SIKU YA WANAWAKE: Wapaza sauti, uongozi, ukatili kingono kwa wanawake

John Haramba

JF-Expert Member
Feb 4, 2022
365
1,373
Wakati wanawake wakiadhimisha siku yao leo, wadau wamesema rushwa ya ngono ni tatizo linalotafuna ndani kwa ndani, huku wakitaka wanawake zaidi kuongoza katika sekta mbalimbali nchini.

Baadhi ya wadau hao ni Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA TAN).

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na TAMWA, ilisema kinaangalia usalama wa wanahabari wanawake katika vyumba vya habari nchini kutokana na kuwapo kwa mwendelezo wa matukio, ushahidi na ripoti za kitafiti zinazoonyesha kuwa wanahabari wanawake bado wanapitia unyanyasaji wa kingono katika vyumba hivyo.

Ilisema maadhimisho ya Siku ya Wanawake kwa mwaka huu, yamebebwa na kaulimbiu isemayo; “Kizazi cha Haki na Usawa kwa Maendeleo Endelevu”.

Kauli hii ni kutaka kuweka usawa katika vyumba vya habari baada ya kubaini kuna mdudu anayetafuna tasnia ya habari kimya kimya.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, utafiti uliofanywa na Asasi ya Wanawake katika Habari Afrika (WIN) ulibaini kuwa, asilimia 41 ya wanawake wanahabari waliwahi kufanyiwa unyanyasaji wa kingono wakiwa katika maeneo ya kazi.

Chama hicho kimesema wakati Siku ya Wanawake Duniani ikiadhimishwa, TAMWA inahimiza wamiliki wa vyombo vya habari, watunga sera, serikali na wanahabari wote kwa ujumla kutupia jicho unyanyasaji na ukatili wa kingono unaofanywa ndani ya vyumba vya habari.

“Unyanyasaji wa kingono kwa wanahabari iwe ndani au nje ya vyumba vya habari, una madhara makubwa katika chombo cha habari, taaluma ya habari, aina ya habari zitakazoandikwa na hata katika maendeleo ya nchi yenyewe,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dk. Rose Reuben.

Alisema, udhalilishaji wa kingono kwa wanahabari wanawake, unachagiza wanahabari wengi wa kike kuikimbia tasnia na hilo limesababisha kupoteza vipaji lukuki ambavyo vingekuzwa kama kusingekuwa na bughudha hiyo.

Alisema katika utafiti uliofanywa na TAMWA kwa kushirikiana na Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT) mwaka 2021, kuhusu hali ya rushwa ya ngono ndani ya vyumba vya habari, ilibainika kuwa wanahabari wanawake wamewahi kukutana na udhalilishaji huu, kimwili, kimaneno na hata baadhi walifukuzwa kazi.

Kwa upande wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA-TAN), ilitoa wito kwa serikali, sekta binafsi na taasisi mbalimbali kuhakikisha wanawake wanapewa nafasi za uongozi kwenye taasisi hizo sawa na wanaume.

“MISA-Tanzania inaunga mkono kauli mbiu ya mwaka huu inayolenga kuvunja upendeleo wa jinsia, yaani #BreakTheBias, kwa kufanya kampeni maalumu kwenye mitandao ya kijamii kwa kuwatambua baadhi ya wanawake vinara kwenye sekta ya habari nchini,” ilisema taarifa hiyo.

"Baadhi ya vyombo vingi vya habari nchini bado vina mfumo dume na wanawake hupata changamoto nyingi kufikia nafasi za juu za uongozi, wengi wameishia kukaimu, wasaidizi na kazi za kawaida licha ya kuwa na uwezo wa kitaaluma na uzoefu wa majukumu husika," alisema Salome Kitomari, Mwenyekiti wa MISA-Tanzania.

“Vyombo vingi vya habari ukiingia unaona ni duniani ya wanaume ‘mens world’. Kinachokosekana ni kuwaamini na kuwaacha watekeleza majukumu hayo licha ya sifa na vigezo vinavyotakiwa, ndiyo maana kwenye vyuo vya uandishi wa habari wanahitimu wanawake wengi, wanaingia kwenye vyombo vya habari wengi hubaki kuwa ripota na inapotokea nafasi ya uongozi hawapewi siyo kwasababu ya uwezo ni kwa sababu ya mfumo, wengine hukata tamaa na kwenda kufanyakazi nyingine,” aliongeza.

“MISA-Tanzania inatoa wito kwa vyombo vya habari na taasisi mbalimbali za tasnia hii, kuwa na sera mahsusi zinazotekelezeka zenye lengo la kuondoa mfumo dume huo kwenye taasisi zao kwa kuhakikisha kuwa wanawake wanajengewa uwezo, wanaaminiwa na kupewa nafasi za uongozi kwa mujibu wa sifa na vigezo."

Taarifa hiyo ilisema utafiti uliofanywa mwaka 2019 na Baraza la Habari Tanzania (MCT), ulibaini kuwa wanawake wanapewa nafasi za kati na za chini kwenye vyombo vya habari vingi nchini na huwa ni ngumu kwao kushika nafasi za juu za uongozi hata kama wana uzoefu au elimu zaidi kuliko wanaume.

Utafiti huo uliopewa jina la "Challenging the Glass Ceiling: Study of Women in the Newsroom in Tanzania", ulibaini pia kuwa waandishi wa habari nchini hupangiwa kuripoti matukio ambayo siyo makubwa au mazito, ambayo mara nyingi hupangiwa waandishi wa habari wanaume.

Ilisema watafiti waliongeza kuwa kuna idadi ndogo ya waandishi wa habari wanawake kwenye vyombo vya habari, licha ya kuwa wanawake wengi huhitimu vyuo vya uandishi wa habari nchini kuliko wanaume.

Source: Nipashe

SIKU YA MWANAMKE.jpg
 
Wagusie na chuki baina yetu/yao. Kwa sasa adui wa mwanamke ni mwanamke mwenzie
 
Hivi katika siku 366, siku ya wanawake inakuwa moja tu...........hawa viumbe ni shida.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom