Siku nyingine usiwe mbishi

Pdidy

JF-Expert Member
Nov 22, 2007
50,462
21,334

Siku nyingine Kikwete usiwe mbishi




amka2.gif

KWA mara nyingine tena taifa lilipatwa na mshtuko wakati Rais Jakaya Kikwete alipolazimika kuondolewa katikati ya sherehe katika Uwanja wa CCM Kirumba mkoani Mwanza baada ya kupatwa na tatizo la kiafya.
Sijui kama ni sahihi kuita tatizo la kiafya baada ya madaktari wake kutueleza kuwa kilichotokea hakina uhusiano na afya ya Rais.
Wanasema vipimo na uchunguzi aliofanyiwa vinaonyesha kuwa hana tatizo lolote kubwa la kiafya.
Wanasema kilichotokea ni kuwa Rais alifikia katika hali ile kutokana na uchovu.
Kabla hajahudhuria sherehe hizo za kutimiza kwa miaka 100 ya Kanisa la Afrika Inland Tanzania (AICT), Rais Kikwete alikuwa amekutana na watu kadhaa jana yake na kushiriki kwenye shughuli za kuanzisha matembezi ya vijana wa CCM kama sehemu ya kumbukumbu ya miaka 10 tangu kufariki kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Kabla ya hapo alikuwa ametokea mkoani Arusha ambako alikuwa ameshafungua mkutano wa mwaka wa mabunge ya Jumuiya ya Madola. Alifika Arusha ikiwa ni saa chache tu tangu arejee kutoka Marekani ambako alikwenda kuhudhiria kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Kwa mujibu wa maelezo ya madaktari wake, safari hiyo ya kurejea kutoka Marekani ni moja ya mambo yaliyomchosha sana kwa sababu alilazimika kusafiri kwa saa 24 bila kupata usingizi wa kutosha.
Rais Kikwete mwenyewe alithibitisha kuwa uchovu ndio uliosababisha azidiwe na kuhitaji huduma ya kwanza kabla ya kuendelea na shughuli za sherehe ya kanisa pale Mwanza. Alikwenda mbali zaidi na kuonyesha kuwa kumbe suala hili lilijulikana lakini ni kutokana na ubishi wake ndio maana lilitokea na kuzusha gumzo kubwa nchini na ndani ya nchi.
Rais Kikwete aliueleza umma pale Kirumba baada ya kupatiwa huduma na kurejea uwanjani kuwa wasaidizi wake walishamshauri apumzike.
Walimshauri hata Arusha asiende, lakini yeye akawa mbishi. Kwa maana hiyo, wasaidizi walishaona kuwa hali ya Rais haikuruhusu yeye kushiriki, lakini akawa mbishi.
Hapa zinaibuka hoja kadhaa. Kwanza mtu unaweza kuhoji, kama afya ya Rais ni timamu kwa kiwango ambacho madaktari wake wanavyosema, inawezekana vipi akafikia hatua ya ‘kuzimika ghfla’ kutokana na kuzidiwa na uchovu? Wataalamu wa afya wanafahamu fika kuwa uchovu unapofikia hatua ya kusababisha hali kama iliyomkuta Rais, basi kuna matatizo sehemu fulani katika mfumo wa afya ya mtu huyo.
Kwa kuwa si rahisi mtu mwenye afya timamu akaanguka ghafla kutokana na uchovu, madaktari wake wanapaswa kutupa maelezo yatakayoonyesha bila shaka tatizo hasa lilikuwa nini hadi Rais akapatwa na hali ile.
Lakini pia inashangaza kwa nini, mtu ambaye analindwa na kutunzwa kuliko mtu mwingine yeyote nchini anafikia hatua ya kuchoka hadi kufikia hali ile? Nimesoma makala ya rafiki yangu Ansbert Ngurumo sehemu fulani wiki hii na yeye anahoji iweje, kuna Watanzania mamilioni ambao mlo wao ni wa mashaka, wanafanya kazi muda mrefu sana na kupumzika kwa muda mfupi mno, lakini hatujasikia wakianguka kwa uchovu.
Hivi hasa kilichotokea kwa rais ni kitu gani? Na mimi niungane naye kujiuliza; iwapo haya yanatokea kwa mti mbichi, itakuwaje kwa mti mkavu?
Lakini Rais naye anatakiwa kuwa makini wakati mwingine. Kama kweli alishauriwa na wasaidizi wake, alipaswa kuwasikiliza. Hakupaswa kuwa mbishi kwa sababu hao wana utaalamu na kutokana na utaalamu waliokuwa nao ndio walifikia hatua ya kutoa ushauri huo.
Inashangaza kuwa sisi tumewaajiri watu hawa kama hatua ya kuhakikisha kuwa kiongozi wetu wa nchi anakuwa salama wakati wote. Tumewapa majukumu wasaidizi hawa kuhakikisha kuwa Rais anakuwa katika hali bora ya kuliongoza taifa kila wakati. Na Rais analijua hili.
Nadhani Rais Kikwete anajua fika ubishi wake umelisababishia taifa usumbufu kiasi gani. Ukiacha mishtuko ya moyo iliyowapata wale waliokuwa wamekaa naye meza moja pale Kirumba, nchi ilianza kutaharuki pale taarifa zilipoanza kusambaa kuwa “Rais amenguka akiwa anahutubia mkutano.”
Tukio kama hili lingetokea kwenye nchi zilizoendelea, mara moja ingeweza kujionyesha hata kupitia kwenye milango ya kibiashara kupitia bei za hisa katika masoko. Hapa itatuwia vigumu kupima tukio lile limeingiza hasara ya kiuchumi kwa kiasi gani katika nchi.
Ni wazi kuwa Rais aliamua kuwa mbishi kwa sababu anataka kuchapa kazi ya kuwatumikia wananchi kama alivyoahidi wakati akiomba ridhaa ya miaka minne iliyopita. Lakini na yeye anafahamu fika kuwa hilo halipaswi kufanywa kwa kupitiliza, lazima kuwe na vipimo.
Na kama angewatumia washauri wake ipasavyo, walishaweka vipimo hivyo. Pamoja na hulka yake ya kutaka kufanya kazi kwa kiwango kikubwa, anapaswa kufahamu kuwa yeye ni binadamu tu, kuna mahali anafika anatakiwa kuweka breki na kupumzika.Kwanza, hata awe na uwezo mkubwa wa kufanya kazi, si rahisi akaweza kuzifanya kazi zote ambazo anawajibika, au anapaswa kuzifanya na kuzikamilisha kwa ufanisi. Ingawa Rais mwenyewe ameahidi kuwa wakati mwingine atazingatia ushauri wa wasaidizi wake, na mimi nasisitiza kuwa apunguze, au ikiwezekana aache kabisa kuwa mbishi, hasa katika mambo ambayo wataalamu wanamshauri.


 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom