“sikutaka kulisema hili, ila kwa kuwa unaonekana mkaidi, nitakueleza” | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

“sikutaka kulisema hili, ila kwa kuwa unaonekana mkaidi, nitakueleza”

Discussion in 'Mahusiano, mapenzi, urafiki' started by vukani, Jul 11, 2012.

 1. vukani

  vukani JF-Expert Member

  #1
  Jul 11, 2012
  Joined: Dec 30, 2009
  Messages: 245
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 35
  Alikuja pale kazini kama mteja, lakini hilo jicho, mwenzangu mpaka niliogopa, maana jicho lake liliniganda mpaka nikaona aibu, hata hivyo alipomaliza shughuli zake aliondoka na kuahidi kurudi eti kunipa lifti nikirudi nyumbani kwangu, nikamwambia kuwa mpenzi wangu atanifuata, hakuonekana kujali maneno yangu aliondoka na kusisitiza kurudi.Ilipofika jioni alirudi lakini nilimkwepa na kuondoka zangu nikimwacha ndani akiongea na Bosi wangu kwani alikuwa na mizigo yake na makontena Bandarini ambayo yalikuwa yanashughulikiwa na kampuni yetu kutolewa bandarini.

  Siku iliyofuata alifika pale ofisini na kuniahidi kunitoa lunch katika Hoteli ya Kitalii ya nyota tano pale Kilimanjaro, nilikataa ofa yake na alionekana kushangaa. Akaniambia kuwa hajawahi kukakataliwa kitu na mwanamke, mimi nitakuwa wa kwanza kumfanyia hivyo, sikumjali sana nilimpuuza.Baadae Bosi wangu alianza kumsifia yule mzee kuwa ni tajiri ambaye anafanya biashara katika nchi za afrika na mashariki na kati aki-supply bidhaa mbalimbali katika nchi hizo. Bosi wangu aliendelea kusema kuwa toka ameanza kufanya kazi na yeye kampuni imeingiza faida kubwa sana na kuna matarajio mazuri mwakani.

  Ilipofika mchana alikuja kijana mmoja akauliza kama anataka kumuona Gift (*sio jina lake halisi) nikamwambia kuwa ni mimi, akatoa bahasha na kunikabidhi, nilipomuuliza kama imetoka wapi akanijibu kwa kifupi tu kuwa imetoka kwa mzee, kisha akaondoka zake.Niliifungua kwa kiherehere ili kujua ina kitu gani, ndani ya bahasha ile nilkutana na kidani cha dhahabu cha Gram 10 na shilingi laki mbili, na ujumbe unaosema,

  "Samahani sana Gift, nilikuahidi kukutoa lunch leo, lakini niko na kikao wizarani, nimeshindwa kutekeleza ahadi yangu, lakini hapajaharibika kitu, hiyo cheni, nilikununulia ili nikupe kama zawadi wakati wa lunch yetu, lakini kutokana na dharura hiyo, basi pokea zawadi yangu hiyo kama ishara ya upendo nilionao kwako na hizo fedha ndio nilikuwa nimeandaa kwa ajili ya hiyo lunch yetu, unaweza kuzitumia kwa kununua kitu chochote ukipendacho."


  Nilishusha pumzi nikabaki nimeduwaa, kisha nikafyonya kwa dharau, na kuitupia ile bahasha kwenye droo ya mezani kwangu.
  Jioni boy friend wangu akanifuata tukaondoka kuelekea kituoni kupanda daladala kurudi nyumbani. Kiukweli Boy friend wangu alikuwa hana kazi bali alikuwa akibangaiza kwenye ofisi ya jamaa yake fulani baada ya kumaliza masomo yake ya Information Technology. Akiwa amesoma ngazi ya Diploma.Nilikuwa na mchanganyiko wa mawazo na kutokana na mawazo hayo nilijikuta nikiwa mbali sana kiasi cha kutosikia yale aliyokuwa akiyasema Boy friend wangu, kuna wakati ilibidi anishtue kwa kuniuliza kama nimemuelewa alichokisema nilimjibu tu ndio lakini kiukweli sikumuelewa kabisa kuwa alikuwa anaongea nini.

  Tulipofika Sinza ambapo ndipo ninapoishi tulishuka na kuelekea kwangu lakini karibu na nyumbani tulipisha na gari moja aina ya RAV 4, ilikuwa ikiendeshwa na kijana ninayemfahamu, alinipigia honi na kunipungia mkono, nami nilimpungia mkono. Mpenzi wangu alionekana kutofurahia kile kitendo kwani tulipofika tu nyumbani maswali yakaaza. Yule ni nani? mmejuana lini? ana uhusiano gani na wewe, mbona simfahamu? yalikuwa ni maswali mengi mfululizo ambayo sikuweza kuyajibu yote.Tatizo la mpenzi wangu ni wivu, yaani alikuwa na wivu utadhani dume la njiwa.

  Kama masihara ulizuka mzozo wa maneno kati yangu na mpenzi wangu kiasi cha kufikia kunipiga, na kisha akaondoka zake. Niliwaza sana, kwa kweli sikuwa na uhusiano na yule kijana na nilimfahamu kupitia kwa shoga yangu anayemiliki saluni ambapo ndipo ninapotengenezea nywele na yule kijana ni boy friend wake.
  Nililia sana na sikuweza hata kula usiku ule nikalala na njaa. Kesho yake nikiwa ofisini yule mzee alifika tena lakini safari hii hakukaa hata kidogo, alionekana kuwa bize sana, Ilipofika mchana Boyfriend wangu alinipigia simu lakini sikupokea, alitumia simu ya mtu mwingine kunipigia, lakini nilipopokea na kusikia sauti yake nilikata ile simu alinitumia ujumbe wa simu akiniomba radhi lakini sikumjibu, nilichukizwa sana na kitendo chake cha kunipiga siku ile.

  Ilipofika jioni yule mzee akaja kunipitia pale ofisini akiwa na gari lake aina ya Toyota GX, niliamua kuondoka naye kwani alinibembeleza sana anipeleke kwangu, wakati tunaondoka nilimuona boy friend wangu akija kunifuata, nilitaka kumuomba yule mzee anishushe lakini nilisita. Yule mzee ambaye ki umri alionekana kuwa sawa na baba yangu alinifikisha nyumbani kwangu, lakini hakushuka kwenye gari, alinipa bahasha nyingine akaniambia ni zawadi yangu, nilipoingia ndani na kuifungua nilikuta dola mia mia kumi, nilishikwa butwaa.......

  Huyu mzee anataka nini kwangu, hivi anadhani mimi ni wa kutembea na vizee, niliwaza.
  Nilishtuliwa na mtu akibisha mlangoni kwangu, nilikwenda kufungua mlango, alikuwa ni mpenzi wangu, nilishtuka sana, aliingia ndani huku akiwa amefura kwa hasira, "niliwaona sana na leo utanieleza" lilikuwa ndio neno lake la kwanza alipoingia ndani, alipitiliza hadi chumbani kwangu na zile dola zilikuwa bado ziko kitandani, nilimfuata kwa nyuma, alipoziona tu akazichukua zote.Sasa nenda kamwambie nimezichukua na akome kutembea na wachumba za watu. aliniambia huku akizitia zile dola mfukoni,

  Nilijikuta nikipandwa na hasira, "Safari hii sikubali" nilijisemea moyoni, nilimrukia na kuanguka nae kitandani niliingiza mkono wangu kwenye mfuko wake alipoweka zile dola na kuzichoimoa, na yeye aliukunja mkono wangu kiasi cha kutaka kuuvunja, niliziachia zile dola zikatawanyika kitandani na pale chini, tulipigana hasa na kuvunja vitu mle ndani kosa jirani yetu mmoja kuingilia kati, tungevunja vitu vyote mle ndani. Aliondoka na kuniacha nikijizoazoa pale chini na kukusanya dola zangu na kuzirudisha kwenye bahasha.
  Nilitoka na kwenda Polisi kuripoti lile tukio na nilipewa PF 3 na RB, sasa mchumba wangu alikuwa akitafutwa na Polisi, Baada ya kusikia kuwa anatafutwa alitoweka.

  Siku iliyofuata nilikwenda kazini, lakini kutokana na hali yangu ilibidi niombe ruhusa ili kujiuguza majeraha ya kupigwa na mchumba wangu.Nilipewa ruhusa ya kupumzika ya siku tatu na Bosi wangu, lakini sikwenda nyumbani kwangu bali nilikwenda kwao na mpenzi wangu Mwenge ili tuyamalize nilipofika nilimkuta shangazi yake anayeishi naye, akaniambia kuwa mpenzi wangu ameenda Moshi. Lakini hakumwambia shangazi yake kuwa tuligombana.Nilimsimulia shangazie tukio zima, shangazi yake alishangazwa na habari ile na alijaribu kumpigia simu lakini simu yake ilizimwa na sikuwahi kuwasiliana naye tena hadi leo.

  Niliondoka na ma kwenda Kariakoo kufanya shopping ya vitu vyangu vilivyovunjika ikiwa ni pamoja na vitu vingine na kurejea nyumbani. Ilipofika jioni nilisikia mlango wangu ukigongwa na nilipofungua nilikutana uso kwa uso na yule mzee, nilimkaribisha huku nikiwa nimetahayari kwani sikutegeme ujio wake, nilimkaribisha ndani.

  Alistushwa na hali yangu kwani macho yangu yalikuwa yamevimba na uso wangu pia, alinidadisi, nilimdanganya kama nilikutana na vibaka usiku nilipotoka kwenda kununua chipsi, alitaka kunipeleka katika Hospitali ya rafiki yake lakini nikataa kwa maelezo kuwa natibiwa na kampuni. Hakukaa sana aliondoka, siku inayofuata alikuja asubuhi kunijulia hali na aliniahidi kunifuata mchana ili tukale lunch pamoja, nilimkubalia.
  Nikweli alikuja na tulitoka pamoja hadi katika Hoteli moja iliyoko katikati ya mji, tulikula na kuongea mambo mengi sana, yule mzee alitaka kujua kama nina matarajio gani juu ya maisha yangu ya baadae nilimweleza kuwa nia yangu ni kujiendeleza zaidi kielimu kwani elimu yangu ya kidato cha sita na diploma ya usekretari sijaridhika nayo aliniuliza kama nataka kusomea nini, nilimjibu kuwa nataka kusomea sayansi ya jamii ngazi ya shahada, aliniuliza kama ningependa kusomea nje ya nchi au hapa hapa nchini.

  Nilishangazwa sana na swali lile, nilimjibu kuwa kwa kuwa sina uwezo kifedha nitasomea hapa hapa nchini, aliniambia kwa upole, "Sikiliza Gift, kwa kuwa mimi nipo, kila kitu kinawezekana, usiwe na wasiwasi nitakusomesha tafuta shule mahali popote nitakusomesha" nilishangazwa na ukarimu wa yule mzee, na aliongea akionekana amedhamiria hasa.Tulipotoka pale aliniambia kuwa anataka kuni-surprise, sikumuelewa kabisa, alinimbia nisubiri kidogo, tulikuwa tumesimama pale nje ya ile Hoteli na mara ikaja Toyota Rav 4 ya kijivu, na kusimama mbele yetu ilikuwa ni mpya kabisa, na yule dereva akashuka na kumkabidhi yule mzee funguo za lile gari.

  Yule mzee ambaye alijitambulisha kwangu kuwa anaitwa Alex, aliniuliza kama naweza kuendesha gari, nilimjibu kuwa sijui, alimuita yule dereva aliyekuja na lile gari ambaye alionekana ni dereva wake na kumuamuru anipeleke kwangu na kisha anipeleke chuo chochote kizuri nikajifunze udereva.
  Aliniambia kuwa lile ni gari langu ameninunulia ili kuniondolea usumbufu wa kugombea daladala. Nilibaki nimeduwaa sikujua hata niseme nini.

  Kwa kifupi nilianza uhusiano na yule mzee na alinishauri niache kazi kisha akanitafutia nyumba kubwa nzuri maeneo ta Mikocheni.
  Nililazimika kuacha kazi baada mpenzi wangu huyo mpya kunifungulia miradi ya Duka la nguo (Boutique) maeneno ya Msasani na Salon ya kike kubwa na Mini Super market. Miradi yote hiyo ilikuwa maeneo ya Kinondoni.Kwa muda mfupi maisha yangu yalibadilika na kuwa ya juu, nilikuwa namiliki magari matatu ya kifahari na nilinunua Kiwanja maeneo ya Mbezi beach na kuanza ujenzi bila kumshirikisha yule mzee, ambaye ndiye mfadhili wangu.

  Siku moja jioni nakumbuka ilikuwa ni Jumapili wakati nikiwa nimejipumzisha nyumbani, nilisikia mlango ukibishwa hodi, nilimtuma mfanyakazi wangu wa pale nyumbani akafungue mlango. Mara aliingia mama mmoja wa makamo hivi.Alikuwa ni mama wa heshima, nilimkaribisha sebuleni na kumuuliza kama angependa kinywaji gani, alikataa kupewa kinyawaji chochote, lakini alionekana kuzungusha macho huku na huko kama vile alikuwa anakagua kitu, nilimuacha amalize hamu yake kwani nilidhani alivutiwa na mapambo ya pale sebuleni.

  Baadae alisema, "Nadhani wewe ndiye Gifti kama sjakosea" nilimjibu kwa utulivu kuwa ndiye mimi….alishusha pumzi na kusema, "Je unamfahamu Mzee Alex?" Nilishtushwa na swali lile na nilijihisi mapigho ya moyo wangu yakienda mbio, lilikuwa ni swali la Kushtukiza sana. Nilijikakamua na kumjibu kuwa simfahamu mtu huyo.
  "Sikilizaa mwanangu, wewe ni sawa na binti yangu, na sijui wa ngapi, maana unaonekana kuwa bado u binti mdogo sana, kwa umri ulio nao haistahili kutembea na na wanaume za watu tena baba zako ambao wanaweza hata kukuzaa, mbona vijana wenzio wako wengi tu, kwa nini usiwatafuate hao, mpaka utembee na mume wangu? Nimeishi naye miaka zaidi ya 40, leo hii binti mdogo wa kukuzaa unataka kunivunjia ndoa yangu?"

  Aliniambia kwa upole kama vile mama aongeae na bintiye Ukweli ni kwamba maneno yale yalinishtusha sana, nilijikuta nikiwa nimemkodolea macho. Nakumbuka niliwahi kumuuliza mzee Alex kuwa familia yake iko wapi na alinijibu kuwa inaishi nchini Malawi na watoto wake wanasoma nchini Uingereza. Nilikuwa najivinjari na huyu mzee kwa uhuru hasa na sikuwa na wasiwasi kuwa kuna siku nitakuja kukutana na mtu ambaye angekuja kunikabili na kuniambia kuwa natembea na mumewe."Mama samahani naona umepotea nyumba huyu mzee simjui na wala sijui unamzungumzia nani hapa,……tena nakuomba uondoke maana mume wangu atarudi hivi punde asije akakufanyia jambo ambalo utalijutia maishani mwako" Nilijikakamua na kumjibu yule mama kwa upole.

  "Binti sikiliza, sipendi niingie kwenye kubishana na wewe, wakati ninao ushahidi wa kutosha kuwa unatembea na mume wangu, lakini……..sikutaka kulisema hili, ila kwa kuwa unaonekana mkaidi, nitakueleza,............ mume wangu si salama, ni muathirika, naomba ukapime afya yako, ili uanze kuishi kwa matumaini" alimaliza kusema na kunyanyuka ili aondoke.
  Moyo ulinilipuka na nilijikuta nikiropoka, "He, Mzee Alex ni muathirika?" nilijikuta nikiongea kwa sauti."Huna haja ya kukata tamaa, bado unayo nafasi ya kuishi, nenda kapime, mimi nilijigundua miaka kumi iliyopita na mpaka sasa ninaishi kwa matumaini, hata wewe unayo nafasi hiyo" Yule mama alinijibu kwa upole na kisha aliondoka zake na kuniacha nikiwa nimeduwaa, nisijue la kufanya, nilikurupuka na kwenda chumbani, nilimeza vidonge vya usingizi na kujitupa kitandani.

  Niliamka usiku wa manane kama saa nane za usiku hivi, nilikuwa na njaa, nilikwenda jikoni nikajitengenezea mkate wa nyama na juisi nikala, kisha nikakaa kitandani na kuanza kutafakari maneno ya yule mama. Niliona kama vile ile ilikuwa ni ndoto na huenda ingekwisha muda wowote, lakini hapana haikuwa ni ndoto ulikuwa ni ukweli mtupu. Siku iliyofuata nilimpigia mzee Alex simu lakini haikupokelewa nilituma ujumbe lakini hakujibu, baadae alinijibu kuwa yuko nchini Uingereza na angerudi baada ya mwezi mmoja, kuanzia siku hiyo namba yake ilikuwa haipatikani na mawasiliano na yeye yakakatika, niakaachiwa segere nilicheze peke yangu.

  Namshukuru shangazi yangu aliweza kuniliwaza na kunipeleka kupimwa na kweli niligundulika ni muathirika, na ninaishi kwa matumaini, sjaanza kutumia dawa ila najitahidi sana kula vyakula vizuri na kufanya mazoezi.
  Kwa kweli nina wakati mgumu sana, kwani kwa jinsi muonekano wangu ulivyo, nasumbuliwa sana na wanaume vijana na wazee, wananitaka kimapenzi na wengine wanataka wanioe, na nikiwaambia kuwa mimi si salama nimeathirika, wanabisha kabisa na wengine wanadiriki kusema hata kama nimuathirika hakuna shida hata akifa powa tu lakini atakuwa amefaidi. Yaani nashindwa kuwaamni wanaume, tena wengine wameoa na wana familia zao, lakini we kutwa kunivizia.

  Namshukuru mungu nimemudu kujikubali na kuyakubali matokeo, najua ni lazima nitakufa, siku moja lakini namshukuru mungu kwa kunipa ujasiri huu nilionao mpaka sasa nimemudu kuishi kwa amani na kuepuka vishawishi. Nawaasa vijana wenzangu hasa mabinti wa shule kuwa sio kila king'aacho ni dhahabu, ukimwi upo na unaua, tujiepushe nao.

  ANGALIZO:
  Huu ni mkasa uliompata rafiki yangu.
   
 2. Nyani Ngabu

  Nyani Ngabu Platinum Member

  #2
  Jul 11, 2012
  Joined: May 15, 2006
  Messages: 73,651
  Likes Received: 35,409
  Trophy Points: 280
  Aya tafadhali.
   
 3. Mkirua

  Mkirua JF-Expert Member

  #3
  Jul 11, 2012
  Joined: Sep 9, 2010
  Messages: 5,667
  Likes Received: 24
  Trophy Points: 135
  Duh.... Nitarudi baadaye...it is too long....
   
 4. Scofied

  Scofied JF-Expert Member

  #4
  Jul 11, 2012
  Joined: Jun 5, 2012
  Messages: 2,017
  Likes Received: 197
  Trophy Points: 160
  dah! Ngoja nipate kwanza lunch.....
   
 5. ram

  ram JF-Expert Member

  #5
  Jul 11, 2012
  Joined: Oct 5, 2007
  Messages: 6,201
  Likes Received: 903
  Trophy Points: 280
  Duh! Ndefu hiyo bt nimejitahidi kuisoma hadi mwisho.

  So sad, inahuzunisha kwakweli, hawa mapedeshee watatumalizia mabinti zetu,kha!
   
 6. SMU

  SMU JF-Expert Member

  #6
  Jul 11, 2012
  Joined: Feb 14, 2008
  Messages: 7,918
  Likes Received: 2,068
  Trophy Points: 280
  Asante vukani kwa mafundisho haya! Ni story nzuri na inafundisha, hasa kwa mabinti.
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 7. PetCash

  PetCash JF-Expert Member

  #7
  Jul 11, 2012
  Joined: Mar 20, 2012
  Messages: 1,679
  Likes Received: 170
  Trophy Points: 160
  Nice of you to share...na pia hongera kwa kujutia na kuwa na matumaini ya ku'live' this life after all...Nakutakia maisha marefu
   
 8. Scofied

  Scofied JF-Expert Member

  #8
  Jul 11, 2012
  Joined: Jun 5, 2012
  Messages: 2,017
  Likes Received: 197
  Trophy Points: 160
  nimerudi aisee...pole sana ni funzo kubwa kwa wadada wengine...tamaa mbayaaaaa sana
   
 9. M

  Mundu JF-Expert Member

  #9
  Jul 11, 2012
  Joined: Sep 26, 2008
  Messages: 2,719
  Likes Received: 28
  Trophy Points: 145
  Hii story inafanana na zile za zamani kidogo, labda miaka kati ya 80's na 90's ambazo ufahamu kuhusi ukimwi na maambukizi yake ulikuwa mdogo sana...sasa hivi kufanya mahusiano bila kujua afya zenu afu hamtumii kinga...ni jambo la hatari na ajabu sana...ma house girls hukumbwa na madanganyiko kama haya kwa kushindwa kujitambua na kutokuwa na maamuzi kwenye ngono...Kwa binti mwenye uelewa kama huyo...mhn haya bana...
   
 10. Mzee wa Rula

  Mzee wa Rula JF-Expert Member

  #10
  Jul 11, 2012
  Joined: Oct 6, 2010
  Messages: 8,177
  Likes Received: 89
  Trophy Points: 145
  Duuuuh unasisimua sana huo mkasa na ua full ujumbe.
   
 11. Viol

  Viol JF-Expert Member

  #11
  Jul 11, 2012
  Joined: Dec 15, 2009
  Messages: 18,982
  Likes Received: 1,087
  Trophy Points: 280
  vukani Duh nilidhani ndo unatuaga aisee.Ila huo mkasa ni funzo kubwa
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 12. N

  Nsuri JF-Expert Member

  #12
  Jul 11, 2012
  Joined: Oct 3, 2011
  Messages: 996
  Likes Received: 183
  Trophy Points: 60
  mhh kweli nimeamini mabinti kwa pesa hawachomoi.....
   
 13. Nivea

  Nivea JF-Expert Member

  #13
  Jul 11, 2012
  Joined: May 21, 2012
  Messages: 7,449
  Likes Received: 71
  Trophy Points: 145
  Mpendwa wangu huwa ananihusia kila siku ogopa njia rahisi rahisi za kujipatia hela mfano kupewa,bahati nasibu gambler etc au hela ambayo hujaitumikia itakukost,na hili ni fundisho na wanawake hawasikii hata uwauwe wanapenda vya bwerereeeee tu,hiki kisa ni kama kile cha wale wanafunzi wa sauti waliozoea kupewa mahela na wapenzi wa fb mwishoye wakaoza na kuyeyuka.
   
 14. Mpitagwa

  Mpitagwa JF-Expert Member

  #14
  Jul 11, 2012
  Joined: Feb 10, 2012
  Messages: 2,296
  Likes Received: 211
  Trophy Points: 160
  So long a letter, yanatokea, uzuri umelikubali na hujanyang'anywa mali. Pole na hongera kwa ujasiri
   
 15. platozoom

  platozoom JF-Expert Member

  #15
  Jul 11, 2012
  Joined: Jan 24, 2012
  Messages: 7,313
  Likes Received: 2,271
  Trophy Points: 280
  Ex B/F yuko wapi.......hivi mtu ulishafikiria kukumkuta mpenzi wako kapakiwa kwenye VX na mjamaa halafu anakutizama kama hakuoni wakati wewe unasubiria daladala za mbagala?
   
 16. platozoom

  platozoom JF-Expert Member

  #16
  Jul 11, 2012
  Joined: Jan 24, 2012
  Messages: 7,313
  Likes Received: 2,271
  Trophy Points: 280
  Ex B/F yuko wapi?.......hivi mtu ulishafikiria kukumkuta mpenzi wako kapakiwa kwenye VX na mjamaa halafu anakutizama kama hakuoni wakati wewe unasubiria daladala za mbagala?
   
 17. MVUMBUZI

  MVUMBUZI JF-Expert Member

  #17
  Jul 11, 2012
  Joined: Jan 8, 2011
  Messages: 4,970
  Likes Received: 666
  Trophy Points: 280
  Hadithi kama za shigogo dada utakuwa mtunzi mzuri wa Riwaya. Ila nilichoona hapa huyo dada alikuwa na uwezo wa kukataa lunch, lift na kila ofa na akawa salama. Tabia ya SITAKI NATAKA pamoja na tamaa za mali ndizo haswa zinazoponza mabinti wengi. Hawaangalii vitu vya muda mrefu bali starehe kubwa za haraka ambazo huwa maranyingi hufupisha maisha yao
   
 18. stroke

  stroke JF-Expert Member

  #18
  Jul 11, 2012
  Joined: Feb 17, 2012
  Messages: 13,372
  Likes Received: 6,553
  Trophy Points: 280

  Asante kwa mkasa ..ila hapo kwenye red apo..marekebisho..Information Technology
   
 19. Blaine

  Blaine JF-Expert Member

  #19
  Jul 11, 2012
  Joined: Jan 11, 2012
  Messages: 2,285
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 0
  naona vukani anataka kumuiga Mtambuzi


  PS: sijui namna ya ku-mention users
   
 20. Sangarara

  Sangarara JF-Expert Member

  #20
  Jul 11, 2012
  Joined: Sep 29, 2011
  Messages: 13,048
  Likes Received: 549
  Trophy Points: 280
  Edit kwenye International Technology, sijawahi kufikiria kuna course ya chuo inayoweza kubeba jina la namna hii.Paragraph ya tano kuanzia neno la mwisho mstari wa tatu. Naendelea kusoma lakini lazima iishie kwa huyu binti kuwa ni muathirika.
   
Loading...