cha mafanikio ya Hans de Pluim, huku pia akirithi matatizo yote yaliyoonekana tangu kipindi cha mtangulizi wake huyo. Mbaya zaidi ameanza kazi katikati ya msimu, ambalo ni kosa kubwa zaidi walilofanya viongozi wa Yanga.

Baadhi ya mashabiki wa Yanga walikuwa wakisema Hans amekwisha, uwezo wake umefikia kikomo, na leo pia hao hao wanadai George hafai. Bahati mbaya hawataji sababu za msingi za kisoka za kupepesuka kwa kikosi cha Yanga. Mvutano huu na kushikana uchawi huku kunakoendelea Jangwani ni habari njema sana kwa mabingwa watarajiwa!


4. SIMBA NI VIPAJI NA KAZI

Sahau yote yaliyotajwa hapo juu, kikosi cha sasa cha Simba kinaundwa na wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kucheza mpira. Ajibu, Mo Ibrahimu, Tshabalala na Kichuya ni wachezaji ambao kila mtu anatamani wawe na mpira muda mwingi. Wanakupatia mchanganyiko wa vionjo vya kipaji na umahiri wa kusakata soka. The boys are extremely talented kwa viwango vya soka la Kibongo. Upande wa pili ni Niyonzima pekee ndio anaweza kukupa wanachoweza kukupatia hawa binadamu.

Mkude, Kotei, na Muzamiri Yassin ni wachezaji viungo wenye kujituma, nguvu na uvumilivu (endurance) uwanjani kiasi kwamba wanaweza kucheza mechi kwa dkk hata 300 huku wakifika karibu kila eneo wanalopaswa kuwepo! Eneo la ulinzi chini ya kiongozi Method Mwanjale, Bokungu na kipa Daniel Agyei limethibtisha kuwa defense bora zaidi ktk ligi.

Eneo la ushambuliaji limekuwa likiacha maswali mengi lakini kiwango cha sasa cha Laudit Mavugo kimeanza kujibu baadhi ya maswali hayo. Kumeonekana muunganiko mzuri kwa siku za karibuni kati ya Mavugo, Ajibu na Juma Luizio japo alichemsha mechi ya watani juzi.

Unapokuwa na mseto wa wachezaji wa aina hii huku benchi ukiwa na silaha kama Mwinyi Kazimoto, Hamad Juma, Jamal Mnyate, Peter Manyika, Jjuuko Murshid, Pastory Athanas n.k unakuwa na kila sababu ya kushika utawala wa mpira wa nchi katika muda mfupi ujao.

Kama Simba itaendelea kuwa hvi ilivyo, huku sehemu kubwa kikosi hiki kikibaki hadi msimu ujao, basi timu nyingi zijiandae kucheza na Simba hata yenye watu 8 uwanjani lakini ikiwa na uhakika wa kuwa na takwimu nzuri zaidi za mchezo!!
 
Umenena vyema sana Mkuu.. Hakuna wa kutuzuia msimu huu.. labda wajaribu tena msimu ujao.
 
Jamaa we ni mkali kwa kuchambua.Yanga bila mbeleko hata hiyo nafasi ya pili wasingefika.Kama mpira ungekuwa unachezeshwa fair, Azam angekuwa nafasi ya pili.Laiti kama tungekuwa na waamzi kama Akrama, simba mpaka sasa angeshatangazwa bingwa.
 
Mkuu unatukana mamba wakati hujavuka mto, vuka kwanza kisha ndiyo uanze kutukana!
Hizi kauli nishazizoea.. Kama tangu mwaka jana, mlikua na hizi hizi porojo.. naamini zitaendelea hata baada ya mnyama kukabihiwa kombe lake.. Amini amini Simba SC ni bingwa wa VPL msimu wa 2016/2017.
 
Hizi kauli nishazizoea.. Kama tangu mwaka jana, mlikua na hizi hizi porojo.. naamini zitaendelea hata baada ya mnyama kukabihiwa kombe lake.. Amini amini Simba SC ni bingwa wa VPL msimu wa 2016/2017.
Mkuu kumbuka kuwa uhalisia ni tofauti na matakwa yako.

Sina shaka yoyote kwa upande wako ungependa kuona mnyama anachukua kombe na kwa upande wangu ningependa kuona Young Africans SC ikichukua kombe la 3 mfululizo!

Kiuhalisia chochote chaweza kutokea, jiandae kisaikolojia ili ''mang'ana gasalike'' yatakapotokea usije kuchanganyikiwa. Mimi nimejiandaa vizuri kisaikolojia na niko tayari kupokea uhalisia utakaotokea.
 
Mkuu kumbuka kuwa uhalisia ni tofauti na matakwa yako.

Sina shaka yoyote kwa upande wako ungependa kuona mnyama anachukua kombe na kwa upande wangu ningependa kuona Young Africans SC ikichukua kombe la 3 mfululizo!

Kiuhalisia chochote chaweza kutokea, jiandae kisaikolojia ili ''mang'ana gasalike'' yatakapotokea usije kuchanganyikiwa. Mimi nimejiandaa vizuri kisaikolojia na niko tayari kupokea uhalisia utakaotokea.

Haha.. Sawa Mkuu. Ila nakumbuka kipindi kile tunagawa dozi hovyo hovyo katika mzunguko wa kwanza mlikua mkisema hizi ni nguvu za soda.. Sasa tupo raundi ya 2 huku zimebaki mechi 7 ligi iishe mnyama akiwa kileleni.. bado mna wasi wasi nae?! sawa. Tukutane April.
 
Haha.. Sawa Mkuu. Ila nakumbuka kipindi kile tunagawa dozi hovyo hovyo katika mzunguko wa kwanza mlikua mkisema hizi ni nguvu za soda.. Sasa tupo raundi ya 2 huku zimebaki mechi 7 ligi iishe mnyama akiwa kileleni.. bado mna wasi wasi nae?! sawa. Tukutane April.
Hakuna noma Mkuu, endapo mtaendeleza ubabe huo hadi mwisho, haitakuwa shida kwa mtu kama Makoye Matale kupotea hapa jukwaani kwa kisingizio cha kuwa katika eneo korofi!;););)
 
Back
Top Bottom