Siku kama ya leo tarehe kama ya leo Miaka 39 iliyopita...

Rubawa

JF-Expert Member
Dec 25, 2015
2,055
3,239
BARAZANI

Kupaa na kuanguka kwa Husni Mubarak (1928-2020)

Na Ahmed Rajab

JUMATANO, Oktoba 14, 1981 mara tu baada ya kuapishwa kuwa Rais mpya wa Misri, Husni Mubarak aliingia ndani ya ofisi ya msaidizi wake mmoja akaanza kurukaruka akipiga kelele: “Mimi rais, mimi rais”.

Alikuwa kama mtoto mdogo aliyefurahi baada ya kupewa peremende.

Mubarak, aliyefariki dunia Februari 25, 2020 akiwa na umri wa miaka 91, alikuwa hakuulalia wala hakuuamkia urais. Ulimjia kama mana kutoka mbinguni. Mitaani watasema urais wake ulikuwa “riziki dudu”.

Miaka yote alipokuwa mwanajeshi akitamani ateuliwe awe balozi nchi za nje lakini urais haukumpitikia hata chembe.

Mubarak alikuwa rais wa mwanzo wa Misri ambaye hakuwa miongoni mwa wale waliokuwa kwenye Vuguvugu la Wanajeshi Huru (Free Officers Movement). Waliokuwa ndani ya duru hiyo ndio waliofanya mapinduzi mwaka 1952 yaliyompindua Mfalme Farouk aliyekuwa na asili ya Albania.

Marais wote watatu waliomtangulia walihusika katika mapinduzi hayo. Nao ni Mohamed Naguib, Gamal Abdel Nasser na Anwar Sadat. Kiongozi wao alikuwa Nasser aliyekuwa na lengo la kumpindua Farouk na pia kuwaondosha Waingereza Misri na Sudan, nchi ambazo wakati huo zikitawaliwa pamoja.

Wakati wa mapinduzi, Mubarak alikuwa na kazi ya kuwafundisha wanajeshi namna ya kuendesha ndege za kivita na mwaka 1959 alipelekwa Muungano wa Jamhuri za Kisovieti kwa mafunzo zaidi ya kijeshi. Alipokuwa huko alipata mafunzo kwenye chuo cha kuwafunza marubani jijini Moscow na pia katika Kambi ya Jeshi la Anga karibu na Bishkek, kwenye Jamhuri ya Kisovieti ya Kyrgyzstan. Alirudi Misri 1961.

Wakati wananchi wa Yemen ya Kaskazini walipokuwa vitani wakipigana wenyewe kwa wenyewe (1961-1970), Misri iliingilia kati kuwasaidia wapinduzi dhidi ya Mfalme. Mubarak alikuwa miongoni mwa marubani wa Misri waliopelekwa kuzipiga mabomu ngome za wafuasi wa Mfalme.

Mwaka 1967 Mubarak alimuudhi Rais Nasser aliposhindwa kutoa ushahidi wa kuthibitisha shtuma zake kwamba ndege za aina ya jet za Marekani zilishiriki katika mashambulizi dhidi ya Misri wakati wa mapigano baina ya nchi za Kiarabu na Israel.

Baada ya kumalizika vita Nasser alimuondosha kwenye wadhifa wake na akampa kazi ya utawala akiwa mkurugenzi katika Chuo cha Jeshi la Anga.

Rais Sadat, aliyemrithi Nasser, alimuangalia Mubarak kwa jicho la rehema. Jambo lililomvutia Sadat ni kwamba Mubarak hakuwa na muelekeo wowote wa kisiasa na wala hakuwa na tabia ya kujitokeza mbele mbele.

Mwaka 1972 Sadat alimteua Mubarak awe kamanda wa jeshi la anga na naibu waziri wa vita. Miaka mitatu baadaye, Sadat alimteua awe Makamu wa Rais.

Uteuzi huo uliwashanganza wengi ndani na nje ya Misri kwa sababu Mubarak hakuwa akijulikana sana. Waliokuwa wakimjua wakijua kwamba siasa hazikuwa zikimwenda katika damu yake. Marais wote wliomtangulia walikuwa na haiba na mvuto wa kisiasa.

Sadat, kwa mfano, alikuwa rais wa aina yake aliyejifanyia mambo kivyake. Aliwashangaza si Wamisri tu bali walimwengu wengi alipofunga safari ya kwenda Jerusalem 1977 na kuhutubu kwenye Knesset, bunge la Israel.

Wananchi katika nchi za Kiarabu na za Kiislamu walikasirishwa bila ya kiasi. Wengi waliiona safari hiyo ya Sadat kuwa ni safari ya usaliti, ya uhaini wa hali ya juu.

Siku mbili kabla ya kufunga safari yake Sadat alikwenda Damascus, Syria, kumbembeleza Rais Hafez al Assad amruhusu, akiwa Israel, azungumze kwa niaba ya Misri na Syria.

Assad alikataa. Alimwambia Sadat kwamba ulimwengu wa Kiarabu hautomsamehe. Huku akikunja uso Assad alimueleza Sadat kuwa ashukuru kwamba hawakumkamata.

Mohamed Hassanein Heikal, aliyekuwa mwandishi nguli wa Misri, aliwahi kuandika kwamba saa za asubuhi kabla ya huo mkutano baina ya Assad na Sadat, viongozi wakuu wa Syria walikutana. Moja ya mambo waliyoyafikiria lilikuwa ni kumkamata Sadat akiwa Syria na kumzuia asisafiri kwenda Jerusalem.

Walikuwa wameshapanga waueleze nini ulimwengu wa Kiarabu. Walikubaliana kuwa watasema kwamba Sadat alibidi azuiwe kwa matibahu kwa sababu aliingiwa na kichaa akiwa Syria.

Ndani ya Misri kwenyewe, waziri wa mambo ya nje, Ismail Fahmy, alijiuzulu akiipinga ziara ya Sadat ya kwenda Jerusalem. Mawaziri wengine walinung’unika chini kwa chini na walimkubalia Sadat kichwa upande.

Inasemekana kwamba Mubarak alikuwa miongoni mwa wachache katika uongozi wa Misri waliomuunga mkono Sadat moja kwa moja. Alikuwa kama kibaraka wake, ingawa inaaminiwa kwamba Sadat hakuazimia kumweka Mubarak kwa muda mrefu zaidi kwenye kiti cha umakamu wa urais.

Sadat hakujua wala Mubarak hakung’amua kwamba cheo kikubwa kabisa cha Misri kilikuwa kimuangukie Mubarak kufuatia yaliyojiri Oktoba 6, 1981. Hiyo ilikuwa siku adhimu kwa Misri. Ilikuwa siku ya gwaride la kila mwaka, “Gwaride la Ushindi”, kuadhimisha ufanisi wa “Operesheni Badr”.

Operesheni hiyo ilikuwa ya jeshi la Misri kuuvuka Mfereji wa Suez na kujinyakulia sehemu ndogo ya ardhi ya Misri iliyokuwa imetekwa na Israel mwaka 1967. Sadat alikuwa akijivunia fanikio hilo.

Siku ile ya Oktoba 6, 1981 ilikuwa ni siku ambayo Sadat alikuwa afe tu. Hakuwa na hila.

Alipoamka asubuhi alikuwa na furaha kwamba ataivaa sare yake mpya ya uamiri jeshi. Sare hiyo ilikuwa imewasili Cairo siku chache kabla kutoka kwa mshoni wake London, Uingereza.

Sadat alikuwa mkaidi na akijiona. Akihisi kwamba yeye akijua kila kitu. Ukaidi wake uliibuka kwa mara ya mwisho alipokuwa anaivaa hiyo sare yake kabla hajenda kwenye gwaride. Alikataa kukivaa kwanza kizibao kinachozuia risasi.

Mkewe, Jihan, alimkumbusha akivae, akakataa. Alikuwa akilalamika kwamba kizibao hicho kikimuonesha kuwa mtu aliyefura kuliko alivyokuwa.

Alipokuwa anatoka chumbani aliipita meza iliyokuwa karibu na mlango. Juu ya meza kuliwekwa kifimbo chake cha uamiri jeshi. Sadat alighafilika na akasahau kukichukua. Jihan alisema kwamba ilikuwa nuksi, dalili mbaya, Sadat kukisahau kifimbo cha uamiri jeshi.

Kulikuwa na uvumi kwamba kutatokea kitu siku hiyo. Inasemekana kwamba hata makamu wake Mubarak alimuonya Sadat asihudhurie sherehe. Lakini Sadat hakumsikiliza.

Kabla ya Sadat kuwasili kwenye uwanja wa gwaride, Mubarak alikuwa tayari ameketi jukwaani. Alipowasili Sadat walikaa bega kwa bega, ubavu kwa ubavu.

Sadat alionekana kuwa na furaha kubwa akitafahari madege ya kivita yalivyokuwa yakiruka na kufanya maajabu yao angani. Ukafika wakati wa kupigiwa saluti na Sadat aliposimama kupokea saluti Mubarak alisimama naye.

Mara magruneti yalionekana yakiripuka hewani na risasi zilipoanza kudata na kummiminikia Sadat, Mubarak alikuwa ubavuni mwake.

Luteni Khaled el Islambouli, aliyemuua Sadat, alidai alipokuwa akisailiwa baada ya kukamatwa kwamba alimpigia kelele Mubarak akimwambia: “Sumile! Usinizinge, ninamtaka mbwa huyu tu”, akimkusudia Sadat.

Hatujui kama kweli Islambouli aliyasema hayo. Na kama aliyasema hatujui iwapo Mubarak kweli aliyasikia na akazikwepa risasi au ilikuwa bahati yake tu. Lakini kunusurika alinusurika.

Kuuliwa kwa Sadat na magaidi Wakiislamu waliokuwa na msimamo mkali wa kidini kulimsafishia njia Mubarak ya kuwa Rais. Baada ya kumuua Sadat, Islambouli, aliyekuwa na umri wa miaka 24, aliwahi pia kusema: “Nimemuua Firauni, na siogopi kifo.”

Siku nane tu baadaye, “firauni” mwengine aliibuka Misri na aliitawala nchi hiyo kimabavu kwa muda wa miaka 30. Alipokuwa akirukaruka dakika chache tu baada ya kuwa Rais, Mubarak moyoni mwake alikwishaanza kuiona nchi nzima kuwa ni milki yake.

Hadharani akionesha uso mwingine. Alikiri kwamba hakuwa na ujuzi wa siasa, kwamba ataomba ushauri wa wengine na zaidi aliahidi kwamba urais utakuwa wa muhula maalum tu. Naye hatoukiuka.

Mara tu baada ya kuwa rais, Mubarak aliunda kamati maalum ya mabingwa wa mambo ya uchumi ili wajaribu kuitathmini hali halisi ya uchumi wa Misri.

Uchumi ulikuwa mahututi. Mzigo wa madeni ya Benki ya Dunia na IMF pekee ukiuumiza mgongo wa nchi hiyo. Kila mwaka Hazina ya Misri ilikuwa ikilipa dola za Marekani milioni elfu mbili ($2,000m) kuyahudumia, yaani kuyalipia riba, madeni ya taasisi hizo mbili tu.

Waliokuwa karibu na Mubarak walipata ureda wakati wa enzi yake. Kwao, hiyo Ilikuwa ni enzi ya neema. Ukaribu wao kwa Mubarak uliwawezesha wapore rasilmali kubwa ya Misri. Walichota watakavyo, walijigeuza mirija wakiinyonya nchi na walijiona wao kuwa ndio mabwana wa nchi hiyo.

Maisha kwa wengine, raia na wanajeshi, yalizidi kuwa magumu. Ukali wa maisha yao ulikuwa ukishindana na ukali wa utawala katika kuikaba demokrasia.

Mubarak alikuwa mjanja. Kuhusu uhusiano baina ya Misri na Israel, kwa mfano, ni wazi kwamba alijifunza kutokana na mauaji ya Sadat. Mubarak aliendeleza sera zaidi ya zile za Sadat katika uhusiano baina ya Misri na Israel. Tofauti ni kwamba wakati huohuo Mubarak akikataa kwenda Israel.

Kuhusu uendeshaji wa mambo ya ndani ya nchi, akijifanya kuwa yeye ni “baba wa taifa” na kwamba Wamisri wote ni wanawe lakini mambo ya ndani yanaendeshwa na serikali.

Utamu wa madaraka ulipomkolea, Mubarak aliivunja ahadi yake ya kutoongeza muhula zaidiwa kutawala. Alitawala akitumia sheria za dharura zilizowapa polisi nguvu kubwa za kuwakandamiza watu, hususan wakosoaji na wapinzani wa utawala wake.

Aghalabu huwa taabu kutabiri lini hasa mapinduzi yatapotokea na taabu zaidi kutabiri mkondo utaofuatwa na mapinduzi yakishatokea.

Hata hivyo, Mubarak aliyetawala kwa miaka 30 aling’oka madarakani siku 18 tu baada ya wananchi kujitosa barabarani. Walilibomoa kuta la hofu na vitisho wakamiminika kwenye medani ya Tahrir jijini Cairo wakidai kwamba Mubarak lazima atoke madarakani.

Jeshi la polisi halikuweza kuzishinda nguvu za umma. Mubarak aliondoka madarakani kwa izara kwani mwishowe hata wenzake katika majeshi walimtema,

Kabla ya kupinduliwa alikuwa akiandaa mipango ya kumwezesha mwanawe, Gamal, amrithi katika urais kama Bashar al Assad alivyomrithi Hafez al Assad nchini Syria. Nguvu za umma ziliizika tamaa hiyo.
 
Mkuu umeandika vitu konki Sana, lakini hebu rekebisha heading Basi, hizo km, km Zina maana gani? Wacha utoto basi
 
Andiko zuri Sana,nilichojifunza siku ya kuanguka ikifika hakuna kitakachoweza kuzuia,mfano Sadat anadharau kuvaa bulletproof,wananchi wanaingia barabarani bila woga wa nguvu ya kijeshi ya mubarak
 
Back
Top Bottom